BWANAHARUSI ALIYEJERUHIWA
SEHEMU YA MWISHO
ILIPOISHIA...
“Anahisi nikiwa mbali naye nitakuwa na mwanaume mwingine.”
“Whaat!!”nilimaka kwa hasira.
Nilimsihi sana nikimtaka aje nyumbani, lakini ndugu yangu aligoma, niliwasiliana na mumewe ambaye kwangu ni shemeji yangu, ili amruhusu mkewe aje kunisaidia kumuuguza mama, jamaa yule naye alinikatalia bila aibu. Dada yangu naye alimtii!
ENDELEA NAYO...
WATU huwa wanasema mtoto wa kike kwa mama, wa kiume kwa baba. Katika familia yetu ilikuwa kinyume chake. Ndugu zangu wa kike ambao ndio walitakiwa kuwa mstari wa mbele katika kumuuguza mama yetu wote walimpa kisogo.
Nadhani ni sahihi kusema dada zangu hawakuwa na uchungu na mama yao. Ukichilia mbali yule dada yangu wa Geita, kuna huyu aliyekuwa akiishi Tanga.
Yeye aliniambia hawezi kuja kumuuguza mama kwa kuwa mumewe alikuwa amekwenda nga’mbo kimasomo hivyo asingeweza kutoka kuja kijijini bila ruksa ya mumewe, akaongeza kuwa sheria ya dini ilikuwa hairuhusu yeye kutoka bila ruksa ya mumewe.
Kwa kweli nilikuwa napitia majaribu makubwa mno maishani. Kitendo cha dada zangu kushindwa kuja kumuguza mama yao kwa kuheshimu maslahi ya waume zao kiliniuma. Hata hivyo, kuna kitu nilijifunza kwenye jambo hilo, japokuwa niliumizwa na fikra zao.
Nilibakia na mama nikimuuguza. Mipango ya kilimo niliisimamisha. Niliendelea na kazi zangu za ufundishaji huku kila wiki nikiwa na kazi ya kumpeleka mama kwenye kliniki ya mazoezi.
Alikuwepo shangazi yangu mmoja ambaye mara nyingi alikuwa akija kunisaidia kumpa huduma muhimu kama kumwogesha, kumbadili nguo na kadhalika.
Kama ungepata bahati ya kumwona mama yangu, usingemtofautisha na mtu mwenye ugonjwa wa kiharusi. Mwanamke mnene mwenye mashavu makubwa, hakuwa yeye tena.
Alikuwa amekonda mashavu yamemnyauka na macho yenye makunyanzi yametumbukia kwa ndani.
Kila nilipokuwa nikimwangalia nilihisi uchungu.
Sikujua mipango ya Mungu ilikuwa ni nini, siri hiyo alibaki nayo yeye aliye juu. Mama ndiye faraja yangu iliyokuwa imesalia duniani.
Mama aliishi na maradhi yake kwa muda mrefu sana. Nadhani miezi karibu saba ama nane alikuwa akipambania uhai wake kitandani.
Kila baada ya ya wiki mbili nilikuwa nikimfanyia dua maalumu ili mwenyezi Mungu aweze kumfanyia wepesi katika maisha yake.
Katika kipindi fulani ilifika, yule shangazi aliyekuwa akinisaidia kumuuguza mama, naye aliugua, akawa haji tena nyumbani.
Ikabidi kazi alizokuwa akikifanya nimtafute mwanamke wa kuwa anamsaidia mama kwa malipo ya fedha.
Wakati ambao sikuwa na fedha, nilikuwa nikimuhudumia mwenyewe.
Nililazimika kungojea hadi giza liingie ndio nimwogeshe mama yangu.
Siku moja mwishoni mwa wiki, nilikuwa nimempeleka mama hospitali ni katika kliniki ya mazoezi. Wakati napita getini, nikasikia sauti ya mwanamke ikiniita nyuma yangu.
“Faraji!!”
Nikageuka kutizima. Lahaulaa!! Sikuamini kumwona Nasra Mfaume, mke wangu wa zamani.
Alikuwa amevaa sketi ndefu ya rangi ya zambarau ambayo iliburuza hadi chini. Juu alivaa blauzi nyeupe ya mikono mirefu, kichwani alijifunga ushungi wa rangi ya zambarau. Moyo wangu ulipiga kite baada ya kumwona mwanamke huyo.
“Ni wewe!!”
“Ni mimi...”alijibu uso wake ukiwa wenye tabasamu. Akaendelea kunichangamkia:
“Babari za siku?”
“Salama tu.” Nilimjibu nikiwa sina tashuishi yoyote usoni.
“Vipi kulikoni tena na mama?” alihoji huku akimwangalia mama aliye kuwa katika baskeli ya magurudumu.
“Anaumwa.”
“Ni nini na Tangu lini?”
“Mwaka sasa.”
“Nini tatizo?”
“Kiuno.”
“Poleni sana Faraji.” Alisema.
Nilimpa tabasamu jepesi lililosema: Ahsante.
“Mimi nimekuja jana.” Nasra aliendelea kusema.
Kimoyomoyo nikajisemea: Nani amekuuliza swali hilo?
“Kila la kheri Nasra.” Nilimwambia. Nikaondoka nikimwacha akinisinidkiza kwa macho.
****
Baada ya chakula cha usiku, nilikuwa nikifanya matayarisho kwa kwenda kumwogesha mama gizani. Maji ya moto nilikuwa nikiyapoza kidogo katika ndoo kubwa.
Wakati napeleka maji katika banda la uwani, nikaona kivuli cha mtu nyuma ya banda la kuku akiwa amejibanza. Kwa kuwa ilikuwa giza, nikahisi labda mwizi. Nikapaza sauti kuuliza:
“We nani?” niliuliza.
Nasra akatokeza kwa mwendo wa kunyata!!.
“Ni wewe tena umefuata nini!!” nilimaka.
“Nimekuja kukusaidia kumwogesha mama.”
“Hebu niondoke bwana.”
“Siendi popote.”
“Wewe si mke wa mtu!”
“Hata kama.” Alijibu, akanisogelea zaidi, uso wake mng’avu uling’aa gizani.
Alikuwa ananukia manukato ya mazuri.
“Kuwa mke wa mtu hainizuu kutoa msaada.” alisema.
“Sitaki matatizo hebu ishia zako.”
“Lau kama nisingekuwa chanzo cha mateso mengi maishani mwako, nisingekuwa hapa muda huu.”
“Kwa hiyo?”
“Nipo kulipa fadhila za mabaya niliyofanya kwako?”
“Kwa kumwosha mama yangu?”
Hakujibu. Nikaendelea kumzodoa.
“Kunisaliti, kumtelekeza mwanao na kuharibu maisha yangu. Inalipwa kwa kumwogesha mama yangu! Eti Nasra?” nilihoji huku nikimwangalia Nasra usoni.
Hakujibu alibakia ameghafirika, maneno yangu ni kama yalimgusa.
“Sikiliza Nasra,” nilisema tena.
“Hakuna jambo lolote la wema utakalofanya litakaloweza kunisahaulisha mabaya uliyonitendea, labda moyo wangu uamue tu kukusamehe. Weka akilini hilo.”
Nasra alishusha pumzi ndefu, akachutama na kuangua kilio cha chini chini.
“Huondoki?” nikamuuliza tena.
Alisimama, akataka kama kusema kitu, lakini akaghairi, akatembea kuelekea getini. Nikamfuata nyuma ili akitoka tu nifunge geti.
“Nimepewa talaka na mume wangu!” alisema huku akitembea.
“Kwa nini?”
“Ni kwa sababu sina kizazi!”
“Eeh!!! Kilikwenda wapi?”
Alisimama na kunigeukia kisha akaniuliza swali ambalo nililiona ni la kipumbavu. Akauliza:
“Unataka nikwambie?”
“Ulitegemea sintahoji kizazi chako kimekwenda wapi?”
Alitabasamu, sikujua kama tabasamu lake lilitokana na kufurahishwa na kauli yangu ama vipi.
Ninachokumbuka Nasra Mfaume alianza kunipa maelezo yaliyonikata maini. Alinisimulia:
“Wakati nakusaliti wewe dhidi ya yule sharobaro mwanamuziki, nilipata ujauzito....” alisema. Akasita kisha akaniangalia usoni, uso wangu ulisawijika kwa sentesi ile.
Nikawa kama nimewekwa kwenye theruji. Mwili wote ulipoa. Kumbe mke wangu aliwahi kupewa mimba na hawara wake. Loh!!.
Japokuwa nilikuwa nimekwisha achana na mwanamke yule lakini jambo lile liliniuma, maumivu yake utadhani tukio lilitokea jana tu.
“Eeh ikawaje?” nikamuuliza. Donge kavu lilinikaba kooni.
“Kwa kutotaka wewe kujua kama nina mwanaume mwingine, nilikwenda kuitoa mimba. Ilikuwa ni siri kati yangu na yule bwana.
Sikujua kama kwa kutoa ile mimba kulikuwa na athari, baada ya kuolewa na huyu bwana mwingine athari zake ndio nimeziona, sina kizazi.
Mume wangu huyo ameshindwa kabisa kuwa na simile na jambo hili, amenitaliki kwa kushindwa kumzalia mtoto. Nina siku nne tangu nitoke mikononi mwake.” Alimaliza.
Uso wa Nasra ulijawa machozi, nilishindwa kutathimini kilio chake kilitokana na nini hasa. Je ni kushindwa kupata mtoto?
Ama kupewa talaka? Aidha ni juu ya upumbavu wake wote kwa ujumla.
“Nimejifunza mengi maishani, nataka nisahihishe makosa yangu Faraji” alisema.
“Usiku mwema Nasra.”
Ndio kitu pekee nilichomwambia usiku ule.
Kauli hiyo ilifanya Nasra aangue kilio kama mtoto mdogo, sijui aliwaza kitu gani binti yule.
Labda alidhani naweza kuwa na huruma dhidi yake. Kwa kweli alikuwa mwanamke aliyevuruga maisha yake kwa ujuha wake mwenyewe.
Nilifunga geti na kurudi ndani kwa ajili ya kumwogesha mama yangu kipenzi.
Usiku ule nilipopanda kitandani, nilifikiria mambo yote aliyonieleza Nasra.
Pamoja na kwamba nafsi yangu ilikiri Nasra alikuwa mkosaji, lakini sauti moja ilinisihi kutomchukia daima mtu yule.
“Hakuna binadamu mkamilifu.
Wakati mwingine tunakosea ili tujifunze.” Sauti moja mawazoni iliniambia.
“Kwa makosa aliyoyafanya Nasra, kwa sasa atakuwa mwanamke bora pengine kuliko yeyote yule, maana amekwishakosea na kajifunza.
Mpe nafasi, ” sauti ile iliendelea kunishawishi.
Kwa kweli hadi kunapambazuka, lile donge kavu sijui hata lilipotelea wapi, nilikuwa na fikra tofauti kuhusu Nasra. Nilitaka niishi naye tena, ikiwezekana nimwoe upya!!!!!
*****
Ilikuwa ni siku mpya. Jumapili tulivu. Nilikuwa nimeamka tangu alfajiri nikifanya usafi wa hapa na pale.
Nilimwandalia mama stafutahi ya chapati za kumimina na mayai.
Akiwa anakunywa chai nikwamweleza kila kitu kilichotokea kwa Nasra. Pia nikamwambia nadhiri ya kurudiana na mwanamke huyo.
Masikini ya mungu mama yangu hakuwa na makuu, alikuwa radhi kwa kila kitu nitakacho.
Wakati tunaendelea na maongezi mara mlango wa geti uligongwa, nikamini kivyovyote vile mgongaji ni Nasra. Niliona itakuwa fursa nzuri kama nitazungumza na mrembo yule ili tuingie kwenye makubaliano ya kuanza maisha mapya pale kijijini.
Nilisimama na kwenda kufungua geti. Mara nilikutana na watu ambao sikuwategemea. Walikuwa ni askari polisi wawili waliovalia kijeshi.
“Wewe ndiye Faraji?”
“Kuna tatizo?” nilihoji. Ilikuwa ajabu, sikuwahi kufuatwa na polisi kwa miaka mingi sasa. Leo vipi tena. Kulikoni.
“Wewe ndiye Faraji!!” jamaa walirudia kuniuliza tena kwa amri.
“Ndio ni mimi, kuna nini?”
“Unahitajika kituoni.”
“Kuna tatizo gani?”
Jamaa hawakunipa jibu. Walinishika na kunipeleka kituoni. Hadi tunafika sikuwa nimejua kwa nini nikamatwe, ingawa kuna wakati nilihisi huenda kuonana kwangu na Nasra kuna uhusino fulani wa mimi kushikwa na polisi.
“Wewe ndiye Faraji Mpangalala?”mkuu wa kituo aliniuliza baada ya kuingizwa ofisini kwakwe.
“Ndio mimi. Kuna nini Afande?”
“Kwani hujaambiwa?”
“Sijaambiwa chochote!”
“Askari waliokuja kukukamata Ilibidi wakwambie wanakukamatia nini.”
“Hawakunieleza!” nilisema.
“Unahusishwa na kifo cha Nasra Mfaume” kamaanda alipasua jipu.
Lilikuwa ni bomu lililonifanya nilihisi ni ndoto inanipitia nikiwa nimelala usingizi.
“Nasra....Nasra ame....Nasra amekufa lini?”
“Jana usiku.”
“Jana usiku!!!!
“Ndiyo.”
“Nilikuwa naye!!!!”nilisema kwa wahaka huku nikimwangalia usoni yule kamanda.
“Tunajua ulikuwa naye, lakini baada ya kuachana naye ndipo alipokutwa na mauti?”
“Kivipi? Ilikuwaje? Kwa nini na wapi?”
“Hayo maswali nikuulize wewe!!”
“Whaat!!” nilimaka.
“Nisikilize bwana mdogo.” alisema kamanda akiwa ananiangalia kwa makini.
“Uchunguzi wa awali unanaonesha Nasra amejiua mwenyewe kwa kisu ndani ya chumba chake.”kamanda yule alisema huku akikuna ndevu zake zilizokuwa zimepunguzwa kwa mtindo wa mustachi.
“Hata hivyo Nasra kaacha ujumbe wenye maelezo yasiyojitosheleza sababu ya kujiua kwake, ujumbe huo unakutaja wewe kuwa moja ya sababu ya yeye kujiua, ndio maana uko hapa kusaidia polisi.”
“Uko wapi huo ujumbe?”
Alinipa kipande cha karatasi kilichoandikwa na Nasra. Nilisoma maneno yaliyoandikwa kwenye ujumbe ule yalinikata maini. Aliandika hivi:
“Faraji mpenzi...
Sioni, sababu ya kuendelea kuishi katika dunia kwa mateso makali ya nafsi. Dunia imenielemea na imenishinda. Hiki ndicho ninanistahili. Nisamehe kwa yote niliyokutendea maishani, angalau nakufa ili nikaungane na mwanetu Mwanda huko akhera.”
“Nooooo!” nilipiga kelele nikalia kama mtoto.
***
Siku mbili badaye niliachiwa huru baada ya uchunguzi wa kipolisi kuonesha sikuwa na kesi ya kujibu, niliwaomba polisi nikapaone mahali Nasra alipojiulia. Nikapelekwa kwao, mtaa wa Bweru.
Chumba cha Nasra kilikuwa kimefungwa kwa amri ya polisi, nilisukuma mlango nuru ya mwanga hafifu ikaangaza chumbani. Kitandani kulikuwa na mashuka yaliyotapakaa damu iliyokaukiana.
Damu ya Nasra Mfaume, damu ya Mwanamwali.
Nilimlilia Nasra hadi macho yakavimba, kifo chake kiliniuma mno, kwa kweli moyo wangu ulikuwa na majeraha makali sana.
Wiki moja badaye, Nasra alizikwa katika makaburi ya Lugongoni.
Mimi bado naishi kijiji cha Nguruka mkoani Kigoma, naendelea kumlea mama yangu ambaye bado hajaweza kusimama.
Mwisho kabisa nakushukuru kwa kusoma simulizi hii ya kweli ya maisha yangu. Naamini kuna funzo umepata maishani.
MWISHO.
Usikose kufutilia simulizi mpya