Siku Muhimu ya Kuadhimisha Siku Yangu ya Kuzaliwa

Jumanne Mwita

JF-Expert Member
Nov 18, 2014
424
1,044

Rafiki yangu mpendwa,

Leo ni siku ya kukumbuka kuzaliwa kwangu.
Tarehe 06/06 ndiyo siku ambayo nilizaliwa, hivyo leo tarehe 06/06/2023 nimetimiza miaka kadhaa ya kuwa hai hapa duniani.


Kwa miaka hiyo michache, nimejifunza mengi sana na pia nimekazana kuwa na mchango kwa wengine kadiri ya uwezo wangu.

Leo hii, katika kumbukizi ya kuzaliwa kwangu nimeona nikushirikishe mambo 3.4 ambayo ninayaamini sana kwenye safari hii ya mafanikio.

Hayo ni mambo ambayo ninayaamini bila ya shaka yoyote na yamekuwa na mchango mkubwa kwa pale nilipofika sasa.

Na ndiyo nitakayoendelea kuyasimamia katika kuziendea ndoto zangu kubwa nilizonazo.
Kabla sijaingia kwenye hayo ninayoamini, nikukumbushe ndoto yangu kubwa ninayopigania na hatua ninazoendelea nazo.
Nilishaweka wazi na nimekuwa narudia kwamba nina ndoto kubwa kwenye maisha yangu.

Ndoto hii ni kuwa mfanya biashara mkubwa (kwa kipimo cha dola) mpaka kufikia mwaka 2030. Maendeleo ya ndoto hizo kubwa ni kwa sasa nipo kwenye mchaka mchaka wa kuwa mfanya biashara mkubwa na hilo litasababisha niwe buze sana.

Kwa sasa akili, nguvu, hisia na umakini wangu wote upo kwenye kupambana kuwa mfanya biashara. Na ninaamini bila ya shaka yoyote kwamba nitafikia ndoto hii, maana ninapambana bila kukata tamaa. Ni labda nitazifikia au nitakufa nikiwa nazipambania, hakuna mbadala wa hilo.
Baada ya kukukumbusha ndoto hizo zangu na maendeleo yake, sasa twende kwenye mambo 3.4 ambayo ninayaamini sana kwenye hii safari ya mafanikio.


1. KAZI.​

Jambo la kwanza ninaloliamini sana kwenye hii safari ya mafanikio ni kazi. Ninaamini bila ya shaka yoyote kwamba rafiki wa kweli na ambaye hawezi kukusaliti kwa namna yoyote ile ni kazi.

Ipende kazi na kuwa tayari kuweka kazi na itakupa chochote unachotaka kwenye maisha yako.

Sisemi haya kwa kubahatisha, bali kwa sababu ni utayari wangu wa kuweka kazi kwa juhudi kubwa ndiyo umenifikisha hapa nilipo.
Nikupe mfano mdogo ambao ushahidi wake upo wazi.


Ninachotaka kwako rafiki yangu ni ujenge imani kubwa kwenye kazi. Ipende sana kazi.
Weka juhudi kubwa kwenye kazi. Na kazi haitakutupa, Kazi itakulipa. Waruhusu watu wakuzidi akili, elimu, fedha, koneksheni na hata vipaji. Lakini kamwe kamwe usimruhusu mtu yeyote akuzidi kwenye kazi.

Kwa chochote unachofanya, hakikisha unakijengea sifa (kwa vitendo na siyo maneno) kama mtu unayeweka juhudi kubwa kwenye kazi kuliko watu wengine wote. Fanya hivyo na utashangaa jinsi fursa nzuri zitakavyokuja kwako.


TAHADHARI;​

Nilichokuambia hapa kuhusu kazi kinaenda kinyume kabisa na jinsi jamii inavyokuambia kuhusu kazi. Jamii inakuhadaa usifanye kazi sana. Inakuambia kuna njia za mkato. Inakuambia usifanye kazi kwa nguvu na juhudi, bali kwa akili tu.
Huo wote ni ulaghai na kama utausikiliza rafiki yangu, maisha yako yataendelea kuwa magumu na hautafanikiwa.

Hakuna yeyote anayekuwa na nyakati nzuri zote kwenye maisha yake. Hata kama unamuona mtu ana furaha namna gani elewa aliwahi kupitia majonzi.
Hali yako ya ugumu usijione kama wewe ndo wakwanza, tambua utapita hapo usisononeke sana.

2. MAARIFA.​

Maarifa ni jambo jingine muhimu sana ninaloliamini kwenye hii safari ya mafanikio.
Ni maarifa ndiyo yaliweza kubadili kabisa mtazamo wangu kuhusu maisha na mafanikio tangu mwaka 2009. Na tangu kipindi hicho nimejionea mengi na kusikiliza ushauri mwingi ambao nimeufanyia kazi na mwingine nikauacha upite.

Kila mtazamo nilionao leo, kila ninachojua leo, havitokani na akili zangu, bali vinatokana na maarifa mengi ambayo nimekuwa nayakusanya kila siku. Kazi kwangu ni kipaumbele cha kwanza kwangu.

Baada ya kugundua akili ni kama tumbo, nilidhamiria kutokuulisha mwili kama sijailisha akili. Hivyo kabla sijala chakula, lazima kwanza nitafakari ya kesho nitakula nini na familia itaishi vipi wakati mimi anenda kushiba sasa hivi? Wengi wanasema kwanini mimi sinenepagi ni wahivi hivi tu.

Hapana mimi niko na afya nzuri sana nikitulia na nikiyapata maisha ila kwa sasa ngoja nipambane kwanza nione nitakapoishia ili nisije kumlaumu yeyote katika uzee wangu maana uzembe nitakuwa nimeufanya mwenyewe. Na hili pia lina ushahidi wa wazi, hata kwenye vitabu vingi vinavyofundisha na kuchambua maisha ya kila siku.

Ninaamini bila shaka yoyote kwamba hakuna tatizo unalopitia sasa kwenye maisha yako ambalo halina suluhisho lililoandikwa kwenye vitabu.

Unachohitaji ni kusoma vitabu sahihi ili kutoka pale ulipokwama sasa. Wito wangu kwako wewe rafiki yangu ni uamini kwenye maarifa na kama ambavyo unalilisha tumbo lako kila siku, basi pia lisha akili yako chakula chake ambacho ni maarifa na acha kuishi maisha ya kukalili.

Na maarifa ninayoeleza hapa ni yale unayopata kupitia maisha yako halisi maana ukitaka kutafakali utafutaji wako unaanzia kwenye maisha uliyoishi hapo nyuma na mpaka sasa unayaishi, ndoto zako unaziishi, kama ukipanga lazima ujenge na hizo ndio ndoto zako acha kujitakisha tamaa kuwa huwezi kwa sababu unaporomoka kibiashara au kimawazo hapo unafeli sana.

Makala zote zinazohusu elimu ya fedha na maisha hazihesabiki, japo zinaweza kuwa na mafunzo mazuri. Kuna vitu unavyojifunza kwenye mitandao ya kijamii pia havihesabiki. Fanya vyote kwa kadiri unavyoweza, lakini cha msingi kabisa ni malengo hakikisha mwaka unapoanza anza na malengo na mwaka ukiisha funga na malengo ya mwaka husika acha kulialia mwaka umeisha umekuacha hakuna kitu ulichofanya usifanye kufuru kama hiyo.


Kingine muhimu sana kwenye utafutaji ni kuchukua hatua.

Haitoshi tu kupambania maisha ya ndoto zako, pia unapaswa pia kufanyia kazi yale uliyojifunza kwa yale yaliyokufelisha. Mimi katika historia fupi mwaka 2017 hadi 2019 mwezi wa 4 nilifeli mpaka nikajiuliza hivi itawezekanaje kurudi kwenye ramani ya maisha haya na malengo yangu yanakwenda kufa naona. Hii haikuwa mwisho wa ndoto na malengo yangu ingawa nilibaki mimi kama mimi hakuna wa kuniambia nipite hapa ila nilijipa matumaini na sasa naandika makala hii nikiwa mtu mwingine kabisa. Sasa wewe rafiki yangu nakusihi endelea kuyafanyia kazi yakiwa bado ni ya moto kabisa. Hivyo unapojifunza kitu kipya kupitia maisha halisi achana na yake ya vitabu vitabu, hebu yaweke kwenye matendo mara moja.

Kwa njia hiyo kila mara utakuwa na mawazo mazuri na ya kibunifu yatakayokupa manufaa makubwa.


TAHADHARI;​

Jamii haitakuruhusu kuona unabadilisha maisha haraka haraka lazima ujitoe na kama unataka kufanikiwa toka mahali uliko zaliwa maana sisi waafirika ndio tuko na tabia hii ya "Nabii hakubaliki kwao" hii ipo na kama huamini kajenge na fanya biashara ulikozaliwa uishi kama utaumaliza mwaka huu ukiwa mzima.

Katika kukukumbusha acha kupoteza muda na kuhadazwa na vipindi vya tv, hasa hasa kwenye mitandao ya kijamii, wengi walioko huku kwenye mitandao ya kijamii ni wale ambao wanaishi nje na vipato vyao na wanafeki maisha halisi wanayotakiwa waishi sasa wewe ukiwafuata utajuta baadae. Na itakufanya ubeze maarifa yaliyopo kwenye malengo yako kwamba hayafanyi kazi. Jamii itakuweka bize na mambo yasiyo na tija ili tu isijitafute.

Kwa sababu unakuwa rahisi kutawaliwa na kutumiwa kwa manufaa ya wengine kama ukiiendekeza jamii kwenye hili, utabaki kwenye maisha duni.



3. WATU.​

Kwenye safari ya mafanikio, watu wana mchango mkubwa sana. Lakini siyo watu wote ni sawa na sahihi kwako. Watu ni jambo jingine ninaloliamini sana kwenye hii safari ya mafanikio. Na siyo kila aina ya watu, siyo watu wote, bali watu sahihi kwako.

Tukianza na kanuni ya msingi kabisa; maisha yako ni wastani wa maisha ya watu watano unaotumia nao muda wako mwingi. Hii ni sheria ambayo hakuna mwenye nguvu ya kuivunja.

Wachukue watu watano wa karibu kabisa kwako, wale ambao unatumia nao muda wako mwingi, kisha yaangalie maisha yao na yako.

Utagundua vitu vingi sana mnafanana. Unadhani hilo limetokea kwa bahati? Hapana, limetokea kwa makusudi kabisa. Unakuwa kama wale unaowapa nafasi kwenye maisha yako. Hivyo jambo muhimu sana la kuzingatia hapa ni kuchagua aina sahihi ya watu wa kuwa nao. Watu ambao tayari wameshafika kule unakoenda au ndiyo wanaelekea huko.

Watu ambao wana ndoto kubwa na kila siku wanapambana kuzifikia. Watu ambao siyo wa kukata tamaa. Watu ambao wanapenda kuona wengine wanafanikiwa. Zungukwa na watu wasio na sifa hizo na hakuna hatua utapiga. Utaweka juhudi kubwa sana, lakini utaishia kubaki pale pale ambapo wenzako wapo. Tunategemeana sana kwenye hii safari ya mafanikio. Lakini siyo watu wote wanaotufaa. Hivyo unapaswa kuchagua watu sahihi kwako na kuambatana nao.


TAHADHARI;​

Jamii imejaa watu wa kawaida ambao hawawezi kupata mafanikio makubwa. Wengi wanaotuzunguka ni wa kawaida sana na hawatapata mafanikio makubwa. Ni wakati sasa wa kuwabadili watu unaowapa muda wako. Tafuta watu waliofanikiwa sana au ambao wanapambana kufanikiwa na hao ndiyo unapaswa kutumia nao muda wako mwingi. Na kama huwezi kupata watu wa aina hiyo, basi tumia muda wako mwingi kwenye kutafakari maisha yako baada ya kazi hiyo kukoma, iliuendelee kujifunza ili kuwa bora na kuweka juhudi zaidi kwenye kazi kwa faida ya maisha yako ya baadae.

Haitachukua muda utaanza kuwavuta watu sahihi kwako. Utakapoanza kukaa mbali na watu wasio sahihi kwako, hawatakuacha salama. Watakuambia umebadilika, Watasema una dharau Na mengine mengi. Wapuuze kama unayataka mafanikio.


3.4. MUDA.​

Watu wote Duniani tuna muda sawa.
Hata mtu tajiri kuliko wote duniani, bado ana masaa 24 kwa siku kama ambavyo masikini wote wanayo. Ni kwenye muda pekee ndipo penye demokrasia ya kweli Duniani. Ndiyo kitu pekee ambacho wote tumepewa kwa usawa.

Sasa kwa kuwa tumepewa kwa usawa, ila wapo ambao wanafanya makubwa sana kwenye muda huo huo, ina maana kuna vitu wanafanya kwa utofauti. Na hapo ndipo muda unapokuwa muhimu sana. Na ndiyo maana muda ni kitu kingine ninachokiamini mno. Naamini ukitumia muda wako vizuri, utaweza kufanya makubwa kwenye maisha yako.

Kwa yote ambayo nimeweza kufanya, ni kwa sababu nimekuwa nakazana kutumia muda wangu vizuri. Na siri kuu ya kutumia muda vizuri ni kusema HAPANA kwenye mambo yote ambayo hayana mchango kwenye maisha yako na mafanikio unayotaka.


Kwa Mfano,​

Haya ni mambo ambayo nilishasema hapana kwenye maisha yangu na kutokuyafanya kumeokoa muda wangu mwingi.
  1. Kufuatilia habari kwa TV, Redio, Magazeti na vyombo vingine vya habari.
  2. Nimepunguza Matumizi ya mitandao ya kijamii, baadhi kwa sababu muda mwingi nilikuwa huko na napoteza muda.
  3. Ushabiki wa mchezo wa aina yoyote ile, sifuatilii michezo yoyote ile iwe ya kubashiri n.k
  4. Ulevi na starehe mbalimbali, situmii kilevi chochote.
  5. Vikao na shughuli nyingi za kijamii, sihudhurii mambo ambayo siyo muhimu kabisa. Kwa kusema hapana kwenye hayo, nabaki na muda mwingi ambao naweza kuutumia kwenye mambo yenye tija zaidi.

Rai yangu kwako rafiki yangu ni hii, linda sana muda wako. Tumia neno HAPANA kwa yote yasiyokuwa na mchango kwenye mafanikio unayoyataka.


TAHADHARI;​

Jamii ina mbinu nyingi sana za kunasa muda wako. Inakulazimisha ufanye yale ambayo kila mtu anafanya ndiyo uonekane wa kawaida. Chagua kama unataka kuwa wa kawaida na usifanikiwe. Au kuwa wa ajabu na ufanikiwe.

Huwezi kufanikiwa bila kuonekana wa ajabu kwenye jamii. Kwamba hufuatilii habari, punguza matumizi ya kwenye mitandao na hushabikii chochote! Wengi watakuona una tatizo, ila wao ndiyo wenye tatizo kubwa zaidi kukiko wewe.


Rafiki yangu, kutoka ndani ya moyo wangu kabisa hayo ni mambo ninayoyaamini bila ya shaka yoyote ile.

Ninakusihi ujenge imani kubwa kwenye mambo hayo na kuyasimamia kila siku bila ya kutetereka.
Na kwa hakika utaweza kufanya makubwa kwenye maisha yako.

Karibu tuendelee kuwa pamoja kwenye hii safari.
 
Back
Top Bottom