Kwa wana Kongamano la Wanafunzi
Ukumbi wa DDC
17/11/2007
Utangulizi
Napenda kwanza kabisa kutoa shukrani zangu za dhati kuweza kutuma salamu za mshikamano kwenu wanafunzi wa Tanzania katika kuadhimisha siku hii ya Wanafunzi Duniani. Pamoja nanyi bila ya shaka wapo wanataaluma mbalimbali na wazungumzaji wengine mashuhuri ambao kwa hakika mawazo na mchango wao katika mjadala wa siku hii ni vitu vya kuonewa wivu, kutamaniwa na kwa hakika kufurahiwa. Kwenu ninyi nyote naomba nitume salamu hizi kwa niaba ya ndugu zenu, na watanzania wenzenu ambao wametanganishwa nanyi na muda, na geographia wakiwa wametawanyika sehemu mbalimbali duniani. Tuko pamoja nanyi katika wakati huu wa pekee katika historia ya nchi yetu. Umbali unaotutenganisha ni wa muda tu, na siku moja Inshallah, tutaonana na kushirikiana katika mapambano haya ya kifikra.
Wakati Huu ni wa Pekee
Wakati huu ni wa pekee kwani haijawahi kutokea katika historia ya nchi yetu ambapo mgongano mkubwa wa mawazo na kifikra unafanyika hadharani, kwa uhuru zaidi na kwa u wazi zaidi huku athari zake zikipiga hodi kuanzia vijijini hadi mijini na mlio wake kusikika kuanzia kwenye mashamba ya mikorosho huko Mtwara na vichuguu vya mawe kandokando mwa Ziwa Viktoria. Tuko kwenye kipindi cha mabadiliko makubwa ambapo kama mama mzazi mwenye utungu wa mwanae ndivyo hivyo tunavyotamani kuona nini kitazaliwa kutoka katika uchungu huu! Miezi ya kusubiri mwana imepita, na sasa tunakaa sawa kumkaribisha mtoto katika familia yetu!
Watanzania walipoichagua serikali ya awamu ya nne walifanya hivyo wakiwa wamejawa imani na matumaini kuwa hatimaye kidonda kimepata tiba na Taifa limepata uongozi. Leo hii katika kona mbalimbali za nchi yetu watu wanapita na kutikisa vichwa vyao kwa masikitiko kuwa waliyemdhania ndiye kumbe siye. Leo watu wameanza kukata tamaa na viongozi wao, leo watu wameanza kuangalia nyuma na kusema kumbe ni wale wale. Leo hii wanavyolindana huko madarakani, wakimega na kumegeana, wakingata, huku wengine wakingatana, na wale wanaotafuna wakitafuna kama kwa zamu!
Leo hii kuna wanakijiji wamechomewa nyumba huko Kilosa na Jeshi lao la Magereza kinyume cha sheria; leo hii kuna wanafunzi 400 toka Arusha wanashindwa kuendelea na masomo ya elimu ya juu kwa sababu wenye dhamana ya mikopo wamejiweka kwenye viti vya enzi; na leo hii kuna wadogo zetu pale Azania wameshindwa kuendelea na masomo kwa kugoma sababu ya mazingira machafu yasiyomstahili mwanadamu, na leo hii wameingiza nchi katika mikataba ile mibovu ambayo wote sasa tunaifahamu na kuikariri utadhani aya za vitabu vitakatifu! Matumaini ya wananchi yameanza kuvunjwa na kupondwa na sasa baadhi ya watu wamefikia kuishi kwa ile falsafa ya kibepari kuwa kila mtu na lwake ila Mungu ni wetu sote!
Ndiyo maana basi kufanyika kwa kongamano hili kwa siku kama ya leo na kwa kuangalia mada yake kuu kuwa Vijana: Nguvu ya Mabadiliko basi kuna mambo machache ambayo binafsi naomba niyaseme kama mchango wangu wa mawazo.
Mambo matatu
Kwanza, wasomi wetu katika nafasi zao mbalimbali (iwe vyuoni au walio maofisini) wanajukumu kubwa la kuamsha dhamira za utumishi kwa nchi yetu. Binafsi ninaamini kuwa Taifa letu limeangushwa hadi hivi sasa kwa kiasi kikubwa na wasomi wake hasa miaka hii kumi na tano iliyopita. Miaka ya mwanzoni mwa uhuru na hasa ile ya sabini Taifa letu lilishiriki kwa kiwango kikubwa katika kuchambua dhana mbalimbali za kisiasa na kifalsafa kiasi cha kutoa wasomi mahiri wengi tu ambao mchango wao unatambulikana duniani. Wasomi wengi tunaowasikia leo hii ni matunda ya wakati huo. Wengine mnao hapa!
Leo hata hivyo baadhi ya wasomi wetu ambao walikuwa mahiri walipokuwa nje ya madaraka wamekuwa kama wamepigwa ganzi pale walipopata vyeo vya kisiasa na hasa walipoona bendera zinapepea kwenye magari yao na wanapigiwa saluti kila wanakopita. Sauti za ndiyo mheshimiwa na ndiyo mzee zimewalesha ugimbi wa madaraka! Leo hii tuliowadhania kuwa watakuwa chachu kwenye uongozi wamebakia kuwa kama alama za barabarani zilizofutika! Na wachache ambao wanaujasiri wa kwenda kinyume na mazoea mabovu wanaonekana ni majasiri kati yao! Ni lazima wasomi wetu waamshe dhamira ya utumishi ndani yao wenyewe na ndani ya wale wote wanaopata nafasi ya kusikia maoni yao na kuona matendo yao!
Pili, Ni jukumu la wasomi kuongoza mazoea ya kukataa sera mbovu, mazoea mabovu, na utendaji mbovu bila kuuonea haya au kuufumbia macho. Mwanzoni mwa wiki hii bila ya shaka mtakuwa mmesikia vijana wa Azania waliogoma kuingia madarasani kwa sababu vyoo na mazingira wanayosomea ni machafu. Mliopata kuona picha za video bila ya shaka mlijihisi kinyaa na kushangaa hali imefikiaje hapo. What transpired there its a metaphor of what is happening in certain quarters in our country! Tumezoea uchafu kiasi cha kwamba tunavaa suti na tai kwenda kwenye vyoo vichafu, tunatilia pafyumu hoteli migahawa michafu, na tunaendesha magari ya kisasa kwenye barabara mbovu! Vijana wa Azania wamefanya kitendo ambacho wengi wetu kwenye vyuo vikuu na taasisi nyingine hatuna ujasiri wa kufanya. Wamekataa kuuzoea uchafu!
Hawa vijana wameonesha kiini cha usomi nacho ni uwezo wa kukataa vitu vilivyozoeleka na uwezo wa kuhoji yanayokubalika kama kawaida. Kwa sababu tunapokataa tunajenga hoja ya kwanini majibu au vilivyopo havitoshi! Ni kukataa mazoea kulikosababisha mapinduzi ya Ufaransa, ni kukataa kulikosababisha mapinduzi ya Marekani, ni kukataa kulikosababisha uhuru wa India, ni kukataa kulikosababisha Martin Luther King Jr kuongoza matembezi ya Selma, Alabama. Ni kukataa kulikosababisha Mapinduzi ya Zanzibar na ni kukataa kulikosababisha Azimio la Arusha! Msingi wa kukataa huku ni imani kuwa mahali fulani kuna tunu zilizobora zaidi na mahali fulani kuna mawazo yenye mantiki zaidi! Leo hii wanapofukuza wanafunzi wa vyuo vikuu na wanafunzi wale wanapiga magoti kwa woga wakiyupa wasamehewe huku wanajua kabisa haki na sheria iko upande wao!
Katika hili niwatambue vijana wetu 29 waliokuwa wamekwama Ukraine na ambao serikali yao iliwatelekeza mchana kweupe. Vijana wale walikuwa na uwezo wa kukubali makosa na kuamua kuyamaliza chini chini. Walikuwa na uchaguzi wa kusema walikosea kujaza fomu na yakuwa walijiondokea kivyao vyao. Hadi wanarudishwa nyumbani hakuna hata mmoja wao aliyekubali makosa ya kutungiwa na aliyekuwa tayari kupiga magoti mbele ya watawala na kusema walisema uongo! Vijana wale wamerudishwa nyumbani kwa sababu hakukuwa na jinsi nyingine; lakini wamerudi wakiwa na heshima yao na dhamira zao zikiwa safi! Wakati watu walidhania suala la vijana hawa lilikuwa ni makosa yao leo mambo yale yale yanasikika Arusha, Dodoma, Dar na hata Urusi, China, India na Cuba ambapo wanafunzi wa Kitanzania wanapata matatizo yanayotokana na bodi mbovu isiyowajibika ya mikopo. Naomba niwapongeze vijana wale kwa moyo wao wa mfano na wale wote waliojitokeza kuwasaidia. Historia itawahukumu vizuri siku moja.
Tatu na mwisho, sisi sote tunao wito katika kuleta mabadiliko tunayoyatamania. Tumesema kuwa Vijana: Nguvu ya Mabadiliko. Naamini kabisa kuwa mabadiliko ya kweli katika nchi hii hayatatokea kwanza kwa kubadili Katiba, au kwa kubadili sheria au kwa kuunda tume teule na tume tukufu! Mabadiliko ya kweli hatatokea kwa kubadili mawaziri na kuongeza wajumbe kwenye kamati juu ya kamati. Na anayedhania kuwa mabadiliko ya kweli yatatokea kwa kuibembeleza serikali ajue amekosea sana. Ndugu zangu, mabadiliko ya kweli ni lazima yaanzie kwenye fikra! Hatutaweza kushinda kwenye sanduku la kura, kama tutashindwa kwenye uwanja wa fikra!
Ndiyo maana ninachokiona kinaendelea Tanzania hivi sasa siyo mgogoro wa kisheria, siyo mgogoro wa kikatiba, na siyo mgogoro wa vyama. Naamini kinachoendelea ni mgogoro wa kifikra, ni mapambano ya kifikra. Mwalimu Nyerere katika ile hotuba yake ya Mei Mosi Uwanja wa Sokoine kule Mbeya aliliona hilo. Na alitambua kuwa tusipokaa chini na kubadili mweleko wa fikra zetu tutajikuta tumepelekwa tusikotaka kwenda na tusijue tumefikaje huko. Leo hii watu kama kina Prof. Shivji anapozungumzia Azimio la Arusha kwa mfano kuna watu wanatetemeka kwa sababu wanakumbushwa enzi za Mabepari walia kunyanganywa mirija. Hakuna kitu kinachowatishia wanyonyaji mambo leo kama mawazo ya msingi ya Azimio la Arusha na hapa sizungumzii utaifishwaji wa mali za umma. Leo hii hatuna mwelekeo wa kiitikadi ambao unaeleweka tunaendelea kuburuzwa tu kwa kufuata nguvu za soko! Mwalimu alitabiri kwa usahihi kabisa kuwa mambo waliyokuwa wameanza kuyafanya baada ya Azimio la Zanzibar yatatengeza mamilionea wachache, lakini yatatengeneza masikini wengi.
Hitimisho
Ndugu zangu wasomi! Mnao wito kwa Taifa letu, wito wa kuamsha fikra za wananchi kuukata ufisadi, kukataa kubebana, kukataa rushwa, kukataa viongozi wababe na kukataa sera za kibaguzi! Ni lazima sisi sote tuweze kuzishinda fikra mbovu na hoja za kitoto kwa kupendekeza fikra bora zaidi na hoja zenye nguvu zaidi! Kabla watawala wetu hawajaanguka kwenye sanduku la kura, ni lazima waanguke kwenye fikra za wananchi wao. Ndiyo ni lazima waanguke huko kwanza. Miezi michache iliyopita imeonesha mwanzo wa mabadiliko haya ya kifikra. Basi mtokapo hapa leo hii, cheche ya mwamko mpya wa mapenzi kwa nchi yenu iwashwe, na mwenge wa moto umulikao wa uzalendo uwake mioyoni mwenu ili siyo tu uangaze pale mlipo nyinyi bali uwaangazie hata ndugu zenu ambao hawajapata au hawatopata nafasi ya kutembelea taasisi zenu za elimu ya juu. Kama wanakijiji wa Buzwagi wameweza nanyi mnaweza; kama wanakijiji Dodoma wameweza nanyi mnaweza, kama wadogo zenu wa Azania wameweza nanyi mnaweza, wakati umefika na nyinyi muoneshe siyo tu mnaweza bali mnayo sababu, uwezo, na nia ya kuweza. Vinginevyo na nyinyi mtabakia kuwa irrelevant, na wananchi watasubiri kizazi kijacho cha wasomi; and my friends, that will be a tradegy for our country, please answer this historic call to duty! Nawatakia kongamano jema!
Ndugu yenu,
M. M. M.