Riwaya: Tamanio la binti Mkwawa

Aug 4, 2017
49
34
Natumaini wadau wa riwaya hamjambo kabisa popote mlipo,

Leo ninawaletea riwaya nzuri kwa ajili yenu, jisomee na kuburudika,

kwa maoni na ushauri/lolote kuhusu kazi zangu za uandishi wa vitabu vya mashairi na riwaya tafadhali njoo PM.


RIWAYA: TAMANIO LA BINTI MKWAWA.

MWANDISHI: Mniko The Poet (Hili ni jina la kisanii siyo jina halisi)

SEHEMU YA KWANZA.

Mzee Mkwawa alikuwa mtu wa watu, huenda ndiyo maana watu wa mji ule wa Matamanio walimfurahia jinsi alivyoishi na jamii iliyomzunguka, pamoja na hayo yote lakini pia wanajamii walimtunuku ubalozi wa nyumba kumi kumi kwa muda mrefu hadi alipokataa yeye mwenyewe kutokana na umri wake wa uzee ambao ungeathiri kazi zake za kiutendaji kwa wananchi wake.

Mzee Mkwawa alifanikiwa kuoa akiwa na umri wa miaka 20 wakati huo mkewe akiwa na umri wa miaka 18 lakini mzee mkwawa alifanikiwa kuishi na huyo mke mmoja tu katika maisha yake yote japokuwa kupata mtoto haikuwa jambo rahisi kwake na mkewe, walipita hospitali mbalimbali kupima ili kujua tatizo lililokuwa likiwasambua lakini madaktari waliwapa majibu yaliyoonyesha kuwa hawakuwa na tatizo lolote katika via vyao vya uzazi, hatahivyo walijiuliza maswali mengi pasipo majibu kuntu kuhusu majibu yale ya vipimo yaliyotolewa na madaktari wa tiba ya uzazi.

Siku moja asubuhi na mapema mke wa mzee Mkwawa aliamka ili kuzungumza na mzee Mkwawa kuhusu changamoto yao ya muda mrefu ya kukosa mtoto, mke wa mzee Mkwawa alifikiri pengine angepata suluhisho zuri la kumsaidia kumpata motto.

Hatahivyo mzee Mkwawa na mkewe waliendelea kuzungumza ila alizungumza kwa kumtia moyo mke wake na kumuonyesha kuwa siku moja angepata mtoto kwa kumtumainia Mola maana yeye huwapatia mema wale wamuombao mema. Katika harakati zao za kutafuta mtoto walipitia machungu na maumivu mengi sana maana hata ukoo wa Mzee Mkwawa uliamua kumtenga kwa kutokuhusiana naye kwasababu alikataa ushauri wao wa kufanya mazindiko ya asili ambayo wao kama ukoo waliamini yangempatia mtoto.

Hatahivyo ukoo uliendelea kufikiri kuwa Mzee Mkwawa alikosa mtoto kwasababu aliwanyima miungu wao chakula cha damu ya wanyama na mazindiko ambayo yangefanyika kwa kumchinja punda mweusi asiye na kilema chochote katika mwili wake.

Ukoo wa mzee Mkwawa ulimuabudu Punda na kumuamini kama mungu na mkombozi wao lakini kadri ya siku zilivyokwenda vijana wa ule ukoo walianza kukataa ibada hizo za mazindiko kwa kuziita kuwa ni ibada za kishamba na ujima, zisizo na maana katika karne ya ishirini na moja.

Mzee Mkwawa na mke wake walihangaika kwa muda wa miaka 20 ndipo wakafanikiwa kumpata mwanao wa pekee aliyeitwa Binti mkwawa. Mtoto ambaye alizaliwa kwa juhudi nyingi za daktari hodari wa masuala ya uzazi, daktari aliyetoa taarifa ya kitabibu kuhusu kuzaliwa kwa binti mkwawa, daktari alisema katika taarifa yake kuwa mke wa mzee mkwawa alikuwa akishindwa kupata mimba kutokana na tatizo la kupatwa na hedhi mfululizo bila utaratibu wa kawaida wa mara moja kwa mwezi.

Daktari alisema baada ya kugundua tatizo hilo kupitia mahojiano ya kina kati yake na mke wa mzee mkwawa aliamua kumsaidia matibabu ya kina hata alipopona na kuweza kubeba mimba ya binti mkwawa. Wazazi wa binti mkwawa walimpongeza yule daktari kwa moyo wake mwema na weledi aliouonyesha katika kumtibu mke wa mzee mkwawa hadi akapona tatizo lake.

MJI WA MATAMANIO.

Karibu sana na ulipo mji wa Matamanio ndipo alipozaliwa binti Mkwawa, binti pekee katika familia ya mzee Mkwawa, mzee ambaye alibarikiwa kuishi siku nyingi katika uso wa dunia hii yenye maswahibu mengi pia na raha kadhaa, huenda aliishi siku nyingi kwasababu ya busara zake au kwasababu ya hekima zake ama ni kwasababu ya majaliwa ya Mola lakini hakuna ajuaye kuhusu hili.

Ninachojua ni kuwa binti mkwawa alipozaliwa alituzwa zawadi nyingi za kila aina ambazo hata hakuzitambua maana yake kwa kuwa alikuwa bado angali mtoto mchanga asiye na ufahamu wowote.

Mzee mkwawa na mke wake walidhamiria kumlea mwanao kwa maadili mema pamoja na kumpatia mahitaji ya muhimu ili kumfanikisha katika maisha yake ya baadaye. Walimuandikisha shule ya awali mara tu alipopata umri wa miaka mitano(5) katika shule ya awali iliyokuwa ikiitwa Shule ya msingi Matamanio, shule ambayo ilikuwa na kauli mbiu iliyosema ‘tamani kuelimika’. Binti Mkwawa aliandikishwa katika ile shule kisha akapewa namba ya usajili SM01.

Katika masomo yake ya elimu ya awali binti mkwawa alikuwa haelewi chochote alichokuwa akifundishwa na walimu wake lakini walimu hawakukasirishwa na hali ile kwani waliamini kuwa binti mkwawa angeendelea kujifunza taratibu na kuelewa vyema kadri ambavyo angekuwa anasogea kutoka darasa moja hadi darasa lingine. Walimu waliwatungia mtihani watoto wa ile shule ili kuhitimu elimu ya awali, mtihani ambao watoto wote walifaulu kwa alama kubwa sana isipokuwa binti mkwawa ambaye alifaulu kwa alama za kawaida sana.

Mzee Mkwawa na mke wake walitembelewa na mmojawapo wa walimu kutoka kwenye shule ya Msingi Matamanio, mwalimu ambaye alibeba ujumbe wa matumaini kwa wazazi wa binti mkwawa, mwalimu aliwapongeza wazazi wa binti mkwawa kwa juhudi zao za kumlea vizuri kiasi cha kupelekea kuwa na mvuto wa tabia njema zaidi kuliko watoto wote walioandikishwa katika shule ile ya msingi. Tabia njema ya binti mkwawa ilipelekea uongozi wa shule kumtunuku zawadi ya kitabu kizuri cha hadithi kilichokuwa kimeandikwa kwa juu ‘TAMANI KUWA NA NIDHAMU’.

Mzee Mkwawa na mke wake walishukuru kwa taarifa nzuri kuhusu mtoto wao ambayo iliwafikia kupitia mwalimu aliyewatembelea nyumbani kwao. Walimpongeza pia mwalimu kwa kuwatembelea kisha wakampatia mbegu za alizeti kama zawadi ambayo angeenda kukamua na kupata mafuta halisi ya kula kwa ajili ya kupikia.

ELIMU YA MSINGI YA BINTI MKWAWA.

Baada ya kumaliza elimu ya awali Binti Mkwawa alianza darasa la kwanza kwa juhudi kubwa katika masomo kwa kuonyesha nidhamu ya hali ya juu maana wazazi wake walimsisitiza kujisomea kwa bidii pamoja na kuwa na nidhamu kwa watu wote.

Alifanya kile walichomshauri wazazi wake, aliendelea kukua kwa kimo na akili pia hata alipofika darasa la nne binti mkwawa alitamani kujifunza stadi za maisha kama vile kulima bustani, kuwa mchoraji, kutunga nyimbo na ngonjera, kujifunza kushona nguo na kudarizi na kulima zao la alizeti ambalo baba yake, mzee mkwawa, alikuwa akililima kwa mafanikio makubwa tangu ujana wake.

Mzee Mkwawa alifurahishwa sana na matamanio ya binti yake kuhusu kujifunza stadi za maisha ambazo zingemsaidia baadae kujitegemea zaidi kuliko kusumbuka kutafuta ajira bila mafanikio. Mzee Mkwawa alimpeleka binti mkwawa na kumuandikisha kwenye shule ya stadi za maisha iliyokuwa katika mji wa Matamanio kwa ajili ya kusoma masomo ya stadi za maisha kila siku jioni baada ya kutoka katika masomo yake ya kitaaluma.

Binti Mkwawa alienedelea na masomo yake hata alipomaliza elimu yake ya msingi kisha akajiunga na Shule ya Sekondari Sogea baada ya kupata ufaulu wa alama za juu sana kwenye masomo yake yote. Pamoja na kufaulu kujiunga na masomo ya sekondari lakini binti Mkwawa aliendelea na elimu ya stadi za maisha, elimu iliyompatia ujuzi wa ushonaji na kilimo cha bustani kwa ajili ya biashara ya mazao.

Mzee Mkwawa na mke wake waliendelea kufatilia maendeleo ya binti yao kipenzi katika taaluma na stadi za maisha ili kuhakikisha kuwa binti yao alikuwa akikua vyema kitaaluma pamoja na kiujuzi kuhusu maisha yake ya kila siku.

SHINDANO LA USHONAJI.

Binti Mkwawa alipofika kidato cha tatu katika shule ya sekondari ya Sogea alifurahi sana kutangaziwa na uongozi wa shule kuwa kuna shirika kubwa la kiserikali lililokuwa limetangaza shindano zuri sana kwa ajili ya Ushonaji wa nguo maalumu ambayo ingekuwa vazi maalumu kwa ajili ya wabunge wote wa jinsia ya kike katika nchi ya Matamanio kwa kulivaa vazi hilo mara tu wawapo bungeni. Taarifa hii ilimfurahisha sana Binti Mkwawa maana alijua ni nafasi ya kuonyesha uwezo wake wa ushonaji wa nguo, uwezo alioupata tangu alipokuwa akisoma shule ya msingi.

Binti Mkwawa alienda kujisajili kwenye shindano na kuendelea na mazoezi akiwa anasubiri siku husika kwa ajili ya mpambano wa ushonaji. Binti Mkwawa alikuwa akiamini kuwa nidhamu ilikuwa jambo la lazima katika mafanikio yoyote kwa mtu yoyote, hivyo basi aliadhimu kuendelea kujiheshimu na kuwa na nidhamu katika kazi hiyo ya ushonaji.

Wakati wote alipokuwa akikutana na changamoto katika ushonaji alimuuliza mama yake maana na yeye alikuwa ni fundi stadi wa ushonaji katika kitongoji kilichokuwa kimepakana karibu sana na mji wa Matamanio. Mama yake alimfundisha mbinu kadha wa kadha kuhusu jinsi ya kutumia muda mfupi kufanya kazi kubwa ya ushonaji lakini pia alimfundisha jinsi ya kusikiliza kwa umakini maelekezo ya shindano ili kufanya vizuri kwa ajili ya kujipatia ushindi katika shindano la Ushonaji.

Hatahivyo siku ya shindano iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu sana iliwadia na washiriki wote walifika mahali husika kwa ajili ya kuanza mtanange wa ushonaji, ndipo . . . . . .

ITAENDELEA IJUMAA HII.
 
Back
Top Bottom