Kalamu ya Mwandishi wa Habari ni Hati ya Kifo

Kinkunti El Perdedo

JF-Expert Member
Nov 28, 2020
5,081
12,476
Mwanadamu hajui wala hatambui siri ya kifo, bali ni aliyeumba ulimwengu huu ndiye anayeijua. Lakini baadhi ya machaguo katika maisha hufanya watu kufanya tathmini ya kifo chako mwenyewe au kujua ni aina gani ya kifo utakachokufa. Kwa mfano, mtu mla sigara mara nyingi hufa kwa kansa ya mapafu, au mnywaji pombe aliyepindukia huweza kufariki kwa sababu ya figo kushindwa kufanya kazi kwa ufasaha. Hivyo basi, aina ya maisha na matendo yako huwa yanatoa mwanga wa aina ya kifo utakachokufa, licha ya kuwa mara nyingine inaweza kuwa tofauti kidogo na matarajio binafsi ya mtu au watu kuhusu aina ya kifo.

Unapochagua kuwa mwandishi wa habari, pasi na shaka kalamu ndio hati yako ya kifo. Maana hukumu ya kifo huwa juu ya kile utakachoandika kwa lengo la kuhabarisha umma, maana hii ndiyo dhima kuu ya uandishi. Kalamu hubeba maana mbili kwa mwandishi—uhai na mauti—hivyo chaguo ni lako kuishi au kufa. Ndio maana mwandishi nguli wa habari nchini ndugu Pasco Mayalla aliwahi kusema, “Kama huwezi kuwapiga, basi jiunge nao” (if you can't beat them, join them).

Mhadhiri Michael Dasu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT-Mwanza) alipo kuwa akifundisha namna ya kuandika makala (How to write features), aliwahi kunukuliwa akisema kuwa kufanya uandishi wa habari za kichunguzi (investigative journalism) ili kujua mambo ya ndani juu ya utendajikazi wa serikali ni kutafuta kifo, mateso, na vitisho vya kupotezwa katika ulimwengu. Maana unaweza kufanyiwa matendo ya kinyama kama kutolewa kucha na meno bila ganzi. Huu ni ukweli ambao ndio uhalisia wa maisha ya mwandishi popote duniani.

Nchi zenye machafuko ya kisiasa kutokana na itikadi kali za kidini, mapingano ya kikabila kuwania madaraka, na mapigano ya kuwania mipaka nk. huripotiwa kuwa na idadi kubwa ya mauaji ya waandishi wa habari wakiwa katika majukumu yao ya kila siku. Mfano ni nchini Somalia, ambapo kundi la itikadi kali la Kiislam la Al-Shabaab lenye mfungamano na kundi la Al-Qaeda limekuwa likihusika katika mauaji ya mara kwa mara ya waandishi wa habari.

Kundi hili limewahi kuhusishwa na mauaji ya waandishi kadhaa wakiwemo Hodan Nalayeh, raia wa Canada na mume wake, katika hoteli ya Assey kwenye shambulio la kujitoa mhanga; mwandishi Ahmed Ado Anshu wa kituo cha Redio Shebelle; na pia kituo cha televisheni cha Independent Universal chenye makao yake makuu mjini London, Uingereza, kimewahi kuripoti juu ya kuuawa kwa mwandishi wake bwana Ahmed Furah Ollas katika mji wa Lasand.

Shirika la Waandishi Wasio na Mipaka (Reporters Without Borders) linaripoti kwamba Somalia sio sehemu salama kwa waandishi wa habari.

Nako Mashariki ya Kati (Middle East), kupitia mgogoro wa miongo kadhaa kati ya Israel na Palestina, kumeripotiwa kuwepo kwa mauaji ya waandishi wa habari kutoka kwa vikosi vya ulinzi na usalama vya Israel kupitia jeshi lake IDF. IDF limekuwa kinara katika rekodi ya mauaji ya waandishi wa habari hasa linapofanya operesheni zake za kijeshi.

Mwandishi Shireen Abu Akleh, Mmarekani mwenye asili ya Palestina ambaye alikuwa akihudumu katika kituo cha utangazaji cha Al-Jazeera, aliuawa na IDF. Adam Harvey wa ABC, Issam Abdollah wa Lebanon, na wengine pia wamepoteza maisha. IDF imekuwa ikihusika na mashambulizi kwenye vituo mbalimbali vya matangazo ya runinga kama Press House Magharibi ya Gaza na kituo cha matangazo cha pamoja kati ya Al-Jazeera na Associated Press kwa madai ya kuwa vituo hivyo vinatoa hifadhi kwa wapiganaji wa Hamas. Mamlaka ya Palestina inadai kuwa zaidi ya waandishi wa habari 124 wameuawa katika mgogoro huo.

Mnamo tarehe 2 Oktoba 2018, vyombo vingi vya habari duniani viliripoti kuhusu kifo cha kikatili cha mwandishi wa habari Jamal Khashoggi, kilichotokea katika ubalozi mdogo wa Saudi Arabia nchini Uturuki. Khashoggi alikuwa mkosoaji wa ufalme wa Saudi Arabia kupitia kalamu yake ya uandishi ambayo ilikuwa hati yake ya kifo. Kifo chake kilisikitisha wengi jinsi wauaji walivyoutendea mwili wake kwa kutumia chainsaw, kama mtu anavyogawa nyama akiwa buchani, na kuhifadhi mabaki yake kwenye begi.

Sio nchi zenye machafuko ya kisiasa pekee ambazo huwa na rekodi ya mauaji ya waandishi wa habari; hata nchi tulivu zinazojinasibisha kuwa za kidemokrasia na zinazozingatia uhuru wa maoni kupitia kile kinachoitwa utawala wa haki na sheria ziko katika hatia ya kumwaga damu za waandishi wa habari.

Nchi yetu Tanzania licha ya kujinasibisha kuwa Kisiwa cha Amani (Island of Peace), damu ya waandishi wa habari nayo imemwagika maana kalamu kwa mwandishi ni hati ya kifo na uhai.

Mwaka 2012, mwezi Septemba tarehe 2, vyombo mbalimbali vya habari vya ndani na nje ya Tanzania viliripoti juu ya kifo cha mwandishi wa habari wa kituo cha Channel Ten, Daudi Mwangosi, kilichotokea katika kijiji cha Nyororo, mkoani Iringa. Mwandishi aliyekuwa akipiga picha pindi jeshi la polisi lilipokuwa likifanya mauaji hayo, Joseph Senga, naye hakuachwa salama na alitangulia mbele ya haki. Hakika kalamu ya mwandishi ni hati ya kifo chake mwenyewe mbele ya mamlaka.

Bado tasnia ya habari Tanzania haijapata majibu yaliyo ya uhakika na wazi juu ya kifo cha utata cha mwandishi wa habari za kichunguzi kuhusu sakata la kuuzwa kwa Logindo, bwana Stan Katabalo, na juu ya kupotea kwa mwandishi wa habari za uchunguzi wa Mwananchi Communications Ltd., Azory Gwanda, mwaka 2017.

Ili kunusuru roho zao, baadhi ya waandishi wa habari wamekimbilia nchi za ughaibuni mfano Anbert Ngurumo na Saimon Kabendera, ambapo kazi za kalamu zao zimekuwa sehemu ya mateso ya maisha yao.

Kulingana na utafiti uliofanywa na Twaweza, MISA-TAN, Jamii Forums, na TAMWA, asilimia 50 ya waandishi wa habari hukumbana na vitisho, ukatili, na unyanyasaji wa kijinsia nchini Tanzania.
 
Back
Top Bottom