RIWAYA : SALA YA SARAH.
MTUNZI : ALEX KILEO.
SEHEMU YA SABINI. (MWISHO)
ENDELEA..................
Siku iliyofuata asubuhi, Sajenti Minja aliamkia hospitali, kuna kitu alikuwa anakihisi, ndio maana baada ya kuuangalia mwili wa Sarah siku iliyopita, alicheka ingawa aliongea maneno mazito.
Sajenti Minja alifika hospitali na kuonana na Daktari, bahati nzuri daktari wa zamu siku hiyo alikuwa ni Dokta Pendo, wakasalimiana,
"mmeshafanyia uchunguzi huo mwili wa Sarah?" Sajenti Minja alimuuliza Dokta Pendo,
"tayari, kila kitu kipo kwenye ripoti, ipo ofisi ya Dokta mkuu" Dokta Pendo alijibu, ila kilichomshangaza Sajenti Minja ni kuona Dokta hana hata uchungu wakati aliekufa ni rafiki yake.
Sajenti Minja akaelekea ofisi ya Dokta mkuu na kuchukua ripoti ya ya mwili wa Sarah, kisha akaondoka huku akiwa hana imani na ule mwili unaosemekana ni wa Sarah,.
Wakati Sajenti Minja akiwa anatoka, alisikia akiitwa kwa nyuma, alipogeuka alikutana na dokta Pendo,
"samahani, una namba ya Vin?" Dokta Pendo alimuuliza Sajenti Minja,
"ndio" Sajenti Minja alijibu,
"naomba unipatie" Dokta Pendo aliongea na kisha Sajenti Minja akatoa simu na kumsomea Dokta Pendo zile namba za Vin, Dokta Pendo akanakiri kwenye simu yake na kisha Sajenti Minja akaondoka huku akiwa na wasiwasi sana juu ya mwili wa Sarah.
Dokta Pendo baada ya kuridhika kuwa Sajenti Minja ameshaondoka eneo lile, aliipiga ile namba ambayo alipewa na Sajenti Minja, simu ikaanza kuita,
"hallow, naongea na Vin?" Dokta Pendo aliuliza baada ya simu kupokelewa,
"yeah, ndo mimi" Vin alijibu kwa sauti ya upole,
"unaweza kuonana na mimi leo?" Dokta Pendo aliuliza,
"wewe ni nani kwanza?" Vin aliuliza,
,
"ooh, kumbe sijajitambulisha? Mimi ni Dokta wa hii hospitali hapa yenye mwili wa dada yako Sarah" Dokta Pendo aliongea,
"kuna nini?" Vin aliuliza,
"tuonane kwanza, utajua tu" Dokta Pendo aliongea,
"nitakuja baadae hapo hospitali" Vin aliongea,
"hapana, sitaki tukutane hospitali, njoo kanisa kuu la roman, mjini nitakuwepo hapo saa moja jioni, ukifika ingia moja kwa moja ndani ya kanisa" Dokta Pendo alitoa maelezo,
"kwanini kanisani?" Vin aliuliza,
"nahitaji tukae eneo lenye amani ili tuongee vizuri" Dokta Pendo aliongea,
"sawa, nitakuja" Vin aliongea na kukata simu, kisha Dokta Pendo akashusha pumzi ndefu na kuirudisha simu mfukoni. Kisha akaenda kuendelea na kazi.
**************
Sajenti Minja aliibeba ile report mpaka ofisini kwa mkuu wake, mkuu wa polisi akaifungua ile report na kuanza kuisoma, aliisoma kwa muda wa dakika ishirini kisha akavua miwani na ile report akairudisha kwenye bahasha.
"ujue huyu mwanamke hajaua polisi watatu pekee?" Mkuu wa polisi aliongea huku akimtazama Sajenti Minja,
"kuna wengine tena?" Sajenti Minja aliuliza,
"kule ambapo kuna mlango wa nyuma, tumekuta polisi wote wamekufa, na pia kulikuwa na michirizi ya damu iliyoenea mpaka juu ya ukuta" Mkuu wa polisi aliongea,
"hapo una maana gani?" Sajenti Minja aliuliza,
"inawezekana watekaji walikuwa wawili, ila mmoja ametoroka" Mkuu wa polisi aliongea na kumfanya Sajenti Minja aanze kuziamini hisia zake juu ya ule wa Sarah,
"kwa hiyo unataka kusema tumtafute huyo mtekaji tena?" Sajenti Minja aliuliza,
"tena hiyo kazi ifanyike usiri mkubwa, yaani ni mimi na wewe, hatakiwi mtu mwingine kujua hii habari" Mkuu wa polisi aliongea,
"sawa mkuu" Sajenti Minja aliongea, kisha mkuu wa polisi akainuka na kutoka nje ya ofisi na kumuacha Sajenti Minja akicheka peke yake.
Sajenti Minja alikaa kwenye ile ofisi kama dakika tano hivi, kisha akainuka na kuelekea nje, akaingia kwenye gari na kurudi hospitali, safari hii alirudi kama mpelelezi, sio kama mtu aliyefuata report.
Sajenti Minja baada ya kufika eneo la hospital, aliingia ndani ya jengo na lengo lake kubwa lilikuwa ni kutaka kujua kama Dokta Pendo bado yupo hapo..
Baada ya Sajenti Minja kukagua kama dakika kumi, aliweza kugundua kuwa Dokta Pendo bado yupo. Sajenti Minja akatoka nje na kuingia kwenye gari lake, kisha akachukua gazeti na kuanza kusoma, kila mtu aliyekuwa anatoka ndani ya jengo la hospitali, Sajenti Minja alikuwa akimuangalia.
Baada ya masaa matato, Sajenti Minja alimshuhudia Dokta Pendo akitoka, kisha Dokta Pendo akaingia kwenye gari dogo na kuondoka, Sajenti Minja akaanza kuifuatilia ile gari.
Dokta Pendo aliendesha gari bila kufahamu kama anafuatiliwa, gari ilienda mpaka kwenye nyumba ya Sarah, kisha Dokta Pendo akatelemka na kuingia ndani ya geti.
Sajenti Minja kama kawaida yake akaegesha gari kwa mbali na kusubiri huku akijiwekea muda kuwa baada ya saa kadhaa atatelemka na kwenda kuchunguza kwa umakini zaidi.
Saa la kwanza likaisha, saa la pili likakatika, la tatu pia. Saa la nne likiwa mwishoni bila kuona mtu akiingia wala kutoka, Sajenti Minja akafungua mlango ili atoke, ila kabla hajashusha hata mguu, alishuhudia geti la nyumba ya Sarah likifunguliwa, Sajenti Minja ikambidi afunge mlango wa gari na kutupa macho getini kuona nani anaetoka.
Alimshuhudia Dokta Pendo akitoka huku akiwa ameongozana na babu yake Sarah, walionekana wakiongea na kucheka kwa furaha, ila Sajenti Minja hakuweza kujua wanachoongea kwa kuwa alikuwa mbali,
"Sarah amekufa kweli? Mbona wanaongea na kufurahi?" Sajenti Minja alijiuliza huku akiiangalia gari waliyopanda Dokta Pendo na babu yake, ile gari iligeuzwa na kisha ikawa inaondoka kuelekea upande aliopo Sajenti Minja, Sajenti Minja kuona hivyo, akalala kwenye siti ili wasimuone, ile gari ikapita na kisha Sajenti Minja akawasha gari yake na kuigeuza, akaanza tena kuifuatilia ile gari.
****************
Mishale ya saa moja usiku, Vin alitelemka Katika gari nje ya kanisa, kisha kwa hatua za haraka akawa anaelekea ndani ya kanisa, alifika na kuingia ndani, kisha akasimama nyuma ya kanisa na kuangaza macho, hakuweza kumuona mtu mwingine isipokuwa mwanamke mmoja aliyekuwa akibandua karatasi sehemu tofauti ndani ya kanisa, alikuwa akibandua kwa kufuata mstari kwa maana karatasi zilikuwa nyingi, Vin akatupa jicho kwenye karatasi moja iliyopo pembeni yake, ilionekana kufanana na zile karatasi zinazoondolewa na yule mwanamke.
Vin akatupia jicho ile karatasi na kuisoma,
"eee Mungu naomba nikiwa mkubwa niwe nawaka kama moto"
"sala hii iliombwa na mtoto mdogo aitwae Sarah Isack mnamo tarehe //-//-//"
Vin akajikuta anashangaa na kumtupia jicho yule mwanamke, kisha yule mwanamke nae akamtupia jicho Vin, Vin akazidi kushangaa kwa maana yule mwanamke alikuwa ni Aisha,
"itoe hiyo karatasi na uje nayo huku" Aisha aliongea na kugeuka kisha akaelekea benchi la mbele na kukaa.
Vin akaitoa ile karatasi na kwenda nayo moja kwa moja mpaka alipokaa Aisha na kisha akampatia ile karatasi,
"Mimi ndiye niliyetaka uje hapa, Kaa hapo" Aisha aliongea na kumfanya Vin ashangae,
"kuna nini?" Vin aliuliza huku akikaa,
"pole kwa msiba wa baba yako, nadhani umeumia sana kwa hilo" Aisha aliongea kwa huzuni,
"uchungu lazima uwepo, nimeumia kwa kweli, ila sina chuki dhidi ya dada yangu Sarah, ingawa amefanya hayo yote, ila nimeumia sana kwa namna alivyokufa, sikutaka afe, niliamini yeye ni mtu pekee mwenye upendo wa dhati kwangu" Vin aliongea kwa hisia,
"ile siku ya hilo tukio hata mimi nilifanikiwa kuingia ndani ya ule moto kuja kumuokoa sarah" Aisha aliongea na kumfanya Vin ashangae,
"kwanini hukumuokoa sasa?" Vin aliuliza kwa pupa,
"ilikuwa hivi, siku ile nilifika pale nikiwa na mtoto wa Trigger, tutakuta askari wamejaa mpaka kule nyuma ya nyumba, sasa itabidi tupambane nao, mimi na mtoto wa Trigger tukafanimiwa kuingia ndani, tukakuta Sarah ameshapigwa risasi tatu, tukambeba ili tutoke nae, tukakuta kule nyuma askari wengine wameongezeka, ikabidi tumuweke Sarah chini kwa maana alikuwa yupo kwenye hali mbaya, kisha mimi na mtoto wa Trigger tukaanza kupambana, mwisho askari tukawapunguza, tukakubaliana mimi nimbebe Sarah kisha mtoto wa Trigger atanilinda kwa kuendelea kuwapiga risasi askari wachache waliobaki.
Ila mtoto wa Trigger akasema njia rahisi zaidi ya kumsaidia Sarah baada ya kutoka, ni yeye mtoto wa Trigger kujisalimisha kwa maana polisi hawatoendelea kumtafuta Sarah kwa maana tulikuwa na wasiwasi huenda polisi wetakuwa wamewekwa njia zote za mtaa ule, basi tukakubaliana hivyo na kisha kile kinyago cha Sarah na mkufu nikampatia yule binti, kisha nikambeba Sarah na kutoka nae nje huku yule binti akipambana na askari kadhaa ambao wangeniletea madhara.
Nikafanikiwa kutoka na Sarah na kisha nikampeleka kwenye gari huku nikiwa na imani yule binti wa Trigger atakuwa amejisalimisha na nikapanga nitaenda kumuokoa usiku mkubwa, ila nikashangaa kusikia wanajeshi wamemuua yule binti" Aisha alimaliza kuongea kwa huzuni,
"kwa hiyo Sarah yupo hai?" Vin aliuliza,
"Sarah yupo" Aisha aliongea na kumfanya Vin apate furaha upya,
"yupo wapi?" Vin aliuliza,
"kabla sijakujibu, Sarah ameniagiza kuwa huo mwili wa huyo binti wa Trigger, uchukue na uuzike kwa heshima, jina la huyo binti anaitwa Sarah, hilo ni jina alilopewa na Taita, ni jina la bibi yao Taita, bibi yao Taita ndio aliowazaa baba yake Taita na mama yenu aliyeitwa Margret" Aisha aliongea,
"nitafanya hivyo, je Sarah yupo wapi?" Vin aliuliza,
"twende nikupeleke" Aisha huku Akiinuka na zile karatasi, Aisha akaelekea moja kwa moja mpaka kwenye shimo la taka na kuzitupa zile karatasi na kisha akazichoma moto, baada ya hapo akaingia kwenye gari la Vin na wakaanza safari, walikuwa wanaenda Kiwanja cha ndege.
Vin ilimbidi aendeshe gari kwa mwendo mkali ili kuiwahi ndege, walifika uwanjani na kisha wakatelemka na kuingia ndani ya jengo, kwa mbali Vin aliweza kumuona Sarah akiwa anaongea na dokta Pendo na mzee asiyemfahamu, Vin ikambidi akimbie kumuwahi Sarah, alipomfikia alimkumbatia kwa hisia,
"nakupenda sana Sarah" Vin aliongea kwa hisia huku akitokwa na machozi,
"nakupenda sana Sebastian isack" Sarah alijibu huku pia machozi yakimtoka, kisha wakaachiana na Sarah akamtambulisha Vin kwa babu yao, basi furaha ikaongezeka maradufu,
"ila huyu mzee naenda nae uingereza, atarudi baada ya miezi miwili" Sarah alimwambia Vin,
"na mimi nitakuja huko kwa ajili yako, nahitaji muda wa kukaa pamoja na nyinyi, baada ya wiki mbili nitakuja" Vin aliongea na wakati tangazo lilisikika likiwataka abiria wanaoenda uingereza kupitia Kenya waende wakafanyiwe ukaguzi ili waingie kwenye ndege, Sarah na babu yake wakaagana na watu pale, kisha Sarah akamsogelea Aisha,
"kuna gari range Rover nyeusi, Dokta Pendo atakupatia utembelee, alafu Vin akija uingereza, uje naye" Sarah aliongea huku akiwa amemkumbatia Aisha,
"usijali" Aisha alijibu huku akitabasamu.
Baada ya lisaa limoja, ndege aliyopanda Sarah iliruka na kuiacha ardhi ya Tanzania.
Vin, Aisha na Dokta Pendo wakatoka nje, kisha Vin akaagana nao na kuingia ndani ya gari na kuondoka, pia Aisha na Dokta Pendo wakaingia kwenye gari lao na wakaondoka.
Pale kwenye uwanja wa ndege kulikuwa na mwanaume akiyafuatilia yale matukio kwa umakini mkubwa, alikuwa ni Sajenti Minja, baada ya kila mtu kuondoka eneo lile Sajenti Minja alitabasamu na kuwasha gari yake,
"hakuna cha kufuatilia, Sarah kaondoka na mambo yamefika mwisho" Sajenti Minja aliongea na kuiondoa gari yake kuelekea upande tofauti kabisa na ule walioondokea wakina Aisha.
***********MWISHO************
the Legend☆