SIRI
MTUNZI: PATRICK CK
PART 1 SEASON 6
EPISODE 10
Baada ya kumaliza
kuzungumza na Lucy Themba
simuni,Dr Evans akasimama na
kushika kiuno
“Mambo yanazidi kuwa
magumu.Nilitegemea hadi
muda huu Mathew awe
amekwisha funguka na tujue
kila kitu kinachoendelea
kuhusu mipango ya IS lakini
ametoroshwa na hajulikani
alipo.Alikuwa ni mtu muhimu
sana kwetu.Devotha amefanya
kitu kibaya mno kuamua
kumtorosha Mathew.Nguvu
kubwa kwa sasa ni kuielekeza
kwa Olivia.Kama bado
ataendelea kuwa mgumu
nitaagiza hata mama yake naye
achukuliwe aunganishwe na
baba yake.Akiwaona wazazi
wake wanavyopata mateso
atafunguka” akawaza Dr Evans
akachukua simu na kumpigia Dr
Mbeula ikiwa ni mara ya tatu
kumpigia toka asubuhi
“Mheshimia rais” akasema
Dr Mbeula
“Dr Mbeula nataka
kufahamu maendeleo ya
mwanangu.Kuna hatua yoyote
mmepiga hadi hivi
sasa?akauliza Dr Evans
“Mheshimiwa rais
tumeendelea na zoezi la
kuvifahamu kwa undani virusi
hivi ili tuone namna ya
kuvikabili lakini kadiri muda
unavyokwenda ndivyo
tunavyozidi kugundua mambo
mengine Zaidi kuhusu virusi
hivi.Kwanza kabisa virusi hivi
vina tabia ya kujibadili
umbo.Kila vinapokutana na
dawa au kemikali aina Fulani
hujibadili umbo lake. Hivyo
inatupa ugumu kupata dawa ya
kupambana navyo.Pili virusi
hawa wakiingia katika mwili wa
binadamu wanatengeneza
kemikali ambayo inaua kinga ya
mwili.Mhes….”
“Dr Mbeula samahani kwa
kukukatisha” Rais akasema
“Endelea mheshimiwa rais”
“Ninachotaka kusikia
kutoka kwako ni kama uwezo
wa kupambana na virusi hivyo
mnao.Kama unadhani hamna
uwezo nijulishe haraka ili
nimpeleke mwanangu nje ya
nchi kwa matibabu Zaidi kabla
hali yake haijawa mbaya”
akasema Dr Evans
“Mheshimiwa rais kwa
namna tunavyoendelea na zoezi
letu nina uhakika mkubwa
tutafanikiwa kuwafahamu
vyema virusi hawa na
kupambana nao lakini
haitakuwa kwa haraka”
“Una uhakika mtafanikiwa
Dr Mbeula?
“Ndiyo mheshimiwa rais
ninao uhakika.Naomba
uniamini”akajibu Dr Mbeula
“Vipi hali ya Coletha hivi
sasa anaendeleaje?akauliza Dr
Evans
“Hali yake inandelea vyema
mheshimiwa rais”
“Sawa Dr Mbeula.Nitakuja
baadae jioni kumjulia hali
mgonjwa.Naombeni mjitahidi
sana” akasema Dr Evans
“Tunajitahidi mheshimiwa
rais lakini bado kuna kitu
nataka kukifahamu” akasema
Dr Mbeula.
“Kitu gani Dr Mbeula?
akauliza Dr Evans
“Mheshimiwa rais ninataka
kujua kama unafahamu kitu
chochote kuhusiana na virusi
hivi.Ninataka kufahamu chanzo
chake na kama kuna wagonjwa
wengine ambao
wameambukizwa virusi hivi”
akasema Dr Mbeula.
“Dr Mbeula kwa sasa
jielekezeni katika kutafuta
ufumbuzi wa kupambana na
virusi hao.Hayo masuala
mengine achana nayo
kwanza”akasema Dr Evans
wakaagana
“Olivia ! Olivia !! akasema
Dr Evans kwa hasira
“Ni Olivia aliyesababisa
haya yote.Kwa nini lakini
akanifanyia kitendo cha kikatili
namna hii?Kwa nini anataka
kumuangamiza mwanangu?
Nimemkosea nini hadi akaamua
kunifanyia hivi?Atapata faida
gani kama Coletha akipoteza
maisha? Ninaapa kama
mwanangu Coletha akifariki
dunia nitaiteketeza familia yake
yote bila kujali kama ni marafiki
zangu.Mwanangu hawezi
kupoteza maisha bila hatia
halafu nikae kimya!! Akawaza
Dr Evans na kumpigia simu
Kaiza
“Mheshimiwa rais”akasema
Kaiza
“Kaiza nipe habari.Nini
kinaendelea mpaka
sasa?akauliza Dr Evans kwa
ukali
“Mheshimiwa rais
tunaendelea kumtafuta Devotha
na tulifanikiwa kumfahamu mtu
ambaye angetupa taarifa
muhimu za kuweza kumpata
Devotha lakini kwa bahati
mbaya tumempoteza”
“Mmempoteza?! Dr Evans
akashangaa
“Tumempoteza
mheshimiwa rais.Aliwahi
kujirusha ghorofani kabla
hatujamkamata akafariki
dunia.Hivi sasa vijana
wanaendelea kupitia kompyuta
yake na ili kufahamu kama
wanaweza wakapata kitu
chochote kitakachopelekea
kumpata Devotha.Kwa sasa
nimefika hapa mahala alipo
Olivia ninataka kuendelea na
mahojiano naye”akasema Kaiza
“Kaiza tafadhali hakikisha
Olivia anafunguka na anasema
kila kitu.Ninakupa huu ni
mtihani wako wa mwisho
ukishindwa kumfungua
nitatafuta watu wengine
wanaoweza kuifanya hiyo kazi”
akasema Dr Evans
“Nitajitahidi kufanya kila
niwezalo kuhakikisha tunapata
kila taarifa kutoka kwa Olivia”
akasema Kaiza na rais akakata
simu kwa hasira
“Rais amepoteza kabisa
Imani na sisi kwa sababu ya
Olivia.Nikishindwa katika hili
hataniamini tena na aligusia
hata kuifutilia mbali idara
yetu.Natakiwa kumfanya
atuamini tena na hii
itawezekana kama tukimfungua
Olivia” akawaza Kaiza wakati
akishuka ndani ya gari.
NAIROBI KENYA
Ndege ya shirika la ndege la
Ethiopia iliwasili katika uwanja
wa ndeje wa Jomo Kenyatta
jijini Nairobi ikitokea Tel aviv
Israel kupitia Adis Abbaba
Ethiopia.Miongoni mwa abiria
wawili waliokuja na ndege hii ni
majasusi wawili wa shirika la
ujasusi la Israel Mossad,Fishel
na Ehud ambao walitumwa
nchini Kenya kwa kazi maalum.
Siku tatu zilizopita roketi
lililorushwa na wanamgambo
wa kipalestina wakishirikiana
na kikundi cha Islamic state
lilitua katika shule ya chekechea
na kusababisha vifo vya watoto
kumi na mbili.Shambulio hilo
lililolaaniwa kila kona ya dunia
lilimpelekea waziri mkuu wa
Israel aitishe kikao cha dharura
na wakuu wa shirika la ujasusi
la Israel Mossad.Katika kikao
hicho waziri mkuu alitaka
kufahamu namna Mossad
walivyojipanga kuwamakata
viongozi wakuu wa kikundi cha
IS ambacho kinashirikiana na
vikundi vingine vya
wanamgambo wa kipalestimna
kuendesha mashambulizi katika
ardhi ya Israel na kuua watu.
Mkurugenzi mkuu wa
Mossad alimueleza waziri mkuu
mikakati ya Mossad kuwa ni
kuwapata wafadhili wakuu wa
vikundi vile ambao ni Habiba
Jawad na Sayid Omar.Alimpa
taarifa za kuwepo kwa mtu
wanayemshikilia katika sehemu
ya siri nchini Kenya anaitwa
Edger Kaka ambaye ana
mahusiano na watu hao wawili
wanaowatafuta
sana.Alimkumbusha kuhusu
operesheni iliyofanyika nchini
Tanzania na Edger akatekwa.
“Baada ya kumteka nchini
Tanzania tulimpeleka Kenya
ambako tumemuhifadhi kwa
miaka mitatu sasa.Aliwahi
kuhojiwa na kutoa taarifa
chache lakini hazikusaidia
kuwapata Habiba Jawad na
Sayid Omar ambao
wameendelea kufadhili vikundi
vya kigaidi vinavyoendeleza
mauaji dhidi ya
waisrael.Tuliamua kumuacha
kwa muda mrefu bila kumuhoji
huku akiishi katika mateso na
upweke mkubwa ndani ya
chumba chenye giza na mateso
mengine ya kumuumiza kiakili
ili kumfanya awe tayari kutupa
taarifa zote za kuwahusu
Habiba na Sayid pale
tutakapoamua
kumuhoji.Naamini sasa ni muda
muafaka wa kumuhoji.Kwa
mateso aliyoyapata kwa miaka
mitatu atakuwa tayari
kuzungumza.”akasema mkuu
wa Mossad
Baada ya kikao kile ndipo
Fishel na Ehud wakatumwa
nchini Kenya kumfanyia
mahojiano Edger Kaka na
kuhakikisha anaeleza kila kitu.
Katika uwanja wa ndege wa
Jomo Kenyatta majasusi hao
walipokewa na afisa kutoka
ubalozi wa Israel nchini Kenya
wakaelekea moja kwa moja
katika hoteli walikoandaliwa
kufikia.Kutoka hotelini
wakachukuliwa na kupelekwa
hadi katika ubalozi wa Israel
nchini Kenya ambako Mossad
walikuwa na ofisi zao.
“Karibuni sana
Nairobi,karibuni sana
Afrika”akasema Avi mkuu wa
Mossad Afrika mashariki
“Tunashukuru sana
tumekaribia” akasema Ehud
“Nini kinachoendelea hapa
kuhusu Edger Kaka?akauliza
Fishel
“Edger yuko hapa ubalozini
kwa muda wa miaka mitatu
sasa na kwa muda huo
ameendelea kuishi katika
mateso bila kufanyiwa
mahojiano yoyote.Tumekuwa
tunamtesa kisaikolojia ili pale
tutakapoanza kumuhoji awe
ameteseka vya kutosha na
aeleze kila kitu.Watu kama
hawa wenye mahusiano na
magaidi kwa kawaida
wanakuwa wagumu mno
kufunguka na kutoa siri hivyo
mateso kama haya huwafanya
wawe tayari kusema kila kitu”
akasema Avi na kuwasha
runinga na mtu mmoja
aliyekuwa mtupu akiwa
amefungwa minyororo
mikononi na miguuni amelala
katika sakafu yenye baridi
akaonekana.
“Yule ndiye Edger
Kaka”Akasema Avi
“Haya ndiyo mateso
ambayo amekuwa akipewa kwa
miaka mitatu sasa.Amekuwa
akipewa chakula mara moja
kwa siku.Chumba alimo kuna
baridi na amekuwa akiishi
hivyo bila mavazi
yoyote.Kikubwa ambacho
tumekuwa tunakiwekea mkazo
mkubwa ni kuhakikisha hapati
magonjwa yoyote.Kila siku
daktari humkagua kujiridhisha
na maendeleo yake.Anaonekana
dhaifu lakini hana tatizo lolote
la kiafya” akasema Avi
Edger kaka alikuwa
amejikunyata katika pembe
akiwa amefungwa minyororo
mikononi na miguuni.Alikuwa
mtupu kabisa Alitia huruma
sana.Alikuwa ameota ndevu
nyingi na haikuwa rahisi
kutambulika kwa haraka.Ehud
akamtazama kwa makini na
kusema
“Kwa namna
anavyoonekana tayari
amekwisha kata tamaa”
“Hatua ya kwanza
tunayoanza nayo ni kumtoa
katika mateso aliyonayo sasa na
kumuweka katika maisha
mazuri.Anatakiwa anyolewe
nywele na ndevu aogeshwe na
avishwe mavazi mengine
mapya.Baada ya hapo
tutaendelea na hatua
inayofuata.Kitu kingine kabla ya
kuanza kumuhoji Edger
tunatakiwa kuifahamu historia
yake alikokotoka hadi hapa
alipofika.Naamini kwa muda
huu mrefu mtakuwa
mmekusanya taarifa za kutosha
za kumuhusu” akasema Ehud na
Avi akapiga simu akaomba
kutumiwa faili la Edger Kaka
katika ile ofisi
alimokuwemo.Baada ya
sekunde chache faili likatumwa
akatoka akawaacha akina Ehud
wakiendelea kupitia taarifa
zilizokuwa zimekusanywa
kuhusu Edger.
“Taarifa yake ni nzuri haina
hata chembe ya mashaka.Ni
mbunge aliyependwa
sana,amekuwa mstari wa mbele
kupambana na mafisadi.Ni
mbunge aliyejizoea umaarufu
mkubwa sana na ni mmoja wa
wanasiasa vijana waliokuwa
wanatajwa kufaa kushika nafasi
ya urais.Imetokeaje mtu kama
huyu akajiunga na kikundi cha
ugaidi?akauliza Fishel
“Hata mimi
inanishangaza.Sikujua kama
alikuwa mtu maarufu nchini
mwao kiasi cha watu kumtaja
hata kushika nafasi ya urais”
akasema Ehud
Edger Kaka alifunguliwa
minyororo akatolewa katika
kile chumba,hakuweza
kutembea akabebwa na
kupelekwa bafuni akaogeshwa
akanyolewa nywele na ndevu
halafu akavishwa mavazi
mengine mapya.Ngozi yake
ambao haikuonja hata tone la
mafuta kwa muda wa miaka
mitatu ilikuwa imekakamaa
hakuwa Edger yule
mtanashati.Alibadilika
mno.Hakuweza kutembea
akawekwa katika kiti cha
magurudumu akasukumwa
hadi katika chumba kimoja
kulikoandaliwa chakula
kizuri.Harufu nzuri ya vyakula
vilivyoandalia ilimsisimua sana
Edger ambaye hakuwa
ameisikia harufu nzuri kama ile
kwa muda mrefu.Alihisi njaa
kali alitamani akivamie chakula
kile akimalize chote lakini mwili
wake haukuwa na nguvu.Baada
ya dakika tatu wakaingia watu
wawili wakakaa mezani na
Edger akasogezwa karibu na
meza akashushwa kutoka
katika kiti kile cha
magurudumu na kuweka katika
kiti cha kulia chakula.Mikono
ilikuwa inamtetemeka alipoona
chakula kile kizuri.
“Edger karibu
chakula,tumia kadiri uwezavyo”
akasema Fishel na kumsogezea
Edger sahani na kumpakulia uji
mzuri katika bakuli.Edger
akajaribu kushika kijiko
akashindwa.Mikono haikuwa na
nguvu.Fishel akasohgeza kiti
akakaa karibu yake
akamnywesha uji ule hadi
bakuli lilipomalizika.Taratibu
Edger akaanza kuhisi mikono
inapata nguvu akaomba tena
chakula kingine.Fishel
akampakulia chakula
akaendelea kumlisha
sambamba na kumnywesha
kinywaji.Edger hakuamini kama
amekula tena chakula kile kizuri
ambacho hakuwa na matumaini
ya kukiweka tena katika ulimi
wake.Hakutaka kuacha alitaka
aendelee kula lakini Fishel
akamzuia akamtaka apumzike
kwanza.Edger akatolewa katika
kile chumba cha chakula
akapelekwa katika chumba
kingine kizuri chenye kitanda
kikubwa na godoro
zuri.Machozi yalimtoka
alipobebwa kutoka kwenye kiti
na kukalishwa kitandani.
“Siamini kama nimeweza
tena kulala katika godoro zuri
kubwa na laini.Sifahamu ni kwa
muda gani nimekaa katika kile
chumba chenye giza lakini
naamini ni muda
mrefu.Nimeteseka na kulala
mtupu katika sakafu yenye
baridi nikiteseka kwa njaa na
kiu.Nini kimetokea leo hadi
wakanitendea hivi?akajiuliza
Edger akiendelea kutiririkwa na
machozi.Taratibu akahisi
macho mazito na haukupita
muda akapitiwa na usingizi
akalala
“Nimemtazama machoni
anaonekana wazi amechoka na
mateso aliyoyapata.Hakuamini
alipoweka tena mdomoni
chakula kizuri.Naamini
tutakapoanza kumuhoji
atakuwa tayari kusema kila
kitu” akasema Ehud
“Ni mateso makubwa sana
miaka mitatu kukaa ndani ya
chumba chenye giza huoni
mwangaza wa jua.Naamini
hatakubali tena kurejea katika
mateso yale” akasema Fishel.
Edger aliachwa apumzike
katika kitanda kile kikubwa
akaamshwa na kupelekwa
katika chumba kingine ambamo
walikuwemo Fishel na Ehud
“Edger Karibu.Tumekutana
tena.Unajisikiaje?akauliza
Fishel
“Kwa sasa ninahisi nguvu
kidogo” akasema Edger kwa
sauti dhaifu ambayo haikuwa
inasikika vyema.
“Edger mimi na
mwenzangu tuna mazungumzo
kidogo nawe lakini kabla ya
kuzungumza nataka upumzike
kwa dakika kumi.Wakati
ukipumzika tunataka uangalie
filamu hii halafu tutarudi
kuzungumza” akasema
Fishel.Edger akashushwa
kutoka katika kile kiti cha
magurudumu akakalishwa
sofani.Fishel na Ehud wakatoka
wakamuacha peke yake.Baada
ya dakika tano toka Fishel na
Ehud watoke mle chumbani
akaingia mtu mmoja akamfunga
Edger kifaa Fulani mkononi
halafu akawasha runinga kisha
akatoka akamuacha Edger peke
yake ndani ya chumba.
“Ifuatayo ni historia fupi ya
mbunge Edger Kaka aliyefariki
katika ajali ya gari siku mbili
zilizopita” Ndivyo ilivyoanza
taarifa ile na kumstua mno
Edger.Alitamani kunyanyuka
lakini miguu haikuwa na
nguvu.Akabaki anashuhudia
picha zake mbali mbali
zikionyeshwa zilizoambatana
na historia yake.Mdomo ulibaki
wazi akishangaa
Wakati Edger akiendelea
kutazama taarifa ile
iliyohusiana na kifo na mazishi
yake Fishel na Ehud walikuwa
katika ofisi yao wakimfuatilia
Edger kwa makini kupitia
kamera.Pamoja nao alikuwepo
mtu mwingine aliyekuwa katika
kompyuta akiangalia grafu
iliyokuwa inapanda na kushuka
“Ameonyesha mstuko
mkubwa sana baada ya taarifa
kuanza.Inaonyesha hafahamu
chochote kilichotokea.Hajui
kama alikwisha fariki na
kuzikwa” akasema yule jamaa
aliyekuwa anafuatilia chati ile
katika kompyuta.Wakati Edger
akiendelea kutazama rekodi ile
runingani akionekana
kuchanganyikiwa mara
akapatwa na mstuko mkubwa
baada ya kumuona mwanadada
mmoja akiwa amevaa gauni
refu jeusi na kilemba cheusi
kichwani na macho yake
aliyafunika kwa miwani
mikubwa akiwa amesimama
katika mimbari akisoma
historia ya Edger
Kaka.Alishindwa kumalizia aya
ya mwisho akaangua kilio
akatokea mwanamke mmoja na
kwenda kumshika mkono
akamrejesha kitini kuketi.
“Olivia !! akasema Edger
Kaka akiwa ameyatumbua
macho.Alipatwa na mstuko
mkubwa sana
“Huyu mwanamke ni
nani?akauliza Fishel
“Huyu ni daktari wake
anaitwa Olivia Themba.Ndiye
aliyekuwa naye nchini
Israel”akajibu yule jamaa
aliyekuwa anafuatilia grafu
“Edger amestuka mno
baada ya kumuona Olivia.Grafu
imepanda hadi kupita kile
kiwango chake cha
kawaida.Kwa mstuko huu
lazima Olivia ni mtu muhimu
sana kwake”akasema yule
jamaa.Ehud na Fishel
waliendelea kumtazama Edger
mara wakastuka baada ya
Edger kuanguka
chini.Walisubiri kwa dakika
mbili kama atainuka lakini
aliendelea kulala pale
chini.Haraka haraka wakatoka
mbio na kwenda katika chumba
alimo Edger na kumkuta
amepoteza fahamu.Wakamtoa
ndani ya kile chumba na
kumuingiza katika chumba
kingine daktari akaitwa akafika
haraka na kumpima na
akawatoa wasiwasi kwamba
Edger hakuwa na tatizo bali
alipoteza fahamu kutokana na
mstuko.
“Ni mstuko uliopelekea
akapoteza fahamu lakini hana
tatizo lolote”akasema daktari.
Edger aliachwa katika
chumba chenye hewa ya
kutosha hadi
alipozinduka.Baada ya
kuzinduka akaachwa kwa muda
wa robo saa halafu akapelekwa
tena katika chumba kingine
walimo Fishel na Ehud
“Edger pole sana kwa
kilichotokea” akasema Fishel
aliyezungumza kwa upole
mkubwa
“Ninyi ni watu wakatili
sana.Kwa nini mmenifanyia
hivi? Kwa nini mmenionyesha
video ile?akauliza Edger
machozi yakimtoka.Bado sauti
yake ilikuwa dhaifu sana
“Jina lako nani?akauliza
Fishel
“Naitwa Edger Kaka”
“Edger unatokea wapi?
“Mimi ni mtanzania”
“Hapa ulipo unafahamu ni
wapi?
“Sifahamu niko
wapi.Maisha yangu yamekuwa
katika chumba chenye giza
nikisubiri Mungu aichukue roho
yangu lakini naye ameniacha
nikiteseka hataki kunichukua”
akasema Edger akionekana
kukata tamaa kabisa na maisha
yake
“Siku 1095,saa 26280 ndizo
ulizokaa humu ndani ambazo ni
sawa na miaka mitatu.Najua
hufahamu muda ambao umekaa
ndani ya kile chumba lakini ni
miaka mitatu sasa.Hiki ni
kipindi kirefu,mambo mengi
yamefanyika duniani.Binadamu
wa kwanza ametua katika
sayari ya Mars.Chaguzi nyingi
zimefanyika katika nchi mbali
mbali ikiwemo
Tanzania.Kikubwa kuliko yote
ulifariki ukazikwa na tayari jina
lako limesahaulika limebaki
katika kumbu kumbu kwamba
aliwahi kutokea mtu anaitwa
Edger Kaka” akasema Ehud
“Mimi sijafariki bado niko
hai.Kilichoonekana katika
filamu ile ni uongo
mkubwa.Mimi niko hai”
akasema Edger
“Video ile uliyoitazama
muda mfupi uliopita ambayo
imesababisha ukapoteza
fahamu imekuonyesha kila kitu
kwamba tayari umefariki dunia
na tayari umezikwa.Umeyaona
mazishi yako namna watu
walivyohuzunika kwa kifo
chako.Wengi walivaa fulana
zenye jina lako
wakikulilia,wakipita mbele ya
jeneza lako wakitoa salamu za
mwisho.Edger wewe tayari
umekwisha fariki”akasisitiza
Ehud
“Nashindwa
kuwaelewa.Kwa nini
mnanisisitiza kwamba
nimekufa wakati niko hai? Mimi
niko hai sijafa ! Mimi ni
binadamu si mzimu.Nini
kimefanyika hadi nionekane
nimekufa?akauliza Edger
“Edger tayari
umekufa.Naomba
nikukumbushe namna
ulivyopoteza maisha.Ulikuwa
unaelekea nyumbani kwako
ukitokea uwanja wa ndege wa
Julius Nyerere jijini Dar es
salaam.Ulikuwa umerejea
nchini kwako kutokea Israel
ulikoenda kwa matibabu.Muda
mfupi baada ya kuondoka
uwanja wa ndege wa Julius
Nyerere msafara wako ulipata
ajali.Tayari umepata picha ya
kilichotokea?akauliza
Fishel.Edger akabaki kimya
“Edger unakumbuka
chochote kuhusiana na ajali
ile?akauliza Ehud
“Ndiyo nimekumbuka kila
kitu na kitu cha mwisho
ninachokumbuka ni kishindo
kikubwa na kukawa kiza
kinene.Sifahamu kama ilikuwa
ni ajali au nini lakini nilipokuja
kupata fahamu nilijikuta katika
chumba chenye giza nikiwa
nimefungwa minyororo na watu
wakaanza kunihoji kuhusu
kikundi cha IS.Nimeshangaa
kuona video ile watu wakinililia
eti nimekufa.Nimestuka sana
sikutegemea kitu kama hiki
ndiyo maana nikapoteza
fahamu.Nini kiliwekwa ndani ya
lile sanduku ili kuwaaminisha
watu kuwa nimekufa”akauliza
Edger
“Edger ulifariki usiku ule na
tayari umekwisha zikwa na hili
hapa ni kaburi lako” akasema
Ehud akatoa picha katika faili
akamuonyesha Edger
akaitazama huku mikono
ikimtetemeka
“Haya mambo nashindwa
kuyaelewa.Kwa nini
nimefanyiwa hivi?kwa nini
mmeniteka na kunizushia kifo
wakati niko hai?Mwili ule
ambao ulizikwa ndani ya jeneza
linalodaiwa ni la kwangui ni
mwili wa nani?akauliza Edger
“Sikiliza Edger.Katika siku
1095 waisrael 59 wamepoteza
maisha.Kumekuwa na
urushwaji wa maroketi kutokea
upande wa Palestina
kunakofanywa na vikundi vya
wanamgambo wa kipalestina
wakisaidiwa na kikundi cha
kigaidi cha IS.Siku tatu
zilizopita roketi limerushwa na
kutua katika shule ya watoto
wadogo na kuua idadi kubwa ya
watoto.Matendo kama haya ya
kikatili yanayofanywa na
wanamgambo wa kipalestina
wakisaidiwa na kikundi cha
kigaidi cha IS yameendelea
kushika kasi kutokana vikundi
hivi kuwezeshwa kwa fedha na
silaha hivyo kuwa na uwezo wa
kujipanga na kufanya
mashambulio katika ardhi ya
Israel.Baada ya uchunguzi wa
kina imebainika kwamba
mfadhili mkubwa wa vikundi
hivi anaitwa Habiba
Jawad.Huyu ni mwanamke
tajiri.Aliwahi kuolewa na
mwanaume tajiri ambaye
alikuwa na asili ya Palestina na
aliutumia utajiri wake kufadhili
makundi ya wanamgambo kuua
waisrael na ndipo vikosi vya
Israel vilipompiga risasi
akafariki.Habiba Jawad alirithi
utajiri wa mumewe na
akaendelea kufadhili vikundi
vya kigaidi.Ili asigundulike
kuwa ni yeye anayefadhili
vikundi hivi anamtumia mtu
anaitwa Sayid Omar.Kwa muda
mrefu Habiba na Sayid
wamekuwa wakitafutwa sana
na serikali ya Israel lakini
hawajapatikana hadi
sasa.Wamekuwa wakisaidiwa
na serikali ya Saudi Arabia
kujificha” Fishel akasema na
kumtazama Edger kwa muda
halafu akaendelea
“Ukiwa hospitalini nchini
Israel ulitembelewa na watu
wawili ambao ni Habiba Jawad
na Sayid Omar ukaonana nao
mkazungumza.Kitendo cha
Habiba Jawad na Sayid Omar
kuhatarisha maisha yao kwa
kuingia katika ardhi ya Israel
wanakotafutwa sana kwa lengo
moja tu la kuja kuonana nawe ni
kiashiria tosha kuwa wewe ni
mtu muhimu sana
kwao.Ukaribu wako na Habiba
na Sayid unakufanya uwe mtu
wetu muhimu sana ndiyo
maana uko hapa kwa miaka
mitatu sasa na yawezekana
ukaendelea kuishi hapa kwa
miaka mingi Zaidi yawezekana
hadi mwisho wa uhai wako
kwani katika ulimwengu wa
kawaida tayari
umefariki,umezikwa na
umesahaulika.Jina lako limebaki
historia.Hakuna anayekutafuta
tena.Tumekuacha kwa miaka
mitatu bila kukuuliza chochote
ili kukuonyesha kwamba
tunaweza kukuacha ukateseka
hadi siku utakapopoteza maisha
yako.Siku ya leo tumekutoa
katika chumba cha giza na
tumekurejesha katika maisha ya
kawaida japo kwa muda mfupi
kukumbusha kwamba unayo
nafasi ya kurejea katika maisha
yako ya kawaida.Bado unayo
nafasi Edger ni juu yako
kuitumia”Fishel akanyamaza
tena akamtazama na kusema
“Edger historia yako
inaonyesha wewe uliwahi kuwa
mbunge wa bunge la jamhuri ya
muungano wa Tanzania ukiwa
ni mbunge mwenye umaarufu
mkubwa.Ulikuwa kinara wa
kupambana na ufisadi na
kutokana na juhudi zako katika
kuwapigania na kuwasemea
wanyonge walianza kukutaja
kuwa ni mmoja wa watu
wanaofaa hata kupewa nafasi
ya kuongoza nchi.Nyota yako
tayari ilikwisha anza kung’ara
lakini hukuweza kutimiza
malengo yako na ukajikuta
mahala hapa ambako kumezima
ndoto zako zote.Edger
tumekufungulia dirisha dogo
ambalo unaweza ukalitumia
kutoka na kurejea katika
maisha yako ya awali.Uchaguzi
ni wako mwenyewe kama utoke
kupitia nafasi hii uliyoipata au
uendelee kubaki hapa kwa
maisha yako yote ukiendelea
kuteseka hadi pale roho yako
itakapokutoka.Kipi
unakichagua?Kutoka au
kuendelea kukaa katika chumba
kile cha giza?Kumbuka hakuna
mtu yeyote anayefahamu kuwa
uko hai au uko hapa hivyo
mwenye kuamua hatima ya
maisha yako ni wewe
mwenyewe” akasema
Fishel.Edger akainamisha
kichwa akatafakari kwa muda
halafu akasema
“Nimechoka na mateso
haya.Mmenitesa vya kutosha
sitaki kurejea tena katika kile
chumba.Niambieni nini
mnakitaka ili kuniondoa katika
mateso haya na kunirejeshea
maisha yangu ya
uhuru?akauliza Edger
“Umefanya uchaguzi
mzuri.Huo ni uamuzi wa busara
sana.Nataka unijibu
unawafahamu Habiba Jawad na
Sayid Omar? Akauliza Ehud
“Ndiyo ninawafahamu”
akajibu Edger
“Tunataka utupe taarifa
ambazo zitatusaidia kuwapata
watu hawa wawili.Habiba
Jawad na Sayid Omar
wanaendelea kufadhili vikundi
vya wanamgambo wa
kipalestina ambao wanafanya
mauaji dhidi ya waisrael.Ni hilo
tu ambalo tunalihitaji na kama
ukitusaidia tukawapata watu
hao nakuhakikishia kwamba
tutakurejeshea maisha
yako.Tutakuachia huru na
tutakupa pia ulinzi mkubwa
pamoja na kukupeleka ukaishi
mahala ambako utakuwa
salama salimini na utaendesha
maisha yako kimya kimya.Uko
tayari kutueleza
ukweli?akauliza Fishel.Edger
akavuta pumzi ndefu
akainamisha kichwa akazama
mawazoni.Fishel na Ehud
wakamuacha atafakari.Zilipita
dakika tatu Edger akainua
kichwa na kusema
“Nimekaa katika chumba
cha giza kwa miaka mitatu na
sielewi chochote
kinachoendelea huko duniani
hivyo ni ngumu sana kwangu
kujua mahala waliko Habiba
Jawad au Sayid” akasema Edger
“Wote wawili walikuja
kukutembelea hospitali nchini
Israel.Una mahusiano gani
nao?akauliza Ehud
“Sina mahusiano yoyote
nao” akajibu Edger
“Kama huna mhusiano nao
kwa nini walikuja
kukutembelea hospitali mara
mbili?akauliza Fishel
“Sikuwa nikifahamiana na
Habiba au Sayid Omar hadi
walipokuja kunitembelea
hospitali.Kilichowaleta hospitali
walitaka niwasaidie kufanikisha
mradi wao wa kuanzisha
kampuni ya mafuta nchini
Tanzania”
“Habiba Jawad na Sayid ni
watu ambao wanatafutwa na
serikali ya Israel lakini
hawakuhofia usalama wao na
wakaingia Israel kwa sababu
moja tu ya kuja kukuona
hospitali.kwa nini wewe na
asiwe mtu mwingine?akauliza
Fishel
“Walipataje taarifa za wewe
kulazwa hospitali Israel?
akauliza Ehud
“Sifahamu walipataje
taarifa zangu na sielewi kwa
nini walinichagua mimi” akajibu
Edger
“Edger hiki unachokieleza
tunajua ni uongo
mtupu.Tunajua unawafahamu
vyema Habiba na Sayid na
hospitali pale haikuwa mara ya
kwanza kuonana.Edger tambua
hapa tunazungumzia maisha ya
waisrael wanaoendelea kuuawa
kila siku,maisha ya wapalestina
ambao wanaendelea kuuawa
kutokana na vurugu
zinazosababishwa na
wanamgambo wa kipalestina
wanaofadhiliwa na akina
Habiba.Vile vile tunazungumzia
hatima ya maisha yako.Najua
unafahamu kila kitu kuhusu
Habiba na Sayid lakini
unaogopa
kusema.Nakuhakikishia Edger
unakosea sana kwani hao
unaojaribu kuwaficha hawana
msaada tena kwako.Tayari
wanajua umefariki na
wamekwisha kusahau.Hakuna
ambaye atakusaidia kukuondoa
mahala hapa.Hatima ya maisha
yako utaiamua wewe
mwenyewe.Tupe kile
tunachokitaka tuokoe maisha
ya watu wetu na sisi
tukurejeshee maisha yako
mazuri.Tunajua kile
utakachotueleza kina gharama
hivyo tuko tayari kutoa malipo
ambayo ni kukusaidia kuanza
maisha mapya.Hii ni nafasi
pekee umeipata na hautaipata
tena nafasi nyingine kama hii
hivyo ukishindwa kuamua leo
utarudishwa tena katika kile
chumba na huo utakuwa ni
mwisho wako” akasema Fishel
“Sipendi kukaa katika
chumba kile nimechoka na
mateso haya ninayoyapata
lakini sina chochote cha
kuwaeleza kuhusu Habiba au
Sayid Omar.Nilichowaeleza ni
ukweli mtupu siwafahamu watu
hawa na mara yangu ya kwanza
kukutana nao ilikuwa ni
hospitali kabla ya hapo
sikuwahi kuonana
nao.Tulipanga kuwasiliana nao
baada ya kufika Tanzania ili
kuwasaidia kwa taratibu za
kuanzisha kampuni ya
mafuta.Habiba alinieleza
kwamba ana visima vya
mafuta.Hakuwahi kunipa
maelezo yoyote kuhusu yeye
wala mahala anakoishi hivyo
sifahamu chochote.Naombeni
mniamini ndugu
zangu.Mnanitesa bure bila kosa
mkinihusisha na watu
nisiowafahamu” akasema Edger
na kwa mbali macho yake
yakalengwa na machozi
“Edger macho yako ingawa
yanalengwa machozi lakini
yanaonyesha wazi
unadanganya.Kwa nini
unakubali kuteseka kwa ajili ya
watu ambao hawatakuwa na
msaada kwako? Kwa nini
unawaficha watu ambao
wanajua umekwisha fariki?
Hakuna yeyote katika dunia hii
ambaye atakusaidia.Uko peke
yako hivyo jiokoe
mwenyewe.Sahau kuhusu
Habiba,Sayid au IS hakuna
ambaye atakuja hapa
kukuokoa.Edger narudia tena
kukuhakikishia kwamba
endapo ukiamua kushirikiana
nasi tutakulinda dhidi ya
IS.Serikali ya Israel itakusaidia
uweze kupata sehemu salama
ya kuishi ambako utaanza upya
maisha yako.Taarifa
utakazotupa ni muhimu sana na
ambazo zitasaidia kuokoa
maisha ya watu wengi hivyo
lazima na sisi tuhakikishe
unakuwa na maisha mazuri
wewe na wale uwapendao”
akasema Ehud.Walimpa tena
Edger nafasi ya kutafakari kisha
akasema
“Natamani sana kupata
nafasi nyingine ya kuishi
maisha mazuri yenye furaha na
amani lakini sintaweza
kuyapata maisha hayo kwa
kuwa sifahamu chochote
kuhusu Habiba Jawad au
mtandao wa IS.Laiti
ningefahamu kitu chochote hata
kidogo cha kuweza kusaidia
kuwapata watu hao
ningewaeleza lakini sina
chochote cha kuwasaidia”
“Uko tayari kurejea tena
katika kile chumba cha giza
kuendelea na mateso? akauliza
Fishel lakini Edger hakujibu
akabaki kimya
“Edger nimekuuliza hivyo
kwa sababu hii ni mara yako ya
mwisho utaipata nafasi kama
hii,kama hautaitumia vyema
hakuna tena dirisha lolote
litakalofunguliwa kukuruhusu
upite.Itumie vyema nafasi hii
kujiondoa kutoka katika mateso
haya.Narudia tena
kukuhakikishia kwamba watu
hao ambao unawaficha na
hutaki kutupa taarifa zao
hawana msaada wowote
kwako.Wakati wewe unateseka
kwa miaka mitatu ndani ya
chumba cha giza wao
wanaendelea na maisha yao
mazuri ya kifahari,wanakula
vizuri wanalala sehemu nzuri
wanasafiri kwa magari ya
kifahari na wanapata kila
wanachokihitaji kwenye maisha
yao.Wewe uko katika chumba
ambacho hakina mwangaza
ukilala katika sakafu yenye
baridi tena ukiwa
mtupu,ukipata chakula kidogo
mara moja kwa siku huku
ukinateseka kwa kiu.Si
Habiba,Sayid au IS wanafahamu
ni mateso gani unayapitia.Edger
nakukumbusha tena uko peke
yako hivyo jisaidie wewe
mwenyewe” akasema Ehud
“Naridia tena
kukuhakikishia kwamba
utakuwa na maisha mazuri
ukitoka hapa,utaishi katika
nyumba nzuri,gari zuri la
kifahari na utapata kila
unachokihitaji.Kama kuna kitu
kingine chochote unataka
tukupatie ili utupe taarifa za
Habiba na Sayid tueleze.Sisi
tukohapa kwa niaba ya serikali
hivyo chochote utakachokitaka
utakipata” akasema
Fishel.Edger akafikiri na
kusema
“Ninataka kurejea tena
katika kile chumba changu cha
giza nikaendelee na
mateso,sihitaji kitu kingine
chochote” akasema Edger
.Fishel na Ehud
wakatazamana.Hawakutegemea
jibu lile
“Edger unalifunga dirisha
ambalo halitafunguliwa
tena.Tumekupa nafasi ya
kuchagua wewe mwenyewe
aina ya maisha unayotaka
kuishi na kama ukichagua
kurudi katika kile chumba cha
giza sisi hatuna kipingamizi
tutakurejesha lakini fahamu
kuwa hakuna tena nafasi
nyingine itakayofunguliwa
kwako” akasema Ehud
“Nirejesheni nikaendelee
kuteseka” akasema Edger.
“Edger kabla ya
kukurejesha tena katika
chumba kile kuna kitu nataka
ukifahamu” akasema Fishel na
kufungua faili akatoa picha
akamuonyesha Edger ambaye
sura yake ilibadilika baada ya
kuiona picha ile.
“Unamfahamu
huyu?akauliza
“Ndiyo.Huyu ni Olivia
Themba daktari wangu ambaye
aliyaokoa maisha yangu
nilipotaka kuuawa kwa sumu”
akajibu Edger
“Kila unapoiona picha yake
unastuka sana.Kuna nini
kinaendelea kati yenu?akauliza
Ehud
“Huyu mtu mwenye
umuhimu mkubwa kwangu.Bila
yeye hivi sasa tayari
ningekwisha fariki na hata ninyi
msingep[ata nafasi ya
kunitesa.Watu walitaka nifariki
dunia lakini yeye alipambana
akayaokoa maisha yangu hivyo
nitaendelea kumshukuru hadi
mwisho wa maisha yangu”
akasema Edger
“Kwa namna
unavyomuangalia Olivia
inaonyesha wazi kuna jambo
linaendelea zaidi ya urafiki wa
kawaida.Unampenda
Olivia?Fishel akauliza
“Olivia ni rafiki
yangu”akajibu Edger
“Jibu swali
unampenda?akauliza Ehud
Edger akawa kimya
“Naomba nikupe taarifa
kwamba Olivia ametekwa na
watu wasiojulikana siku mbili
zilizopita na mpaka leo hii
hajulikani mahala alipo”
akasema Fishel
Mstuko mkubwa
ulionekana usoni kwa Edger.
“Mstuko mkubwa ulioupata
unaonyesha jinsi gani Olivia
alivyo muhimu kwako”
akasema Fishel na
kumuonyehsa Edger taarifa
mbali mbali za kuhusiana na
tukio la kutekwa Olivia kupitia
kompyuta yake.
“Nani wamemteka
Olivia?akauliza Edger
“Edger ni vipi kama
tukikusaidia ukakutana tena na
Olivia na ikiwezekana
mkaanzisha maisha yenu
sehemu tulivu ambako hakuna
atakayewasumbua?akauliza
Fishel.Edger akaitazama tena ile
picha
Ya Olivia.
“Mnao uhakika wa
kumuokoa Olivia kutoka kwa
watekaji?akauliza Edger
“Sisi tuna mtandao mkubwa
na tunaweza kukusaidia
kumpata Olivia na
tukakukutanisha naye tena”
akasema Fishel
“Tafadhali kama mnao
uwezo wa kumuokoa Olivia
fanyeni hivyo.Ni mwanamke wa
kipekee kabisa ambaye huwezi
kumfananisha na wengine na
hastahili kufanyiwa kitendo hiki
alichofanyiwa” akasema Edger
“Edger tunaweza
kumuokoa Olivia kwa vile wewe
umetutuma tufanye hivyo lakini
kabla ya kuandaa operesheni ya
kumtafuta Olivia tunataka
kufahamu kwa nini unataka
tumuokoe?Ni kwa sababu
alikusaidia kuokoa maisha yako
au kuna sababu nyingine?Tupe
sababu ya msingi ili tuone uzito
wake”Akauliza Ehud
“Olivia ni mwanamke
nimpendaye kuliko
wote.Sijawahi kupenda
mwanamke kama
ninavyompenda Olivia”
akasema Edger
“Ulipotoweka tayari
mlikuwa wapenzi?
“Sikuwa nikimfahamu
Olivia hadi nilipofumbua macho
na kujikuta hospitali nchini
Israel na ndipo nilipomuona
Olivia kwa mara ya
kwanza.Nilimpenda sekunde ya
kwanza nilipomtia
machoni.Nilimueleza hisia
zangu na tulikubaliana kulipa
suala hilo nafasi ya kutosha
tutakaporejea nyumbani kwa
bahati mbaya hilo halikutokea
tena mlinichukua na kunileta
hapa sikumuona tena Olivia
hadi nilipomuona leo katika ile
filamu.Ninampenda Olivia
tafadhali muokoeni kama
uwezo mnao”
“Ahsante kwa kutueleza
ukweli.Tutakusaidia katika
hilo.Tutakwenda Tanzania
kumtafuta Oliviana lakini kabla
ya kufanya hivyo na sisi
tutaomba utueleze kuhusiana
na Habiba Jawad na Sayid
Omar” akasema Fishel
“Nitawaeleza kila kitu pale
nitakapomuona Olivia mbele ya
macho yangu”akasema Edger
“Usihofu Edger sisi
tunakwenda kumtafuta Olivia
na tuna uhakika wa kumpata
lakini kabla hatujaingia katika
operesheni hiyo nataka kwanza
utupe maelezo kuhusu Habiba
na Sayid Omar ni jinsi gani
tutaweza kuwapata?
“Nimewaambia nitawaeleza
kila kitu lakini hadi hapo
nitakapomuona Olivia mbele ya
macho yangu niishike mikono
yake na kuhakikisha kweli ni
yeye mwanamke nimpendaye”
akasema Edger
“Sawa Edger tunakwenda
kufanya operesheni katika nchi
ya watu na kumchukua raia wa
nchi nyingine bila ruhusa au
kibali cha mamlaka husika,hili
ni jambo kubwa sana hivyo
kabla hatujafanya hivyo
tunataka kupata uhakika kuwa
hiki tunachokwenda kukifanya
kina manufaa kwetu”
“Awali uliniambia kwamba
nichague kitu chochote
ninachokitaka kutoka kwenu ili
niweze kuwapa taarifa
mnazozihitaji.Ninachokihitaji ni
kumpata OIlivia Themba na
nitawaeleza kila kitu
mnachokihitaji.Kingine nataka
mniandalie nyumba mahala
ambako nitaishi na Olivia kwa
amani” akasema Edger
“Sawa Edger.Tutafanya
kama unavyotaka.Tutamleta
Olivia mbele ya macho yako
lakini kama hautakuwa tayari
kutueleza kile tunachokitaka
utakuwa umemuweka Olivia
katika matatizo makubwa
kwani hautamuona tena na kwa
kuwa atakuwa ameifahamu siri
hii na yeye pia atafungwa katika
chumba cha giza kwa maisha
yake yote.Nataka uwe na
uhakika kuwa utatupa taarifa
zote za kuwahusu Habiba Jawad
na Sayid Omar kabla
hayujamleta Olivia” akasema
Fishel
“Naombeni mniamni
nitawaeleza kila kitu pale
nitakapomuona Olivia mbele
yangu.Kwa ajili yake niko tayari
kuweka kila kitu bayana hivyo
hakikisheni mnafanya kila
mnaloweza kumpata
Olivia.Aliyaokoa maisha yangu
na sasa ni zamu yangu
kuyaokoa maisha yake”
akasema Edger
“Sawa Edger nimeyapokea
maneno yako na sisi tutafanya
kila lililo ndani ya uwezo wetu
kuhakikisha tunampata Olivia
lakini ukumbuke
nilivyokueleza.Kama ukienda
kinyume na makubaliano yetu
utakuwa umempoteza pia Olivia
kwani hautamuona tena na
utakuwa umemsababishia
mateso makubwa” akasema
Fishel
“Msiwe na wasiwasi na
mimi.Nitawaeleza kila kitu
nikimuona Olivia” akasema
Edger.
“Vizuri.Kwa kuwa
umetuhakikishia kwamba uko
tayari kuzungumza na
kutueleza ukweli wote
hatutakurejesha tena katika kile
chumba cha giza utaendelea
kuishi maisha mazuri katika
chumba kipya ukipata kila
unachokihitaji” akasema Ehud
kisha wakamuita Avi na kumpa
maelekezo kwamba Edger
aendelee kuishi maisha mazuri
katika kile chumba kipya
asiendelee tena na mateso
Fishel na Ehud wakarejea
katika ofisi yao kujadiliana
kuhusiana na kile walichokipata
kutoka kwa Edger
“Hatimaye Edger amekubali
kueleza ukweli wote kama
akimuona Olivia.Ninaiona
nguvu ya mwanamke.Kikubwa
sasa ni namna ya kumpata huyo
Olivia.Nani kamteka na kwa
nini? Akauliza Fishel
“Fishel japo tumemuahidi
Edger kwamba tunao uwezo wa
kumpata Olivia lakini si jambo
rahisi hata kidogo.Hatujui hata
tuanzie wapi” akasema Ehud
“Ehud hilo lisikupe
shida.Tulichokuwa tunakitafuta
ni kupata taarifa kutoka kwa
Edger ambaye amekubali
kueleza kila kitu lakini hadi
atakapomuona Olivia hivyo ni
jukumu letu kuhakikisha
tunampata Olivia.Tunakwenda
Tanzania na tutahakikisha
tunampata Olivia” akasema
Fishel
“Fishel kwa mtazamo
wangu tumetengeneza
operesheni mpya ambayo
haikuwa na
ulazima.Tungetumia nguvu
tungeweza kupata taarifa zote
kutoka kwa Edger bila
kulazimika kuingia tena katika
operesheni nyingine.Tayari
amekwisha choshwa na mateso
yale na lazima angefunguka”
akasema Ehud
“Kuna siri kubwa ambayo
Edger anaificha hapa na ndiyo
maana alikubali kurejea tena
katika kile chumba akaendelea
kuteseka kuliko kuisema na
hata kama tungetumia nguvu ya
kiasi gani asingeweza kusema
chochote.Ameteseka kwa miaka
mitatu lakini ameona ni bora
arudi tena katika mateso
akaendelee kuteseka kuliko
kusema chochote hadi
tulipomgusia Olivia ndipo
akawa tayari kufunguka.Nina
uhakika mkubwa sana
tukimleta Olivia atafunguka na
atatueleza kila kitu” akasema
Fishel
“Una uhakika atatueleza au
atakuwa anacheza na akili zetu?
“Atafunguka.Niamini mimi”
akasema Fishel
“Fishel bado moyo wangu
unakuwa mgumu sana katika
suala hili kwani litatuingiza
tena gharama za kufanya
operesheni katika nchi nyingine
na hatuna uhakika kama
tutampata Olivia kama
ulivyomuahidi Edger” akasema
Ehud
“Ehud kwa ajili ya taifa
teule la Israel kila kitu
kinawezekana.Lazima tufanye
kila linalowezekana
kuhakikisha taifa teule
linakuwa salama.Tutaingia
Tanzania na kumtafuta Olivia
tutamleta hapa ili Edger aweze
kutueleza mahala alipo Habiba
Jawad na Sayid Omar ambao
kwa kutumia fedha zao
wanaendelea kufadhili vikundi
vya wana mgambo ambavyo
vinaendesha mauaji dhidi ya
waisrael” akasema Fishel na
kutazama na Ehud kwa muda
halafu akasema
“Tuwasiliane na makao
makuu tuwajulishe kuhusu
suala hili” akasema Fishel na
kuomba waunganishwe na
makao makuu baada ya muda
mkurugenzi mkuu wa Mossad
akawa hewani
“Fishel habari za
Nairobi?Nimeambiwa mnataka
kuzungumza nami.Kuna kitu
gani kinaendelea huko?Kuna
chochote mmeshakipata kutoka
kwa yule jamaa?akauliza
mkurugenzi
“Mkurugenzi tumefika
salama kabisa Nairobi na bila
kuchelewa tumeanza kazi
iliyotuleta hapa.Tumemtoa
Edger katika chumba cha giza
na kumrejesha katika maisha
mazuri kisha tukaanza
kuhojiana naye.Alikana
kuwafahamu Habiba Jawad na
Sayid Omar na akatuomba
tumrejeshe katika chumba cha
giza akaendelee
kuteseka.Hakuwa tayari
kusema lolote hadi
tulipomuonyesha picha ya
mwanamke mmoja anaitwa
Olivia.Huyo mwanamke ni
daktari ambaye ndiye
aliyeyaokoa maisha yake kwa
kumpeleka Israel baada ya
kupewa sumu.Edger amekiri
kumpenda Olivia na ameahidi
kutueleza kila kitu tunachohitaji
kama tukimkutanisha tena na
Olivia” akasema Fishel
“Hiyo ni hatua nzuri
sana.Kama amekubali kueleza
kila kitu endapo atampata huyo
mwanamke ni jambo zuri
sana.Huyo mwanamke
anapatikana wapi?akauliza
mkurugenzi
“Mkurugenzi hapa kuna
tatizo kidogo.Huyo mwanamke
anapatikana nchini Tanzania”
“Tanzania ni karibu sana na
Kenya na tuna ubalozi wetu
pale hivyo kumpata huyo
mwanamke itakuwa kazi
nyepesi.Tutatuma timu ya watu
kwenda kumtafuta na kumleta
Nairobi.Mossad tunao utajiri
mkubwa wa majasusi mahiri”
akasema mkurugenzi
“Tatizo lililopo mkurugenzi
ni kwamba mwanamke huyo
ametekwa nyara siku mbili
zilizopita na watu wasiojulikana
na hadi leo hii bado
hajapatikana”
“Ametekwa?!!
“Ndiyo
mkurugenzi.Ametekwa nyara
na watu wasiojulikana”akajibu
Fishel
“Pamoja na kutekwa nyara
lakini bado ni mtu wa muhimu
kwetu.Edger anazo taarifa nyeti
sana tunazozihitaji hivyo ni
jukumu letu kuhakikisha
tunampata huyo
Olivia.Tutatuma majasusi
wetukwenda Tanzania
kumtafuta Olivia lakini kabla ya
kutuma kikosi cha majasusi
Tanzania ninataka wewe na
Ehud mtangulie
Tanzania.Nitatoa maelekezo
kwa balozi wetu ili muweze
kupatiwa kila msaada
mnaouhitaji mkiwa
Tanzania.Nataka mkafanye
uchunguzi wa tukio hilo la
kutekwa kwa Olivia na kisha
mnipe taarifa haraka namna
gani tunaweza kufanya yetu ya
kumtafuta na kumpata
Olivia.Naombeni mlipe uzito
suala hili muhimu
mno.Maroketi yanaendelea
kurushwa katika ardhi ya Israel
na ili kuwadhibiti wanamgambo
hao wanaofanya mashambulio
haya lazima tukate mrija
unaowaunganisha na kisima
cha fedha kwa kuwakamata
Habiba na Sayid.Tuwasiliane
mtakapofika Tanzania”
akasema mkurugenzi na kukata
simu.Fishel na Ehud
wakatazamana
“Fishel tumenunua kazi
nyingine ambayo haikuwa na
ulazima wowote.” akasema
Ehud
“Ehud nini hasa tatizo
lako?Unaonekana hujafurahia
kabisa suala la kumtafuta Olivia
ili Edger aweze kutupa taarifa
muhimu” akasema Fishel
“Ni kweli sijafurahishwa na
jambo hili.Tulikuja hapa
kumfanya Edger afunguke na
atupe taarifa zile muhimu sana
tunazozihitaji lakini
mwenzangu umekuwa mwepesi
sana kukubali matakwa
yake”akasema Ehud
“Ehud hakuna ambacho
tungekipata kwa Edger,yuko
tayari kuendelea kuteseka
kuliko kueleza chochote.Hata
kama tungetumia nguvu
kumtesa tungeweza kumuua
kabla ya kupata chochote toka
kwake kwani afya yake ni
dhaifu mno.Lakini baada ya
kumgusia kuhusu Olivia
amekubali kutueleza kila kitu
kama tukimleta Olivia,huoni
kama hayo ni mafanikio
makubwa Ehud” akasema
Fishel.
“Japokuwa mkurugenzi
ameridhia lakini binafsi
sijapendezwa na hili jambo”
akasema Ehud
“Ehud nakufahamu wewe
unapenda matumizi ya nguvu
lakini kwa hali aliyonayo Edger
hatuwezi kutumia
nguvu.Tutatumia nguvu
kumsaka Olivia na kisha
tutapata taarifa nyeti toka kwa
Edger.Haya tayari ni maelekezo
tumepewa hatuna haja ya
kuendeleza mjadala
kinachotakiwa kwa sasa ni
kuanza kujiandaa kuelekea
Tanzania.Twende tukaonane na
balozi kwa ajili ya maandalizi ya
kuelekea Tanzania” akasema
Fishel.
TANZANIA..
Hali ya Olivia Themba
iliendelea kuwa mbaya kadiri
muda ulivyozidi
kusonga.Hakuwa na fahamu.Hii
ilitokana na mateso makali
aliyopewa na Kaiza akiwa na
watu wake.Dr Alex alikuwa
amefungwa katika kiti pembeni
akishuhudia Olivia alivyokuwa
akiteswa baada ya kutokea
mzozo kati yake na Kaiza
kuhusiana na mateso aliyokuwa
akimpa Olivia.Pamoja na
jitihada zote za Kaiza lakini
hakuweza kupata chochote
kutoka kwa
Olivia.Alichanganyikiwa kwani
tayari kiza kiliingia na hakuwa
amekamilisha kazi aliyopewa
na rais.Akamgeukia Dr Alex
“Dr Alex unatakiwa ufanye
kila linalowezekana
kumuamsha Olivia.Lazima
afunguke.lazima aseme kila kitu
leo!! Akasema Kaiza kwa ukali
“Siwezi Kaiza.Siwezi
kufanya chochote
tena.Umekataa kusikia ushauri
wangu na hayo ndiyo matokeo
yake.Olivia is going to die and
you’ll get nothing !! Ungenisikia
ushauri wangu usingefika hapa
ulipofika.Sina chochote cha
kukusaidia kwa sasa.Let her
die!! Akasema Dr Alex maneno
yaliyompandisha hasira Kaiza
akamrukia Dr Alex teke zito la
kifua lililompeleka
chini.Akaenda ukutani na
kupiga ukuta kwa mikono yake
alipandwa na hasira.Akageuka
kumtazama Olivia hali yake
bado haikuwa nzuri.
“Dah ! nitafanya nini?Hali
ya Olivia ni mbaya na huyu
daktari amegoma kufanya
chochote.Lazima nitafute
msaada siwezi kumuacha Olivia
akafariki kwani ni my muhimu
sana kwetu” akawaza Kaiza
akatoka ndani ya kile chumba
na kumpigia simu Dr Evans
“Kaiza naamini tayari zoezi
limekamilika” akasema Dr Alex
mara tu alipopokea simu
“Mheshimiwa rais”akasema
Kaiza
“Nini Kaiza?akauliza Dr
Evans
“Zoezi halijafanikiwa
mheshimiwa rais.Mpaka sasa
hatujafanikiwa kupata chochote
kutoka kwa Olivia.Nimetumia
kila aina ya mateso lakini
hajafungua mdomo wake
kusema chochote na kwa bahati
mbaya hali yake imebadilika
ghafla hana fahamu nina
wasiwasi anaweza akapoteza
maisha muda wowote”
“What?! Akauliza Dr Evans
kwa mstuko
“Ndiyo mheshimiwa
rais,hali yake si nzuri hata
kidogo”
“Kaiza don’t let her die !!
Umenisikia?
“Mheshimiwa rais..”
“Sikiliza Kaiza,nimetoka
hospitali kumtazama
mwanangu Coletha na hali yake
si nzuri hata kidogo.Madaktari
wanahangaika kutafuta tiba
lakini mpaka sasa
hawajafanikiwa.Mwenye
kuifahamu tiba ya mwanangu ni
Olivia pekee ambaye ndiye
aliyetengeneza virusi
vinavyomtesa mwanangu.Kwa
namna yoyote ile Olivia
hatakiwi kufa bado namuhitaji
sana” akasema Dr Evans
“Mheshimiwa rais….”
“Kaiza sihitaji maelezo
nataka kusikia Olivia
anazinduka na anakuwa salama
tena asiendelee kupatiwa
mateso yoyote.Namuhitaji sana
kwa ajili ya uhai wa
mwanangu.Olivia akifa utakufa
naye!!
“Mheshimiwa rais
ninahitaji msaada natakiwa
kumpeleka Olivia hospitali kwa
matibabu” akasema Kaiza
“Dr Alex yuko hapo mtumie
kuhakikisha Olivia anakuwa
salama” akasema Dr Evans
“Mheshimiwa rais hata Dr
Alex mwenyewe amekiri hawezi
kufanya kitu.Olivia anatakiwa
kupelekwa
hospitali.Mheshimiwa rais kuna
kitu ambacho nadhani itakuwa
vyema ukakifahamu kuhusu Dr
Alex.Sifahamu kwa nini lakini
amekuwa mgumu sana kutoa
ushirikiano kwetu na kuna
wakati nilimkamata
akizungumza na mtu kwenye
simu kuhusu Olivia na
nilipomuhoji akadai
anamzungumzia Olivia
mwanae.Mheshimiwa rais sina
imani na huyu mtu kabisa kuna
mchezo anatuchezea” akasema
Kaiza na ukimya mfupi ukapita
halafu Dr Evans akasema
“Sikiliza Kaiza,Olivia
hatakiwi kupelekwa
hospitali.Kila mtu anafahamu
Olivia amepotea hivyo
akionekana tayari kila kitu
kitakuwa kimeharibika na
tutashindwa kupata taarifa za
muhimu.Nitakuelekeza
shambani kwangu,mtoe Olivia
hapo na utampeleka shambani
kwangu kuna nyumba kubwa
pale.Ninamtuma daktari wangu
anakwenda kule akiwa na vifaa
vyote vinavyotakiwa mtamkuta
kule na yeye ndiye atakayebeba
jukumu la kuhakikisha Olivia
anazinduka.Inaniuma kusema
hivi lakini wakati mnaondoka
hapo muue Dr Alex na watu
wake wote.Sehemu hiyo
itakuwa chini yenu.Umenielewa
Kaiza? Akauliza Dr Evans
“Nimekuelewa mheshimiwa
rais” akasema Kaiza na Dr
Evans akamueleza mahala lilipo
shamba lake na bila kupoteza
muda maandalizi ya kuondoka
mahala pale yakaanza.Dr Alex
akafunguliwa na kusaidiana na
akina Kaiza kumtoa Olivia mle
ndani na kumpakia garini.Kabla
hawajaondoka Kaiza
akamuomba Dr Alex warejee
ndani wakazungumze.
“Dr Alex imelazimu
kumuhamisha Olivia
tunampeleka hospitali.Ahsante
sana kwa msaada wako
mkubwa uliotupatia na
ninakuomba samahani kwa yale
yaliyotokea.Kuna uwezekano
tukarejea tena hapa kuendelea
na zoezi letu pale Olivia
atakapokuwa tayari”akasema
Kaiza
“Hata mimi ninashukuru
sana Kaiza.Tusahau yaliyopita
tuangalie ya mbele.Kabla
haujaondoka ninaweza kuipata
simu yangu tafadhali?akauliza
Dr Alex.Kaiza akaingiza mkono
mfukoni kama vile anaitoa simu
yake lakini kwa kasi ya ajabu
mkono wake ukaenda katika
bastora aliyokuwa
ameichomeka nyuma kiunoni
akaichomoa na kuachia risasi
mfululizo Dr Alex akaanguka
chini na hakuwa na uhai tena
Kaiza akamtazama halafu
akamtemea mate na kutoka mle
ndani.Wakati Kaiza akiwa ndani
ya ofisi vijana wake ambao
tayari alikwisha wapa
maelekezo waliwavamia wale
watu wa Dr Alex na kuwamaliza
wote Kaiza alipotoka alikuta
kazi imemalizika.
“Kila kitu tayari?akauliza
Kaiza
“Ndiyo mkuu kila kitu
tayari”
“Good.Let us go” akasema
Kaiza wakaingia katika magari
na kuondoka eneo lile kuelekea
mahala walikoelekezwa na rais
shambani kwake.