***SURA YA KUMI NA TANO***
(MSIMU WA 02)
Ila wakiwa njiani, simu ya inspekta iliita. Alikuwa ni mama Miraji anampigia, inspekta alipokea akaiweka sikioni;
“Haloo … Enh? … Upo sehemu gani? …. Haya sawa nakuja sasa hivi … Hakikisha haukai sehemu yoyote peke yako …”
Simu ikakata.
“Vipi, kuna nini tena?”
“Mama Miraji! … Anasema kuna mtu anamfuatilia kwa nyuma tokea anampeleka mtoto shule! … Embu geuza haraka twende!”
“Wapi?”
“Mbele ya St Marry mbezi beach.”
Haraka gari liligeuzwa na kuanza kwenda Mbezi beach kwa mwendokasi mkali. Wakiwa wamekaribia kufika, inspekta alimpigia simu mama Miraji amuelekeze alipo, mama Miraji akafanya hvyo na ndani ya dakika Kaguta na inspekta wakawa wameshafika mbele ya mama Miraji.
“Yuko wapi?” Inspekta aliuliza kwa jazba.
“Yulee! … Yulee anakimbia! … Anakimbia!” Alikuwa ni mwanaume mwembamba aliyevalia suti. Aliwapa wakina inspekta mgongo huku akikimbia kwa kasi.
“Ingia kwenye gari, haraka!” Inspekta alimuamuru mama Miraji. Mama Miraji aliingia kwenye gari, gari likaondolewa kwa kasi kumfukuzia yule mwanaume akimbiaye. Yule mwanaume alipoona gari lamsogelea aliacha njia kuu akashika vichochoro.
Gari lilisimama kwa breki kali, inspekta akashuka na kuanza kumkimbiza mwanaume yule kwa kasi mno. Ndani ya sekunde chache, inspekta akawa tayari amemkaribia yule mwanaume, alimshika koti akamvuta akampa ngumi nzito ikampeleka mwanaume yule chini na kumvujisha damu puani.
“Wewe nani?” Inspekta aliwaka. Mwanaume yule hakujibu, badala yake alitabasamu na kumuonyesha inspekta ishara ya kidole cha kati. Inspekta alighafirika, alikunja mikono ya shati lake na kuacha tattoo yake wazi, mwanaume yule akaiona. Inspekta alimnyanyua mwanaume yule juu juu kwa staili ya kumkwida. Ajabu mwanaume yule hakuonyesha kupinga lolote, badala yake alipeleka mkono wake ndani ya suruali akawa anakunja na kunyoosha vidole kama mtu ajikunaye.
Ghafla, inspekta alimuacha mwanaume yule na kushika kichwa chake akilalamika maumivu. Mwanaume yule hakukoma, aliendeleza zoezi lake huku akionyeshwa kufurahishwa na ile hali aipitiayo inspekta ya kulalamika kichwa. Baada ya muda, inspekta alidondoka chini akapoteza fahamu. Mwanaume yule akapotea.
“Mbona harudi?” Mama Miraji aliingiliwa na hofu, Kaguta alishuka garini akaenda kumtafuta inspekta. Baada ya dakika kumi alimpata inspekta akiwa amelala hajielewi. Alimuita lakini hakuitika. Alimnyanyua akampeleka garini.
“Mungu wangu! Amefanya nini?” Mama Miraji aliuliza macho yakimtoka.
“Sijui! Tumuwahishe hospitali.”
Gari liliondoshwa kwa kasi na Kaguta kuelekea hospitalini. Inspekta akafanyiwa vipimo, daktari akawapasha majibu hakuna kitu chochote kikubwa alichopata kuona, labda tu mgonjwa alikuwa na uchovu wa jua kali. Kaguta na mama Miraji wakashangazwa na hayo majibu. Walingoja inspekta aamke warushe mashaka yao kwa njia ya maswali. Ikiwa lisaa limepita ndipo inspekta akaamka akirudi fahamuni.
“Vitalis, nini shida?” Kaguta alirusha swali, mama Miraji naye akaonyesha shauku kubwa la kutaka kufahamu.
Inspekta alishika kichwa chake akakunja sura. Macho yalikuwa yamemlegea akionekana kutawaliwa na uchovu. Alimtizama mama Miraji kisha akayarudisha macho yake kwa Kaguta.
“Kichwa kinaniuma.”
“Pole sana, inspekta.” Mama Miraji alisabahi.
“Vipi kwani ilikuaje?” Kaguta aliuliza.
“Sijui hata ilikuaje! … Wakati napambana na yule jamaa kichwa kilianza kuniuma ghafla kwa maumivu makali.” Inspekta alieleza, “Nilishangaa, badala ya yule adui kujilinda na kushambulia, alipeleka mkono wake ndani ya suruali hapo hapo kichwa kikaanza kunikata.”
Kaguta akaguna.
“Uliona alichokuwa anakifanya huko?”
“Hapana. Nashindwa kuelewa ni sayansi gani ilitumika. Tokea nianze mapambano na hawa watu sijawahi kukumbana na kitu kama hiki.”
Walitulia kwa muda kidogo wakifikiria Kaguta akalipuka na wazo; “Tattoo. Itakuwa ni tattoo.”
“Tattoo kivipi?” Inspekta aliuliza huku akirembua.
“Sijui kivipi, ila kwa njia moja ama nyingine itakuwa inahusiana na agano la mchoro.”
Baada ya masaa matatu ya kupumzika na kurudi kwenye hali yake ya kawaida, inspekta akiongozana na Miraji walielekea hospitalini kukutana na Jombi wakiwa wamebebelea chakula vya wagonjwa. Inspekta alimueleza Jombi kila kilichotokea, Jombi akaguna na kumtizama inspekta kwa jicho la mshangao.
“Inspekta, umechorwa tattoo?”
Inspekta na Kaguta wakatazamana.
“Ndio, tumechorwa wote wawili.” Inspekta alijibu na kuuliza, “Umejuaje?”
Jombi akatikisa kichwa chake kusikitika, “hilo huwa linatokea kwa wale tu wanaokuwa na tattoo hiyo. Unapokula kiapo maana yake unaridhia kufanya kazi ya mkuu kwa pamoja. Yeyote anayekuwa na hiyo tattoo hana uwezo wa kumshambulia mwenzake.
Endapo yule anayeshambuliwa atakapokuna au kukwangua sehemu ya tattoo na kufanya ichuruze damu, mshambuliaji atapata matatizo kama hayo yaliyokukuta wewe ukafikia hiyo hali.”
Inspekta aliweka mikono kichwani, “Mungu wangu. Sasa tunafanyaje?”
“Hapo kusema ukweli sijajua.” Jombi alijibu kwa sauti yenye lafudhi ya kukata tamaa, akauliza. “Wamewachora eneo gani?”
“Mkononi.” Kaguta aliwahi kujibu.
“Mkononi? … Kwanini?”
“Hatujui, kwani kuna utofauti wowote?” Kaguta aliuliza kwa pupa.
“Ndio. Kuna utofauti. Kuna wengine huchorwa kiunoni kama sisi, it means tupo grade ya pili. Walio juu yetu wao huchorwa mgongoni. Na wa juu zaidi, wanakuwa na tattoo shingoni.”
“Kwahiyo wewe ungepanda grade inayofuata wangekufuta hiyo ya kiunoni? Au?” Inspekta alipeleleza.
“Hapana, siwezi kufutwa. Hizi tattoo milele hazitoki. Na milele mimi nitabakia grade ya pili. Ni hivi, mtu wa grade ya kwanza ambao ni nyie wanaochorwa mkononi, wao huwa wamelazimishwa, si kwa matakwa yao. Grade ya pili, wanakuwa wameridhia kufanya kazi wakijua matokea yake. Grade ya tatu, ni wale wanaowafunda wote wa chini. Grade ya nne na ya mwisho, ni waanzilishi ama waasisi, mfano Mr Kim.”
“Umewezaje kusema hayo yote na ni ya siri?” Inspekta alidadisi.
“Si siri tena kwenu. Nyie mmekuwa wenzetu, kuwataarifu nyie si kuvujisha siri kwa kuwa nyie wenye agano ndio vinywa vyenu vimeuliza.”
“Naomba nirudie swali, Jombi. Kwanini wewe walitaka kukuua na ingali una tattoo huwezi kutoa siri?”
Jombi alitabasamu kwanza ndio akajibu, “Hiyo ni kawaida. Mtu anapokamatwa na kuwa chini ya adui, sharti auwawe, kwani akishatoa siri haijalishi tu ataangamizwa, bali siri inakuwa si siri tena.”
“Unatushauri tufanye nini sasa, Jombi?” Kaguta akauliza.
“Kama habari yenu ya kuwa na tattoo itakuwa imesambaa kote, hamtokuwa na la kufanya. Lakini kama sio, mnaweza mkaendelea na shughuli zenu. Ila ninachowashauri, kwa sasa inabidi msipige matawi ya miti, anzeni mizizi.”
“Kumaanisha?” Inspekta alidakia.
“Kumaanisha kwamba, nyie mnapambana na matawi ya miti lakini hamtafuti mizizi. Hamuwezi mkawamaliza wafuasi wa Mr Kim nchi hii, kila siku wanazalishwa wapya huko sehemu wanapopewa training. Inabidi muangamize kwanza hivyo viwanda, mengine ndio yafuate.”
“Unaweza ukatutajia hizo sehemu?” Inspekta aliuliza.
“Ndio, naweza nikawatajia. Ila sizifahamu zote, nitakutajia baadhi lakini mkae mkijua zipo kila mkoa wa Tanzania zikiendeshwa kwa siri mno. Kumbukeni hamuwezi mkaripoti hiki kitu popote pale, mkifanya hivyo utakuwa ni mwisho wenu.”
“Sawa. Nina swali la mwisho kwako.” Inspekta alisema.
“Uliza tu.”
“Ni kumhusu yule jitu. Mbona kwa sasa hapatikani? … Yani sioni wala sisikii akifanya mambo yake kama alivyokuwa akiwaendesha wakina Mtemvu. Kwanini watu wa Mr Kim wahangaike ingali jitu yupo?”
Jombi alishusha pumzi ndefu akajitengenezea kitako. Akamtizama inspekta.
“Kwanza awali ya yote, hakuna mtu awezaye kupambana na yule jinni. Ana nguvu mno na akidhamiriacho hakuna budi kutokea. Ila anaendeshwa, na anayemuendesha hupokea amri kutoka kwa mkuu juu ya nini cha kufanya. Mtu anayemuendesha huyo jinni anaishi Bagamoyo, anaitwa Alwatan Kombo, ni mzee maarufu sana ukimuulizia humkosi. Hayo mengine sifahamu.” Jombi alifunguka. Inspekta akaguna,
“Kazi ipo. Sijui hata tunaanzia wapi?”
“Popote pale.” Kaguta alitoa jibu jepesi.
“Ila kama mtahitaji, mnaweza mkaningoja. Tabibu amesema kesho nitaruhusiwa. Naomba niwarudishie fadhila kwa kuwasaidia.”
Inspekta alimtizama Kaguta, Kaguta akawahi kujibu; “Sawa, tutakungoja.”
Maongezi hayo yalipokoma, Kaguta aliwataka inspekta na mama Miraji waende kupumzisha akili zao ufukweni mwa bahari kwa kuwa ni mwisho wa wiki. Mama Miraji akapinga;
“Mimi siwezi, namsubiria mwanangu atoke shule.”
“Oooh! … Haina shida. Mpaka Jombi amalize kula muda muda utakuwa umeshawasili, tutamchukua mwanao alafu twende wote tukasahau ya ulimwengu kidogo.”
Mama Miraji akatabasamu, “Sawa, haina shida.”
Jombi alikula akamaliza, walimpitia pia Miraji kumjulia hali baada ya hapo wakaenda kumchukua Marietta shuleni akabadili nguo wakaelekea ufukweni mwa bahari ya indi. Ndani ya hoteli ya White sand ndimo walipokuwepo. Walipata chakula, kisha wakaenda jilaza kwenye vitanda vyembamba virefu vya ufukweni upepo ukiwa unawapuliza na simuliza za hapa na pale zikipigwa.
“Twendeni tukaogelee!” Inspekta alipendekeza.
“Tutaendaje sasa na hatujaja hata na nguo ya kuogelea?” Mama Miraji alisema, alikuwa amevalia suruali pana na top miguuni akiwa kavalia viatu vya wazi. Inspekta alikuwa amevaa pensi na tisheti jepesi wakati Kaguta akiwa kavalia bukta fupi juu ya magoti. Marietta alikuwa kavalia katop keupe na taiti nyeusi.
“Twende basi hata tukachezee maji tutoe kanuksi.” Inspekta alizidi kushawishi.
“Nyie tangulieni, nakuja.”
“Aaah jamani twendeni bana.” Kaguta alichochea.
“Kweli, nyie tangulieni naja.” Mama Miraji alisisitizia. Inspekta alinyanyuka pamoja na Kaguta, Inspekta akamnyooshea mkono Marietta, mtoto wa mwisho wa mama Miraji.
“Twendee!”
Marietta alimtizama mama yake kama mtu aombaye ruksa, mama akamruhusu aende. Inspekta alimnyanyua mtoto akamuweka mabegani wakayafuata maji. Wakiwa pamoja na Kaguta walichezea chezea maji kwa kurushiana rushiana.
Marietta alikimbia huku na huko wakifukuzana na inspekta. Walirushiana maji, wakalala kwenye michanga na kwenda tena kuoga. Mama Miraji alikuwa amekaa tu akiwatizama tabasamu likitambalia uso wake.
“Twende kwenye maji marefu!” Inspekta alimwambia Marietta huku akitabasamu.
“Akaa naogopa!”
“Kwanini?”
“Si n’tazama!”
“We ulishawahi kumuona mtu anazama?”
“Ndio! Tena kuleee!” Marietta alionyeshea kidole upande wake wa mashariki.
“Leo unaendaaa…!” Inspekta alisema kwa utani, Marietta akaanza kukimbia. Hao wakaanza kufukuzana huku na kule, “Njooo!”
“Sitakiii!”
Inspekta alimkamata Marietta akaanza kumrusha rusha juu juu. Wakiwa katika hilo zoezi, haraka Kaguta alikuja akitokea kwenye maji ya marefu alipokuwa anaoga.
“Vitalis, umeona kule?” Kaguta alielekezea uso wake kule alipokuwa amekaa mama Miraji. Inspekta alitizama akamuona mwanaume amejilaza juu ya kitanda alichokuwa amelala yeye.
“Nani yule?”
“Sijui! Nenda katizame.”
Inspekta alianza kusogea eneo la tukio mtoto akiwa kambebelea mgongoni. Macho yake alikuwa kayarusha kule aendapo akijitahidi kung’amua akionacho.
“Unaenda kumchukua mama?”
“Eeeh na yeye aje kucheza na sisi. Au hutaki?”
“Nataka. Alafu tukimchukua tunaenda kenye maji makubwa?”
“Ndio. Tunaenda kuleee kwa bluu.”
“Kule kwenye maboti?”
“Enhee huko huko!”
“Wewe huogopi?”
“Siogopi mimi.”
“Unajua kuogelea?”
Inspekta alikaa kimya, akili yake ilitekwa kidogo na kumtizama mwanaume aliyekuwa ameketi na mama Miraji kwani alikuwa tayari amekaribia na bado hajamng’amua ni nani hasa.
“Unajua kuogelea? Mbona hunijibu!” Marietta alipaza sauti yakekumuuliza inspekta.
“Eeeh najua kuogelea.” Inspekta alijibu huku akimtua Marietta ambaye moja kwa moja alimfuata mamaye.
“Habari yako?” Inspekta alimsalimu mwanaume yule aliyejilaza; alikuwa na kifua kilichotuna kwa kiasi chake wakati tumbo lake likiwa limepambwa na matuta. Nywele zake ndefu alizitia dawa zikawa zinameta meta.
“Njema tu, vipi?”
“Shwari. Unaweza ukanambia wewe ni nani?”
Mwanaume yule alitabasamu kidogo akalamba lips zake.
“Naitwa Hervey. Au unaweza ukaniita the handsome African. Vipi kwani?”
“Hapo unafanya nini?”
“Nimechil tu na mrembo hapa, kuna ubaya?”
“Wewe kuwa na adabu …” Mama Miraji aliingilia kati, inspekta akamtuliza na kuendelea kuongea na yule jamaa.
“Umechil ukiwa unataka kufanya nini?”
“Aaah bro, maswali gani hayo? Unauliza nini sasa?”
“Jibu swali langu.”
“Kwani vipi kaka?” Mwanaume yule alisimama. “Wewe ni bahasha wake nini huyu manzi. Mbona maswali ya kijinga jinga, si unasema tu unaeleweka.”
Inspekta alimtandika kofi la nguvu mwanaume yule akadondoka chini.
“Potea hapa!”
Mwanaume yule alinyanyuka kwa hasira akamtizama inspekta.
“Hivi wewe unanijua mi nani?” Alifoka huku akimfuata inspekta. Alirusha ngumi, inspekta akaidaka na kuiviringita kisha akamsukuma, mwanaume yule akadondoka chini.
“Ngoja sasa nikuonyeshe. Nisubirie hapo kama wewe mwanaume kweli.” Alisema mwanaume yule huku akitokomea. Inspekta alitikisa kichwa chake akamgeukia mama Miraji,
“Vipi upo sawa?”
“Nipo fresh tu. Alikuwa ananisumbua sumbua tu huyo mtu.”
“Pole sana. Twende basi tukatembee tembee hapa naona tumeshageuka kideo.”
Mama Miraji alinyanyuka na mwanae wakaongozana kuelekea kule alipo Kaguta. Inspekta alimbeba Marietta mabegani, mkono wake wa kulia akiwa amemshikilia mama Miraji. Kaguta alitoka kwenye maji akaungana nao, ila aliona jambo;
“Vitalis, kuna watu kama vile wanakufuata.”
Inspekta aligeuza shingo akaona wanaume wanne, mmoja wapo akiwa yule mwanaume aliyemzaba kofi. Inspekta alimshusha mtoto chini, akamtaka mama Miraji akae nyuma yake.
“Wakina nani hao?”
“Yule fala aliyekuwa amekaa na mama Miraji, kaenda kuita wenzake.”
“Wanataka nini?”
“Wanataka kuvunjwa vunjwa.”
Kaguta alitabasamu akaweka mkono wake kifuani mwa inspekta, “Niachie mimi. Sijanyoosha viungo muda kidogo.” Alisema kisha akasogea mbele kukutana na wanaume wale wanne.
“Tunaweza tukawasaidia?”
“Wewe nani wa kutuuliza hivyo? … Tunamtaka huyo mbwa mwenzako. Au amekutuma wewe umsaidie?” Mwanaume yula aliyezabwa kofi alitema cheche.
“Kwa ushauri tu wa bure. Kimbieni angali mnaweza.” Kaguta alisema huku akikuna kichwa chake. Wanaume wale walitizamana, mmoja akarusha teke, Kaguta alidaka kisha akammanua mwanaume yule na kupiga sehemu zake za siri kwanguvu, kamlio ka mbwa koko kakasikika … “Uuuuuu!” Wakati mwanaume yule akidondokea chini huku akiugulia. Mwaume mwingine alirusha ngumi, Kaguta naye akarusha ngumi zikakutana kwanguvu. Jamaa aliyerusha ngumi naye akatoa sauti yake kilio huku akiugulia kwa kuuning’iniza mkono wake mpaka chini alipodondokea.
Mwingine alinyanyua mguu akilenga kurusha teke lakini kabla halijafika popote, Kaguta alirudisha teke hilo kwa teke lake kama mtu anayesinya taka kisha akatoa teke lake sasa matata ambalo lilimkumba mwanaume yule kifuani akarukia kwenye maji. Sasa akabakia yule aliyeenda kuita wenzake.
“Njoo basi fasta, sina muda wa kupoteza.” Kaguta alimwambia yule mwanaume. Yule mwanaume akataka kukimbia, Kaguta alimshika akamvuta.
“Niliwaambia mkimbie wakati mnaweza.”
Mwanaume alirusha ngumi, Kaguta akarudisha uso wake nyuma ngumi ikavuka alafu akafunguka na ngumi yake kali iliyotua kwenye uso wa mwanaume yule na kumdondosha chini. Mwanaume aliyevunjwa mkono alinyanyuka, Kaguta akamrudisha chini na teke la kichwa lililomziraisha mlengwa.
“Vitalis, mbona umenipa visharobaro hivi havina hata changamoto!”
Inspekta alitabasamu; “Si uliwataka mwenyewe.” Muda huo watu walikuwa wamejazana wakitizama. Waliamua waondoke zao kufuata gari wakaondoka hilo eneo na kuelekea nyumbani.
Siku iliyofuata, ilikuwa tulivu na labda ilikuwa inatofautiana na jana yake kwa tarehe tu. Ila inspekta na Kaguta waliamka wakiwa tayari wamedhamiria kuifanya iwe ya pekee. Walimbeba Marietta wakampeleka shule, baada ya hapo wakaelekea hospitali na kumtwaa Jombi safari ikaanza kuelekea bagamoyo kwa Alwatan Kombo.
Baada ya lisaa na madakika kadhaa wakawa tayari wameshatia miguu yao ndani yabagamoyo. Walishuka garini wakaanza kumuulizia mzee Alwatan Kombo.
“Mmmh yule mzee amekwisha hama pale. Saa hii anakaa kuleeee … unapaona kulee!” Muelekezaji alionyesha kidole chake kisiwani. “Kule ndipo anakaa.”
“Kisiwani?” Inspekta alishangaa.
“Ndio, kisiwani. Nyie nendeni pale kwa wale wavuvi wanaweza wakawapeleka huko.”
Kaguta, Jombi na inspekta walishika njia wakaelekea huko walipoelekezwa. Walipowafikia wavuvi, inspekta akaelezea haja. Wavuvi walikuwa watano, wote waliacha kazi zao wakawatizama wageni.
“Hatuwezi kuwapeleka huko!”
“Kwanini?” Kaguta aliuliza.
“We jua hivyo, hatuendi.” Alijibu mvuvi mmoja kwa niaba kisha wakaendelea na kazi zao. Wengine wakipara samaki zao walizovua usiku, wengine wakitengenezea nyavu wapate kuanza safari.
Wakina inspekta walitizamana wakajadili cha kufanya, Kaguta akapata wazo;
“Tuwatajie pesa ya maana, watakubali tu.”
Wakakubaliana.
“Mnataka shilingi ngapi kutupeleka?” Kaguta alichombeza.
“Tumesema hatutaki. Hatuendi sisi huko! … Kha!” Aling’aka mvuvi mmoja kisha zogo likazuka miongoni mwao,
“Hawa jamaa vipi, wanataka wakatutoe kafara nini? … Nani aende kufa huko?”
“Nashangaa. Japo maisha magumu, hatutaki kufa.”
Wakina inspekta walitizamana kwa nyuso za maswali.
“Jamani kwani kuna nini huko?” Kaguta aliuliza. Inspekta akapandisha mabega yake juu. Jombi akabinua mdomo wake. Kaguta aliwageukia wavuvi akawashawishi tena;
“Kuna elfu hamsini hapa kwa atakayetupeleka.”
Wavuvi wanne wakaendelea kung’aka kwamba hawataki hata kwa pesa gani. Mmoja akasema;
“Twendeni. Ila tunawashusha na kugeuza papo hapo!” Wenzao wakamshangaa;
“We Bakari wewe wataka makubwa?”
Mvuvi yule hakujali, aliwapandisha wakina inspekta na safari ya kuelekea kisiwani ikaanza. Baada ya dakika ishirini, walifika. Mvuvi aliwashusha akadai pesa yake, Kaguta akampatia. Mvuvi alipogeuka apande mtumbwi wake alishangaa kuuona umesogea kwenda mbali kama vile kuna mtu ameusogeza.
****
☆Steve