Siku100 Ikulu: Rais Samia anavyotibu siasa za utapiamlo

Deogratias Mutungi

Senior Member
Oct 1, 2019
137
179
#Siku 100 za Samia: Rais Samia anavyotibu siasa za utapiamlo

Deogratias Mutungi.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anatimiza siku mia moja hapo Juni, 26 tangu kuapishwa kwake tarehe 19 mwezi wa tatu, kufuatia kifo cha mtangulizi wake JPM, ndani ya siku hizi mia moja za awali katika utumishi wa umma tumeona mengi yenye mkondo chanya wa kulivusha taifa hili kutoka tulipo kuwa awali kuelekea kwenye siasa za utu, usawa, demokrasia na uwajibikaji, Sharti kupitia Makala haya tukubaliane kuwa siasa za awamu ya tano ziligubikwa na “utapiamlo kisiasa” hivyo afya yake ilikwenda alijojo, na ni sharti sasa tupate daktari wa kuliponya taifa letu Kiafya.

Makala haya kwa ufupi na kwa kuzingatia utafiti wa hali ya siasa za kabla ya kifo cha JPM na baada ya kifo chake yataangazia kwa undani ufanisi wa rais Samia katika utendaji wake kisiasa na kwa namna anavyozingatia na kuitumikia katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uwazi, weledi sambamba na kurudisha imani kwa Watanzania juu ya mifumo ya kisiasa na utawala bora iliyokuwa imeenda likizo isiyo na mwisho.

Tukirejea kwa ufupi na kwa muhtasari, Serikali ya awamu ya tano iliyokuwa inaongozwa na hayati John Pombe Magufuli ilifanya mazuri yake kadri ilivyoweza, lakini ombwe lililojitokeza wakati wa utawala wa JPM ilikuwa ni pamoja na kubana misuli ya upumuaji wa “uhuru wa maoni” Ukosefu wa uhuru wa maoni ulizalisha mifumo ovu ya ukosefu wa demokrasia, uminywaji wa haki, viongozi wa umma kujichukulia sheria mkononi na ufisadi ulichukua hatamu ndani ya baadhi ya ofisi za umma, Waliotenda yote haya walijua hakuna wa kupaza sauti, aidha aliyejaribu kupaza sauti hakusikilizwa kamwe napengine cha mtema kuni alikipata.

Yote haya yalijitokeza kwa sababu mifumo iliyokuwepo katika utawala ilikuwa inajikita ndani ya mfumo wa mkono wa chuma hili kutawala na kuleta maendeleo, Jambo ambalo wasaidizi wa JPM walishindwa kutambua na kushauri mamlaka husika ni kuwa nadharia ya utawala wa kibabe na kiimla uzalisha jamii yenye usugu na upinzani imara, hivyo kuwa na ukosefu mkubwa wa watu wenye fikra za kutaka maendeleo zaidi, ila tu kujikita katika kudai haki na uhuru wao.

Kisiasa na Kiutawala hakuna nadharia inayoonyesha hadi sasa kuwa utawala unaotumia mabavu kutawala ulifanikiwa kujenga misingi imara ya maendeleo ya watu na vitu zaidi ya kujenga chuki, hofu na machafuko ya ndani baina ya kabila moja kwenda jingine, mtu na mtu, kikundi kwa kikundi na hivyo kuhatarisha amani ya wananchi na mali zao.

Afrika baada ya kupata uhuru wa bendera kutoka kwa mkoloni, uhuru mambo leo wa mwana wa Afrika ni uhuru wa kujieleza na kuishi huru ndani ya taifa lake bila nongwa ya watawala waliopo madarakani, Muhtasari wa tafakuri hii unaonyesha wasaidizi wa rais walipuuza na kudharau mantiki ya nguvu ya umma na kusimama katika nguvu ya dola. Kisiasa kuna utofauti mkubwa kinzani kati ya nguvu ya umma na dola, mara zote umma ni imara kuliko dola.

Turejee Sasa kwenye kiini cha hoja yetu ya msingi ndani ya makala haya tukiangazia ufanisi wa rais Samia Suluhu Hassani kwa utawala wake wa siku mia moja akiwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makala haya yamefanya utafiti wake na kugundua hadi sasa rais Samia amegusa “kero kuu na kuntu” ambayo Watanzania wengi walikuwa waki ililia kwa takribani miaka mitano iliyopita, Kero hii ni pamoja na uhuru wa maoni na kujieleza sambamba na utawala wenye kufata misingi ya haki na utawala bora.

Kimantiki hili ni eneo ambalo rais Samia Suluhu amechagua kuanza nalo, hadi sasa makala haya yanaweza kusema kuwa amefanikiwa kwa asilimia 90% kukonga nyoyo za Watanzania bila kujali itikadi za vyama vyao kurejesha tumaini jipya la utawala wenye kuzingatia sheria, utu na nidhamu katika utumishi wa umma, hadi sasa tuna viongozi wa umma wanaotumikia umma na si kujitutumua kama kifutu “Puff Adder” kama ilivyokuwa awali.

Bila shaka hili kwa rais Samia halifanyiki kwa bahati mbaya bali anatambua misimamo na falsafa za mtangulizi wake zilisimamia nini, wapi na lipi, na kwa lengo gani? Inawezekana maswali haya yasieleweke kwa sababu Mama Samia alikuwa msaidizi wa Karibu wa rais, lkn hoja na jibu ya swali hili iwe ni kuwa mabadiliko ya sasa ndani ya serikali ya awamu ya sita ni matokeo ya kile ambachao Mama Samia kifalsafa hakukubaliana nacho hata kidogo, ndio maana tupo hapa tulipo kwa mabadiliko haya yanayoendelea kufanywa na rais Samia.

Aidha ndani ya siku mia moja za utawala wa rais Samia makala haya yamebaini kuwa, Mama Samia ni kiongozi anayeshauriwa na kukubali kupokea ushauri si kutoka kwa watendaji na wasaidizi wake wa karibu ndani ya mifumo ya serikali tu, bali pia kutoka hata nje ya mifumo ya serikali kwa maana ya vikundi mbalimbali vyenye uwakilishi wa watu kama NGO’S, Vikundi vya akina Mama, Vyama vya siasa, Wazee na Vijana.

Mara kadhaa tumemsikia rais akikubali kupokea ushauri na kwenda kuufanyia kazi pale anaposhauriwa na baadhi ya makundi yatokanayo na umma wa Watanzania, Kwa dhana hiyo rais ni msikivu na kiongozi anayeonyesha nia ya kusikiliza, kutatua na kutenda kadri alivyoguswa na kero iliyowasilishwa mbele yake na mezani kwake, Kisiasa hii ni mojawapo ya sifa kuu ya uongozi, Kiongozi sio malaika wala mjukuu wa Mungu kutokubali kushauriwa, hivyo kupata ushauri na kusikiliza raia anao waongoza wanataka nini ni utimamu na tafsiri ya uongozi uliotokanana na watu na ndio mantiki ya uwajibikaji wa kiongozi yoyote yule wa umma.

Pia Makala haya yamebaini kuwa rais Samia ni mwanademokrasia wa kweli anayetawala ulingo wa siasa kwa vitendo na si kwa porojo za kisiasa, hadi sasa ndani ya siku mia moja za utawala wake upo utashi wa kisiasa unaolenga kurudisha “amani ya kisiasa” Kati ya chama tawala CCM na Vyama vya Upinzani, Awamu ya tano ilionyesha udhaifu mkubwa katika kusimamia mifumo na fursa sawa baina ya siasa za upinzani, Wapinzani kuna wakati waliishi kama mashetani na watu wasio stahili kupata haki zao za kikatiba kama ilivyo kwa mtanzania yoyote Yule, wakati mwingine ilionekana kuwa mpinzani Tanzania ni sawa na “Uhaini”

Hoja hii ina mashiko kwa mantiki dhuluma dhidi ya upinzani zilitendeka kwa uwazi na mchana kweupe. Hata hivyo kwa kipindi hiki cha siku mia moja za Mama Samia upepo wa kisiasa umebadilika kabisa, Wapinzani wamepumua, na siasa zinafanyika bila hiyana wala ghiriba au ubaguzi wa aina yoyote ile, na sasa vyama vya upinzani vinafanya siasa zao bila bugudha wala nongwa ya aina yoyote ile, Kwa nchi inayofuata mfumo na sera za vyama vingi hili ni jambo la heri kabisa na la kupongezwa kwa rais wetu Mama Samia Suluhu Hassani.

Hata hivyo, Jicho la Mama katika siasa za usawa, uhuru na haki zimetamalaki, kusudio lake la kutaka kukutana na vyama vya siasa na kuzungumza nao juu ya mustakabali wa taifa letu kisiasa, Kiuchumi na kurejea misingi ya amani yetu kwa kufanya siasa safi, ni nia njema na mafanikio ya kimkakati kwa rais Samia katika jitihada zake za kuirejesha nchi kwenye mikono ya utawala wa kidemokrasia na kisheria kwa maslahi ya watanzania wote kwa maana ya kizazi cha sasa na hapo badae.

Mbali na hayo, Mama Samia ameonyesha weledi wa kusimamia mifumo ya ukusanyaji wa kodi kwa kutumia njia rasmi na zinazoeleweka bila kutumia mabavu na “dhuluma” Makala haya katika utafiti wake yamebaini hapo awali kuwepo mianya ya taasisi za kikodi kukusanya kodi kwa nguvu na dhuluma isiyokuwa na tija kwa taifa letu kwa upande mmoja au mwingine.

Ukusanyaji wa kodi kwa kutumia dola ulijenga hofu na hivyo baadhi ya wawekezaji kukimbilia nje ya nchi na kwenda kuwekeza kwingine na hivyo taifa kukosa mapato, ndani ya siku mia moja za rais Samia tumeona nia yake ya dhati inayonuia kurudisha mifumo rafiki ya ukusanyaji wa kodi bila kutumia shuruti wala nguvu ya dola, Ufanisi wake upo wazi na sasa wawekezaji wanaanza kurejea nchini kutokana na mifumo kubadilika kwa kiwango cha hali ya juu.

Kwa ujumla wake kisiasa sera za rais Samia Suluhu Hassani ni zenye tija na ustawi wa kiuchumi na kidiplomasia kwa maana ya diplomasia ya kikanda na kimataifa kwa mantiki ya kusaka fursa za kuwasaidia Watanzania kujikomboa kiuchumi na kiteknolojia kwasabu dunia inatuhitaji nasi tunahiitaji pia, uwepo wa misimamo dhidi ya korona kutoka kwa serikali ya awamu ya tano ulitutenganisha na dunia na kuonekana Tanzania ya wakati huo ni ya watu wasioeleweka wala kutabirika wanaamini nini kati ya sayansi na mitishamba.

Misimamo ya sasa ya awamu ya sita dhidi ya korona inatutambulisha upya katika anga za kimataifa na kurudisha hadhi ya Tanzania na Watanzania wote, Ukweli upo wazi kuwa hadi sasa rais Samia amefanikiwa kwa hali ya juu kubadili upepo wa siasa za Tanzania ambazo zilionekana kuwa siasa za chuki, ubabe na zenye kufuata mawazo na falsafa za mtu badala ya taasisi, Mtindo unaoegemea siasa za namna hii ujulikana kama siasa za “maji taka” Mantiki ikiwa ni kuwa hazina tija kwa maendeleo ya Mtanzania wa kawaida zaidi ya kutengeneza chuki na ombwe la amani ndani nchi.

Makala haya yana imani na rais Samia Suluhu Hassani kutokana na mwanzo wake mzuri aliouonyesha ndani ya siku hizi mia moja, ni rai ya makala haya kuomba rais Samia kuendelea na spidi hii aliyoanza nayo, aidha tahadhari kwa rais ni kuwa makini na wanasiasa ambao ni wasaka tonge wanaoweza kutumia fursa ya maslahi yao binafsi kumpotosha na kumchonganisha baina yake na watanzania wenye imani na serikali yake.

dmutungid@yahoo.com
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom