Sehemu ya 04
Tulitoka nje ya chumba cha maiti huku nikiziacha pua zangu kuvuta hewa safi baada ya kuwa kwenye hali mbaya. Baada ya kutulia Somati aliniambia:
“Nina imani umeiona kazi yangu?” alisema huku akifungua kichupa kidogo cha kinyagi na kunywa kidogo.
“Nimeiona lakini bado naona maluweluwe.”
“Ya nini?”
“Bado siamini kazi hii ya mshahara wa laki mbili uwe kwenye hali uliyonayo kwa sasa.”
“Nitakujibu jioni, la muhimu chukuahuu mzigo niliokuitia nitaukuta kwako.”
Kwa vile sikuhitajikuwa eneo lile kutokana na hali yangu kubadilika kwani toka nilivyoiona maiti iliyopata ajali nilikosa amani moyoni mwangu. Nilijiuliza Somati ana moyo mgumu kiasi gani kuziona maiti kama kitu cha kawaida.
Nilichukua mzigo alionipa na kuondoka zangu kurudi nyumbani huku njiani nilijiuliza kama mimi kuona mtu mmoja tu nimechanganyikiwa nilijiuliza kama ningewaona wote kumi sijui ingekuwa kwenye hali gani, kila dakika nilihisi kichefuchefu na kutema mate ovyo.
Nilipofika nyumbani kwa vile nilitoka usikuusiku nilioga na kupanda kitandani, usingizi haukuchelewa kunichukua.
Usingizini niliiota ile maiti moja kati ya kumi niliyooneshwa na Somati ya mtu aliyopata ajali. Nilijikuta nikiweweseka na kupiga kelele kitu kilichomshtua mke wangu.
“Vipi mume wangu leo una nini?”
“Ha..ha..pana,”nilijikuta nikibabaika huku akitweta na jasho kumtoka.
“Kwani mume wangu umeota nini?” Mke wangu aliniuliza huku akiwa amesimama pembeni ya kitanda. Macho yangu yalikutana na mwanga mkubwa wa nje kuonesha kumekucha kitambo, nilijiuliza nimepiga kelele kiasi gani.
“Kwani umesikia nini?” nilimuuliza mke wangu.
“Nilikuwa nje sauti yako kama umekutana na shetani imenitisha sana na kuingia nimekukuta akihema huku jasho likikutoka hebu niambie umeona nini mume wangu,” mke wangu alinibembeleza kwa shauku ya kutaka kujua nimeota nini.
“Niliota nataka kugongwa na treni,” nilitengeneza uongo ili kuficha kilichonitisha usingizini.
“Pole mume wangu.”
“Asante.”
Mke wangu aliniletea maji ya kunywa ili kuipoza hofu, baada ya kunywa maji, nilimuuliza mke wangu:
“Muda huu ni saa ngapi?”
“Saa nne asubuhi.”
“Ooh! Kumbe nimelala sana.”
“Labda uchovu wa kudamka alfajiri.”
“Vipi shemeji amekuja?”
“Mmh! Sijamuo...”
Mazungumzo yetu walikatishwa na hodi iliyokuwa ikibishwa mlangoni, mke wangu alikwenda hadi mlango wa sebuleni na kumsikia akisema:
“Karibu shemeji.”
Kauli ya kukatibishwa mgeni ilininyanyua kitandani na kukaa, nilitulia kwa muda mpaka mkewe wangu alipokuja kunieleza.
“Mume wangu shemeji amekuja.”
Sikutaka kuuliza shemeji gani kwa vile mtu aliyekuwa amezoeleka kwangu ni rafiki yangu Somati, nilinyuanyuka nikiwa nimejifunga kanga ya mke wangu na kutoka chumbani, nilimkuta Somati amejaa tele sebuleni.
“Karibumzee.”
“Asante, za muda?”
“Mmh! Nzuri.”
“Mbona umelala sana?”
“Si unajua nilitoka usiku.”
“Tuachane na hayo, naomba ule mzigo.”
Nilikwenda chumbani na kuchukua mfuko alionipa Somati na kumpelekea, baada ya kupokea na kuingiza mkono kwenye mfuko ule na kutoa bunda la noti na kunikabidhi.
“Za nini?” nilimuuliza.
“Za kwako kwa kazi uliyoifanya.”
“Kazi! Kazi gani?” nilishtuka.
“Kwani umeamka saa ngapi?”
“Usiku.”
“Ukaenda wapi?”
“Nikaja kwako.”
“Basi ndiyo kazi uliyofanya leo.”
“Asante.”
“Basi mi’ nikuache upumzike tutaonana jioni.”
“Sawa, unataka kuniambia zote hizo ni pesa?”
“Ina maana hukuziangalia?”
“Walaa, sikuwa na idhini ya kupekua.”
“Ni pesa, na hii ndiyo biashara inayoyabadili maisha yangu.”
“Duh! Sasa pale una biashara gani?”
“Tutazungumza jioni.”
“Sawa.”
Somati aliaga na kuondoka na kuniacha nimekaa sebuleni pesa zangu mkononi, nilinyanyuka na kurudi chumbani. Nilipofika chumbani nilifungua burungutu nililopewa na Somati na kuzihesabu noti zile. Sikuamini zilikuwa shilingi milioni moja taslimu.
Nilijiuliza kama burungutu moja ni milioni moja mule kwenye mfuko zipo kiasi gani. Nilijikuta nikiwa na maswali yasiyo na jibu juu ya fedha nyingi kiasi kile ambazo nilikwenda kuzichukua kwa Somati. Nilijiuliza kuna biashara gani iliyopo pale hospitali.
Kutokana na kuchanganyikiwa na kiasi kikubwa cha fedha nilijikuta nimesahau niliyokutana nayo mochwari na kubakia moja la rafiki yangu kupata kiasi kikubwa cha fedha huku nami nikiingusa milioni kwa mara ya kwanza. Nilijikuta nikiwa na shauku ya kutaka kujua rafiki yangu anapataje kiasi kikubwa cha fedha wakati kule mochwari hakuna biashara yoyote.
Mazingira ya kazi yake hayakuonesha dalili zozote ya kuwa na kitu cha kumuingia fedha nyingi kiasi kile. Lakini niliamini majibu ya maswali yangu nimeyapata kwa Somati mwenyewe jioni ya siku hiyo. Nilijikuta mwenye mawazo mengi juu ya matumizi ya fedha niliyopewa na rafiki yangu.
Nilimwita mke wangu na kumwelea kuwa nimepewa fedha na Somati, akiwa katika hali ya kutoamini wingi wa fedha alinipa ushauri wa kununua kiwanja. Wazo la mke wangu nililiunga mkono na kupanga kutafuta kiwanja kwa ajili ya kujenga nyumba angalau chumba na sebule.
Pamoja na mipango yote bado akili yangu ilikuwa kwenye fumbo la kutaka kujua Somati anapata wapi fedha nyingi kama ile na kwa biashara gani. Nilijikuta nikikosa raha kusubiri kujua siri ya fedha za rafiki yangu. Mwanzo nilidhani labda ana fedha za ndagu kutokana na jinsi alivyokuwa akijiweka.
Somati alikuwa halingani na uwezo wake wa kifedha, gari zake alikuwa akipanda mkewe na watoto yeye alikuwa akipanda mpaka sehemu kuanzia hapo hupanda daladala mpaka kazini.
Lakini nilipofika kazini kwake na mzigo alionipa ulibadiliwazo la kutumia ndagu. Niliamini kama si ya haramu nami lazima nijiunge naye ili niyabadili maisha yangu ambayo muda wote yalikuwa tegemezi kwa kumtegemea rafiki yangu. Nilisubiri muda ufike nipate jibu la fumbo langu.
***
Siku zote jioni kabla ya kuingia kazini tulikuwa tunakaa pamoja mpaka saa mbili usiku ndipo huondoka kwenda kazini na mimi kurudi nyumbani. Muda huo huwa tunazungumza mengi huku tukipata vinywaji vikali japo sikuwa mnywaji kama Somati lakini nami nilikuwa mwanachama.
Toka mambo ya Somati kuwa mazuri alikuwa akinywa pombe kali, lakini jibu la unywa pombe kali nililipata ilitokana na kazi yake ambayo kama una moyo mdogo huwezi kuifanya. Kwangu siku moja nilichanganyikiwa mpaka kuota mchana bila kunywa pombe unaweza kutoka mbio.
Lakini siku ile tulipokutana nilikuwa nataka kujua kule mochwari anafanya biashara gani iliyokuwa ikimuingizia kipato kikubwa kiasi kile.Pia nilitaka kujua kipi kilichomvutakufanya kazi ngumu kama ile ambayo kwa mtu kama yeye mpaka kuikubali.
Kwa kweli nilivyokuwa nikimfahamu Somati na kazi niliyomuona anaifanya haikuwa rahisi kukubali mara moja. Lakini aliamini siku ile ningepata majibu ya maswali yasiyo na jibu yaliyouzunguka ubongo wangu. Kama kawaida tulikutana sehemu yetu lakini siku hiyo tulikaa meza ya pembeni tofauti na tuliyoizoea.
Kama kawaida tuliagiza vinywaji vyetu kwa mimi kuagiza bia na mwenzangu kuagiza konyagi kubwa.
Kila mmoja alimimina kinywaji chake kwenye glasi na kunywa taratibu, lakini Somati alikunywa glasi nzima kwa mtindo wa tarumbeta kisha alirudisha glasi tupu juu ya meza na alitikisa kichwa kuonesha imefika sehemu yake huku mishipa ya kichwa ikimsimama na macho kugeuka rangi.
Alifuta mdomo kwa kiganja cha mkono na kuniangalia kwa macho makali kitu kilichonitisha na kunifanya nimuulize.
“Vipi, mbona hivyo?”
“Mmh! Imefika kwenyewe, unajua rafiki yangu kila siku nakueleza kazi anayoifanya mwanadamu mwenzako wewe usikushinde. Mwanzo nilikuwa na mawazo kama yako lakini nilikutana na mtu mmoja aliyenibadili akili yangu na kuwa na mtazamo mwingine kabisa ambao nataka na wewe kuanzia leo ubadili mtazamo wa mawazo yako na kuhamia dunia ya upambanaji.
“Najua uwezo wangu wa kipesa umekushangaza kwa vile nimelipuka kama bomu, pia leo alfajiri kuna kitu umekiona ambacho najua kimekuchanganya sana?”
“Ni kweli, unajua mpaka sijui pale kuna biashara gani yenye kukuingia fedha nyingi kiasi kile pia uliwezaje kuipata lkazi kama ile na nini kilikusukuma kuifanya kazi ile?”
Kabla ya kujibu Somati alicheka kidogo na kupuga funda la konyagi bila kuitia kwenye glasi na kusema:
“Kwanza ningependa kukueleza mwanadamu tumeumbwa na moyo wa uoga ambao umekuwa siku zote ukiturudisha nyuma katika kutafuta mafanikio. Lakini amini siku zote mwanadamu akiondoa woga mafanikio huwa usoni mwake. Kwa kweli wakati nikiwa nafanya kazi ya ulinzi nilikuwa nakutana na watu wengi.
“Baada ya matatizo ya kikazi na kukaa benchi, nashukuru rafiki yangu hukunitupa ndiyo maana leo nipo pamoja na wewe sitakuacha katika hali yoyote kwa vile nafahamu umuhimu wako kwangu.Si wewe tu wapo watu niliowasaidia wakati nikiwakazini kabla ya kusimamishwa.
“Nakumbuka nilikutana na jamaa yangu mmoja Titonilikuwa nikifanya naye kazi siku za nyuma ambaye naye alifukuzwa kama sisi. Baada ya kufukuzwa hakuacha kutupitia washkaji zake pale alipokuwa hana kitu nasi tulimtoa kiaina. Baada ya muda alipotea ghafla, hatukujua amekwenda wapi.
Baada ya miaka miwili kukatika wakati huo nipo benchi, siku moja jirani yangu kulikuwa na msiba, mimi nilikuwa mmoja wa watu tuliofuata mwili wa marehemu hospitali. Tulipofika chumba cha kuhifadhia maiti nilishtukakumkuta rafiki yangu Timo akiwa ndiye mhudumu wa chumba cha maiti.
Kilichonishangaza alikuwa mtu mwenye afya nzuri na kitambi juu, aliponiona alishtuka na kunishangaa nilivyokuwa kwani nilipoteza haiba ya zamani niliyokuwa nayo wakati nina kazi nilipungua na kuwa kama mgonjwa. Baada kutupatia mwili wa marehemu tuliyemfuata aliniita pembeni na kuniuliza kulikoni au naumwa.
Sikumficha nilimweleza kila kitu kilichonitokea kama kilichomkuta yeye, alinionea huruma na kunipa pole. Aliniuliza kama bado nipo nilipokuwa nakaa zamani nilimweleza bado nipo pale ila nilikuwa nina mpango wa kukirudisha chumba kimoja baada ya mambo kuwa magumu kila kukicha.
Bila kutegemea alinieleza nimsubiri, alikwenda ndani na kutoka na bahasha ya kaki aliyonipa na kunieleza akitoka kazini atakuja tuzungumze.Niliipokea bila kujua kuna nini japo mawazo yangu yalinipelekea labda kuna pesa. Tuliuchukua mwili wa marehemu na kuupeleka msibani kwa ajili ya maandalizi ya mazishi jioni ya siku ile.
Kwa vile tulikuwa tunazika jioni nilirudi nyumbani mara moja huku nikiwa na shauku kujua kwenye bahasha kuna nini.Nilipoingia ndani niliifungua bahasha, nilishtuka kukuta kuna shilingi laki mbili taslimu. Huwezi kuamini nami nilishtuka kama wewe kwani mtu kunipa laki mbili kipindi kile tena afya yake ilikuwa nzuri na kitambi juu tofauti na pale tulipokuwa pamoja kazini.
Nilimpa mke wangu pesa ya kula kisha nilirudi msibani huku nikiwa na hamu ya kuonana na rafiki yangu. Muda mwingi nilikuwa mtu wa mawazo juu ya hali ya rafiki yangu Timo pia kufanya kazi yenye kutisha kama ile ya kuhudumia maiti. Mwanzo hata mimi nilikuwa naogopa maiti pengine kushinda hata wewe.
Lakini nilibadilishwa mawazo na kuiona kazi ya mochwari ni kazi kama kazi nyingine na maiti wanahitaji kuhudumiwa na wanadamu na si malaika japo ilikuwa vigumu, lakini maneno ya ujasiri niliyopewa yaliondoa woga moyoni mwamngu na leo nina maisha mazuri kama unayoyaona.
Basi nilikuwa msibani lakini mawazo yote kwa rafiki yangu,” rafiki yangu Somati aliendelea kunieleza sababu zilizomwingiza kwenye kazi ya hatari kama ile wakati mimi nilikuwa najua yeye ni mlinzi.
“ Basi rafiki yangu, majira ya saa moja na nusu usiku Tito alifika nyumbani, nilimpokea na hakuwa mgeni nyumbani kwani alipokuwa na shemeji yako naye alimshangaa jinsi alivyokuwa kwani alikuwa na afya nzuri yenye kuonesha maisha mazuri. Kwa hali aliyokuja naye Tito ilionesha maisha hayana fomula.
Baada ya muda aliomba tusogee pembeni kwa mazungumzo, tulikwenda kwenye grosary iliyokuwa jirani.
Tulitafuta meza ya pembeni ambayo ilikuwa imejitenga na nyingine.
Tuliagiza vinywaji mwenzangu aliagiza konyagi mimi niliagiza bia, baada ya ukimya mfupi huku tukiendelea kunywa, Tito aliniita jina langu.
“Somati.”
“Naam.”
“Kwanza pole kwa matatizo.”
“Asante, ni sehemu ya maisha ya mwanadamu.”
“Ni kweli, lazima nami nirudishe shukurani zangu kwenu, waswahili wanasema kipande cha muhogo wakati wa njaa si sawa na biriani wakati umeshiba.Kidogo mlichonisaidia wakati nikiwa na shida si sawa na nilichokupa leo. Nina imani ulishtuka kupotea kwangu ghafla?”
“Ni kweli, wazo langu nilijua labda umepata kazi na upo bize ndicho tulichokuwa tukiomba wote siku moja mwenzetu uwe na maisha mazuri.”
“Ni kweli, lakini amini usiamini nilijiona nimegeuka ombaomba hivyo nikaona kama nawasumbua pili hata mimi niliona kama hadhi yangu inapungua. Nikaona kuna umuhimu wa kurudi kijiji. Kuna siku niliwaomba fedha kuwa mke wangu anaumwa, ile pesa mliyonipa ndiyo niliyofanya nauri ya kurudi kijijini mimi na familia yangu.
“Kwa kweli maisha ya kijijini yalikuwa magumu sana hasa nikizingatia niliisha zoea mjini. Lakini sikuwa na jinsi zaidi ya kujipanga upya ili nirudi mjini na kuiacha familia yangu kijijini ili nije peke yangu.
Maisha ya kijiji ilikuwa kila kukicha afadhali ya jana, lakini sikuwa na jinsi kwani hata pesa ya nauli ilikuwa tatizo.
“Siku moja nilikutana na mzee mmoja jirani yetu aliyekuwa akiishi mjini, alishangaa kuniona nipo kijijini wakati tulishawahi kukutana mjini.
Hali aliyonikutana nayo ilikuwa ikisikitisha nlikuwa nimebakia mfupa na ngozi.Aliniuliza nina mpango gani na maisha yangu.
“Nilimweleza nikipata fedha ningerudi mjini kwani kuendelea kuwa kijijini ni kupoteza dira ya maisha.
Yule mzee alisema anaweza kunipa nauli lakini mjini nitafanya kazi gani? Nilimweleza yoyote nikifika mjini sitachagua kwa muda ule. Basi alinieleza kuwa kuna nafasi moja ya kazi kama nikiweza nitaondoka naye siku ya pili. Kwa kweli kauli ile ilikuwa faraja kubwa moyoni mwangu.
“Nilimshukuru yule mzee kwa kuwona kama Mungu wa duniani japosikujua ni kazi gani nakwenda kuifanya. Kutokana na muonekano wake niliamini kazi yake ni nzuri, baada ya makubaliano niliagana na familia yangu kuwa nimepata kazi mjini.Familia yangu ilifurahi na kuwaeleza baada ya hali kutulia ningewafuata.
“Siku ya pili niliondoka na mzee Kubo hadi mjini ambako tuliwasilia majira ya saa mbili usiku na kufikia kwake. Alikuwa na nyumba kubwa lakini hakuwa na mke ila alikuwa na msichana wa kazi na watoto wake watatu ambao walikuwa wakubwa mmoja alikuwa ameolewa na wadogo walikuwa chuo.
Siku ya pili mzee Kubo aliondoka asubuhi kwenda kazini na kuniacha na msichana wa kazi na kurudi usiku majira ya saa tatu usiku.Baada ya chakula tulikaa nje ya nyumba peke yetu, yule mzee alikuwa mvutaji mzuri wa bangi alivuta kwanza kama misokoto miwili kisha tulipata muda wa kuzungumza.
Alianza kuonesha furaha usoni mwake kitu kilichongeza matumaini moyoni mwangu, kisha aliniita jina langu.
“Tito.”
“Naam.”
“Mambo yamekwenda vizuri kazi utaanza kesho.”
“Asante mzee wangu Mungu atakulipia kwa kila akifanyacho,” nilitamani kumlamba miguu.
“Najua kazi yenyewe itakushtua, nataka uyaweke moyoni haya nitakayo kwambia, chochote anachokiweza kukifanya mwanadamu mwenzako wewe kisikushinde hasa ukiwa mtoto wa kiume.
Ni kosa kubwa kuchagua kazi kwa kuyaogopa macho ya watu au kuamini ya watu fulani.”
Nilijiuliza ni kazi gani hiyo ambayo ilinitisha ambayo ilianza kutangulizwa taadhali.
“Ndiyo nimekuelewa, ni kazi gani hiyo?”
“Ni kazi ninayoifanya mimi na ndiyo iliyonipa maisha haya.”
“Sawa mzee, ni kazi gani mbona unanitisha?” Nilijikuta nikiingia wasiwasi huenda ni kazi ya ujambazi ambayo sikuwa radhi kuifanya japo wenzangu wanaiweza.
“Mimi ni mhudumu wa mochwari.” Timo alishtuka.
“Eti umesemaa!” nilimsikia lakini sikumwelewa.
“Mimi ndiye mhudumu mkuu wa chumba cha maiti.”
“Sasa mimi nimekuja kufanya kazi gani?”
“Kazi ninayoifanya mimi ndiyo utakayoifanya wewe.”
“Mzee, yaani mimi niwe mhudumu wa maiti?”
“Ndiyo.”
“Mzee kwa nini hukuniambia toka nyumbani nisingekuja huku.”
“Nilijua ningekueleza mapema usingekuja, lakini haya ndiyo maisha unatakiwa kujitoa na kupambana. Kilicho mbele yako ni wasiwasi wa moyo, lakini ile ni kazi kama kazi nyingine nakuhakikishia ukiizoea hutaiacha.”
“Nisiiache kwa sababu gani?” Timo alimshangaa mzee Kubo.
“Mshahara wake kwanza ni mkubwa, pia una malupulupu kutoka kwa watu wanaofuata marehemu wao. Wengine wapo wanaotaka maiti wao kuoshwa lazima watakupa pesa, kijiwe kikichanganya kuna siku unatoka na la laki mbili mpaka tatu.
Kila siku pesa ya chini kutoka nayo tofauti na mshahara elfu ishirini umekosa nini?”
“Mzee, ile kazi ni ngumu yataka moyo wa chuma mtu kukaa na kiume kisicho na uhai yataka moyo.”
“Najua ni wasiwasi umekutawala lakini nakuhakikishia kabla ya kukukabidhi kazi peke yako tutakuwa pamoja nitakufundisha taratibu utaielewa na kuiona ya kawaida tu.”
“Mmh! Sijui kama nitaiweza,” nilijikuta kwenye mtihani mzito maisha mwangu.
“Narudia kazi anayoiweza mwenzako wewe isikushinde.”
“Ni kweli lazini kazi ya mochwari mmh! Hapana.”
“Mawazo, hata mimi siku ya kwanza nilikuwa kama wewe, haya maneno aliyo yasema Timo ndiyo niliyo mwambia mwanzo aliponiomba niifanye kazi ile na kuachana na kazi yangu ya ulinzi.Niliona kama ni maneno tu ya kwenye kanga lakini baada kukomaa nilithibirisha kauli yangu,” Somati alisema na kuendelea kunipa mkasa wa rafiki yake Timo.
Basi rafiki yangu Somati aliendelea kunieleza jinsi rafiki yake Timo alivyoweza kuingia kwenye kazi ya uhudumu wa chumba cha maiti:
“Basi rafiki yangu Timo aliendelea kunielezea mkasa wake na kusema: Mzee Kubo aliweza kunishawishi na siku ya pili nilikwenda kazini huku nikiwa mtu niliyejaa aibu na woga.
Aibu ilikuwa kwa watu kuniona nafanya kazi ya mochwari, woga wa kukaa na maiti. Siku ile nilifanya kazi kama msaidizi, kazi kubwa aliifanya mzee Kubo kama kuweka maiti kwenye droo na kumsaidia kuzipanga.