SURA YA ISHIRINI NA TANO:
Saa ya ukutani ilisema ni saa moja na nusu asubuhi, Mtemvu na inspekta Vitalis wakiketi sebuleni. Mezani kulikuwa na vikombe viwili vikubwa vilivyobebelea kahawa nyeusi ikifuka moshi. Pembeni kidogo ya vikombe hivyo kulikuwa na magazeti mawili yamejiweka hapo kana kwamba nayo yanafanya kikao.
Mtemvu alishika tama asionekane na dalili za kunywa wala kutaka kahawa. Inspekta alikuwa amekunja nne, mguu wake ulio juu akiutikisa tikisa kwa mbali. Taratibu yeye alikuwa anapeleka kahawa mdomoni akiinywa kwa tahadhari asiunguze mdomo.
“Yani sina amani kabisa. Nashindwa kufanya kazi zangu kwasababu ya kuwindwa mithili ya swala. Sijui nifanye nini?” Mtemvu alilalama akitikisa kichwa.
Inspekta alipeleka kwanza kahawa mdomoni ndipo akafungua kinywa;
“Usihofu, mkuu. Mimi nipo na nitajitahidi kadiri ya uwezo wangu kukuhakikishia usalama. Muda si mrefu nitawatia nguvuni kuna mipango nimekwishaipanga na nina uhakika lazima watanasa. Ninachokuomba tu ubaki nyumbani kwa majuma mawili. Yanatosha sana kumaliza kazi yangu.”
“Nitajitahidi kwa hilo, Inspekta. Sina mahala pa kwenda sasa tangu rafiki yangu pekee aliyekuwa amebakia, Pius, naye kuvamiwa na kuwawa.” Mtemvu alisema akiongezea:
“Ila nashukuru sana, Inspekta, hata hivyo unajitahidi sana. Naomba uwatie nguvuni hao watu haraka iwezekanavyo. Kuendelea kwao kuwa huru ni hatari kwa usalama wangu na wa watu wengine pia.”
“Ondoa shaka.” Inspekta Vitalis alisema kisha akanywa fundo moja la kahawa.
“Ila mkuu, nadhani huu ni wakati muafaka wa kunijuza kinaga ubaga kwanini mtoto wa rafiki yenu ahangaike kutaka kuwaua. Kuna nini kati yenu?” Inspekta Vitalis alidadisi.
Mtemvu alimtizama Inspekta alafu akajilazimisha kutabasamu. Kwa mara ya kwanza alinyanyua kikombe cha kahawa akanywa fundo moja.
“Sijajua kwanini. Mimi na baba yake tulikuwa marafiki mno tuliosaidiana kwa kila njia. Mpaka baba yake anakufa mie nilikuwa pembeni ya kitanda chake.”
Inspekta alitulia kwanza. Alikunywa mafundo matatu ya kahawa kisha akauliza:
“Unamkumbuka Jeniffer?”
Mtemvu akatikisa kichwa.
“Yes. Si yule mtoto wa K square aliyechora picha ya muhalifu?”
“Ndiye huyo.”
“Enhe …”
“Nilipata wasaa kidogo wa kuongea naye. Aliniambia muuaji kabla hajafanya mauaji, alidai amekuja kuchukua roho ya K square kama wao walivyoichukua roho ya baba yake, Malale. Unasemaje kuhusu hilo?”
Mtemvu alipaliwa na kahawa. Alikohoa kwa muda kidogo kusafisha koo lake kabla hajatia neno:
“Unajua vijana wa siku hizi sijui wamerukwa na akili. Sijui wanakula nini kinatibua bongo zao – nadhani ni bange tu. Miraji hajui aongeacho. Puuzia hayo maneno, fanya kazi yako. Umesikia Inspekta? Masikio hayalali njaa. Utasikia ya kila aina.”
Mtemvu alisema kwa mkazo kisha akanywa fundo la mwisho na kuaga anaelekea chumbani atarudi punde.
Inspekta alikunywa fundo moja akabinua mdomo wake akitikisa kichwa.
“Kuna kitu hakipo sawa.” Alisema na kuongezea:
“Ni lazima nijue.”
Muda mfupi mbele, Mtemvu alikuja akiwa amevalia suti wakaondoka na inspekta Vitalis kuelekea kituo cha polisi. Huko Mtemvu alikutana na Bernadetha aliyekuwa rumande, akaomba faragha apate kuongea naye.
“Unataka nini kwangu? Bado hujatosheka, sio?” Bernadetha aliongea kwa jazba.
Mtemvu alitabasamu akamwambia:
“Sijaja hapa kuzozana na wewe, Bernadetha. Ila nimekuja kukusaidia,”
“Wewe mwanahayawani unisaidie mimi?” Bernadetha alijikuta akitabasamu.
“Unataka kuonana na wanao, ama hutaki?” Mtemvu aliuliza. Bernadetha akamtizama kwa macho ya husda.
“Kama ukitaka kunijua mimi ni nani, gusa watoto wangu. Nitahakikisha nakuanika uchi hadharani!”
Mtemvu alitabasamu akitikisa kichwa.
“Nimekuambia sijaja kuzozana. Nataka nikuache uende ukakutane na familia yako. Hujammisi mwanao, Marietta? Je Miraji?”
Bernadetha alinyamaza kimya. Mara akaanza kulia.
“Shhh! Usilie. Nipo tayari kukupa nafasi nyingine ya kuonana nao.”
“Unataka nini, kwangu?” Bernadetha aliuliza. “Najua kuna kitu unataka, nini hiko?”
“Sasa hapo umeongea.” Mtemvu alisema akitikisa kichwa.
“Let us make a deal. Nakuachia huru ukaonane na wanao, ila kwa masharti mawili.”
Mtemvu aliweka kituo ameze mate, alafu akaendelea:
“Kwanza, ufunge mdomo wako kabisa. Sitaki kusikia unasema chochote kuhusu mimi na mumeo kwa yeyote yule. Pili, umwambie mwanao, Miraji, aache kunifuatilia, nami nitajitahidi kufanya sakata lake lipotee pasipo watu kugundua. La sivyo nitampotezea mbali kimya kimya. Tumekubaliana?”
Bernadetha hakujibu. Alimtizama Mtemvu na macho mekundu ya hasira.
“Tumekubaliana ama niondoke usiione familia yako milele?”
Bernadetha kimya. Mtemvu aligeuka akatishia anaondoka, mara Bernadetha akamuita.
“Sawa, nimekubali.”
Mtemvu akatabasamu na kuonya:
“Endapo utakiuka tulichokubaliana, nitakufanya kitu mbaya hutonisahau maishani mwako. Umesikia?”
Bernadetha hakujibu. Aliishia tu kumtizama Mtemvu kana kwamba anataka kummeza. Mtemvu alitabasamu akamuaga akimuahidi kutimiza walichoadhimia.
******
Muendelezo soma hapa