Simulizi: Kaburini ama Gerezani

Kudo

JF-Expert Member
Nov 2, 2017
1,809
6,081
KABURINI AMA GEREZANI!
NA; BAHATI MWAMBA
SIMU; 0658564341/0758573660.

1: KIKAO…

Ilikuwa ni ndani ya baa moja maarufu sana ndani ya jiji la Dar es laam, baa ambayo milango yake haikuwahi kufungwa, iwe ahsubuhi, mchana ama usiku, burudani ziliendelea kama kawaida. Kilichokuwa kikibadilika kwenye baa ile ni wahudumu ambao walipeana nafasi ya kuhudumu kila baada ya saa nane. Wahudumu hao walikuwa kwenye jinsia zote, yaani walikuwepo wahudumu wa kike na wa kiume na walikuwa katika mgawanyo wa majukumu, wapo ambao kazi yao ilikuwa ni kuhudumia chakula, wengine vinywaji vikali na laini, wengine walihusika na kuchoma nyama tu huku wengine kazi yao ilikuwa ni kuhakikisha meza zote zipo safi muda wote. Kama zilivyo baa zingine kuwa na meneja, meneja wa baa ile alikuwa ni mtu mzima karibu miaka hamsini na tano hadi sitini, lakini alikuwa ni aina ya wazee ambao hawajawahi kukubali umri unanafasi kwenye maisha, wao waliibua msemo wao kwamba umri ni namba na walihalalisha huo msemo ili wapate nafasi ya kuyarudi ya ujanani na vijana wadogo ama mabinti wadogo.

Meneja huyo ambae wafanyakazi wake waliamua kumpachika jina la Baba usinipite, alijikuta akilowea kwenye maisha ya anasa na kuiweka kazi kama pitio la kuharakisha anasa zake, kwa tabia yake hiyo alijikuta akilazimika kuwa nje ya kazi kwa saa nyingi zaidi, hapo ndipo alipopata wazo la kumwamini mmoja wa wafanyakazi wake, na turufu hiyo ikamuangukia kijana mtiifu ambae wenzake walimfahamu kwa jina la Gunga. Gunga halikuwa jina lake halisi na hakuna aliyewahi kulijua jina lake kwenye hayo mazingira yake ya kazi. Umri wake ulikuwa kwenye makadirio ya miaka ishirini na nane hadi thelathini.

Elimu yake ilikuwa ni elimu ya chuo kikuu na aliwahi kufanya kazi kwenye kampuni fulani wakati akingojea ajira, ajira hazikutoka na bahati mbaya kampuni aliyokuwa akiifanyia kazi ikatetereka kiuchumi na wafanyakazi wakapunguzwa na yeye akiwa mmoja wao. Kazi aliyoifanya kwa miaka mitatu ikaota mbawa na bahati mbaya zaidi wakati huo alikuwa ameshaoa, alimuoa mwanamke wake wa tangu balehe. Tangu asimamishwe kazi ilikuwa imekatika miaka miwili na miezi sita, ukiunganisha na ile miaka mitatu ya kazi na na ndoa, jumla ilikuwa miaka mitano na miezi sita.

Gunga kwenye ile baa alikuwa na zaidi ya miezi tisa, kazi yake ilikuwa ni kuhakikisha meza zote zinakuwa safi wakati wote na jioni alikuwa anapewa ujira wa shilingi elfu tatu hadi elfu tano kama posho ya kazi aliyoifanya. Kitendo cha meneja wake kumuamini na kumuongezea jukumu la kusimamia ile baa wakati akiwa hayupo, kwake ilikuwa ni furaha kubwa. Posho yake iliongezeka na kuwa elfu saba hadi elfu kumi na wakati mwingine hadi elfu kumi na tano. Saa za kazi nazo zikaongezeka na wakati mwingine alikesha na wakati mwingine alilazimika kutoka usiku mnene.

Licha ya kuwa msaidizi wa kuaminika wa meneja, lakini Gunga hakuwahi kuzidisha posho yake wala hakuwahi kutamani kujiongeza kwa kupiga pesa kwa namna yoyote, alikuwa mwaminifu haswaa kiasi hata chenji ya shilingi hamsini alihakikisha haibaki mfukoni mwake. Wafanyakazi walimpenda na wateja walimpenda, alipendwa na kila mtu hapo kazini kwake. Licha ya kuwa na nyota ya kupendwa lakini hakuna aliyewahi kujua anaishi wapi wala hakuna aliyewahi kujua anamke nyumbani, tena mke wa ndoa, yote tisa, kumi ni kwamba hakuwa akiifurahia ndoa yake, aliishi kwa karaha kubwa lakini licha ya karaha hizo, hakuwahi kuinua mdomo wake na kumtusi mke wake wala kumpiga, ijapokuwa, mke wake alikuwa akimtusi na kumkejeli sana. Kwa nini? Kwa sababu mke wake ndiye alikuwa kichwa cha familia ya watu wawili tu, hawakuwahi kupata mtoto na sababu siyo kama walikuwa wagonjwa, la hasha, sababu ni mwanamke hakuwa tayari kuzaa kwa sababu aliamini mume wake hawezi kumtunza mtoto.

Siku hiyo akiwa amekaa kwenye kaunta ya meneja huku macho yake yakitalii huku na huko kuhakikisha wahudumu wapo kwenye maeneo yao, kumbukumbu za maisha yake na mke wake zikamzonga, akatikisa kichwa kupambana nazo lakini hakufua dafu, zikambeba.

“Siwezi kuzaa na mwanaume ambae najua hawezi kununua nepi ya elfu moja.” Ilikuwa ni kauli chungu kutoka kwenye kinywa cha mke wa Gunga, tena haikuishia kuwa kauli tu bali na msonyo ulifuatia huku macho ya mke wake yakicheza kinyalinyali, kama haikutosha, mwanamke akajigeuza na kumsukuma mwanaume kwa guu lake la kulia, Gunda akaenda chini kitako kutoka sofani alipokuwa amekaa na mke wake.

“Lakini wewe ni mke wangu halali kabisa, kwa nini unanifanyia hivi? Kwa nini hutaki kuzaa na mimi ambae nimefunga ndoa na wewe?” Gunga alimuuliza mkewe huku akiinuka kutoka chini. Mwanamke akasimama na kushika kiuno, mishipa ya uso ikiwa imemsimama kama kiazi kitamu kilichopigwa na jua la saa saba mchana.

“Eti mke wako, ni lini umenipeleka saluni? Lini umekuja na nguo ya dukani, lini umewahi kununua hata mafuta ya kulembesha midomo yangu? Umewahi kununua vocha angalau nitume ujumbe mfupi?” Mwanamke alimkoromea huku akitikisa kalio moja kwa namna ya kusuta.

“Lakini vyote ulivipata wakati nina kazi, hata sasa sina kazi lakini nguo za Mwenge najitahidi kupitia ila huwa unazikataa, unataka niibe?” Gunga aliongea kinyonge.

“Ukiiba nitakuwa wa kwanza kukukamata na kukutia ndani, mwanaume pambana…. Au una hawara mahali fulani ambae unamjali? Ratiba zako zimebadilika siku hizi na sijui huwa usiku unatoka wapi na unakaidi amri yangu ya kukutaka urudi nyumbani kabla sijafika kutoka kazini.”

Gunga alitabasamu kidogo kisha akamtazama mke wake kwa sekunde kadhaa na kusema,..

“Unataka nichakarike na bado unataka niwahi kurudi nyumbani kama kondoo. Usijisahau ukahisi umeota ndevu na unaweza kunifanya lolote.” Alipiga hatua na kuelekea chumbani akiwa anasindikizwa na maneno ya kejeli na dhihaka kutoka kwa mke wake, hakujali, aliingia chumbani na kujitupa kitandani, mawazo yakambeba.

“Mh!” Gunga alijikuta akiguna peke yake huku akirejesha mawazo ndani ya eneo lake la kazi, akazungusha macho yake huku na huko na mwisho akaishia kuinua mkono wake wa kushoto na kutazama majira ya saa yake, ilikuwa inakaribia kutimia saa tano na dakika arobaini na tano usiku. Akashuka kwenye kiti na kuutazama mlango wa VIP, akafikiria kidogo kisha akainua mguu wake na kusogea karibu na mlango ule ambao kwa siku hiyo ulipambwa na kibao kilichokuwa kimeandikwa.. ‘CLOSED' ilimaanisha hakukutakiwa mtu kuingia huko na kwa siku hiyo wale wanaopenda kujikweza maeneo ya starehe, hawakuruhusiwa kabisa kwa madai kwamba, kulikuwa na matengenezo kidogo ndani ya ukumbi huo mdogo ndani ya baa hiyo maarufu jijini Dar es laam.

Gunga alifika hadi mlangoni na kisha akatoa ufunguo na kuingiza kwenye kitasa cha mlango, akazungusha na kabali za kitasa zikaachia kisha akausukuma mlango na kuingia ndani. Dakika tano zilikatika akiwa huko VIP, dakika ya sita akatokea mlangoni na kuuacha bila kuufunga, aliugesha.

Alirejea kwenye kiti cha meneja huku macho yake yakiwa kwenye mlango wa kuingilia ndani ya baa. Akili yake akaiweka hapo licha ya sekunde chache kulazimika kuzungusha kichwa huku na huko ili kuhakikisha kazi zinaendelea. Licha ya watu kuwa wengi na wengine kuinuka na kucheza, lakini jicho lake lilikuwa makini sana na mlango wa kuingilia na alikuwa akimuona kila aliyekuwa akiingia na kutoka. Gunga kuna jambo alikuwa analisubiri na alilitarajia kuanzia saa sita za usiku, muda ambao tarehe hubadilika.
 
a kujikweza maeneo ya starehe, hawakuruhusiwa kabisa kwa madai kwamba, kulikuwa na matengenezo kidogo ndani ya ukumbi huo mdogo ndani ya baa hiyo maarufu jijini Dar es laam.

Gunga alifika hadi mlangoni na kisha akatoa ufunguo na kuingiza kwenye kitasa cha mlango, akazungusha na kabali za kitasa zikaachia kisha akausukuma mlango na kuingia ndani. Dakika tano zilikatika akiwa huko VIP, dakika ya sita akatokea mlangoni na kuuacha bila kuufunga, aliugesha.

Alirejea kwenye kiti cha meneja huku macho yake yakiwa kwenye mlango wa kuingilia ndani ya baa. Akili yake akaiweka hapo licha ya sekunde chache kulazimika kuzungusha kichwa huku na huko ili kuhakikisha kazi zinaendelea. Licha ya watu kuwa wengi na wengine kuinuka na kucheza, lakini jicho lake lilikuwa makini sana na mlango wa kuingilia na alikuwa akimuona kila aliyekuwa akiingia na kutoka. Gunga kuna jambo alikuwa analisubiri na alilitarajia kuanzia saa sita za usiku, muda ambao tarehe hubadilika.

Saa sita na dakika tatu kile alichokuwa akikisubiri kikatokea, macho yake yalimuona jamaa mmoja akiingia kwa wasiwasi na kutojiamini. Gunga alitabasamu huku akichukua simu yake na kuanza kuandika ujumbe mfupi kisha akautuma. Sekunde chache baadae yule jamaa aliyekuwa akiingia alijipapasa mifuko yake na kutoka na simu, akafungua sehemu ya ujumbe mfupi na kuirejesha kisha akapiga hatua na kuelekea mlango wa VIP.
Gunga aliendelea kukaa palepale alipokuwa na bado macho yake yaliendelea kuwa mlangoni, aliendelea kuhesabu matumbo ya watu waliokuwa wakiingia na kusoma namba za visogo vya watu waliokuwa wakiondoka. Saa sita na dakika nane kuna mtu mwingine nae aliingia huku akiwa ni mwenye wasiwasi na kutojiamini, mtu yule nae alisimama mlangoni huku akihangaisha kichwa chake huku na huko, muda mfupi baadae alijipapasa mfukoni mwake na kutoa simu yake na kuitazama kidogo kisha akairejesha mfukoni na kupiga hatua na kuelekea ulipo mlango wa VIP.
Gunga hakuondoka kwenye kiti wala hakuondoa macho yake kwenye mlango wa kuingilia. Saa sita na dakika kumi na tatu alimuona mtu mwingine aliyemtegemea na kama ilivyokuwa kwa wengine, alimtumia ujumbe na yule mtu alielekea VIP. Saa sita na dakika kumi na nane mtu mwingine aliingia mlangoni kwa wasiwasi kama walivyokuwa wale waliotangulia, alijipapasa kidogo na kutoa simu yake na kusoma ujumbe na pasipo kusubiri alipiga hatua kuelekea ulipo mlango ulioandikwa VIP.

“Ikawe kheri!” Gunga alijinong'oneza huku akishuka kwenye kiti kirefu alichokuwa amekalia, akageuza shingo yake huku na huko kama anaetafuta kitu kisha akatabasamu na kumfuata mhudumu wa kike aliyekuwa akipokea pesa za biashara zote za pale baa.

“Mafundi wamekuja, simamia hapa kwa dakika kumi tu, ngoja nionane nao.” Alimwambia huku akimtupia tabasamu la amani, likapokelewa kama alivyolipeleka.

Gunga alipiga hatua taratibu kuelekea VIP, akausukuma mlango taratibu na kuingia ndani ambapo alikaribishwa na hewa safi kutoka kwenye kiyoyozi, utulivu mkubwa ulikuwa ni himaya halali ya sehemu ile maalumu. Kushoto mwa mlango kulikuwa na milango miwili ya vyoo, mlango mmoja ulikuwa maalumu kwa wanawake na mwingine wanaume. Gunga alitazama ule unaotumiwa na wanawake, akapiga hatua fupi na kuufikia kisha akauvuta na kupata nafasi ya kuingia. Kama vilivyo vyoo vingine vya maeneo ya kujidai, kulikuwa na sinki la kunawia na sinki la kumaliza haja zako ambapo pembeni ya sinki la kutiririsha salamu zako, kulikuwa na bomba nyembamba na ndefu ambayo ilikuwa maalumu kwa kutiririsha maji kwa wale wenye dharura za mwili mzima. Juu ya ile bomba kulikuwa na soksi nyeusi yenye ukubwa wa kutosha kichwa cha mtu mzima, Gunga aliichukua huku akitabasamu, akaivaa na kufunika kichwa chake chote na kubakiza macho na pua tu.

“Mafanikio ya kwanza ni kila mmoja kufuata masharti bila kukosea.” Alijisemea baada ya kukuta ilibaki soksi moja kati ya tano alizokuwa ameziweka pale saa chache zilizopita. Alipohakikisha kichwa chake na mwonekano wake hautaweza kutambulika, akavua shati aliyokuwa ameivaa na kubakiwa na fulana ya mikono mifupi kisha akasukuma mlango na kutoka chooni, akahakikisha korido zote za kuingilia kumbi za VIP zipo kimya na hakuna mtu, akashusha pumzi zake na kujiweka sawa kisha akatembea kuelekea kwenye ukumbi mdogo uliokuwa na uwezo wa kumiliki watu wasiozidi sita. Kwanza alisukuma mlango wa kuingilia na hakufanya jitihada zozote za kuingia, lengo lake alitaka watu waliokuwa mle ndani waweke matarajio kwa kiumbe aliyekuwa amesukuma mlango. Ikapita dakika moja ndipo akatanguliza mguu wake na kisha kiwiliwili chote kikaishia ndani, kwa uvivu akageuka na kuweka komeo la mlango kisha akageuka na kuwatazama watu wanne waliokuwa wamekaa kwa kuachiana mita moja, vichwa vyao wakiwa wamevifunika kwa soksi iliyoziba sehemu kubwa ya nyuso zao na kuwaachia macho na pua pekee.

“Nani aliyemsemesha mwenzake tangu mlipoingia hapa ndani?” Gunga aliwauliza wale mabwana wanne ambao walikuwa wamekodoa macho wasielewe kilichotakiwa kuendelea.

“mhmh!” Alikwangua koo huku akitikisa kichwa chake kama anaekubali jambo fulani kisha akarejea swali lake ambalo halikuwa limejibiwa na yeyote aliyekuwa mle ndani.

“Nani alijaribu kumsemesha mwenzake?”

Kimya! Hakuna aliyejibu wala kuweka ishara yoyote ile, zaidi waliendelea kuyakodoa macho yao kwa mtu aliyekuwa mbele yao, hawakumfahamu ijapokuwa sauti yake siyo ngeni kwenye masikio yao kwa sababu alikuwa akiwasiliana nao mara kadhaa kupitia namba zao za simu.

“Good!” Gunga alisema huku akijiweka sawa kisha akatupa jicho kwa kila mtu aliyekuwa mle ndani, aliporidhika akasema..

“Nafurahi kuona nyote hamna wasiwasi licha ya kwamba mpo sehemu ngeni ambayo hamjawahi kuingia na kizuri zaidi, mmeingia baa wakati ninyi nyote hamjawahi kulewa. Wale mabwana kwa mara ya kwanza tangu waingie pale ndani wakageuza vichwa vyao na kutazamana, lakini waliishia kuonana pua na macho tu.

“Mmekosea!” Gunga alifoka na kwa mara nyingine wale mabwana wakatazamana tena.

“Mnazidi kukosea!” Gunga akafoka zaidi huku akizungusha kichwa chake kutoka kwa mmoja kwenda kwa mwingine, aliona mshangao wa dhahiri nyusoni mwao lakini hakuwajali.

“Ujumbe wangu uliwaambia nini? Niliwaambia mkiwa hapa ndani msigeuze shingo zenu kutazamana. Kila mmoja atazame upande wake bila kuvunja sharti hilo.” Akanyamaza kidogo na kulainisha koo kwa mvumo wa mate kisha akaendelea..

“Mimi na ninyi sote ni masikini, mnajua kwa nini? Kwa sababu hatuzingatii kanuni za pesa na ili tuzingatie kanuni hizo ni lazima tuheshimu hizo kanuni. Ninyi mnavunja kanuni ndogo yenye maana kubwa kwetu, je, nilichowaitia hapa kitafanikiwa kama tunavunja kanuni nyepesi namna hii?”

Chumba kikabebwa na ukimya mkubwa macho yote yakiwa kwa Gunga na macho ya Gunga yakiwa kwa wageni wake. Hakuna aliesema wala kutikisika, nidhamu ikabeba mkondo.

“Good! Nimependa mlivyoonesha nidhamu kwangu licha ya kwamba hamnifahamu na hamfahamiani. Mafanikio yetu ya kwanza yapo kwenye nidhamu, nidhamu iwe ngao ya kila jambo.”Gunga alinyamaza kidogo kisha akaendelea..

“Nilitarajia kuwa na ugeni wa watu zaidi ya wanne, lakini ni wanne pekee mliofanikiwa kufika hapa. Hii ina maana mpo tayari kwa jambo litakalo kuja mbele yenu bila kujali matokeo yake ya baadae. Najua,..” Gunga alikohoa kidogo kisha akatupia macho upande wake wa kulia walipokuwa wamekaa jamaa wawili ambao vimo vyao vilikuwa sawa, urefu na ukubwa wa miili yao.

“Najua tukitoka hapa kila mmoja anakesi kwa mke wake huko nyumbani. Wengine naweza kuwa sina shaka nao kwa kuwa wanaweza kuhimili mihemko ya wake zao, shinda yangu ipo kwa huyu bwana hapa.” Alisema huku akinyoosha kidole kwa jamaa wa kwanza aliyekuwa kulia kwake, licha ya kufanya hivyo lakini wenzake hawakugeuza shingo zao kumtazama, kanuni ilizingatiwa.

“Huyu anapigwa na mke wake. Kwa hiyo kesi kubwa ipo kwa mwenzetu.”
Kauli yake hiyo ikaibua vicheko vya wale mabwana akiwemo aliyesemwa, kwa mara ya kwanza kila mmoja aliisikia sauti ya mwenzake. Dakika moja baadae utulivu ukarejea na Gunga akaendelea..

“Inaweza kuwa yafurahisha lakini haipendezi mwanaume kupigwa.. Lakini licha ya kuwa haipendezi, hata mimi napigwa na mke wangu..”

Kwa mara nyingine kicheko kikatamalaki na wakati huu wawili walijikuta wakijisahau na kugongeana mikono, lakini Gunga hakuwakemea, kwa nini? Kwa sababu alitaka wale watu watengeneze mahusiano, mahusiano mazuri ya kuelewana. Soga zake za wao kupigwa na wake zao hazikuwa za bahati mbaya, alikusudia kuweka kiungo cha mahusiano kupitia maisha yao halisi
 
“Huyu anapigwa na mke wake. Kwa hiyo kesi kubwa ipo kwa mwenzetu.”
Kauli yake hiyo ikaibua vicheko vya wale mabwana akiwemo aliyesemwa, kwa mara ya kwanza kila mmoja aliisikia sauti ya mwenzake. Dakika moja baadae utulivu ukarejea na Gunga akaendelea..

“Inaweza kuwa yafurahisha lakini haipendezi mwanaume kupigwa.. Lakini licha ya kuwa haipendezi, hata mimi napigwa na mke wangu..”

Kwa mara nyingine kicheko kikatamalaki na wakati huu wawili walijikuta wakijisahau na kugongeana mikono, lakini Gunga hakuwakemea, kwa nini? Kwa sababu alitaka wale watu watengeneze mahusiano, mahusiano mazuri ya kuelewana. Soga zake za wao kupigwa na wake zao hazikuwa za bahati mbaya, alikusudia kuweka kiungo cha mahusiano kupitia maisha yao halisi.

“Kila mmoja najua maisha yake na mke wake.” Alisema huku akigeuza shingo na kumtazama jamaa mwingine aliyekuwa kushoto kwake, akaendelea..

“Huyu yeye najua kapata nafasi ya kuja usiku huu kwa sababu mke wake hayupo ndani ya nyumba, ukimuuliza najua hajui alipo usiku huu na ahsubuhi akirejea, ndugu yetu huyu hana ubavu wa kumuuliza alipolala. Kwa nini? Kwa sababu kodi ya nyumba inalipwa na mke wake, chakula kinanunuliwa na mkewe, yeye ni mtafuta pesa ya kachumbari kwa kuwa ya unga huwa haitoshi.” Gunga aliweka kituo huku bado macho yake yakiwa juu ya paji la uso la yule bwana aliyekuwa upande wake wa kushoto.

“Maisha yako ni magumu kusimulika. Nguvu unazo lakini kazi hupati, kila unachogusa hakifanikiwi, marafiki huna kwa sababu wanahisi unanuksi na mikosi, kila wanapopata kazi na kukushirikisha huwa mnaishia kubaya na malipo hampati. Juzi niliona unaenda kwa sangoma aliyeweka tangazo kwenye nguzo za umeme barabarani. Pesa alikupa nani?”

“Mke wangu alinipa!” Jamaa alijibu huku akiinamisha uso wake chini, aibu ilimshika na alitamani yule mtu aliyekuwa akimsimulia aache lakini hakuweza kufanya hivyo, alishindwa kwa sababu hakujua lengo la yule bwana aliyewaita pale na kuwafunika sura zao kiasi walishindwa kufahamiana. Alichagua kusikiliza hadi mwisho.

“Mkeo anakupenda, lakini hawezi kuendelea kukupenda zaidi. Ngoja nikwibie siri kuhusu mkeo.. Wiki ijayo anahamia sehemu nyingine aliyopangishiwa na mwanaume wake. Najua kodi yenu inaisha wiki hii mwishoni, anakuachia msala wa kodi, hivyo jipange.” Gunga alitua mshale kifuani kwa yule bwana ambae wakati huo alikuwa akihema kama fuso lilozidiwa na uzito wa mchanga, mawazo dukiduki kichwani mwake.

Gunga alihamisha macho yake na kumtazama jamaa aliyekuwa kushoto kwake, nyuma ya yule anaetarajiwa kukimbiwa na mkewe.

“Nadhani ili tuelewane vema ni lazima tupeane majina.” Alisema huku akiwa bado amegandisha macho yake kwa yule jamaa ambae alikuwa na kimuhemuhe cha kutaka kusikia yaliyomhusu.

“Ni vema kila mmoja asimfahamu mwenzake kwa jina halisi na kabla sijaendelea ni vema nikagawa majina kwa kila mmoja aliyeko hapa.” Gunga alisema huku akitupia macho yake kwa kila mmoja kisha akainua mkono wake na kunyoosha kidole kuelekea upande wake wa kulia walipokuwa wamekaa jamaa wawili wanaorandana mwonekano.

“Wewe unaepigwa na mkeo jina lako utaitwa Tina na wewe wa nyuma yake utaitwa Zena.”
Jamaa wakageuka na kutazamana kwa mshangao hawakudhani kama katika majina yao mapya kungelijitokeza majina ya kike. Si wao pekee bali hata wenzao ambao nao bado walikuwa hawana majina mapya, walipigwa na mzubao kwa kuwa hawakuwa wametegemea majina ya namna ile. Licha ya mshangao kuwakumba washirika wake, haikuwa sababu ya Gunga kughairisha majina hayo na badala yake, akahitimisha kwa kuwapa majina waliokuwa wamesalia.

“Wewe unaetarajia kukimbiwa na mkeo utaitwa Tatu na huyo aliyenyuma yako, ataitwa Tano.” Gunga akanyamaza kidogo kisha akajikohoza na kuuliza…

“Kuna mwenye shaka? Swali? Maoni?”

Ukapita ukimya mfupi kabla Tano hajanyoosha mkono na kuruhusiwa kusema…

“Binafsi nimekubali kuitwa Tano, lakini nahitaji kujua mambo mawili.” Jamaa akanyamaza kidogo kisha akaendelea..

“Hatujajua jina lako licha ya kwamba umeshatupa yetu. Lakini kubwa zaidi ningependa kujua umetufahamu vipi kwa namna ya undani kiasi hicho?” Tano akanyamaza ikiwa na maana, hana cha ziada.

Gunga akacheka kidogo kisha akatumia sekunde thelathini kugeuza kichwa chake, kuwatizama wageni wake. Aliporidhika na alichokiona machoni mwao, akaamua kujibu alichoulizwa.

“Kabla sijajibu maswali ya bwana Tano, ningeomba kujua kama Tatu, Zena na Tina wamekubaliana na majina yao?”

Vichwa vya waliotajwa vilitikisika mara mbili kutoka juu kwenda chini na kutoka chini kwenda juu, walikubali.

“Good!” Gunga alisema huku akitikisa kichwa kabla ya macho yake kuyatupa kwa Tano ambae alikuwa na shauku ya kusikia maswali yake yakijibiwa.

“Nimechukua zaidi ya mwaka mmoja na miezi miwili kuwafahamu nyote, nawajua nje na ndani, najua maisha mliyonayo, najua wake zenu hadi michepuko yenu, vijiwe vyenu vya majungu na madili ya kuwapa pesa ya chai na siagi..” Alinyamaza kidogo na kulainisha koo lake kwa funda mbili za mate yake, akaendelea..

“Mfano wewe hapo najua ulikuwa mwizi mkubwa kabla ya kunusurika kuchomwa moto na wananchi wenye hasira zao, baada ya kunusurika huko ukaamua kubadili aina ya wizi, ukaanza kutengeneza pesa bandia na huko ukaishia kupelekwa gerezani kwa hukumu ya miaka miwili baada ya upande wa mashitaka kushindwa kuwa na vielelezo kamili vya kukutia na hatia ya uhujumu uchumi. Ulipotoka gerezani ukaishia mikononi mwa jimama ulilonalo, najua linakufanyisha kila aina ya kazi ikiwemo kuliuzia mkaa, kukusanya madeni ya vijora, kupeleka pesa za vikoba na wakati mwingine hadi sokoni unaenda na kikapu… Yote tisa, kumi ni kwamba huwa mara mojamoja unachezea mbata hasa ukichelewa mahali ulipoagizwa. Najua unafanya haya yote kwa sababu huna pa kukaa na huna uwezo wa kupanga chumba na hutaki kurudia kutengeneza pesa bandia.” Gunga akatua maelezo kumhusu Tano, lakini hakuishi hapo, akamalizia kujibu swali lingine..

“Nilichagua kuwafuatilia na maisha yenu kwa sababu nilichoka kuwaona masikini na kuteseka kwa wake zenu.. Hili nisijitoe, hata mimi nateseka sana. Sisi sote hapa tunapigwa na wake zetu lakini najua uwezo wa kuwabonda tupo nao, nguvu tunazo na uwezo tunao lakini tatizo ni kwamba, kuna mahali wametushikia na kutufanya tuwape umuhimu mkubwa sana kiasi kwamba, sauti yao ni mamlaka kwetu… Niliache hilo, Tano ulitaka kujua ni kwa nini sijajitambulisha kwenu.. Sijajitambulisha kwa sababu najua kila mmoja amenisevu kwa jina lake kwenye simu yake, lakini nawapa nafasi hapa ya kunichagulia jina ambalo nyote mtalitumia..”

Haraka Tano akanyoosha tena mkono, akaruhusiwa kusema..

“Binafsi nitakuita Sister, yaani wewe ni kama Dada wa Tina, Zena, Tatu na Tano..”

Vicheko vilitawala kwa zaidi ya sekunde arobaini kisha ukimya ukachukua nafasi yake.

“Zena!” Gunga alimuita jamaa aliyekuwa nyuma ya yule jamaa aliyekuwa amepewa jina la Tina. Jamaa akainua kichwa na kumtazama Gunga huku akili yake ikiwa tayari kusikia yanayomhusu kwa sababu, ni yeye pekee ambae hakuwa ameambiwa yanayomhusu.

“Umekubali niitwe Sister?”Gunga alimuuliza.

“Sioni sababu ya kubadili, hata mie nitakuita Sister..” Jamaa aliyepewa jina la Zena, akajibu huku akitisa kichwa kuhalalisha alichojibu.

“Sawa bwana Zena. Naomba nimalizie kwako ili wenzio nao wajue unayopitia ndani ya nyumba yako..” Gunga alisema huku akikaa sawa kwenye kiti na kumtazama Zena.

“Huyu mwenzetu yeye mke wake ni mganga wa kienyeji, pesa za uganga zinamlisha na kumvisha mwenzetu. Licha ya elimu aliyonayo lakini mkewe kashindwa kuroga apate kazi na badala yake, kamgeuza kuwa mchuma dawa na msisitiza masharti kwa wagonjwa. Mke wake huwa wakikosana anajifanya kupandisha maruhani na kuanza kumbonda Zena wetu, akishapigwa hutulizwa kwa kupewa vipande vya nyama za kuku wa dawa.” Gunga alinyamaza kidogo kupisha vicheko kutoka kwa Tano, Tina na Tatu ambao walikuwa hawajiwezi kwa vicheko. Walipotulia, aliendelea..

“Bwana Zena nikwambie ukweli, mkeo ni tapeli ila anatumia ujinga wa watu kujipatia kipato kidogo kinacholisha familia yako. Ukitaka uamini mkeo ni tapeli, kumbuka ile siku uliyomchomolea laki mbili na kumtumia mama yako kijijini, hakuwahi kumpata mwizi na hata alipoweka tego kuwatisha, bado halijakufanya chochote hadi leo. Lakini bado wewe ni tapeli na huwa unawatapeli wagonjwa wa mkeo” Gunga akanyamaza na kumtazama Zena ambae alikuwa kimya bila kusema neno.

“Tuachane na hayo, najua kila mmoja ameshafahamu kidogo kuhusu mwenzake, na sifa mbili tulizonazo wote hapa ni sifa mbili; sifa ya kwanza, sisi sote tunapigwa na wake zetu na sababu ni kwa kuwa hatuna makali ya kuwafanya watuheshimu. Sifa ya pili ni kwamba, sisi sote ni wezi kwa namna moja ama nyingine. Lakini kwa sasa naomba tukubaliane jambo moja..” Gunga alinyamaza kidogo na kuzungusha macho yake kwa wageni wake wote, alipoona usikivu ni mkubwa, akaendelea…

“Kuanzia sasa inatulazimu kuwa watulivu sana, tusijihusishe kwa namna yoyote ile na udokozi na kikubwa zaidi inatulazimu kuwa na siri kwa hili nitakalo washirikisha na ambalo limefanya niwaite hapa..” Alinyamaza na kumeza mate..

“Inatubidi tuweke nadhiri ya kutokuvujisha hili jambo popote pale hadi wakati utakapofika na baada ya wakati huo, kila mmoja ataenenda kivyake bila kujali uwepo wa mwenzake.. Lakini inabidi tukubaliane wote na endapo hata mmoja wetu akionesha mashaka, itabidi tuahirishe huu mpango na tutaachana bila kufahamiana. Jambo lenyewe ni wizi, wizi wa pesa kwenye moja ya benki hapa nchini..”
 
kivyake bila kujali uwepo wa mwenzake.. Lakini inabidi tukubaliane wote na endapo hata mmoja wetu akionesha mashaka, itabidi tuahirishe huu mpango na tutaachana bila kufahamiana. Jambo lenyewe ni wizi, wizi wa pesa kwenye moja ya benki hapa nchini..”

Wageni wa Gunga wakatazamana kwa mshangao, hakuna aliyetarajia kusikia jambo kama hilo, jambo ambalo kila mmoja alipojitathimini aliona hawezi kulifanya.

“Sister! Ukweli hadi sasa naona ugumu kushiriki jambo hilo, wizi benki unahitaji nguvu na umwagikaji damu na ikibidi kuua au kuuwawa, hata baada ya kufanikiwa kutoroka na pesa, bado tutaishi maisha ya kujificha na kukimbiakimbia kuwahofia maofisa wa polisi ambao watahitaji kujua ni kinanani waliohusika, mkono wa serikali ni mrefu sana, unakuna hadi mgongo na hatutakuwa na pa kujificha, lazima tutanaswa!.” Jamaa aliyepachikwa jina la Tina, aliongea kwa kuhamaki kidogo.

“Ninachojua wizi wa pesa kwenye sehemu inayolindwa kama benki, itahusisha matumizi ya silaha. Binafsi sijawahi kutumia silaha wala siijui kwa ukaribu inafafanaje ukiacha zile ninazoona kwenye sinema na wanazokuwa nazo maofisa wa polisi. Naona kuna ugumu hapo na siko tayari kuua kisa pesa, acha niendelee kupigwa na wife.” Tatu nae alijiweka mbali na hilo dili.

“Kama sitakuwa mmoja ya watu watakaojitokeza kuingia ndani ya benki, nipo tayari kushiriki lakini kama nami nitatakiwa kuwa mstari wa mbele, nitaomba nijiengue kwenye mpango huo.” Tano nae alijiweka mguu ndani, mguu nje.

“Hadi sasa naona ni jambo lisilowezekana, ugali wa nje ya gereza ni mtamu sana kuliko ugali wa kutikisa mabega gerezani, askari nyuma yako na bunduki mkononi.. Hapana!” Zena nae aliungana na wenzake.

Ukapita ukimya mfupi kila mmoja akingoja kusikia maamuzi ya mwisho kutoka kwa Gunga au sister kama wenzake walivyoamua kumuita. Gunga nae alikaa kimya kungoja kama atasikia maoni mengine kutoka kwa wageni wake. Alipoona ukimya unaendelea kutawala, akauvunja..

“Naona mmeamua kukimbia maili nyingi kuliko mimi niliyewaita hapa. Sijawambia tutaiba kwa upanga au bunduki, sijawaambia tutamwaga damu au jasho la mtu. Sijajua ninyi hayo mawazo mnayatoa wapi.” Alinyamaza kidogo kisha akaendelea..

“Halafu naona mnajifanya malaika.. Wote mnasema hamjawahi kuua, mnauhakika? Mnataka kunidanganya kirahisi namna hiyo? Mh! Ninyi nyote mmewahi kuua mkiwa kwenye harakati za kutafuta pesa. Hapa mtu pekee ambae hajawahi kuua ni mimi peke yangu.. Sikieni, nilipoawatafuta nilijua nakutana na watu wa aina gani, na sifa kubwa iliyonifanya nikawakusanya hapa na kuwashirikisha mpango huu ni kwa sababu najua mnavyovifua vya kutunza siri. Kama mliweza kutunza siri zenu za kuua watu kiasi hata wake zenu hawajui, hamwezi kushindwa kuficha siri ndogo ya wizi. Lakini naelewa mnachomaanisha, hamtaki kurudia kuua na hata mimi sitaki muue wala sitaki kushiriki mauaji kwa sababu, tukishiriki kuua ni rahisi kukamatwa na ni rahisi kuhukumiwa miaka mingi na tutakuwa useless hapa Duniani, sitaki tufike huko ninao mpango madhubuti sana, haui mtu wala hauawi mtu. Tutaiba kwa akili kubwa sana na sitegemei kosa litakalo tuweka mahali pabaya. Niwahakikishie, hatuui, hatushiki silaha wala kutisha mtu, je mpo tayari kushirikiana nami au niwaache mwendelee na shughuli zenu?” Gunga aliamalizia kwa swali.

Wageni wake waligeuza shingo na kutazamana kisha kila mmoja aliinama chini na kujipa muda wa kutafakari kivyake.

“Kama kweli hakuna umwagaji damu, kushika silaha, nipo safari moja na wewe.” Jamaa aliyepachikwa jina la Zena, aliongea.

“Kama ni hivyo, nami nipo safari moja na wewe”Tano alisema.

“Hata mimi” Tatu aliungana na wenzake.

“Twende na mpango wako.” Tina nae alikubali.

“Mna uhakika mpo nami kwa asilimia zote?” Gunga aliwauliza.

“Hakika komredi” Wote walijibu kwa pamoja.

“Niwakumbushe kitu… Licha ya kwamba hatutumia silaha wala nguvu, lakini kumbukeni wizi ni wizi tu, tunaweza kutegeka na kuishia kumiminiwa risasi na kufa au kukamatwa na kuishia gerezani, je? Mpo tayari kwa matokeo hayo?” Aliuliza kwa mara nyingine.

“Kwa maisha yangu ya sasa na umenipa siri kwamba mke wangu anatimka wiki ijayo, hakika nipo tayari kuingia kaburini ama gerezani. Pesa ni heshima kaka.” Tatu alisema kwa hisia kiasi wenzake wakaishia kutikisa kichwa kukubali.

“Kiufupi, ni kaburini ama gerezani, lakini lazima tupate mkwanja. Kikubwa tusiue mtu.” Tano alikubali na kauli yake ikaungwa mkono na wenzake wote.

“Good! Sasa tunaongea lugha moja. Naombeni kuanzia sasa tuanze kuishi kwenye mipango yetu…” Gunga aliwaambia wenzake.

“Mpango wa kwanza itatulazimu kuacha kutumia simu kuwasiliana, tuziweke pembeni simu zetu. Mpango wa pili itatulazimu kuanzisha migogoro na wake zetu ili tukiwa tunakutana kama hivi, kusiwe na pingamizi. Kama unaweza kumtandika na akatulia, mtandike na ajue uwezo wa kumpiga unao, kiufupi, tubadili mtindo wa maisha lakini uwe ni mtindo ambao utatuweka kwenye migogoro na wake zetu.” Gunga aliwaambia.

“Kwa nini iwe hivyo?” Jamaa aliyeitwa Zena, aliuliza.

“Hivi sasa mnaishi kwa amri za wake zenu, hamna kazi na mnawategemea. Mkiwa kwenye unyenyekevu huo na mkaanza kutoka itatia shaka na wasiwasi. Mfano, inaweza kutokea siku moja tukalala pamoja tukipanga mipango yetu, lakini kama nyumbani kwako mkeo atakuwa anajua ratiba yako kwamba hujawahi kulala nje, au kuchelewa, unaweza kukuta akikimbilia polisi kutoa taarifa zako, jambo ambalo litatia doa kwenye mpango wetu. Mgogoro kwa sasa ni muhimu na kuanzia sasa, anzeni kukataa habari zao.”

“Lakini jeuri hiyo haitaweza kudumu kwa sababu tunawategemea kwa kila kitu huoni tutajiletea taabu na mwisho tutashindwa kuishi kwenye mpango?”

“Hilo nilishajiandaa nalo. Nitawapa kila mmoja laki moja ya kuulinda mfuko wake, wiki moja itatosha kwa matumizi kisha tutakutana hapa jumapili muda uwe saa sita usiku kwa ajili ya kupokea mpango namba mbili. Kumbukeni, hakuna kupigiwa simu, utafika hapa kwa utashi wako na kama hutafika, rasmi utakuwa umejitoa kwenye mpango wetu na ukitoa siri yetu, nami natoa siri yako ya kuua mtu, ushahidi wote ninao na nitahakikisha unafungwa. Siri ni muhimu kwa usalama wetu wote.” Gunga alimalizia kwa mkwara.

“Sawa! Lakini mimi mke wangu kama unavyojua ni bonge la mtu, ananizidi nguvu nisiwe muongo na kila nikijaribu kulitwanga, huwa naambulia kutwagwa mimi. Nitaweza kweli?” Tano aliongea kinyonge sana.
Gunga alimtazama kwa muda na kumwambia…

“Nitakusaidia kwa hilo. Alhamisi ukitoka kwenye kikoba jioni muda wa saa moja na nusu, utanikuta nyuma ya ukumbi wa kanisa lilojirani na hapo kwenu. Hakikisha, umefika saa moja na nusu na isizidi dakika kumi za kukusubiri..”

“Sawa!” Tano alijibu.

“Tusambae, usiku umeshakuwa mkubwa. Tukutane jumapili kuelekea usiku wa jumatatu. Utaratibu ni uleule tukishafika hapa kila mmoja awe na soksi yake kichwani na mtazikuta mlipozikuta leo.” Gunga alisema huku akiinuka na kuondoka na kuwaacha wageni wake ambao walijua kila mmoja anatakiwa kuondoka kwa kumwacha mwenzie kwa dakika nane au kumi, hawakutakiwa kuondoka kwa pamoja.


2: MPANGO NAMBA 1.

Siku ya Alhamis ilikuwa ni siku maalumu kwa Gunga, aliacha mambo yake mengine na kuamua kukaa nyumbani huku akisubiri jua lizame, aende kuonana na Tano. Kuwepo nyumbani kulimshangaza mkewe ambae kwa siku za karibuni, hakuwahi kumuona mumewe akishinda nyumbani.

“Naona leo umefukuzwa na malaya wako na umeamua kujishindisha hapa nyumbani.” Mwanamke alifoka huku akitupa viatu vyake kwenye kona ya sebule, alikuwa ametoka kazini.

“Huwa nakwambia unamke mwingine huko nje unanikania, haya, leo kilichokufanya ushinde hapa ni kitu gani? Kazi imeisha? Umepewa likizo au ume…”

“Hebu vua kwanza nguo zako za kazi kisha uje ufoke vizuri. Ukinifokea huku ukiwa na sare zako za kazi, ni kama unataka nisikujibu vibaya kwa kuwa nitaheshimu sare zako ulizolia kiapo kulilinda taifa na watu wake…” Gunga alimkatisha mkewe ambae maneno yalikuwa yakimtoka mfululizo.

Mwanamke akasonya huku akielekea chumbani kuvua gwanda zake, dakika mbili baadae alirejea akiwa na upande wa khanga pekee mwilini mwake, nywele amezivuruga na uso umempauka kwa ghadhabu.

“Skadi! Leo utanambia huwa unalala na kushinda wapi siku zote hizo. Mwanaume nikulipie kodi ya nyumba, nikulindie nyumba bado unifikirishe unapokuwa siku zoote hizo? Hapana! Leo utanambia vizuri.” Mwanamke alifoka huku akipiga hatua za haraka kumfikia Gunga ambae alimwita Skadi. Jina halisi la Gunga, aliitwa Skadi Magibho huku mkewe akiitwa Naomi Kisaka.

“Ni lini uliwahi kujali uwepo wangu kwenye maisha yako? Leo ndo nasikia huwa unaniwaza, lakini naamini huniwazi kwa kingine zaidi ya hicho cha kulala nje na kushinda nje.” Skadi p.a.k Gunga au Sister, alimwambia mkewe kwa sauti tulivu isiyo na ishara yoyote ya ubaya.

“Ulitaka nikuwaze kwa lipi mwanaume suruali wewe? Nikuwaze wakati kodi nalipa mwenyewe, nikuwaze wakati kifurushi cha kisimbuzi nanunua mwenyewe? Nikuwaze wakati hata taulo ya kike nanunua mwenyewe?” Naomi alifoka huku akiwa mbele ya Gunga, mkono mmoja ameshika kiunoni na mwingine akiutumia kumsoka mumewe.

“Kwenye hii nyumba nilikwambia tuhame ukakataa, uwezo wangu hauwezi gharama za hapa. Nikikaa hapa sina amani kama ilivyo sasa, unafoka muda wote bila hata kupumzika. Unawaza ugomvi na majungu dhidi yangu, unyumba nikiomba unaishia kunisonya… Nishinde hapa kwa lipi? Nilale hapa kwa lipi ndugu afande?” Gunga alimalizia kwa swali.

“Usijibaraguze! Hapa ni kwako na mimi ni mkeo, unashindwa vipi kunambia hata sehemu unayofanyia kazi? Huoni kama unanikosea?” Naomi alizidi kufoka.

“Leo ndo unajua nakukosea? Leo unajua umuhimu wangu? Leo hii?” Gunga aliuliza maswali mfululizo huku akitabasamu kwa mshangao.

“Sina maana unaumuhimu kwangu, ninachomaanisha ni kwamba, ni wajibu wako kunishirikisha mambo yako..” Naomi aliongea kwa sauti ya chini kidogo.

“Kama sina umuhimu basi si wajibu wako kujua mambo yangu. Endelea kushikilia uliposhika ili mwisho kila mmoja awe hiyari kumtaliki mwenzie.” Gunga alimwambia Naomi huku akikata simu yake iliyoanza kuita kwa fujo.

“Unakata kwa sababu upo na mimi na hutaki kuongea na Malaya wako. Naomba upokee hiyo simu tafadhali.” Naomi aliongea kwa ghadhabu huku akipiga hatua moja na kumsogelea zaidi mumewe.

Gunga hakumjibu wala hakuhangaika kuichukua simu yake, badala yake akachukua kitenzambali cha runinga na kuwasha, kisha akaongeza sauti ya radio kwa kutumia kitenzambali cha radio kilichokuwa kwenye mkono wake mwingine.

Jambo lile likawa kama mkuki wa moto kifuani kwa Naomi, aliona kadharauliwa kupita kiasi, aliona ni kama dhihaka anayofanyiwa na mwanaume ambae si chochote kwake, mwanaume ambae ni raia wa kawaida huku yeye akiwa ni ofisa wa jeshi la polisi
 
nitaheshimu sare zako ulizolia kiapo kulilinda taifa na watu wake…” Gunga alimkatisha mkewe ambae maneno yalikuwa yakimtoka mfululizo.

Mwanamke akasonya huku akielekea chumbani kuvua gwanda zake, dakika mbili baadae alirejea akiwa na upande wa khanga pekee mwilini mwake, nywele amezivuruga na uso umempauka kwa ghadhabu.

“Skadi! Leo utanambia huwa unalala na kushinda wapi siku zote hizo. Mwanaume nikulipie kodi ya nyumba, nikulindie nyumba bado unifikirishe unapokuwa siku zoote hizo? Hapana! Leo utanambia vizuri.” Mwanamke alifoka huku akipiga hatua za haraka kumfikia Gunga ambae alimwita Skadi. Jina halisi la Gunga, aliitwa Skadi Magibho huku mkewe akiitwa Naomi Kisaka.

“Ni lini uliwahi kujali uwepo wangu kwenye maisha yako? Leo ndo nasikia huwa unaniwaza, lakini naamini huniwazi kwa kingine zaidi ya hicho cha kulala nje na kushinda nje.” Skadi p.a.k Gunga au Sister, alimwambia mkewe kwa sauti tulivu isiyo na ishara yoyote ya ubaya.

“Ulitaka nikuwaze kwa lipi mwanaume suruali wewe? Nikuwaze wakati kodi nalipa mwenyewe, nikuwaze wakati kifurushi cha kisimbuzi nanunua mwenyewe? Nikuwaze wakati hata taulo ya kike nanunua mwenyewe?” Naomi alifoka huku akiwa mbele ya Gunga, mkono mmoja ameshika kiunoni na mwingine akiutumia kumsoka mumewe.

“Kwenye hii nyumba nilikwambia tuhame ukakataa, uwezo wangu hauwezi gharama za hapa. Nikikaa hapa sina amani kama ilivyo sasa, unafoka muda wote bila hata kupumzika. Unawaza ugomvi na majungu dhidi yangu, unyumba nikiomba unaishia kunisonya… Nishinde hapa kwa lipi? Nilale hapa kwa lipi ndugu afande?” Gunga alimalizia kwa swali.

“Usijibaraguze! Hapa ni kwako na mimi ni mkeo, unashindwa vipi kunambia hata sehemu unayofanyia kazi? Huoni kama unanikosea?” Naomi alizidi kufoka.

“Leo ndo unajua nakukosea? Leo unajua umuhimu wangu? Leo hii?” Gunga aliuliza maswali mfululizo huku akitabasamu kwa mshangao.

“Sina maana unaumuhimu kwangu, ninachomaanisha ni kwamba, ni wajibu wako kunishirikisha mambo yako..” Naomi aliongea kwa sauti ya chini kidogo.

“Kama sina umuhimu basi si wajibu wako kujua mambo yangu. Endelea kushikilia uliposhika ili mwisho kila mmoja awe hiyari kumtaliki mwenzie.” Gunga alimwambia Naomi huku akikata simu yake iliyoanza kuita kwa fujo.

“Unakata kwa sababu upo na mimi na hutaki kuongea na Malaya wako. Naomba upokee hiyo simu tafadhali.” Naomi aliongea kwa ghadhabu huku akipiga hatua moja na kumsogelea zaidi mumewe.

Gunga hakumjibu wala hakuhangaika kuichukua simu yake, badala yake akachukua kitenzambali cha runinga na kuwasha, kisha akaongeza sauti ya radio kwa kutumia kitenzambali cha radio kilichokuwa kwenye mkono wake mwingine.

Jambo lile likawa kama mkuki wa moto kifuani kwa Naomi, aliona kadharauliwa kupita kiasi, aliona ni kama dhihaka anayofanyiwa na mwanaume ambae si chochote kwake, mwanaume ambae ni raia wa kawaida huku yeye akiwa ni ofisa wa jeshi la polisi.

Hapana! Haiwezekani, hawezi kudharauliwa na mtu aliyepoteza thamani mbele yake. Kwa kasi kubwa na wepesi wa ajabu, Naomi alifyatua mkono wake wa kulia na moja kwa moja ukatua shavuni kwa Gunga, huku ukiacha sebule ikipokea sauti ya mgusano mkubwa wa shavu la kushoto la Gunga na mkono wa kulia wa Naomi.
Macho ya Gunga yaliingiwa na ukungu kwa sekunde kadhaa, huku maumivu makali yakisambaa kwa kasi upande wake wa kushoto, kuanzia shavuni na kuenea kichwa kizima. Wakati huohuo mkono wake wa kulia alihisi ukighasiwa na kitenzambali cha runinga kikimponyoka na kuishia mikononi mwa Naomi, kabla hakijatupwa mbali na kusambaratika chini.
Gunga alitulia kwa dakika moja pasi kusema lolote huku masikio yake yakiendelea kupata karaha za masimango ya mke wake, koo lake alihisi linashindwa kupitisha hewa sawasawa, pua nazo alihisi zinashindwa kuhimili wingi wa pumzi zake zilizokuwa zimejaa pumipumi kifuani mwake.

Hasira!

Naam, Gunga alibanwa na hasira zisizomfanowe, kila alichokiwaza ndani ya dakika moja ya utulivu, hakuona kama kina maana yoyote kwake. Akawa kama mzimu, akasimama pasikujielewa, mikono yake yenye nguvu ikaidaka shingo ya Naomi kisha ikaanza kuibana kwa namna ya kunyonga.

Mwanzo Naomi alihisi ataachiwa mapema kwa kuwa alimfahamu Gunga si mgomvi, lakini matarajio yake yakawa ndivyo sivyo, shingo yake ikaendelea kusokotwa bila huruma kiasi kwamba hata zile pumzi za kurashia, zikaanza kukata, macho yakamtoka pima, midomo akaiachamisha hadi mate yakamatoka pasipokutarajia. Jitihada zake za kupambana kujinasua hazikuzaa matunda na ufahamu ukaanza kumtoka, asijue alikuwa anafanya nini mikononi mwa Gunga.

Gunga nae ufahamu ulimrejea alipoanza kuhisi mkewe ameacha kufurukuta, akamtazama usoni na kuona namna kabali ilivyokuwa imeanza kumwingia na kubadili hadi rangi ya ngozi yake.

“Siku nyingine uhakikishe umebadilika via vyako vya uzazi na kuwa na mwanaume, ndipo urushe mkono kuja mwilini mwangu.” Gunga alifoka huku akimwachia Naomi, kisha akamsindikiza na kofi zito lililotua sawia shavuni mwake na kumpepesua hadi chini, upande wa khanga ukimdondoka na kumwacha mtupu.

“Nisa--me—he!” Naomi alijikuta akiomba radhi pasipo kutarajia, aliomba radhi huku akikohoa mfululizo ili kuweka sawa koo lake, hakujali kama yupo mtupu mbele ya mumewe ambae alikuwa amesimama kwa ghadhabu.

“Hapana! Naomba usinipige tafadhali..!” Naomi alilalama kwa sauti halisi ya kike baada ya kumuona Gunga akipiga hatua kumfuata pale alipokuwa ameangukia.

“Unajifanya unawivu na mimi wakati haki ya msingi hunipi? Unajua imepita miezi mingapi sijui ulivyo? OK! Unaona ajabu mie kukusaliti wakati wewe siku tatu zilizopita umetoka Duma hotel na kile Kisajenti cha Kihaya? Unahisi sijui unamahusiano na mmiliki wa duka la nguo za kike pale mtaa wa Temboni? Unaniona mjinga kwa kuwa huwa sikuulizi kila mnapoenda kukutana na huyo jamaa pale Kebys hotel? Au unataka nikwambie na chumba namba ngapi huwa mnaingia ghorofa ya tatu? Au unataka nikwambie unaratiba nae kila jumapili saa sita mchana hadi saa mbili usiku? Unahisi sina wivu? Unahisi siumii na dharau zako hapa ndani? Unahisi sina nguvu za kukupiga? Au kukamata wezi wa nyanya mtaani ndo unahisi unaweza kunifanya utakacho?” Gunga aliongea kwa uchungu mkubwa huku akimtazama mkewe kwa namna ya ajabu kabisa, namna ambayo Naomi hakuwahi kuona hapo kabla.

“Naomba unisamehe sana mume wangu..! Sitarudia!” Naomi alioomba radhi huku uso wake ukiwa chini, nafsi ilimsuta kwa namna maovu yake yalivyokuwa wazi kwa mumewe, hakuwahi kudhani ipo siku ataanikwa kwa kila kitu tena na mume wake wa ndoa.

“Sikia, muombe Mungu akusamehe kwa lile tukio lako la kutoa mimba ya Sajenti miezi miwili iliyopita. Uliua kiumbe asiye na hatia ambae wakati mnapeana utelezi hakuwepo, raha zenu hazimhusu na matokeo yake ukamhukumu kwa kumuua. Eti ofisa wa jeshi la polisi! Mh! Unatoa mimba, utawezaje kumkamata mwanamke mwenzio ambae alikuwa akitoa mimba?” Gunga aliendelea kumsimanga mke wake.

“No! Skadi basi! Inatosha! Naomba radhi sana. Nisamehe jamani!” Naomi alisihi huku akitokwa na machozi, kwa mara ya kwanza alijikuta akipiga magoti mbele ya mume wake. Hakujali kama yupo mtupu, haikudhuru kwa sababu alikuwa utupu mbele ya mumewe.

“Pete ya ndoa ipo wapi?” Gunga alimuuliza. Naomi akainua mkono wake wa kushoto na kutazama vidole vyake, vilikuwa vitupu. Pete haikuwepo.

“Aah! Nadhani ipo kwenye mkoba au kwenye meza ya chumbani.” Naomi alijibu kwa mashaka, hakuwa na uhakika.

“Anyway! Tuachane na hayo. Inuka.” Gunga alimwambia mke wake huku yeye akitangulia kuinuka.

“Chukua hii pesa, nina njaa na ninahitaji kula.” Alimwambia huku akitabasamu na kumpa noti ya shilingi elfu kumi. Naomi aliipokea bila kujiuliza, akainama na kuokata khanga yake kisha akajisitiri na kuelekea chumbani.
Gunga aliishia kumtazama huku akitabasamu kwa uchungu, hakuwa amependa kilichotokea lakini aliona kimerejesha heshima kwa muda, hakujua heshima itaendelea au ni kwa kuwa mwanamke aliona ataumia na kuamua kujishusha.

“Naomba iwe mara ya mwanzo na mwisho, kumpiga huyu kiumbe.” Gunga aliwaza huku akikaa kwenye sofa na kuutazama mlango wa kuingilia chumbani. Aliwaza mambo kadhaa kuhusu mke wake, lakini mwisho akaishia kujisonya na kutikisa kichwa.

“Pesa ni kiungo muhimu sana kwenye ndoa. Wanawake vichwa maji kama huyu wangu, ni wengi sana kuliko wenye moyo wa kujua waume zao hawana kitu wanachohitaji. Huyu kaamua kuzini nje ya ndoa kwa sababu ambayo ukimuuliza, hatoweza kukujibu.” Alizidi kuwaza hadi pale mlango wa chumbani ulipofunguliwa, mkewe alitoka akiwa amevaa dera la rangi ya zambarau, lilimpendeza haswaa.

“Samahani! Naomba tuzungumze kidogo.” Naomi alisema huku akitazama pembeni, hakutaka kumtazama mumewe usoni, aibu na majuto viliufinya moyo wake.

“Unataka tuzungumze kitu gani? Kuhusu kutoa mimba? Au kuhusu kuchepuka kwenye hotel za Duma na Kebys?” Gunga alimuuliza huku akimtazama usoni mkewe.

“Ndiyo!” Naomi alijibu.

“Sikia, nimekwambia ninanjaa na ninahitaji kula. Nimekumbuka kula chakula chako, mwaka mzima sijawahi kupikiwa na mkono wako. Leo tu, inatosha, pengine nitarejesha tabasamu langu lililopotea. Kuhusu hayo mambo yako, naomba uyamalize na watu wako kwanza, ukishamalizana nao, rejea kwangu tuzungumze. Kwa sasa siwezi kuzumgumza na wewe kwa sababu simu yako bado inapokea ujumbe na simu za watu wako, malizana nao kwanza kisha nitakuwa radhi kukusikiliza.” Gunga aliongea kwa kirefu na msisitizo, Naomi alibaki gendaeka, asijue kipi cha kufanya, hakuwahi kujua mambo yanabadilika kwa namna ile, hakuwahi kudhani kama mambo yake yanajulikana kwa mume wake, licha ya kwamba alikuwa amepoteza thamani kwake lakini ilikuwa haiondoi ukweli kwamba, aliyekuwa mbele yake ni mume wake wa ndoa na walikuwa kwenye ndoa kwa miaka mitano na miezi kadhaa. Moyo wa Naomi ukajikunja na kusinyaa, maumivu yakakizonga kifua chake, akili nayo ikashindwa kuchagua upande.

“Nenda sokoni! Lakini wakati ukiwa njiani, hakikisha unawaza hatima yetu. Nipo tayari kwa maamuzi yako na nipo tayari kutoa talaka wakati wowote ukihitaji” Gunga alimwambia huku akiinuka na kuelekea chumbani akimwacha Naomi akiwa amesimama na noti nyekundu mkononi mwake, machozi yalimtoka na asijue anacholilia.

**********

SAA kumi na mbili na nusu jioni, ilimkuta Gunga akiwa chumbani kwake akimalizia kuusitiri mwili wake baada ya kuoga. Nguo alizovaa hazikuwa na weupe bali weusi wa kukolea; viatu vyake, fulana yake na hata suaruali yake, vyote vilikuwa vya rangi moja. Alipomaliza kujiweka vile alivyotaka, akatoka chumbani na kuelekea sebuleni ambapo alimkuta mke wake akiwa amekaa na sonona, uso ulisawajika na furaha ikiwa mbali naye.

“Natoka, nitarudi baadae kidogo.” Gunga alimwambia mke wake.

“Lakini nilihisi leo unaweza kuwa hapa muda wote.” Naomi aliongea kwa sauti ya kukwaruza, alionekana kulia kwa muda mrefu sana, ijapokuwa kilio chake kilikuwa cha kimyakimya mithili ya Kobe.

“Ni kweli, leo nipo, lakini natoka kidogo na kurejea ndani ya saa mbili kuanzia sasa.” Gunga alimjibu na bila kusubiri neno la zaidi, akapiga hatua kuufuata mlango na kutokomea nje.

Licha ya kwamba Naomi alikuwa anashindana na nafsi yake kuhusu aliyokuwa akimtenda mumewe, lakini kitendo cha kuachwa peke yake na aina ya mavazi aliyokuwa amevaa mumewe usiku ule, vikazua hisia za maswali kichwani mwake kiasi akafanikiwa kutowesha msongo wa mawazo ya kujuta na kuingiza msongo wa mawazo ya maswali fikirishi.

“Mbona kavaa nguo nyeusi kama aenda msibani?” Naomi alijiuliza huku akipunguza sauti ya radio.

“Yote kuhusu mimi kayajuaje? Kila kitu kasema kweli, lakini kajuaje? Ina maana kaweka watu wa kunifuatilia? Lakini anawalipa nini na kazi hana! Kama anifuatilia mwenyewe, mbona hakuwahi kunambia chochote? Lengo lake ni nini?” Naomi alizidi kujiuliza pasipo na majibu.

“Kuna kitu sikijui kuhusu mume wangu Skadi, huyu anaeza kuwa ni zaidi ya nimjuavyo.” Aliwaza huku akiinuka na kuelekea chumbani, akachukua simu yake na kuzitafuta namba fulani, akapiga.

“Boss!” Iliitika sauti upande wa pili, ilikuwa sauti ya kike.

“Nina kazi ya dharura naomba nikupe. Hii nitakulipa mwenyewe.” Naomi alisema.

“Kiasi gani utanipa?” Upande wa pili uliuliza.

“Sijajua gharama halisi kwa sababu sijui ukubwa wa kazi utakuwaje.”

“Kazi gani?”

“Nataka umfuatilie mume wangu kila hatua anayopiga ndani ya wiki moja, utakalopata hakikisha unaliwasilisha kwangu moja kwa moja.”

“Unamaanisha nimfuatilie Skadi?”

“Kwani unawajua wanaume wangu wangapi?”

“Sawa boss!” Upande wa pili ulijibu na kukata simu.

“Ooghfuu! Lazima nijue aliwazaje kujua ninachofanya. Inawezekana sijamjua vema huyu mwanaume. Mimi ni mkosefu kwake, lakini ninahaki ya kumfahamu.” Aliwaza huku akijitupa kitadani, msongo wa mawazo ukasafiri nae jumla.

Naomi alikuwa ni ofisa wa jeshi la polisi na alikuwa na cheo cha U'koplo. Mbali na cheo chake, lakini alikuwa ni miongoni mwa maofisa waliokuwa wakihudumu kwenye idara ya upelelezi ya makosa ya jinai, ndani ya jeshi la polisi. Kwa kuwa alikuwa ni mmoja wa maofisa mahiri kwenye suala la kupeleleza, kitengo kikamkutanisha na ofisa wa siri aliyeitwa Domika. Domi alikuwa akisaidiana kwa ukaribu na Naomi, huku akiwa mtaani na Naomi akiwa kazini. Ni maofisa wachache waliojua uwepo wa ofisa mpelelezi ambae hayupo kwenye kituo cha kazi, alifanya kazi zake kama kivuli na kwa kusaidiana na Naomi, walijikuta wakifanikiwa kurahisisha kazi nyingi sana. Sifa alipewa Naomi, lakini aliyesitahili kwa kiasi kikubwa ni Domi, mwanamke mfukunyuzi asiyemfanowe
 
Licha ya kwamba Naomi alikuwa anashindana na nafsi yake kuhusu aliyokuwa akimtenda mumewe, lakini kitendo cha kuachwa peke yake na aina ya mavazi aliyokuwa amevaa mumewe usiku ule, vikazua hisia za maswali kichwani mwake kiasi akafanikiwa kutowesha msongo wa mawazo ya kujuta na kuingiza msongo wa mawazo ya maswali fikirishi.

“Mbona kavaa nguo nyeusi kama aenda msibani?” Naomi alijiuliza huku akipunguza sauti ya radio.

“Yote kuhusu mimi kayajuaje? Kila kitu kasema kweli, lakini kajuaje? Ina maana kaweka watu wa kunifuatilia? Lakini anawalipa nini na kazi hana! Kama anifuatilia mwenyewe, mbona hakuwahi kunambia chochote? Lengo lake ni nini?” Naomi alizidi kujiuliza pasipo na majibu.

“Kuna kitu sikijui kuhusu mume wangu Skadi, huyu anaeza kuwa ni zaidi ya nimjuavyo.” Aliwaza huku akiinuka na kuelekea chumbani, akachukua simu yake na kuzitafuta namba fulani, akapiga.

“Boss!” Iliitika sauti upande wa pili, ilikuwa sauti ya kike.

“Nina kazi ya dharura naomba nikupe. Hii nitakulipa mwenyewe.” Naomi alisema.

“Kiasi gani utanipa?” Upande wa pili uliuliza.

“Sijajua gharama halisi kwa sababu sijui ukubwa wa kazi utakuwaje.”

“Kazi gani?”

“Nataka umfuatilie mume wangu kila hatua anayopiga ndani ya wiki moja, utakalopata hakikisha unaliwasilisha kwangu moja kwa moja.”

“Unamaanisha nimfuatilie Skadi?”

“Kwani unawajua wanaume wangu wangapi?”

“Sawa boss!” Upande wa pili ulijibu na kukata simu.

“Ooghfuu! Lazima nijue aliwazaje kujua ninachofanya. Inawezekana sijamjua vema huyu mwanaume. Mimi ni mkosefu kwake, lakini ninahaki ya kumfahamu.” Aliwaza huku akijitupa kitadani, msongo wa mawazo ukasafiri nae jumla.

Naomi alikuwa ni ofisa wa jeshi la polisi na alikuwa na cheo cha U'koplo. Mbali na cheo chake, lakini alikuwa ni miongoni mwa maofisa waliokuwa wakihudumu kwenye idara ya upelelezi ya makosa ya jinai, ndani ya jeshi la polisi. Kwa kuwa alikuwa ni mmoja wa maofisa mahiri kwenye suala la kupeleleza, kitengo kikamkutanisha na ofisa wa siri aliyeitwa Domika. Domi alikuwa akisaidiana kwa ukaribu na Naomi, huku akiwa mtaani na Naomi akiwa kazini. Ni maofisa wachache waliojua uwepo wa ofisa mpelelezi ambae hayupo kwenye kituo cha kazi, alifanya kazi zake kama kivuli na kwa kusaidiana na Naomi, walijikuta wakifanikiwa kurahisisha kazi nyingi sana. Sifa alipewa Naomi, lakini aliyesitahili kwa kiasi kikubwa ni Domi, mwanamke mfukunyuzi asiyemfanowe.

Naomi akampa kazi Domi. Kazi ya kumfuatilia Gunga.

Wakati Naomi anaweka kando simu yake, ni wakati huo ambao Gunga alikuwa anafika nje ya kanisa lililokuwa jirani na alipoishi bwana Tano. Muda ilikuwa ni saa moja na dakika ishirini, dakika kumi kasoro kutimia saa moja na nusu jioni, muda wa makutano.

Saa moja na dakika thelathini na moja, Tano alitokea sehemu ya miadi.

“Unakosea sana bwana Tano. Nilikwambia tukutane saa moja na nusu na si hii dakika moja iliyoongozeka. Unatakiwa kujifunza kutunza muda.” Gunga alimwambia huku akiwa anazidi kuishusha kofia yake hadi usawa wa pua, iliziba sehemu kubwa ya uso wake, hakutaka Tano aione sura yake.

“Nadhani dakika moja imeongezeka kwa sababu ya kutafuta uelekeo wako uliosimama.” Tano alijitetea.

“Siyo sababu ya muhimu, kikubwa jitajihidi kutunza muda.” Gunga alisisitiza, akameza mate na kusema…
“Mkeo yupo?”

“Yupo, amerudi muda mfupi uliopita na kaniagiza sokoni.” Tano alijibu.

“Good! Nyumba yenu ikoje?” Gunga alimuuliza.

“Nyumba yetu ni ya kupanga, ina korido ndefu iliyotenganisha vyumba kila pande. Chumba chetu kiko mwisho upande wa kulia.” Tano alijibu.

“Ina maana shughuli za wapangaji wenzako zote zinafanyika hapo koridoni; kupika, kufua, kuzogoa na ishu nyingine!” Gunga alizidi kusaili.

“Upo sahihi!”Tano alijibu.

“Hapo koridoni kuna taa ngapi?”

“Ipo moja.”

“Unaweza kuifikia?”

“Yeah! Ipo chini ili kumrahisishia kila mmoja kuifikia pindi ikileta hitilafu na ikahitaji kuondolewa na kuwekwa nyingine.”

“Wapangaji huwa wanapikia hapo koridoni?”

“Mara chache sana. Wengi wanamajiko ya gesi.”

“Nenda ukorofishe hiyo taa kisha urudi hapa ndani ya dakika tano.” Gunga alimwagiza Tano. Haraka agizo lake lilitekelezwa, Tano aliondoka kwa kasi huku akiwa na maswali luluki kichwani mwake, alishindwa kuelewa dhamira ya mtu aliyemtambua kama Sister.

“Huyu jamaa kwa nini anajifichaficha? Lengo lake ni nini? Ni kwa usalama wake au anajambo la ziada kuliko lile la wizi wa pesa? Mmh!” Tano aliishia kuguna huku akiwa anahangaika kuinyofoa taa kwenye kiambata chake, muda mfupi baadae, korido ilifunikwa na giza zito.

Tano akarejea kwa Gunga.

“Tayari komredi!” Tano alisema punde baada ya kurejea alipokuwa mgeni wake.

“Good!” Gunga alijibu kisha akanyamaza kidogo na kumtazama Tano, akauliza..

“Upo tayari kumtawala mkeo?”

“Hakuna kitu ninachotamani hapa Duniani kama hicho, nafedheheshwa sana madhira ninayopitia.”

“Upo tayari kwa mpango wangu?”

“Hakika nipo tayari!.”

“Good! Yakupasa unisikilize kwa umakini sana…. Tutaongozana hadi nje ya mlango wa chumba chenu, ukishaingia usiseme lolote hadi atakapokuuliza kuhusu mahitaji ya sokoni, usimjibu ili apatwe na ghadhabu…”

“Na asipoghababika!”

“Kiumbe yeyote dhaifu akimpata mnyonge wake, kila muda atatamani kumuadhibu. Wanawake ni dhaifu kwa wanaume, kwa kuwa kapata wa kukuonea, kila kosa lako atarusha ngumi.”

“Sahihi! Kila jambo huwa ananibonda mbwa yule.”

“Sasa, akianza kukufokea na wewe usiwe mnyonge, inuka na uanze kufoka. Atagadhabika zaidi na kuanza kukushambulia. Jibu mapigo, shambulia na wewe lakini, kuwa makini sana asije kukutia roba na ukashindwa kuchomoka. Akifanikiwa hilo kila kitu kitakuwa kimeharibika.”

“Kwa hiyo nifanye nini?”

“Hakikisha unakaa upande ambao kuna kizima taa na akili yako uiweke hapo tu. Akishajaa kwenye mtego wetu hakikisha unawahi kuizima taa na kisha haraka kimbilia kwenye kona ya mlango, nitaingia na kuanza kumshushia kipigo kitalaamu kabisa. Ndani ya dakika tatu nitakugusa na utaendelea kumpiga huku ukiongea..! Mimi nitakuwa mbali na nyumba yako na tutaonana siku tuliyokubaliana.”

“Nimekuelewa kaka!”

“Sawa! Tuongozane kuelekea hapo kwenu na utaniacha nje ya mlango wa chumba chenu. Hakikisha hufungi mlango.”

“Umeeleweka kaka mkubwa.”

Dakika mbili baadae, Tano na Gunga walikuwa wanaingia kwenye korido ndefu iliyotenganisha vyumba kila pande. Giza halikumeza korido yote kwa sababu baadhi ya vyumba vilikuwa milango wazi na kuruhusu mwanga hafifu, ubarizi pale koridoni. Licha ya mwanga huo lakini haukutosha kumfanya mtu amuone mwenzie aliyembele yake hatua sita.

Tano alimuacha nje mgeni wake na kuingia ndani, alifuata maelekezo aliyopewa na Gunga. Dakika tano tangu aingie zilitosha kuzua mzozo mkubwa baina yake na mke wake. Mzozo ulidumu kwa dakika mbili zaidi kabla ya kuzuka ugomvi wa kutupiana makonde. Tano alisikika akimtishia mke wake.

“Leo nitakuonesha kwa nini huwa naamua kukaa kimya unaponirushia vingumi vyako.”
Mke wake nae alijibu kwa kejeli na dharau, ghafla ndani ya chumba kukawa na giza zito, hiyo ikawa nafasi kwa Gunga kuingia ndani na kusimama kimya na kwa tahadhari.

Mke wa Tano aliendelea kubwata huku akihangaika kumtafuta mumewe aliyemponyoka kwenye mazingira tata.

“Uko wapi kibwengo wewe, umekimbilia kuzima taa ili ukimbie? Nitakupata tu hanisi mkubwa wewe.” Mke wa Tano alizidi kubwabwaja huku mikono na miguu yake ikijongea kwenye giza zito. Akiwa kwenye hekaheka za kumtafuta mumewe, ghafla mikono yake ikagusa kiumbe aliyekuwa kasimama.

“Ulihisi utaweza kuniponyoka?” Alibawata huku akifanya kuharakisha kumdhibiti mtu aliyemgusa.

Mke wa Tano kama alihisi hiyo siku ilikuwa sawa na siku zote, alikosea sana. Siku hiyo ilikuwa ni siku na tarehe tofauti kwenye maisha yake. Lakini kwa kuwa ninge huja yakishatokea, hakuwa na budi kuyavagaa asiyoyaweza. Naam, Mrs Tano alikutana na kubwa kuliko.
Wakati akijaribu kumdhibiti mtu aliyemgusa, akashangaa kukutana na upinzani ambao hajuutarajia, akajaribu tena kupeleka makonde kadhaa lakini yaliishia juu ya mikono ya mtu aliyehisi ni mumewe.

“Unajifanya nunda, utalegea tu!” Alibawata huku akipanga kumdaka mnyonge wake ambae alikuwa akijitetea, lakini haikuwa alivyotarajia, badala yake alijikuta akigeuziwa kibao cha onyo, onya ya makonde mfululizo na kila sehemu ya mwili wake ikajikuta ikipokea maumivu makali kuliko kawaida. Mrs Tano kila alipojaribu kujitetea kwa namba alivyoweza, alishindwa. Alipojaribu kurudisha mapigo napo alishindwa na mwili nao ukaanza kushindwa kuhimili maumivu, pumzi zikaanza kumsaliti na viungo vikamlegea. Hakuwa na namna zaidi ya kupiga kelele za uchungu na hasira.
Kelele za uchungu na hasira sizo walizozihitaji Tano na Gunga, walichohitaji ni kelele za majuto na woga. Naam, kipigo kiliendelea kwa dakika saba zaidi hadi Mrs Tano alipokubali yaishe, akalia na kukaa chini huku akiweka mikono usawa wa kichwa chake kukinga mapigo ya mtu aliyeamini ni mumewe. Na hivyo ndivyo Tano na Gunga walihitaji, walihitaji kusikia kilio cha majuto na uoga, lengo likatimia. Kwa kuwa kilichokuwa kimempeleka pale Gunga ni kuhakikisha mke wa Tano anaadabishwa, hilo alilifanya kwa weledi mkubwa na mwisho akampiga teke Tano aliyekuwa pembeni mwa mlango kisha akatimka bila kuacha kiulizo kwa yeyote aliyekuwa akifuatilia ugomvi wa Tano na mkewe.

“Huwa nakwambia huna ubavu wa kupigana na mimi lakini unajifanyaga wewe ni Hawafu mwenye nguvu.” Tano alitamba huku akiendelea kumtandika makonde mke wake aliyekuwa chini akilia kwa majuto ya kupigana na mume wake.

“Na leo hii naondoka ndani ya hii nyumba, tafuta mwingine atakaekubali umpelekeshe kama gari bovu.” Tano alizidi kupiga mkwara.

“Nisamehe mume wangu, sitarudia kutaka kupambana na wewe.” Mke wake aliongea kwa huzuni na sauti iliyokauka kwa kilio.

“Haya inuka!” Tano alimfokea. Haraka mwanamke aliinuka huku akitweta kwa wasiwasi.

“Ulinipa elfu tano ya mahemezi, chukua pesa yako.” Alimwambia huku akimkabidhi noti ya elfu tano kwa mkono wa kulia, mkono wa kushoto nao ulifuata ukiwa na noti ya elfu kumi.

“Chukua hii nenda kahemee mahitaji ya hapa ndani jioni hii kisha uje upike na ule peke yako.” Alitoa maagizo kisha bila kungoja aligeuka na kuuendea mlango, akatoka na kiubamiza kwa nyuma yake kitendo kilichozua vicheko vya pongezi kwa baadhi ya wapangaji wengine waliokuwa wakifuatilia ugonvi wao. Walifurahi kusikia Tano nae kaukataa unyonge ndani ya chumba chao. Walimsifu na kumuona shujaa aliyejitahidi kumheshimu mke wake ambae hakujali heshima hiyo. Lakini ukweli hawakuujua bali aliujua Mr Tano pekee ambae usiku huo alikuwa akitembea njia nzima akiwa anatamba kwa furaha na kwa kukazia furaha yake, alipanga kutokulala nyumbani kwa usiku wa siku hiyo. Kweli, Tano hakulala nyumbani na ahsubuhi aliporudi hakuulizwa zaidi ya kupikiwa chai ya mayai, akanywa na kubeua shibe. Mpango kazi ulitiki na siyo kwa Tano tu bali kwa kila aliyekuwa kwenye timu yao ya watu watano yaani, Tano, Tatu, Tina, Zena na Sister.

Wakati wengine wakifurahia kuanza kula matunda ya ubabe wao kwa wake zao, Gunga yeye alikuwa na kazi nyingine aliyoiita ya muhimu zaidi kuelekea kwenye mpango kazi nambari moja. Ilikuwa ni ahsubuhi tulivu kwake, aliamka na kujikuta peke yake kitandani na haikumshangaza kwa kuwa alitambua mke wake atakuwa kawahi kuelekea kazini, akajinyanyua kitandani na bila kupoteza muda akaelekea maliwatoni, akajiswafi haraka na kurejra chumbani kujipamba kwa mafuta na kujisitiri kwa nguo safi zilizomweka kwenye mwonekano halisi wa kijana wa kileo. Alipohakikisha yupo kama alivyohitaji, akaelekea sebuleni na macho yake yakatangulia kuangukia mezani; chupa ya chai na sahani iliyofunikwa vizuri ndivyo vitu alivyotangulia kuviona, akatabasamu kivivu huku akipiga hatua kuelekea mezani, akafunua sahani na kukutana na chapati tatu za mayai, naam, zilikuwa chapati tatu ambazo ni idadi ya halisi ya kiwango alichokuwa akipendelea kukitumia.

“Siku zote alikuwa wapi kufanya haya?” Alijiuliza huku akimimina chai kwenye kikombe na kuanza kufakamia chapati huku akishushia na chai ya maziwa ya unga. Dakika kumi na tano zilimtosha kukamilisha mlo wake, akakusanya vyombo na kuviweka kwenye beseni kisha akachukua simu yake na kuizima kabla hajaitupa sofani, akatoka akiwa hana simu yake. Kutoka nyumbani kwake hakutaka kutumia usafiri wa haraka, alitembea taratibu kuelekea barabarani akiwa hajui apande daladala au bajaji ili kuelekea katikati ya mji. Njiani hakuwa akiwaza lolote kwa kuwa kila kitu alikuwa anakijua na hakutaka kujiwekea mzigo mwingine wa mawazo kwa kuhofia kuharibu ufanisi wa kile alichokuwa amekipanga kwa siku hiyo. Licha ya kukiepusha kichwa chake na mawazo yoyote lakini hakuwa tayari kuacha kujia tahadhari yake, alifanya vile kwa kuwa bado hakuwa akiwaamini washirika wake na alijionya, kama yeye alifanikiwa kuwafuatilia zaidi ya watu wanne pasi ya wao wenyewe kujua, haishangazi hata yeye kuwa akifuatiliwa na MTU au watu wengine kwa namna yoyote na kwa nia yoyote au, wale jamaa zake pengine mmoja akajiongeza na kuanza kumfuatilia kwa ukaribu ili kumfahamu zaidi. Tahadhari ilikuwa kubwa lakini hakuruhusu yeyote ajue kama alikuwa anachukua tahadhari. Muda wote macho yake yalikuwa makini kufuatilia kila aliyekutana nae huku akili yake nayo ikiwa tayari kukariri angalau pikipiki au gari binafsi zilizokuwa zikimpita.
Yes! Tahadhari kabla ya hatari ilikuwa ni nguzo sahihi kwake kwani, muda mfupi baada ya kutoka nyumbani kwake kuna pikipiki kubwa kiasi ilimpita kwa mwendo wa kawaida huku dereva akiwa amefunika sura yake kwa kofia ngumu. Pengine asingeliweza kuizingatia sana kama pikipiki ya aina ile ingelikuwa ikiendeshwa na mwanaume lakini kwa kuendeshwa na mwanamke ilikuwa ni kivutio machoni mwake, akaitazama pikipiki kisha akaishia mgongoni mwa mwanamke ambae umbo lake lilionekana kuwa si haba.

“Ngumu sana kuona mwanamke akikatiza mjini na pikipiki kubwa namna ile.” Aliwaza huku akitabasamu kisha akaachana na mawazo ya pikipiki ile na dereva wake, akainua mkono wake wa kushoto na kutazama mishale ya saa.

“Nipo ndani ya muda.” Alijisemea huku akizidi kukata mitaa kuelekea bila kujali atatembea kwa umbali gani, kichwani mwake ni kama mtu ambae hakuwa na uhakika wa aina ya usafiri atakaoutumia kuelekea aendako. Safari yake hiyo rasmi iliishia kwenye moja ya kituo cha daladala cha magari ya kwenda alikokutaka. Alisimama kituoni bila kuwa na haraka ya kugombea usafiri, alisimama huku akishuhudia watu wakijisukuma na kugombea milango ya daladala za kuelekea maeneo waliokuwa wakienda. Akiwa anabarizi mitaa ya kituo kile ambacho alikizoea, umbali fulani aliiona pikipiki kama ile iliyokuwa imempita njiani, akaitazama kwa kuhakikisha na akagundua alikuwa sahihi kuifananisha, ilikuwa ni yenyewe na hakukosea. Dereva wake yuko wapi? Alijikuta akitamani kujua alipo dereva wa pikipiki ile. Kwa nini? Kwa sababu alikuwa anataka kujihakikishia kile alichokuwa amekiwaza kuhusu uzuri wa mwanamke yule ambae umbo lake lilivutia vema.
Dakika kadhaa baadae akiwa hajamuona dereva wa ile pikipiki, akaamua kuachana nae na kuanza kupiga hatua kuelekea karibu na mahali gari zilipokuwa zikisimama. Hatua ya kwanza ilienda vema lakini hatua ya pili haikusha, akasimama huku akili yake ikianza kupokea hisia tofauti na za awali. Kivipi? Kwa sababu aligundua yule aliyekuwa akitamani kumuona kumbe hakuwa mbali nae, mwanamke yule alikuwa miongoni mwa abiria waliokuwa wamekaa kwenye kimbweta cha kupumzika abiria wakati wakingoja gari za kuwapeleka walikoenda.

“Anaweza kuwa anasubiri daladala?” Alijiuliza huku akimtazama kwa kuibia, aliwahi kumgundua kwa sababu ya aina ya nguo alizokuwa amevaa.

“Miwani iliyoficha macho yake imeninyima kuushuhudia uumbaji wa Mungu kwa asilimia zote, mwanamke mzuri sana huyu; mbichii na anavutia” Aliwaza huku akiwa bado kasimama palepale bila kufanya harakati zozote kama alivyokuwa amepanga.

“Anasubiri mgeni wake hapa au?” Alijiuliza huku hisia fulani zikipambana kuiteka akili yake, hazikuwa hisia za mapenzi wala matamanio kwa yule mwanamke bali zilikuwa ni hisia za wasiwasi. Naam, wasemavyo watu kwamba wasiwasi ni akili, Gunga akaamua kukubaliana na hisia zake na wakati huohuo akaahisrisha kupanda daladala na badala yake akatembea kuelekea kilipokuwa kituo cha bajaji na bodaboda ambacho hakikuwa umbali. Alitembea bila kuonesha mchecheto wowote, achetekee nini ikiwa anajiamini siyo mhalifu?

Kituoni alichukua bajaji ya dereva ambae hawakuwa wakifahamiana, siku hiyo akawatosa wale waliomfahamu pale kituoni kwa kuwa mara kadhaa alikuwa akiwatumia kwenye baadhi ya safari zake.

“Nipeleke mjini.” Alimwagiza dereva baada ya kuwa amekaa na upande aliochagua ni kukaa sehemu ambayo angeliweza kuitazama sidemirror ya dereva, alitaka kubashiri kama angeliweza kuiona ile pikipiki kwa mara nyingine. Safari ilianza huku akiwa amechagua kutokubandua jicho lake kwenye hicho kioo.
Baada ya kutembea umbali wa zaidi ya dakika kumi na tano hatimae wasiwasi wake ukawa akili halisi, aliiona ile pikipiki ikiwa nyuma yao na dereva akiwa ni yuleyule mwanamke,kilichomvutia zaidi ni namna ambavyo dereva wa pikipiki ile hakuonekana kujali kuwapita wala kuzipita gari chache zilizokuwa mbele yake.

“Ni mawazo yangu au kweli huyu mwanamke ananifuata?” Alijiuliza huku akiwaza jambo la kufanya ili kuepuka kufungiwa tela na yule mwanamke, alichagua kuziamini hisia zake. Akiwa bado anawaza cha kufanya, ile pikipiki ikawapita kwa kasi ya kawaida kama vile dereva hakuwa na haraka ya kwenda popote, hilo kwake akachagua kuwa ni hakikisho sahihi kwa kile alichokuwa akikitilia shaka. Kama alivyokuwa akihisi ndivyo ilivyokuwa, mbele kidogo waliikuta ile pikipiki ikiwa imeegeshwa kando ya barabara na dereva wake alikuwa akinunua vipande vya miwa.

“Akinifuata tena nitaamini mimi ndiye ninaefuatwa.” Aliwaza huku wakati huu akianza kuwa makini zaidi kuliko awali, maswali mengi yalikuwa kichwani mwake kuhusu yule mwanamke ni nani na alikuwa akimfuata kwa sababu gani, je, amenusa kile alichokuwa akiwaza kukifanya? Au alikuwa akimfuata kwa sababu zipi?.

“Mbona mapema sana?” Aliwaza huku akiwa makini kutazama kama ile pikipiki ingelimfuata tena. Kama alivyohisi ndivyo ilivyokuwa, pikipiki ile ilipita tena na mwendo ukiwa ni uleule na dereva hakuonekana kuwa na haraka yoyote ile.

Gunga alijikuta akitabasamu kinyonge huku akiwa ameshawaza cha kufanya ili kuepuka kufungiwa tela na mtu yule ambae hakuwa akionekana kuwa mwema kwake.

“Nishushe hapo.” Alimwambia dereva.

“Lakini ulisema twaenda mjini na mwendo bado kidogo tu.” Dereva alimjibu huku akionekana kutokujali takwa la mteja.

“Nitakulipa pesa ya mjini usiwe na shaka.” Alimwambia.

“Lakini hapa hamna sehemu ya kushushia abiria kaka, kituo kipo hapo mbele mwendo wa dakika tatu au nne hivi.” Dereva alimwelekeza.

“Punguza mwendo kidogo na unitazamie gari za nyuma ili mimi niruke bila kupata madhara, nawe uendelee na safari yako hadi utakaporejea kituoni kwako.” Alisisitiza na dereva nae hakuwa na kipangamizi, akaamua kufanya kama alivyoombwa na hiyo ni baada ya kupokea pesa yake.
Baada ya kushuka salama kwenye bajaji akajipa sekunde kadhaa za kutazama usalama wa pale aliposhukia, hakukuwa na watu wengi na watu hao walikuwa ni wale waliokuwa kwenye safari zao na hawakuonekana kujali namna alivyoshuka kwenye bajaji kwa kuwa ile ilikuwa ni aina ya ushukaji ambao ulizoeleka kwa baadhi ya watu. Alivuka barabara na kuhamia upande wa pili huku akiwa makini kuhakikisha haioni tena ile pikipiki wala yule mwanamke, alipohakikisha hakuna anaemzingantia akachomoka kwa kasi na kuingia kwenye kichochoro kilichokuwa kinaenda kwenye makazi ya watu na akapotelea huko huku akiwa ni mwenyeji wa njia za mtaa ule, alijua ni wapi ataenda kutokea ili akutane na usafiri wa bodaboda na njia wangeliitumia kufika mjini na kuingia kwenye moja ya maeneo yake aliyohitaji kufika kwa siku hiyo.

Dakika kumi na tano baadae Gunga alikuwa akiingia kwenye ofisi moja iliyokuwa ikijihusisha na uuzaji wa santuri, alipoingia ndani akapitiliza upande ambao ulikuwa umetengwa na kufunikwa kwa pazia. Alipoingia huko alikutana na vidato vilivyoelekea juu, akavipanda na kuishia kwenye moja ya ofisi ambayo ni wachache waliojua ilikuwa ikijihusisha na kazi gani na mmoja wa wamiliki was ofisi ile alikuwa ni Gunga.
 
Waandishi huwaga tukiandika tunaandika kazi zaidi ya Moja kutokana na mood.

Leo unaweza ukawa na mood ya kuandika Stori inayoendelea lakini kesho ukapata Idea nyingine ya Stori mpya
Sawa bwana taikon ngoja tuwe tunasubiria vipande vipande vyenu mi nilifikiri unaandika riwaya nzima kabla ya kutupia hata kipande kimoja humu jukwaani kumbe sivyo
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom