Riwaya: Sala ya Sarah

41

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Asante sana the legend.nitammiss Sarah Ana ni remind na peniella ila tofauti ya Sarah sio mtu wa mabwana
 
Asante sana the legend.nitammiss Sarah Ana ni remind na peniella ila tofauti ya Sarah sio mtu wa mabwana
Kakudanganya Nani?
Sarah ana Babu wa kizungu nduguye na boss wa marehemu Isaack so why hashobokei ngozi nyeusi japokuwa yule mchaga Domo zege anamtaka
 
RIWAYA : SALA YA SARAH

MTUNZI : ALEX KILEO

SEHEMU YA SITINI NA TANO.

ENDELEA..................

"weka silaha chini" Sajenti Minja aliongea kwa ukali huku akimuangalia Vin, Vin akaweka silaha chini huku akitabasamu, maana alikamatwa na ushahidi kabisa.

"ongoza mbele" Sajenti Minja aliongea kwa amri na kufanya Vin aanze kupiga hatua huku akiwa bado anatabasamu, tabasamu la mshangao kutokana na tukio lililotokea ghafla. Wakati Vin akitaka kuanza kupiga hatua, Daktari Aliyepigwa risasi alimshika mkono,

"kumbe hajafa?" Vin aliuliza kwa mshangao huku akimuangalia,

"majibu ya vipimo vyako yapo ndani ya ofisi yangu" Daktari aliongea kwa tabu huku akiwa anatoka damu puani na mdomoni,

"Dokta mimi ndiye niliyekupiga risasi?" Vin alimuuliza huku akiwa amemuinamia, Daktari akatingisha kichwa kwa maana ya kukataa, Sajenti Minja akampiga kikumbo Vin na kusogea karibu na Daktari,

"unamjua huyu?" Sajenti Minja aliuliza huku akimuonesha picha ya Trigger, Daktari akaitikia kwa kichwa kumaanisha anamjua,

"huyu ndiye aliyekupiga risasi mwanzo?" Sajenti Minja aliuliza na Daktari alitingisha kichwa na kujibu ndio,

"ndio huyo huyo amempiga na sasa hivi" Vin aliongea kwa sauti,

.

"eti ni kweli?" Sajenti Minja aliuliza na Daktari akakubali kwa kutikisa kichwa na kumfanya Vin ashukuru Mungu kwa kumuepusha na balaa lile,

"huyo mtu alikuwepo humu?" Sajenti Minja aliuliza tena ila daktari hakujibu tena, mwili ulikakamaa na kisha akatema damu nyingi kwa mkupuo na kukilaza kichwa chake pembeni, kwa maana hiyo daktari alikuwa amekufa,

"sogeeni tutoe huduma" Dokta mwingine aliwapangua wakina Sajenti Minja na kisha akamsogelea yule daktari aliyekufa na kuanza kusikiliza mapigo yake ya moyo, hakutaka kuamini kirahisi kama mwenzake amekufa.

"wewe twende" Sajenti Minja aliongea kibabe huku akimvuta Vin,

"unanipeleka wapi sasa wakati daktari amesema mimi sijampiga risasi?" Vin aliuliza kijeuri,

"wewe twende, una kesi nyingi za kujibu ukiitoa hii ya kumshambulia daktari kwa risasi" Sajenti Minja aliongea na kumsukuma mbele Vin,

"sawa, basi ngoja nipewe majibu yangu, si umemsikia daktari amesema yapo ofisini kwake" Vin aliongea huku akimtazama Sajenti Minja,

"we dada, ebu njoo" Sajenti Minja alimuita dada wa mapokezi,

"abee" Dada wa mapokezi aliitikia baada ya kufika, alikuwa ni lydia,

"ingia kwenye ofisi ya yule daktari aliyepigwa risasi, kuna cheti cha mtu nakihitaji, wewe jina nani?" Sajenti Minja aliongea kisha akamgeukia Vin,

"Vin Denis, kama yatakuwa yapo ndani ya bahasha, basi juu ya bahasha kutakuwa kumeandikwa "DNA TEST, Vin Denis and Sarah isack" Vin aliongea,

"wewe umejuaje yameandikwa hayo yote, kama sio lenu moja kati yako na yule aliyempiga risasi daktari?" Sajenti Minja aliuliza huku akimuangalia Vin,

"mara nyingi hospitali nyingi duniani uwa zinatumia mfumo huo" Vin alijibu,

"wewe kama utayapata majibu au utayakosa uje nje unipe taharifa" Sajenti Minja alimwambia lydia,

"sawa" lydia alijibu huku akielekea ofisini kwa Dokta mkuu kwenda kumuomba ruhusa ya kuingia kwenye ofisi ya daktari aliyepigwa risasi.

Sajenti Minja akatoka na Vin mpaka nje na kumpakia kwenye gari, kisha akawa anamsubiria dada wa mapokezi.

Baada ya dakika kumi na tano dada wa mapokezi aliwafuata na kuwapatia bahasha ya kaki yenye majibu ya vipimo vya Vin, Vin akatabasamu,

"nipe, ni majibu yangu hayo na wala sio yako" Vin aliongea baada ya kumuona Sajenti Minja akiyapokea na kuyaweka pembeni yake. Sajenti Minja hakutaka kujibu kitu, aliwasha gari na kuiondoa.

Walifika mpaka kituo cha polisi, na kisha wakashuka wakawa wanaelekea ndani,

"koplo Rama anaendeleaje?" Sajenti Minja alimuuliza askari aliyekuwepo kaunta, alimuulizia yule askari aliyekanyaga bomu na kupoteza fahamu.

"imebidi apelekwe hospitali, inaonekana presha inamsumbua" Askari aliyeulizwa alijibu na kumfanya Sajenti Minja aelekee ofisini kwake huku akitabasamu.

Sajenti Minja aliingia ofisini kwake na kupanga vitu vizuri kutokana na purukushani ya Bomu feki la Aisha, baada ya hapo akakaa kwenye kiti,

"kuna maswali machache nataka unijibu kwa ufasaha zaidi ili urudi uraiani" Sajenti Minja aliongea huku akimtazama usoni Vin,

"nitajibu ninavyojua, sasa wewe ndio utajua nimejibu kwa ufasaha au lah!" Vin aliongea huku nae pia akimuangalia usoni Sajenti Minja,

"sawa, je unaweza kunionesha kibali cha umiliki wa silaha yako?" Sajenti Minja aliuliza,

"ninavyo vibali, vipo nyumbani" Vin alijibu,

"swali la pili, huyu mtu aliyempiga risasi daktari, jana tu nimemkuta upo nae kwenu, wewe na Taita, kwa maana hiyo ni lazima kuna kitu mnakijua juu ya hilo tukio alilolifanya" Sajenti Minja aliongea,

"nadhani naweza nikawa najua, ila kwa hisia tu" Vin alijibu,

"nieleze unachokijua" Sajenti Minja aliongea,

"ni hayo majibu ya hospitali, nadhani hakutaka niyapate hayo majibu ya hospitali kutokana na sababu nisizozijua" Vin aliongea,

"siku ile kwenye kifo cha familia ya Harry, mlinzi alikuona na wewe ukiingia nyumbani kwa Harry kabla familia ya Harry haijauawa, mimi napenda nikuweke hatihani kutokana na vifo hivyo" Sajenti Minja alimueleza Vin,

"ni kweli nilionekana, ila sikuua mtu" Vin aliongea,

"Sarah ni nani yako?" Sajenti Minja huku akimuangalia,

"Sarah sikuwa namjua wala sikuwahi kumjua, ila inasemekana ni ndugu yangu wa damu" Vin alijibu,

"kwanini useme humjui, alafu useme inasemekana, kwani hamjawahi kukua pamoja?" Sajenti Minja aliuliza,

"bado nasema inasemekana kwa maana inadaiwa wakati mdogo nilifutwa kumbukumbu zangu na nikaanza upya" Vin alijibu,

"hiyo haiwezekani, mtu kufutwa kumbukumbu?" Sajenti Minja alibisha huku akicheka,

"hata mimi iliniwia vigumu kuelewa hilo jambo, ila nilielewa baadae nilipokutana na Daktari aliyefanya hilo jambo" Vin alimueleza Sajenti Minja,

"hilo jambo lilifanyika katika hospitali za hapa nchini?" Sajenti Minja aliuliza,

"ndio, uzuri ni kuwa hata daktari wake bado yupo hai ingawa jambo hilo lilifanyika zamani sana" Vin alijibu

"mwaka gani?" Sajenti Minja aliuliza,

"miaka ishirini iliyopita, inasemekana baada ya nyumba yetu kuchomwa moto na wazazi kufariki" Vin alijibu, na kufanya Sajenti Minja aikumbuke ile report iliyofungwa mara baada ya askari aliyekuwa akiifuatilia ila kesi ya nyumba ya baba yake Sarah kuuawa, ile report iliandikwa miili iliyopatikana imeteketea kwa moto ni mitatu, yaani wa baba yake Sarah, mama yake Sarah na mfanyakazi wa ndani, huku mwili wa mtoto wa kike aitwae Sarah ulikutwa nje ya nyumba, na mwili mmoja wa mtoto wa kiume hakuonekana,

"wewe ni Sebastian?" Sajenti Minja aliuliza,

"Sarah uwa ananiita hivyo, ila mimi naitwa Vin" Vin alijibu na kumfanya Sajenti Minja achukue ile bahasha yenye majibu ya vipimo vya DNA na kuifungua, kisha akaanza kusoma taratibu, ilimchukua dakika tano kuisoma kisha akamtupia jicho Vin,

"ulisema daktari aliyekufuta kumbukumbu yupo, anakaa wapi?" Sajenti Minja aliuliza ila safari kwa upole zaidi na kumfanya Vin ashangae, kisha Vin akamuelekeza Sajenti Minja,

"hivi unajua ugomvi wa Sarah na Taita ni ugomvi wa kisasi baada ya wazazi wa Sarah kuuliwa na Taita?" Sajenti Minja alimuuliza Vin,

"ndio" Vin alijibu,

"utafanyaje ukigundua kuwa Taita sio baba yako ila aliwaua wazazi wako?" Sajenti Minja aliuliza,

"siwezi kufanya kitu, kwa maana siwajui wazazi wangu, Taita ndio mzazi wangu" Vin alijibu,

"sawa, nenda, ila uje kesho ukiwa na nyaraka za umiliki wa silaha uliyonayo" Sajenti Minja aliongea na kumfanya Vin ajisachi, kisha akatoa kitambulisho na kukitupa juu ya meza ya Sajenti Minja, Sajenti Minja akakiokota na kukiangalia, akashtuka,

"nitakutafuta nitapokuhitaji"Sajenti Minja aliongea huku akimrudishia kitambulisho,

"naomba na majibu yangu ya hospitali" Vin aliongea kwa upole kisha Sajenti Minja akaichukua ile bahasha na kumpatia,

"kafungulie nje, nataka kutoka" Sajenti Minja aliongea baada ya kuona Vin anataka kutoa karatasi iliyopo ndani ya bahasha.

Vin akatabasamu na kutoka nje huku Sajenti Minja nae akiwa kwa nyuma yake, Sajenti Minja alipanga kuelekea kwa Dokta Innocent Malle muda huo, alikuwa anataka kwenda kumuhoji kutokana na maelezo ya Vin.

*****************

Trigger alivyotoka hospitali alirudi nyumbani kwa Taita na kumkuta akiwa sebuleni,

"umefanikisha?" Taita alimuuliza Trigger,

"kazi imefanyika, ila Vin yupo hatarini" Trigger aliongea,

"yupo hatarini kivipi?" Taita aliuliza huku akionekana kushtuka,

"wakati nampiga daktari risasi, Vin alikuwa katika chumba cha daktari, na isitoshe polisi walikuwa eneo hilo" Trigger alijibu,

"umekosea sana, je Vin amekuona?" Taita alimuuliza,

"ameniona ndio" Trigger alijibu,

"umekosea Trigger, sasa atakufikiriaje?" Taita aliuliza kwa kulalamika,

"kama kutufikiria vibaya mbona tayari ameshatufikiria vibaya, muda wote wanaongea na Sarah, wanasaliana, unadhani wanaongea nini kama sio kutumaliza, huoni hata Sarah hatusumbuhi siku hizi? itakuwa kuna mipango wanaipanga na ikikamilika watatudhuru" Trigger aliongea,

"Vin hawezi kunifanyia hivyo" Taita aliongea kwa kujiamini,

"ulijua ipo siku hatokuamini wewe kama baba yake na akaamua kwenda kupima ili apate ukweli, usimuamini mtoto asiekuwa wako, maana anakugeuka muda wowote" Trigger aliongea na kumfanya Taita afikiri kidogo,

"basi nitamwambia arudi marekani akaendelee na mambo yake" Taita aliongea,

"mzee Vin ni wa kuuawa tu, maana ukweli ameshaanza kuujua ukweli kuhusu kifo cha wazazi wake" Trigger aliongea,

"siwezi kumuua vin" Taita alijibu huku akitabasamu,

"mzee utakurupuka kukiwa kumekucha, elewa pia jana Vin alikuwa kwa Dokta Malle" Trigger aliongea na kumfanya Taita ashtuke,

"alienda kufanya nini?" Taita aliuliza kwa hofu,

"sijui kilichoongelewa, ila wewe unadhani wataongelea nini kama sio habari zile zile za miaka ishirini iliyopita?" Trigger aliuliza,

"wewe umejuaje Vin alienda kwa Dokta Malle siku iliyopita?" Taita aliuliza,

"nilimfuatilia jana kwa kila hatua, maana hata Strategic nakosa imani nae" Trigger alijibu,

"basi nenda kwa Dokta ukamuohoji Vin alifuata nini pale?" Taita alimuagiza Trigger,

"sawa" Trigger alijibu na kuondoka huku akiwa na hasira.

******************

Sajenti Minja hakupata tabu kuipata nyumba ya Dokta Innocent Malle kwa maana Sajenti Minja aliujua mji vizuri.

Sajenti Minja alifika na kuiegesha gari yake nje ya nyumba ya Dokta Innocent Malle, kisha akabonyeza kengele, baada ya dakika moja yule kijana aliyewapokea wakina Vin siku iliyopita alienda na kufungua geti,

"habari yako? Dokta nimemkuta?" Sajenti Minja aliuliza,

"yupo, karibu" Kijana aliongea huku akiacha nafasi Sajenti Minja apite, Sajenti Minja akaingia ndani ya geti na kumkuta Dokta Innocent Malle akiwa amekaa kwenye viti vya nje akinywa kahawa, Sajenti Minja alimsalimu,

"mzee mimi ni polisi, kuna maswali kidogo naomba unisaidie kujibu" Sajenti Minja aliongea huku akiweka kitambulisho juu ya meza kisha Dokta Innocent Malle akakichukua na kukikagua na mwisho akaridhika kuwa Sajenti Minja ni polisi kweli,

"mimina Kahawa kwanza alafu ndio tuendelee kuulizana" Dokta Innocent Malle aliongea huku akitabasamu, kisha Sajenti Minja akamimina kahawa kwenye kikombe na kugida fundo moja,

"mzee naomba unisaidie kueleza tukio la mtoto aliyeletwa kwako kufutwa kumbukumbu, hilo tukio lilitokea miaka ishirini iliyopita" Sajenti Minja aliuliza na kumuangalia Dokta Innocent Malle,

"kweli mmeamua, jana tu huyo mtoto alikuja hapa kuniuliza, hama kweli ukweli haufichiki, hata uhufiche miaka Mia, ipo siku utajitokeza tu" Dokta Innocent Malle aliongea na kisha akaelezea mkasa mzima ulivyokuwa, hakuficha kitu,

"huyo kijana mweupe mwenye michoro mwilini uliyemtaja kama kijana wa kazi wa Taita, amefanana na huyu?" Sajenti Minja alimuuliza Dokta Innocent Malle huku akimuonesha picha ya Trigger iliyokuwa kwenye simu ya yake,

"ndio huyu haswa, ingawa hapa anaonekana mtu mzima kidogo" Dokta Innocent Malle aliongea huku akiiangalia ile picha,

"hii picha nimeipiga leo, nilikuwa kwa Taita nafuatilia ile kesi yake ya kutekwa na kutupwa" Sajenti Minja aliongea,

"sasa mbona juu ya hiyo picha umeandika muuaji?" Dokta Innocent Malle aliuliza,

"choo kipo wapi, nikitoka chooni nitakujibu hilo swali, hapa haja ndogo imenishika kidogo kutokana na kahawa" Sajenti Minja aliuliza na yule kijana akamuelekeza Sajenti Minja akaelekea chooni.

Kipindi Sajenti Minja akiwa chooni ndicho kipindi ambacho Trigger alikuwa anaingia kwa Dokta Innocent Malle. Trigger aliingia na kukaa kwenye kiti kile kile alichokalia Sajenti Minja, kisha akamsalimia Dokta Innocent Malle,

"bado upo imara, ni muda sana tangu tuonane" Trigger aliongea huku akitabasamu,

"siku mbili hizi mmenikumbuka, jana kaja Vin, leo wewe" Dokta Innocent Malle aliongea huku akitabasamu,

"na kilichonileta ni suala hilo hilo la Vin" Trigger aliongea,

"ebu hama kwenye hicho kiti, kuna kijana mmoja polisi ndio amekaa hapo, ameingia uwani, nae amekuja kwa masuala hayo hayo ya Vin," Dokta Innocent Malle aliongea na kumfanya Trigger ashtuke na kuitupia jicho simu ya Sajenti Minja iliyokuwepo mbele yake na kuiona picha yake ya ikiwa na maandishi " MUUAJI" Trigger akashtuka zaidi,

"yuko wapi polisi mwenyewe?" Trigger aliuliza huku akiibeba simu ya Sajenti Minja,

"ameelekea uko nyuma, chooni" Dokta Innocent Malle alijibu na wakati huo Sajenti Minja alikuwa akirejea, Sajenti Minja alipotokezea akamuona Trigger akiwa ameshika simu yake, Sajenti Minja akashtuka na kusimama, kitendo chake cha kusimama tu ghafla, Trigger akatoa bastola na kumnyooshea,

"kumbe ulivyokuwa pale kwa Taita hukumfuata yeye ila ulinifuata mimi?" Trigger aliuliza huku bastola yake ikimuangalia Sajenti Minja,

"kwanini unasema hivyo?" Sajenti Minja aliuliza huku akiwa anajua kabisa kuwa Trigger ameiona picha yake kwenye simu yake yeye Sajenti Minja, na kipindi hicho Dokta Innocent Malle na mwanaye walikuwa wamepigwa na butwaa huku wakiwa hawajui la kufanya,

"hii picha umenipiga leo maana hata nguo nilizovaa ni hizi hizi, alafu unajifanya ulimfuata Taita" Trigger aliongea huku akionesha ana hasira,

"telemsha bastola basi nikueleze vizuri" Sajenti Minja aliongea huku huku akiweka tabasamu la bandia na kumfanya Trigger pia atabasamu,

"Trigger uwa hashushi silaha mpaka itoe risasi" Trigger aliongea huku akiendelea kutabasamu na kuikoki bastola yake, Sajenti Minja akashtuka,

"una maana gani kusema hivyo?" Sajenti Minja aliuliza huku akitetemeka, ila Trigger hakujibu, akamfyatulia risasi Sajenti Minja, Sajenti Minja akatupwa chini na kunyooka kama mti mkavu, Dokta Innocent Malle na mwanae wakabaki wameshika midomo kwa mshangao,



"hiyo ndio maana yangu" Trigger aliongea huku akimuangalia Dokta Innocent Malle na pia akitabasamu............

***********ITAENDELEA*************

the Legend☆
 
RIWAYA : SALA YA SARAH

MTUNZI : ALEX KILEO

SEHEMU YA SITINI NA SITA.

ENDELEA..................

"kumbe hili jambo sio jepesi kama nilivyodhani?" Dokta Innocent Malle aliongea huku akimuangalia Sajenti Minja aliyekuwa amelala sakafuni,

"ili nisilete madhara makubwa zaidi, naombeni tuondoke wote kama mlivyo" Trigger aliongea huku akimtazama Dokta Innocent Malle,

"tuondoke twende wapi?" Kijana wa Dokta Innocent Malle aliuliza kwa ukali,

"usibishane na mtu ambaye ana silaha moto" Dokta Innocent Malle alimuonya kijana wake,

"simameni na mfanye nitakacho mimi" Trigger aliongea kwa mamlaka kisha Dokta Innocent Malle na Kijana wake wakasimama,

"ila ulikuja kwa lengo la kutaka kujua nilichoongea na Vin?" Dokta Innocent Malle aliuliza,

"mzee sitaki maswali, tii nilichosema kabla sijatumia risasi nyingine" Trigger aliongea huku akimuangalia Sajenti Minja aliyekuwa anainuka huku akiwa na damu nyingi begani, Trigger akamkimbilia na kuichomoa bastola ya Sajenti Minja iliyokuwepo kiunoni,

"naona leo umeamua kuonesha uhodari wako wa kuua?" Sajenti Minja alimuuliza huku akitabasamu,

"sijakuua bado, ila hilo linaweza kutokea saa zijazo" Trigger aliongea huku akimsukuma Sajenti Minja. Kisha Trigger akatoka nao mpaka nje alipoegesha gari yake,

"we dogo Kaa upande wa dereva, mzee utakaa nyuma pamoja na mimi, wewe mwela utakaa mbele na dogo" Trigger aliongea na kisha watu wakafanya kama Trigger alivyoagiza,

"utaendesha gari kulingana na maelezo yangu, usipofuata maelezo utakuwa umeniruhusu nikuue" Trigger aliongea huku akiwa ameikamata bastola yake vyema, ila hakumuelewa hakumuelekezea mtu.

Yule kijana aliendesha gari huku kukiwa na ukimya wa kutosha baina ya mateka, sauti iliyosikika ni ya Trigger tu, ilikuwa ni sauti ya maelekezo iliyoambatanishwa na vitisho.

Ile gari iliingia moja kwa moja kwenye nyumba moja ambayo ndiyo kambi ya Taita, ila kipindi hiki haikuwa na walinzi kama zamani, nyumba ilikuwa na mlinzi mmoja tu wa getini.

Baada ya gari kuingia, wa kwanza kushuka alikuwa Trigger, kisha na wengine wakashuka, walielekea moja kwa moja mpaka nyuma ya ile nyumba ha kukuta kuna viti vitatu vikiwa vimeizunguka meza moja na pembeni ya vile viti kulikuwa na nguzo za chuma kama tano zilizochimbiwa chini na kulikuwa na kamba zimezungushiwa kwenye hizo nguoo,

"wafunge kila mmoja na nguzo yake" Trigger alimwambia Sarah yule kijana waliyemkuta getini, yule kijana akaanza na Sajenti Minja kumfunga, kisha akamalizia na wengine,

"wewe rudi getini, hakikisha mtu yoyote haingii humu, isipokuwa Taita tu" Trigger aliongea kwa kumsisitizo,

"haina shida mkuu" Kijana alijibu huku akiondoka na kumuacha Trigger na mateka wake.

"sasa tunaweza kuendelea, naanza na wewe askari, kwanini unanitafuta mimi?" Trigger aliuliza huku akivuta kiti na kukikalia mbele ya Sajenti Minja,

"sikuwa nakutafuta, kama ningekuwa nakutafuta ningeshakukamata" Sajenti Minja alijibu,

"unanituhumu kwa mauaji, nimemuua nani?" Trigger aliuliza swali la pili,

"Dokta wa polisi, umefanya hayo mauaji leo hii" Sajenti Minja alijibu huku akimtazama Trigger,

"kuna ushahidi gani labda?" Trigger aliuliza,

"kabla hajafa aliongea mwenyewe" Sajenti Minja alijibu,

"aliongea? amenijuaje?" Trigger aliuliza kwa kebehi huku akicheka,

"nadhani kutokana na ile picha ya kwenye simu yangu, kwa maana siku ya kwanza unafanya jaribio la kumuua alikuona" Sajenti Minja alijibu,

"Alafu siku hizi nimekuwa mzembe sana, nalenga ila siui, sijui kwa nini?" Trigger aliongea huku akitabasamu kwa dharau,

Kisha akanyanyua kiti na kusogea usawa wa Dokta Innocent Malle, ambaye muda wote alikuwa akitabasamu,

"mzee utanisamehe sana, ila sitokuua endapo utanijibu swali langu vizuri, je Vin umemuambia ukweli kuhusu familia yake?" Trigger aliuliza huku akimuangalia Dokta Innocent Malle,

"ukweli kuhusu familia yake ipi? Mimi nimemwambia ukweli kuhusu tukio lake la kufutwa kumbukumbu, na sijui kuhusu kitu kingine'' Dokta Innocent Malle aliongea huku akitabasamu,

"ooh vizuri sana, je kulikuwa na umuhimu gani wa kumwambia hayo yote?" Trigger aliuliza,

"nadhani kila mwanadamu anatakiwa ajitambue" Dokta Innocent Malle alijibu na kumfanya Trigger atikise kichwa huku akitabasamu,

"je kuna mtu ana swali?, kabla sijafanya kitu cha kutisha yoyote mwenye swali aulize" Trigger aliongea huku akiinuka kwenye kiti,

"Mimi nina maswali matatu tu, naomba ushirikiano wako" Sajenti Minja aliongea huku akimuangalia Trigger,

"uliza kamanda'" Trigger aliongea huku akicheka, alikuwa akimdhiaki Sajenti Minja,

"nataka kujua kuhusu familia ya Sarah, ni kweli Taita aliichoma moto?" Sajenti Minja aliuliza na kumfanya Trigger afikirie kidogo,

"sasa hivi vitu vyote vipo wazi, kila mtu anaujua huo ukweli, jibu la hilo swali unalo, labda kama una swali jingine" Trigger alijibu na kumfanya Sajenti apate uhakika kuwa Taita ndio aliyeiangamiza familia ya Sarah,

"leo nimeona majibu ya Vin, yanaonesha yeye na Sarah ni ndugu, je mlitumia njia gani kuwatenganisha?" Sajenti Minja aliuliza,

"maswali yako ya kipuuzi, yanapoteza muda tu, hilo swali ulilouliza jibu lake analo huyo mzee Dokta" Trigger alijibu huku akivua shati,

.

"ni muda wa kuua huu, nitaanza kwako kwenda kulia" Trigger aliongea huku akitoa risasi tatu kwenye mfuko wa suruali na kuzipachika kwenye bastola yake, kisha akamtupia jicho Sajenti Minja na kumnyooshea bastola usawa wa kichwa,

"Trigger akikunyooshea bastola uwa haishushi mpaka itoe risasi" Sajenti Minja aliyakumbuka maneno hayo ya Trigger kisha Sajenti Minja akafunga macho na kuuma meno kwa nguvu, alijua kinachofuata ni kifo, Trigger baada ya kumuona Sajenti Minja akiwa kwenye hali ile, Trigger akaachia cheko moja baya sana huku akiwa Bado ameielekeza bastola yake usawa wa kichwa cha Sajenti Minja.

******************

Vin alipotoka polisi alirudi hospitali na kuchukua gari yake, kisha akaelekea moja kwa moja nyumbani kwa Taita na kumkuta Taita akiwa anatazama runinga,

"Trigger yupo wapi?" Vin aliuliza huku akikaa,

"sijui hata alipoelekea, vipi kwani?" Taita aliuliza,

"mzee kwanini mnatumia silaha kufanya mauaji ili mfiche tu ukweli juu ya chimbuko langu?" Vin aliuliza kwa sauti tulivu na kumfanya Taita ashtuke,

"kwanini unasema hivyo mwanangu?" Taita aliuliza kwa upole,

"Sarah ni ndugu yangu, hata ungeniambia mapema tu wala nisingebadilika, wewe bado ni baba kwangu" Vin aliongea huku akiwa ameangalia chini,

Huyo Sarah atakudanganya mpaka lini? majibu si uliyaona yalionesha hamna undugu wowote" Taita aliongea kwa ukali,

"yale majibu aliyaleta Trigger, mimi nimekuja na majibu yangu niliyopewa na Daktari mliyemuua leo" Vin aliongea na kuitupa ile bahasha juu ya meza, kisha Taita akaikota na kuitoa karatasi ya ndani, akaanza kusoma na kisha akatabasamu,

"wewe unaamini hii? Huu ni ujanja wa Sarah tu wa kukuharibu akili" Taita aliongea huku akitabasamu,

"huu ni ujanja ee? Na hii je?" Vin aliongea na kuitoa simu yake kisha yakaanza kusikika maneno ya Dokta Innocent Malle wakati alimueleza Vin habari za miaka ishirini iliyopita, Taita alikaa kimya huku akifuatilia yale maneno,

"sasa hata huyu Dokta huenda ametumwa na Sarah, mbona wewe Vin ni msomi tu ila unashindwa kujua upi ni ukweli na upi ni uongo?" Taita aliuliza huku akiyatupa yale majibu juu ya meza,

"sasa aongee nani ndio nimuamini? Maana kila anayeniambia ukweli unadai anatumwa" Vin aliongea,

"hakuna wa kumuamini, labda ningeongea mimi au Trigger, hapo ndipo ungeamini" Taita aliongea huku akimtazama Vin,

"wewe au Trigger ee? Sawa, je na hii sauti ndio unaiamini?" Vin aliuliza huku akifungua lap top yake kisha akaweka yale maneno ya Trigger aliyotumiwa Strategic kama mtego, baada ya maneno kuisha, Taita alihisi nguvu kumuishia miguuni, maana Trigger ndio mtu pekee ambaye alikuwa akimuamini muda huu, alishangaa kusikia kuwa nae ametoa siri hiyo.

"bado unapinga?" Vin aliuliza huku akimuangalia Taita aliyekuwa amekaa kimya,

"Strategic ameamua kunigeuka, umemtumia ili uujue ukweli" Taita aliongea kwa sauti iliyokata tamaa,

"Trigger ameongea maneno mengi, ila ninachotaka ukubali tu kuwa mimi sio mwanao na pia unihakikishie Sarah ni ndugu yangu" Vin aliongea huku akimtazama Taita aliyekuwa ameinamisha kichwa chini,

"Sarah ni ndugu yako, mimi sio baba yako" Taita aliongea huku akimtazama Vin,

"hicho ndicho nilichokuwa nakihitaji, sasa nipo huru, pamoja na yote hayo bado wewe ni baba yangu, sina baba mwingine mwenye kunipa upendo kama wewe" Vin aliongea huku machozi yakimtoka, ila Taita hakuonekana kusikiliza maneno ya Vin, Taita alikuwa kama amechanganyikiwa, yaani siri aliyoificha muda mrefu imekuja kugundulika kizembe namna hiyo, tena mtu wa karibu ndiye aliyeivujisha.

"Baba, Trigger yupo wapi?!" Vin aliuliza huku akiwa bado analia,

"ameenda kwa Dokta Malle" Taita alijibu bila kutarajia,

"tafadhali mzuie asiue zaidi, ukweli umeshajulikana na haina haja ya kuua zaidi" Vin alimsisitiza Taita huku akilia,

"hapana, siwezi kumzuia, wote waliosababisha ukweli ukajulikana ni lazima wafe" Taita aliongea huku akiwa hana mzaha,

"unachosema kitatokea moyoni kwako?" Vin aliuliza huku akitokwa na machozi,

"uwa sitanii, na sasa nataka nikuoneshe roho yangu ilivyo, nilificha sana tabia yangu nilipokuwa na wewe" Taita aliongea kwa ujasiri,

"hapana aisee, ngoja nikamsaidie Dokta Malle" Vin aliongea huku akiinuka,

"Vin subiri, nenda chumbani kwangu kaniletee dawa kwenye droo ya chini ya kabati" Taita aliongea kisha Vin akakimbia ndani haraka, Vin aliyoingia tu chumbani, Taita akainuka na kukimbilia mlango, kisha akamfungia Vin kwa nje, Vin akashtuka,

"mzee ndio unafanya nini sasa?" Vin aliuliza kwa hamaki huku akiwa ndani,

"Vin tulia uko kwanza, acha Trigger atimize majukumu yake" Taita aliongea na kurudi kukaa kwenye kiti, kisha akampigia simu Trigger na kumuamuru amuue Dokta Innocent Malle na wote wataokuwa kikwazo eneo hilo.

Wakati huo ndani Vin alikaa kitandani huku akiwa hana la kufanya, wazo likamjia, akachukua simu na kumpigia Sarah,

"vipi Seba" Sarah aliongea baada ya kupokea simu,

"Dada wahi kwa Dokta Malle, anauawa muda wowote" Vin aliongea na kumfanya Sarah ashangae kuitwa dada na Vin,

.

..

"anauawa na nani?" Sarah aliuliza,

"mzee amemtuma Trigger akamuue, tafadhali kamsaidie" Vin aliongea kwa haraka haraka,

"huyo Dokta Innocent Malle ndio nani?" Sarah aliuliza,

"ndio huyo aliyenifuta kumbukumbu, sasa mzee anataka amuue kwa sababu alinieleza ukweli" Vin alijibu,

"anaishi wapi?" Sarah aliuliza na kisha Vin akamuelekeza na kukata simu, Vin akajilaza kitandani huku akiwaza na kuwazua.

****************

Sarah baada ya kukata simu, aliondoka Moja kwa moja na kwenda kuchukua boda boda iliyomfikisha mpaka mtaa alioelekezwa, akashuka na kumlipa dereva boda boda, kisha akakaa sehemu pembezoni mwa ukuta huku akiwa na mshangao, kwa maana aliikuta gari ya Sajenti Minja ikiwa nje ya ile nyumba pia,

"huyu nae amejuaje hili tukio? Au Vin alimwambia?" Sarah aliwaza huku akiiangalia gari ya Sajenti Minja, Sarah akataka atoe simu ili amfahamishe Vin juu ya uwepo wa Sajenti Minja pale, ila kabla hajapiga simu aliona geti la mlango wa nyumba ya Dokta Innocent Malle ukifunguliwa, kisha akawaona watu wakitoka ndani ya ile nyumba, wa kwanza na wa pili hakuwatambua, ila wa tatu alimtambua, alikuwa ni Sajenti Minja aliyeonekana ana damu nyingi begani, na mtu wa nne akamtambua, alikuwa ni Trigger, alikuwa amemshika bastola na alionekana akiwa anawaamrisha wenzake,

"mshenzi huyu amewateka wenzake" Sarah aliongea huku akicheka na kuwashuhudia wakiingia kwenye gari na kuondoka.

Sarah hakutaka Kupoteza muda, akaangaza kushoto na kulia hakuona usafiri wa kuchukua, akakunja uso kwa hasira, akaamua aanze kukimbia kuelekea upande ule wakina Trigger walipoelekea, ila kabla hajapiga hatua za kutosha, kuna gari ilikuja kusimama pembeni yake,

"ingia" Alikuwa ni Aisha, aliongea huku akitabasamu, Sarah hakutaka kubisha, akafungua mlango na kuingia, kisha Aisha akaiondoa gari kwa kasi,

"unajua ninapoenda?" Sarah alimuuliza Aisha,

"si unamfuatilia Trigger na mateka wake?" Aisha aliuliza,

"yap, umejuaje?" Sarah aliuliza,

"popote uendapo nipo nyuma yako, ulipowaonea wewe, na mimi niliwaonea hapo hapo" Aisha alijibu kisha ukimya ukachukua nafasi yake.

Waliifuatilia ile gari mpaka walipoona imeingia kwenye nyumba moja hivi, hiyo nyumba wote waliitambua, Aisha akasimamisha gari,

"pale kuna walinzi wengi, tutaingiaje?" Aisha aliuliza,

"wewe pitia getini, mimi nitazunguka nyuma ya nyumba" Sarah alitoa wazo,

"Alafu? yaani sijaelewa maana yako" Aisha aliuliza,

"wewe si wanakujua baadhi ya walinzi? Nenda kawapotezee muda kwa kuwalaghai na hadithi za uongo, utanisubiri mimi niingie kwa ndani, ukiniona tu anza kushambulia" Sarah aliongea,

"poa" Aisha alijibu kisha akaelekea getini, Sarah yeye akaamua kuizunguka nyumba na kupitia kwa nyuma.

Aisha akaenda mpaka getini na kumkuta kijana akiwa anaimarisha ulinzi,

"niitie Trigger" Aisha aliongea bila salamu,

"hayupo, kwanza wewe nani?" Kijana aliuliza huku akiwa amemkazia sura Aisha aliyekuwa anashangaa ndani kuona kweupe, hakuna walinzi kama alivyozoea, aisha akaona asipoteze muda, akakishika kisha cha yule kijana na kukibamiza getini, geti likapiga kelele,

"aaaaagh, nimebugi" Aisha alijilaumu huku akimuachia yule kijana na kudondoka chini kama mzigo, kisha Aisha akawa anakimbia kuingia ndani, hakujua kama mateka wapo nyuma ya nyumba na Trigger.

Huko nyuma kile kishindo cha geti kilimshtua Trigger na kumfanya haache zoezi la kumpiga risasi Sajenti Minja ambaye alikuwa amefunga macho akisubiri kumalizwa.

Trigger akashusha bastola chini na kuanza kunyata taratibu kuelekea mbele ya nyumba ili aone kuna nini, alipotokeza ndipo akamuona mwanamke akikimbia kuelekea ndani,

"stop, weka mikono juu" Trigger aliongea huku akimuangalia Aisha,

"Trigger, mi Aisha" Aisha aliongea huku akitabasamu, Trigger akafyatua risasi kumtisha,

"Mikono juu, habari zako ninazo" Trigger aliongea kwa hasira na kumfanya Aisha anaswe kwa urahisi, kisha Trigger akamkokota Aisha mpaka nyuma ya nyumba na kuanza kumfunga kwenye nguzo kama wenzake,

"nilikuwa nakutafuta sana wewe, tulikukosa kukuua na bomu nikasikia eti na wewe umepanga kutuua? Trigger hauliwi na malaya" Trigger aliongea kwa dharau huku akiwa anamalizia kumfunga Aisha, kisha Trigger akageuka nyuma ili arudi kwenye kiti, ila alishtukia kishindo chepesi nyuma yake, akageuka kwa haraka akakutana na teke kali lililotua kwenye mkono na kufanya bastola yake iruke mbali,

"Trigger, professional killer" Sarah aliongea huku akiwa amemuelekezea bastola Trigger, Trigger akapigwa na bumbuwazi, huku asijue namna sarah alivyoingia na wakati huo Sajenti Minja na Aisha wakipata ahueni wakiamini Sarah atawaokoa,

"nenda mbele, twende tukakae pale kwenye viti" Sarah aliongea na kumfanya Trigger atembee mpaka kwenye kiti na kukaa, kisha Sarah nae akakaa upande wa pili na meza ikawa kati yao,

"ule mchezo tulioucheza mara ya mwisho tulipokutana, nataka tucheze na leo ingawa siku ile ulinizidi kete" Sarah aliongea na kufanya Trigger atabasamu huku wale wengine waliofungwa wakiwa hawaelewi ni kitu gani kinaendelea,

Sarah akatoa bastola kiunoni na kuitupa mbele ya Trigger, kisha nae akazitoa risasi zote kwenye bastola aliyoishika mkononi na bastola akaiweka mezani, alafu akachukua simu yake na kuitega sekunde thelathini na kuiweka mezani, hapo wote wawili wakawa wanaziona sekunde zinavyohesabu.

Sajenti Minja akashtuka baada ya kugundua mchezo wa Sarah, na wakati huo Aisha akatabasamu akiamini Sarah yupo na wepesi sana, kwa hiyo atamshinda Trigger,

"wewe Sarah acha upuuzi njoo utufungue, atakuua huyo" Sajenti Minja aliongea kwa sauti ila wala Sarah hakuonekana kumjali, akili na macho yake yalikuwa makini na bastola mezani.

Zilipobaki sekunde kumi, Sarah akatoa risasi mbili, moja akaiweka mbele ya Trigger na nyingine akaweka mbele yake. Sekunde zikazidi kuhesabu kwa kushuka chini, ilipofika sekunde ya sifuri hapo Sarah kwa Kutumia wepesi wake aliiokota risasi na kuiweka kwenye bastola kwa kasi ya ajabu sana, ila wakati akiinuka kichwa kumuangalia Trigger, hapo Sarah alikutana na ajabu la mwaka, tayari Trigger alikuwa ameshamaliza kila hatua na bastola yake ilikuwa inaangaliana na uso wa Sarah. Sio Sarah tu aliyeshangaa hilo tukio, mpaka Sajenti Minja na Aisha walikuwa midomo wazi kwa namna Trigger alivyokuwa mwepesi kwenye masuala hayo ya michezo ya silaha za moto.

Sarah akainuka ili akimbie, ila alijigonga kwenye kiti na kuanguka chini, kisha bastola ikamponyoka na kudondoka mbali, Sarah akaishiwa ujanja na wakati huo Trigger aliinuka na kumfuata Sarah aliyekuwa amelala chini, Trigger alivyomfikia Sarah aligusisha bastola yake na paji la uso wa Sarah, Trigger akatoa cheko kubwa sana, huku Sarah jasho likimtoka,

"Trigger akikuoneshea bastola uwa haishuki chini mpaka itoe risasi" Sajenti Minja alijikuta anaongea peke yake bila kujua ila sauti yake ilisikika vyema kwa kila mtu,

"yeah, hiyo ndio kanuni yangu" Trigger aliongea huku akicheka na kufyatua risasi kwenye kichwa cha Sarah, watu wote katika eneo hilo walifunga macho.....................

.

*********ITAENDELEA***********

the Legend☆
 
Ahsante kunitag ila mi nishamalizana nayo jikoni!!
Nipo kwakina Ray na Yusufu
 
Tukutane tena usiku kwa episode nyingine, na hatimae kesho asubuhi kwa episodes zitakazobaki. Na hapo tutakua tumefikia mwisho wa Sala ya Sarah. Muwe na jioni njema wakuu

the Legend☆
 
Tukutane tena usiku kwa episode nyingine, na hatimae kesho asubuhi kwa episodes zitakazobaki. Na hapo tutakua tumefikia mwisho wa Sala ya Sarah. Muwe na jioni njema wakuu

the Legend☆
Asante sana dear
 

Similar Discussions

Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…