Riwaya: Mzalendo Kizimbani (Mwalimu Makoba)

Abtali mwerevu

JF-Expert Member
May 5, 2013
637
432
Angalizo:
Nchi inayotajwa kama Nchi yetu, haina uhusiano wowote na nchi ya Tanzania.

Sehemu ya Kwanza

Komandoo Mako alikimbia akiwa kashika kidege kidogo kisichokuwa na rubani, baada ya umbali fulani, akakiachia nacho kikapaa peke yake. Pembeni alilala Komandoo Bwii, huyu alikuwa na kitu mfano wa runinga ndogo akikiangalia kile kidege kidogo na pengine yeye ndiye alikiongoza. Mbele kidogo, walilala Makomandoo wawili, Ado na Moli. Hawa walikuwa wadunguaji. Watu wengi hudhani kazi ya wadunguaji ni kulenga shabaha na kupiga pekee, si kweli, kazi kuu ya wadunguaji ni kufuatilia mienendo ya adui. Komandoo Ado na Moli walikesha usiku kucha wakifuatilia mienendo ya adui, akilala huyu anamwachia huyu, hata sasa mchana wa leo, kila kitu kilikuwa sawa.

Kidege kisicho na rubani kiliifikia kambi ya adui, kikadondosha mabomu pande zote, milipuko ikaitikisa kambi. Adui wengi wakafa, lakini wengine wakabaki. Waliobaki wakajiandaa kupambana, wamezishika vyema bunduki zao tena wamejaa taharuki.

Mako, Bwii, Ado na Moli walishapanda kifaru. Mako alikuwa kiongozi, pengine angetoa amri ya kufanya jambo fulani. Bwii alikuwa dereva wa kifaru hiki, Ado alikuwa mpigaji, ungeona kombora limerushwa, basi hiyo ilikuwa kazi ya Ado. Moli kazi yake ndani ya kifaru ilikuwa kuweka makombora mahali pake tayari kwa kupigwa.

Kifaru kilivurumusha makombora makali yaliyoiharibu kambi ya adui katika namna ya kutisha. Halafu walipofika eneo la kambi ambalo lilitimka vumbi, makomandoo wakashuka ndani ya kifaru. Komandoo Ado na Moli wakapanda juu ya paa katika namna ambayo sijawahi kuiona, huko wangewadungua adui waliosalia, pia wangewalinda wenzao waliokuwa chini. Bwii alitembea taratibu tena kwa tahadhari akiua kila adui aliyekutana naye. Maadui ni wagumu kufa, pamoja na milipuko ile, wapo ambao walisalia na walijaribu kupambana.

Makomando walisafisha kila hatua na sasa hapakuwa na dalili za adui kuwepo. Adui aliteketezwa yeye pamoja na kambi yake. Hakuna chochote cha maana kilichosalia.

Bwii aliwafanyia ishara Ado na Moli, nao wakamfanyia ishara fulani, halafu wakashuka. Wakasimama pembezoni mwa kifaru chao.

“Mwalimu yuko wapi?” aliuliza Bwii.

“Sijamwona… Wewe vipi?” alijibu Ado akimgeukia Moli ambaye hata hivyo alikataa kwa kupeleka kichwa kulia kisha kushoto.

“Huko juu mlikuwa mnafanya nini?” alihoji Bwii.

Mako walimuita Mwalimu. Ni yeye ndiye kawafundisha vijana hawa wakiwa katika kambi ya Makomandoo katika nchi yetu. Ado, Moli na Bwii walifanya mafunzo ya awali ya Uzalendo katika kambi moja, tena wamesoma shule moja ya sekondari walipoishia kidato cha nne na kuamua kuwa wazalendo. Wakiwa pamoja, wakafanya mafunzo ya Jeshi la Wanachi wa Nchi Yetu. Halafu hawakutosheka, wala hawakukaa kazini, wakaunganisha moja kwa moja katika kambi ya Makomandoo, huko wakakutana na Mwalimu wao Mako, tena Mako ndiyo lilikuwa darasa lake la kwanza kufundisha, akiwa kijana kama wao.

Komandoo Bwii alimpenda Mako, bila Mako pengine Bwii asingekuwa Komandoo. Kuna wakati wa mafunzo Bwii aliishiwa nguvu wakati wa zoezi la kutembea umbali mrefu wakiwa wamebeba boti vichwani, Mako alimbeba Bwii mpaka alipopata nguvu za kuendelea mwenyewe.

Kuna wakati Bwii alishindwa kusoma ramani na kuwapoteza wenzake. Wakubwa wakahoji kama Bwii alistahili kuwa hapo, Mako akamtetea kwa kutoa hoja kuwa, Bwii ana vipaji ambavyo ni yeye pekee anayeviona, akaomba apewe muda.

Wakati wa kuruka na parachuti, almanusura Bwii apoteze maisha akiwa angani, badala ya kubofya kitufe upande wa kulia, yeye alipapasa upande wa kushoto akisema, “Parachuti haina kitufeeeee… nakufaaa.” Mako aliruka na parachuti lake, akamfikia Bwii na kumweleza, “Kitufe kipo kulia Komandoo.” Bwii akapapasa upande wa kulia na kukiona kisha akakiminya na kuokoa maisha yake. Baada ya tukio hilo, Bwii akawa mtu jasiri, akafanya mafunzo kwa weredi mkubwa. Akawa jasiri asiyeogopa tena mwenye akili ya mapigano katika mazingira magumu kuliko mtu yeyote, halafu akaibuka kuwa na mwili mkubwa uliojaa misuli. Watu wote wakamuogopa Bwii. Kwa uwezo wake, endapo angebadilika kidogo, angetosha kuleta madhara makubwa.

“Mwalimu yuko wapi?” Bwii aliuliza tena, safari hii kakasirika.

“Hatujamuona,” walijibu Ado na Moli.

“Huko juu mlikuwa mnafanya nini?” aliuliza tena Bwii. Ado aliyechoshwa na swali lake akamdhihaki, “Tulikuwa tunalinda makalio yako yasipigwe risasi.”

Bwii akarusha ngumi. Ado akaikwepa. Moli akashangaa! Halafu Bwii akamkamata Ado, Moli akamkamata Bwii, makomandoo watatu wakasukumana mpaka katika kifaru, halafu Bwii kwa maguvu yake akawasukuma Ado na Moli wakadondoka chini kama furushi.

Haikuwa kizembe wala rahisi kiasi hicho, Ado na Moli wakanyanyuka, miguu yao ya kushoto imetangulia. Halafu Bwii akabeba kipande cha tofali, Ado akapaza sauti, “Bwii, achana na Systema, hapa tunapiga kung’fu… umejaa mwili unadhani tunakuogopa, mpumbavu wewe, raia!”

“Ndiyo, raia!” Moli akadakia. Bwii aliyekasirishwa na kuitwa raia, akatupa tofali chini, akarusha mateke matatu, mawili yakampata Ado, moja likamkosa Moli. Halafu Ado na Moli wakashambulia kwa pamoja, Bwii akarudi nyuma kujihami, vumbi likatimka!

Inaendelea...

Kuwa wa Kwanza Kupokea mwendelezo wa Riwaya hii Kwa kujiunga katika Group la bure WhatsApp. Kujiunga, Gusa Hapa

Tupate Wadhamini:

Soma: Jinsi ya Kuomba Chuo na Mkopo
 
Sehemu ya Pili

“Nyieee, acheni hiyooo… mbayaaa!” alisikika Mako akifoka. Kamshika kiongozi wa kambi ya waasi, mikononi kamfunga pingu.

“Wazi afande,” makomandoo watatu waliitika wakiwa wamekakamaa kwa heshima hata ikawa kama hakuna kilichotokea muda mchache uliopita.

Makomandoo walikaa chini wakiwa na mfungwa wao pembezoni mwa kifaru cha kisasa aina ya Abraham. Kifaru hiki kiliwahi kutumiwa na jeshi la Marekani wakati wa vita vyake na Iraq na kilifanya maangamizi makubwa kiasi cha kupendwa na mataifa mengine. Pamoja na kwamba kifaru kimoja cha aina hii kiliuzwa Shilingi Bilioni 15 za Nchi yetu, tulimudu kununua hata maadui zetu walishangazwa!

Mako aliikamata simu ya kivita, baada ya kubonyeza kwa muda akaanza kuzungumza kwa utulivu mkubwa tena taratibu kiasi cha kila neno kusika vyema.

“Mzalendo moja, Mzalendo nne, ova,” alisema Mako.

“Endelea Mzalendo nne, ova,” ulijibu upande wa pili.

“Mzalendo moja adui ameangamizwa kilomita mbili magharibi… mateka mmoja anashikiliwa, kiongozi wao mkuu, ova.”

“Nendeni Kilomita nane mashariki, Nyangumi Camp, ova.”

“Wazi afande, ova.”

“Nzuri, ova.”

“Wilco, over.”

“Roger, out,” upande wa pili ulihitimisha mazungumzo.

Serikali ya Congo ilikuwa ikisumbuliwa na kikundi cha waasi cha M23. Maelfu ya wakimbizi kutoka katika baadhi ya vijiji vya kando na milima ya Chanzu na Runyoni walionekana wakivuka mpaka kuelekea nchi jirani ya Uganda kufuatia mapigano makali yaliyoendelea kwa muda mrefu.



Vyanzo kutoka asasi za kiraia vilithibitisha kutekwa kwa milima ya Runyoni na Chanzu wilayani Rutshuru ambayo walikuwa wanatumia kama ngome yao kuu chini ya kamanda Sultani Makengeza.

Halafu kukazuka madai kuwa nchi jirani ya Rwanda inasaidia waasi wa M23 kupambana na serikali ya Congo. Madai hayo yalitolewa na serikali ya Congo. Mwenzako akinyolewa, zako tia maji. Hatungekuwa salama kama jirani yetu anashambuliwa. Hapo ndipo jeshi la nchi yetu lilipoingilia kati mzozo huu.

Jeshi lililoshindwa kuteketezwa kwa muda mrefu, lilipigwa dhoruba moja tu na Makomandoo wanne. Naye kiongozi wa Waasi hao, Kamanda Sultan Makengeza, alikuwa chini ya mikono ya Bwana Mako. Sultani Makengeza alikamatwa kama kuku alipokuwa akijaribu kutoroka.

Kifaru aina ya Abraham kilifika na kuingia katika lango la kambi ya Nyangumi. Juu katika mkonga wa kufyatulia makombora, Kamanda Sultani Makengeza alifungwa kamba mikono na miguu hata akawa kama ndafu.

Kifaru kilisimama, wakashuka makomandoo wanne, askari wengine waliokuwa katika kambi hii, walifika kuwapokea hawa mashujaa. Mako alipokea saluti kadhaa kutoka kwa askari aliowazidi cheo na alitoa saluti kadhaa kwa waliomzidi ambao hata hivyo mpaka wakati huo walikuwa watatu. Wenzake, walitoa saluti kwa kila aliyetokea!

Ukiachilia mbali ukomandoo wake, Mako katika jeshi alikuwa na cheo cha kepteni, hata ungeangalia juu ya bega, ungeziona nyota tatu zikimetameta, ishara ya uzalendo uliotukuka. Bwii, Moli na Ado hawakuwa na cheo chochote. Mako aliwaambia baada ya misheni ile kuisha, angewafundisha masomo ya kidato cha nne, kisha wafanye tena mtihani wa kidato cha nne, wakifaulu kwa kupata C tatu, angewafundisha masomo ya kidato cha sita. Kama wangefaulu mtihani wa kidato cha sita, wangechagua waende moja kwa moja chuo cha mafunzo ya uofisa, au waende chuo kikuu halafu waende chuo cha uofisa. Kwa upande wake Mako, yeye alipata kwanza mafunzo ya chuo kikuu, ndipo akaingia katika majeshi, pengine ndiyo sababu ya cheo chake kuwa kikubwa. Halafu Mako hakuyachagua majeshi kama ilivyokuwa kwa wenzake, majeshi yalimchagua Mako. Baadae nitawaeleza!

Mako alikaa ndani ya ofisi ambayo hata hivyo lilikuwa hema. Bila shaka Nyangumi Camp ilikuwa kambi ya muda tu. Alikuwa na wenzake watatu na mbele yao walikaa wakubwa zaidi.

“Mmefanya kazi nzuri, hongereni wazalendo. Kesho mtaanza safari kurejea nyumbani, tayari kuendelea na maj…” mkubwa hakumaliza kauli yake, mlipuko mkubwa ukatokea nje, halafu bunduki za rasharasha zikasikika zikimwaga risasi kwa sauti ya kuogofya.

Inaendelea...

Kuwa wa Kwanza Kupokea mwendelezo wa Riwaya hii Kwa kujiunga katika Group la bure WhatsApp. Kujiunga, Gusa Hapa

Tupate Wadhamini:

Soma: Jinsi ya Kuomba Chuo na Mkopo

Soma: Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi na CV
 
Sehemu ya Tatu

Mashambulizi ya risasi na mabomu yaliendelea kwa muda wa saa 13. Waasi wachache waliosalia walirudi kutaka kumuokoa kiongozi wao, Kamanda Sultani Makengeza.

Mako alijificha pembezoni mwa tanki la chuma, begani kaiweka NLAW, kwa wajuzi wa silaha, silaha hii inafanana na RPG, lakini ina ufanisi zaidi hasa katika ulipuaji wa umbali mfupi. Mako alilenga shabaha yake vizuri, halafu akaachia kombora, kifaru cha adui kikasambaratishwa vipandevipande. Mlipuko ule kule ulaya wanauita ‘fire and forget’ yaani lipua kisha sahau kwani hakuna kitakachosalia baada ya mlipuko.

Silaha hii ya kisasa ilihitimisha mapigano. Bila shaka kama kuna adui aliyefanikiwa kupona, angewaeleza wenzake kuwa Jeshi la Nchi yetu linatumia silaha za kisasa kama ‘Next Generation Light Anti-armour Weapon (NLAW)’ wasingekubaliana naye, wasingeweza kuamini na kama wangefanya uchunguzi, basi wangeliogopa mno jeshi letu.

Baada ya kuhakikisha sasa kila kitu ni salama, askari walikusanyika kukagua nani yupo nani hayupo. Katika kagua kagua ya hapa na pale, iligundulika kuwa shambulio lile la kushtukiza, lilisababisha kupoteza uhai wa askari 14 wa Nchi yetu. Ado, Bwii, Mako na Moli, walihuzunishwa mno na habari hiyo. waliomba waendelee kubaki ili walipe kisasi, lakini walielezwa warejee nyumbani kwani misheni ilikwisha, waliovamia yalikuwa masalia ambayo nayo yameteketezwa. “Hawana nguvu tena, na kamanda wao tunaye,” alisikika kiongozi mwenye cheo kikubwa zaidi, halafu akaongeza, “Nendeni nyumbani wazalendo… mmeleta heshima kubwa kwa nchi yetu.”

Zamani nilijua kuwa, Makomandoo huwa hayalii kwa sababu yamekomaa sana na siyo majitu ya kawaida. Lakini jioni ya leo mambo ni tofauti, makomandoo yalilia, yalilizwa na taarifa ya habari kutoka radio Sauti ya Amerika. Mtangazaji kwa utulivu alisikika akisoma habari, “JESHI la Nchi yetu, limesema kuwa miili ya askari 14 wa Jeshi hilo waliouawawa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) inatarajiwa kuwasili nchini Jumatatu jioni.

Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Nchi yetu, Luteni Jenerali James Matobolwa anaelezea shambulizi la Disemba 7, halijaivunja moyo Nchi yetu katika operesheni zake za amani.

Kwa mujibu wa mkuu wa majeshi huyo shambulizi hilo dhidi ya askari wake wanaolinda amani Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ni baya na halijawahi kutokea tangu vikosi vyake vianze kushiriki Ulinzi wa Amani huko kupitia Umoja wa Mataifa mwaka 2011.

Kutokana na shambulio hilo lililodumu kwa saa 13, Jeshi la Nchi yetu imepoteza askari 14 na wengine 44 wamejeruhiwa, wawili wakiwa hawajulikani walipo na jitihada za kuwatafuta zinaendelea.

Luteni Jenerali Matobolwa amesema shambulio lililotokea DRC ni shambulio ambalo kwa mara ya kwanza jeshi hilo liliamua kutoa taarifa. Ameeleza kuwa shambulio hilo limeleta madhara makubwa.

Hata hivyo amesema kuwa kikosi chao kilichopo DRC bado kina uwezo wa kutekeleza majukumu kwa uhodari, ushupavu, weledi na umahiri stahiki.

Wakati huohuo vyanzo vya habari vimeeleza kuwa Jeshi la Nchi yetu na Serikali ya Tanzania zinaendelea kuchukua hatua stahiki ikiwemo kufanya uchunguzi katika eneo husika.

Desemba 07, mwaka huu jioni sehemu ya Kikosi cha askari wa Jeshi la Nchi yetu kilichopo DRC kulinda amani kilivamiwa na waasi katika kambi ndogo iliyopo eneo la daraja mto Simulike barabara ya kutokea Oicha kwenda Kamango mpakani mwa Uganda Kaskazini Mashariki ya Wilaya ya Beni, jimbo la Kivu Kaskazini. Hata hivyo, shambulio hilo la kuvizia lilizusha mapigano baina ya kikosi cha Jeshi la Nchi yetu na waasi hao ambapo askari wa Jeshi la Nchi yetu waliuawa na wengine kujeruhiwa vibaya. UN imethibitisha,” ilimaliza habari ambayo hata hivyo sina hakika kama ilitaja eneo kwa usahihi. Makomandoo yakalia kwa uchungu. Moli akapandwa na mori, akaipiga teke redio ikaenda kutua mbali ikiwa katika mgawanyiko wa vipande viwili.

Halafu Mako akanyanyuka, mkononi kaikamata M16, akaanza kutembea taratibu kuitoka kambi.

“Mako unakwenda wapi?” Bwii aliuliza.

“Nakwenda kuwatafuta wazalendo wawili ambao hawajulikani walipo!” alijibu Mako.

“Mako… unafanya misheni hiyo kwa ruhusa ya nani?” alihoji Moli.

Inaendelea...

Kuwa wa Kwanza Kupokea mwendelezo wa Riwaya hii Kwa kujiunga katika Group la bure WhatsApp. Kujiunga, Gusa Hapa

Tupate Wadhamini:

Soma: Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi na CV
 
Sehemu ya Nne

“Komandoo hahitaji ruhusa!” alijibu Ado ambaye alikwisha wafikia. Kauli ya Ado iliwashtua wote, hata Mako aliyeanzisha safari hiyo, alishtuka! Halafu Ado akamshika bega Mako, “Twenzetu…” akasema akiongoza njia, halafu akageuka, “atakayebaki ni mwanamke, raia.”

“Taarifa imesema wawili wanatafutwa!” alisisitiza Bwii.

“Umeona hata askari mmoja katumwa kwenda kuwatafuta? Usiwe Bwege Bwii…”

Makomandoo haya, yakakubaliana kwenda kuwatafuta wawili waliotekwa, lakini Bwii akabaki nyuma hata dalili zikaonyesha hakutaka kuungana nao.

Waasi walisambaratishwa, wachache wakarejea kufanya uvamizi, wakasambaratishwa tena, halafu wakateka askari wawili. Pengine wangefika mbali, wangewatumia askari hao kama kinga ama njia ya kulazimisha kutimiziwa maombi fulani. Mako na wenzake walilibaini hilo, ndiyo sababu wapo njiani wanafuatilia nyayo za adui. Kwa vyovyote adui asingefika mbali kwa muda huo, walikuwa na uhakika watu hao hawakuondoka kwa gari bali walitembea.

Wakati wakiendelea kutembea kwa tahadhari wakifuata nyayo za adui, mbele yao waliona pande la jitu nalo likitembea mwendo wa haraka. Wakasimama wakitafakari ni nani jitu lile, lakini ghafla jitu likasema, “Twendeni… fanyeni haraka adui hayuko mbali, ngome yake iko pale ng’ambo ya mto.”

“Sawa Bwii!” alijibu Mako na wenzake, halafu wakaangua kicheko wakishangazwa na ufundi wa Bwii.

Walifika kando ya mto uliotiririsha maji mengi. Giza lilikuwa limekolea na mbu waliwatafuna vilivyo hata ikaonekana ni kama mbu wale waliwasubiri wao. Bwii akachomoa darubini akitazama mbele halafu akaanza kumweleza Mako aliyekuwa pembezoni, “Kilomita mbili baada ya kuvuka mto, tutampata adui.” Halafu akaendelea, “Wakubwa wametupa baraka na wamesema iitwe ‘Oparesheni Okoa.”

“Una akili sana Bwii,” alipongeza Mako.

“Asante mwalimu,” alijibu Bwii. Ado na Moli wakatazamana, wakacheka. Bwii akamkanyaga teke Moli, halafu akampiga kofi Ado. Kimya!

Walitakiwa kuvuka mto uliojaa mamba na viboko wenye njaa, kwa vyovyote vile, walitakiwa kuvuka bila kuyakanyaga maji. Komandoo Moli akishirikiana na Ado, walishughulika na kamba ndefu, Mako alijiegemeza katika mti akiua mbu taratibu, Bwii aliwatazama Ado na Moli.

Ado alirudi nyuma hatua saba, kisha akakimbia mbele hatua saba na kuirusha kamba ambayo ilifungwa kitu kama chuma kwa mbele na ilinasa moja kwa moja katika mti uliokuwa ng’ambo ya mto. Moli kwa msaada wa mbalamwezi, alikwea juu ya mti na kuifunga sehemu ya kamba iliyobakia, wakawa wametengeneza daraja la kamba.

Hawakuwa na wasiwasi juu ya kipande kilichofungwa na Moli, hofu ilikuwa katika ile ncha iliyorushwa na Ado. Kama haikunasa vyema, yeyote ambaye angeanza huenda kamba ingeachia na kutumbukia majini, humo angegeuzwa chakula cha mamba.

Makomandoo walisimama pamoja wakilitazama daraja lao la kamba. Ilionekana kila mmoja alitegea kuwa wa kwanza kuvuka. Baada ya kimya cha dakika mbili, Mako alianza kuukwea mti, ili awe wa kwanza kuvuka.

“Mwalimu…” aliita Moli. Mako akageuka asiyesema kitu. “Mwalimu anayetakiwa kuanza ni yule aliyepewa misheni.”

“Mmiliki wa Oparesheni Okoa, anza kuvuka,” aliamrisha Ado. Bwii akakubali na kuanza kuusogelea mti ili akwee na kupanda juu ya daraja lile la kamba. Lakini ghafla Ado akamsukuma Bwii na kumwambia, “Nitapanda mimi. Wewe una kilo nyingi utakata kamba.”

Moli mwenye wasiwasi akashauri, “Kuwa makini Ado.”

Ado alikwea juu ya mti, akalifikia tawi ambalo lilifungwa kamba, halafu akalala juu ya kamba nayo kamba ikapita katikati ya kifua chake. Halafu mguu wa kushoto akaukunja kidogo ili kupata uwiano, nao mguu wa kulia ukanyooka kuelekea chini. baada ya sekunde kadhaa, akavuta pumzi kisha akaanza kujivuta kwa kutumia mikono yake kuelekea mbele. Jinsi alivyotambaa, ungemuona, ungedhani ni nyoka. Alitambaa kwa kasi bila kuchoka, mamba walipohisi harufu ya chakula, wakaanza kuruka juu wakijaribu kumdaka. Wenzake kule ng’ambo, roho zilikuwa mkononi.

Inaendelea...

Kuwa wa Kwanza Kupokea mwendelezo wa Riwaya hii Kwa kujiunga katika Group la bure WhatsApp. Kujiunga, Gusa Hapa

Tupate Wadhamini:

Soma: Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi na CV
 
Sehemu ya Tano

Akiendelea kujivuta, alifika sehemu ambayo kamba ilikuwa karibu zaidi na maji. Mamba mmoja akaruka kiasi cha kumkaribia, akachomoa bisu lake na kuliachia liingie ndani ya mdomo wa mamba yule, mamba kwa kukwamwa na lile bisu akayapiga maji kwa nguvu, Ado akajitahidi kujivuta, lakini kwa sababu ya mtikisiko ule, kamba ilianza kuachia taratibu upande wa ng’ambo alikoelekea.

Wenzake walishazishika bunduki zao na walielekeza alikokuwa, hata hivyo hakuna ambalo wangeweza kufanya, haingekuwa rahisi kulenga shabaha kumpiga mamba, kosa dogo lingesababisha risasi impate Ado.

Ado alipogundua kamba inaachia, akaanza kujivuta kwa kasi zaidi. Akajivuta… akajivuta… mpaka akautoka mto, akaendelea kujivuta mpaka alipolifikia tawi la mti ambalo ncha ya kamba ilijishikiza. Haraka akakamata tawi, halafu akaichomoa kamba ile na kuifunga upya, safari hii kwa uimara zaidi. kisha akawafanyia ishara wenzake, ishara ya kupiga mluzi ulioashiria njooni wote kamba ipo imara.

Alianza Mako, akafuatiwa na Bwii, nyuma akamalizia Moli. Kamba ilikazwa ikawa juu zaidi hivyo hapakuwa na hofu tena ya kuguswa na wale mamba. Makomandoo walijivuta kwa kasi na tazama, kufumba na kufumbua walikuwa ng’ambo ya mto. Juu ya tawi imara la mti. Walishuka bila kuitoa kamba ile, pengine waliamini wangeitumia baadae wakati wa kurudi.

Sasa makomandoo walikuwa chini ya mti, walipanga namna ya kushambulia kwani tayari eneo la tukio walishalitambua.

Ado na Moli walichukua nafasi. Wote walilala chini na Ado alikuwa ameishika vyema bunduki yake, Barrett M82. Bunduki hii imekuwa kipenzi cha wadunguaji wengi. Silaha hii ina historia ya kustaajabisha. Ilitengenezwa na Bwana mmoja aitwaye Ronnie Barret ambaye alifanya kazi ya kupiga picha na hakuwahi kuwa na uzoefu wa masuala ya silaha. Pamoja na kukosa ujuzi huo, aliweza kutengeneza silaha hiyo akiwa katika gereji yake tena kwa kutumia vifaa vya humohumo gereji. Baadae silaha hii ilijipatia umaarufu na kuanza kuboreshwa zaidi na serikali ikiwemo Marekani.

Makomandoo waligundua kwamba, maadui walikuwa wawili pekee ambao hata hivyo walikuwa mahali pale kwa muda tu na pengine kuna sehemu walitamani kuwafikisha mateka wao.

Watekaji walikuwa wakizunguka hapa na pale na waliweza kuonekana kupitia dirisha dogo. Ado na Moli walisubiri angalau mtekaji mmoja asimame katika usawa wa dirisha kwa angalau sekunde tatu ili waweze kumpiga risasi. Walisubiri kwa muda mrefu na sasa Ado alichoka akamwachia Moli ambaye alilala nyuma ya Barret M82, jicho moja likitazama katika darubini ndogo ya silaha hiyo.

Haikuchukua muda tangu silaha iwe mkononi mwa Moli jambo lililotarajiwa kutokea. Adui alisimama usawa wa dirisha, hakutoka usawa huo, aliganda kwa sekunde zilizotakiwa, halafu ukasikika mlio, “Tuuuuuh…” mtekaji mmoja akadondoka, lakini kumbe chini ya dirisha alikuwepo Bwii, kwa kuwa adui mmoja alibabaishwa na kuanguka kwa mwenzake, Bwii akapanda juu ya dirisha akiwa kaishika bastola aina ya Sig Sauer, akapiga risasi, adui wa pili akadondoka. Wazalendo wakaokolewa!

Ilikuwa furaha katika kambi ya muda baada ya kuwaona Makomandoo wakirudi na askari wawili waliotekwa na waasi. Wazalendo walipongezwa kwa ushujaa wao, waliookolewa wakakumbushwa kuwa, hawakuwa mateka tena na wawe tayari kuendelea na majukumu yao.

Siku iliyofuata, Komandoo Mako, Bwii, Ado na Moli wakarejea nyumbani, wakarejea katika Nchi Yetu, wakiwa kifua mbele kwa uzalendo uliotukuka. Sasa wamo katika dege la kijeshi na muda si mrefu watatua nyumbani.

“Wazee…” Mako alivunja ukimya, wenzake wakamsikiliza kwa makini kwa sababu alionekana anataka kuongea kitu cha maana. Alipoona wote wako makini kumsikiliza, akatengeneza sauti yake, halafu akawatazama kwa sekunde tatu, kisha akasema, “Nilikuwa siamini kama kila kitu kinawezekana hapa Duniani mpaka siku nilipoota nakimbizwa na konokono.”

Makomandoo wakacheka, walizani jambo la msingi kumbe ulikuwa mzaha tu.

“Nisikilizeni,” alidakia Ado, akiwa bado anacheka, halafu akaendelea. “Leo nimegundua maana ya ujinga. Ujinga ni kumaliza darasa la saba bila kujua sifuri inaandikwaje katika namba za kirumi.” Makomandoo wakatazamana, halafu wakacheka.

“Hivi sifuri inaandikwaje kwa kirumi,” aliuliza Moli.

“Humu wote wajinga, hata rubani pale mbele hajui.” Alidakia Bwii, wote wakacheka, hata rubani wa dege lile la kijeshi, mzalendo Tata Marwa, akacheka. halafu dege likaanza kutua, wazalendo wamerudi nyumbani.

Inaendelea...

Kuwa wa Kwanza Kupokea mwendelezo wa Riwaya hii Kwa kujiunga katika Group la bure WhatsApp. Kujiunga, Gusa Hapa

Tupate Wadhamini:

Soma: Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi na CV
 
Sehemu ya Sita

Baba na mwana walikaa katika viti vya rangi ya machungwa katika jukwaa la uwanja wa mpira. Hawakuwa peke yao, watu wengine walifurika katika uwanja huo. Baba na Mwana walikuwa juu kwa idadi ya ngazi tano kutoka mwanzo na mbele yao walilitazama jukwaa la VIP, katika jukwaa hili wangekaa watu waliozaniwa kuwa muhimu ilihali afya zao ziliashiria bado kidogo wa RIP.

Baba alivaa fulana nyeusi, kaptura ndefu ya michezo na chini alivalia makubadhi ya kisasa. Mtoto alivalia suruali ya kubana aina ya ‘traki’, juu alivalia sweta lililoendana na traki yake na rangi yake kijivu, chini alivalia kama baba yake, makubadhi ya kisasa. Wote baba na mwana, sura zao nzuri za kupendeza na juu walifunika vipilipili vyao kwa kuvalia kofia. Baba akivalia kofia nyeusi, na mtoto akivalia kofia nyekundu lakini yenye mistari ya bluu na kutengeneza kitu mfano wa drafti.

Ilikuwa siku ya kusherekea uhuru wa Nchi Yetu, watu wengi walikusanyika ili waweze kushuhudia maonyesho hayo. Ilitakiwa kuingia mapema uwanjani, lasivyo ungeikosa nafasi. Mgeni rasmi alikuwa Rais wa Nchi Yetu, mfupi mnene, jina lake Makapa. Baba na Mwana walifika uwanjani saa mbili asubuhi, na sasa ilitimia saa tano asubuhi na mgeni rasmi alikuwa bado hajafika. Hata hivyo, dalili zilionyesha kuwa, muda wowote Rais Makapa angefika.

Hayawi hayawi hatimaye yalikuwa; aliyesubiriwa sasa alifika. Rais Makapa aliingia akisindikizwa na walinzi wengi, watu wengi uwanjani walisimama kumshangilia, mtoto alipotaka kusimama, baba yake alimshika mabega na kumtaka aendelee kukaa. Halafu akasema na mwanaye, “Wengi wanaosimama wamelipwa, usifuate mkumbo!”

Baada ya shamrashamra za kumkaribisha rais, watu walikaa na ratiba ya maonyesho ikasomwa. Watu walisubiri kwa hamu maonyesho ya Makomandoo yakivunja tofali kwa vichwa na kukaa juu ya misumali. Hata hivyo, tangu wakiwa nyumbani Baba alimweleza mwanae kuwa, tofali wanazovunja Makomandoo hao ni mbichi, hata yeye akipewa anavunja, mtoto hakuelewa, akacheka.

Jukwaa walilokaa baba na mtoto lilitazamana na jukwaa alilokaa rais Makapa.

“Dogo…” baba alimuita mwanae.

“Naam…” mtoto aliitika. Baba akaendelea, “Unaona pale alipokaa Rais Makapa?”

“Ndiyo.”

“Pale analindwa kwelikweli. Ulinzi wake upo katika duara mbili…” baba alieleza, kisha akatoa karatasi na kalamu akaanza kumchorea mtoto huku akizungumza, “Duara la kwanza ni wale jamaa unaowaona karibu yake, unawaona vizuri… wale wenye suti nyeusi, wembamba.”

“Nawaona, lakini natamani ningesogea karibu zaidi ili niwaone vizuri,” alijibu mtoto, baba akatoa darubini kwenye mkoba akampatia. “Chukua hii, sasa tazama unaona vizuri.”

“Ndiyo…” mtoto alijibu akitazama katika darubini. Halafu akaishusha ili kumsikiliza baba.

“Sasa, lile ndiyo duara la kwanza. Duara la pili wapo mbali kidogo. Unamuona yule kulee, duara la pili yule… tazama kwenye darubini, yule kule kwenye kona ya mlango… hebu nipe na mimi nimtazame vizuri… asante… haya na wewe tazama.”

“Unawezaje kuwatambua?” aliuliza mtoto.

“Nywele zao fupi, wamevaa suti na namna wanavyosimama. Lakini wengine hatuwezi kuwatambua. Wamevaa kama sisi na wamejichanganya humuhumu.”

Baba alikohoa, akafikicha macho kidogo halafu akazungumza, “Kuna kosa la usalama naliona, pakitokea mtu mwenye nia mbaya anaweza kummaliza kiongozi wetu.”

“Kosa gani?” aliuliza mtoto.

“Kosa lililofanywa na walinzi wa Muhammad Anwar el-Sadat. Unakumbuka nilikusimulia namna rais huyu alivyouawa akiwa uwanjani kwenye tukio kama hili la leo.”

“Ndiyo nakumbuka!”

“Sasa nyanyua darubini yako, tazama halafu uniambie makosa unayoyaona,” alisisitiza baba, mtoto akanyanyua darubini akatazama kwa udadisi. Baada ya muda akasema, “kwanza kiongozi katika eneo la mbele hana kitu kinachomzuia asipigwe risasi, hata mimi naweza kushambulia ukizingatia getini tulipita bila ukaguzi wowote. Pili naona magari ya majeshi hayana alama yoyote zaidi ya rangi ya kijani. Wahalifu wanaweza wakaingia na magari yanayofanana na yale ya kijeshi, watu wote na vyombo vya usalama vikajua ni sehemu ya maonyesho, halafu wahalifu hawa wanaweza kusogea karibu kabisa na kiongozi wetu kwa mwendo wa haraka na kumsababishia madhara. Kingine naona kosa kubwa sana, hili…” hakumaliza kauli yake, mtoto alinyang’anywa darubini na mwanamume mrefu aliyevalia suti, alipotazama mbele, alimuona baba yake akikokotwa na jamaa mwingine mrefu, walipokutanisha macho baba akatabasamu hata hivyo tabasamu lake liliashiria alikuwa katika matatizo.

Inaendelea...

Kuwa wa Kwanza Kupokea mwendelezo wa Riwaya hii Kwa kujiunga katika Group la bure WhatsApp. Kujiunga, Gusa Hapa

Tupate Wadhamini:

Soma: Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi na CV
 
Sehemu ya Saba

Baba na mwana walitolewa uwanjani katika namna ambayo watu wengi hawakuelewa. Zoezi liliendeshwa taratibu, wachache walishangazwa lakini wakapuuza kwani hakukuonekana purukushani yoyote. Vyombo vya usalama vya nchi yetu huwa havipuuzi kitu. Japo jambo hilo lilionekana dogo, huku nyuma ulinzi uliimarishwa mara dufu!

Baada ya kutembea kwa gari kuelekea kusikojulikana, hatimaye Baba na mwana waliingizwa ndani ya chumba kilichokuwa na viti vinne na meza moja. Walikwenda moja kwa moja wakakaa katika viti viwili vilivyofuatana.

“Dogo,” baba aliita, akamtazama mwanae aliyekaa tulivu katika kiti. “Hiki ni chumba cha mahojiano, jamaa wametuhisi vibaya kuhusu ile darubini yetu na tuliyokuwa tukizungumza uwanjani.”

“Watatufanya nini?”

“Watatuhoji. Sema ukweli tu, usidanganye jambo hata moja… nami nitasema ukweli. Lakini nitawasumbua kidogo.”

“Ha ha haaa!” Mtoto alicheka, halafu akauliza, “Tutakaa humu mpaka saa ngapi?”

“Muda wowote watakuja kutuhoji. Lazima wawe wawili. Mmoja anasimama kama shahidi wa mwingine. Halafu wamekosea, hatukutakiwa kuwekwa sehemu moja, ilitakiwa wewe ukae peke yako na mimi peke yangu.”

Baada ya saa mbili za kuwa ndani ya chumba, waliingia watu wawili kama alivyosema Baba. Wote walivalia suti nyeusi na walikaa katika viti viwili vilivyosalia hata wakawa wanatazamana uso kwa uso na washukiwa wao. Katika watu hawa wawili walioingia, mmoja alikuwa mnene na mwingine mwembamba. Yule bwana mnene akachomoa bastola na kuiweka mezani. Baba kwa masikitiko, akaweka kiganja cha mkono wake juu ya macho ya mwanaye, hakutaka aone jambo hilo. Bwana mnene kwa kutambua hilo, akaitoa silaha na kuirejesha kiunoni, Baba naye akatoa viganja juu ya macho ya mtoto.

Yule bwana mwembamba akamkazia macho baba na kumuuliza, “Naweza kukuuliza maswali?”

“Unaweza kuniuliza maswali mengi utakavyo. Lakini siwezi kujibu mpaka awepo mwanasheria wangu,” baba alijibu kwa kujiamini, mtoto akatabasamu.

“Unaweza kuwasiliana na mwanasheria wako ili tukuhoji ukiwa naye?” bwana mnene aliongeza.

“Hapana… sina mwanasheria,” baba alijibu, safari hii mtoto hakuishia kutabasamu, akaangua kicheko.

“Unajua kwa nini uko hapa?” mwembamba aliuliza.

“Hapana.”

“Umetumwa na nani kumdhuru mtawala wetu?”

“Sijatumwa na mtu, wala sina nia ya kumdhuru mtawala.”

“Maarifa gani yalikupa ufahamu wa mapungufu ya walinzi wa watawala?”

“Swali limezunguka sana. Lakini mimi husoma katika vitabu kujipatia maarifa pekee. Yote ninayoyafahamu hayahusiani na kundi lolote ovu.”

“Kwa nini unachunguza masuala ya usalama wa mtawala?”

“Ni kiongozi wangu, sioni ubaya nami kuhakikisha kweli yupo salama.”

“Jina lako nani?”

“Baba,” Baba alijibu.

“Baba nani?”

“Baba Mako.”

“Jina la tatu?”

“Baba. Sasa kamilisha hivi: Baba Mako Baba.”

“Mtoto jina lako nani?” Mnene aliuliza akitabasamu.

“Siwezi kujibu chochote bila mwanasheria wangu,” mtoto alijibu.

“Mpigie simu mwanasheria wako aje.”

“Sina mwanasheria,” mtoto alijibu. Baba akamtazama, akaangua kicheko.

“Jina lako nani?”

“Mako.”

“Jina la pili.”

“Ongeza jina la huyu mzee.”

“Jina la tatu?”

“Shuleni jina langu kamili ni hilo, sina jingine.”

“Ulijifunza wapi kuhusu usalama wa watawala na mapungufu yake.”

“Kanifundisha Baba.”

“Yeye kajifunza wapi?”

“Kuna wakati husoma vitabu, kuna wakati hutazama mtandaoni na kuna wakati hutunga hoja zake mwenyewe.”

“Una miaka mingapi?”

“Saba.”

“Unasoma darasa la ngapi?”

“Darasa la pili.”

“Asante kwa ushirikiano,” Mwembamba alisema akimshika mkono Mako.

“Baba upo huru kurejea nyumbani,” Mnene alizungumza, Baba akamshika mkono mwanaye ili watoke. “Mtoto bado tuna mahojiano naye, atarudi yakikamilika,” Mwembamba alisisitiza akiamuru Baba aondoke mwenyewe.

Baada ya mabishano ya muda, Baba alikubali kuondoka. Siyo kwa sababu alizidiwa hoja, lakini hakuwa na nguvu za kuweza kutoka na mwanaye. Kwa upole akaaga, “Baki salama Mako… Sema ukweli, usiwasumbue bila mimi kuwepo watakuumiza ukileta mchezo,” mtoto asiyeamini kama alitakiwa kusalia mule akajibu kwa upole, “Sawa.”

Inaendelea...

Kuwa wa Kwanza Kupokea mwendelezo wa Riwaya hii Kwa kujiunga katika Group la bure WhatsApp. Kujiunga, Gusa Hapa

Tupate Wadhamini:

Soma: Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi na CV
 
Sehemu ya Saba

Baba na mwana walitolewa uwanjani katika namna ambayo watu wengi hawakuelewa. Zoezi liliendeshwa taratibu, wachache walishangazwa lakini wakapuuza kwani hakukuonekana purukushani yoyote. Vyombo vya usalama vya nchi yetu huwa havipuuzi kitu. Japo jambo hilo lilionekana dogo, huku nyuma ulinzi uliimarishwa mara dufu!

Baada ya kutembea kwa gari kuelekea kusikojulikana, hatimaye Baba na mwana waliingizwa ndani ya chumba kilichokuwa na viti vinne na meza moja. Walikwenda moja kwa moja wakakaa katika viti viwili vilivyofuatana.

“Dogo,” baba aliita, akamtazama mwanae aliyekaa tulivu katika kiti. “Hiki ni chumba cha mahojiano, jamaa wametuhisi vibaya kuhusu ile darubini yetu na tuliyokuwa tukizungumza uwanjani.”

“Watatufanya nini?”

“Watatuhoji. Sema ukweli tu, usidanganye jambo hata moja… nami nitasema ukweli. Lakini nitawasumbua kidogo.”

“Ha ha haaa!” Mtoto alicheka, halafu akauliza, “Tutakaa humu mpaka saa ngapi?”

“Muda wowote watakuja kutuhoji. Lazima wawe wawili. Mmoja anasimama kama shahidi wa mwingine. Halafu wamekosea, hatukutakiwa kuwekwa sehemu moja, ilitakiwa wewe ukae peke yako na mimi peke yangu.”

Baada ya saa mbili za kuwa ndani ya chumba, waliingia watu wawili kama alivyosema Baba. Wote walivalia suti nyeusi na walikaa katika viti viwili vilivyosalia hata wakawa wanatazamana uso kwa uso na washukiwa wao. Katika watu hawa wawili walioingia, mmoja alikuwa mnene na mwingine mwembamba. Yule bwana mnene akachomoa bastola na kuiweka mezani. Baba kwa masikitiko, akaweka kiganja cha mkono wake juu ya macho ya mwanaye, hakutaka aone jambo hilo. Bwana mnene kwa kutambua hilo, akaitoa silaha na kuirejesha kiunoni, Baba naye akatoa viganja juu ya macho ya mtoto.

Yule bwana mwembamba akamkazia macho baba na kumuuliza, “Naweza kukuuliza maswali?”

“Unaweza kuniuliza maswali mengi utakavyo. Lakini siwezi kujibu mpaka awepo mwanasheria wangu,” baba alijibu kwa kujiamini, mtoto akatabasamu.

“Unaweza kuwasiliana na mwanasheria wako ili tukuhoji ukiwa naye?” bwana mnene aliongeza.

“Hapana… sina mwanasheria,” baba alijibu, safari hii mtoto hakuishia kutabasamu, akaangua kicheko.

“Unajua kwa nini uko hapa?” mwembamba aliuliza.

“Hapana.”

“Umetumwa na nani kumdhuru mtawala wetu?”

“Sijatumwa na mtu, wala sina nia ya kumdhuru mtawala.”

“Maarifa gani yalikupa ufahamu wa mapungufu ya walinzi wa watawala?”

“Swali limezunguka sana. Lakini mimi husoma katika vitabu kujipatia maarifa pekee. Yote ninayoyafahamu hayahusiani na kundi lolote ovu.”

“Kwa nini unachunguza masuala ya usalama wa mtawala?”

“Ni kiongozi wangu, sioni ubaya nami kuhakikisha kweli yupo salama.”

“Jina lako nani?”

“Baba,” Baba alijibu.

“Baba nani?”

“Baba Mako.”

“Jina la tatu?”

“Baba. Sasa kamilisha hivi: Baba Mako Baba.”

“Mtoto jina lako nani?” Mnene aliuliza akitabasamu.

“Siwezi kujibu chochote bila mwanasheria wangu,” mtoto alijibu.

“Mpigie simu mwanasheria wako aje.”

“Sina mwanasheria,” mtoto alijibu. Baba akamtazama, akaangua kicheko.

“Jina lako nani?”

“Mako.”

“Jina la pili.”

“Ongeza jina la huyu mzee.”

“Jina la tatu?”

“Shuleni jina langu kamili ni hilo, sina jingine.”

“Ulijifunza wapi kuhusu usalama wa watawala na mapungufu yake.”

“Kanifundisha Baba.”

“Yeye kajifunza wapi?”

“Kuna wakati husoma vitabu, kuna wakati hutazama mtandaoni na kuna wakati hutunga hoja zake mwenyewe.”

“Una miaka mingapi?”

“Saba.”

“Unasoma darasa la ngapi?”

“Darasa la pili.”

“Asante kwa ushirikiano,” Mwembamba alisema akimshika mkono Mako.

“Baba upo huru kurejea nyumbani,” Mnene alizungumza, Baba akamshika mkono mwanaye ili watoke. “Mtoto bado tuna mahojiano naye, atarudi yakikamilika,” Mwembamba alisisitiza akiamuru Baba aondoke mwenyewe.

Baada ya mabishano ya muda, Baba alikubali kuondoka. Siyo kwa sababu alizidiwa hoja, lakini hakuwa na nguvu za kuweza kutoka na mwanaye. Kwa upole akaaga, “Baki salama Mako… Sema ukweli, usiwasumbue bila mimi kuwepo watakuumiza ukileta mchezo,” mtoto asiyeamini kama alitakiwa kusalia mule akajibu kwa upole, “Sawa.”

Inaendelea...

Kuwa wa Kwanza Kupokea mwendelezo wa Riwaya hii Kwa kujiunga katika Group la bure WhatsApp. Kujiunga, Gusa Hapa

Tupate Wadhamini:

Soma: Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi na CV
Jaman nzuri
 
Sehemu ya Nane

Mara baada ya kukitoka chumba cha mahojiano, Baba alivikwa kitambaa cheusi. Akaongozwa na watu wawili mpaka ndani ya gari muundo wa SUV nyeusi. Waliendesha mpaka mahali ambapo Baba alivuliwa kitambaa hicho, breki zikakanyagwa, mlango ukafunguliwa halafu akasukumwa nje akadondoka kama mzigo. Isingekuwa tabia ya kufanya mazoezi na kula mlo sahihi, Baba angevunjika mfupa wa paja.

Baba akiwa chini, alishuhudia gari ikienda mbele, kisha ikakunja kona na kurudi ilipotoka, ikampita kwa kasi ikimtimulia vumbi. Alifanikiwa kumuona dereva wa gari ile, kijana mdogo mwembamba, nywele zake fupi, bila shaka hata aliyemsukuma naye alikuwa kijana mdogo tu. Hata akawaza hasa kama vijana wale walitambua maana ya kuaminiwa na kuwa sehemu ya usalama wa Nchi Yetu. Halafu akawaza, vipi kama mwanaye angeshushwa kwa mtindo ule, mifupa yake laini, mtoto Mako asingeweza kuhimili!

Baba alijizoazoa pale chini aliyekatishwa tamaa na walioaminiwa kutulinda. Aliposimama akapiga mikono yake akitingisha kichwa ishara ya kukata tamaa. Akaanza kutembea akijaribu kutafakari ni wapi mahali hapo. Alitembea mwendo mfupi akiifuata barabara ile ya vumbi, mbele akaiona barabara ya lami na kama bahati akaiona daladala iliyosimama ikisubiri wapandaji. Konda alimuona Baba. “Dingii, Kumbukumbu unaenda?”

Kusikia hivyo, Baba akaongeza mwendo na kuingia ndani ya daladala ile. Alibaini kuwa, mahali pale palikuwa Manunio. Akiisha kukaa katika kiti, mwisho kabisa wa daladala tena dirishani, akatazama njia ya vumbi alikotokea, kule alikosukumwa na vijana wadogo walinzi wa usalama wa Nchi Yetu, kwa sauti ya chini, akakohoa laana, akawalaani vijana wale, akawaombea jambo baya liwakute. Kisha akaganda kama barafu gari ilipoanza kuelekea Kumbukumbu.

Alipofika kumbukumbu alipanda gari nyingine iliyompeleka nyumbani kwake. Alifika nyumbani saa moja usiku, akaingia chumbani akimpita Mama aliyekaa sebuleni. Mama alisubiri dakika mbili, kisha akapaza sauti, “Mmeondoka wawili umerudi peke yako. Mtoto yuko wapi?”

“Dume lile. Limechukuliwa na baba yake mdogo, litakuwa limeshafika Magomeni muda huu,” Baba alidanganya. Mama akanyamaza, maamuma asiyejua kitu.

Kulikucha asubuhi, Baba akakaa nje akisubiri kumuona mtoto akiletwa au akija peke yake. Asubuhi ikapita bila mtoto kufika. Ukafika mchana, mtoto hakufika, kuelekea jioni, Baba akakodi gari binafsi mpaka Manunio, kule alikotupwa na wale vijana wadogo. Alifika eneo lile, akakagua, lakini hapakuwa na dalili ya kushushwa mtu. Hapakuwa na dalili ya nyayo za Mako. Baba akarejea nyumbani.

Baba alimpita Mama sebuleni, akaenda moja kwa moja mpaka chumbani. Mama akapaza sauti, “Baba mdogo alifika hapa kututembelea jioni. Ulipotoka yeye akaingia. Nimemuuliza mbona kaja peke yake bila mtoto hajajibu. Sasa nieleze, mtoto yuko wapi?”

“Kwani mwanao ana baba wadogo wangapi?” Baba aliuliza.

“Wengi.”

“Sasa huyo Baba mdogo aliyekuja una uhakika gani kuwa ndiye aliyemchukua mtoto?”

“Ulisema Magomeni, wa Magomeni kaja.”

“Nilisema atakuwa ameshafika Magomeni, yaani katikati ya safari yake kulekea Magambani.”

“Ahaaa kumbe kaenda kwa baba yake wa Magambani Mwasonga! Basi nikawaza sana…”

“Acha hizo, toto la kiume halichungwi,” Baba alihitimisha. Lakini atadanyanya mpaka lini? Njia ya muongo fupi!

Inaendelea...

Kuwa wa Kwanza Kupokea mwendelezo wa Riwaya hii Kwa kujiunga katika Group la bure WhatsApp. Kujiunga, Gusa Hapa

Tupate Wadhamini:

Soma: Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi na CV
 
Sehemu ya Tisa

Katikati ya huzuni baba alipata chembe ndogo ya furaha. Mama aliaga kwamba, kesho angesafiri kwenda kwao kumuuguza mama yake aliyekuwa mgonjwa mahututi. Kusikia hivyo, Baba akasisitiza, “Kesho mapema sana uanze safari. Mama ni Mungu wa pili.” Jambo hili lingempunguzia makelele na maswali arudipo nyumbani. Hata hivyo halikuwa suluhisho la muda mrefu.

Asubuhi Baba alitoka akimsindikiza Mama mpaka kituo cha magari ambako Mama alipanda na kuianza safari. Baba aliendelea na msako wa mtoto wake. Leo alipita kituo hiki cha polisi akaenda kile. Kisha hapa halafu pale, huku tena kule lakini kote alikopita hakumpata mtoto. Tena vituo vingi vilimwambia havijapokea mtoto mahabusu tangu mwaka uanze.

Baba akaanza kutembelea mahospitali, nako hakumpata mwanae. Hakukuwa na dalili, hakukuwa na chochote. Aliyechoka sana, akarejea tena Manunio, barabara ile aliyotupwa na walinzi wa Nchi Yetu, alipofika, hapakuwa na dalili, Mako hakuwako!

Baba alirudi nyumbani kachoka hoi bin taabani, sisimizi mdogo angetosha kumpiga kikumbo na kumdondosha chini, ni bahati tu, sisimizi hawakulijua hilo. Alipitiliza moja kwa moja mpaka chumbani akalala usingizi wa mang’amung’amu, japo hakushusha chandarua, mbu hawakujisumbua kumnyonya damu, walikuwa waungwana, hawakutaka kuongeza matatizo kwa mtu mwenye matatizo.

Saa kumi na mbili asubuhi Baba aliamka. Akaenda moja kwa moja bafuni ambako alifanya shughuli za kusafisha mwili kisha akerejea chumbani akiongea peke yake, “Inawezekanaje mtoto apotee mikononi mwa wanausalama? Wamemuua? Ama wanataka kumfanya muuaji? Wanataka kunitenga naye? Wanataka nini kwa mwanangu? Ndiyo kusema sitamwona tena Mako?”

Baba akavaa nguo zake, shati pana na suruali pana kidogo. Juu akavaa kofia iliyokaa kama sufuria katika kichwa chake cha duara, halafu akavaa kiatu ambacho huvaliwa na wachezaji wa mpira wa kikapu. Kisha akasikika akisema, “Vita imeanza… dhuluma humfanya mwanadamu awe mwovu.”

Baba akaenda katika chumba anacholala mwanae. Alipofika humo akapatwa na uchungu mkali, akadondoka chini akifikia magoti, akainamisha kichwa chake na kuangua kilio kikubwa! Akanyamaza ghafla kama jenereta lililoishiwa mafuta, akaiendea kabati kubwa ambayo huwekwa vitu vya kuchezea mwanae, hapo akaichukua bastola ndogo nyeusi, akaifungua taratibu na kuiweka kipande cha mbao humo ndani ili kuipa uzito unaofaa.halafu akasogea katika kioo, akajitazama kuanzia juu mpaka chini, mkononi akiwa na bastola, akafuta machozi yaliyokuwa yanachuruzika, akacheka! Mara akanuna! Akacheka tena! Akanuna, kisha akawa katika hali ya kawaida.

Baba anayo gari ndogo yenye muundo wa ‘hatchback’, huiendesha kwa nadra sana kwani mara nyingi hupendelea kutumia usafiri wa umma. Yeye husema kuwa, usafiri wa umma ni nafuu kuliko gari binafsi. Aliifuta vumbi, akafungua na kukagua injini, akakagua tairi na kuona mambo yako sawa, akakaa nyuma ya usukani, akaiwasha, akaiacha ichemke kidogo, akakanyaga breki, halafu gia akaisogeza palipoandika D, akaachia breki, gari ikaserereka, akakanyaga pedali nyingine, gari ikaserereka zaidi.

Baada ya kuendesha kwa muda, alikunja kushoto akaiingia barabara iliyoelekea Poste. Akaendelea kuendesha mpaka alipofika katika kituo cha daladala, akashuka na kuiacha gari mahali pale.

Alitembea taratibu akiangalia askari waliolinda benki ile. Walikuwa wawili, mmoja ana bunduki, akaona si rahisi kuwavamia, akatembea taratibu akifuata njia iliyonyooka, halafu akakunja kushoto, akatembea hatua kama sitini na tano hivi na kuufikia ubalozi wa Ufaransa. Hapo napo akaona askari wawili, mmoja ana bunduki, mwingine hana. Alipokutanisha nao macho, akavuka barabara, akazunguka na kurudi pale alipoegesha gari. Kisha akaona jambo la kuvutia, askari mmoja hakuwepo, yule mwenye bunduki aliiegesha katika bega, na alikuwa amesogea usawa wa barabara tena anaongea na simu akiwa kachuchumaa. Alisogea taratibu mpaka usawa wa askari yule, akasimama mbele yake, askari alipoinua uso, akakutana na mdomo wa bastola. “Tulia hivyo hivyo… ukijitingisha namwaga ubongo wako,” ilisikika sauti, kisha bunduki ile aina ya SMG ikapigwa teke na Baba na kudondoka chini, baada ya Baba kuona askari yule akitetemeka, aligundua asingeweza kumletea shida, hivyo akaiokota SMG na kuivaa kamba ikishika bega la kushoto na kuzuiwa na shingo, silaha ikining’inia upande wa kulia. Baba hakuchelewa, akatoa pingu na kumfunga askari yule aliyekuwa akitetema kama trekta. Haraka aliyefungwa pingu, askari akaingizwa nyuma ya mlango wa ngari ndogo ya Baba, alipomfikisha hapo, akamsukuma na kuufunga halafu akaingia na kumfunga kamba za miguu pamoja na plasta ngumu mdomoni, halafu akamuonya, “Sisi ni genge baya, ukijaribu kuleta ujanja, tutafyeka ukoo wako mzima, sawa poti?” Poti akakubali kwa kutikisa kichwa, Baba akaiwasha gari na kuendesha.

Kuwa wa Kwanza Kupokea mwendelezo wa Riwaya hii Kwa kujiunga katika Group la bure WhatsApp. Kujiunga, Gusa Hapa

Tupate Wadhamini:

Soma: Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi na CV
 
Sehemu ya 10

Gari ilifika nyumbani, Baba akamshusha mateka wake na kumpeleka katika chumba kilichokuwa tupu. Kwa kuwa alikuwa amefungwa kamba miguuni, alitembea kwa kurukaruka mpaka alipofika kwenye chumba ambacho kilifungwa na kilikuwa giza.

“Jina lako nani?” Baba aliuliza akimtoa plasta ngumu mdomoni mtuhumiwa wake.

“Afande Emma,” alijibu mateka akitetemeka. Baba akamtazama, akagundua afande Emma alikuwa kijana mdogo. Umbo lake dogo, mwembamba hana nyama, kanyoa denge na mwoga wa mapambano.

“Wewe ni hawa vijana wa ajira mpya?”

“Ndiyo, nina miezi mitatu.”

Baba alisitisha mazungumzo, akakumbuka kitu ghafla na kushtuka sana, haraka akamkagua mateka wake mifukoni ambako hakupata kitu.

“Huna simu?” Baba aliuliza.

“Nimeacha nyumbani, huwa sikai nayo napokuwa lindo, siyo salama.”

“Vizuri,” Baba alijibu akishusha pumzi. Halafu akaongeza, “Umesema una miezi mitatu kazini, una miaka mingapi?”

“Kumi na tisa. Nisameheni… naombeni mnisamehe msiniue… familia yangu ni masikini, nategemewa na mama...”

“Genge letu halitakuua, umri wako mdogo sana. Fuata maelekezo na usijaribu kuleta ujanja wowote utakuwa salama,” Baba alisisitiza, halafu akamsogelea mtuhumiwa akimtazama usoni na kumkazia macho kama mchawi, “Usiulize maswali, genge letu halipendi maswali.”

Baba alitoka akimwacha mtuhumiwa wake chumbani. Ilitosha kumfunga kamba za mikono na miguu, hakujali kumziba mdomo, aliamini bwana mdogo asingeleta ujanja wowote.

Baba alizunguka sebuleni, akishika hiki anaacha kile, anawaza na kuwazua, anapanga na kupangua. Halafu aliyekunja sura akaikamata simu ndogo wengine wakiita kiswaswadu. “Hallo RPC!”

“Hallo… karibu nani mwenzangu?”

“Watu huniita Baba… ninataarifa muhimu.”

“Taarifa gani Baba?”

“Nimemteka askari wako mwenye namba E 1324 akiwa lindo katika benki njia ya kuelekea posta… pia ninayo silaha yake, Chinese 56 SMG moja yenye namba PT. 70B… silaha hii nitatumia kumuua endapo hutafuata maelekezo yangu. Halafu nikimuua, nitatoka nayo na kuhakikisha kila risasi iliyosalia inaua mtu fulani! Upo tayari kutoa ushirikiano?”

“Nipo tayari, unataka nini?”

“Siku chache zilizopita, palikuwa na mkutano wa Rais katika uwanja wa taifa, mimi nilikuwa hapo na nilikamatwa na vijana wa usalama wa taifa nikiwa na mtoto wangu. Mimi niliachiwa, lakini mtoto wangu walibaki naye na mpaka sasa sijampata na sina maelezo zaidi kumhusu wala sijui yupo eneo gani. Namtaka mtoto huyo ndani ya saa kumi na saba kuanzia sasa.”

“Umesema usalama wa taifa, jeshi la polisi limeingiaje?” aliuliza RPC lakini asiyeamini kama ni yeye aliuliza swali lile.

“Acha upumbavu RPC, hata jeshi la polisi ni usalama wa taifa, tofauti yenu mshahara. Wasiliana na vitengo vyote vya usalama, waambie nilichokuambia, zimebaki saa kumi na sita,” Baba akakata simu baada ya kumaliza kufoka.

Baba alimchungulia mateka wake, akahakikisha hakusikia kilichosemwa. “Poti, hakuna msosi, genge langu ambalo ni baya sana limesema utakula kesho.”

Akarudi sebuleni, akawa akitembea taratibu, simu ikaita. “Hallo… Baba hapa, mtoto kapatikana?”

“Twende polepole… jina langu ni Mshona, huyo askari na silaha wapo salama?”

“Yupo salama na silaha ipo salama.”

“Uko wapi?”

“Nipo eneo hili ambapo nimepiga simu na nyinyi mmeshafahamu mahali nilipo. Najua kwamba mnaweza kuja kuvamia hapa, lakini nawaahidi, mtu yeyote atakayeingia ndani ya nyumba yangu, atakutana na maiti ya askari.”

Akiisha kusema hayo, akaikoki silaha, nayo ikaitika, “kwacha,” akafungua usalama na kupiga risasi moja juu.

“Baba ngoja… usifanye hivyo… sikiliza…” alilalama Mshona.

“Namtaka mwananguuuuuu!” alilalama kwa nguvu, akapiga risasi nyingine, halafu akafunga usalama na kukata simu.

“Zimebaki ishirini na nane!” alisema akiitazama bunduki, jasho limemtoka, akachungulia nje kutazama kama majirani walipatwa na mshituko, akaona kuko kimya. Akafunga madirisha na milango.

Kuwa wa Kwanza Kupokea mwendelezo wa Riwaya hii Kwa kujiunga katika Group la bure WhatsApp. Kujiunga, Gusa Hapa

Tupate Wadhamini:

Soma: Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi na CV
 
Sehemu ya 11

Akiwa kakaa katika kochi, Baba alisikia msafara wa magari, haraka akachungulia kupitia dirisha akifunua pazia kidogo. Aliona magari manne meusi muundo wake MPV wengine wakiyaita ‘Shangingi’ na wengine huyaita V8. Msafara ule uliposimama, alishuka mwanamume mnene akafuatiwa na mtoto mwenye umri wa miaka saba. Baba alimtambua mwanamume yule, hakutaka kusubiri zaidi, alimchukua mateka wake. “Rafiki zako wamekuja kukuokoa,” Baba alisema akimtazama mateka wake ambaye alimfungua kamba za miguu ili aweze kutembea, halafu akamfungua na ile pingu ili ajihisi huru. “Haya, tangulia mbele,” Baba aliamrisha akiwa kamuelekezea bunduki. Mateka akatembea mpaka ulipo mlango, akazungusha funguo na kukiminya kitasa mlango ukafunguka.

“Babaaaaaah,” Mako aliita kwa sauti. Baba akaitupa silaha, mtoto alikwisha ponyoka katika mikono ya aliyemshikilia, akakimbia na kumrukia Baba ambaye alikuwa na furaha isiyo na kipimo.

“Makooo!” Baba aliita kwa mshangao baada ya kumbeba mwanae na kuamini haikuwa ndoto, bali alikuwa mtoto wake kweli.

Basi akiisha kumbeba na kumzungusha kwa furaha, alimshusha chini. Alipotazama mbele, Baba akashtuka kuona bunduki nne ziikimwelekea. Zilikamatwa vyema na askari wa Nchi Yetu ambao walivaa sare za kaki na katika viuno walifunga mkanda wenye bendera ya taifa kitambulisho cha Nchi Yetu.

“Chini ya ulinzi, weka mikono juu na tembea kuelekea mbele,” alimrisha askari aliyeijua vyema kazi yake. Baba akatii, akatembea mpaka katika gari aliyoelekezwa, akaambiwa aingie humo, lakini kabla hajaingia, akaacha ujumbe. “Mako, kila kitu kipo ndani, baki salama ukiogopa nenda kwa mjomba, mama yako kasafiri… nitarudi usiogope.”

Leo ni siku ya pili Baba yupo mahabusu. Akiwa anawaza hili na lile zaidi akihofia usalama wa mwanae, akasikia sauti ikiita, “Baba.” Hakuitika, alitembea mpaka katika mlango kisha akasema, “Mimi hapa.” Lango likafunguliwa, alipofika sehemu ya kukaa, akamuona Mako akiwa na yule mwanamume mnene.

Zilifanyika taratibu zote Baba akarejeshewa vitu vyake na kutolewa mahabusu. Hata hivyo hakufahamu kilichofanyika na hakuamini kama ilikuwa kweli au ndoto tu.

Wakiwa wamesimama nje, Mako katikati, Baba kulia na mwanamume mnene kushoto, yule mwanamume mnene akanyoosha mkono wake kumpa Baba, Baba akaupokea. “Baba… Umefanya jambo la kipumbavu sana. Kuteka askari ni ugaidi na kosa lake halina msamaha, hata hivyo tumeamua tulimalize jambo hili na tusiende mahakamani kwani kufanya hivyo hakuna faida yoyote. Tukuombe, uhifadhi siri hii lakini huruhusiwi kusafiri nje ya mkoa huu kwa muda wa mwaka mmoja. Tukikuhitaji, kuwa tayari kufika kwa mahojiano na nikutakie utekelezaji mwema.”

Waliachana bila Baba kujibu chochote. Yule bwana mnene akaingia katika gari nyeusi akawasha na kuondoka. Baba na Mako wakatembea kwa mguu kuelekea nyumbani.

“Siku zote una hoja lakini leo umekaa kimya, kulikoni hukuweza kumjibu mtu yule?” aliuliza Mako.

“Naweza kubishana na maprofesa sabini na wote nikawashinda kwa hoja. Lakini siwezi kubishana na mjinga mmoja!” alijibu Baba kwa majigambo. Mako akacheka, wakashikana mikono kuelekea nyumbani wenye furaha tele kama ngedere.

Kuwa wa Kwanza Kupokea mwendelezo wa Riwaya hii Kwa kujiunga katika Group la bure WhatsApp. Kujiunga, Gusa Hapa

Tupate Wadhamini:

Soma: Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi na CV
 
Sehemu ya 12

Wakati haya yanatokea mtoto Mako alikuwa darasa la pili. Maisha yaliendelea vyema, akaingia darasa la tatu, la nne, halafu alipofika darasa la tano, baba akiwa matembezini akakutana na mwalimu.

“Mwalimu salama?”

“Salama… vipi mbona kijana hajaonekana shule wiki nzima hii, na imekuwa kawaida yake, akionekana Jumatatu, basi wiki nzima atakuwepo, lakini asipoonekana Jumatatu wiki nzima hafiki…”

Baba aliyeshtushwa na taarifa ile akamkazia macho mwalimu. “Vipi lakini, ulijaribu kumuuliza huwa anakuwa wapi kwa sababu siku zote anatoka hapa akisema anakwenda shule.”

“Vijana waongo hawa, atakuwa kaanza makundi mabaya… nilimuuliza akasema kuna wakati anabaki kumuuguza bibi yake anayeugulia hapo nyumbani.”

“Kweli dogo muongo, Bibi yake alifariki tangu akiwa darasa la pili!”

“Haaaaah!” mwalimu alishtushwa na habari hiyo, mdomo akaachama na kuufanya uonekane kama pango la wanyang’anyi.

“Lakini mwalimu mimi nakushukuru kwa taarifa. Tukimhoji ataendelea kutudanganya, wewe niachie mimi nitamfuatilia halafu nikibaini anakokuwa, nitakujulisha. Ili tumshikishe adabu kwa pamoja.

Mako aliamka asubuhi, akafanya maandalizi yake ya kwenda shule, akavaa sare, kidume wa miaka tisa kuelekea kumi akatoka na kutembea taratibu. Baba kwa siri, alimfuata nyumanyuma kijana wake aliyeanzisha tabia mpya.

Mako alitembea hatua mia tatu na kumi, mlango wa gari nyeusi ukafunguliwa, akaingia gari ikaendeshwa. Baba akatazama uelekeo wa gari ile, naye akakimbia haraka mpaka nyumbani na kuchukua gari yake, akaitia moto na kuendesha kwa kasi.

Hakuchukua muda mrefu, Baba aliipata gari ile nyeusi, akawa nyuma ya bajaji ili kuepuka kujulikana.

Aliendelea kuifuatilia gari ile kwa mwendo uliochukua dakika arobaini. Ili asijulikane kama anaifuatilia, aliruhusu gari moja mbele ama mahali fulani pasipokuwa na magari mengi, aliacha umbali mrefu.

“Kuna gari inatufuatilia,” ilisikika sauti ya mwanamume akiwa nyuma ya usukani.

“Nimeona muda tu…” aliongeza jamaa aliyekaa pembeni ya dereva.

“Ni Baba yangu… ile gari yake,” alijibu Mako akitazama katika kioo.

“Mfahamishe kwamba tumejua anatufuatilia,” aliagiza jamaa aliyekaa kiti cha pembeni.

Gari ile nyeusi ilikunja kushoto, ikaenda ikakunja kushoto tena, halafu kushoto tena, halafu kushoto tena kwa hivyo ikawa inazunguka sehemu ileile moja. Baba pasipokujua, akajikuta akizunguka eneo lile na mwisho akabaini aligundulika lakini potelea mbali akaendelea kuzunguka.

Mwisho gari ile nyeusi ilifunga breki, mlango ukafunguka Mako akashuka na gari ile ikaenda.

“Vipi mzee kuna tatizo?” aliuliza mtoto Mako akitembea kuelekea alipokuwa Baba ambaye alifungua mlango wa gari na kusimama nje, lakini mguu mmoja ukiwa ndani. Baba hakujibu, Mako hakujali, akaingia na kukaa kiti cha nyuma.

“Ni kina nani wale?” Baba aliuliza baada ya kuweka gia tayari kuendelea na safari.

“Endesha gari,” alijibu Mako. Baba akainama kuchukua bakora, Mako kulijua hilo akajitetea, “Ni hadithi ndefu, nakusimulia tukifika nyumbani.”

Kuwa wa Kwanza Kupokea mwendelezo wa Riwaya hii Kwa kujiunga katika Group la bure WhatsApp. Kujiunga, Gusa Hapa

Tupate Wadhamini:

Soma: Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi

Soma: Jinsi ya Kuandika CV
 
Sehemu ya 13

Nyumbani Mama alikaa sebuleni mwanamume na mtoto wa kiume walipopita kimyakimya. Waliingia chumbani wakafunga mlango lakini Mama akapaza sauti. “Kulikoni, hakuna salamu ndani moja kwa moja kama nyoka?”

“Mambo ya kiumee!” alijibu Baba huku akihakikisha kama kitasa kilifunga vizuri.

“Ni kina nani wale?” aliuliza baba akimtazama mwanae.

“Ni wale watu, unajua tangu kipindi kile tumekamatwa hawajawahi kukuamini na mara mojamoja huniita na kuniuliza maswali kadhaa kisha hunirudisha nyumbani.”

“Wanakuuliza maswali gani?”

“Baba yako amesafiri ndani ya wiki mbili? Akiwa nyumbani hufanya kazi gani? Wageni gani wanakuja nyumbani, anajua lugha ngapi, anamiliki silaha yoyote?”

“Wewe unawajibu nini?”

“Sina cha kuwajibu zaidi ya kuwaeleza ukweli.”

“Safi,” alipongeza Baba. Akanyanyuka na kujinyoosha. “Wakati mwingine usizungumze nao, wakikuuliza habari zangu waambie wanifuate waniulize mwenyewe.” Akiisha kusema hayo, Baba akatoka na kuelekea katika chumba ambacho kilikuwa ofisi ya biashara zake za mtandaoni. Alipofika na kuwasha kompyuta, Mako aliingia naye, hana shati, kavaa kinjunga.

“Bora umekuja… peleka hii laki mbili kwa wakala, weka pesa kwenye namba hii,” alisema akitoa hela na kuonyesha kikaratasi chenye namba.

“Pesa ya nini hii mzee?”

“Kuna video nataka ni hariri, nataka kulipia software itakayoniwezesha kufanya hivyo.”

“Window wanayo software ya bure humohumo kwenye kompyuta yako,” alishauri Mako.

“Ni kweli, lakini haina vitu ninavyotaka. Haiwezi kuongeza sauti zaidi ya iliyopo, na haina video and picture overlay. Mengine ya kitaalamu nitakuchanganya.”

“Ndiyo hii unayotaka kulipia?” aliuliza Mako akitazama katika kompyuta.

“Ndiyo.”

“Zipo njia nyingi tu za kuipata bure, kama ku download software ambayo itacrack mara moja tu na kufanya iwe kama umelipia. Hakuna haja ya kutumia hela nyingi kwa kitu kinachoweza kupatikana bure.”

“Mmmmh…” Baba aliunguruma akishika kichwa. “Ni kweli unayosema bwana mdogo, lakini baada ya kuinstall software unayosema, itafanya zaidi ya kile unachotaka ifanye. Itafanya jambo baya ambalo litakuingiza hasara kubwa pengine kuliko hiyo laki mbili. Nyingi ya mifumo hiyo ukishaiweka, inaweza kufanya unachotaka au isifanye, lakini sasa itafungua mlango wa kompyuta yako na kutuma taarifa kwa aliyeitengeneza. Mojawapo ya taarifa hizo, ni ‘password’ zako zote. Na mwizi ataweza kuingia katika account zako za mitandao ya kijamii na nyinginezo. Nilipokuwa kijana, nilitumia njia hizi, nikashambuliwa na Trojan ambaye aliweza kuingia katika akaunti zangu zote na kufanikiwa kuichukua kabisa akaunti yangu fulani ya mitandao ya kijamii niliyoipenda sana.”

“Trojan?” aliuliza Mako akihamaki.

“Ndiyo, Trojan ni kirusi ambaye akiingia katika kompyuta yako, anaiba nywila zote na kuingia katika akaunti zako. Huko atafanya utapeli kwa kutumia jina lako na mengine mengi yasiyoelezeka.

“Kwa nini anaitwa Trojan?”

“Ooooh… ni mkasa mrefu sana, hebu kaa pale nikusimulie,” Baba alishauri, Mako akasogea katika kiti akakaa akimtazama Baba ambaye alianza kusimulia.

“Wagiriki walipigana vita na Waturuki kwa miaka mingi. Askari wa Kigiriki walishindwa kuwashinda Waturuki kwa sababu ya lango lao imara. Hakungekuwa na namna nzuri ya kuiteka Uturuki, ila kuweza kupita katika lango lao lililokuwa imara sana.

Baada ya majaribio ya miaka kumi kushindwa kuiteka Uturuki, Wagiriki wakaja na mbinu mpya. Walitengeneza farasi wa mbao mkubwa, ndani ya farasi wakaficha askari wao halafu wakaenda mpaka katika lango la Waturuki, wakapigana na Wagiriki wakajifanya kushindwa vita na kukimbia. Basi Waturuki walimchukua yule farasi wa mbao aliyetelekezwa na Wagiriki na kumuingiza ndani ya himaya yao kama ishara ya ushindi wa vita.

Usiku askari wa Kituruki wakiwa wamelala, wale askari waliofichwa ndani ya farasi yule wa mbao, walitoka na kwenda kufungua lango la kuingia mji mkuu wa Uturuki. Askari wa Kigiriki waliokuwa nje, wakaingia kwa wingi na kuiangusha kabisa Uturuki! Sasa hebu niambie habari hii inahusianaje na usalama wa kompyuta?” alimaliza Baba kwa swali.

“Kwamba… utainstall hiyo app ukizani itakusaidia kupata kitu fulani bure, lakini kumbe ndani yake ina askari wa siri ambao watafungua mlango wa kompyuta yako na kutuma taarifa zako zote. Kwa kifupi ni mbinu ya kumuingiza adui sehemu salama!”

“Safi dogo…” Baba alipongeza. “Sasa haraka sana, nenda kaweke hiyo laki mbili tulipie software.”

Mako akatoka kama mshale, Mama akaita lakini hakuitika, kiguu na njia kuelekea kwa wakala.

Kuwa wa Kwanza Kupokea mwendelezo wa Riwaya hii Kwa kujiunga katika Group la bure WhatsApp. Kujiunga, Gusa Hapa

Tupate Wadhamini:

Soma: Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi

Soma: Jinsi ya Kuandika CV
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom