A. WALIOSHIRIKI MOJA KWA MOJA KATIKA VITENDO VYA UFISADI
6. NIMROD ELIREHEMA MKONO
Mheshimiwa Nimrod E. Mkono ni Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijiji na Mshiriki Mkuu wa kampuni ya mawakili ya Mkono & Company Advocates ya Dar es Salaam. Barua ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu ya Serikali inaainisha kuwa Benki Kuu imekuwa ikilipa malipo makubwa kwa Mkono & Co. Advocates hasa yale yanayohusu kesi ya Valambhia ambapo Benki Kuu inadaiwa jumla ya shilingi bilioni 60. Kwa mujibu wa barua ya wakaguzi tayari Mkono & Co. Advocates wamekwishalipwa shilingi 8,128,375,237 kwa fedha taslimu kwa kesi hiyo ambayo bado iko mahakamani. Malipo haya ni sawa na asilimia 13.5 ya deni lote inalodaiwa Benki Kuu. Hoja ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu ni kuwa kesi hii haina muda maalumu wa kumalizika na hivyo inawezekana kabisa malipo ya wanasheria yakazidi kiasi cha fedha inachodaiwa Benki Kuu.
Lakini hoja nyingine ya kimsingi ni kama malipo haya kwa mawakili yanaruhusiwa chini ya Kanuni za Malipo ya Mawakili na Uamuzi ya Gharama za Kesi za mwaka 1991, Tangazo la Serikali Na. 515 la mwaka 1991 (Advocates Remuneration and Taxation of Costs Rules, 1991). Kanuni hizi zimeweka kiwango cha malipo ya mawakili katika kesi ambazo fedha inayodaiwa ni zaidi ya Shilingi milioni 10 kuwa ni asilimia tatu. Kwa kufuata masharti ya sheria hii ya malipo ya mawakili, kampuni ya Mkono & Co. Advocates ilipaswa kulipwa Shilingi bilioni 1.8.
Kampuni ya mawakili ya Mkono & Co. Advocates imekuwa ikitajwa kuhusiana na kashfa kubwa za ufujaji na/au ubadhirifu wa fedha za umma kwa muda mrefu. Kwa mfano, Taarifa ya Uchunguzi Kuhusu Tuhuma Dhidi ya Makampuni ya Tanfarms Ltd., Makinyumbi Estates Ltd., Centrepoint Investments Ltd., na Arusha Farms Ltd. Yanayomilikiwa na V.G. Chavda Kuhusiana na Matumizi Mabaya ya Fedha za Debt Conversion Programme iliyotolewa Bungeni na aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati Ndogo ya Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi, Mheshimiwa Edward Oyombe Ayila mwezi Novemba 1994 ilisema yafuatayo kuhusu Mheshimiwa Nimrod Mkono: Mhe. Spika si nia yangu kulichosha Bunge lako tukufu na hotuba ndefu lakini ni vizuri nikaelezea juu ya uhusiano unaotia mashaka kati ya V.G. Chavda na Mashamba yake na Subash Patel mwenye makampuni ya DECO ART, MM Motors, MM Garage, Hotel Sea Cliff, City Bureau De Change na Nimrod Mkono, Wakili wa kujitegemea ambaye pia ni Mkurugenzi katika makampuni ya AZANIA AGRICULTURAL ENTERPRISES, LIBERTY LEATHER SHOE LTD., AZANIA EXIMCO, n.k. (AIMS GROUP OF COMPANIES)
Baada ya kuelezea uhusiano huo ulivyokuwa Mheshimiwa Ayila alimalizia kwa kusema yafuatayo: Mheshimiwa Spika, ni vigumu kabisa katika hali ya kawaida kwa mtu yeyote kuamini kwamba makubaliano haya na uhusiano uliojitokeza hapa haukuwa wa hila. Chavda kwa kupitia wakili wake Nimrod Mkono, aliomba Mahakama Kuu kuzuia kabisa shughuli za Kamati (permanent injunction). Aidha ni wakili huyo huyo ambaye ameshuhudia uuzaji wa deni la Deco Art (reassignment) kwa Chavda. Mheshimiwa Spika, hali hii ukiitazama kwa undani utaona kwamba pengine kuna kitu kinafichwa. Nimrod Mkono alikuwa Mkurugenzi Mkazi wa Kampuni ya Oxford Services Ltd. na pia anamiliki Kampuni ya Marcus Ltd., makampuni ambayo kwa pamoja yamefaidika kwa kuupata jumla ya Shs. 4,477,870,279.61 chini ya utaratibu wa DCP.
rudi...