Sabaya, Kakoko ngoma nzito

Suley2019

JF-Expert Member
Oct 7, 2019
1,813
4,545
Dar/Tabora. Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imeeleza namna ilivyofichua sakata la aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya, huku wananchi kadhaa wakijitokeza kuelezea malalamiko yao dhidi yake kwa Takukuru.

Wakati hayo yakijiri, Takukuru imewasilisha majalada ya baadhi ya vigogo wa Mamlaka ya Bandari nchini (TPA) katika Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (DPP) kwa ajili ya hatua zaidi.

Suala la Ole Sabaya liliibuka juzi mkoani Tabora wakati wa mafunzo yaliyotolewa na THBUB kwa madiwani wa manispaa hiyo, ambapo Mkurugenzi msaidizi wa utawala bora katika tume hiyo, Mbwana Mussa Mbwana aliposema walifanyia kazi malalamiko ya wananchi na kuyafanyia uchunguzi.

Sabaya (34) na wenzake watano wanakabiliwa na mashtaka sita yakiwamo mawili ya ujambazi wa kutumia silaha na kesi yao iliyotajwa Julai 2, iliahirishwa tena hadi Julai 16, 2021.

Ilipotajwa mara ya mwisho, wakili wa Serikali, Tarsila Gervas aliomba kupangwa siku nyingine, ili mashahidi waanze kutoa ushahidi wao na hakimu mkazi mkuu, Salome Mshasha alikubali maombi hayo na kuahirisha kesi hiyo hadi Julai 16.

Katika mkutano huo, Mbwana alisema juhudi za tume hiyo ziliwezesha kiongozi mmoja mkoani Kilimanjaro kukamatwa baada ya kutokea malalamiko ya wananchi kuhusu mwenendo wake.

Hata hivyo, hakutaja jina la kiongozi huyo katika mkutano huo wa madiwani, lakini alipoombwa ufafanuzi na Mwananchi, aliamua kufunguka na kusema:

“Ni kweli kiongozi huyo ni Lengai Ole Sabaya. Baada ya kuona kwenye mitandao ya jamii, tulifanya uchunguzi na mapendekezo tuliyapeleka kwenye mamlaka yetu ya uteuzi.”

Awali, Mbwana aliwaeleza madiwani kuwa Tume haifanyi kazi kama asasi za kiraia alizosema zinapenda kutangaza mambo wanayofanya katika kutekeleza majukumu yao.

“Sisi tunafanya mambo mengi lakini mengine hatujitangazi kama asasi zisizo za kiserikali zinazopenda mambo yake yajulikane,” alisema.

Alibainisha kuwa wanatekeleza majukumu yao huku pia wakifuatilia vyombo vya habari na kufanyia kazi taarifa za vyombo hivyo zinazohusiana na uvunjifu wa haki za binadamu na utawala bora.

Malalamiko zaidi dhidi ya Sabaya
Kwa upande mwingine, Takukuru imesema inaendelea na uchunguzi wa malalamiko ya baadhi ya wananchi waliojitokeza kulalamika dhidi ya Ole Sabaya ambaye yuko mahabusu kwa tuhuma mbalimbali ikiwamo ya unyang’anyi kwa kutumia silaha.

Akizungumza kwa simu juzi, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Salum Hamduni alisema wanaendelea na uchunguzi wa tuhuma za wananchi kadhaa waliojitokeza na kuelekeza tuhuma zao kwa Sabaya ikiwa ni mwendelezo katika kesi inayomkabili.

Miongoni mwa wananchi waliojitokeza ni mfanyabiashara maarufu mjini Moshi, Elioth Lyimo ambaye alidai kuwa Sh25 milioni zake zilichukuliwa na Sabaya isivyo halali.

“Kuna chunguzi zinaendelea kwa kuwa kuna wananchi walijitokeza kulalamika, tumepokea malalamiko yao na tunayafanyia kazi,” alisema Hamduni ambaye alianza kushughulikia suala hilo muda mfupi baada ya kuteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Mei 15.

Takukuru na uchunguzi TPA
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi huyo wa Takukuru alisema taasisi yake imekamilisha uchunguzi wa baadhi ya vigogo wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), na kwamba baadhi ya majalada yameshafikishwa katika Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.

Tuhuma za ubadhirifu katika mamlaka ya bandari zilianza Desemba 2020, baada ya Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa kuunda kamati ya uchunguzi na baadaye baadhi ya watendaji wa TPA kusimamishwa kazi kutokana na kutuhumiwa kuwa walihusika katika ubadhirifu huo.

Hata hivyo, Machi 28 wakati akipokea ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Takukuru, Rais Samia alisema ripoti ya CAG inaonyesha ubadhirifu mkubwa, lakini waliochukuliwa hatua ni watendaji wa chini pekee.

Baadaye, Rais Samia alimsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari, Mhandisi Deusdedit Kakoko ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu wa fedha kiasi cha takribani Sh3.6 bilioni ambazo zilitumiwa na mamlaka hiyo.

Akizungumzia uchunguzi huo, Hamduni alisema wanaendelea na uchunguzi, huku baadhi ya maeneo ya uchunguzi yakikamilika na majalada kupelekwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.

“Bado tuko katika hatua za uchunguzi ukiondoa yale majalada machache ambayo tayari yameshawasilishwa Ofisi ya Taifa ya Mashitaka, na kuna majalada mengine siyo vizuri sana kuongelea, kwa sababu kuna watu wengine walishafikishwa mahakamani kwa upande wa Kigoma na Mwanza,” alisema Hamduni.

Uchunguzi huo unawahusu waliokuwa watendaji wa TPA katika badari zake za Kigoma na Mwanza pamoja na makao makuu Dar es Salaam. Tayari Kakoko aliondolewa TPA kabla ya kukamatwa Machi 30 na kuhojiwa na Takukuru dhidi ya tuhuma zinazomkabili.

Ripoti ya CAG
Taarifa ya CAG ya ukaguzi maalumu katika Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kwa miezi mitatu kuanzia Januari hadi Machi, ilibainisha kwamba baadhi ya malipo yaliyokuwa yanatoka hazina kwenda taasisi mbalimbali za Serikali yalibainika kuwa na upungufu.

Upungufu uliobainishwa katika taarifa hiyo iliyowasilishwa kwa Rais Samia, Julai Mosi, ni pamoja na baadhi ya taasisi kama vile Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) na TPA kufanya malipo mara mbili kwa kazi moja au kuchelewa kutumia fedha zilizoidhinishwa kwa ajili ya malipo ya kazi husika.

“Vilevile yamejitokeza mapungufu ambapo baadhi ya makandarasi waliotoa huduma kucheleweshewa malipo yao, hali inayosababisha madeni ya makandarasi hao kuwa makubwa kutokana na riba ambayo ni mzigo kwa Serikali,” ilieleza sehemu ya taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu.

Mbali na upungufu huo taarifa ya Ikulu ilieleza kuwa kulikuwa na upungufu mwingine wa kuwapo kwa miradi ambayo haikupangwa hivyo kusababisha malipo kufanyika nje ya bajeti ya Serikali.

Credit: Mwananchi
 
Uzuri ni kua kesi ni serikali na watumishi wake.

Sasa Ngoja tuone kati ya serikali na watumishi wake ni nani mwenye nguvu mahakamani!

Mawakili wake ndio hao.

Sidhani kama kuna akina kibatala huko
 
Kwahiyo takukuru wameacha shughuli nyingine wameamua kudeal na sabaya na kakoko tu.

Sawa tumewaelewa.
 
Kakoko ni escape goat km ilivyokua kwa Bashiru, watu wanaagiza uchunguzi maalumu mwisho wa siku hawakuti kitu matokeo yake wanaizima kimya kimya.
 
“Vilevile yamejitokeza mapungufu ambapo baadhi ya makandarasi waliotoa huduma kucheleweshewa malipo yao, hali inayosababisha madeni ya makandarasi hao kuwa makubwa kutokana na riba ambayo ni mzigo kwa Serikali,” ilieleza sehemu ya taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu.
Kwanini watumishi wa umma hawalipwi riba kutokana na serikali kuchelewa kuwalipa haki zao?
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom