RIWAYA : SALA YA SARAH
MTUNZI : ALEX KILEO
SEHEMU YA AROBAINI NA SABA
ILIPOISHIA.............................
Baada ya nusu saa Sarah aliweza kutoka chumbani huku akiwa amevaa nguo za mazoezi na kwenda moja kwa moja kwenye friji na kuchukua juisi, akaimiminia kwenye kikombe na kuinywa kwa haraka,
"kuna habari gani mpya?" Sarah aliuliza huku akitabasamu
"hakuna mpya, habari ni zile zile" Babu alijibu huku akijichekesha,
"mmekula mmeshiba?" Sarah aliuliza huku akiendelea kutabasamu,
"tumeshiba mama, ila mama mpaka leo hajawahi kuniambia ni lini utanipeleka kwangu, maana naishi na wewe hata sikujui" Babu aliuliza kwa sauti kavu,
"tatizo nini mzee, si unakula na unalala vizuri tu, hayo masuala ya kujuana yatakuja mbele ya safari" Sarah aliongea huku akiweka utani,
"usiseme hivyo binti, kama suala la kula hata kwangu ningekula na Kulala vizuri tu" Babu aliongea kwa kujiamini,
"mzee usijifanye huna shida, mzee wewe toka amekufa mwanao Isack na maisha yako yalibadilika na kuwa mabaya sana" Sarah alitoa kauli iliyomshangaza babu yake,
"Isack, wewe umejuaje hayo yote?" Babu yake alimuuliza,
"Pendo twendezetu matizi, mzee anazingua" Sarah alipuuza swali la babu yake na kisha akamuongelesha Dokta Pendo,
"mjibu mzee kwanza" Dokta Pendo aliongea huku akicheka,
"twende bwana, ipo siku atapata majibu" Sarah aliongea huku akimsaidia Dokta Pendo kunyanyuka,
"ipo siku ee? Au utanijibia kituoni?" Babu yake Sarah aliuliza kama utani ila alikuwa amedhamilia,
"mzee leo husomeki ujue, umeonja nini?" Dokta Pendo aliuliza kwa utani,
"twende shoga, kwani alitoka leo?" Sarah alimuuliza Dokta Pendo huku wakitoka kwenye mlango wa sebuleni
"alitoka kuanzia asubuhi, amerudi muda sio mrefu" Dokta Pendo alijibu,
"alikuambia alipoenda?" Sarah aliuliza,
"hajaniambia, ila nahisi itakuwa alienda mjini, maana alirudi na gazeti ambalo lina picha yangu inaonesha nimepotea na natafutwa" Dokta Pendo aliongea na kisha akacheka,
"huyu mzee kichaa, ngoja nikirudi niongee nae, maana alivyo na akili finyu anaweza kwenda kutoa taharifa polisi, na hivi wametangaza na donge nono" Sarah aliongea huku akiushika mguu wa Sarah na kuuvusha kwenye geti.
"Sarah" Dokta Pendo aliita baada ya geti kufunguliwa,
"sema shoga" Sarah alijibu huku macho yake yakiwa bize kuuvusha mguu wa Dokta Pendo uliobakia ndani ya chuma cha geti,
"Sarah" Dokta Pendo aliita tena huku macho yakiwa mbele,
"unaniita, nahitika ila hata huongei" Sarah aliongea huku akirudishia geti, kisha akageuza shingo yake kuangalia mbele, kidogo aanguke kwa kitu alichokiona, walikuwa polisi zaidi ya kumi na wote walikuwa na silaha na walizinyoosha kuelekea sehemu aliposimama Sarah na dokta Pendo,
"wewe mtekaji weka mikono juu" Polisi mmoja aliyeonekana kiongozi aliongea huku akiwa amemkazia macho Sarah, Sarah akajikuta akiinua mikono juu huku na hakiwa hataki kuamini kama lile tukio ni la kweli kwa maana limetokea ghafla sana, alilazimisha iwe ndoto lakini haikuwezekana, Sarah maji yalizidi Unga. .........
***********ENDELEA***********
Sarah akaamua atii amri ya polisi huku akishangaa hao polisi wamepajuaje nyumbani kwake?
"mfungeni pingu huyu muharifu" Kiongozi wa kikosi kile cha polisi alitoa amri ambayo askari wawili walimsogelea Sarah na kuchukua mikono yake na kuifunga pingu.
"naombeni muda kidogo niingie ndani nikaache maagizo" Sarah aliongea kwa huruma huku akimuangalia kiongozi wa kikosi kile cha polisi, ila kabla kiongozi yule hajatoa jibu, babu yake Sarah alitoka ndani huku akiwa kifua wazi na kujongea eneo ambalo Sarah na kiongozi wa polisi walikuwa wamesimama pamoja, Sarah alitegemea babu yake ameenda eneo lile kwa ajili yake, lakini cha kushangaza alishuhudia tukio lililomfungua ubongo, alimshuhudia babu yake akipeana mkono na yule kiongozi wa polisi,
"kazi nzuri mzee, tunamshukuru kwa taharifa yako iliyosaidia kumkamata muharifu" Kiongozi wa polisi aliongea kwa tabasamu pana,
"usijali kiongozi, sisi raia wema lazima tufichue maovu" Babu yake Sarah aliongea huku akitabasamu,
"mzee kumbe ni wewe ndio umeniletea polisi?" Sarah aliuliza huku akimuangalia babu yake,
"mpelekeni bwana, ananipigia kelele" Babu yake Sarah aliongea huku akigeuka nyuma,
"mzee mzigo wako uje uchukue kesho asubuhi, pale pale kituoni ulipotoa taharifa" Kiongozi wa kikosi kile cha polisi alimwambia babu yake Sarah,
"usijali, nitafika hiyo kesho mapema" Babu yake Sarah aliongea huku akirudi zake ndani ya geti.
Wale polisi walimpakia Sarah ndani ya gari huku Sarah akiwa na mawazo dhidi ya babu yake ingawa hakutaka kujenga chuki dhidi yake. Baada ya Sarah kupakiwa ndani ya gari, kupitia kwenye kioo cha gari aliweza kushuhudia Dokta Pendo nae akipakiwa kwenye gari nyingine, alimshuhudia Dokta Pendo akiwa na furaha huku akiongea na baadhi ya askari waliokuwa wanamsaidia kupanda gari. Sarah akawa anajitahidi kuangalia uso wa Dokta Pendo ili ajaribu kumsoma hisia zake, lakini haikuwezekana kwa maana muda wote macho ya Dokta Pendo yalikuwa makini na askari aliokuwa anaongea nao na alionekana akiongea kwa furaha huku akicheka, na hata Dokta Pendo alimpomtazama Sarah, wakikutanisha macho yao Dokta Pendo aliyakwapesha macho yake kwa haraka sana.
Safari iliishia ndani ya kituo cha polisi na Sarah akawekwa lupango. Dokta Pendo alipelekwa moja kwa moja katika ofisi na kuambiwa amsubiri mpelelezi ambaye atakuja kumfanyia mahojiano, lakini hiyo ofisi tayari Dokta Pendo aliijua vizuri hii ofisi, alikumbuka kuwa hii ni mara yake ya pili kuingia ofisini hapo, alijua fika kuwa ofisi hiyo ni ya Sajenti Minja.
Dokta Pendo akiwa amekaa akizungusha macho ndani ya ofisi ile, aliweza kushuhudia mlango ukifunguliwa na aliingia Sajenti Minja, Dokta Pendo akaachia tabasamu laini na kumfanya Sajenti Minja nae atabasamu huku akiwa anashangaa namna Dokta Pendo alivyonenepa. Sajenti Minja akampa mkono Dokta Pendo kisha akaenda kukaa kwenye kiti,
"kwanza pole" Sajenti Minja aliongea kwa utulivu,
"pole ya nini?" Dokta Pendo aliuliza huku akijifanya kushangaa,
"ya kutekwa, au unaona hilo sio tatizo?" Sajenti Minja aliuliza huku akijifanya kutabasamu,
"nani alitekwa??? Wewe unavyodhani Sarah anaweza kuniteka mimi?" Dokta Pendo aliuliza huku akijifanya kushangaa na kumshangaza zaidi Sajenti Minja,
"ndio alikuteka, alikuchukuaje hospitali bila taharifa na kwanini hakuwai kuniambia wewe ulipo ingalikuwa nimeshawahi kufika mara kadhaa nyumbani kwake?" Sajenti Minja aliuliza kwa ukali baada ya kuona kama Dokta Pendo anataka kumtetea Sarah,
"Mimi ndio nilimwambia aniondoe hospitali na mimi ndiye nilimwambia asimwambie mtu yoyote ni wapi nilipo" Dokta Pendo alijibu kwa kujiamini,
"usimtetee Sarah, unamteteaje mtu ambaye amehatarisha maisha yako?" Sajenti Minja aliongea kwa jazba,
"amehatarisha maisha yangu? Kivipi amehatarisha maisha yangu wakati alikuwa akinihudumia kwa kila kitu, ningekuwa kwenye matatizo ningenenepa hivi?" Dokta Pendo alihoji,
"ila inafikia kipindi unatakiwa uwe mkweli Pendo" Sajenti Minja aliongea huku akiwa amepunguza jazba,
"ukweli gani unaoutaka?" Dokta Pendo aliuliza,
"Sarah sio mtu mzuri, nisaidie kuthibitisha hilo" Sajenti Minja aliongea huku akimuangalia Dokta Pendo,
"siwezi kuthibitisha kwa kuwa sijawahi kuuona ubaya wake" Dokta Pendo aliongea huku akicheka,
"sasa alikutoroshaje hospitali na camera zisiweze kuona hilo tukio, si ina maana alizichezea camera, na kama alizichezea, basi hiyo ina maana kuwa yule mwanamke ni muharifu mzoefu" Sajenti Minja aliongea huku akiwa na hasira,
"wewe hujui kitu, usiwe unaongea vitu kwa hisia tu. Sarah hayupo kama unavyomfikiria na siku ile mimi ndio nilimwambia aniondoe hospitali baada ya kuwaona wale watu walioniteka na kunivunja miguu wakiwa wanazunguka zunguka eneo lile, sasa labda huenda wale watu ndio walioharibu camera ili wafanye tukio eneo lile" Dokta Pendo aliongea na kumfanya Sajenti Minja ashushe pumzi ndefu,
"Mimi naona hatutaelewana hapa, ebu ngoja nikupeleke nyumbani ukapumzike, nitakuhoji kesho" Sajenti Minja aliongea huku akinyanyuka kwenye kiti,
"nyumbani wapi?" Dokta Pendo aliuliza kwa mshangao,
"nyumbani kwako" Sajenti Minja alijibu huku akimshangaa,
"nyumbani siwezi kurudi, sio eneo salama kwangu, ninapotaka kwenda ni kwa Sarah tu, hapo ndipo palipo na usalama kwa muda huu" Dokta Pendo alizidi kumvuruga Sajenti Minja,
"sasa hata nikikupekeka kwa Sarah, nani atakuhudumia?" Sajenti Minja aliuliza,
"sasa hata ukinipeleka kwangu nani atanihudumia?" Dokta Pendo aliuliza,
"sasa unatakaje?" Sajenti Minja aliuliza,
"muacheni Sarah, kwa maana yeye ndiye mtu pekee anayeniangalia kwa ukaribu" Dokta Pendo alijibu na kumfanya Sajenti Minja akune kidevu chake,
"ni ngumu kumuacha Sarah kwa kuwa ni mtuhumiwa" Sajenti Minja aliongea huku akiwa bado amesimama,
"mtuhumiwa wa nini? Kama kuondoka hospitali ni mimi ndiye nilietaka, kama hilo ni kosa, basi nikamatwe mimi" Dokta Pendo aliongea,
"basi ngoja nikupeleke hotelini, Sarah tutamuachia baadae, tunataka kumfanyia mahojiano" Sajenti Minja aliongea kwa lengo la kumfanya Dokta Pendo akubali kuondoka,
"naweza kuonana nae muda huu?" Dokta Pendo aliuliza,
"hapana, mtaonana baada ya mahojiano" Sajenti Minja aliongea huku akimtazama Dokta Pendo,
"sawa, naomba msifanye kitu chochote" Dokta Pendo aliongea kwa msisitizo,
"usijali kuhusu hilo, twende nikupeleke hotelini utakaa mpaka jioni Sarah atapokuja" Sajenti Minja aliongea huku akimsaidia Dokta Pendo kumtoa kumpeleka nje, walipofika alimuingiza ndani ya gari na kumpeleka hotel iliyo karibu na kituo cha polisi na kumuacha Dokta Pendo hapo.
********************
Habari ya kukamatwa kwa Sarah ilimfikia Harry, akaamua awaite watu wake, Trigger, strategic, Tekso na Aisha.
"Sarah yupo kituo cha polisi, nimesikia amekamatwa kutokana na lile tukio la kumteka mtu hospitali" Harry aliongea,
"ni jambo zuri, au wewe mkuu unasemaje?" Trigger aliuliza,
"hivi hatuwezi kummalizia pale pale kituoni?" Harry aliuliza,
"inawezekana, kama tutatumia bomu kulipua kituo chote" Tekso aliongea huku akiwa bize kobonyeza lap top yake,
"sasa hapo mtaua mpaka wasiohusika, angalieni njia nyingine tofauti na hiyo ya kulipua" Aisha alitoa ushauri,
"basi tufanye kitu kimoja, Aisha unaweza kuingia ndani mule na kumtorosha Sarah?" Strategic aliuliza na kufanya wenzake wamshangae,
"una lengo gani?" Harry alimuuliza Strategic,
"kama tutafanikiwa kumtoa Sarah mikononi mwa polisi, itakuwa rahisi kumuangamiza akiwa chini yetu" Strategic aliongea,
"je Aisha unaweza kufanya hiyo kazi ya kumtorosha Sarah mikononi mwa polisi?" Harry alimuuliza Aisha,
"inawezekana, ila inahitaji akili sana, kwa hiyo kwa leo haiwezekani mpaka tutengeneze mipango" Aisha aliongea,
"hii kitu inahitajika ifanyike leo, tutakusaidia, nitakupa nguo yenye mawasiliano ambayo tutakuwa tunawasiliana" Tekso aliongea na kisha akamuangalia Harry, na Harry nae akamuangalia Tekso, kuna kitu kinaendelea kati ya hawa watu wawili,
"sawa" Aisha alikubali kisha Tekso akanyanyuka na kuingia kwenye chumba kimoja na kurudi na kizibao, au wengi wamezoea kukiita kijamba koti, kisha akakitupa juu ya meza mbele ya Aisha,
"usiku ukienda kuvamia kituo cha polisi, utavaa hiki kikoti juu ya nguo yako, kineunganishwa na mawasiliano, nitakuwa eneo la polisi kukupa maelekezo" Tekso aliongea huku akikaa kwenye kiti, Aisha akakichukua kile kikoti na kuanza kukikagua, kilikuwa na vufungo vitatu vyenye rangi tofauti,
"hiki kifungo cha juu mbona kikubwa alafu kizito?" Aisha aliuliza baada ya kupata hofu,
"hicho kina camera, njia zote utazopita mimi nitakuwa naziona" Tekso alijibu, lakini ukweli ni kwamba kile kifungo kilikuwa na bomu,
"na hivi vifungo vingine vina nini?" Aisha aliuliza,
"kimoja cha katikati kina kinasa sauti, ila hicho cha chini hakina kitu, ni urembo tu" Tekso aliongea,
"naweza kuondoka na hili koti?" Aisha aliuliza huku akiendelea kulikagua,
"hapana, ikifika muda wa kazi utakuja kulichukua" Tekso alijibu,
"kwanini iwe hivyo?" Aisha aliuliza huku akimuangalia Tekso kwa jicho la udadisi,
"chukua nenda nalo" Harry alijibu baada ya kumuona Tekso akibabaika kutoa jibu,
"beba tu, haina shida" Tekso aliongea huku akitabasamu,
"nadhani tukutane saa mbili usiku, Vin hatakiwi kujulishwa huu mpango, mpaka ufanikiwe ndio tutamjulisha" Harry aliongea huku akiinuka kwenye kiti,
"vipi nikupeleke au una usafiri" Trigger alimuuliza Aisha,
"nipeleke", Aisha alijibu huku akiinuka kisha akatoka huku ameongozana na Trigger, ndani wakabaki Harry na Tekso na Strategic,
"sasa kulikuwa na umuhimu gani wa kumpa Aisha nguo yenye bomu wakati anaenda kumdhibiti Sarah?" Strategic aliuliza,
"Mimi simuamini kabisa, nitatumia mwanya watapokuwa karibu na Sarah wakati wakitoroka, hapo nitalipua bomu, maana hatuna uwezo wa kumfunga Sarah bomu, acha tumtumie Aisha kama mtego" Harry aliongea huku akimuangalia Tekso,
"hatutofanya kosa kipindi hiki, remote ya Bomu nitakuwa nayo mimi" Tekso aliongea huku akiioneha remote ndogo iliyokuwa kwenye mfuko wake wa shati.
***********************
Mishale ya saa nne usiku, ndani ya gari alikuwepo Harry na Trigger waliokuwa siti ya mbele na siti ya nyuma walikuwepo Aisha na Tekso.
Walikuwa wanaelekea maeneo ya kituo cha polisi kwenda kumtorosha Sarah.
Na kwa upande wa kituo cha polisi Sarah alikuwa amewekwa juu ya kiti huku akiwa pembeni yake amekaa Sajenti Minja na askari mwingine ambaye walikuwa walikuwa wanamuhoji Sarah,
"je tukisema una hatia ya kumteka mgonjwa na kumtorosha ndani ya hospitali, utakubali?" Sajenti Minja alimuuliza Sarah, lakini Sarah hakujibu,
"huyu tumpige kidogo ili alainike, la sivyo atatusumbua sana" Askari mwingine aliekuwepo hapo aliongea kwa hasira,
"muache kwanza" Sajenti Minja aliongea huku akimsogelea jirani Sarah,
"sasa mtu gani tunamuuliza maswali muda wote na wala hajibu?" Askari mwingine alihoji huku akiona Sajenti Minja anamlea sana Sarah,
"Sarah, kesho itabidi upelekwe mahakamani, acha tufanye una hatia na una kesi ya kujibu" Sajenti Minja aliongea huku akimtazama Sarah, ila Sarah hakujibu,
"mpige hata kofi" Askari aliongea huku akionekana kutamani sana kumuhadhibu Sarah,
"mpige" Sajenti Minja alimruhusu yule askari, yule askari akawa anamfuata Sarah kwa hasira, ila kabla hajamfikia wakasikia mlio wa bunduki nje ya ofisi, Sajenti Minja na mwenzake wakatizamana,
"kuna nini" Sajenti Minja aliuliza huku akiwa hategemei jibu,
"nipo mimi" Aisha aliongea huku akiingia kwa fujo ndani ya ile ofisi na kufanya watu wote kuchanganyikiwa, Aisha alikuwa na bastola mbili mikononi,
"nipeni huyo mwanamke kwa amani au nipeni kwa kumwaga damu" Aisha aliongea huku bastola akiwa amewaelekezea Sajenti Minja na mwenzie,
"wewe ni nani unayetutisha polisi?" Askari mwingine aliuliza huku akimtazama Aisha, ila Aisha hakujibu alimfyatulia yule askari risasi ya kifua, akadondoka na kufa pale pale,
"mfungue huyo demu, au hujanielewa bado?" Aisha alimuuliza Sajenti Minja huku akitabasamu, wakati huo Sarah alikuwa ahamini ni kwa nini Aisha amekuja kumuokoa?
Sajenti Minja akamsogelea Sarah na kuanza kumuondoa pingu mkononi, kisha alipomaliza, Sarah akasimama,
"Sarah mfunge pingu huyo polisi" Aisha alitoa amri, Sarah akachukua mikono ya Sajenti Minja na kuifunga,
"nifuate" Aisha aliongea na Sarah akawa anamfuata kwa nyuma, njiani alipishana na askari kadhaa wakiwa wamefumgwa kamba na wengine wakiwa wamekufa, Sarah akawa anajiuliza hiyo shughuli yote amefanya Aisha?
Walifanikiwa kutoka mpaka nje, kisha Aisha akamshika mkono Sarah na kuanza kukimbia nae, walikimbia mpaka kwenye daraja walilokubaliana na wenzake, muda wote Tekso alikuwa juu ya jengo moja refu akiwasiliana na Harry huku akimuangalia Aisha,
"mkuu, wameshafika darajani" Tekso aliongea kupitia kifaa maalum, aliongea na Harry,
"walipue" Harry aliongea na kisha Tekso akatoa remote yake ndogo na kuishika mkononi, akatabasamu.
Harry Trigger walikuwa ndani ya gari wakimsubiri Tekso amalize kazi ili waondoke. Wakiwa hapo ukasikika mlipuko mkubwa mpaka gari yao ikatingishika, Harry akatabasamu na kisha akashusha kioo cha gari,
"good job" Harry aliongea huku akitabasamu, kwa maana kazi ilikuwa imeisha rasmi.....................
************ITAENDELEA***********
the Legend☆