Sheikh Alhad atoa pole maandamano Kenya

Oldmantz

JF-Expert Member
Jan 24, 2023
428
996
Mwenyekiti wa Jumuiya za Amani na Maridhiano Tanzania, Sheikh Alhad Mussa ametoa pole kwa waathiriwa nchini Kenya kufuatia madhara yaliyosababishwa na maandamano vikiwemo vifo na uharibifu wa mali nchini humo.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jana jijini hapa Sheikh Alhad amesema Jumuiya hiyo ya Maridhiano inatoa pole kwa wakenya kwa madhara yaliyotokea Jumatatu wiki hii kufuatia maandamo nchini humo.

"Uharibifu uliotokea ni jambo ambalo halikubaliki, kuchoma nyumba za ibada kama ule msikiti na lile kanisa pamoja na uharibifu mkubwa uliotokea ni mambo yasiyofaa na yametusikitisha sana," amesema Sheikh Alhad.

Sheikh Alhad ameongeza kuwa Kenya ni ndugu na Tanzania na wanajumuiya wa Afrika Mashariki hivyo uvunjifu wa amani nchini humo unaweza kuambukiza au kusababisha wakimbizi ambao watakimbilia nchi jirani na kwamba asingependa kuona taifa hilo likifikia huko.

Aidha Sheikh Alhad ametoa Wito kwa serikali ya Kenya na wanasiasa nchini humo kuona namna ya kutafuta maridhiano huku akiwataka kutanguliza mbele maslahi ya taifa kabla ya udini na ukabila.

"Tunawaomba Wakenya kuchukua mfano mzuri wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu kwa kusimamia maridhiano ya kweli ya kisiasa na Kuwafanya Watanzania kuishi kwa salama na amani," amesema Alhad.

Pia amewataka Wakenya na wanasiasa nchini humo kuona thamani ya amani na kukaa pamoja kuridhiana kama ambavyo Rais wa Tanzania alivyofanya nchini.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo Askofu Dk. Israeli Maasa alitilia msisitizo suala la mapatano na maridhiano kwa taifa hilo jirani.

"Ndugu zetu wa Kenya wajue kuwa amani ni bora kuliko cheo, na ni muhimu kila mtu kutambua faida ya amani ndani ya nchi," amesema Askofu Maasa.

Aidha, Askofu Maasa ameendelea kueleza kuwa maslahi ya nchi ni bora kuliko maslahi ya mtu binafsi, hivyo ni vizuri kutanguliza maslahi ya taifa ili kuwa na amani kwa watu wote.

"Mazungumzo yanajenga maridhiano kuliko maandamano na vurugu. Ninawaomba viongozi wa Kenya wafanye mazungumzo ya maridhiano na mapatano ya pamoja," aliongeza Askofu Maasa.

Tangu maandamano yaanze wiki iliyopita nchini Kenya, takribani watu watatu wameuawa katika ghasia hizo.

Katika mtaa wa Kibera jijini Nairobi, ambako kiongozi mkuu wa upinzani nchini humo Raila Odinga anaungwa mkono sana, polisi waliwarushia vitoa machozi waandamanaji waliokuwa wakiwarushia mawe Jumatatu wiki hii.

Odinga na muungano wake wa Azimio la Umoja kwa mara ya kwanza waliitisha maandamano mapema mwezi huu kupinga kushindwa kwa serikali kudhibiti kupanda kwa gharama za maisha na kile anachosema ni ushindi wa udanganyifu wa Rais William Ruto katika uchaguzi wa Agosti mwaka jana.

Ingawa ushindi huo uliidhinishwa na mahakama ya juu zaidi nchini Kenya, Odinga anasisitiza kuwa uchaguzi huo "uliibiwa" na ameitisha maandamano kila Jumatatu na Alhamisi.

Wakati muda wa aliyekuwa Rais Kenyatta ukikaribia mwisho, alichagua kumuunga mkono aliyekuwa mpinzani wake Odinga badala ya naibu wake Ruto.

MWANANCHI
 
Back
Top Bottom