RIWAYA : SALA YA SARAH
MTUNZI : ALEX KILEO
SEHEMU YA SITINI NA NNE.
ENDELEA..................
Sajenti Minja akawasha gari yake na safari ya kwenda kituoni ikaanza, njia nzima hakuna aliyemuongelesha mwenzake, Sarah alikuwa akisali msaada utokee, huku Sajenti Minja alikuwa akishangilia kwa kumkamata muharifu wake kwa urahisi namna ile,
"hivi wewe uwaga unanitafutia nini?" Sarah alimuuliza Sajenti Minja, alionekana ana hasira,
"swali gani la kipuuzi hilo unauliza wakati unajua mimi ni polisi na wewe ni muharifu" Sajenti Minja aliongea kwa dharau,
"itafika kipindi nitaanza na wewe kwa maana umekua kama kikwazo kwangu, nitakuondoa wewe kikwazo ili nifanye kazi yangu kwa uhuru" Sarah aliongea kwa hasira,
"sasa haya ni maajabu yametokea, kikwazo ndio kimekuzidi uwezo leo" Sajenti Minja aliongea na kucheka,
"sawa, huu ni mchezo, bado haujaisha, yoyote anaweza kushinda" Sarah aliongea kwa sauti ndogo ila ilimfikia kwa uzuri tu Sajenti Minja,
"mchezo eeh? Kuua watu ni mchezo?" Sajenti Minja aliongea huku akiegesha gari nje ya kituo,
"wewe ndio unaona naua, ila wao ndio wanajua ninachokifanya dhidi yao" Sarah alijibu wakati Sajenti Minja akitelemka katika gari,
"hiyo hainihusu, mimi nipo upande wa sheria tu" Sajenti Minja aliongea huku akifungua mlango wa upande wa Sarah, kisha akamfungua kamba na kisha akamfungua pingu zote, za mikononi na miguuni.
"Sidhani kama utaleta usumbufu eneo hili, mimi sio mkofofi, ila nikichokozwa uwa sio mtu mzuri kabisa" Sajenti Minja alimuonya Sarah mara baada ya kumfungua pingu, kisha akamtelesha na kumshika mkono, wakawa wanaelekea ndani ya kituo.
"twende ofisini kwangu, kuna maswali ya kujibu" Sajenti Minja aliongea huku akiwa bado amemshika mkono Sarah.
Wakaelekea moja kwa moja mpaka ofisini kwa Sajenti Minja na Sarah akawekwa kwenye kochi,
"nina maswali machache tu, Taita ni nani yako?" Sajenti Minja aliuliza,
"mjomba angu" Sarah alijibu,
"mbona yeye anadai hakujui?" Sajenti Minja na Sarah akacheka,
"inaweza kuwa sawa, kwani hajawahi kuona ndugu hawajuani?! " Sarah alihoji,
" kwanini ulimuua Harry?" Sajenti Minja aliuliza,
"Mimi? Ooh sawa ndio ni mimi niliyemuua, ila alitaka mwenyewe kufa" Sarah alijibu huku akitabasamu,
"alitaka mwenyewe kufa? alitakaje kufa?" Sajenti Minja aliuliza,
"aliyesema amechoka kuishi, hana furaha kwa maana familia yake imeuawa yote" Sarah alijibu,
"na mahakamani ukisema huo ushenzi unaweza kupona?" Sajenti Minja aliuliza huku akimshangaa Sarah,
"mahakamani? Sidhani kama naweza kufikishwa mahakamani kwa kitendo hicho" Sarah alijibu kwa kujiamini,
"kwanini uliiua familia ya Harry?" Sajenti Minja aliuliza,
"na wewe upo kama mpuuzi, nitaiuaje familia isiyo na hatia? Najua ni uchungu kiasi gani mtu anaupata anapopoteza familia, nisingeweza kuiua familia Harry" Sarah alijibu,
"sasa kama unajua ni uchungu kupoteza watu muhimu maishani, kwanini ulimuua Harry?" Sajenti Minja aliuliza,
"nilimuua baada ya familia yake kufa, hakuwa na furaha tena, alitaka akaungane na familia yake" Sarah alijibu,
"umesema wewe hujaua familia ya Harry, ni nani ameiua familia ya Harry?" Sajenti Minja aliuliza,
"Taita, Taita na vibaraka wake" Sarah alijibu na kumfanya Sajenti afikirie kidogo, kisha akaitoa simu yake na kubonyeza bonyeza,
"unamjua huyu?" Sajenti aliuliza huku akimuonesha picha ya Trigger,
"Trigger, huyu ndio kiongozi wa mauaji yanayotokea chini ya Taita" Sarah alijibu,.
"unajua kuwa huyu ndiye aliyefanya shambulio la kumuua daktari pale hospitali ulipotoka?" Sajenti Minja aliuliza,
"sijui" Sarah alijibu baada ya kuhisi hilo swali ni la mtego,
"Alafu na yule kijana mwingine anayependa kuvaa suti, ni nani kwa Taita?" Sajenti Minja aliuliza baada ya kumkumbuka Vin na maneno aliyowahi kuambiwa na mlinzi wa Harry kuwa kabla familia ya Harry haijaangamia, mtu wa mwisho kuingia alikuwa ni Trigger na huyo kijana mmoja anapenda kuvaa suti,
"yule anaitwa Vin, hata ile Vin hotel inatokana na jina lake" Sarah alijibu,
"ndiye mtoto wa Taita?" Sajenti Minja aliuliza,
"hapana, yule ni mdogo wangu" Sarah alijibu na kumfanya Sajenti Minja amtolee macho,
"mdogo wako? Au mdogo wako kwa kuwa Taita ni mjomba wako?" Sajenti Minja aliuliza na kumfanya Sarah atabasamu,
"mdogo wangu kwa maana ya kuchangia baba na mama" Sarah alijibu na sasa ikawa zamu ya Sajenti Minja kucheka,
"kivipi?" Sajenti Minja akauliza,
"kivipi, vipi? Hujaelewa nilichokueleza?" Sarah akauliza huku akimshangaa Sajenti Minja,
"iweje Vin awe ndugu yako alafu awe anakaa vyema na Taita, ingali wewe hauishi vyema na Taita?" Sajenti Minja aliuliza,
"yupo gizani yule, na siku akipata mwanga, hakutakuwa na wa kumzuia" Sarah alijibu na kumfanya Sajenti Minja abaki ndani ya Fumbo,
"nitakuuliza swali la mwisho, je ugomvi wako wewe na Taita ulitokana na kifo cha wazazi wako?" Sajenti Minja aliuliza,
"liweke vizuri swali lako hili jibu liwe jepesi, kwa maana wakati wazazi wangu wakifa nilikuwa na miaka sita tu, nisingeweza kugombana na mtu mzima" Sarah alijibu,
"Taita baada ya kuiangamiza familia yako ndipo ulipomchukia?" Sajenti Minja alimuuliza Sarah,
"hilo sio swali, ni jibu" Sarah alijibu,
"na mwisho wa yote ni nini?" Sajenti Minja alimuuliza,
"mwisho ni chini, ama yeye ama mimi" Sarah aliongea huku hasira zikionekana wazi machoni mwake,
"mwisho ni jela, tena kabla vifo havijatokea zaidi, ni lazima ufungwe sasa, ni lazima ushtakiwe Sarah" Sajenti Minja aliongea kwa sauti tulivu,
"hilo halitotokea, mkae mkijua kwamba mimi sishikiki, mimi ni moto. Kama mlishindwa kumkamata Taita na mlijua ana tuhuma, basi msitegemee kunishka mimi, hakuna atayebaki salama" Sarah aliongea kwa hasira na kumfanya Sajenti Minja acheke,
"we mpuuzi kweli, yaani upo mikononi mwa polisi alafu unaleta jeuri?" Sajenti Minja aliuliza huku akicheka,
"labda mniweke ndani ya chupa, tena chupa ya chuma" Sarah aliongea huku bado akiwa na hasira, na kipindi hicho mlango wa ofisi ya Sajenti Minja ulikuwa unagongwa,
"ingia" Sajenti Minja alijibu hodi na kutupia macho mlangoni, aliingia mwanamke aliyevaa kofia ya cap, alipoingia alifunga mlango kwa ndani, wakati Sajenti Minja akishangaa tukio hilo, yule dada aligeuka na mkononi alikuwa na bastola, kisha akaiondoa ile kofia kichwani na kubaki uso wazi, alikuwa ni Aisha,
"afande tulia hivyo hivyo, ukijitingisha sikuachi, si unakumbuka nilichomfanya mwenzako mara ya mwisho ndani ya ofisi hii?" Aisha aliuliza huku akitabasamu na kumfanya Sajenti Minja atulie kama gogo, alikumbuka tukio la Aisha alilowahi kulifanya hapo,
"na wewe unazubaa nini? Nyanyuka na umfunge huyo afande" Aisha aliongea huku akimtazama Sarah, Sarah hakuupenda ule msaada wa Aisha, aliamini unamuongezea matatizo tu, ila kwa muda huo hakuwa na la kufanya, alitaka kuwa huru.
Sarah aliinuka na kwenda kumfunga pingu Sajenti Minja, kisha Aisha akatoa bomu na kuchomoa pin na kumuwekea lile bomu mdomoni mwa Sajenti Minja, kisha akamfunga na plasta ngumu,
"sasa bomu la nini, usimuue bwana" Sarah aliongea kwa ukali huku akimtazama Aisha,
" twende, hii kwa ajili ya usalama wetu" Aisha aliongea huku akifungua mlango kisha wakatoka taratibu huku Aisha akiwaaga polisi wengine kwa furaha zaidi na kumfanya Sarah ashangae huku akijiuliza hilo tukio Aisha alipanga kulifanya kwa kushirikiana na askari wengine au?
Aisha aliongoza nje kwenye gari moja dogo jeusi na kuingia, kisha Sarah nae akaingia upande wa pili,
"kwanini sasa umemuwekea bomu?" Sarah aliuliza huku akimuangalia Aisha,
"ni bomu ndio, ila haliwezi kulipuka kwa kuwa nilishaliharibu, na bila kumfanyia hivyo huenda angepiga kelele baada ya sisi kutoka" Aisha aliongea na kumfanya Sarah ashushe pumzi,
"ulijuaje nipo hapa?" Sarah alimuuliza Aisha,
"nilishajitolea kukusaidia, popote uendapo nipo nyuma yako" Aisha aliongea,
"lakini kumbuka kuwa huu msaada unaonipa unazidi kuniharibia tu, kwa maana hapo umeniongezea kosa polisi, nimeonekana nimemtoroka askari" Sarah aliongea,
"nataka uwe huru ukamilishe kisasi chako" Aisha aliongea,
"na mbona wakati tunatoka polisi ulikuwa ukiagana vizuri na askari?" Sarah alimuuliza Aisha,
"wakati naingia nilijitambulisha ni mpenzi wa Sajenti Minja na niliongea nao kwa ucheshi kabla hawajanielekeza ilipo ofisi ya Minja" Aisha aliongea,
"nishushe hapa" Sarah aliongea na kisha Aisha akasimamisha gari na Sarah akashuka,
"nashukuru, ila nakupa onyo tena, sihitaji msaada kutoka kwako, vinginevyo na wewe utakuwa katika hatari" Sarah aliongea ila Aisha hakujibu kitu, aliondoa gari huku akiongeza sauti ya radio,
"kama ungekuwa hutaki msaada si ungeendelea kubaki polisi, kwanini ulikubali kuondoka na mimi" Aisha aliongea peke yake huku akitabasamu.
Sarah baada ya kuachia na Aisha, alichokifikiria kwa muda huo ni kumpigia simu Vin na kumpa taharifa juu ya daktari aliyepigwa risasi kuwa hajafa. Sarah akaitoa simu mfukoni na kuitafuta namba ya Vin na kupiga.
*******************
Sajenti Minja hakuwa katika hali nzuri, mikono yake ilifungwa pingu iliyoambatanishwa na kiti na mdomoni alikuwa na bomu lilipachikwa na juu ya Bomu kulikuwa na plasta ngumu iliyolizuia bomu lisitoke mdomoni kwa Sajenti Minja. Sajenti Minja hakuweza kutoa hata sauti, muda wote alikuwa kimya huku akimuomba Mungu amletee msaada na pia miale ya machozi ilikuwa ikimchomoza machoni.
Baada ya kukaa muda mrefu bila kupata msaada, Sajenti Minja aliinuka na kiti na kwenda mpaka mlangoni, kwa kuwa mlango ukifunguliwa unafungukia kwa ndani, hiyo ikawa shida shida nyingine, hakuweza kuuvuta mlango, ikabidi augonge mlango kwa kutumia kiti. Baada ya kuugonga kwa muda kidogo, wenzake wa nje walisikia, mmoja wao akaenda na kuusukuma mlango, akamkuta Sajenti Minja akiwa amefungwa kila sehemu, yule askari akakimbilia moja kwa moja kubandua plasta ya mdomoni, Sajenti Minja akakwepesha mdomo na kumuonesha kwa ishara kuwa amfungue pingu, yule askari akafungua pingu Sajenti Minja, kisha Sajenti Minja akaibandua plasta taratibu na kisha akalitoa bomu mdomoni na kutoka nalo nje kwa lengo la kwenda kulitupa baharini, ofisi yao na bahari vilikuwa jirani, baada ya yule askari mwingi kugundua Sajenti Minja amemshika bomu, ikabidi nae aanze kukimbia kutoka nje na wakati huo Sajenti Minja nae alikuwa anaanza kukimbia, tatizo mlango ulikuwa mdogo, wote wakakutaniana mlangoni na kudondoka chini, bomu likamponyoka Sajenti Minja, wakilalamika chini huku wote wakipiga kelele wakijua mwisho wao umefika, lakini wakashangaa bomu halilipuki, mwenzake akanyanyuka bila kuangalia mbele, alitaka akimbie akajikuta akilikanyaga lile bomu, akaanguka tena chini ila bomu halikulipuka, liliseleleka mpaka jirani kwa Sajenti Minja, Sajenti akalitupia jicho na kuona lile bomu lina uwazi mkubwa kwa juu, akashangaa, maana hakuna bomu la namna ile duniani, Sajenti Minja akaliokota na kuliangalia kwa karibu, akagundua ndani ya lile bomu kuna karatasi, akazitoa zote na kuziweka pembeni, bomu halikuwa na kitu, lilikuwa "empty"
Sajenti Minja akajicheka mwenyewe huku akimuangalia mwenzake ambaye alikuwa ameshapoteza fahamu muda mrefu tu mara baada ya kukanyaga bomu.
"hawa wanawake wapumbavu sana" Sajenti Minja aliongea huku akitabasamu, kisha akakumbuka kitu,
"Sarah alivyotoka hospitali alifuata nini?" Sajenti Minja alijiuliza kisha kwa haraka sana akawa anatoka nje, alipanga kwenda hospitali,
"nendeni mkamtoe mwenzenu ofisini kwangu, mlazeni nje chini ya miti" Sajenti Minja aliwaambia askari wawili waliokuwa wamesimama wakipiga soga, kisha Sajenti Minja akaenda kwenye gari yake.......................
.
*********
Vin, Taita na Trigger wakiwa sebuleni wanaongea, simu ya Vin iliita, ilikuwa karibu na Trigger, Trigger akaiokota na kumpa Vin, ila Trigger alibahatika kuona jina la mpigaji, alikuwa ni Sarah,
"vipi?'" Vin aliongea baada ya kupokea simu,
"yule daktari aliyekupima hajafa, nilienda hospitali kufanya uchunguzi" Sarah aliongea na kumfanya Vin ashtuke,
"Daktari hajafa? Yupo wapi?" Vin aliuliza,
"amelazwa pale pale" Sarah alijibu,
'pale pale?, poa ngoja niende" Vin aliongea na kukata simu, kisha akatoka kwa haraka bila kuaga mtu na kufanya Taita amtupie jicho Trigger,
"alikuwa anaongea na Sarah, nimeona jina kwenye kioo" Trigger aliongea,
"Daktari gani ambaye wanamzungumzia?" Taita aliuliza,
"hata mi sijui" Trigger alijibu
"wewe, sio yule uliyempiga risasi juzi ukaondoka na majibu?
" Taita aliuliza kwa mshangao na kumgutusha Trigger,
"ila hata Vin akienda haitomsaidia, majibu si ameyaona na hayaoneshi undugu walionao" Trigger aliongea,
Usiwe mjinga wewe, je huyo daktari akihojiwa na akikutaja wewe kwa Vin, ni picha gani Vin atapata?" Taita aliuliza kwa hasira,
"kwa hiyo?" Trigger aliuliza,
"nenda kammalize muda huu kabla hawajaongea chochote na Vin" Taita aliongea,
"Ila kweli eeh?" Trigger aliuliza na kunyanyuka kwa haraka, nae akatoka ndani kwa kasi kuwahi gari ili aende hospitali na kufika kwa haraka kabla ya Vin.
***, **************
Alitangulia Trigger kufika mapema hospitali, haikuingia ndani, akawa anazunguka nje ya jengo huku akitumia madirisha kumtafuta daktari anayemtaka na mkononi akiwa na bastola.
Vin alifika hospitali na kwenda mapokezi, akajitambulisha na kisha akauliza kama ni kweli Dokta yupo hai, akajibiwa ndio, akaomba kuongea nae kidogo, wadada wa mapokezi wakaenda kumpa ombi la Vin yule daktari, Daktari akakubali kwa maana aliona huo ndio muda muafaka wa kumpatia Vin majibu ya kweli.
Vin akaingia mpaka katika wodi aliyolazwa daktari na kumkuta akiwa amekaa, Daktari alipomuona Vin alifurahi sana, wakasalimiana,
"bora umekuja, maana nilikuwa naweza nitakupataje?" Daktari aliongea,
"nilikuja hata siku ile ulipopigwa risasi, nikakukuta haupo kwenye hali nzuri, pole sana" Vin aliongea kwa furaha,
"sasa kijana kuna mtu alifuata majibu yako, nikampatia kwa sababu alikuja kishari, ila majibu ambayo yamethibitishwa kitabibu yapo" Daktari aliongea na kumfanya Vin atoe macho,
"yapo wapi daktari?" Vin aliuliza huku akitabasamu, ila wakati daktari anataka kujibu alisita na macho akayatupia dirishani ambapo Vin aliupa mgongo upande huo wa dirisha, Vin ikambidi atake kugeuka ili aone daktari anachotaka kusema, ila kabla hajageuka alisikia mlio wa risasi na kushuhudia mwili wa Daktari ukiwa umejaa damu na ilionesha amekufa, Vin akatoa bastola yake na kugeuka upande wa dirishani kwa kasi, akamshuhudia Trigger akiipachika bastola yake kiunoni kisha akatabasamu na kutoka akikimbia. Vin akapigwa na butwaa huku bastola yake ikiwa mkononi, akaona bora atoke nje ajaribu kumfukuzia Trigger, ila Vin hata kabla hajainua mguu, mlango wa wodi ulifunguliwa na Sajenti Minja akiwa mkononi na bastola na nyuma yake walikuwa wafanyakazi wa ile hospitali,
"weka bastola chini, nyanyua mikono juu" Sajenti Minja aliongea kwa amri huku bastola yake akiwa ameelekeza usawa wa kichwa cha Vin...... Vin akanyong'onyea akatupa bastola chini, hakuwa na ujanja kwa maana alikamatwa akiwa na ushahidi wa bastola mkononi.....
***********ITAENDELEA***********
the Legend☆