SURA YA KUMI NA TISA
Asubuhi iliwasili. Siku ilikuwa kavu isiyo na dalili zozote za kunesha. Anga lilikuwa na rangi ya bahari, mawingu yakijitengeneza umbo la mawimbi.
Mbele ya nyumba ya Mtemvu, ilisimama gari dogo nyekundu Toyota Vitz. Mlango ulifunguliwa akatoka mzee mrefu mweusi mwenye ndevu nyingi na kiwaraza kikali akiwa amevalia kaunda suti ya kijivu, mkononi akibebelea rambo kubwa nyeusi. Moja kwa moja mzee huyo alifuata geti akabonyeza kengele.
Mlinzi alifungua kidirisha kidogo kilichopo kwenye geti akamtazama.
“Nikusaidie nini?”
“Samahani. Naitwa Ali wa Fatuma. Nina shida ya kuonana na mwenye nyumba.”
“Shida gani?”
“Za kibiashara.”
“Zipi?”
“Ni mambo binafsi.”
“Yapi?”
“Ndugu, ambacho hatuelewani ni nini? Mwambie bosi wako kuna mgeni anaitwa Ali wa Fatuma, yupo nje anamsubiri.”
“Ametoka.”
“Ameenda wapi?”
“Kwenye biashara zake.”
“Zipi?”
“Ni mambo binafsi.”
Ali wa Fatuma alitikisa kichwa akitabasamu.
“Wewe ni mgeni hapa, enh?” Aliuliza na kuendelea: “Si bure ndio mana huna adabu. Mwambie mama Mtemvu, Ali wa Fatuma yupo nje. Tusigombane bure.”
Mlinzi alimtizama mgeni yule kuanzia juu mpaka chini akatikisa kichwa. Aliondoka akimuacha Ali wa Fatuma nje ya geti, baada ya muda akarudi na Mama Beatrice.
“Ndio huyu hapa!” Mlinzi alimnyooshea kidole Ali wa Fatuma kana kwamba anamshtakia.
“Ooh Mtaalamu!” Mama Beatrice alilipuka kwa furaha. “Karibu! karibu sana!”
“Ahsante, mama.”
“Wewe! Ebu fungua geti!” Mama Beatrice alimuamuru mlinzi, haraka geti likafunguliwa mgeni akaingia.
Ali wa Fatuma alimtizama mlinzi na jicho kali asiseme kitu. Mlinzi alinywea kana kwamba amemwagiwa maji ya baridi.
“Mtaalam, umeacha gari leo?”
“Kuna mtu analitumia, amenishusha hapa na kwenda zake.”
“Oooh! Karibu bwana.” Mama Beatrice alisema akifungua mlango. Waliingia wakaketi sebuleni.
“Unapendelea kinywaji gani, mtaalam?”
“Nashukuru, wala usijichoshe mama. Mzee nimemkuta?”
“Hapana. Vipi hujawasiliana naye?”
“Simu yangu imeharibika kioo jana baada ya kuikalia hivyo nilishindwa kabisa kumtaarifu. Lakini anafahamu kwamba ningekuja, niliwaambia wasinifuate, nitawafuata mwenyewe.”
“Basi wacha nimpigie.”
“Itakuwa vema.”
Mama Beatrice alienenda chumbani baada ya muda kidogo akatoka akishikilia simu mkononi.
“Anakuja.” Alimpa taarifa Ali wa Fatuma ambaye alitikisa kichwa kwa mapokeo.
Ndani ya muda usiozidi robo saa, Mtemvu alitia mguu ndani. Tabasamu lake lilikuwa pana alipomuona mgeni, walikumbatiana kwa furaha wakaketi kwa karibu. Mwanamke akawapa faragha.
“Kama nilivyokueleza juu ya tatizo letu. Tumekuwa watu wa mikasa mikasa na sisi, hatupati usingizi vizuri, hatuli kikashuka kabisa!”
Ali wa Fatuma alicheka akitingisha mabega yake. Aliponyamaza aliweka uso wa kutisha kama vile si yeye aliyetoka kukenua.
“Tatizo lako limeisha!” Alisema kwa kujiamini, “Alimradi Ali wa Fatuma ameshafika, tatizo lako limekwisha!” alisema huku akitikisa kichwa kwa uhakika.
“Nitashukuru sana, Mtaalam. We niambie tu nini vinahitajika, mimi nitakupatia.”
“Sawasawa.” Ali wa Fatuma aliitikia.
Alifunua rambo lake akatoa vibuyu viwili, moja kikubwa na kingine kidogo. Alitoa mkia wa ng’ombe akauweka pembeni kisha akatoa na kaniki nyekundu na nyeupe zikifuatiwa na kioo cha saizi ya kati.
Alisimama akajivesha kaniki yake. Aliendea kona ya nyumba akasimama hapo mkononi akishikilia mkia wa ng’ombe ambao aliupeleka kushoto na kulia, kulia na kushoto. Baada ya hapo alipangusia makalio yake hapo na kusimama akiwa anarusha rusha macho yake kama vile anatafuta kitu kinachotambaa kwenye dari.
Alitikisa kichwa akisonya. Alifuata kioo chake akakipangusia na mkia wa ng’ombe, akawa anakitizama.
“Bwana Mtemvu, huyo mtu anayekusumbua ndie huyu?” Ali wa Fatuma aliuliza akimuoneshea Mtemvu kioo.
Mtemvu alitizama macho akajikuta akiropoka: “Ndiye yeye huyo huyo!”
Ali wa Fatuma akacheka.
“Matatizo yako yamekwisha. Nilikuambia.”
“Sasa mtaalam nilikuwa nataka kujua. Huyo mtu katumwa na nani?”
“Ili tupate kujua mengi inabidi tutoe kafara. Kuku mweupe anahitajika kwa ajili ya kujua nani kamtuma na mbuzi mweupe kwa ajili ya kumdhibiti.”
“Hilo halina shida. Lini sasa?”
“Hata leo kama inawezekana.”
“Sawa! Basi ningoje hapa mtaalam nika …”
Simu ya Mtemvu iliita. Aliitizama akapokea.
“Eeenh shem, habari yako? … Mmevamiwa? Usiku huu wa kuamkia leo? ... He! Wewe! … Nakuja nakuja! Sasa hivi!”
Alikata simu akamgeukia Ali wa Fatuma na uso wenye mashaka na woga akamtaarifu aliyopashwa kwenye simu.
“Naomba urudi kesho. Sina jinsi tena kwa sasa.”
Ali wa Fatuma aliridhia. Mtemvu alimkabidhi noti kadhaa nyekundu kisha akamuita mke wake na kumpa taarifa alizozipata. Akaaga na kwenda zake.
“Inspekta, upo wapi? ... Naelekea kwa Raheem, ameuwawa jana usiku na majambazi … Basi nakupitia hapo muda si mrefu … Sawa.”
Simu ikakatwa na kurushiwa kwenye kiti jirani.
Dakika chache kupita gari likazima katikati ya barabara. Mtemvu alishuka akafungua boneti asione tatizo. Alipiga tairi teke akilaani. Alifungua mlango wa gari akachukua simu yake. Alikuta ujumbe umetumwa na namba ngeni muda mfupi uliopita:
‘Sasa kuna mawakala wawili wa kifo. Jiandae vema kwa yeyote atakayekutangulia.’
Alimaliza kuusoma huo ujumbe, ghafula gari kubwa aina ya Scania likabamiza nyuma ya gari lake kwanguvu. Mtemvu alirushwa mbali vioo vikimfuata na kumchana chana.
Gari lake liliserereka kwa kusukumwa na Scania, likaenda kubamiza gari lingine kwa mbele.
Ni kama vile maigizo yakitukia mbele ya macho ya Mtemvu. Alijaribu kunyanyuka lakini ghafula mkono ulimzuia tokea nyuma.
“Tulia kwanza mzee.”
Alikuwa ni kijana mwembamba aliyevalia hovyo, mdomoni mwake akibebelea sigara.
Ndani ya muda mfupi, watu walisogea na kujaa eneo la tukio. Mtemvu aliwekwa katikati ya umati akidhaniwa amechachawa na ajali. Mashahidi walisogelea Scania kumtizama dereva ila hawakumkuta.
“Ameshakimbia!”
“Ametokea wapi?”
“Sijui! Labda dirishani!”
“Vipi mzee unajisikiaje?” Shahidi mmoja alimuuliza Mtemvu kama aliyeguswa.
“Ni mgongo tu unanivuta kwa maumivu.” Mtemvu alijibu akijikanda mgongo. Mara akajipapasa mifukoni.
“Simu yangu? ... Kuna yeyote amenionea simu yangu?”
Hakuna aliyejibu. Watu wengine walianza kuondoka eneo la tukio.
Mtemvu alinyanyuka akafuata gari lake akishikilia kiuno chake na kujikongoja. Kabla hajalifikia alirudishwa alipotoka na mlipuko mkali!
Gari lake liliwaka moto kama kifuu. Kwa haraka lilianza kuyaambukiza magari mengine yaliyo karibu – eneo likageuka tanuru. Makelele na mayowe yakarindima. Kila mtu alikimbilia alipopahisi yeye ni salama.
Hapo ghafula Mtemvu alikurupuka akihema kwa pupa. Kumbe alikuwa anaota. Bado alikuwa ndani ya gari lake lililozima.
Alitizama kwenye kochi la pembeni akaona simu yake, aliichukua akaitizama. Mara ikaita namba kwa namba ngeni. Mtemvu aliitizama bila ya kuipokea. Simu ikakata.
Iliita tena na tena, badala yake Mtemvu aliamua kuizima kabisa. Ajabu ikaita tena! Mtemvu alikodoa macho ya mshangao. Alitoa betri akaitenganisha na simu, ajabu simu ikaendelea kuita.
Aliinyanyua akairushia nje kisha akafunga kioo. Alihema juu juu macho akiyakodoa kwa kutoamini. Kama vile haitoshi, simu iliita tena! Mara hii sauti ikitokea viti vya nyuma.
Mtemvu aligeuza shingo kutizama akamkuta mtu mwesu ti akiwa amejivika joho. Mtu huyo alimdaka koo kwanguvu akamminya. Mtemvu akahangaika mno kutafuta hewa bila ya mafanikio. Macho yalimtoka na mishipa ikamsimama. Alijua sasa kifo chake kimewadia japokuwa bado alikuwa mgumu kukubali.
Ilikuwa ni kama bahati, Inspekta akawasili hilo eneo kana kwamba alitaarifiwa kinachoendelea. Alijaribu kufungua milango ya gari la Mtemvu kwa nguvu zake zote bila ya kufanikiwa. Alichungulia ndani akamuona Mtemvu anazidiwa na isingechukua muda zaidi ya dakika moja tu apoteze uhai.
Alipiga ngumi kioo cha mlango wa gari akakivunja kisha akafungua mlango kwa ndani. Mtu mweusi akapotea kufumba na kufumbua.
“Mkuu, upo sawa?”
Koh! Koh! Koh! Mtemvu alikohoa akijitahidi kutafuta hewa kwanguvu. Inspekta alitizama kushoto na kulia, nyuma na mbele. Honi za magari zilikuwa zinaita, magari mengine yaliwavuka yakipita pembeni.
Baada ya Mtemvu kuvuta hewa ya kutosha, Inspekta alimtazama akamuuliza:
“Nini kimetokea?”
Mtemvu alibung’aa kama mtu mtu aliyeshushwa katikati ya jiji asilolijua. Alifagia uso wake na kiganja mara mbili, akamtizama Inspekta.
“Tuondoke!” Aliropoka. “Tuondoke hapa, Inspekta!” Inspekta akamshika mkono.
“Naomba niendeshe, Mkuu. Tafadhali.” Inspekta alipendekeza. Alijiweka kwenye kiti cha dereva akakanyaga mafuta, gari likasonga mbele kinyume kabisa na hapo mwanzo lilipogoma.
“Tunaelekea kwa Raheem kama kawaida, Mkuu?”
“Ndio. Tuelekee huko.”
Kisha kimya kikatawala miongoni mwao.
Walifika kwenye nyumba ya Raheem wakakuta watu tayari wamejazana. Walishuka wakaungana na kadamnasi.
Mtemvu alimfuata mke wa Raheem kumuuliza kilichotukia. Muda mfupi, Pius na K square nao wakafika eneoni kuungana na jumuiya ya waombolezaji. Wakati huo Inspekta alikuwa ameketi, lakini macho yake yalikuwa yamesimama yanatembea huku na huko kutizama usalama.
Haukupita muda mrefu, Pius, K square na Mtemvu wakaitana kando kuteta. Ilikuwa siri, hata Inspekta hakuhusishwa. Macho yao yalikuwa yanazurura mara kwa mara kutizama na kuhakikisha kama kweli wapo wenyewe.
“Mke wake amesema walivamiwa na mtu wasiyemjua. Hajachukua chochote zaidi ya kumuulizia na kumuua Raheem.” Mtemvu aliwaambia wenzake.
“Mmmh.” K square akaguna. “Jamani, mbona tunaishi kwa hofu hivi? Huku mambo ya ajabu huku majambazi! Roho zipo mkononi! Tutapona kweli?”
“Vipi kumhusu mtaalamu?” Pius aliuliza. K square akatikisa kichwa kama mtu aliyependezwa na hilo swali.
“Mtaalamu yupo.” Mtemvu alijibu. “Nimemuambia aje kesho nyumbani. Alikuja leo lakini taarifa za msiba zikaingilia kati.”
“Hawezi akaja hata hiyo kesho!” K square alitamka. “Itabidi tuwe tunashughulikia mazishi ya Raheem. Labda umwambie aje keshokutwa.”
Baada ya mabishano kidogo, walikubaliana juu ya hilo.
“Ila mnahisi ni nani atakuwa kamuua Raheem? Kuna mtu yeyote aliyekosana naye?” K square aliuliza.
“Sijui!” Mtemvu akajibu. “Sina taarifa yoyote juu ya hilo. Una ufahamu wowote kuhusu hilo?” Mtemvu aliuliza huku akimtazama Pius.
“Hapana. Sina.” Pius alitikisa kichwa. “Unajua Raheem si mtu wa kuweka wazi sana mambo yake. Ni mtu wa kujivuna muda mwingine. Huwezi jua alikuwa na maadui gani.”
“Ila hao maadui hawana uhusiano wowote na sisi?” Mtemvu aliuliza. Walitizamana kwa macho ya viulizi. Hakuna mtu aliyejibu swali. Mwishowe walifikia makubaliano kama ya awali, kuongeza ulinzi miongoni mwao lakini mara hii wakingojea ya mtaalamu.
****
Muendelezo soma hapa