KAZI YA MZUNGU 20
Alipoingia tu kwenye apartment ya Issa, Molio alimkumbatia kwa furaha kubwa. Akambusu shavuni, shingoni, puani, machoni, kwenye paji la uso, kote kote akiacha mdomo pekee kwenye so wa Issa. Halafu bila kusema neno, Molio Huku akijipigisha mluzi wa furaha, akaingia jioni kuandaa chakula cha jioni. Issa alibaki anamtazama tu, huku akifurahi. Alijua chanzo cha furaha ya mpenziwe, na kulijua hilo kulimpa faraja moyoni mwake. Issa akaonelea vema kujitazamia zake runinga ajue kinachoendelea duniani.
Katika taarifa ya habari iliyorushwa na kituo kutoka Tanzania, kulikuwa na taarifa za kukamatwa kwa mtu aliyejulikana kwa jina la Sheikh Abuubakr Ramadhan huko kisiwani Zanzibar. Taarifa zilisema Sheikh Abuubakr alikamatwa kwa kile kilichoitwa kushirikiana na wahuni na kusababisha Askari wa jeshi la polisi kudhurika walipokuwa wanapambana na wahuni hao. Sheikh huyo hakuwataja wahuni hao Ni Nani kwa madai hakuwafahamu. Jeshi la polisi kupitia msemaji wake liliapa kuwasaka wahuni hao, huku likitangaza donge nono kwa mtu ambaye angejitokeza kutoa taarifa za mwonekano wao.
Habari hiyo ikavuta makini ya Issa Musa. Jina la Sheikh Abuubakr halikuwa geni kwenye maskio yake. Wapi alipata kulisikia? Ilipompambazukia, akajua jina Hilo Ni jina la baba mzazi wa Mwamvita. Yule binti aliyesafiri naye. Akapiga hatua na kuingia jikoni, alikokuwa Molio, akiandaa chakula kwa ajili yao.
'Dear, umeisikia habari toka Zanzibar? Inasemekana Sheikh Abuubakr Yuko mikononi mwa polisi. Baba yake Mwamvita.'
'Wee. Kulikoni?'
'Inasemekana ameshirikiana na wahuni kuwashushia kipigo polisi, haha!'
'Sheikh kawapiga polisi? Haiwezekani. Ila nahisi kitu kimoja tu, Sheikh Abuubakr alikuwa anashirikiana na polisi dhidi ya wahuni, wahuni wamewashinda nguvu, Sasa wanamgeuka mtu wao.'
'Mh, hao wahuni lengo lao Nini, na Kama wahuni TU wanaweza kuwatandika polisi, Ni dhahiri polisi ya bongo Sasa inazingua.'
'Hahaha, Kuna wahuni watata wewe!'
'Hatari'
Ukweli Ni kwamba, polisi walimweka ndani Sheikh Abuubakr kufuatia kipigo walichopewa, kwa sababu ya kizushi. Hilo likitokana na kukiri kwake kuwa alijua bintiye Yuko wapi na Yuko na Nani na bado akataka kuwabambikiza makosa vijana wale waliowashushia kipigo. Hata majirani wale waliokuwepo kwenye tukio waliposikia dau likitangazwa, walipoenda kituoni kuwaelezea Masu na Yusuf ili wajipatie Hilo dau, waliishia kupigwa biti na polisi wakae kimya. Hakukuwa na pesa ya kugawa.
Chakula kilipoiva, Molio alipakua na kuweka mezani. Wakala wakatosheka. Hapo Sasa, ule mshawasha wa Molio ukaanza upya.
'Enhee babe, yamenifika hapa,niambie habari njema tafadhali.' Molio akatamka akionesha shingoni yalikomfika hayo aliyosema.
'Yaraslav Yuko Zanzibar, Safari hotel. Yupo huko kwa likizo. Nimemgusia suala lako kwa kifupi na nikapendekeza aje kumalizia likizo yake hapa Oman. Amesema hakuna shida. Kwa hiyo mahabuba, kaa ukijua tutamudu kulipatia jibu suala lako mapema sana.'
'Waoo mpenzi. Nakupenda sana Issa wangu. You're the best. Mmmmwaah!' Molio akaonesha furaha yake, halafu akaongezea.
'Leo nimekutana na Mwamvita. Nimesungumza naye. Amenipatia namba za bwanake. Utazihitaji?'
'Ndiyo mpenzi, namuonea Sana huruma huyo binti hasa kwa vile Ni mdogo halafu Tena mjamzito, kwa Kweli ni ukatili wa kijinsia. Sijapenda kabisa utaratibu huo wa entry. Kwa nini wanateka watoto wadogo, mabinti wadogo hivyo?'
'Mh, entry biashara zao Ni zile haramu. Watoto unaosema wewe,kwa entry Ni watu wazima. Tena shukuru Mwamvita kaangukia mikononi mwa Halfani Nassor. Kwa maana kwamba anakuwa mke wake, Tena kwa kuridhia kwa wazazi wake vinginevyo angepelekwa kwenye makasino.'
'Dah, hatari Sana. Hivo wataka kunambia wazazi wake wanalifahamu hili?'
'Ndiyo, Sema hawajui Kama huyo bwana mwenyewe Ni mtu hatari. Wenyewe wanajua Ni mtu mwenyewe pesa na hivyo Kwao wanaona mtoto wao atakuwa na maisha mazuri. Mzazi gani hapendi mwanae awe na maisha Bora? Na, iko hivi, huyo boyfriend wake,Hana maisha ya kumpa binti yao, ndio maana wamefanya Kama kumtorosha, inaelekea binti hakutaka kusikia la adhana Wala mnadi swala, alikuwa miguu juu, kichwa chini jinsi alivyoangukia kwenye penzi la huyo mwanaume wake'
'Mh, napata picha sasa. Sasa, huyo bwana yake tukimjulisha atafanya Nini Kama Hali yake pangu pakavu Tia mchuzi?'
'Kusema Kweli hakuna Cha maana atakachofanya, ila siye tutakuwa tumetimiza ahadi yetu kwa Mwamvita. Lakini, nahisi tutakuwa tumemsaidia huyo Jamaa kukabili maumivu yake kiume, kwa Sasa bila shaka Yuko kwenye sintofahamu.' 'Hebu nipatie hizo namba za Masu.' Molio akamtajia, Issa akazihifadhi kwenye rununu yake.
'Kwa hiyo dear, Yaraslav Huku anaingia lini?' 'Keshokutwa!'
'Anhaa, oh Asante Sana mpenzi. Hatimaye, hatimaye nakuwa huru.'
'Kabisa mpenzi, hebu ngoja nimpigie Masu.' Issa akamweleza Molio. Akaweka code ya simu ya Tanzania, akapiga namba ya Masu aliyopewa.
Simu ikaita Kidogo ikapokelewa kwa sauti thabiti.
'Masuke Masuke, Nani mwenzangu?'
'Naitwa Issa Musa, mwenyeji wa huko Zanzibar, kwa Sasa Niko Dubai. Nilikutana na binti mjamzito akanipa namba yako nikupigie. Alisema nikikupa taarifa hii utaelewa maanake Nini, anaitwa Mwamvita. Nafahamu alipofikia, ingawa nahisi alipo SI mahali pazuri kwake. Anatia huruma Sana.'
'What?' Masu akahamaki. Lakini akajiambia, hakuna haja ya kupaniki, akatulizana halafu akatamka.
'Ok braza,Asante kwa taarifa ndugu Issa. Kesho naingia huko Oman. Vipi tunaweza kuonana nikifika huko? Kwa bahati mbaya Sana sio mwenyeji kabisa huko. Itakuwa safari yangu ya kwanza. Itanifaa Sana nikipata mwenyeji.' Masu akaongea kwa ushawishi. Issa Musa akashituka. 'Au tumekosea namba?' akajiuliza, lugha na jibu la Masu, halikuyumkinika vipi awe huyo maskini aloelezewa habari zake. Huyo alisikika Kama mtu tajiri, mwenye kila dalili ya uweredi wa Mambo tofauti na alivyodhania hapo awali alipokuwa akielezewa na Molio.
'Usijali juu ya kuonana. Kusema Kweli, kwa lolote utalohitaji, Wala usisite kunijulisha, ukitaka pia kampani yangu kwenye hiyo misheni, count me in (Hesabu kuwa nipo ndani)'
'Nashukuru Sana Kaka. Basi Kumbe nitahitaji mengi na Nina bahati kukupata wewe.'
'Pamoja sana.'
Aliposhusha simu yake chini, Issa Musa akamgeukia Molio na kumtazama kwa jicho la kutafuta majawabu!
'Nini?' Molio akamuuliza baada ya kuuona ule mtazamo.
'Una hakika Jamaa Ni hohe hahe?'
'Yeah, I mean, ndivyo nilivyoambiwa! Kwa Nini wauliza hivyo?'
'Ah, jinsi alivyozungumza, haelekei kuwa mtu duni kwa jinsi nilivyochukulia Maelezo yako, ukiongezea na kwamba Jamaa Kesho anaingia Salalah! Kama angekuwa msukuma mikokoteni tu, bila shaka Hilo lisingewezekana.'
'Mh, unanifanya na Mimi kufikiri aisee. The guy could be one of those government agents or worse one of the terrorists gang members.'( Jamaa asijekuwa Ni shushushu wa serikali au mbaya zaidi akawa miongoni mwa magenge ya kigaidi)
'Hahaha, I can't wait to meet the guy. Naanza kuona picha la hatari na msukuma kokoteni akiwa staring!'
'Unajua hiyo ina maana gani mpenzi?' Molio akauliza kwa unyonge.
'Ina maanisha Nini?' Issa akauliza Kama mbulula.
'Ina maana Kwamba naweza kuingia kwenye mpambano na huyo Jamaa. Nisingependa kuwa kwenye Vita hiyo. Maana kutoka moyoni mwangu, natamani huyo Masu ashinde, na hiyo ina maana nishindwe Mimi. Shida ya Vita, Ni kwamba, utaua au utauwa.!'
'Lakini mpenzi, wewe na Mimi tutakuwa zetu mbali. Usinambie unafikiria kuingia kwenye huo mpambano?'
'Unajua Sina namna Kama wataniamrisha kufanya hivyo. Yaani natamani Kweli huyo Yaraslav angekuwa keshaingia Huku tayari na kuniweka huru.!'
'Ok, nimekusoma. Cha kufanya, kwanza tumcheleweshe huyo Masu ili mishe zake zianze baada ya Yara kufanya muujiza wako. Hilo Nina hakika tunaliweza.'
***
Nzinyangwa akiwa ameambatana na bodyguard wake mpya. Huyu alikuwa raia wa Marekani, mwamerika mweusi, mwenye mafunzo ya juu ya kikomandoo. Kumuajiri mtu huyo kukitokana na lile tukio la kupoteza milioni mia moja hamsini kwa sababu aliyoiita 'ya kizembe'. Alikuwa amejifunza kigumu.
Hapa walikuwa kituo Cha polisi kufuatia ile taarifa ya polisi kuwa wahuni wawili walimudu kuwachakaza polisi wenye mafunzo. Taarifa ile, kwa Nzinyangwa haikuwa ya kupuuzwa hata Kidogo, la hasha, alikuwa na biashara kubwa ya kulinda. Biashara kubwa ya kutanua. Alikuwa na ndoto ya kuwa tajiri nambari moja Africa mashariki. Hao wahuni aliwahitaji kwenye genge lake.
'Ndio bwana Nzinyangwa, karibu sana.' Askari wa Zamu alimkaribisha. Hawa kina Nzinyangwa walikuwa Ni watu maarufu hapo kituoni. Walikuwa miongoni mwa VIP hasa kwa wale Askari potofu kwa maadili ya kazi yao. Nzinyangwa na matajiri wengine wengi walijua jinsi ya kudili na wanausalama ili kujihakikishia maslahi yao hayaguswi aslani. SI ajabu kuwa walikuwa na fungu maalum kwa ajili ya kulipa Askari hao.
'Asante Sana kamanda Shamte. Nimesikia Kuna wahuni walifanya kulitia doa jeshi la polisi. Ningependa kupata taarifa kamili kuhusu watu hao. Nataka nitumie watu wangu kuwapiga tafu Kidogo haha!' Nzinyangwa alizungumza na kumaliza kwa kicheko Cha kebehi. Angekuwa Ni Askari mwadilifu, bila shaka angeshitukia kicheko hicho, lakini pia, taarifa za kipolisi, huwa na mtiririko wake, huyu raia, Nzinyangwa, hakupaswa kuelezwa chochote kinachoendelea kwenye idara hiyo muhimu seuze kupendekeza kulisaidia jeshi Hilo? Mtu mmoja awezaje kulisaidia jeshi kazi yake? Mtu mwenyewe akiwa raia mhalifu ambaye genge lake lilihusishwa na vifo vya watu, kufilisi biashara halali, na kuwafanya wengine kupata stroke kutokana na madhila waliyowasababishia.
Lakini, Shamte na Askari wengi kituoni hapo walipokea masurufu kemkem kutoka kwa bwana huyo, Sasa akawa Kama mwajiri wao pia. Aliwatumia atakavyo. Angeweza kuwachukua wakamkamata mtu aliyedaiwa na Nzinyangwa, wakamsulubu, na hata kumnyang'anya Mali yake kwa maelekezo ya bwana huyo. Walichojali zaidi Ni ile habari ya masurufu na bakshishi zake za Mara kwa mara.
Shamte akajichekesha Kama punga,
'Hehehe sawa bosi. Ungependa nikupatie taarifa zao. Hehehe!'
'Ee, hili hapa faili lao, hehehe Nzinyangwa buana!'
Msaidizi wake akalichukua faili na kupitia Maelezo yaliyokuwamo.
Huyo Sheikh Abuubakr naweza kuonana naye?'
Ah hehe, kwa vile Ni wewe hehe, hatakiwi aonane na mtu.'
Nzinyangwa na bodyguard wake wakaingia lockup kuonana na Sheikh Abuubakr. Alipotaka kufuatana nao, Shamte akazuiwa.
'We endelea na majukumu hapo, Usijali!' Nzinyangwa akamuamrisha Shamte.
'Hehe sawa tu!'
Hawakuwa na muda wa kupoteza, walikuwa na maswali muhimu ya kujibiwa waende zao.
'Mzee Abuubakr, nimeelezwa kuwa Kuna wahuni ulishirikiana nao kuwapa kisago Hawa polisi. Nataka majina na anuani zao, hicho tu, Basi!' Nzinyangwa alimkoromea Sheikh.
'Mimi nishawaeleza polisi siwajui hao naoambiwa nimeshirikiana nao. Waulize watakuambia.'
'Najua hujawaambia pia. Lakini Mimi Ni Nzinyangwa, Mie sio polisi. Kama hutaki wawajue, Mie Sina shida na huo msimamo wako. Nachotaka Mimi, uniambie Mimi TU, Wala sitawaeleza hao, itakuwa Siri yetu Mimi na wewe.!'
Sikiliza bwana Nzinyangwa, Mimi hao watu siwafahamu. Hivi aliyepigwa ashindwe kuwatambua Mimi nayezushiwa Ndiyo niwatambue? Miujiza Basi!'
Nzinyangwa akamkonyeza bodyguard wake. Mzee Abuubakr hakutarajia hili. Alijikuta amepokea kibao kikali kwenye shavu la kushoto akaangukia upande wa kulia.
'Utatueleza ama utaanza ngonjera za karudi baba mmoja?' Nzinyangwa akamnong'oneza, Huku akilivuta sikio la kulia la Sheikh Abuubakr na kumsababishia maumivu makali.
Sheikh Abuubakr akajaribiwa awataje,lakini akalikumbuka jicho la onyo alilomzodoa nalo Masu. Ha! Hakutaka kurudia kosa Tena. Kama polisi waliwafahamu na kuamua iwe Siri, yeye Nani hata atoe Siri hiyo?. Sheikh Abuubakr akaamua liwalo na liwe, hatoi jina. Na hapo akapata Wazo la kuondokana na shuruba ya Nzinyangwa. Mzee huyo akapiga yowe kwa sauti Kali ya kuugulia maumivu.
'NAKUFAA!'
Nani alitaka uchunguzi wa kifo Cha mahabusu?, Shamte akatoka mbio kwenda kwenye chumba Cha lockup, mlangoni akapishana na Nzinyangwa na bodyguard wake. Ni Kama hawakumuona. Wakalifuata gari lao, gari la kifahari aina ya Range, wakaondoka hapo kituoni.
'Twende nyumbani kwa huyo Sheikh. Kwenye Maelezo pale wameandika anaishi Mwembe makumbi.' Nzinyangwa akamweleza bodyguard.
David Ngocho Samson