Mogambi
JF-Expert Member
- May 25, 2012
- 213
- 357
- Thread starter
- #121
KAZI YA MZUNGU 35
DAVID NGOCHO SAMSON
0629077792
Agent Li baada ya kuitia mkononi briefcase ya marehemu Dkt Wu, alijua nini cha kufanya. Aliwasiliana na mkuu wake wa kazi. Mkurugenzi wa shirika la ujasusi la China MSS. MSS ilikuwa na idara iliyohusika na tafiti kama za Dkt Wu. Hivyo agent Li alielekezwa kwenda kituoni mapema ili chanjo ianze kuzalishwa.
Siku mbili baadaye tiba ya Dkt Wu ilifanyiwa majaribio kwa wagonjwa kumi ambao walikuwa wanachungulia kaburi. Maajabu. Wagonjwa wale walipona ndani ya siku mbili.
MSS walijua hili lilipaswa kuwa siri, na ndivyo ambavyo sasa ugonjwa huo ulivyozidi kudhibitiwa nchini humo. Wakati ambao huko Marekani idadi ya vifo ikifikia hadi 500 kwa siku, kwa upande wa pili, China ilikuwa imepata ufumbuzi wa tatizo, lakini kwa kiburi cha Marekani na uhasama baina ya mataifa hayo makubwa, tiba hiyo ilibaki kuwa siri China.
Jimbo la Wuhan ambalo kwa miezi miwili sasa lilikuwa kwenye lockdown, sasa watu waliruhusiwa kwenda makazini kuendelea na shughuli zao za kiuchumi. Marekani ndio kwanza walikuwa wanaanza lockdown huku idadi kubwa ya Raia wakiwa na sintofahamu. Vilio vyao vikiwa dhidi ya serikali yao kuingia kwenye vita ya kibayolojia na China. Propaganda za wajuaji mitandaoni zikiwaaminisha raia wengi kwamba kirusi kilichotengenezwa na mmarekani sasa kimeboreshwa na mchina na kurudishwa tena Marekani, wamarekani wakiwa hawajui jinsi ya kukikabili.
Masu na mwenzake Yusuf walipoingia China walikuta taratibu zimebadilishwa. Hali ilikuwa shwari kwa sehemu kubwa na kama ni machungu ya misiba, watu walikwishaomboleza na machozi kukauka. Walihitaji kuimarisha uchumi wao. Siku za karantini zilipoisha, Masu na Yusuf walianza kazi yao rasmi.
Walijitambulisha kama ujumbe wa SRI kwenye taasisi ya CRC. Kulikuwa na Mkurugenzi mpya wa CRC baada ya Dkt Futodo kupotea bila taarifa, uchunguzi ukionesha alishiriki kwenye njama ya usaliti kwa kutaka kuiingiza ACVV mikononi mwa maharamia wa Earth Vision 2050. Dkt Wang Chung aliyechukua nafasi ya Futodo aliwakaribisha na kuwajulisha kuwa alifahamu nia njema ya SRI na kwamba walikuwa wafuatiliaji wa kazi wa kampuni hiyo hasa mafanikio ya ile programu yake maalum ya mama na mtoto. Dkt Wang Chung hakusita kuwajulisha kuwa, kwa mujibu wa uchunguzi wao, watoto na mama zao waliopata huduma ya mama na mtoto kutoka SRI nchini humo hawakushambuliwa kabisa na SARS covid 2. Hivyo, walikuwa tayari kushirikishana uzoefu wao na hata kuendelea na mazungumzo ya mauziano ya ile formula kwa mfumo wa kusajiliwa leseni chini ya CRC.
Hizo zilikuwa habari njema sana kwa Masu na Yusuf na SRI kwa ujumla. Zaidi ya hayo Masu na Yusuf walijifunza namna gani shujaa Dkt Wu alivyojitoa maisha kutetea uhai wa dunia. Alikuwa shujaa kwa hakika. Nchi ya China ilimpa heshima ya kipekee Dkt Wu, kwa kutengeneza sanamu kubwa kabisa ya ukumbusho wake, iwe kumbukumbu kwa vizazi vijavyo. Masu na Yusuf sasa walibaini uhusika wa Earth Vision 2050 na gonjwa hilo pamoja na agenda yao ya kuokoa dunia kwa kuangamiza watu.
Masu alifanya mawasiliano na tajiri Steve Curl na kumjulisha yaliyojiri. Steve Curl akiwa mwenye furaha sana akaomba kushiriki kwenye kikao ambacho Masu angesaini mkataba wa mauziano ya ACVV kwa niaba ya SRI. Steve alishiriki kwa njia ya video conference na aliwashukuru sana CRC kwa kuona umuhimu wa kushirikiana katika mapambano dhidi ya SARS covid 2. Dkt Wang Chung hakusita pia kumshukuru Steve kwa juhudi zake ambazo zilichangia kuokoa mamilioni ya mama na mtoto nchini humo. Akaongezea kusema kwamba alijua kuwa hata nchi yake mwenyewe ilimpiga vita lakini sasa alikuwa ni shujaa wa dunia.
***
Majasusi wa FSB waliingia Zanzibar jioni ya saa kumi na moja. Hawakupokelewa na Yaraslav Yvanovitch kwa kuwa alikuwa anauguza maumivu ya risasi, hata hivyo, alikuwa amewafanyia reservation kwenye Hotel aliyokuwa kafikia hapo awali. Hivyo, majasusi hao walipokelewa na gari aina ya Noah ya Hotel husika na kupelekwa Hotelini. Majasusi hawa wakiongozwa na Mikhail Vahdeem, walikuja kwa kazi, hivyo, hawakuhitaji kupoteza muda, walihitaji taarifa muhimu za kuwezesha kumtia mikononi mwao kiongozi wa ENTRY kusudi wajue ilipo chanjo ambayo ilisemekana kuibwa na genge hilo. Yara aliwapa taarifa muhimu. Silaha na maandalizi muhimu pia alikuwa amewaandalia. Alikuwa anafahamu yalipo makazi ya mzee Kisiki kwa Zanzibar na Oman. Aliwachorea ramani. Kitu ambacho kingewakwamisha ingekuwa ulinzi na uwezo wa genge hilo kwa ujumla. Hapo ndipo walipomhitaji yule mateka wao.
Yara aliondoka na majasusi wenzake akawapeleka mahali alikomficha mateka. Walidhani ingekuwa rahisi, lakini haikuwa hivyo. Walimkuta jamaa keshakufa. Alijiua kwa kidonge cha sumu ambacho ilivyoonekana, watu wa ENTRY walikuwa na namna ya kuvihifadhi vidonge hivyo kinywani bila madhara hadi pale ambapo wangeamua kuvitumia kwa kusudi hilo la kujiondoa uhai wao wenyewe. Inaonekana mtu huyo alipozinduka usingizini, akajikuta kafungwa vema kwa kudu kwenye kiti, aliona kuepuka fedheha kwa genge lake basi heri ajitoe uhai.
Kwa namna moja au nyingine, majasusi wa FSB walikuwa wamerudi nyuma hatua moja. Iliwafaa kujipanga upya. Bila hivyo wangeingia kitanzini kwa chaguo lao.
Taarifa za mauaji ya watu makini wa ENTRY, ziliwasha taa ya alamu kwa genge hilo. Haraka sana, wakajua wako vitani na sasa walipaswa kufanya chini juu kuhakikisha ngome yao inabaki imara. Mara moja walianza kulinda maeneo yao. Hapo tena brigedia mstaafu Halfani Nassor ama muite Kisiki, aliamua kuajiri uzoefu wake vitani. Alisambaza macho kila pembe ili kusudi awaone adui wanapokaribia ngome yake.
Majasusi wa FSB walipoingia uwanja wa ndege Kisauni, macho ya Kisiki yaliwaona, yakawa yanawafuatilia kila hatua. Hata pale walipoenda mafichoni kwa mateka wao, macho ya Kisiki yaliongozana nao. Walipoondoka eneo lile, macho ya Kisiki yakaona maiti ya mtu wa genge lao ENTRY likathibitisha hali hiyo kuwa ni tangazo la Vita.
Hawakufika mbali. FSB hawakufika mbali, walikutana na genge la ENTRY ana kwa ana. Haikuwa kuviziana tena. Ilikuwa ni vita katika mtindo wa zamani za zamani, vita za mapanga, mishale na marungu, vita ya ana kwa ana. Mashambulizi dhidi ya majasusi wa FSB yakaanzishwa. Mmoja akadondoka chini, maiti. Majibizano ya risasi yakakolea. Katika harakati hizo, Yara hakufua dafu. Alianguka na kupoteza maisha katika uwanja wa mapambano. Alikufa kishujaa akiwa kazini, hivyo ndivyo alivyoamini. Yalikuwa mashambulizi ya kushitukizwa, mashambulizi ya kulipiza kisasi. Mikhail Vahdeem alipatwa na risasi ya begani, hata hivyo alimudu kuingia kwenye gari na kusepa. Watu wake huku nyuma walisalia wakipigania uhai wao wakati kiongozi wao akiwaacha uwanja wa Vita bila neno.
Hawakuchua muda, ENTRY wakiwa uwanja wa nyumbani walikuwa na uzoefu zaidi, wakiwa wavamizi pia walikuwa na nafasi kubwa ya ushindi. Kikosi cha FSB kiliangamia mkononi mwa ENTRY.
Mikhail Vahdeem alipoamua kuondoka uwanja wa mapambano, alikuwa amekokotoa kwamba wasingeweza kupona. Hata hivyo, alikusudia kuweka alama ya FSB kwenye kundi hilo, hata kama wangekufa wote. Kwa kutumia ramani aliyochorewa na Yaraslav Yvanovitch, aliliongoza gari kwenda yalipo makazi ya Kisiki. Alivalia koti refu baada ya kukifunga kidonda chake cha risasi begani ili kuzuia damu kutoka.
Mzee Kisiki alikuwa anapokea taarifa ya operesheni jinsi ilivyofanikiwa, wakati walinzi getini wakimruhusu mgeni kuingia ndani ya jumba lake. Aliposhitukia kuwa mgeni huyu hakuwa mgeni wa kawaida, Kisiki alikuwa amechelewa tayari. Risasi ilipenya upande wa kushoto wa kifua chake. Akaanguka chini. Walinzi wanaposhangaa nini kimetokea nao wakala shaba na kuanguka. Mikhail akausukuma pembeni uliokuwa mwili wa mtata Halfan Nassor, halafu akaketi kwenye kiti alichokuwa amekalia mzee huyo.
Milio ya risasi iliyosikika nje iliwafanya wakeze Kisiki wajifungie ndani ya vyumba vyao kwa uoga. Mikhail Vahdeem aliendelea kutulia, akisubiri vijana wa Kisiki waliopoteza watu wake warejee. Silaha za Kisiki na walinzi wake zilikuwa mkononi mwake.
Yule kijana aliyekuwa anazungumza na mzee Kisiki kwenye simu, alishangaa ghafla mzee huyo anasita kuzungumza na kutoa sauti ya maumivu ya 'Aaah!' Akawashitua wenzake warudi kambini. Kulikuwa na dalili kuwa huko kwa mzee Kisiki, mambo si mambo.
Waliporejea na kufika hapo kwa bosi, walikuta geti liko wazi. Wakajua mambo yamekwishaharibika na mzee atakuwa kachukuliwa mateka maana hakukuonekana mtu. Wakaingia kizembe sana mle ndani ili kutathmini madhara yaliyotokeza.
Yalikuwa ni makosa makubwa sana. Mikhail Vahdeem alikuwa analenga risasi zake kwenye macho tu. Kikosi kizima kikalala chini. Wafu. Bwana huyo akaondoka zake na kuishilia mitaani. Kesho yake, Mikhail Vahdeem alikuwa angani akirejea Korea kaskazini. Huku nyuma, vyombo vya habari Zanzibar, bara na vile vya kimataifa, vilikuwa vinaripoti mauaji ya kutisha yaliyopoteza takribani watu 22 kule kwenye ghofu alikofichwa mateka wa Yara na nyumbani kwa mzee Kisiki. Ajabu kubwa ikionekana ilikuwa ni vita ya magenge mawili ya uhalifu. Genge la Kisiki na genge la warusi ambao hawakujulikana ni wakina nani.
***
Wakati risasi zinarindima nyumbani kwa Kisiki, Halfan Nassor, Sheikh Abuubakr aliyekuwa kahifadhiwa katika moja ya chumba cha ardhini ndani ya kasri la mzee Kisiki alisikia hizo purukushani. Hofu ikamjaa tele. Hata baada ya kelele zile kuzima, Sheikh Abuubakr aliyekuwa amechanyikiwa kwa zile kelele, akawa yeye sasa ni zamu yake kupiga kelele. Aliendelea kupiga kelele kwa sauti kubwa.
Wakeze mzee Kisiki ambao sasa walikuwa wametokeza nje baada ya kelele zile za risasi kupotea, walikuwa wanahojiwa na askari upelelezi. Wanawake hao walishitushwa na kelele za Sheikh Abuubakr. Hali hiyo, ikamshitua hata yule afisa upelelezi. Akalazimika kufuatilia ni nini kilikuwa kinaendelea. Bwana huyo mwenye mustachi mithili ya mtangulizi wa ukoloni, mpelelezi Carl Peters wa kutokea Ujerumani, alitembea kwa kunyata na kurukaruka kama alivyokuwa akifanya mchekeshaji wa zamani hizo za wazee wetu, Charlie Chaplin. Mwendo huo, haukuwaacha salama wakeze Kisiki, wakiwa katika majonzi ya kuondokewa na mume wao katili, waliweza kupata kicheko cha kuwasahaulisha huzuni yao, japo kwa muda mfupi.
Chumba alichokuwamo Sheikh Abuubakr kilikuwa upande wa nyuma wa jengo hili, na kulikuwa na ngazi maridadi kabisa za kushukia huko. Mpelelezi huyu mwenye mbwembwe za kila namna aliziteremka ngazi hizo kwa staili ya aina yake. Kuna wakati ungemuona anajongea kama nyoka juu ya marumaru, mara ungemuona akiruka kichura na hata kuruka sarakasi kwa ule mtindo wa somasoti. Kwa hakika, alijua kuifurahia kazi yake. Hatimaye aliufikia mlango wa chumba kile. Kulikuwa na kufuli kubwa kwa nje. Askari huyo shupavu, alijaribu kulitikisa kufuli lile kwa vidole vyake na kulipapasa, kisha alitega sikio lake kwenye kufuli hilo kama kuna mtu alokuwa anamnong'oneza kutokea upande wa pili wa mlango huu. Mara tena alishuhudiwa akikitikisa kichwa chake kama anayeafiki jambo. Hapo tena aliwageukia wakeze Kisiki na majirani ambao sasa walikuwa wanaongezeka katika eneo la tukio, halafu akapiga hatua kuwafuata. Wakamsikia kamanda huyo akitamka kwa yakini; 'Mnaweza kuwa na funguo za mlango huu?' Kauli hiyo, aliitoa akiwa usoni kabandika sura ya kazi. Lakini, ilivyo ajabu, kadamnasi ile iliangua kicheko kikubwa kwa furaha badala ya kulijibu swali lake. Hata hivyo, mmoja wa wakeze mzee Kisiki, bila shaka mkubwa miongoni mwa wakeze Kisiki, akapiga hatua moja ikifuatiwa na ya pili, haraka haraka, akatembea na kuingia ndani ya kasri la mzee Kisiki, aliporejea alikuwa na lundo la funguo za kila aina. Akampokeza afisa yule lundo hilo la funguo. Katika kuonesha umahiri wake, afisa huyu mweredi, alichagua funguo moja tu na kurudisha zile funguo zingine kwa yule mama. Akaufuata mlango ule na kuutia ufunguo ule kwenye tundu. Hola! Ufunguo ule haukufungua. Kitendo hicho nacho kikaamsha kichekesho miongoni mwa mashuhuda wa harakati zake. Jamaa huyo, ama kwa hakika alikuwa kituko. Baada ya kadamnasi hii kucheka, yeye aliwageukia na kuwatazama. Wote wakawa kimya, halafu akafanya kitendo cha kushangaza. Aliangua kicheko kikubwa akiwacheka watazamaji wake. 'Hahahahah!' Watu wote wakashikwa na mshangao. Bila shaka wakihisi yule jamaa ni hamnazo. Lakini wakiwa bado wamezubaishwa na hali ile, askari huyu mwenye mbwembwe, akaugeukia mlango ule na halafu, akatumbukiza tena ule ufunguo kwenye tundu la kufuli, alipowageukia, alikuwa na funguo pamoja na kufuli mkononi.
Kadamnasi ile sasa ilikuwa inacheka huku ikimpongeza kwa makofi. Mlango ulipofunguliwa, Sheikh Abuubakr alitokeza nje akiwa amekonda na mdhaifu sana. Ama kwa hakika, majuto ni mjukuu. Kauli hii ya wahenga, ilifanya kujirudia rudia kichwani mwa Sheikh Abuubakr kama ilivyo kwa wimbo ulio kwenye chati ya kumi bora unaosikika mara kwa mara kwenye vyombo vya habari na burudani.
***
Baada ya formula ya ACVV kuingia mikononi mwa SRI, Steve Curl alifungua maabara katika kanda maalumu 16 kote duniani. Dawa hizo zikasambaa kote duniani. Watu wakawa wanapona, SARS covid 2 ilikuwa ukingoni kupotea. Hadi kufikia mwezi August 2022, gonjwa hilo lilitokomezwa kabisa. Lakini Steve Curl bado aliendelea kugawa dawa na chanjo kwa kila mtu ambaye hakuwa ameipata bado. Alijua genge la ENTRY, na marafiki zao Earth Vision 2050 wangejipanga upya kuachia virus hivyo miaka 10 baadaye. Kama kila mtu angepata chanjo hiyo, hapo baadaye gonjwa hilo lisingepata kujidai.
Operesheni hii ilipaswa kwenda kimya kimya ili kuepuka kuwapa sababu wabaya hao waliodhani wana nia nzuri na dunia lakini wakikusudia mabaya kwa wenye kuishi ndani ya dunia. Hivyo, si Marekani wala Ulaya waliojua kuwa gonjwa hilo liliteketezwa kwenye mataifa yao na SRI. Viongozi wa mataifa hayo kama ilivyo kawaida ya wanasiasa, walijivika vazi la ushujaa na kutangazia dunia jinsi ambavyo wamepambana hadi kuutokomeza ugonjwa huo.
ITAENDELEA...