Miaka ya 1980, Pablo Escobar, bepari mzito aliyefanya biashara ya madawa ya kulevya na mpenda anasa kutoka Medellín, Colombia akiamini mambo ya kawaida hayamtoshi, akaamua kunogesha makazi yake binafsi.
Bustani ya kijani na bwawa la kuogelea? Mbwa wakali? Twiga? Hayo yalikuwa ya matajiri wa kawaida. Yeye alikuwa wa kipekee zaidi. Akasafirisha viboko wanne kutoka Afrika, pamoja na wanyama wengine wa porini, na kuwaleta kwenye bustani aliyojijengea ya wanyama iliyoitwa Hacienda Nápoles.
Kwa macho ya wengi, lilionekana jambo dogo na la kupita tu.
Wengine waliliona kama ishara moja tu kati ya nyingi walizozizoea ziliyoonyesha maguvu na utajiri aliyokuwa nayo bwana huyu. Kuna walioshangazwa, lakini wengi zaidi walicheka na kupuuza jambo hili, likawa soga za mjini za kipindi hiko.
Escobar aliuawa mwaka 1993. Serikali ya Colombia ikataifisha mali zake. Haukuwekwa mpango wa usimamizi wa Hacienda Nápoles, wanyama waliokuwepo wakakosa wa kuwatunza. Hii ilipelekea serikali kufanya maamuzi ya kuwahamisha wanyama hao.
Hata hivyo, viboko hawakuhamishwa. Sababu mbalimbali zilitolewa, zikiwa ni pamoja na ukubwa wa viboko uliofanya zoezi la uhamishwaji kuwa gumu kilojistiki na kigharama (wakati huo, Colombia ilikuwa inakabiliana na vurugu na vita dhidi ya masalia ya magenge ya madawa ya kulevya kwa hiyo uhamishwaji wa viboko haukupewa kipaumbele), na hatari kwa binadamu watakaofanya zoezi la kuwasafirisha kutokana na hasira na ukubwa wa wanyama hao.
Haishangazi kwamba kuna baadhi waliotoa hoja kwamba “Ah, ni viboko wachache tu, hawawezi kusababisha madhara makubwa.” Na pia kuna walioona uwepo wa viboko hao Medellín utaendelea kuwa urithi wa kipekee na kumbukizi la Escobar na mbwembwe za "don" huyu, na hata kivutio cha utalii.
Hivyo basi, viboko wakaachwa tu wakiogelea kwenye ziwa dogo. Hakuna baya litakalotokea.
Lakini viboko walikuwa na mipango yao, wakazaliana. Wakati wenzao walioachwa Afrika wakipambana na maadui wa asili, mazingira ya Colombia yakawapenda mno. Kwa chakula kingi na mito yenye rutuba, polepole wakaanza kuongezeka. Miaka ikapita wakawa kumi, kumi wakawa mia. Leo idadi yao ni zaidi ya 150.
Si mzaha tena.
Wamekuwa hatarishi kwa maisha ya binadamu. Viboko hao wameshambulia wakulima mashambani na wavuvi mitoni na maziwani. Kiboko mmoja huweza kuachia zaidi ya kilo 20 za kinyesi kila siku. Kwa mamia yao, wameathiri kemia ya maji kwenye mito na kujaza virutubishi visivyo vya kawaida. Samaki na viumbe vingine wa majini wanakufa, mifumo ya ikolojia imebadilika.
Riziki za wavuvi zimepokwa. Afya ya jamii kwa binadamu imeathiriwa. Mbinu za kuwadhibiti kama "uzazi wa mpango" ni gharama kubwa zaidi na ngumu kutekeleza, uhamishwaji ni hatari kwa binadamu na ghali, na kuwaua si jambo linalomezeka kirahisi katika dunia ya leo inayoheshimu haki za wanyama. Mijadala tu ya namna sahihi ya kukabiliana na tatizo inaugharimu umma wa wacolombia.
Mzaha wa jana umezaa mzigo wa kitaifa wa leo na kesho. Nikimnukuu mwendawazimu mmoja, "hakuna cha kuchekesha hata ucheshi ungetakiwa"