Mtanzania,
Maelezo yako hayo yanatosha kabisa, sasa naijua Mbeya vizuri. Hoja na dataz za watu kama wewe ndio zinatufanya wengine tuwe addicted na JF, ubarikiwe sana! Umenisaidia pia ku-confirm yale niliyokuwa nayajua kuhusu Dk wetu Mwakyembe. Haya mimi yalinikuta wakati tunamfanyia kampeni za ubunge za EAC, wewe acha kabisa, huyu jamaa ni kiboko. Huwezi kumjua Mwakyembe kwa kumsoma kwenye magazeti hadi ukae naye ana kwa ana kwa muda.
Tena hupaswi kabisa kumchukulia Mwakyembe on a face value. Yeye huwa anakubali kutumiwa na kutumia akili zake kufanikisha matakwa ya kisiasa ya watu wengine. Unakumbuka Mkapa alivyomtumia kuhalalisha yale mauaji ya polisi kule Zanzibar, alijenga hoja kidogo watu wakubali, kilichosaidia kusambaratisha hoja zake ni hoja maridadi za prof Haroub Othman. Hivyo basi hata kwenye hii report ambayo tunamsifu sana huyu mheshimiwa, mimi ninajua kuna wajanja wachache waliamua kutumia akili zake ili kufanikisha ajenda zao kisiasa. Uzuri wa haya mambo ni kwamba ukweli siku zote hujitenga na uongo, sio muda mrefu tutajua zaidi kuhusu dhamira ya ndani kabisa ya ile report!
In the meantime, ukweli ni kwamba hii report imeinyanyua nyota ya kisiasa ya Dk Mwakyembe ambayo ilikuwa inazidi kufifia; sasa swali ni je, itadumu hadi lini? Time will tell.
NJAMA nzito za kutaka kudhibiti mapokezi ya Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe, yaliyoandaliwa na wananchi yasifanikiwe, zikiwa zimeongozwa na mkuu wa wilaya hiyo hatimaye zimefichuka.
Kufichuka kwa njama hizo kunatokana na barua za siri zilizoandikwa zikilielekeza Jeshi la Polisi wilayani humo kudhibiti nyendo za waandaaji wa mapokezi hayo na jinsi michango inavyochangwa, ili kufanikisha shughuli hiyo.
Mkuu wa wilaya hiyo (DC), Mashimba Mashimba, katika kile kinachodaiwa kuwa yumo kwenye mpango madhubuti wa kuhujumu mapokezi hayo amediriki kumtumia nakala ya barua hiyo, John Mwakipesile kama barua binafsi na si ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya.
Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima umegundua kuwapo barua aliyoiandika Februari 21 mwaka huu kwenda kwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Kyela, ikiwa inamtahadharisha juu ya mapokezi hayo na nakala yake kutumiwa Mwakipesile ikiwa haijaonyesha wadhifa wa mkuu wa mkoa kama ilivyo kawaida kwa barua za serikali.
Barua hiyo inamwelekeza Mkuu wa Polisi wa wilaya hiyo kufuatilia kwa karibu mchakato mzima wa maandalizi hayo kwa madai ya kuzingatia usalama wa raia na mali zao na taratibu za michango nchini.
Taarifa yako imejaa aina fulani ya utetezi kana kwamba jambo hilo ni la kawaida na halina madhara ya aina yoyote ya kiusalama ndani ya wilaya, alisema DC huyo ikiwa ni sehemu ya barua yake inayoonyesha msisitizo na hofu aliyonayo kuhusu mapokezi hayo.
Msimamo wa mkuu wa wilaya hiyo unakinzana na taarifa iliyomo kwenye barua ya mkuu wa polisi (OCD) kuhusu nia yake ya kutokuwa na mashaka na mapokezi hayo hasa ikizingatiwa usalama mkubwa uliopo sambamba na kazi ya Jeshi la Polisi kulinda usalama wa raia na mali zao.
Katika barua ya Mkuu wa Polisi wa wilaya hiyo ambayo Tanzania Daima imefanikiwa kuipata, imemtaka mkuu wa wilaya hiyo kutokuwa na wasiwasi wowote juu ya mapokezi hayo wakiamini kuwa ulinzi wa kutosha upo kwa ajili ya kudhibiti vurugu zozote zinazoweza kutokea.
Ujasiri ulioonyeshwa na OCD wa Kyela kwa kiasi kikubwa unaonyesha kumkera mkuu wa wilaya hiyo na watendaji wengine wa serikali kiasi cha kuandika barua yenye maelekezo hayo yakiipinga barua ya polisi ya Februari 19 inayoelezea kuruhusu mapokezi hayo.
Kufumuka kwa matukio hayo, ni njama za kudhoofisha mapokezi ya Dk. Mwakyembe ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati teule ya Bunge iliyokuwa ikichunguza mkataba wa Kampuni ya uzalishaji wa umeme wa dharura ya Richmond.
Mlolongo mzima wa njama hizo pia umesababisha watendaji wote wa serikali wilayani humo kuandaa safari za dharura ili siku ya mapokezi hayo wasiwepo kwenye wilaya hiyo na nafasi zao zimeachiwa wasaidizi wao.
Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Martin Mulwafu, alipohojiwa alikana kuiona barua yoyote inayotoa maelekezo ya kufuatilia nyendo za mapokezi hayo kutoka kwa mkuu wa wilaya hiyo na kwamba hajaachiwa msimamo wowote na DC huyo kuhusu kupokewa kwa Dk. Mwakyembe.
Source: Tanzania Daima