***SURA YA MWISHO***
MTUNZI: Stevie Mollel
No: 0685 758 123
Jua la siku hiyo lilikuwa kali kupitiliza. Wakati ikiwa tu ni saa sita, tayari miale yake ilivuma kiasi cha kukufanya uwe na sababu mujarabu ya kubebelea mwamvuli, kuvaa shati jepesi na kaptula.
Ilikuwa kinyume kabisa na siku za nyuma ambapo kaubaridi kalitawala kwa mujibu wa majira ya mwaka. Jua lilikuwa linaonekana kwa wazi saa saba na saa nane mchana kabla ya tena kupotezwa na mawingu mazito yaliyotawala anga. Labda kibahati ungekuja kuliona majira ya jioni likizama huku likirandana na sifa yake ya kugeuza anga jekundu.
Siku hiyo ilikuwa tofauti. Tunaweza kuhitimisha kwa kusema hivyo. Lakini kipi kilichofanya ikawa tofauti?
Ndani ya majira ya saa kumi na mbili asubuhi pasingekuwepo na kiumbe ndani ya jiji la Hamilton ambaye angeweza kubashiri siku hiyo. Ilikuwa ni kama siku zingine za kawaida. Manyunyu yalikuwa yanadondoka. Baridi likishika kila kona. Lami ilikuwa imelowana na kama ungetoka nyumbani kwako pasipo kubebelea chanzo cha joto, watu wangekuona mgonjwa. Na ilikuwa hivyo mpaka saa tatu ya asubuhi.
Lakini haikuwa hivyo kuanzia hapo na kuendelea.
“Samahani sana, Rajul.” Alisema Vitalis akimtazama Rajul aliyekuwa amefungwa kamba mwili mzima. Si kamba za kawaida, bali zile nene zikiwa zimeshindiliwa na kukazwa vizuri. Pembeni ya Stanis alikuwa amesimama Stanis mkononi akibebelea bilauri la kioo, wote walikuwa wanamtazama Rajul kwa uso wa huruma. Wote walikuwa wamesimama kwenye ardhi ya juu ya fukwe upepo ukiwapuliza.
Rajul ambaye alikuwa na macho mekundu, alikuwa amelazwa au amejilaza kwenye uso wa fukwe hiyo ya bahari asionekane kujitambua. Uso wake ulikuwa mweusi. Nywele zake zilisimama wima. Mdomo wake ulikuwa unachuruza mate macho yake yakimimina damu. Mishipa ilikuwa imemsimama usoni na jasho likimtiririka pia.
Si tu kwamba alionekana mithili ya mwendawazimu, alionekana kama shetani. Alikuwa ananguruma kama simba dume akionekana ana uchu wa nyama.
Stanis alitazamana na Vitalis kisha akaliendea jiwe kubwa lililokuwa pembeni. Alilifunga jiwe hilo na kamba na kulifungia kwenye shingo ya Rajul kwanguvu. Rajul alihangaisha kichwa chake huku na kule mwishowe akamng’ata Stanis kidole cha mwisho.
Damu zilimchuruza Stanis wakati Rajul akijilamba kana kwamba mwehu. Stanis asijali sana, alimalizia kazi yake.
Baada ya kulifunga jiwe hilo, Stanis akatazamana na Vitalis. Ni kama vile walipeana ishara, Vitalis akaweka bilauri chini wakambeba Rajul na kumrushia baharini. Walipofanya hivyo waligeuza migongo yao wasione Rajul anavyozama.
Kama kipande cha chuma, mwili wa Rajul ulizama majini ukichukua dakika moja kugota sakafuni mwa bahari. Mwanaume huyo alihangaika kujikwamua asiweze abadani. Alikunywa maji na kukosa hewa. Alihangaika ndani ya kamba zake kama samaki nchi kavu. Macho yalimtoka na aliachama mdomo ambao kwa bahati mbaya badala ya kumpa hewa ukamnywesha maji. Ilipopita dakika moja, akatulia tuli.
Alikuwa ameenda.
Ilikuwa ni saa tatu na dakika ishirini na tano.
Mawingu yalitawanyika na kuliacha jua uchi. Hali ya hewa ikabadilika kabisa.
“Yamekwisha.” Stanis alisema.
“Naam, naona yameisha.” Vitalis akaitikia na kuongezea. “Sasa tumebakia wanadamu pekee.”
Stanis akatazama saa yake ya mkononi na kusema:
“Tufanye upesi. Si unajua ratiba inatutaka mida ya mchana tuwepo eneo la tukio?”
Walifuata chombo chao cha usafiri – lile gari walilohangaika nalo na kulichakaza jana yake. Walikwea ndani ya gari hilo na kutimka upesi. Walifuata barabara wakakomea kwenye makazi ya zamani ya Stanis. Huko walijiweka sebuleni na kuanza kusuka cha kufanya ndani ya jumba kubwa la Kim.
Ramani ikiwa mezani walielekezana wapi pa kuingilia na pa kutokea. Ufahamu mdogo wa Vitalis juu ya jengo hilo ukapanuliwa na Stanis aliyemdadavulia kila korido, kila chumba asiache hata kitu kikielea.
Kisha hapo Stanis akaenda chumbani kwake na kusogeza kitanda pembeni. Sakafu mwa uvungu wa kitanda akapandakamiza na mguu wake pakatengeneza shimo. Humo ndani alitoa vidude vitano vyeusi vya pembe nne na rimoti yake. Alitabasamu akivitazama vitu hivyo kabla hajarudi sebuleni kukutana na Vitalis.
Sasa ulikuwa ni muda wa kutenda.
Wakiwa na pesa walizokabidhiwa na Rajul kabla hajapata kunywa dawa ndani ya bilauri, waliendea kununua visu vingi na vibegi vya kubebea visu hivyo. Hawakuona umuhimu wa kuwa na bunduki. Kudhamiria kufanya mambo yao kwa ukimya kuliwachangia wasipate presha kubwa ya kutafuta silaha hiyo ya moto. Haikuwa mipangoni.
Walivitia visu hivyo kwenye gari wakatia moto chombo na kuondoka. Ndani ya dakika chache wakawa karibu na jengo kubwa la bwana Kim. Waliruka ukuta wakazama ndani, vibegi begani. Kwa maelekezo ya Stanis walifuata jengo hilo wasionekane.
Walielekea chumba cha kuongozea na kutizamia kamera zilizosambazwa karibia maeneo yote ya jengo. Huko walimnyonga mwanaume aliyekuwemo humo kisha wakatazama jengo zima.
Kwa mujibu wa video za kamera hizo wakajua wapi pa kupita na wapi pa kupaacha. Ila pia wakaelekezana zaidi kwa msaada wa picha zitembeazo.
“Kila kitu kwenye hili jengo kinaendeshwa na umeme.” Stanis alisema huku akitazama video za kamera.
“Umeona hapo? Hapo ndipo zilipo stoo za utunzaji wa silaha.” Stanis alionyeshea video moja kiooni. “Ndipo napotakiwa kupachika mabomu haya niliyoyabeba.”
Akaonyeshea video nyingine.
“Hii ni mojawapo ya maeneo mateka wanapofungiwa. Haipo mbali saana na stoo za silaha na uwanja wa mateso. ”
“Sasa tukilipua maeneo hayo, mateka hawawezi wakauwawa?” Vitalis aliuliza.
“Hapana.” Stanis akajibu. “Umbali huo si wa karibu kiasi hiko.”
“Lakini vipi kama tukiwafungua mateka hao ndipo tukapambane na Kim?” Vitalis aliuliza.
“Tummalize kwanza Kim.” Stanis akajibu msisitizo kisha akaongezea: “Unajuaje kama hao mateka watakuwa hoi kwa kupewa mateso. Wanaweza wakawa mzigo tukashindwa kuhitimisha kazi.”
Kwa namna moja ama nyingine ikamuingia Vitalis kichwani.
“Hawatokuwa wameuwawa?”
“Hapana. Kim si mtu wa kuua upesi kiasi hiko, tena watu ambao anajua anaweza akawatumia kutimiza jambo lake fulani. Alisita kuniua mimi kwasababu tu ya kunitumia kama sampo ya kuwafunzia wengine.”
Walikubaliana wakatoka ndani ya chumba hicho na kufuatisha maeneo yale waliyoyaona ni salama. Korido waliyoichukua waliifuata kwa hatua thelathini kabla hawajakata kona ya kushoto. Huko napo walitembea hatua chache kabla hawajakata kona ya kulia.
Wakamuona mwanaume mmoja akiwa anafungua chumba. Alikuwa mfupi ila aliyejaza misuli kiasi cha kubana shati lake jeusi alilolivaa.
Kabla mwanaume huyo hajakukuruka kufanya kitu, Vitalis alichomoa na kurusha kisu kilichotoboa koo la mwanaume huyo na kumdondosha chini kama mzigo.
Walimjongelea upesi wakafungua kile chumba na kuufungia mwili huo ndani. Kabla ya kuendelea na safari yao, Stanis alibandika vile vidude vyeusi viwili ndani ya chumba hicho kisha wakaendelea na korido hiyo kwa hatua kama kumi. Walipotaka kukata kushoto, walisita upesi, walisikia sauti za watu zinakuja.
Walijibanza na kuwangojea watu hao ambao walichukua sekunde kama kumi kuwafikia. Walikuwa wawili kwa idadi. Walikuwa warefu wenye miili iliyojaza. Mmoja alikuwa mweupe ya uzungu wakati mwingine akiwa chotara.
Walidakwa wakakatwa shingo wakifunikwa midomo, kisha wakaachwa hapo Stanis na Vitalis wakaendelea na safari yao.
Walitembea hatua chache tu ndani ya hiyo korido kabla hawajakumbana na wanaume watano waliotokeza ghafula konani. Upesi wanaume hao walipata kuona wenzao waliouwawa umbali wa hatua kadhaa hivyo haikuwia vigumu kukokotoa wale walipo mbele yao walikuwa ni maadui, tena hesabu hiyo ilirahisishwa zaidi kwa uwepo wa Stanis.
Walitazamana kisha wakawafuata maadui zao kwa mkupuo.
Wepesi ulikuwa ni kwamba wanaume hao hawakuwa na silaha yoyote.
Stanis na Vitalis walitumia visu vyao vema kuwamaliza kwa urahisi. Ndani ya muda mfupi walitengeneza dimbwi la damu maeneo hayo kwa kuwachanachana na kuwachoma wanaume hao pasi na huruma kisha wakaendelea na safari, ila sasa wakiwa wameongoza zaidi kasi ya mwendo wao.
Wakiwa njiani, Stanis alibandika vidude vyake mpaka pale vilipoisha.
Kitendo cha kuwamaliza wanaume kadhaa na kuwaacha koridoni ilikuwa ni hatari kwa usalama wao ukizingatia bado walikuwa na safari ndefu kufikia ofisi ya Kim, na safari ilikuwa ndefu zaidi kutokana na uchaguzi wao wa njia salama.
Sasa ilibidi wafanye mambo yao kabla maiti zile hazijagundulikana na taarifa ikasambaa kote. Na kuonekana kwa maiti zile si jambo ambalo unaweza sema kwa uhakika litachukua muda fulani, ni muda wowote tu laweza likachafua mazingira!
Walisonga wakapanda ngazi nne. Walikamata korido waliyoenda nayo ndani ya muda mfupi kabla hawajakata kona ya kushoto iliyowaongoza mpaka eneo la kupatia chakula. Lilikuwa ni eneo kubwa lenye madirisha makubwa ya vioo. Humo ndani palikuwemo na watu hamsini ama zaidi kidogo. Miongoni mwao wakiwemo wahudumu na wapambanaji wa bwana Kim waliokuwa wanapata chakula cha mchana.
Kwa mujibu wa saa ya ukutani ndani ya jengo hilo ilikuwa ni saa nane na nusu mchana. Televisheni kubwa iliyokuwemo humo ilikuwa inaonyesha michezo ya olimpiki: watu wakishindana kukimbia, kuruka, kuogelea, kutupa tufe na kadhalika. Watazamaji walikuwa wamegawana watu wa kuwashabikia kwahiyo wakati wanakula macho yao yalikuwa yameganda kwenye kioo cha kideo.
Hiyo ikawa fursa nzuri kwa Stanis na Vitalis.
Muda wa kuingia ndani ya jengo hilo ulikuwa maridhawa. Kama ingelikuwa ni muda mwingine basi bila shaka wangekuta wanaume hao wote ambao wamekusanyana ndani ya jengo hilo wakiwa wanarandaranda huku na kule. Ingekuwa hatari zaidi.
Wakiwa wamechuchumaa wasionekane kwenye madirisha, walipita upesi na korido hiyo kabla mbele ya hatua kama kumi hawajajificha upesi waliposikia sauti ya viatu ikisonga.
Walijibana kwenye kingo moja ya ukuta, akapita mwanamke aliyekuwa amevalia kinadhifu; suti nyeusi na viatu vyenye kisigino kirefu. Alikuwa anatembea kana kwamba hakanyagi chini.
“Ni sekretari wa Kim.” Alisema Stanis. “Anaenda kuchukua chakula chake na cha bosi wake.”
Walitoka kingoni wakaendelea na kutembea.
Baada ya dakika mbili za kujificha kuibuka, waliikaribia ofisi ya Kim. Mbele ya ofisi hiyo walikuwa wamesimama wanaume wawili: wale wanaume wa kazi, wakiwa wamevalia suti na miwani nyeusi tayari kwa ajili ya kufanya kazi zao. Walikuwa na miili mikubwa, mabega na vifua vipana. Walikuwa wamevimba kana kwamba ndani ya muda mfupi wanapasuka. Ingawa walikuwa wanalinda mahali na mtu mwenye mashiko makubwa, hawakuwa na silaha yoyote mikononi. Labda walikuwa wanaamini uwezo wao. Silaha ya nini?
Stanis na Vitalis wasipoteze muda, wakatokeza mbele ya wanaume hao.
“Ni muda sasa wa kujaribu kile alichokisema Rajul.” Alisema Stanis.
Wanaume wale wawili waliwafuata Stanis na Vitalis kwa mbio, ila kabla hawajafika walikutana na visu njiani vilivyokita na kuzama kifuani, ni mipini tu ndiyo ilibakia nje.
Wanaume hao wa kazi wakistaajabu hayo ya Musa, walidondoka chini habari yao ikaishia hapohapo.
Kabla Stanis na Vitalis hawajasogeza miguu, ving’ora vikaanza kuita!
“Hata hivyo tuna bahati!” Alisema Vitalis.
Haraka waliufuata mlango wa ofisi ya Kim, Vitalis akamwambia Stanis:
“Lipua!”
“Bado.” Stanis akajibu. “Watakuwa ndio wapo njiani kufuata silaha zao.”
Ni kweli. Wanaume wale waliokuwa wanapata mlo waliacha mara moja walichokuwa wanakifanya wakakimbia kuelekea kwenye stoo zao za utunzaji wa silaha punde tu baada ya kusikia king’ora. Sio wao peke yao tu, ikiwemo pia na wengineo waliokuwa wanarandaranda.
Stanis na Vitalis walivunja mlango kwa mateke ya nguvu, uso kwa uso wakakutana na Kim. Mkononi alikuwa amebebelea bunduki yake ndogo lakini uso wake ukijawa na woga.
“Sta – nis!” Kim alishangaa. Alimtazama na Vitalis akabakiwa ameachama mdomo kana kwamba anatafuta cha kusema.
Stanis, kwa siri asionekane, alibonyeza kitu kilichokuwa mfukoni mwake. Ghafla milipuko kikubwa ikasikika! Jengo lilitikisika likipitia tetemeko kubwa la ardhi.
Wanaume wale waliokuwa wanajihudumia silaha stoo hawakutoka salama hata kidogo. Aidha walipokonywa uhai wakitawanywa vipandevipande ama walibakizwa wakiwa na majeraha makubwa.
Ofisi ya Kim iligeuka shaghalabaghala. Alikuwa ameinama baada ya kusikia tetemeko hilo. Alipotazama awaone maadui zake waliokuja kudai roho yake, alikutana na kisu kilichotoboa mkono wake uliobebelea bunduki. Bunduki ikadondoka chini.
Sasa alikuwa analia kwa maumivu machungu aliyokuwa anayasikia.
Stanis alichukua bunduki ndogo ya Kim kisha kwa kushirikiana na Vitalis wakamtwaa mlengwa wao huyo na kumpeleka uwanja wa mateso walipomfunga kamba kwenye mstimu, kama vile alivyoamuru Stanis afanyiwe kipindi cha nyuma.
Walipomaliza kumfunga, walisogea mbali kwa hatua kadhaa wakipuuzia sauti ya mwanaume huyo iliyokuwa inapaza kuomba msamaha huku machozi yakimtiririka.
Walimtazama kwa sekunde kadhaa, Vitalis akatikisa kichwa chake alipokumbuka yale yote aliyoyapoteza kwasababu ya mwanaume yule.
Alijikuta anabinua mdomo wake, akafoka:
“Huwezi ukafa kirahisi Kim. Japokuwa hauwezi kusikia maumivu yale yote uliyoyasababisha juu ya ulimwengu huu, basi angalau kuyasikia kwake kidogo kutanipa ahueni ya moyo.”
Aliposema hayo alimtazama Stanis.
Ajabu akamkuta mwanaume huyo amemnyooshea mdomo wa bunduki.
“Samahani sana, Vitalis.” Alisema Stanis. “Inabidi nifanye hivi.”
Ghafla uso wa Vitalis ukanywea. Macho yalikuwa mekundu na mdomo wake mkavu ukaachama kabla hajajikuta akiuliza:
“Kwanini unafanya hivi Stanis?”
“Kwasababu ya pesa.” Stanis akamjibu kwa wepesi kisha akamuamuru aweke kibegi cha visu chini na kusogea mbali. Vitalis akatii.
Kwa kutumia bunduki yake, Stanis alimuamuru Kim ataje alipoweka nyaraka zake zote za siri pamoja na taarifa za benki kwa ahadi ya kumuachia uhai. Kim akamtajia pasipo kusita.
Alipopata taarifa hizo alirudisha mdomo wa bunduki kwa Vitalis akamtaka asali sala zake za mwisho. Vitalis akatema mate pembeni na kusema kwa kiburi.:
“Niue wewe malaya msaliti. Unasubiri nini?”
Stanis akacheka.
“Nilipokuwa nasikia matendo yako, nilidhani una akili sana, kumbe hamna lolote! Nimefanikiwa kukupata kwa akili ndogo sana. Ndogo sana!”
Akacheka tena.
“Okay, tuanze mwanzo kwanza. Tokea mara ya kwanza nilipokuona nilijua sasa ndoto zangu zinaenda kutimia kwa kukutumia wewe, lakini wewe mwenyewe haukujua, si ndio?”
Akabinua mdomo wake.
“Moja, ulidhani ni bahati mbaya nilipong’atwa na Rajul. Hapana, nilikuwa nimepanga. Ile ndiyo ilikuwa fursa yangu adhimu kupata nguvu nilizonyimwa kwa muda wote huo. Na kupata nguvu zile maana yake naenda kuwa Kim mpya, na bahati mbaya ama nzuri hatokuwepo tena Rajul wakunisimamisha.”
Akabinua tena mdomo wake.
“Pili, nilipokukataza usiwafungulie wenzako kabla ya kumaliza tulilopanga, ulifikiria nini? Haukuona hiyo ilikuwa ni njia rahisi ya kukufanya uwe mpweke nikumalize upesi? Kama kweli uliamini watakuwa waliteswa na wamechoka, kwanini haukuomba hata utizame zile video zilizotunzwa na kamera kwa kurudisha nyuma ili uone? Uliniamini sana, si ndio?”
Akabinua mdomo wake.
“Na tatu basi, ulipoona nimekimbilia bunduki ya Kim uliwaza nini? Bila shaka ulidhani nilifanya vile kwa sababu ya usalama wetu, eti enh?”
Akacheka kwa dharau.
Ila hakuchukua muda uso wake ukanywea. Vitalis alikuwa anatabasamu akishika kiuno.
“Sawa, naona ulikuwa umepanga mengi sana na ukatumia akili nyingi sana.” Alisema Vitalis. “Ila kamwe usidhani huwa naacha akili yangu nyuma ninapopanga jambo, kwahiyo acha na mimi nikukumbushe vitu.”
Stanis akanyamaza kimya akitoa macho.
“Moja, ulinambia kila kitu kwenye jengo la Kim kinaendeshwa na umeme, maana yake hata lile lango la wafungwa pia. Sasa ulivyolipua mabomu yale yote bado ulidhani umeme ndani ya jengo upo? Na kama haupo, maana yake nini? Acha nikusaidie kujibu; maana yake mateka wapo huru. Kwahiyo bado hakukuwa na sababu ya kuhofia ukizingatia ulinipa sababu ya kuamini kwanini watakuwa salama hata baada ya mabomu kulipuka.”
Vitalis akabinua mdomo wake na kuendelea:
“Pili, ulivyokuwa mjinga ukasahau na uliniambia wazi kabisa kwamba sehemu ya mateka ipo karibu na uwanja wa mateso. Kwahiyo ukichanganganya na ile ya kwanza kwamba wateka sasa wapo huru, maana yake watakuwa na uwezo wa kujongea eneo hili kwa wepesi kuliko maeneo mengine. Na sasa mateka hao wapo nyuma nyuma yako umbali si mrefu.”
Stanis akageuza macho yake kutazama.
Hilo likawa kosa.
Kwa kasi ya radi, Vitalis aliinama akachomoa kisu kwenye kibegi na kukirusha kulenga mkono wa Stanis. Pasipo kukosea aliutoboa mkono huo ukadondosha bunduki chini.
Stanis akiwa anagugumia maumivu, alijaribu kuokota bunduki na mkono wake wa kushoto ulio salama, ila nao kabla haujafanikiwa ukatobolewa na kisu kingine kilichorushwa upesi. Sasa akawa analia kwa maumivu makali.
“Tatu, ulivyo zuzu ukaamini ninayoyasema.” Alijigamba Vitalis.
“Sasa kama lango la wafungwa linaendeshwa kwa umeme ndio lifunguke umeme ukikatika?”
Akaacheka kwa dharau.
“Mbali na hayo naomba nikushukuru kwa kunisaidia kupata taarifa nyeti za Kim, pamoja pia na taarifa za benki. Nikutakie usiku mwema.”
Alipomaliza kusema hayo alimkandika Stanis teke zito la kichwa likamrusha mwanaume huyo samasoti kabla hajatua chini kama furushi na kupoteza fahamu.
Baada ya hapo juu ya nini kilitokea huko jiji la Hamilton, Bermuda, kilikuja kusemwa na muda. Vyombo vya habari nchini Tanzania vilieleza kinaganaga picha zikipendezesha majalada.
‘KIM ATOBOLEWA VISU MWILI MZIMA NA KUNYONGWA!’
‘KIM AUWAWA KINYAMA NA WATU WASIOJULIKANA: Kundi la ‘Wageni’ lahusishwa.
‘MWEKEZAJI MKUBWA NCHINI AUWAWA KIKATILI: Polisi washutumiwa kuchelewa kutoa msaada.’
‘MAOVU YA KIM YAANIKWA BAADA YA KUUWAWA KIKATILI: Nyaraka zake zawekwa wazi mitandaoni.’
‘VIGOGO SERIKALINI WAFA KWA PRESHA: Ni baada ya nyaraka za siri za Kim kuwahusisisha.’
Kila nakala ya magazeti hayo ilikuwepo mezani wakati Kaguta akiwa anakunywa chai majira ya asubuhi ndani ya nyumba kubwa ya kifahari.
Alijikuta anakunja sura yake alipoutazama mwili wa Kim kwenye picha mojawapo gazetini kabla hajatikisa kichwa chake na kusema:
“Kitendo cha kumuacha baradhuli huyu akiwa anatambulika kwa kumtazama usoni ni kosa kubwa sana. Sijui kwanini Vitalis alinizuia?”
Akashushia maneno hayo na chai.
Hakukaa hapo muda mrefu Miraji na Bakari wakajiri. Walikuwa wamevalia suti safi nyeusi, tai nyekundu na viatu vya ngozi vilivyokuwa vinametameta.
Kaguta aliwatazama vijana hao vizuri kama anawachambua kisha akatabasamu.
“Mmependeza!”
Mara wakatokea Vitalis na Bernadetha. Vitalis alikuwa amevalia suti taxedo iliyomkaa vema huku Bernadetha akiwa amevalia gauni jeupe lililominya kiuno chake na kujimwaga kwenye nyonga. Alikuwa kama malkia ingawa hakuwa amejipara na pembeni yake Vitalis alionekana kama mfalme.
Kila mtu aliwasifia wamependeza na kushauri kwanguvu nguo hizo zivaliwe siku ya harusi yao.
Wakati furaha hiyo ikiwa imewatawala huku, ilikuwa kinyume kwa Stanis, kule Hamilton, Bermuda.
Hakuwa amekufa, la hasha! Bali alikuwa mwendawazimu asiyeelewa nini anafanya, kula ama kunywa. Alikuwa hivyo punde tu baada ya kuzinduka toka kwenye usingizi mzito aliopewa na teke la Vitalis.
Roho ya mashetani aliyopandikizwa na meno ya Rajul ndiyo pekee ilikuwa imebakia juu ya uso wa dunia ikidai na kushikilia taasisi za Kim.
Na kama waswahili wasemavyo; mtoto wa nyoka ni nyoka, basi ndivyo ilivyokuwa kwa wale wote waliokuwa kwenye makampuni ama mashirika ya baradhuli yule mfu. Waliishia kuchanginyikiwa wakikimbia hovyo. Wengine waliishia kujiua ama kufa kwa kugongwa na magari.
Hakuna aliyebaki salama.
***
☆Steve