Ninakubaliana na Mtatiro kuhusu pesa nyingi inayotumika katika kuandaa chaguzi ndogo lakini sikubaliani nae pendekezo la kurithishana kichama. Kwani wananchi wanapopiga kura hawachagui chama bali wanachagua mgombea.
Kwahiyo kama mgombea waliyempenda na kumchagua amefariki, wanayo haki ya kuchagua mtu mwingine wa kuwawakilisha, chama hakiwezi kupora madaraka ya wananchi na kuwachagulia muwakilishi wao.
Jambo la msingi kwa sasa ni kuhakikisha kwamba kunakuwa na udhibiti wa matumizi makubwa ya fedha katika chaguzi zetu. Kwakuwa sheria ya gharama za uchaguzi ipo ni vizuri vyombo husika yaani serikali, vyama vya siasa, msajili wa vyama vya siasa pamoja na vyombo vya dola vikasimamia utekelezaji wa sheria hiyo, na kama ina mapungufu ifanyiwe marekebisho ili tuweze kudhibiti matumizi makubwa na yasiyokuwa ya lazima katika chaguzi ndogo.
Tatizo lililopo katika utekelezaji wa sheria ya gharama za uchaguzi kwa sasa ni kwamba watumiaji wakubwa fedha nyingi katika chaguzi ni ccm kwahiyo serikali na msajili wa vyama wanashindwa kuiwajibisha.
Ushauri kwa mdogo wangu mtatiro, aache kuwaza ki-ccm, ni muhimu akajitahidi kuwa na mawazo ya kimapinduzi na mtazamo wa mageuzi wenye kuruhusu demokrasia shirikishi. Kutoa wito wa kutaka chama kiteue muwakilishi wa wananchi bila ridhaa yao huo ni uvunjwaji wa makusudi wa demokrasia kwa wananchi kumchagua muwakilishi wao. Kama cuf nayo imefika mahali sasa inataka kufifisha mamlaka ya umma, basi huko inakoelekea ni kaburini.