nngu007
JF-Expert Member
- Aug 2, 2010
- 15,860
- 5,803
JUMAPILI, MACHI 24, 2013 08:52 NA MWANDISHI WETU
SIKU moja baada ya Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, kupinga malalamiko yaliyotolewa na wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kuwa hawashirikishwi, akisema ni ya ajabu na hayana ukweli, majibu hayo yameonekana kumchefua kiongozi wa wabunge hao.
Akijibu kauli hiyo ya Sitta kupitia taarifa yake aliyoitoa kwenye vyombo vya habari jana, Katibu wa Bunge la Afrika Mashariki, Shy-rose Bhanji, aliitaka Wizara ya Afrika Mashariki kuacha ubabaishaji kwa kutoa kauli za uwongo kwa Watanzania na badala yake akaitaka iongeze kasi ya uwajibikaji.
Juzi Sitta aliitwa mbele ya Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje iliyotaka kupata ufafanuzi kuhusu malalamiko yaliyotolewa na Katibu wa Bunge la Afrika Mashariki, Shy-rose kuwa Wizara hiyo imekuwa ikiwatenga na haiwashirikishi katika masuala mbalimbali.
Katika majibu yake, Sitta alisema malalamiko hayo hayana ukweli wowote na kumshutumu waziwazi Katibu wa wabunge hao, Shy-rose kuwa ndiye anayeongoza kwa kutohudhuria mikutano anayoalikwa kutokana na kuwa na mambo mengi.
Jana Shy-rose katika majibu yake kwa Sitta, alimtaka Waziri huyo pamoja na Naibu wake kutoa vielelezo dhidi ya madai yao.
Kama nilivyosema kwenye kikao cha Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Wizara imejitenga sana katika kutoa mwongozo na vile vile katika kuwafikia Watanzania walio wengi kwa kigezo kwamba Wizara haina fedha, alisema Shy-rose.
Nimekuwa nikiwasiliana moja kwa moja na Naibu Waziri Abdullah Juma Sadallah kuhusu masuala mengi, kwa maana ya kushirikiana na kupeana mwongozo, lakini majibu ya Naibu Waziri daima yamekuwa ni ya ubabaishaji na ya kukatisha tamaa, akisema kwamba Wabunge wa EALA hawako chini ya Wizara, alisisitiza Mbunge huyo.
Shy-rose amemtaka Waziri Sitta kukaa na viongozi wa wizara yake ili apate ukweli wa mambo kuliko kurukia kujibu hoja kwa ubabaishaji, kwani nia ni kuweka maslahi ya nchi mbele na si binafsi kama alivyofanya juzi yeye na Naibu wake, kwenye kikao cha Kamati.
Kuhusu suala la posho, Shy-rose alisema walialikwa mara moja tu Bungeni, lakini waliambiwa kila mtu ajigharamie malazi na usafiri.
Hivi inaingia akilini kweli ualikwe kwenda safari halafu unaambiwa ujigharimie? Yeye Sitta na Naibu Waziri kwa vile wanatumia magari ya Wizara na kuwekewa mafuta na kupewa posho kufika Bungeni ndio maana inamwia rahisi kuongea kiubabaishaji.
Hii hoja ya posho si ya kweli hata kidogo, kilichoongelewa ni vipi tunafika Dodoma iwapo hatujui tutalala wapi na tutakula nini .sijaomba gharama hizi kama Shy-rose, bali kama Katibu wa Wabunge, alisema.
Akizungumza na Kamati hiyo, awali kabla ya majibu hayo ya Sitta, Shy-rose alisema wabunge hao wa Afrika Mashariki wamekuwa kama watoto yatima, kwani hawajui waende wapi baada ya Wizara ya Afrika Mashariki kuonyesha kutowajali.