Sera Mbadala: Sheria Ndiyo itakayotawala na hakuna mtu yeyote aliye juu ya Sheria

Mwanahabari Huru

JF-Expert Member
Mar 9, 2015
14,260
2,000
#SeraMbadala

UKURASA WA 6

UTAWALA WA SHERIA

- Sheria Ndiyo Itakayotawala na Hakuna Mtu Yeyote aliye juu ya Sheria.

- Kuzuia Utawala Usiozingatia Sheria.

- Kudumisha Uhuru na Kupiga Marufuku Ukamataji wa Wananchi Usiozingatia Sheria.

- Kutolimbikiza Madaraka kwa mtu mmoja.

HII INA MAANA GANI KWETU:

Chadema inaamini katika utawala wa sheria ambao unatoa uhuru, ambapo sheria ndiyo inayotawala na hakuna mtu aliye juu ya sheria. Chadema itazuia utawala usiozingatia sheria, mathalani ukamataji wa holela na ubambikizaji wa kesi. Katiba itaweka mamlaka za uhakika kwa ajilli ya kulinda na kuhakikisha kwamba sheria ndiyo inayotawala Dola na sio utawala wa mtu mmoja.

MALENGO TUNAYOTAKA KUYAFIKIA:

Nchi inatawaliwa na sheria na kwamba hakuna aliye juu ya sheria. Watumishi wa umma, vyombo vya ulinzi na usalama, viongozi waliochaguliwa, Majaji na Mahakimu wanaheshimu na kuzingatia utawala wa sheria.

Vyombo vya ulinzi na usalama vinajiepusha na ukamataji holela usiozingatia sheria, kuwaweka watu kizuizini kinyume cha sheria na utesaji.

Kupiga vita aina ya udikteta na utawala wa wachache na hivyo kuwafanya watu waishi kwa uhuru na ustawi.

Sheria zinazoongoza nchi zitatungwa na Bunge na hazitotokana na matakwa ya mtu mmoja. Watu wataishi katika jamii ambapo utaratibu wa kisheria utafuatwa na kuheshimiwa na watu wote.

Kuzuia ulimbikizaji wa madaraka makubwa kwa mtu mmoja ambayo husababisha udikteta na utawala kwa matakwa ya watu wachache.

Mbinu madhubuti za usimamizi ambazo zitadhibiti na kuzuia matumizi mabaya ya madaraka au ofisi katika taasisi mbalimbali za Serikali.

Tanzania itaendelea kushuhudia vitendo vya kihalifu dhidi ya binadamu kama vile mauaji, utekaji, utesaji, ubakaji na aina nyingine za udhalilishaji wa kijinsia ikiwa hatutazuia utawala usiozingatia sheria kupitia mikakati madhubuti ya uangalizi na kuzingatia utawala wa sheria.

Hali ya kutozingatia sheria ni pale ambapo wavunaji wa haki za binadamu hawaadhibiwi, sheria haziwawajibishi wahalifu, madai ya matumizi ya nguvu kupita kiasi hayatiliwi maanani na madai ya haki za kiuchumi, kijamii na kiutamaduni hayawezi kushughulikiwa katika mfumo wa kimahakama. Hali kama hiyo hudumaza ufanisi wa Serikali kutoa huduma za kijamii kwa wananchi.

NAMNA WANANCHI WATAKAVYONUFAIKA:

Sheria itafanya kazi ya kusimamia na kulinda haki za wananchi.

Serikali na mamlaka nyingine zitafanya kazi kwa kufuata utaratibu wa kisheria na hazitakuwa. juu ya sheria.

Watu watanufaika na maendeleo ya kiuchumi, hii ni kwa sababu ya ukweli kwamba sheria za kodi, mchakato wa bajeti, fedha za Mahakama na taasisi nyinge za Serikali zilizoidhinishwa na Bunge au Mamlaka za Serikali za Mitaa zitatumika ipasavyo kutokana na mchakato wake kuwa wa wazi.

Utawala wa Sheria hudhibiti utawala holela usiozingatia sheria na kuongeza weledi na ufanisi wa Serikali katika kutoa huduma za kijamii kwa wananchi. Faida hizi hupunguza pia urasimu miongoni mwa taasisi za Serikali na hivyo kurahisisha upatikanaji wa haki kwa urahisi.

#SeraMbadala
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom