Mshana Jr
Platinum Member
- Aug 19, 2012
- 280,732
- 729,900
Kwenye mada nyingi tumeona uhayawani wa mwanadamu tumeona kwa sehemu kubwa jinsi kiumbe hiki kiitwacho binadamu kilivyo kipumbavu na kisicho na chembe ya uelewa kuhusu yale yatokeayo na ayafanyayo kila siku.
Binadamu anaongozwa na hisia zaidi ya vile avipendavyo kuliko uhalisia na uelewa wa yale yanayotokea kila sekunde kila dakika na kila saa ya pumzi yetu
si mara haba tumeona tumeona picha zinazowakilisha matukio mbalimbali ya kutisha na kusikitisha matukio ya ajali nk. Wengi tumeyaandikia maelezo ya mbwembwe kulingana na hisia zetu na umahiri wetu katika kuonyesha uchungu lawama hasira nk.
Matukio hayo ni wenzetu ambao tayari hatunao tena ni marehemu wameshamaliza safari yao hapa duniani na sasa wako mahali pengine wakipumzika au wakiendelea na safari yao lakini katika hatua nyingine.
Hawa tunawaita wafu, kila mmoja akiwa kafikia umauti wake kwa style yake.
Wengine kwa mateso makubwa wametuachia majonzi na huzuni ambazo zina chukua muda kufutika katika hisia na kumbukumbu zetu, lakini pamoja na hayo yote natuangalie kwa mtazamo mwingine hiki kitu kinachoitwa KIFO ili tuweze kuwa na ufahamu mwingine tofauti na ule tuliozoea kuwa nao huko nyuma kwa njia hii ile huzuni simanzi na majonzi kwa wapendwa wetu vinaweza kupungua na kutufanya tuishi kwa utulivu zaidi.
------------------------------
Si watu haba ambao hawatakubaliana nami kwa kile nitakachoandika hapa wengi watanihukumu kwa namna ya ajabu kabisa siwalaumu kwakuwa ni mazoea ya wengi kuwa wanafiki na waoga kupindukia, na kuwa na ile dhana ya kuwa kinachosemwa na wengi ndio sahihi ndio ukweli ndio uhalisia
Hatutaki kubadilika Hatutaki kujifunza mambo mapya hatutaki kusoma na kuzitafsiri hisia zetu za ndani kabisa kwa muktadha mwingine.
Tunakumbuka kusahau kuwa ni katika hizo hisia zetu za ndani kabisa ndimo kweli yetu inapotoka na kweli hiyo tunapobahatika kuifahamu hatuna budi kuitafsiri kwa wengine bila woga wala kuficha ficha hata kama tutaitwa majina yote mabaya na kuonekana tunakwenda kinyume na kanuni za kutunga za mwanadamu.
****************************
Sehemu ya pili
Kifo kwa tafsiri ya rahisi na iliyozoeleka kwa mwanadamu si neno zuri si neno la kuvutia wala kutajwatajwa hovyo ni neno lililonakshiwa kwa vikolombwezo vyote kwa kutisha na kuogofya sana lakini Kifo ni jambo bora na la bahati nadra kutokea, kifo ni daraja la kuvukia kwenda kwenye hatua nyingine ya maisha ya juu zaidi mepesi zaidi mazuri zaidi! Kifo ni mwendelezo wa uumbaji ni kama tunaposema elimu haina mwisho uumbaji nao hauna mwisho.