KAZI YA MZUNGU 26
MTUNZI
😀AVID NGOCHO SAMSON
Usiku ule ule, Molio aliondoka kwenye apartment ya Masu akarejea kwa Issa. Asubuhi alimfuata Masu akiwa kamwandalia stafutahi maridhawa kabisa.
'Karibu kifungua kinywa Shem'
'Asante sana shem, kuhusu jana…'
'Hakuna kilichotokea shem. Natumaini ulipata wasaa wa kupunguza uzito wa mawazo. Nambie, una mpango gani sasa?' Molio aliuliza. Masu akabaki na sintofahamu. Huyu mwanamke alikuwa fumbo. Alivyokuwa jana na anavyoonekana leo, utadhani ni watu wawili tofauti. Duku duku likamkaba moyoni. Haiwezi kuishia hivi. Sharti ajue kinagaubaga nini hasa kilimaanishwa kwa wao kufanya lile tendo. Je, mwanamke huyo alimpenda? Kama hakumpenda, mbona akajitoa vile kwake? Maswali hayo na mengineyo yakamkereketa moyoni.
'Shem, kuhusu jana…' Masu akataka kujua undani wa kile kilichojiri kati yao.
'Shemejii, nimekwambia hakuna kilichotokea…'
'Mbona…'
'Jamani we mwanaume, unataka nini kwani?'
'Nataka kujua ni nini kile tulichofanya.'
'Ok, let's say I was curious, is that enough? (Sawa, tuseme nilikuwa nataka kujua tu vile inaweza kuwa, umeridhika?')
'Ni kusema….'
'Ni kusema, kama unanitaka tena usisite kuniambia, itakuwa siri yetu. Na najua unataka nikwambie nilijisikiaje, nilifurahi mno' Molio akatamka tena, safari hii, akionesha aibu nyingi.
'Njoo Molio' Masu akamvuta mkono Molio. Molio akamsogelea na kukaa pajani mwake.
‘Asante sana! Najua unajali sana. Lakini, najihisi hatia sana kwa kile tulichofanya…'
'Mhh, hapana' Molio akaweka kidole mshazari na midomo ya Masu. Akamzuia asizidi kuongea.
'Hakuna cha hatia. Hakuna makosa, kwa sababu hakuna kilichotokea. Ambia akili yako hivyo, sawa. Iambie hakuna hatia wala makosa, hakuna kilichotokea.' Molio akambusu tena Masu kwa kushitukiza na kusimama. Akaangalia saa yake ya mkononi. Saa kumi na moja na nusu.
'Natoka shem, nawahi kazini.'
'Ah shem, unaniachaje hivi bwana'
'Baadaye!' Molio akaaga na kutoka.
***
Salalah airport. Molio alikuwa na bango lenye majina 'Anastela Kilapi'. Zaidi ya picha iliyokuwa kwenye simu yake, hakuwahi kumuona msichana huyo aliyekuwa anaenda kumpokea. Hiyo haikuwa shida kwake. Ilikiwa ni kazi ambayo ameizoea. Kupokea wageni ambao ENTRY Ilikuwa inawaingiza kazini. Siku ya kwanza wangepokelewa na kufikia kwenye hotel yenye hadhi kubwa. Baada ya siku mbili tatu, wangehamishiwa katika moja ya jengo kubwa kabisa ndani ya kiwanda cha usafishaji mafuta ya kula. Humo ndimo walikofikia watu hao, ukiacha wale waliokuwa wakeze Kisiki. Jengo hilo lilikuwa mfano wa bweni, kulikuwa na vitanda, huduma ya bafu na choo, bwalo la chakula na maabara! Huduma za salon pia wangezipata huko huko.
Mara nyingi wasichana walioletwa kwenye jengo hilo, ni wale ambao walikuwa tayari kutafuta maisha nchi za arabuni na Ulaya baada ya kusota nchini mwao. Lakini si wote, ENTRY ilikuwa na mfumo wa kuwapata. Kigezo kikubwa kilichozingatiwa ni urembo, umri, halafu siha njema. Walitumia mitandao ya kijamii kutoa matangazo yao, katika nchi husika. Matangazo yenyewe hayakuonesha kazi hizo zilikuwa nje ya nchi zao, ilionekana kama kazi hizo zilipatikana ndani ya nchi. Warembo walipoenda kwenye usahili, hapo watu wa ENTRY walikagua vigezo vyao. Urembo, Siha na umri. Hawakuchukua wasichana wa zaidi ya miaka 25.
Warembo hawa walipofuzu vigezo, ndipo walipoambiwa kazi ipo Oman, Saudi Arabia, Zanzibar, Dubai, Marekani au Ufaransa n.k. Genge la ENTRY lilijikita kwenye nchi hizo. Waliandaliwa Visa na passport ya kusafiria. Walipofika kwenye nchi husika, vitu hivyo vilibaki kuwa mali ya genge hilo. ENTRY, hawakutumia jina hilo, walikuwa na makampuni tanzu ambayo yaliendesha biashara halali. Hayo ndiyo yaliyotumika kuwaajiri warembo hao.
Molio aliendelea kumsubiri mgeni wake. Mara akatokeza msichana mrembo, mrembo hasaa. Picha aliyokuwa nayo kwenye simu yake, haikumtendea haki mrembo huyo. Molio akasikitika. Huyu naye alikuwa ameteuliwa kuingia kwenye genge la ENTRY. Akamhurumia. Alipomuona Molio, Anastela Kilapi akatoa tabasamu la furaha. Mara nyingi ilitokea hivyo. Walikuja wakiwa na furaha. Wakadumu na furaha hizo kwa miezi miwili au mitatu, walipokuwa wanaandaliwa kwa kazi. Tabu ilianza baada ya miezi hiyo.
Miezi mitatu ya maandalizi, wasichana wale wakifurahia maisha, walirembwa wakarembeka watumike kama chambo cha kuvutia wengi kwenye mitandao ya kijamii. Hasa hasa Instagram. Walikuwa wanatupia picha nzuri nzuri wakiwa kwenye mahoteli ya kitalii na vivazi vya kikahaba, wakapata like nyingi na comments kibao. Wakila bata. Walionekana kwenye maeneo ya starehe. Walikula kwenye migahawa ya nyota tano, waliendesha magari ya kifahari, Ferrari, Bentley, Range, BMW nk. Walitalii dunia wapendavyo. Halafu. Uliwadia muda wa kulipia starehe hizo. Kazi rasmi ndani ya ENTRY ilianza. Kulikuwa na vitengo mbalimbali. Walipewa ruksa ya kuchagua. Isipokuwa chaguo moja tu, halikuwepo. Kujitoa. Molio alimwangalia Anastela Kilapi akitoa tabasamu, akajiuliza mrembo huyo angeangukia kitengo gani. Kusafirisha dawa za kulevya au kuigiza video za ngono? Akamhurumia. Shida ya ENTRY, haikujali. Walipofika umri wa miaka 26, wakiwa wametumikishwa na kujichokea, wakiwa hawana mvuto tena, ENTRY iliwatelekeza mitaani. Wengi hawakupona. Madawa ya kulevya waliyovutishwa, kuchomwa mwilini, yaliwafanya mateja. Waliopona waliishia jela baada ya kukutwa na madawa, wengi walikufa kwa arosto.
'Karibu sana Anastela Kilapi. Karibu Oman.'
Anastela akatoa tabasamu na kujibu.
'Asante sana dada.' sauti yake nzuri, haiba yake upole. Molio akamsikitikia zaidi.
'Oman kuzuri sana.' Anastela aliongezea.
'Kwa kweli ni kuzuri aisee. Nimeambiwa tu nikufuate asubuhi hii, vipi umepata kazi gani huku?'
'Oh, kumbe wewe si mhusika wa kampuni?'
'Hapana, mimi ni kama bodaboda kule bongo, huwa napigiwa simu na kuelezwa kuna mgeni anaitwa fulani anaingia muda fulani, nenda kampokee umlete ofisini. Hivyo yaani.'
'Oh sawa, nimeitiwa kazi ya mapokezi international hotel.'
'Hongera sana. Nasikia wanalipa vizuri sana hao wahindi.' Molio akadadisi, alikuwa anamchimba tu alimradi, ukweli wote alikuwa nao.
'Ndio bado sijafika nikajua zaidi. Nitafahamu zaidi huko huko dada..!'
'Mariamu, naitwa Mariamu.' Molio akamweleza Anastela Kilapi
'Ndiyo da Mariamu, nadhani nikishaanza ndio nitajua mbivu na mbichi.'
'Sawa. Kwa leo utafikia huko hotelini, international hotel, nadhani wenyeji wako watakupata hapo hapo.'
'Asante sana dada Mariamu.'
'Usijali, umesomea mambo ya Hotel?'
'Ah, hapana, niliona tangazo Facebook, na kwa vile nimeshamaliza kidato cha sita nikawa sina kazi, wazee wangu wenyewe fedha hawana za kuniendeleza, basi nikaona nichangamkie fursa. Nilipoenda nikaambiwa watanifundisha kwa mwezi mmoja na nitaweza kazi. Kigezo kikubwa walichosema kinanibeba ni mwonekano. Kwamba kazi zingine wanachozingatia ni uzuri, afya, halafu mafunzo na kazi vinafuatia.'
'Uzuri wenyewe dada umebarikiwa, sipati picha unavyosumbuliwa na vidume! Lakini, unawafahamu vizuri watu wenyewe? Maana siku hizi dunia imebadilika mdogo wangu. Watu wanaweza kukueleza uzuri wako ni mtaji halafu ukajikuta wanakupa kazi, sawa, kwenye mahoteli lakini ikawa ya kuburudisha wanaume.'
'Hilo nalo neno da Mariamu, sikuliwaza kabisaa. Ila unajua nini? Kama kuna tahadhari zinachukuliwa na kazi ikawa ina maslahi, ni bora kuliko kukaa mtaani huna kitu, na wakati mwingine unajikuta unachukuliwa na wahuni ili tu upate pesa walau ya lunch.'
'Ukiwa na mtazamo wa hivyo basi utafanikiwa. Maana heri kuingia miguu yote ndani kuliko kuingiza mmoja na mmoja ukasalia nje. Unaweza kujikuta unachanika msamba, kwa maana ndani unavutwa na nje nako unavutwa haha'
'Hahahaha, na kweli da Mariamu. We mwenzangu una bahati ushajiajiri. Sasa sie, ah wacha tu nijaribu. Maana kusema kweli da Mariamu kuja huku mie naona kama cheo kimepanda. Nilikuwa sina ishu ya maana na maisha yalikuwa yameanza kunikejeli.'
'Sawa basi Anastela, mimi nakutakia kila la heri mdogo wangu.'
'Asante dada.'
Walikuwa tayari wanaliona jengo la Hotel ya international mbele yao. Geti lilifunguliwa na Molio' akaliingiza gari ndani. Akaelekea mapokezi na kumkabidhi mgeni kwa wahusika. Akaagana na Anastela Kilapi akarudi zake kwenye apartment za Jawhareit Al Kheir.
***
Ilikuwa imesalia wiki Masu kuanza kazi ya Mzungu Steve Curl. Akaona heri awahi kurudi ili apate siku mbili walao za kumsalimia mama yake kijijini Malonje kabla ya kuingia kazini rasmi. Alipokea na kutafakari kwa kina, aliona heri kukubaliana na ushauri aliopewa na Yara. Aache mtoto azaliwe, akikua kiasi cha kutosha, atamtafuta na kumweleza ukweli. Aliyaona mazingira anayoishi Mwamvita, yalikuwa si mabaya. Na kama aliona penzi la Kisiki ni bora zaidi au kama alizuzuka na utajiri wa mzee huyo, vyovyote vile alivyoamua, aliona heri kumwacha huru. Afanye anachotaka. Akaamua kwa ajili ya mtoto wao, amwache huru mwanamke huyo. Hata kama aliamua hilo kwa ajili yake, aliona heri iwe hivyo hadi pale atakapojifungua mtoto, akakua na hapo sasa angerudi kuwachukua. Wakiwa wazima. Kama hata baadaye ya hapo Mwamvita angeonekana kumng’ang’ania mzee Kisiki. Angemwacha jumla. Hayo ndio maamuzi aliyokuwa ameamua kuchukua. Wakati Molio' anarejea, tayari alikwisha amua kuwa anarejea Zanzibar kesho yake.
'Shemeji huyoo!' Molio alimwita Masu.
'Nambie shemeji. Mbona mapema sana, nilijua kazini mnatoka saa za jioni?'
'Nimeomba ruhusa kwa ajili yako. Nataka nishinde na wewe kutwa yote.'
'Haha, sawa shem, Mie sina pingamizi hataa. Ila leo natakiwa kuwa na tiketi mkononi, kesho narejea zangu Zanzibar'
‘Ooh, Masu unaondoka kesho? Jamani sasa itakuwaje?'
‘Itakuwaje nini Molio?'
‘Masu nakupenda sana!'
‘Molio, pliz, mmekuwa wakarimu sana wewe na mumeo. Nisingependa kuonekana nisiyekuwa na shukrani. Ukisema hivyo wataka nisemeje mimi?'
‘Sema kilicho moyoni mwako. Sema unanipenda.'
‘Halafu nikishasema hivyo?'
‘Nitakuwa wako daima!
‘Shida shem, una utani mwingi hadi kwenye mambo siriazi. Mosi, hujanipenda bali umenitamani. Pili, Mie bado nina mpango na Mwamvita.'
'Lakini Mwamvita ni mke wa mtu Masu!'
'Kama ambavyo wewe pia ni mke wa mtu Molio.'
'Hapana, sisi ni boyfriend na girlfriend. Uhusiano wetu unaweza kuisha muda wowote. Lakini pia nikutoe wasiwasi Masu, sijasema nataka unioe mara moja. Nataka ujue napatikana ukinihitaji. Nataka uwe wangu daima, lakini sikuzuii kuoa, na sijasema namwacha Issa. Nawapenda wote wawili. Nampenda sana Issa, na nakupenda sana wewe. Nataka nibaki na Issa na vile vile niwe na wewe. Sitakusumbua. Wala sitaharibu mahusiano yako mengine. Lakini nitakuhitaji na itakuwa inakuwa siri daima.'
Masu alianza kuona tatizo. Huyu mwanamke ni wa aina gani? Haoni hata aibu kusema hayo anayosema. Akili yake ikamtuma kumwepuka kabisa. Lakini macho yake na mwili wake vilikuwa dhaifu mbele ya mrembo huyo. Toka aliporuhusu mwili wake kukutana na Molio, Ilikuwa kama amenasa mtegoni. Mwili wake ulikuwa kama umewekewa sumaku ya kuvutika kwa Molio.