Shilingi kushuka thamani na hali mbaya ya uchumi wetu: Sababu ni nini na nini kifanyike?

Siamini kama ni Zito kaandika kuwa Ubinywaji wa Demokrasia ndio umesababisha kushuka kwa uchumi. Haha.
 
Hata huko Iran kuna afadhali, wao ni development country inakaribia third world, tz tuna a nini? Hata bei ya mafuta na gas inatoka huko huko USA, halafu unakuwa na mdomo mrefu kuwaita mabeberu, kwetu pemba Beberu maana yake kidume, kwa hio watanzania mtakuwa nani nyie,

Sent using Jamii Forums mobile app
Development Country au Developing Country.
 
Excellent mh Zitto.
Shilingi Kushuka Thamani na Hali Mbaya ya Uchumi Wetu: Sababu ni Nini na Nini Kifanyike?

Thamani ya sarafu ya Tanzania imezidi kuporomoka kwa kasi dhidi ya Dola ya Marekani katika wiki za hivi karibuni. Mwishoni mwa wiki iliyopita dola moja imeuzwa mpaka TZS 2415, mporomoko wa karibia 15% kulinganisha na thamani ya Dola katika mwezi wa Januari Mwaka 2018. Kwa maoni yangu, Watanzania wanapaswa kujua kuwa Haya ni matokeo ya Mambo Matatu Makubwa:

Mosi: Ni maamuzi ya hovyo juu ya Zao la Korosho, ambalo ndio zao kiongozi katika kuleta fedha za Kigeni nchini. Kutokana na maamuzi mabaya ya Serikali ya kutaka sifa za muda mfupi za kisiasa, mwaka 2018 Tanzania haikuuza Korosho nje ya nchi kutoka msimu wa 2018/19. Pia kitendo cha Serikali kuingia mkataba na kampuni ya kitapeli kutoka Kenya ili kununua Korosho kumesababisha Tanzania kuchelewa kuwahi soko la korosho kabla ya msimu wa mavuno wa nchi za Nigeria, Guinea Bissau, Benin, Ivory Coast na Indonesia kuingiza Korosho zao kwenye soko la dunia. Hasara ya Korosho itafikia TZS 1 trilioni na zaidi.

Pili: Ni ubinywaji wa Demokrasia nchini, msingi wake Mkuu ukiwa ni kuporwa kwa ushindi wa Chama cha CUF katika ngazi ya Uwakilishi na Urais kwenye Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa mwaka 2015. Kisha vitendo vya kuzuia Bunge Live, kuzuia mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa vya Upinzani (ya CCM ikiruhusiwa), na kuwabambikia kesi mbalimbali wanasiasa wa upinzani, kupigwa risasi kwa Mbunge Tundu Lissu akiwa kwenye eneo la Bunge, na Kutungwa kwa sheria mpya ya vyama vya siasa inayoua kabisa siasa za vyama vingi nchi.

Mfululizo wa matukio hayo yanayoua Demokrasia yetu nchini umepelekea Nchi Wahisani (wafadhili) kutoleta fedha za kigeni nchini. Pia uminywaji huu wa Demokrasia pamoja na matukio mengine ya ukandamizwaji wa haki za binadam vimesababisha mahusiano ya Tanzania na nchi zinazofadhili na kuchangia Bajeti na hata mashirika ya kimataifa kudorora. Baadhi ya mashirika na nchi zikifuta kabisa misaada na huku wengine wakizuia au kuchelewesha kutoa fedha za kusaidia bajeti yetu ya Maendeleo.

Tatu: Ni kushuka kwa Fedha za Kigeni zitokanazo na mitaji ya uwekezaji nchini. Tangu Serikali ya awamu ya tano iingie madarakani mitaji kutoka nje imeshuka kutoka 5% ya Pato la Taifa kwa mwaka 2015 mpaka kufikia 2% ya Pato la Taifa kwa mwaka 2018. Msingi wa kushuka huko kwa uwekezaji wa mitaji ni kutokuwepo kwa hali ya uhakika kwenye usimamizi na uendeshaji wa Sera za Uwekezaji nchini.

Athari Gani Zitarajiwe Kutokana na ya Hali Hii?

1. Uwezo wetu wa kulipa madeni ya Mikopo na ya Wakandarasi wa Miradi mikubwa utashuka mno. Inatarajiwa kuwa Serikali itashindwa kulipa wakandarasi wa miradi yake mikubwa au kama ikiwalipa basi ita’default’ malipo ya madeni ya Taifa yaliyowiva au kuchelewesha mishahara ya watumishi wa umma. Athari za jambo hili zimeshaanza kuonekana, kwa nusu mwaka wa Fedha wa 2018/19 kiwango cha fedha za umma zinazotumika kuhudumia deni la Taifa kimeongezeka sana, hiyo ni kwa sababu madeni kadhaa yamewiva na pia Serikali ya Rais Magufuli inachukua mikopo mingi yenye riba ghali na ya muda mfupi kutoka kwenye Benki za Biashara. Kwa miaka miwili sasa mikopo ya kuendesha Bajeti inatoka Benki kama HSBC, CreditSuisse na mabenki mengine ya Nje yenye riba kubwa na kutukopesha kwa fedha za kigeni.

2. Athari ya pili kubwa itakuwa ni kupanda kwa gharama za kuhudumia deni la Taifa. Nionavyo, Kwa kuwa Serikali hii ni kiburi na isiyo sikivu, itaamua kuendelea kukopa kutoka benki za nje kwa fedha za kigeni ili kuficha aibu kwa Wananchi na hivyo kuingiza nchi kwenye madhara makubwa zaidi. Gharama za kuhudumia deni (debt services) litakuwa kubwa kiasi cha Serikali kushindwa kutoa fedha kwa matumizi mengine kama vile Elimu na Afya. Kwa sasa, katika Kila TZS 100 inayokusanywa nchini, zaidi ya shilingi 80 inakwenda kwenye kuhudumia deni la Taifa na mishahara ya watumishi wa umma. Kwa kushuka huku kwa thamani ya Shilingi pamoja na ukopaji wetu wa Kiholela kwenye Benki za Kibiashara, ni dhahiri kuwa fedha zote tunazozikusanya tutaishia kulipa madeni na mishahara tu.

3. Gharama za Uzalishaji Viwandani itakuwa kubwa zaidi, hasa kwa upande wa Sekta binafsi. Viwanda vyetu hutegemea sana ununuzi wa mitambo, vipuri, na malighafi za kuzalishia bidhaa za viwandani kutoka nje ya nchi, kwa kushuka thamani ya shilingi yetu dhidi ya Dola ya Marekani, ununuzi wa vyote hivyo utakuwa ghali zaidi kwa sababu malighafi nyingi zinatoka nje ya nchi na hunuliwa kwa dola ya Marekani. Matokeo ya jambo hilo itakuwa ni kuongezeka bei ya bidhaa za Viwandani na hata kushindwa kununulika na wananchi, na kushindwa kushindana kwenye soko na bidhaa za Nje ya nchi ambazo gharama zake zitakuwa ndogo zaidi. Wananchi watatumia shilingi nyingi zaidi kununua bidhaa ile ile waliyokuwa wakinunua kwa bei ndogo wakati sarafu yetu ilipokuwa na nguvu sokoni. Tayari Wafanyabiashara Katika sekta binafsi wameanza kuhangaika kupata fedha za kigeni maana hazipatikani sokoni. Sekta binafsi itajikuta inafunga Biashara na kusababisha watu wengi kukosa Ajira.

Nini Kifanyike Kuokoa Hali Mbaya Iliyoko?

1. Serikali Irudishe hali ya soko la Korosho ilivyokuwa kabla ya mwaka 2018/19, kwanza kwa kufanya marekebisho ya sheria na kurudisha Fedha zote za Export Levy kwa Wakulima wa Korosho ili zitumike kuwapa bure mbolea, salfa na madawa mengine ili kuwapa motisha na hali ya kukata tamaa iliyotokana na msimu huu wa manunuzi. Serikali iwalipe kwa haraka wakulima wote waliopeleka korosho kwenye vyama vya msingi, izichukue korosho inazozirudisha sasa kwa wakulima na iwalipe, na kisha itafute masoko ya korosho hizo hata kwa kuuza kwa Serikali kwa Serikali.

2. Serikali ikae chini kufanya mazungumzo ya kutafuta muafaka juu ya Ushindi wa Chama cha CUF ulioporwa kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 wa Zanzibar. Muhimu zaidi Rais kama Mkuu wa Nchi na mkuu wa chama kilichopora ushindi wa CUF, aombe kikao na Katibu Mkuu wa CUF na aliyekuwa Mshindi wa Urais kwenye Uchaguzi huo wa mwaka 2015 wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad ili kujenga msingi wa kupata suluhisho la haki ya Wazanzibari kupata Serikali waliyoichagua Oktoba 25, 2015.

3. Serikali ikubali kufanyika kwa uchunguzi huru wa shambulio na jaribio la kuuawa kwa mnadhimu mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, mbunge Tundu Lissu ili kupata ukweli juu ya nani hasa alihusika na shambulizi husika na hatua zichukuliwe juu ya wahusika hao. Jambo hili litaondoa hali ya shutuma juu ya Serikali kuhusika na shambulizi hilo. Uchunguzi huru wa namna hiyo ufanyike juu ya kupotea kwa Ben Rabiu Saanane, mwanasiasa na mwanaharakati kijana, Mwanahabari Azory Gwanda, na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kibondo, Simon Kanguye.

4. Kurudisha hali ya ufanyaji siasa huru kwa vyama vya Upinzani iliyokuwepo kabla ya Serikali ya Awamu ya Tano kuingia madarakani, jambo hilo lihusishe kufutwa au kurekebishwa kwa Sheria Kandamizi kama Sheria ya Habari ya mwaka 2016, Marekebisho ya Sheria ya Takwimu, Sheria Mpya ya Vyama vya Siasa, Sheria ya Mtandao (Cyber Crime) nk, pamoja na kuondoa zuio haramu la mikutano ya Vyama vya Siasa vya Upinzani nchini, kuunda Tume Huru ya Uchaguzi pamoja na kuwaondoa Wakurugenzi wa Halamashauri (ambao ni Makada wa CCM) kuwa Wasimamizi wa Uchaguzi nchini.

5. Serikali iache siasa huru na wazi nchini kwa kurudisha Bunge Live na kuzifuta kesi zote ilizowafungulia wanasiasa, wafuasi na wanachama wa vyama vya Upinzani nchini. Kufutwa kwa kesi hizo ambazo nyingi ni za kubambikia kutapunguza chuki ya kisiasa inayojengeka kwa kasi nchini na kurudisha umoja wa kitaifa unaopotea kwa kasi.

6. Iundwe Kamati ya Kitaifa ya Vipngoni na Wanasiasa wa Vyama vyote nchini ya kusaidia mazungumzo na mashirika na nchi wahisani ili kurudisha mahusiano mabaya ya sasa kati yao na nchi yetu, mahusiano yanayowafanya wakatishe, kuzuia au kuchelewesha michango yao ya kifedha kwenye Bajati ya Taifa.

2. Mabadiliko makubwa yafanyike Wizara ya Fedha na Benki Kuu ili kuwezesha uendeshaji mzuri wa sera za kiuchumi (Fiscal Policy) pamoja na usimamizi imara wa Fedha za Umma. Ripoti Maalum ya CAG juu ya Kutoonekana kwa TZS 1.5 Trilioni imeonyesha Hazina imeoza, na Athari zinazoonekana sasa kwenye uchumi, hasa kuporomoka kwa mitaji ya uwekezaji, zinataka mabadiliko makubwa yafanyike BOT.

Rais anaweza kumuomba Gavana wa zamani, Profesa Beno Ndulu, au mtu yeyote mwenye Kaliba yake, kuwa Mshauri Mkuu wa Uchumi kwa angalau mwaka mmoja wa mpito wa kurekebisha Uchumi.

MUHIMU:

Najua Rais magufuli hatafanya hata moja kati ya haya niliyoyashauri licha ya yeye mwenyewe kujua hali ni mbaya sana kiuchumi nchini, Lakini kama Kiongozi wa Taifa hili ninao wajibu wa kutoa mchango wangu wa mawazo wa kututoa kutoa kwenye hali mbaya tuliyonayo.

Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Mbunge, Kigoma Mjini
Kiongozi wa Chama, ACT Wazalendo
Februari 25, 2019

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Back
Top Bottom