Simulizi: Bwana Harusi aliyejeruhiwa

SEHEMU YA 101

“Haya nashukuru, waweza kundoka.” Nilimwambia. Tatu alipondoka, nikarudi macho kwenye kile kipande cha karatasi na kusoma maandishi yaliyoandikiwa na Nasra Mfaume.

Mke wangu wa zamani. Ujumbe ule ulikuwa ulisomeka hivi: Mpenzi Faraji. Awali ya yote nakupa pole kwa shughuli za mchana kutwa. Dhumuni la ujumbe huu ni kukueleza machache juu ya hatima yangu nawe, mpenzi.

Tangu nimefahamiana ni nyakati chache sana ilipatikana furaha baina yetu, muda mwingi tumepitia katika machozi na maumivu makali. Utukufu wa ndoa yangu niliukanyagia viatu vya maliwato, nimesalimu amri kushindwa kwa kushindwa kuuteka moyo wako .

Nitajiulumu mwenyewe kwa mpumbavu huo milele. Utoto na ushamba wa mji ulinifanya nilivamie jiji ambalo lilinipokea kwa uso wa tabasamu, jiji likanitafuna kisha likanitema kama ganda la muwa.

Kila mmoja anahadithi yake yenye maumivu maishani na moyo unatudhihirishia ni kiungo pekee chenye kujali na kuhifadhi hisia.

Matatizo ni kioo, hata wazuri na wabaya hujitazama kwa jicho tofauti, lakini hakuna anayejisifu mbele ya kioo hicho. tunaishi kwakuwa tulikosea, maisha ni makosa na msamaha ni furaha.

Faraji mpenzi, nisikuchoshe kwa semi za Kiswahili na tungo zenye kufikirisha akili, jambo kubwa napenda utambue ni hili: Kuanzia sasa nitakuwa mbali na wewe milele.

Nimepata mwanaume mwingine mswalihina, mwenyeji wa huko Chakechake Zanzibar Kisiwani Pemba, nimekiri makosa yangu yote kwakwe, yuko amekuwa radhi na mimi na natarajia kufunga naye ndoa. Faraji baba, naomba umtunze vema mtoto wetu, Mwanda, hata wewe pia ujitunze.

Nimeshindwa kumlea mwanangu. Tunu pekee niliyopewa na Mungu. Acha basi niawachie wenzangu wafanye kazi hiyo, mchunge na mlinde na hila za mama wa kambo.

Mwisho napenda nikuombe radhi kwa makosa mengi niliyokutendea maishani mwako, lakini pia nakusihi uache pombe, na utafute mwanamke mwingine mwema uoe.
Ni mimi mkeo wa zamani.

NASRA MFAUME.
Nilirudia tena kusoma ule ujumbe, kadiri nilivyokuwa nikiyapitia maandishi yale ilikuwa ni kama vile naisikia sauti ya Nasra ikinieleza waziwazi maneno yale.
 
SEHEMU YA 102

Nisiwe mwongo, barua ya Nasra ilizidisha mfadhaiko wa nafsi kwa usiku huo, japokuwa moyo wangu ulikuwa haumtaki mwanamke yule, ajabu nilijikuta najisikia wivu kwa maamuzi yake.

Hasira iliyochanganyikana na simanzi ilitanda moyoni mwangu. Hata hivyo sikuwa na lolote la kufanya kuzuia maamuzi ya Nasra.

Nilisonya nikaifinyanga kile kipande cha karatasi nikakitupilia mbali. “Umalaya tu! Kaona amkimbie kabisa mwanaye kisa mwanaume,” nilinong’ona.

Mkandamizo mkubwa ukazidi kunijaa kichwani,ujumbe wa Nasra ulikuwa ni mkasa wa tatu kunitokea ndani ya masaa machache mno baada ya visa kadhaa kunikuta. Na hakika ulikuwa ni mwiba mkali kifuani.

Kwa kuwa muda ulikuwa umekwenda, nilichofanya ni kuingia chumbani kupumzika. Nikiwa kitandani sikuambulia japo lepe la usingizi. Nilikuwa nikipitia katika bahari kubwa ya mawazo. Kwa zaidi ya masaa manne, nilikuwa nikigaragara kona moja hadi nyingine kitandani, nilikuwa nikiwaza na kuwazua.

Katika kuwazawaza huko, nikabaini mali pekee iliyokuwa imesalia mikononi mwangu ni ile nyumba niliyokuwa nikiishi, sanjari na kiasi fulani kidogo cha fedha kilichokuwa kwenye akaunti yangu ya benki.

Mapenzi yalikuwa yameharibu maisha yangu kwa kiwango kikubwa sana, hadithi ya mateso katika siku za ujana wangu zilihusiana moja kwa moja kati ya maisha ya ndoa na mapenzi.

Kabla ya kuoa, nilikuwa mvualana mwenye mafanikio makubwa maishani, kila siku nilikuwa mvulana mwenye tabasamu na furaha kubwa, lakini mambo yote hayo yamebakia kuwa historia. Wanawake walikuwa wameniingiza katika mateso na majuto makubwa.

Kila nilipofikiria hali hiyo, nilishikwa na uchungu mkubwa sana. Kuna wakati nilikuwa nikiona, heri ningendelea na mienendo yangu ya mwanzo.

kubadilisha wanawake kila nilipojisikia, kuliko majanga niliyoyavaa. Nikiwa katika lindi la mawazo, nilistushwa na sauti ya mlango wa chumbani kwangu uliokuwa ukigongwa kwa nguvu. “Nani!!” nikafoka.

“Mimi Tatu, hali ya mtoto ni mbaya.” Sauti ya dada wa kazi ilisikika. Nilisimama nikafungua mlango.Tatu alikuwa amesimama wima akionekana kuchanganyikiwa.

“Hali ya Mwanda ni mbaya, anakoroma na kurusha mikono na miguu kama anataka kufa,” aliniambia.
 
SEHEMU YA 103

Moyo ukapiga kite, nikakimbilia chumbani kwao. nilimkuta mwanangu anatapatapa huku akitoa mkoromo kama wa gari bovu.

“Mungu wangu nini hiki!” “Tumpeleke hospitali!” Tatu alisema.

“Harakaharaka nikarudi chumbani nikavaa shati, suruali, saa ya mkononi, ilikuwa ni ni saa kumi alfajiri. Nilimrudia mwanangu chumbani nikambeba mgongoni.

“We bakia hapa uangalie usalama wa mji.” “Sawa baba.” Nikatoka nje na mtoto wangu mgongoni, nilitembea upesi kuelekea kituo cha tax.

“Endesha twende Regency,” nilimuamulu dereva. Mtoto aliendelea kutapatapa, na kukoroma, kwa udadisi mdogo nilioufanya nikabaini mtoto alikuwa havuti pumzi ya kutosha. “Ana tatizo gani huyu mtoto?”

“Endesha gari,”nilifoka, dereva hakufungua mdomo wake hadi tulipofika regency. Wauguzi walimpokea mwanangu kisha akaingizwa katika chumba cha wagonjwa mahututi, mimi nikabakia kwenye benchi.

Lisaa limoja badaye, mtoto akatolewa akiwa kwenye kitanda huku mashine za kupumulia zikiwa puani kwake. Alikuwa amefumba macho.

“Njoo mara moja.” Daktari aliniita ofisini kwakwe. Nikaingia. “Mwanao alishawahi kuwa katika hali hii kabla?” “Hapana Dr. Kwani anatatizo gani hasa?” “Sasa nisikilize…”alisema kisha akaendelea.

“Katika moyo wa mwanao Valve zake zinaonekana kuzorota, hivyo anatakiwa afanyiwe upasuaji ujulikanao kama heart valve replacement. Hata hivyo, upasuaji huo kwa hapa nchini haufanyiki. “Whaat!” nilimaka.

“Nitakuandikia transfer ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, huko utapata transfer nyingine ya kwenda nchini India.” Dokta alimaliza. Nguvu ziliniishia, nilihisi dunia inazunguka kwa kasi sana.

Kwa dakika nzima, nilibakia nimeketi kitini bila kujua nawaza nini hasa. Alinipa fomu ambayo aliiita ‘transfer’ nikalipia ile huduma aliyopewa kisha Nikatakiwa kuingia kwenye gari la wagonjwa ili kumkimbiza mtoto Muhimbili.

Ifahamike, kipindi hicho kulikuwa hakuna taratibu za bima za afya, kadhalika ilikuwa ni kabla ya kuanzishwa kwa taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete. Dakika kumi na tano zilitufikisha Muhimbili.

madaktari walipopitia ripoti kutoka hospitali ya Regency, wakaniambia watamfanyia tena vipimo mtoto wangu ili wajiridhishe, kisha ningepewa kibali maalumu cha kumpeleka mwanangu nchini India.
 
Mmh! hii dunia ni nzuri ila ikiamua kuberuka..unaweza kukuhusu.. .mapenzi mabaya sana! ni basi tu tamaa za maumbile zinatupeleka huko!
 
Maskini, Dunia imempa kisogo Faraji, atauza nyumba kwa bei ya hasara ili ampeleke mtoto India, akitika India safari ya Nguruka itakuwa imeiva, dar ataanza kuisikia kwanye radio na kuiona kwenye TV tu......Pole sana Faraji
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom