Siku ya Vijana Duniani iwe chachu ya kuzitambua, kuzianisha na kupinga sheria zinazominya demokrasia ya uchaguzi kwa vijana ikiwemo wenye umri 18-21

Emekha Ikhe

Member
Jul 14, 2021
43
62
SIKU YA VIJANA DUNIANI IWE CHACHU YA KUZITAMBUA, KUZIANISHA NA KUPINGA SHERIA ZINAZOMINYA DEMOKRASIA YA UCHAGUZI KWA VIJANA IKIWEMO VIJANA WENYE UMRI KATI YA MIAKA 18-21 KUGOMBEA NAFASI YA UBUNGE TANZANIA. KESI (ALPHONCE LUSAKO Vs. ATTORNEY GENERAL, CIVIL CASE NO.06 OF 2022).

Hatuwezi tukawa na Mifumo ya sheria katika Taifa inayotoa Haki ya Kupiga kura kwa Vijana wenye umri kati ya Miaka 18 na 21 na Kupoka Haki kwa Vijana hao hao Kupigiwa Kura. Ni kinyume cha Katiba Yenyewe (Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977), Ni kinyume cha Mikataba ya Kikanda (EACT-East African Community Treaty), (ACPHR-African Charter on People and Human Rights, 1986) na nikinyume cha Mikataba ya Kimataifa (ICCPR-International Convention on Civil and Political Rights,1976) na Tangazo la Ulimwengu la Haki za Binadamu- UDHR,1948 kama nitavyofafanua katika Makala hii.

Kesi hii ya Kikatiba na ya kimkakati (Strategic case), inalengo kuu la kuibua vuguvugu la vijana nchini (Youth Movement) katika Kudai na Kutetea Haki zao za kidemokrasia ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikinyimwa kutokana na mifumo ya kisheria ambayo ni ya kibaguzi na kandamizi kiasili na imeshapitwa na wakati, haswa katika masuala ya Uchaguzi ili washiriki kwenye masuala ya utawala wa nchi yao bila kubaguliwa wala kupokwa haki zao kama ilivyo sasa. Hii imechagizwa sana na kukosekana kwa chombo cha vijana, Mathalani BARAZA LA TAIFA LA VIJANA ambalo lingekuwa Nguzo kuu katika kutetea haki za vijana nchini.

Kesi hii inapinga kifungu cha Sheria, Kifungu cha 67(1) cha Katiba ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania,1977) kinachokataza vijana wenye umri kati ya miaka (18-21) wanaokadiriwa kuwa Milion (2-4) kwa mujibu wa takwimu za Watu na Makazi, kupigiwa kura au Kuchaguliwa kuwa wawakilishi katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huku Sheria za Uchaguzi zikitoa Haki moja tu ya Kupiga Kura.

Kifungu cha 67(1) cha Katiba kinasema;- Bila ya kuathiri masharti yaliyomo katika ibara hii, mtu yeyote atakuwa na sifa za kustahili kuchaguliwa au kuteuliwa kuwa Mbunge endapo- (a) ni raia wa Jamhuri ya Muungano aliyetimiza umri wa miaka ishirini na moja, na ambaye anajua kusoma na kuandika katika Kiswahili au Kiingereza; wakati Kifungu cha 10 (1) cha Sheria ya Uchaguzi Tanzania (National Election Act, Cap 343) kinasema; ili raia wa Tanzania asajiliwe na awe na sifa ya Kupiga kura, ni sharti awe na umri wa miaka 18 au wakati wa kupiga kura atakuwa amefikisha umri wa miaka 18.

Ukisoma vifungu hivyo viwili vya Sheria za Uchaguzi; Vinakinzana na Katiba yenyewe; Vinapingana na Kifungu cha 8, 9 (g,h) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 kinachosisitiza; misingi ya demokrasi, uhuru na haki ya kijamii, Usawa wa raia wote bila ubaguzi wa aina yoyote. Na Kifungu cha 13(1)(2)(5) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 kimefafanua juu ya Haki sawa na Usawa mbele ya Sheria bila kuweka masharti ambayo kwa taathira yake ni ya kbaguzi.

Kifungu cha 21(1) cha Katiba; Kinatoa haki ya Uhuru wa raia kushiriki shughuli za umma wakati Kifungu cha 29(1) cha Katiba kinatoa; haki ya kufaidi haki za msingi za binadamu, na matokeo ya kila mtu kutekeleza wajibu wake kwa jamii, kama zilivyofafanuliwa katika ibara ya 12 hadi 28 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,1977.

Mikataba ya Kikanda na Kimataifa; EACT, ACPHR1986, ICCPR,1976, UDHR,1948
  • Kifungu cha 67(1) cha Katiba kinapingana na kifungu cha 6(d) na 7(2) cha Mkataba wa Afrika Mashariki (EACT) unaotoa wajibu wa serikali kuheshimu kanuni za kidemokrasia, kuweka mazingira bora ya utawala wa Sheria, fursa sawa, Haki za kijamii, Kuheshimu Haki za Binadamu katika Mkataba wa Kikanda (African Charter on Peoples and Human Rights(ACHPR) na zile zilizokubaliwa duniani.​
  • Kifungu cha 2 na 13(1) Cha Mkataba wa Watu na Haki za Binadamu Afrika (African Charter on People And Human Rights (ACPHR kinatoa haki kwa Raia wa nchi za Afrika Kushiriki katika Shughili za serikali ya nchi yake, kufurahia uhuru na Haki zinazotambuliwa na Mkataba huu wa Afrika bila kubaguliwa kwa namna yoyote.​
  • Kifungu cha 3 na 25(a) na(b) kinacho toa haki kwa raia kushiriki katika haki za kiraia na Kisiasa, Vile vile Haki kwa raia kupiga kura na Kupigiwa kura, Kushiriki katika shuguli za umma bila ya ubaguzi.​
  • Kifungu cha 21 (1)(2)(3) cha Tangazo la Ulimwengu la Haki za Binadamu (UDHR,1948) ambalo limetambuliwa na Kifungu cha 9(f) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,1977 kinatoa Haki ya Raia kushiriki katika shughuli za kiserikali ikiwemo Uchaguzi unaoandaliwa nan chi husika.​
Kihistoria, Sheria zetu nyingi zikiwemo za Uchaguzi tumezirithi kutoka kwa Waingereza ambao walitawala baada ya Mjerumani; hivyo Sheria zetu nyingi hurandana na Sheria za Jumuia ya Madola (Common Law); Nimefanya mawasiliano na Bunge (House of Common-United Kingdom) kwa barua pepe (email) Kujua Sheria zao za Uchaguzi haswa katika umri wa kugombea nafasi ya Ubunge. Wamekili walikuwa na Sheria kama yetu inayotaka Mgombea wa nafasi ya Ubunge kuwa na miaka 21+ lakini walifanya Mabadiliko ya Sheria husika (Electoral Adminstration Act, 2006), Kifungu cha 17 cha Sheria husika kwa sasa kinaruhusu raia aliyefikisha umri wa miaka 18+ kugombea nafasi ya Ubunge na Mwaka 2015. Mh. Mhairi Black akiwa na umri wa miaka 20 alifanikiwa kuchaguliwa kuwa mbunge wa Paisley & Renfrewshire

Ikumbukwe, Sheria ya Mtoto Tanzania (The Law of Child Act, Cap 13), Mkataba wa Kikanda wa Haki na Ustawi wa Mtoto (The African Charter on the Rights and Welfare of the Child) na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watoto (Convention on the Righs of Child) umefafanua Kwamba Mtoto ni mtu mwenye umri chini ya miaka 18. Sheria hii haimpi mtoto Haki ya Kupiga kura katika Uchaguzi kwa kuwa inanadharia (Assumption) kwamba mtoto mdogo hawezi na hajakomaa kufanya yoyoye yakiwemo ya Uchaguzi. Mtu anapofikia umri wa miaka 18 anachukuliwa ni mtu mzima (Adult) na sheria imeweka nadharia(Assumption) kwamba anaweza kufanya maamuzi sahihi kwa kuwa anakuwa amekomaa kiakili na ndio msingi wa Sheria za Uchaguzi Kutoa Haki kwa Vijana kati ya Miaka 18-21 kupiga kura.

Hakuna Hoja za Kisayansi, za Kitafiti zinazoweza kuthibitika kwamba kijana mweye umri wa miaka 18, 19, 20 na 21 kasoro hana utashi hivyo kukosa Haki ya Kugombea Ubunge. Hata kama kungekuwa na Hoja Husika; Basi waliopaswa kupiga kura walipaswa kuwa watu wenye umri wa miaka 21+ na sio wenye umri wa miaka (18-20)

Na, Alphonce Lusako M, Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Utetezi Katika shirika liitwalo PLAO-Policy And Legal Assistance Organisation, linalojihusisha na Masuala ya Uchambuzi wa Sera na Sheria ili kuendeleza utamaduni wa kulinda na Kutetea Sheria na Sera zinazolinda na Kutetea Haki za Binadamu​
 
Back
Top Bottom