" Huwezi kumfanyia jambo jipya msafiri au mtu aliyepitia misukosuko ya kila namna.
Ni sawa na bure kabisa kumlewesha aliyelewa"
Nitazingatia mawazo yenu, kama mlivyojichagulia hapa, ijapokuwa najua mtakosa mambo mengi muhimu na nyeti zaidi niliyopanga kuwafunulia hapa.
Namaanisha kila kitu mtaambulia juu kwa juu tu na hakuna mtakachojifunza zaidi ya makapi ya kawaida tu.
" HEKIMA NA SIRI ZITAKUFA NA WENYE BUSALA"
Tunaendelea. (Ufupi wa habari umezingatiwa.)
Baada ya kuchelewa kwa usafiri asubuhi ya siku ya kwanza pale Mafinga. Kesho yake tulifanikiwa kufika maeneo ya panapoitwa Songwe kwa sasa.
Tuliishia hapa kwa sababu ya mtindo wetu wa kuunga unga safari. Na kuna mengi muhimu yaliyotusibu wakati wa safari ya kipande hiki cha kati ya Mafinga na hapo Songwe.
Miaka hiyo hakukuwa na maendeleo sana Tanzania, maeneo mengi hayakuwa na vitu kama vilivyopo nyakati hizi.
Kuna mtu ameuliza swali kwenye komenti, akitaka kujua kiasi cha pesa tulizokuwa nazo na je? tuliifadhi vipi?
Nasikitika sita andika hapa kila kitu, ili tu wale wenye mashauri tofauti tusiwakwaze.
Kule Botswana, watu ni wakalimu sana. Watu wanaheshimu mawazo na hisia za wengine mara elfu zaidi ya ujuavyo.
Ni sawa na kutomshangaa Mtanzania mlevi aliyelowea Urusi.
Tabia zetu zinabadilishwa na mazingira tuliyopo.
Tulifanikiwa kufika border ya Nakonde. Haikuwa nzuri na salama kama sasa.
Tunduma ilitupasa tukae sana, maana kwanza hatukuwa na nyaraka zozote, pili hatukuwa na moja wala mbili kuhusu namna ya kuwasiliana kwa ufasaha kwa lugha yoyote ng'eni zaidi ya kiswahili, tatu pesa yetu haikuwa nyingi na kuibadili haikuwa kazi rahisi.
Nne tulipaswa kuwa na connection na wazamiaji wengine zaidi ili iwe rahisi kwetu kutimiza azma yetu.
Mipango si ukuta, mwenzetu mmoja baada ya kunogewa na mji na watoto wa karii pale border, aliamua kabisa kughaili safari na kutekwa na mtoto wa kinyakyusa.
Almanusura tukwame wote pale Nakonde one stop border. Haikuwa sehemu salama kabisa kama wewe sio mjanja mjanja.