Sababu tatu za kisheria za kumnyima urithi mrithi halali

Bashir Yakub

Member
May 27, 2013
84
1,562
SABABU 3 ZA KISHERIA ZA KUMNYIMA URITHI MRITHI HALALI.

Na Bashir Yakub.
+255 784 482 959.


Warithi halali ni pamoja na watoto wa marehemu na wake/mke wake halali. Kanuni ya 31 Sheria ya Wosia(1963),Tangazo la Serikali Namba 436/1963 inazitaja sababu 3 ambazo mtoa wosia anaweza kuzitumia kumnyima mrithi halali haki ya urithi kama ifuatavyo ;-

MOSI, ikiwa mrithi amezini na mke wa mwenye kutoa wosia. Mathalan, mtoto wa kiume amezini na mke wa baba yake.

PILI, ikiwa mrithi amejaribu kumuua au amemshambulia au kumdhuru mtoa wosia au amefanya hivyo kwa mke wa mtoa wosia.

TATU, ikiwa mrithi bila sababu za msingi hakumtunza mtoa wosia katika shida ya njaa au ugonjwa.

Ipo sababu nyingine ya kuwa mrithi ameharibu mali ya mtoa wosia, lakini sheria inasema sio sababu ya kumnyima bali apewe halafu kile alichoharibu kikatwe kwenye mgao wake.

Basi, nje ya hizo sababu huwezi kumnyima mrithi halali urithi. Haijalishi mali ni zako, watoto ni wako na kila kitu ni chako.

Na hii ni kwasababu WOSIA ni zao la sheria na hivyo kuandaliwa kwake, kuhifadhiwa kwake, na kutekelezwa kwake ni lazima kufuate sheria. Wosia sio suala la matakwa ya mtu 100% kama wengi wanavyojua, bali matakwa ya sheria kwa karibia 100%.

HATUA 2 ZA KUMNYIMA URITHI MRITHI HALALI.

Ikiwa ni halali kwa vigezo hivyo hapo juu kumnyima mrithi halali urithi basi mtoa wosia kabla hajafanya hivyo ni lazima atekeleze haya mawili ;-

KWANZA, awe amempa nafasi ya kujitetea mrithi anayelenga kumnyima. Hata hivyo, hili si lazima kwa mujibu wa maamuzi katika kesi ya PAULO FERDINAND vs F. BIGUTU(1968) HCD Na. 29. Anaweza kumpa nafasi ya kujitetea kabla hajafa au asimpe.

PILI,ikiwa ataamua kumnyima/kuwanyima ni LAZIMA wosia uwe umeeleza sababu za kwanini mrithi/warithi wamenyimwa. Hii ni lazima kwa mujibu wa kanuni ya 34-39 ya Sheria ya Wosia(1963),Tangazo la Serikali Namba 436/1963.

Ni lazima mtoa wosia/marehemu awe ameeleza katika wosia wake sababu za kwanini fulani na fulani ameamua kuwanyima.

Nini matokeo ikiwa mtu/watu wamenyimwa urithi katika wosia na sababu hazikuelezwa.

Kanuni ya 38 ya Sheria ya Wosia(1963),Tangazo la Serikali Namba 436/1963 inatujibia . Inasema kuwa ikiwa mrithi halali amenyimwa urithi katika wosia, na wosia huo haukueleza sababu ya kumyima au umeeleza sababu lakini zisizokuwa za msingi, kwa maana si zile zinazotajwa na sheria(tulizoona hapo juu), basi wosia huo UNAVUNJWA.

Nini matokeo ya kuvunjwa kwa wosia.


Kanuni hiyohiyo inasema kwamba wosia unapovunjwa basi mali zote zinaanza kugawiwa upya kama vile ambavyo marehemu angekuwa amefariki bila kuacha wosia.

Ni upi utaratibu wa kugawa mali upya kama marehemu hakuacha wosia.

Kama marehemu alikuwa mkristo Sheria ya Urithi ya India ya 1865 ( Indian Succession Act 1865) itatumika kugawa mali zake. Ambapo kwa mujibu wa kifungu cha 27 cha sheria hiyo mgao utakuwa hivi ;-

MOSI,kama mume amefariki na akaacha mjane na watoto basi moja ya tatu ( 1/3) ya mali zote za marehemu zilizo kwenye mirathi anatakiwa apewe mke wake(mjane). Mbili ya tatu( 2/3) ya mali hizo zote itaenda kwa watoto wake wote.

PILI, kama hakuna watoto walioachwa na marehemu katika familia husika lakini kuna mjane,mali ya marehemu hugawanywa katika mtindo ambao ndugu hupewa nusu (1/2), na mjane hupewa nusu ya mirathi ya marehemu(1/2). Hii ni sawa kwa sawa.
N.k., n.k. nk.

Kama marehemu alikuwa mwislamu basi sheria ya kiislam(Quran na Hadith) vitatumika kugawa mali zake.

Kadhalika, kama marehemu hakuwa mwislam wala mkristo bali mtu wa mila basi sheria ya kimila ya THE LOCAL CUSTOMARY LAW (DECLARATION) ORDER 1963 itatumika kugawa mali zake sambamba na taratibu za mila za kabila/koo yake.

Nani ana mamlaka ya kugawa mali upya.

Kanuni ya 39 ya Sheria ya Wosia(1963) inatujibia kuwa wana ukoo wanaweza kufanya hiyo kazi kama kuna maelewano, au mahakama yenye mamlaka.

Nisisitize kuwa WOSIA au MIRATHI ambayo haikufuata au haikurandana na sheria inavyotaka ni BATILI.

Na zaidi, ni kweli mali ni zako, watoto ni wako, na kila kitu ni chako ila zingatia kuwa WOSIA na taratibu za MIRATHI sio zako, ni za sheria na lazima utii, au ujiandae WOSIA wako kutofuatwa baada ya kifo chako.

MWISHO lakini si kwa umuhimu, makala haya hayamlengi yeyote au tukio lolote lililotokea katika jamii yetu hapo nyuma, hivi karibuni, au hapo baadae.
 
Mbona sheria inazungumzia tuu kama marehemu ni mume tuu?
Vipi kama ni mke na ana mume lakini ana watoto wa waume tofauti? Hapo sheria inasemaje? Kwani mke Mali zake pekee zina hesabiwaje?
Kama hao watoto walioletwa na mwanamke mwingine hawaja kua adoptes na huyo baba yao mlezi hao watoto hawapati kitu, bali wataenda kurithi vitu vya baba yao au mali mahususi za huyo mama yao...endapo mama anafariki na alikua na mali za kwake binafsi utaratibu wa kawaida utafatwa kama ulioelezwa hapo juu ila.mara nyingi mama akifariki kama alikua mfanyakazi i.e. mafao yake mali zake zitagawiwa ila kama alikua mama wa nyumbani itakua kama vile hakijatokea kitu hadi baba mtu atakapo fariki
 
There is NO SUCH THING AS MRITHI HALALI

Watu wangekuwa hawana haja ya kuandika wosia kama sheria zinataja nani ni MRITHI HALALI

Weka nukuu ya sheria inayosema MRITHI HALALI WA MAREHEMU NI FULANI NA FULANI NA SHANGAZI NA MJUKUU NA KAKA....
 
Asante,ila sheria hii ni kandamizi kwa marehemu na mwenye mali.Mwenye mali angeachwa amue yeye nani wa kumpa.Na sioni sababu kwa nini watoto wakubwa wapewe urithi, kwa kuwa hawa wanaweza kujitegemea. Urithi wangepewa watoto ambao bado hawajaweza kujitegemea.

Waliotunga sheria hizi frankly wana matatizo ya kufikiri.Urithi anapewa ndugu, amechangia nini katika kutafuta hiyo mali.To me logically mali yangu ni yangu na mke wangu,huyu ndiye tumesumbuka naye kuipata, wengine inawahusu nini,infact hata watoto kwa nini wapewe urithi hasa kama ni wakubwa. Watafute yao kama mimi nilivyotafuta. Logically angeachiwa mwenye mali aamue nani ampe urithi.Kutungia sheria mali ya mtu is not fair.Hii ni kuleta migongano kati ya mjane, ndugu na watoto.
 
Mbona sheria inazungumzia tuu kama marehemu ni mume tuu?
Vipi kama ni mke na ana mume lakini ana watoto wa waume tofauti? Hapo sheria inasemaje? Kwani mke Mali zake pekee zina hesabiwaje?

Tunapodai Gender equity and Gender equality tunamaanisha vitu Kama hivi.
 
Ina maana hawa Wanasheria wa Mzee Machache walikuwa hawajui hili? Wamemtia Aibu kwa kujua halafu hawakumwambia.
 
Asante,ila sheria hii ni kandamizi kwa marehemu na mwenye mali.Mwenye mali angeachwa amue yeye nani wa kumpa.Na sioni sababu kwa nini watoto wakubwa wapewe urithi,kwa
kuw hawa wanaweza kujitegemea.Urithi wangepewa watoto ambao bado hawajaweza kujitegemea.
Waliotunga sheria hizi frankly wana matatizo ya kufikiri.Urithi anapewa ndugu,amechangia nini katika kutafuta hiyo mali.To me logically mali yangu ni yangu na mke wangu,huyu ndiye tumesumbuka naye kuipata,wengine inawahusu nini,infact hata watoto kwa nini wapewe urithi hasa kama ni wakubwa.Watafute yao kama mimi nilivyotafuta.Logically angeachiwa mwenye mali aamue nani ampe urithi.Kutungia sheria mali ya mtu is not fair.Hii ni kuleta migongano kati ya mjane,ndugu na watoto.
Unaweza kusema wamechangia Nini ila ukiangalia unaweza kukuta wana mchango mkubwa sana.

Marehemu baba yetu hakumjumuisha mtoto mmoja wa Kaka yake kwenye mgao. Ila yule Kaka alikua na mchango mkubwa sana na mbaya zaidi hakua akilipwa kwa mkataba Wala makubaliano yoyote. NI mzee alikua anampa chochote. Kikao Cha mirathi yule kijana aliomba asaidiwe mbao tu za kupaulia nyumba yake. Watu walimshangaa sana. Mimi na kakaangu anaenifatia hatukuongea ila baadae tukateta tukaona anastahili kupata kitu kwa sababu alimtumikia Mzee tangu kijana mdogo kabisa.

Kabla hujasema walichangia Nini au kusema wengine ni wakubwa angalieni vizuri.
 
Back
Top Bottom