Mkulo, mkopo huu unaleta wasiwasi
Wednesday, 26 May 2010 04:36
Majira
SERIKALI imesema itakopa dola za Marekani mil.250 (sawa na sh. bil.350) kutoka benki ya Stanbic ili kuziba mapengo kwenye bajeti ijayo ya mwaka wa fedha wa 2010/11.
Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni jijini Dar es Salaam na Waziri wa Fedha na Uchumi, Bw. Mustafa Mkulo wakati akizungumza na waandishi wa habari .
Bw. Mkulo, alisema hatua hiyo imetokana na uamuzi wa baadhi ya wafadhili kupunguza michango yao kwenye Mfuko wa Bajeti (GBS) kwa jumla ya kiasi cha dola za Marekani 220
Akabainisha kwamba serikali ipo kwenye hatua za mwisho za mazungumzo kati yake na benki hiyo (Stanbic), ambayo imekubali kutoa mkopo huo utakaolipwa kwa kipindi cha miaka mitano na wakati huo huo, aliwatoa wasiwasi wananchi kwamba hatua hiyo kamwe haitaongeza mzigo kwa walipa kodi.
Pamoja na nia nzuri ya kuziba mapengo hayo, tunachelea kuunga mkono moja kwa moja hatua ya serikali kukopa fedha kwenye mabenki ya biashara kwa ajili ya matumizi yake.
Duniani hakuna serikali inayokopa kutoka kwenye mabenki ya kibiashara (commercial banks) kwa ajili ya matumizi yake. Hii inatokana na ukweli kwamba riba za benki hizo ziko juu na masharti ya marejesho yake, ni kwa muda mfupi.
Mashirika ya fedha ya kimataifa kama Benki ya Dunia (WB), Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Benki ya Maendeleo ya Afrika na mengine ya namna hiyo yenye riba nafuu, ndiyo yanayopaswa kuzikopesha serikali kama Tanzania na kamwe benki za kibiashara, haziwezi kukopesha nchi kwa ajili ya kuendesha shughuli zake kwenye bajeti ya serikali.
Mikopo inayotolewa na benki hizo inaweza kutumika tu kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwa maana ya kuongeza wigo wa kukusanya kodi.
Ni ukweli ulio bayana kwamba benki nyingi za kibiashara nchini riba zake ni kubwa kwa wastani wa asilimia 18 wakati vyombo kama IMF, WB, ADB riba zake ziko chini na vinatoa muda wa kutosha kurejesha fedha hizo na masharti nafuu ya kulipa.
Wasiwasi wetu ni kwamba pamoja na kauli ya Waziri Mkulo kuwa mkopo huu hauwezi kuwabebesha mzigo walipa kodi, bado tunaona jambo hilo haliepukiki.Ili kuzuia hilo, serikali itafute vyanzo vingine vya kuziba mapengo ya bajeti badala ya kukimbilia kukopa kwenye mabenki ya kibiashara.