RIWAYA : SALA YA SARAH
MTUNZI : ALEX KILEO
SEHEMU YA HAMSINI NA MBILI.
ENDELEA..................
Sajenti Minja aliamua kumrudia babu yake Sarah, aliona kupitia huyo mzee anaweza kupata kitu kingine cha ziada, Sajenti Minja alitelemka mpaka chini ya jengo na kuingia kwenye gari lake, akawasha na kutaka kuliondoa, ila alisikia mtu akigonga kioo cha upande wa pili, akamtupia jicho na kukuta ni yule mzee, babu yake Sarah,
"ingia ndani ya gari, nilikuwa nakufuata" Sajenti Minja aliongea huku akishusha kioo cha gari, Babu yake Sarah akafungua mlango na kuingia ndani ya gari,
"kuna nini tena? Mbona unanistua?" Babu yake Sarah aliuliza huku akirudishia mlango wa gari,
"kuna maswali nilisahau kukuuliza" Sajenti Minja aliongea huku akizima gari, aliamua amuulizie hapo hapo,
"uliza, tena hapa nitakujibu vizuri kwa kuwa kule juu yule mwanamke alikuwa anaingilia sana mahojiano" Babu yake Sarah aliongea,
"mzee uliposema kwamba ulitekwa na nyumba yako ikachomwa moto, kuna kesi kama hiyo ilitokea miaka kumi na tisa iliyopita, kuna bwana mmoja anaitwa Isack, aliteketezwa yeye na familia yake, na walikufa wote akabaki mtoto mmoja mdogo wa kike,. Je huyo mtu una uhusiano nae gani?" Sajenti Minja aliongea na kumfanya babu yake Sarah apoe kidogo, akatulia kwa sekunde kadhaa,
"huyo mtu unayemzungumzia ni mwanangu, alichomwa akiwa ndani ya nyumba, aliteketezwa yeye na familia yake" Babu yake Sarah aliongea kwa upole,
"hujawahi kufuatilia kituo cha polisi na kuhoji juu ya upelelezi wa hiyo kesi unaendelea au lah!? Au ulishakubaliana na matokeo?" Sajenti Minja aliuliza,
"kipindi cha mwanzo baada ya tukio, kulikuwa na polisi ambaye alikuwa akifuatilia na alikuwa anajitahidi sana kuniambia kila hatua anayopiga, ila kwa bahati mbaya, yule polisi nae alikufa baadae hospitali wakati akijitahidi kumlinda huyo binti wa mwanangu ambaye alikuwa amesalimika" Babu yake Sarah alijibu,
"huyo binti yupo wapi sasa hivi?" Sajenti Minja aliuliza,
"yupo uingereza, aliondoka akiwa mdogo sana na sasa hivi ni muajiriwa wa uko, nadhani hata uraia amechukua wa uko" Babu yake Sarah alijibu,
"mara ya mwisho kuwasiliana nae ilikuwa lini?" Sajenti Minja aliuliza,
"muda kidogo, kabla sijatekwa" Babu yake Sarah alijibu,
"jina lake unalikumbuka?" Sajenti Minja aliuliza,
"nitalisahau vipi wakati alipewa jina la marehemu mke wangu. Binti anaitwa Sarah, Sarah isack" Babu alijibu na kumfanya Sajenti Minja akubaliane na hisia zake, sasa Sajenti Minja alishajua kuwa Sarah mwenyewe anaezungumziwa ni huyo Sarah ambaye babu anamponda kila siku na kumuita mtekaji,
"huyo Sarah ukimuona utamjua?" Sajenti Minja aliuliza,
"hapana, ni muda sana sijamuona, miaka kumi na tisa ni mingi sana" Babu yake Sarah alijibu na kufanya Sajenti Minja ajiulize kwanini Sarah anamficha ukweli babu yake?,
"na Taita Unamjua?" Sajenti Minja aliuliza,
"namjua vizuri, mwanangu ambaye ni baba yake Sarah alimuoa mdogo wake Taita" Babu yake Sarah alijibu,
"je, kulikuwa na ugomvi wowote kati ya Taita na Dada yake?" Sajenti Minja aliuliza swali lililomfanya babu ashangae,
"Mimi nitajuaje sasa? Hayo ni mambo yao" Babu yake Sarah alijibu kwa mshangao,
"sawa mzee, nashukuru kwa majibu yako" Sajenti Minja aliongea,
"sasa nipeleke basi nyumbani" Babu yake Sarah aliongea,
"nyumba yako si imeungua mzee?" Sajenti Minja aliuliza kwa hamaki,
"kwa yule mtekaji ndio nyumbani, maana sina sehemu nyingine" Babu yake Sarah aliongea na kumfanya Sajenti Minja acheke,
"wewe mzee ni mtu wa ajabu sana, yaani mtu anakuifadhi lakini bado unamchongea polisi?" Sajenti Minja aliuliza huku akiwa bado anacheka,
"sasa unataka nifiche maovu?" Babu yake Sarah aliuliza,
"endelea kufichua, ila kuwa muangalifu" Sajenti Minja aliongea huku akiindoa gari yake na kuiingiza barabarani.
**********************
Vin alikuwa pembeni ya kitanda cha baba yake, hali ya baba yake haikuwa mbaya kwa maana Aisha alipiga sehemu ambazo hazina madhara sana.
"mzee samahani, ningependa unipe habari za Sarah, maana haiwezekani Harry amuogope kiasi hicho mpaka atake kukuua" Vin aliongea huku akimtazama Taita,
"unataka kujua ukweli kuhusu Sarah?" Taita aliuliza huku akitabasamu,
"ndio, atakuwa ana sababu ya kufanya hivyo, sio mwendawazimu yule kiasi kwamba atake kuua watu hovyo" Vin aliongea kwa kujiamini,
"Sarah ni mtu anayenituhumu kuwa nimemuulia wazazi wake, sasa anataka kulipa kisasi" Taita aliongea na kumfanya Vin ashangae,
"ni kweli uliua wazazi wake?" Vin aliuliza,
"hapana, hata mimi sijui ni kitu gani kiliwaua, ila mama yake ni ndugu yangu, alikuwa ni mtoto wa baba yangu mdogo" Taita aliongea na kumzidishia maswali Vin,
"sasa si bora ufanye mpango wa kumfikisha mahakamani?" Vin aliuliza,
"mahakamani? Haiwezekani, ukae ukijua kuwa mama yako aliuliwa na Sarah, hicho ndicho kinachofanya nishindwe kumpeleka mahakamani, nataka na mimi nilipe kisasi" Taita aliamua kumdanganya Vin ili amtie hasira, na kweli Vin alipata hasira baada ya kusikia kuwa mama yake aliuliwa na Sarah,
"sasa kama ni hivyo, basi naomba hiyo kazi ya kumuua Sarah niifanye mimi" Vin aliongea kwa hasira huku akiwa amekunja ngumi, Taita akageukia upande wa pili na kucheka, aliamini kuwa ameshaanza kumjaza chuki dhidi ya dada yake,
"ukifanya hivyo, hakika hata nikifa, nitakufa kifo cha amani, nilikuwa nampenda sana mke wangu" Taita aliongea kwa huzuni na kufanya Vin azidi kupata uchungu, na kipindi hicho Trigger alikuwa akiingia ndani ya wodi,
"salama hapa?" Trigger aliuliza huku akiwatizama kwa zamu,
"uzima haupo, mwenzako amefanya kitu cha ajabu sana, amenipiga risasi mbili na kisha akampiga Vin risasi moja ya bega" Taita alijibu kwa ukali,
"nani aliyefanya hivyo!?" Trigger aliuliza huku akishangaa,
"Harry, namuhitaji Harry, fanya kila uwezacho kumleta Harry hapa, nahitaji akiwa mzima ili nimuue mwenyewe" Taita aliongea kwa hasira na kumfanya Trigger ashangae zaidi, hakuamini anachokisikia,
"Harry huyu huyu?" Trigger aliuliza kwa mshangao
"fanya nilichokugiza, maswali tutaulizana ukishamleta" Taita aliongea na kufanya Trigger atii amri, Trigger akapiga hatua za kuanza kuondoka, ila ghafla akageuka,
"umesema nimlete hapa? Utamuua hapa hapa?" Trigger aliuliza huku akimuangalia Taita,
"Trigger umri umeenda ujue, acha bangi mdogo wangu, sasa hapa nitamuuaje? Mpeleke kule kambini" Taita aliongea na kumfanya Trigger aondoke zake huku akitabasamu,
"Harry umenyea shuka kipindi cha baridi" Trigger aliongea peke yake huku akitabasamu na pia akitingisha kichwa chake kwa masikitiko.
********************
Sarah alivyotoka kazini, aliamua kupitia katika hotel aliyokuwepo Dokta Pendo, aliingia moja kwa moja mpaka chumbani na kumkuta Dokta Pendo akiwa ameinamia kitandani akiwa na mawazo sana,
"shoga vipi, unamuwaza nani?" Sarah alimuuliza huku akitabasamu, Dokta Pendo akainua kichwa chake na kumkuta Sarah akimuangalia,
"umeingia muda gani?" Dokta Pendo aliuliza huku akijilazimisha kutabasamu,
"sasa hivi tu, vipi umekula?" Sarah aliuliza,
"tayari, nasikia umewapiga polisi asubuhi, Minja alikuwa anakutafuta" Dokta Pendo aliongea kwa utulivu,
"nitaenda kujisalimisha baadae, sasa wangenikamata si ningeshindwa kusaini mikataba, alafu ningeonekana mswahili" Sarah alijitetea,
"umekula lakini?" Dokta Pendo aliuliza,
"bado, nikifika nyumbani nitapika" Sarah alijibu,
"hivi shoga, kumbe Taita ni mjomba wako?" Dokta Pendo aliuliza swali la ghafla lililomstua Sarah,
"nani amekuambia?" Sarah aliuliza kwa mshtuko,
"Minja, Minja alikuja na babu yako, alikuwa akimuhoji na mwisho wa mahojiano tukagundua yule mzee ni babu yako, na pia Taita ni mjomba wako, je ni kweli?" Dokta Pendo aliuliza, ila Sarah hakujibu na badala yake aliinamisha tu kichwa chini bila kujibu,
"na yule mzee amenijua mimi ni nani?" Sarah alimuuliza Dokta Pendo,
"hapana, mzee hajakujua bado" Dokta Pendo aliuliza,
"nadhani wakati umefika, nahitajika kuvua gamba na kubaki na ngozi yangu halisi" Sarah aliongea kwa sauti ya chini ila iliyomfikia vyema Dokta Pendo,
"unamaanisha nini!?" Dokta Pendo aliuliza na kumfanya Sarah ashtuke, maana hakutegemea kama sauti yake ingemfikia Dokta Pendo,
"tunaweza kwenda nyumbani mara moja?" Sarah aliuliza,
"kufanya nini?" Dokta Pendo aliuliza,
"nahitaji kujitambulisha mbele yako na yule mzee, sihitaji kujificha tena" Sarah aliongea kwa sauti tulivu,
"sawa, twende" Dokta Pendo aliongea baada ya yeye mwenyewe kupata shahuku ya kutaka kumjua vizuri Sarah.
Sarah akamsaidia Dokta Pendo na kutelemka nae mpaka chini na wakaingia ndani ya gari, Sarah akawasha gari yake na safari ya kuelekea kwake ikaanza.
Baada ya muda mfupi waliweza kufika nyumbani kwa Sarah, Sarah akatelemka na kufungua geti, kisha akarudi kwenye gari na kuliingiza ndani ya geti, akarudi na kurudishia geti, kisha akamshusha Dokta Pendo na kumuingiza ndani, walimkuta mzee akiwa amekaa sebuleni kifua wazi akitazama runinga, Sarah akamkalisha Dokta Pendo kwenye kiti, kisha yeye akaelekea chumbani kwake, hawakumsemesha kabisa mzee.
Mzee akanyanyuka taratibu na kuelekea nje, alivyofika nje ya geti, mzee akatoa simu na kupiga, alikuwa anawapigia polisi, tena hakupanga kabisa kumpigia Sajenti Minja, aliona hawezi kumkamata Sarah.
Baada ya kumaliza kupiga simu polisi na kuwafahamisha kuwa Sarah yupo pale muda huo, mzee alirudi ndani na kujitupa juu ya kochi bila kumsemesha neno lolote Dokta Pendo.
Baada ya muda Sarah alirudi sebuleni akitokea chumbani, mkononi alikuwa na picha chache za zamani. Sarah akajitupa juu ya kochi na kumsalimia babu yake, kisha akamtupia zile picha mbele yake juu ya meza, mzee akamuangalia Sarah,
"chukua hizo picha uziangalie, labda kuna mtu unaweza kumfahamu" Sarah aliongea huku akimuangalia babu yake, mzee akaokota zile picha na kuanza kuziangalia, akawa anastuka kila anapoangalia picha moja, aliziangalia zote mpaka akazimaliza,
""hizi picha umezitoa wapi?" Babu yake Sarah aliuliza,
"ni za kwangu, na hiyo ndiyo familia yangu, yaani baba yangu, mama yangu na mdogo wangu" Sarah aliongea na kumfanya mzee ashtuke zaidi,
"wewe binti wewe?" Babu yake aliongea huku akitetemeka,
"naitwa Sarah, Sarah Isack" Sarah aliongea na kujitambulisha rasmi kwa babu yake, babu yake akapigwa na bumbuwazi, akainuka kama mshale na kwenda sehemu alipokaa Sarah, akaushika mkono wa Sarah na kugeuza kwa nyuma, akaangalia kwa sekunde kadhaa kisha akamkumbatia Sarah,
"ni kweli, wewe ni Sarah mjukuu wangu, kwa nini ulikaa kimya muda wote huo? Umesababisha nakuchukulia kama muharifu" Babu yake Sarah aliongea kwa huzuni huku akiwa bado amemkumbata Sarah na kipindi hicho akiwa anajiuliza ni kipi babu yake alichokiangalia nyuma ya mkono,
"mzee mbona umemuangalia nyuma ya mkono, kuna nini?!" Dokta Pendo aliuliza,
"kwenye ukoo wetu uwa tunawapaka dawa za asili ambazo uwa zinakuwa kama doa jeusi juu ya kiwiko, wa kwanza anawekwa doa moja na wa pili anawekwa madoa mawili, yaani madoa yanawekwa kwa idadi" Babu yake Sarah aliongea na kumfanya Sarah agundue hicho kitu, maana hilo doa alikuwa analionaga ila alijua limetokea lenyewe tu.
"sasa babu kuna kitu nataka nikuambie, familia yangu haikuungua kwa bahati mbaya, ni Taita ndiye aliyechoma moto nyumba yetu huku baba na mama wakiwa wamefungwa kamba, mimi na sebastian(vin) tulitolewa nje ila baadae nilirudidhwa ndani na kuachwa kisha moto ukawashwa, Sebastian aliondoka na taita. Na mimi nilipona kwenye moto kwa sababu mfanyakazi wa ndani aliniokoa ila yeye alikufa" Sarah aliongea huku akilia na kipindi hicho sasa babu yake na dokta Pendo wakabaki midomo wazi baada ya kusikia kuwa muhusika mkuu ni Taita, na hapo Dokta Pendo ndiye akaelewa ni kwanini Sarah anadili na Taita tu.
"kumbe Taita ndiye muuaji?" Babu yake Sarah aliuliza,
"ila hili jambo msimwambie mtu yoyote, nataka kulimaliza mwenyewe" Sarah aliongea na kumfanya babu yake ashangae,
"na hata ulivyotekwa na kuchomewa nyumba yako, walikuwa wakinitafuta mimi, walidhani wakikuteka wewe, basi watanipata kwa urahisi" Sarah aliongea huku akiwa anatoka machozi na kipindi hicho polisi zaidi ya hamsini walikuwa wameizunguka nyumba ya Sarah baada ya kuarifiwa na babu yake Sarah.
"wote mliopo ndani tunaomba mjisalimishe, msipofanya hivyo itatubidi tutumie nguvu kubwa kuwashurutisha" Sauti ya tangazo kutoka nje ilisikika, walikuwa ni polisi. Sarah akanyanyuka haraka na kuchungulia dirishani na kuona askari kibao, akikimbilia upande wa nyuma napo akakuta askari wengi wakiwa wameizunguka nyumba, Sarah akarudi sebuleni na kujitupa kwenye kochi, alikuwa amekata tamaa, hakuwa na uwezo wa kupambana na askari zaidi ya hamsini. Kipindi hicho babu machozi yalikuwa yakimtoka na kujiona ana hatia,
"ni kosa langu, mimi ndiye niliyeita polisi" Babu yake Sarah aliongea huku akilia na kujilaumu mwenyewe, na wakati huo polisi wapatao kumi wakiwa na silaha mkononi walikuwa wameshavuka geti na walikuwa wakiuendea mlango wa kuingilia sebuleni kwa sarah, sura zao zilionesha kuwa na hasira nyingi sana juu ya mtu wanayemtafuta kwa maana alihaibisha jeshi la polisi kwa kuwapiga na kuwajeruhi askari wenzao kadhaa nyakati za asubuhi..............
**********ITAENDELEA***********
the Legend☆