MFANYABIASHARA, James Rugemalira ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ameandika barua kwenda kwa Kamishna Generali wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), akielezea ni jinsi gani benki ya Standard Charter Hong kong walivyokuwa wakikwepa kodi na ushuru wa forodha.
Rugemalira aliyaeleza hayo jana Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi wakati kesi ya uhujumu uchumi namba 27 ya mwaka 2017 inayomkabili.
Mbali na Rugemalira, wenzake ni Harbinder Sethi ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Kufua Umeme (IPTL) na aliyekuwa mwanasheria wa kampuni hiyo, Joseph Makandege.
Rugemalira alieleza hayo baada ya Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Maghela Ndimbo kueleza kesi ilipangwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake bado haujakamilika.
Rugemalira alidai kuwa Januari 24, 2020 aliongea na mwakilishi wa Takukuru alipotembelea gerezani na akamkabidhi nakala ya barua hiyo aliyoandika kwenda kwa Kamishna wa TRA lakini hadi sasa hajapata jibu lolote. "Naomba kesi ikitajwa upande wa Mashitaka walete jibu kwa sababu wanaostahili kushitakiwa katika kesi hii ni benki hiyo na ninashangaa kuona wengine wanaongezwa katika kesi kwa madai upelelezi haujakamilika," alidai Rugemalira.
Pia alidai upelelezi wa kesi hiyo hautakamilika na ili ukamilike wafuatilie hiyo barua aliyowapelekea.
Baada ya Rugemalira kueleza hayo,Hakimu Shaidi aliiahirisha kesi hiyo mpaka Februari 13, 2020 kwa ajili ya kutajwa ili kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika ama la.
Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 27/2017, Makandege anakabiliwa na mashtaka matano likiwemo la kuisababishia serikali hasara ya dola za Marekani 980,000 pia yapo ya utakatishaji wa Fedha.
Mshtakiwa huyo alisomewa mashtaka hayo Desemba 20,2019,baada ya kuunganishwa na washtakiwa Seth na Rugemalira katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi.
Miongoni mwa mashtaka hayo ,Makandege anadaiwa kuwa, kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19, 2014 katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam, Kenya, Afrika Kusini na India, akiwa na wenzake walikula njama ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Pia anadaiwa kuongoza genge la uhalifu, katika nchi hizo, akiwa si mtumishi wa Serikali akishiriki
Chanzo: Jamhuri