Serikali irudishe hadhi ya shule za Umma

DolphinT

JF-Expert Member
Mar 9, 2016
1,308
1,828
Kuanzia kipindi cha mwaka 2010 mpaka hivi sasa tumeshuhudia juhudi za makusudi zikifanywa na serikali katika kuhakikisha kuwa sekta ya elimu licha ya kukua pia inatoa huduma bora kwa wahusika.

Miongoni mwa juhudi hizo ni pamoja na mpango wa ujenzi wa maabara katika kila shule ulioasisiwa na mheshimiwa Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete. Jambo hili kwa dhamira ya uanzishwaji wake lilikua na dhamira bora ya kuhakikisha kuwa wanafunzi wanasoma masomo ya sayansi kwa vitendo na sio kwa nadharia tena.

Mpango huu madhubuti ulishirikisha wadau mbalimbali wa elimu pamoja na washirika wa maendeleo na kwa kiasi kikubwa maabara nyingi zilijengwa na nyingine zikiwa katika hatua za mwisho za ujenzi.

Juhudi nyingine ni kuhakikisha upatikanaji wa madawati shuleni ili kutatua kero ya wanafunzi kukaa chini jambo ambalo liliwapa pia waalimu changamoto wakati wa ufundishaji. Sambamba na hili la madawati ambalo lilitokana na agenda ya elimu bure pia serikali imejitahidi kuhakikisha kuwa vyumba vya madarasa vinaongezwa ili kukabiliana na ongezeko la wanafunzi katika shule za umma.

Hali kadhalika serikali kupitia wizara ya elimu imeipandisha hadhi idara ya ukaguzi na kuifanya kuwa mamlaka ya kudhibiti ubora wa elimu huku ikihakikisha kwa kadri ya upatikanaji wa fedha wanawezeshwa kwa rasilimali watu na mahitaji mengine ili kufanikisha majukumu yao ya usimamiaji wa ubora wa elimu.

Sambamba na hilo ujazaji wa fomu maalum za mapitio ya utendaji kazi kwa watumishi wa umma yani "OPRASS" Ili kwafanya walimu kujiwekea malengo na mkataba na mwajiri ili kuhakikisha ufanisi katika kazi kwa kipindi cha nusu mwaka na mwaka mzima. Lengo kuu ni kuinua kiwango cha ufaulu kwa kubresha suala zima la ufundishaji na ujifunzaji.

Licha ya juhudi hizi zinazofanywa na serikali bado yapo maeneo kadhaa ambayo yanahitaji kutupiwa jicho ili kuhakikisha kwamba shule za umma ambazo ndio kimbilio la watanzania wengi zinakua na hadhi na ubora kama ilivyokuwa hapo siku za nyuma ili watanzania weweze kunufaika nazo.

Sekta binafsi imepewa nafasi kushirikiana na serikali katika suala la utoaji wa elimu, na hivyo kutoa mchango mkubwa kuhakikisha kuwa watanzania wanapata elimu. Kinachotokea hapa ni sekta binafsi kuboresha huduma ya elimu na kuwafanya watanzania wenye kipato cha juu kuzikacha shule za umma na kukimbilia katika shule binafsi ambapo hapo awali mambo yalikua tofauti.

Ukitizama kwa makini utagundua kwamba shule za umma hasa za msingi na zile za sekondari kidato cha kwanza mpaka cha nne haziaminiki katika kutoa elimu iliyo bora. Ndiyo maana watu wenye uwezo kifedha hawako tayari kuwapeleka watoto wao katika shule hizo.

Hii imeendelea kujenga madaraja miongoni mwa watanzania walio wengi kwani shule za umma zimebakia kuwa za maskini na zile za binafsi kuwa za watu wenye uwezo mkubwa kifedha

Kwa mkakati wa serikali kwa sasa kusimamia suala la nidhamu kazini naamini kwamba kutakua na mabadiliko makubwa katika sekta ya elimu kwa siku za mbeleni suala ambalo linakwenda sanjari na upelekaji wa fedha za elimu bure kwa wakati na kwa kiwango kinachohitajika huku waliopewa dhamana ya kuzisimamia wakifanya hivyo kwa uaminifu mkubwa.

Ili kurudisha imani kwa watanzania kuziamni shule zetu za umma hasa za msingi na sekondari za kata serikali inapaswa kuhakikisha kuwa inaajiri walimu wa kutosha katika masomo yote kwa kutumia mfumo ambao unahikisha walimu bora na wenye weledi katika masomo husika kinadharia na katika ufundishaji.

Kuhakikisha kuwa maafisa elimu pamoja na idara ya usidhibiti ubora wa elimu wanafanya kazi kwa pamoja kuhakikisha kuwa walimu waliopo wanafanya na kutimiza majukumu yao kwa mujibu wa ratiba na maelekezo yanayotolewa. Wakuu wa shule wawezeshwe kimafunzo ili waweze kuwaongoza walimu na wanafunzi katika kufikia malengo yao.

Serikali ihakikishe kuwa inaajiri mafundi sanifu maabara wa kutosha ili waweze kuwasaidia walimu wa masomo ya sayansi kuwafundisha wanafunzi kwa vitendo na nadharia ili kujenga kizazi cha wataalamu wa sayansi watakoijenga Tanzania ya viwanda tunayoitaka.

Hali kadhalika serikali ihakikishe kuwa vifaa vya maabara na kemikali vinapatikana kwa uhakika na kwa wakati katika maabara zilizojengwa ili kuwasaidia wanafunzi kujifunza kwa ufanisi zaidi.

Bila kusahau masomo ya sayansi ya jamii ni vyema serikali kwa kua imejizatiti kuhakikisha kwamba watanzania wote wanapata elimu bora ihakikishe kuwa vitabu vya masomo ya sayansi ya jamii vinapatikana mashuleni na kwa uwiano unaostahili ili kila mwanafunzi aweze kutimiza malengo yake akiwa shuleni hapo.

Ni dhahiri kwamba wamiliki wa shule binafsi wamejihakikishia ushindani katika soko la huduma ya elimu kwa kuhakikisha kuwa mambo yaliyotajwa hapo juu yanafanyiwa kazi kwa uhakika mkubwa

Utoaji wa elimu bora hauzingatii tu huduma bora kwa wanafunzi pamoja na mazingira bora ya kujifunzia hali kadhalika upatikanaji wa vitabu pekee bali pia uwepo wa walimu bora wenye ari ya kufundisha na kupeleka maarifa kwa wanafunzi.

Iwapo tunataka kurudisha hadhi ya shule zetu za umma serikali inapaswa kuhakikisha kuwa utaratibu wa kuwapata walimu nao unakua katika mfumo imara na unaoeleweka. Sekta binafsi hutumia mfumo wa usaili wa nadharia na vitendo; Hii ni kuhakikisha kuwa walimu wanaoajiriwa wanakidhi matakwa na mahitaji ya wateja kwa maana ya kuwa weledi katika masomo husika na katika mambo yaliyo nje ya ufundishaji mathalani malezi ya wanafunzi pia kuweze kufundisha kwa usahihi na ufasaha wawapo madarasani. Na baada ya hapo kupewa kipindi maalumu cha uangalizi kabla ya kupewa mikataba ya kudumu ya ajira zao

waswahili husema "kama elimu ni ghali, jaribu ujinga" Ni dhahiri kuwa wapo watakaokosoa suala hili kufanyika katika shule za umma hasa kwa kuzingatia suala la gharama. Ni dhahiri kuwa serikali yetu imeweka kipaumbele katika maendeleo hasa katika bajeti zake. Tukubaliane kwa pamoja kuwa elimu ni suala la maendeleo. Taifa lolote linalopiga hatua katika suala zima la maendeleo ni lazima liwekeze katika elimu. Hivyo serikali lazima ikubali kuingia gharama katika kurudisha hadhi ya shule zake.

Katika shule binafsi suala la maslahi na stahili za walimu limekuwa likiwe kipaumbele. Ingawa hakuna malipo yanayoweza kulipa kazi ya ualimu lakini kwa ulinganifu maslahi ya walimu katika shule za umma yanakatisha tamaa na hivyo kuwafanya walimu kufanya kazi bora liende au kwa mazoea.

Ikumbukwe kwamba kazi ya ufundshaji matokeo yake hupimwa na mitihani baada ya kipindi fulani na mwalimu halazimishwi kufundisha ila hutakiwa kufundisha akiwa katika hali ya kuipenda kazi yake. Serikali ipitie upya maslahi ya walimu kwa kutambua mchango wao katika maendeleo ya taifa hili. Stahili za likizo, nyongeza ya mishahara pamoja na suala la upandishwaji wa madaraja ni kilio cha walimu wengi.

Imefikia hatua walimu wanajiuliza "kwanini serikali imeamua kuwapunguzia hata mishahara? Hii inatokana na ukweli kwamba wanaishi katika mwaka mpya wa bajeti ambao gharama za maisha zimepanda huku mshahara ukiwa uleule jambo ambalo halina utofauti na kupunguziwa mshahara.

Tumeskia matamko na maagizo ya viongozi wa serikali kuwa walimu wa shule za umma wasijishughulishe na shughuli nyingine kama kupiga picha na kuendesha boda boda. Kimsingi hawapendi kufanya hivyo lakini je ni vipi watakabiliana na ugumu wa maisha bila kujiongezea kipato huku wakiamini kuwa serikali yao imewasahau? Tujiulize walimu wa sekta binafsi wanafanya haya? Kama hawafanyi kwanini hawafanyi?

Walimu wenye ari ambao jamii na serikali inawajali watafundisha kwa moyo na ari kama wale wa shule binafsi.
Suala la makazi ya walimu au nyumba za walimu ni kazi nyingine ambayo serikali inabidi ifanye kazi ya ziada. Binafsi naamini Serikali hii inaweza hata kwa awamu kwani tumeona mengi yamewezekana. Tuna imani na mheshimiwa Rais ambae licha ya kuwa mwalimu anazijua changamoto za walimu hasa kwenye suala la makazi.

Ikiiwa imeshindikana kutokana na ufinyu wa bajeti basi ni vyema serikali ikatenga kiasi fulani cha fedha kama posho ya nyumba "housing allowance" kwa walimu ili kuwavutia katika kufanya kazi yao kwa ufanisi mkubwa na kuongeza ushindani. Kuwalazimisha walimu kukaa katika mazingira duni na yasiyo rafiki kamwe hakutaboresha elimu bali kutaifurahisha jamii ya eneo husika kuwa kuna walimu. Cha msingi ni kuwaboreshea walimu mazingira ya kazi.

Suala la mafunzo kazini liwekwe mstari wa mbele, kutokana na mabadiliko ya mara kwa mara katika sekta ya elimu ni vyema walimu wakapewa mafunzo kazini ili kunolewa na kuweza kuendana na mabadiliko hayo na sio kuishia kuewa maagizo ambayo wakati mwingine huwatatiza na kuwaweka njia panda.

Sanjari na hilo ni vyema serikali pia ikaziboresha shule za bweni hasa zilizoko vijijini kwa kuhakikisha kwamba zinaongezewa mabweni pamoja na mahitaji mengine ikiwemo madarasa na maabara ili kupokea wanafunzi wengi zaidi ambao watakaa sehemu moja na kuweza kupata elimu.

Hali kadhalika shule hizi zijengewe utaratibu wa lazima wa kujifanyia shughuli za uzalishaji mali ikiwemo kilimo na ufugaji ili ziweze kujitiosheleza kwa chakula na kuacha kuitegemea serikali. Shule zilizopo katika maeneo ambayo ni rafiki kwa kilimo zijengewe utaratibu huo, hii itasaidia pia kuwafanya wanafunzi kufanya na kujifunza shughuli za uzalishaji mali ambazo zitawasaidia pindi watakapomaliza masomo yao.

Tunatamani siku moja majina ya shule zetu za umma kulingana na michepuo yake yatamkwe miongoni mwa wazazi, walimu na wanafunzi mfano, Ifunda girls, Moshi Technical, Ndanda, Kantalamba, Galanos, Minaki, Pugu, Azania, Tambaza, Mirambo, Ilboru, Lyamungo, Mtwara Technical, Ashira, Weruweru, Bwiru, na nyingine nyingi.

Nitoe rai kwa wadau, wanasiasa, watunga sera na wananchi kwa ujumla, kwa jinsi tunavyozungumzia maswala mengine ya kimaendeleo kama miundombinu, maji, umeme na afya, suala la elimu tena elimu bora kwa shule za umma liwe kinywani mwetu hasa tukizingatia mambo yote niliyoyaainisha hapo juu moja moja na kwa ujumla wake.

Kuboresha na kuhakikisha kuwa shule za umma zinakuwa na hadhi na ubora ni jambo linalowezekana kwani licha ya kuwa ni kiu ya watanzania lipo pia katika ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi Sura Ya 4, inayozungumzia huduma za jamii ikiwemo elimu. Na kwakua ni ahadi basi serikali yetu ina wajibu wa kulifanyia kazi ipasavyo ikiwashirikisha wananchi na wadau wa maendeleo hasa sekta ya elimu na mafunzo.

Binafsi naamini kwamba utekelezaji wa mambo haya kwa kiasi kikubwa utasaidia kurudisha hadhi na ubora wa shule zetu za umma na kuzifanya kuwa kimbilio la watanzania wote bila kujali kipato chao na mazingira wanayotoka.​
(Angalizo: Makala hii nilipata kuiandika katika gazeti moja la kila siku na ukurasa wa facebook)
 
Back
Top Bottom