Shajara ya Madikteta

MALCOM LUMUMBA

JF-Expert Member
Jul 26, 2012
20,897
63,783
UTANGULIZI
Nawasalimu katika Jina la Bwana Yesu na Asalaam Aleykum ndugu watanzania wenzangu,

Katika kusoma kwangu historia ya ulimwengu toka nikiwa kijana mdogo mpaka hii leo, nimetambua kwamba madikteta wote duniani huwa wanafanana: Awe katokea Ulaya, Asia, Amerika Kusini au Afrika wote huwa wanafanana. Kwanini wote huwa wanafanana ???

Tofauti na wengi wanavyoamini kwamba udikteta ni mfumo wa kiutawala wa kutumia mabavu, binafsi nimetambua kwamba Udikteta ni MFUMO WA KIIMANI AMBAO HUZAAA DINI ambayo hutumika kama chombo kutawala nchi husika katika kipindi chote cha utawala wa huyo dikteta. Huu mfumo wa kidini na kiimani huonekana hata kwenye nchi zile ambazo haziamini katika uwepo wa Mungu.

Mfumo huu hujikita zaidi katika kumfanyia ibada binafsi ya sanamu mtawala (A Cult of Personality) kwa kuangalia sifa zake binafsi ambazo waumini wake, ambao ni wananchi huamini kwamba zinaweza kuwasaidia wao kufika nchi ya ahadi. Mwanafalsafa wa Ujerumani Max Weber aliyeishi mnamo karne za 19 na 20 aliita huu mfumo wa kikarismatiki (Charismatic Leadership), ambapo nchi hutegemea sana sifa binafsi za mtawala kuliko mfumo wa kikatiba na sheria.

Nimefuatilia madikteta mashughuli duniani kuanzia Dola ya Roma ya Kale, Urusi ya Kisovieti, Ulaya ya Kifashisti na Uchina ya Kikomunisti. Kaisari Caligula (The Mad Emperor), Joseph Stalin (The Man of Steel), Adolf Hitler (The Fuhrer), Benito Mussolini (The Duce) na Mao Zedong (Chairman Mao) wanafanana sana tabia unaweza kudhani ni watoto wa baba moja, japo wametawala katika nyakati na nchi tofauti .

Kinachofanya hawa madikteta wafanane ni mfumo wa kidini wa wao kuabudiwa, ambao walijetengenezea kipindi cha utawala wao. Muhimu cha kukumbuka ni kwamba wote hawa walifanya mambo makubwa mno kwa nchi zao kwa muda wa kipindi kifupi sana; hadi kupelekea nchi zao kuwa mataifa makubwa sana duniani yenye nguvu kubwa kiuchumi na kijeshi huku mamilioni ya watu wakiachwa wamekufa, masikini wa kutupwa na wasiofurahia uhuru wao binafsi.

Lakini kikubwa ambacho kimenifanya niandike hii mada, ni kile ambacho hutokea punde baada ya hawa madikteta kutoka madarakani. Madola yote yaliyotajwa hapo juu yaliachwa kwenye songombingo kubwa za kisiasa ambazo zilisababishwa na ombwe la uongozi ambalo liliachwa na hawa madikteta. Hebu nilithibitishe hili kwa kupitia dikteta moja baada ya mwingine:

SEHEMU YA KWANZA: DIKTETA KAISARI CALIGULA WA ROMA
Huyu jamaa alitawala Roma ya kale, moja ya dola ambalo limeshawahi kuwa na nguvu kubwa sana duniani kwa miaka zaidi ya elfu moja. Utawala wa Caligula utakumbukwa kama moja ya kipindi ambacho Roma ya kale ilidharaurika sana kwasababu wengi waliamini kwamba mfalme alikuwa ni kichaa.

Caligula alileta maendeleo Roma kwa haraka sana, atakumbukwa kwa kujikita kutengeneza mfumo imara wa kodi, na kufanya miradi mikubwa sana ya ujenzi mingi ambayo ilikuwa haina faida kwa Roma bali kwake binafsi. Alitoza kodi kwenye harusi, kesi za mahakamani hadi kwenye biashara ya ukahaba. Pia alifanya miradi mikubwa sana ya ujenzi kama madaraja ili aweze kuvunja historia ya wafalme wa Umedi na Uajemi. Lakini atakumbukwa kwa kujenga bandari kubwa ambayo ilisaidia Roma kupata wingi wa nafaka kutoka Misri.

Lakini sasa, wanahistoria kama Flavius Josephus wanasema Caligula atakumbukwa kwa kuwa mtu mwenye hasira za haraka na ambaye alikuwa anaua watu bila kuwapeleka mahakamani kama walishindana naye. Inasemekana Caligula alifanya matumizi makubwa kwenye miradi yake hadi kupelekea mlipuko wa njaa nchini Roma. Alitengeneza miundombinu mikubwa kama barabara, mahekalu, ikulu ya mfalme na madaraja makubwa: Miradi mingine haikuwa na umuhimu lakini alikuwa anataka kuwathibitishia maadui zake waliowahi kumtukana kabla hajawa mfalme kwamba yeye siyo kitu na hawezi kuwa mfalme.

Ili kupambana na hili baa la njaa, alilosababisha yeye mwenyewe, Caligula kwa matumizi mabaya ya rasilimali za umma, alianzisha mfumo wa kuteka, kutishia na kuua raia matajiri ili awanyang'anye mashamba na mali zao huku akitumia majasusi wake hatari wa Pritorio (The Praetorian Guards). Ikumbukwe hadi leo wanahistoria wanasema baada ya wale wanajeshi wa Ugiriki ya Sparta (The Spartans) na Samurai wa Japan ya Kikabaila (The Feudal Japan) hawa wanajeshi wa Pritoria wa Roma (The Praeotorian Guards) wanakumbukwa kwa kuwa na mafunzo makali na uwezo mkubwa sana wa kijasusi na kijeshi, hivyo ilikuwa silaha kubwa sana ya Caligula.

Matendo ya Caligula yalimfanya aingie kwenye mtafaruku mkubwa na Bunge la Roma (The Senate), ambapo katika kushindana nao aliamua kuongeza wabunge wengi ili kupunguza nguvu za Bunge. Ikumbukwe viongozi wa zamani wa Roma, hasa wabunge walikuwa wanatoka familia za kibwanyenye au wanajeshi mashujaa. Lakini Caligula aliingiza watu wa kila namna huku akijinasibu kusema kwamba yeye ni muwazi na anataka watu washindane lakini kumbe yote ni kupambana na bunge ili watu wake waingie.

Hakuishia hapo, Caligula atakumbukwa kwa kuwa mtawala mwenye majivuno mbele ya umma. Inasemekana alikuwa akienda mbele ya watu au kwenye matukio alikuwa akimwaga mapesa sana na zawadi kedekede. Lakini pia alikuwa akipenda kujisifia hadharani hata pale alipolala na wake za watu. Kikubwa atakochokumbukwa kukifanya kwenye majivuni yake ni kutengeneza meli mbili kubwa sana ambazo alizitumia yeye binafsi, inasemekana kwa miaka ile hizi ndizo zilikuwa meli kubwa zaidi duniani.

MWISHO WA CALIGULA NA MADHARA YA KISIASA ALIYOYAACHA ROMA
Caligula alifikia mahali pabaya sana, ambako aliwaaminisha baadhi ya watu kwamba yeye ni mwana wa miungu ya kale ya Ugiriki na Roma. Alikuwa akienda kutembea nje, basi ni lazima avae dirii ya kifuani ya mfalme Alexander Mkuu (Alexander The Great), au Zeu (Zeus) huku akitaka watu wamwabudu. Ikafika mahali akataka kujenga sanamu lake na kuliweka ndani ya hekalu la Mfalme Suleima kule Yerusalemu ili aabudiwe kama Mungu.

Mambo haya yalimtengenezea maadui wengi, ambapo alifanyiwa majaribio mengi sana ya kuuwawa lakini walinzi wale wa Pritoria (The Praetorian Guards) walimlinda vizuri. Aliuwa wabunge, kutesa matajiri na mahakimu. Lakini kama ambavyo Bunge la Roma lilimfanya mfalme Julius Kaisari (Julius Ceaser) kwa kumchoma visu ili kuliokoa taifa, vivyo hivyo njama kubwa ilipangwa dhidi yake ili kuiokoa Roma.

Walinzi wake wa Pritorio ambao aliwapa nguvu kubwa kinyume na matakwa ya bunge, walikuja kutumika kumgeuka na kumuua Kaisari Caligula na kuchagua Kaisari wao mpya waliomtaka wao. Mwanahistoria nguli kutoka Uingereza, Guy de la Beboyere kwenye kitabu chake kiitwacho PRAETORIAN: THE RISE AND FALL OF ROME'S IMPERIAL GUARS, anaeleza kwamba baada ya walinzi kumuua Caligula walikimbilia kwenye kambi yao kujificha huku kila mtu kutoamini kilichotokea nchini.

Baada ya kuona hakuna madhara na kuna ombwe kubwa sana la madaraka ambalo lilitokana na Caligula kuvuruga mifumo ya utawala, hawa walinzi wa Praetorian wakajikuta wao ndiyo wana nguvu kubwa ndani ya Roma. Hivyo wakaamua wao wenyewe kufanya jambo la kishenzi la kufanya mnada kiti cha kifalme kwa mtu yeyote aliyetoa dau kubwa; hili lilileta matatizo makubwa sana na mtifuano mkubwa kisiasa hadi kupelekea nchi kuingia kwenye kipindi kigumu ili kuirudisha nchi kwenye mstari.

TUNAJIFUNZA NINI KWENYE HILI?
Ukifuatilia utashangaa kwanini Roma ambayo ilikuwa ni kitovu cha ustaarabu barani Ulaya ilifikia hatua hii kihistoria. Lakini katika hii shajara nayoandika, nimetambua kwamba baada ya madikteta wengi kuondoka madarakani, lazima waache majeraha makubwa kisiasa na kiuchumi ambapo kama nchi itakosa watu wenye hekima na busara basi yanaweza kutokea matatizo makubwa sana.

Uchumi unaweza kuporomoka, unaweza kutokea mtifuano wa kugombania madaraka (Power Stuggle) ambao unaweza kuzaa uhaini au vita ya wenyewe kwa wenyewe na mauaji makubwa kutokana na kulipizana visasi. Haya madhara kihistoria hayakutokea Roma ya Caligula peke yake, bali yalitokea nchini Urusi ya Kisovieti mwaka 1953 baada ya kufariki Stalin, Mwaka 1945 baada ya Ujerumani kutambua kwamba imeshindwa vita, Mwaka 1943 baada ya Mussolini kuishiwa nguvu ya kisiasa nchini Italia na mwaka 1976 baada Mao Zedong kufariki.

Kilichotokea Roma baada ya Caligula kufariki, ndicho kilitokea Urusi, Uchina, Italia na Ujerumani. Lakini hili halijatokea kwenye hizi nchi peke yake, mifano iko mingi kuanzia hapa Afrika hadi kule Amerika, lakini kwa lengo la kujifunza hebu tujikite zaidi kwa haya mataifa makubwa.

SEHEMU YA PILI: JOSEPH STALIN WA URUSI YA KISOVIETI
Itaendelea............​
 
Ndicho kilichoikuta Zaire ya Mobutu, Somalia ya Siad Bare, Libya ya Gaddafi na Misri ya Mubarak. Mfumo wa kidikteta ni hatari sana, pindi unapoanguka kila kitu kibaya na kizuri katika taifa kinaweza kusambaratika.
Tuombe yasitukute.
 
Umesema kweli! Kweli! Kweli!

Hii hali nimeihisi, nilihisi pengine ni hisiya tu kwa vile mahesabu yenyewe ni ya makadirio na niliyafanya kwa kichwa na nikakadiria pia.

History ni fact na muda ni mwalimu mzuri, ngoja tuone kama ilipandwa mbegu, miti au maarifa. Nimeongeza vitu pia kutoka kwenye huu Uzi.

Nasubiri mwendelezo!
 
Ahsante Mkuu kwa makala murua

Ya Caligula yanafanana na Dikteta uchwara mmoja katika nchi za Afrika aliyekuwa akielekea kuwa Dikteta kamili. Ila ukubwa na mapenzi ya Mungu kwa Taifa lile akawaondolea Dikteta yule asilete madhara zaidi

Cha kuongezea Madikteta huwa ni marafiki wa wao kwa wao.
 
werevu tumejua unachotaka hadhira ielewe sawa tuu lakini..
 
Usiwasahau na madikteta walioleta uchumi imara.
Lee Kuan Yew
Na Yule wa Chile mzee wa economic miraclealisaidiwa na vijana wa chicago university nadhani.
 
Mkuu hapo kwenye kifo cha Joseph Stalin, ungerekebisha mwaka. Alifariki kati ya mwaka 1952/3 kwa kumbukumbu zangu.

Na baada ya kifo chake, nadhani USSR ilikuja kutawaliwa na Nikita Kruschev, kabla ya baadae kuja kupewa yule mjuaji Mikhail Gorbachev mwaka 1984 na kujikuta anaangukiwa na jumba bovu. (Kuanguka kwa Shirikisho la Kisoviet)

All in all, Udikteta ni mbaya sana! Uusikie tu kwa majirani. Ndani ya hii miaka 5/6, hakika baadhi yetu chamoto tumekiona! Miaka 6 hakuna kupanda daraja, hakuna nyongeza ya mshahara! Kisa, tunanunua ndege kwanza!!! ๐Ÿค”
 
Genius........utawala wa Mzee sidhani kama ulikuwa na tofauti na Stalin nimesoma historia yake na ile circle ake ya kina Beria na maamuzi yake

Mkuu unazidi kunifungua kumbe wengi madikteta walikuwa wana traits ZA kufanana

ngoja ni subscribe
 
Unajua kama ni msomaji wa vitabu heading ya title itakufunua au kukuangaza the content ambayo mwandishi anaenda kuandika

Shida watz wengi si wasomi ni watu wakwenda na habari na trends plus udaku
Exactly
 
Naamini ukiwa mwalimu wa History wanafunzi wako wataelewa sana na kufurahia somo lako. Hongera sana, umepangilia story vizuri,uchambuzi makini na nimeelewa sana. Be blessed
 
Back
Top Bottom