RIWAYA; MVAMIZI
NA; BAHATI K MWAMBA
SIMU; 0758573660/0656741439...
Pito Fizo alijua namna ya kufanya na taa ilirudi kuwaka vema, kisha alianza kuizingusha kama alivyokuwa akifanya mlinzi aliyekuwa zamu usiku huo. Alimulika kila kona ambayo alihitaji kuimulika na wakati akiendelea kumulika, macho yake yaliangukia upande wa kaskazini mwa pale alipokuwa. Upande huo ulikuwa umefunikwa vema na msitu mkubwa, huku nyasi zikikamilisha msemo wa ‘msitu' msitu mnene kwa kufunga vema ardhi ya upande huo. Upande huo ndiyo ulikuwa mgongo wa kambi na kulionekana barabara nzuri ikiwa inaelekea katikati ya msitu uliokuwa upande huo wa kasikazini.
Wazo moja la hatari likapita kichwani mwake na alihitaji kulifanyia kazi kabla hajaelekea ndani ya kambi kufanya kilichokuwa kimempeleka pale.
Alihitaji kuweka taharuki ndani ya kambi ili iwe rahisi kwake kuingia na kutoka bila kikwazo, pia alihitaji kupata mavazi ya kawaida ambayo aliamini atayapata ndani ya kambi, mavazi ambayo yangempa hadhi ya mtu wa kawaida endapo angelifanikiwa kuingia mjini Chipipa au sehemu nyingine yoyote ambayo angelifanikiwa kuingia.
Aliteremka haraka juu ya kidungu na alipofika chini aliiweka sawa bunduki yake ambayo alikuwa ameining'iniza mgongoni wakati alipokuwa anapanda juu. Alitizama pande zote ambazo zingeliweza kuwa hatarishi kwake alipoona kila kitu sawa, alianza kujongea kwa umakini huku akitumia vivuli vya miti na vichaka vya nyasi kama kinga ya kutokuonekana kirahisi.
Alifanikiwa kufika bila kuonekana. Hakuhitaji kutumia muda mwingi kutafakari alilokusudia, haraka alitoa kiberiti kutoka kwa moja ya mifuko iliyokuwa kwenye bukta yake kisha aliwasha nyasi kavu na kilichofuata ni moto mkubwa kuanza kuunguza nyasi na miti iliyokuwa imeachwa kwa kuikinga kambi na pia eneo lile lilitumika kimkakati.
Baada ya kuwasha moto alikimbilia sehemu nyingine na kuwasha pia kisha alitoroka eneo lile na kuelekea upande mwingine wa kambi ambao aliamini utakuwa salama. Alifika eneo alilolikusudia bila kizuizi na alitulia tuli akitizama hekaheka za baadhi ya wanajeshi walivyokuwa wakihangaika kupiga filimbi ili kuwaamsha waliolala. Dakika mbili baadae kambi nzima ilikuwa kwenye hekaheka nzito na ni wakati huo ambao aliuhitaji kuliko wakati mwingine kwenye maisha yake. Haraka bila kujiuliza alivuta wavu uliokuwa umezungishiwa kama uzio wa kuingia kambini, alipata nafasi kidogo ambayo aliitumia kupenya na kuingia ndani ya kambi huku bunduki yake ikiwa mkononi tayari kwa lolote ili kutetea uhai wake.
Pilikapilika za wenyeji wa kambi zilimrahisishia kutoonekana kirahisi, kwa sababu wakati wao wanapigana vikumbo kuchukua silaha na wengine kuchukua vifaa vya kuzimia moto kwa dharura, yeye alitumia mwanya huo kupenya kwa kasi kuelekea ilipokuwa jenereta ya umeme ambayo ilikuwa inasambaza umeme kambi nzima. Alipoifikia alitumia nusu dakika kufungua mfuniko wa tanki la mafuta na kutia fumba kadhaa za mchanga, kisha alifunga vizuri na kukimbilia upande wa vyoo vya wanawake vilivyokua kusini mwa kambi.
Alifika vyooni na kuingia moja ya choo na ambacho alikilenga tangu awali. Choo kile hakikuwa choo cha kawaida, kwani hakikuwa kinatumiwa na mtu yeyote na mlangoni kuliandikwa bango kubwa liloonesha choo kile hakitumiki kwa haja yoyote. Pengine wenyeji walijua ni kwa nini, lakini wageni wengi hawakuruhusiwa kabisa kukitumia choo kile. Alipoingia ndani yake alikuta kukiwa na mlango mwingine kwa ndani ambao ulikuwa haujafungwa. Aliusukuma na macho yake yakakutana na sinki la choo ambalo lilionekana kusahaulika kufanyiwa usafi kwa muda mrefu. Hakuwa na shida na sinki lile ambalo alijua liko pale kwa sababu gani. Kwa kutumia nguvu kidogo alifanikiwa kuliondoa sehemu yake na hapo macho yake hayakukutana na tundu la choo bali kulikuwa na mlango mdogo wa mbao. Aliuvuta mlango ule na kukutana na njia ndogo iliyoruhusu mtu kupita.
Hakuwa na muda wa kupoteza, haraka aliingia kwenye njia na kabla hajazama kabisa aliuvuta mlango na kujifungia kisha alianza kushuka ngazi chache ambazo zilimfikisha kwenye njia iliyokuwa imefunikwa kwa giza kubwa. Alitembea huku akihesabu hatua za miguu yake na alipofikisha hatua mia, alisimama. Baada ya kusimama alichukua kurunzi yake yenye ukubwa wa kalamu ya wino na kuiwasha, aliangaza huku na huko hadi alipofanikiwa kuziona ngazi nyingine zilizokuwa umbali wa hatua kumi kutoka pale alipokuwa, alizifuata na kuanza kuzipanda hadi alipofika mwisho na kulikuwa na mlango mwingine mdogo sawa na ule aliongilia. Aliusukuma taratibu hadi ulipofunguka, hakufanya haraka kutoka nje, alitulia kwa sekunde chache akipima utulivu. Aliporidhika na utulivu aliamua kutokeza upande wa juu ambapo alijikuta akitokea kwenye chumba kilichokuwa kimebebwa na utulivu mkubwa. Chumba kile kilikuwa na ukimya mkubwa huku taa yenye mwanga hafifu ikimulika mule ndani. Kitanda chenye ukubwa wa sita kwa sita na godoro lake, viti viwili na meza moja vilikuwa ni miongoni mwa vitu vilivyokuwa ndani ya chumba kile.
Pito Fizo alisimama katikati ya chumba huku shingo yake ikizunguka kila pembe. Ndani ya kile chumba kulikuwa na kabati kubwa na la kisasa; alilitizama kwa umakini mkubwa huku akijaribu kushindana na hisia zake kuhusu kitakachokuwa ndani yake.
Aliamua kuachana nalo na alipiga hatua kuufuata mlango uliokuwa hatua moja kutoka lilipokuwa kabati, kabla hajaufungua alisimama pembeni yake huku mkono wake wa kushoto ukiwa umeshika kitasa cha mlango na mkono mwingine ukiwa umeishika vena bunduki yake. Alifumba macho na kuvuta pumzi kisha alitulia tuli akijaribu kuotea uwepo wa kiunbe hai yeyote nje ya ule mlango. Hakusikia sauti wala mjongeo, akazishusha pumzi zake na kufumbua macho kisha akaivuta mlango kwa kasi huku mwili wake ukichomoka kwa kasi zaidi na kujitupa kwenye nje ya kile chumba alichokuwemo huku bunduki yake ikiwa tayari kumchakaza yeyote ambae angeliingilia majukumu yake.
Hakukuwa na mtu, haraka alinyanyuka na kuangaza kwa umakini pale alipokuwa. Naam, alikuwa ameingia kwenye ofisi ya mkuu wa kamandi ya Chipa kikosi namba ishirini na sita. Ukutani mwa ile ofisi kulikuwa na picha kubwa ya rais wa Angola na kulikuwa na picha ya mkuu wa jeshi la Angola, lakini kulikuwa na picha nyingine ya mwenye ile ofisi. Aliifuata picha ya mkuu wa kambi na kuitizama kwa ukaribu, sura yake ikakaa vema kwenye ubongo wake. Aliachana na picha hiyo, macho yake akayatupia kwenye meza ya kiofisi iliyokuwa mle ofisini na akavutiwa na vitu vichache vilivyokuwa juu yake huku ikioneka mhusika wa ofisi ile, alitoka muda mfupi uliopita. Haraka alipiga hatua na kusogea pale mezani na kabla hajafanya lolote, umeme ulikatika na taa zikazima. Kiza kikatamalaki nje na ndani ya ile kambi. Kwa Pito Fizo haikuwa ajabu kwani alishalitegemea hilo na yeye ndiye chanzo cha umeme kukatika baada ya kuweka mchanga kwenye tanki la mafuta na kwa kufanya vile, mirija ya inayosambaza mafuta ilishindwa kupitisha kiasi cha mchanga kilichofanikiwa kupenya na hiyo ilisababisha jenereta kujizima kwa sababu mafuta hayakuwa yakitembea inavyotakiwa.
Wakati watu wakipambana na giza zito liloikumba kambi pasipo kutarajiwa, Pito alikuwa anawasha kurunzi yake na kuanza kukagua vile alivyoviona juu ya meza. Kulikuwa na simu ndogo na kulikuwa na karatasi tatu ndogo ambazo zilikuwa ni tiketi za ndege. Tiketi mbili zilionesha zilishatumika siku moja nyuma na jina la mtumiaji lilikuwa ni Carlos Guerimales. Tiketi nyingine ya tatu ilikuwa hajatumika na muda wa matumizi ulionesha ni siku iliyofuata mida ya saa tano ahsubuhi na jina la mtumiaji lilimshitua kidogo, alilifahamu vema kabisa.
“Huyu mjinga anatimka. Hii ni hatari kama bado atakuwa anaule mzigo.” Aliwaza huku akitupia macho upande wa pili ambao ulikuwa na nyaraka zilizokuwa zimepangwa vema. Akilini mwake hakuona umuhimu wa kuzitawanya ili kutafuta chochote kitu, hakutaka kujipa tumaini hasi kuhusu kutokuwa makini kwa watu wale waliomfanya afike ndani ya ofisi ile nyeti. Hakutaka kuamini kuwa chochote kinachohusu mkasa ule kitakuwa kinahifadhiwa sehemu nyeupe kama ile, hakutaka kupoteza muda wake.
Aliachana na ile ofisi kwa kuwa lengo la kuingia pale ofisini halikuwa kukagua nyaraka bali aliingia pale ofisini kwa kuwa, mtu waliemhitaji alikuwa akiishi kwenye kile chumba kilichokuwa nyuma ya ofisi na alikuwa akikaa na kuishi hapo kwa muda wote ambao alikuwa anatafutwa na vyombo vya ulinzi na usalama wa nchi ya Tanzania. Alienda pale kuhakikisha kama yule mtu atakuwa bado yupo au atakuwa ameshatoroshwa baada ya kugundulika uwepo wake pale, pia alitaka kujiridhisha na hujuma walizofanyiwa na kwa mazingira yale ilihalalisha hisia zao kuwa, walikuwa wanahujumiwa na mtu aliyekuwa karibu na yule waliekuwa wanamfuata.
Aliondoka ndani ya ofisi ile kupitia njia iliyokuwa imemfikisha pale, lakini baada ya kufika kwenye chumba kilichokuwa kinamhifadhi mbaya wake, aliamua kufanya ukaguzi mdogo lakini lengo lake alikuwa anahitaji kupata mavazi ili kuusitiri mwili wake, hakuhitaji kuendelea kukaa vile hadi mapambazuko. Mkono wake wa kulia uliendelea kuimiliki bunduki huku mkono wa kushoto ukifungua mlango wa kabati. Macho yake makali yakisaidiwa na mwanga wa kurunzi aliyokuwa ameing'ata mdomoni, yaliona vitu viwili kwa wakati mmoja; kulikuwa na nguo chache zilizokuwa zimekunjwa vema na kuhifadhiwa, pia kulikuwa na bunduki aina ya pump action. Shida yake haikuwa ile bunduki, alihitaji mavazi na alianza kuzipangua nguo kuona kama atapata inayomtosha. Haikumchukua muda mrefu kupata tisheti nyeusi na suruali ya jinzi nyeusi pia, aliichukua suruali na kujipima ukubwa wa kiuno chake kwa kuikunja na kuizungusha shingoni mwake ambapo ilitosha vema, alitabasamu huku akiikunjua na kuivaa harakaharaka bila kuhitaji kuvua viatu vyake. Baada ya kuvaa nguo zote ambazo zilimkaa vema mwilini mwake, macho yake yalirejea kwenye rundo lingine la nguo ambazo hakuwa amezifikia. Alizitizama kwa sekunde chache kisha alizipangua mojamoja huku akiwa makini bila kujua alimakinika na kitu gani. Hakupangua nguo nyingi hatimae mikono yake ikakutana na kitu kilichomfanya azipangue nguo zile, kitu ambacho wakati anapangua aliongozwa na hisia tu na si uono wa kile alichokikuta.
Kompyuta mpakato ikiwa imekunjwa na kuhifadhiwa katikati ya rundo la nguo safi na chafu zilizokuwa zimekunjwa na kuwekwa kabatini. Aliishika ile kompyuta huku akisoma jina la kampuni iliyounda kompyuta ile, kisha aliipiga pigo moja na kuivunja. Hakuwa na haja kompyuta nzima, shida yake ilikuwa ni Hard disc ambayo aliichukua na kuiweka kwenye mfuko wa suruali yake.
Wakati akijiandaa kuondoka macho yake yalirudi ilipokuwa bunduki, aliitazama huku roho ya matanio ikimzoga, alitamani kuichukua lakini alisita kufanya hivyo baada ya kuhisi atajiongezea mzigo mwingine usio na manufaa mikononi mwake ukizingatia, bunduki ile haikuonekana kuwa na risasi za kutosha. Aliitazama bunduki iliyokuwa mkononi mwake na wazo fulani likapita kichwani mwake na alihitaji kulifanyia kazi haraka iwezekanavyo. Kama mwizi aliyevamia nyumba ya kutunza sarafu, alianza kukagua kile chumba kama asiye na akili nzuri; alivuta hiki na kile hadi alipofanikiwa kupata alichokuwa anakihitaji ijapokuwa hakikuwa kinakidhi mahitaji yake.
Aliupata mkasi mdogo uliokuwa umehifadhiwa kwenye droo ya kitanda. Alishika ule mkasi na kuibinua bunduki yake ambapo bomba lake lilitazama juu, kisha aliuchukua mkasi na kuingiza kwenye tundu la kutolea risasi na ulipokaa kama alivyohitaji, alianza kupanua ukubwa wa tundu la bunduki hadi upana aliouhitaji, kisha aliondoka ndani ya kile chumba kama alivyokuwa ameingia.
Dakika tatu baadae alikuwa anatokea kwenye vyoo vya wanawake, alitulia kidogo kupima usalama kabla hajatokeza nje na masikio yake yalizisikia hekaheka zilizokuwa zikiendelea huko nje hasa maeneo ilipokuwa jenereta ambapo hapakuwa mbali na vile vyoo.
Kwa hatua fupifupi huku akitanguliza ncha ya kiatu chake ardhini ili asitoe vishindo, alitokeza nje ya vyoo na kukutana na giza kubwa likiwa limeiteka kambi huku upande wa pili akiona moto ukizidi kuteketeza pori na kelele za makamanda zilisikika wakijipa morali ya kuuzima moto ule.
Pito Fizo hakutaka ile kambi ipoe wala makamanda watulize nyoyo zao baada ya kuona hakuna tishio, alipanga kuwavuruga upya na yeye apate mwanya wa kutoroka ndani ya kambi kwa sababu utulivu ungeendelea kuwepo, ilimaanisha kwake ingelikuwa ni ngumu kutoroka kwa sababu, umakini wa walinzi ungelimfanya aonekane kirahisi, lakini kama angetia fujo yoyote huku akitumia giza kama silaha yake ya ulinzi, ingemrahisishia kazi ya kutoroka kwa kuwa kila kamanda angehaha kujua adui alipo na wapo wangapi.
Pale alipokuwa aliona kuendelea kutembea ni kurahisisha kivuli chake kuonekana na yeyote ambae angalikuwa maeneo yale,aliona ni vema atumie mbinu za kimedani kuweza kufika lilipokuwa jenereta, alilala chini kifudifudi kisha alianza kutambaa kwa mwendo uliotwa Low Crow ambapo, alitambaa kwa kuuvuta mguu mmoja huku mikono yake hasa viwiko vikifanya kazi ya kuuvuta mwili mzima na kichwa chake akiwa amekilaza chini na huku mara chache akikiinua na kutazama alipokuwa akielekea. Kufanya vile ilikuwa inamrahisishia kuonekana kama kifusi kinachotembea kwenye nyasi fupi zilizokuwa zimekatwa kwa urefu sawa na ingelimfanya adui yeyote kuingiwa na udadisi wa kujua ni kitu gani badala ya kushambulia na hiyo ingemrahishia kujitetea kama angelionekana.
Komando Pito Fizo alitambaa kwa mita chache kisha aliinua kichwa na kutizama mbele yake ambapo alizidi kukaribia ilipokuwa jenera na mafundi waliokuwa wanajitahidi kuirudisha kwenye ubora wake. Baada ya kushusha kichwa chini hakuendelea kutumia low crow tena, aliona ni kama anachelewa kuwafikiwa wale jamaa ambapo aliamua kutumia mtindo wa High Crow ambapo aliiweka bunduki juu ya mgongo wa mkono wake, kisha alitumia viwiko vyake kusogea mbele huku miguu yake akiwa ameitanua na ikipishana kufuata viwiko vya mikono yake, aliamua kuongeza kasi ya kutambaa chini huku kichwa akiwa amekiinua na macho yakitazama mbele hatua mia moja. Kama ungelifanikiwa kumuona ungelivutiwa na aina ya mwendo wake lakini bahati mbaya wakati huo hakuwa anampango wa kumfurahisha yeyote, bali alikuwa yupo kwenye majukumu mazito ya kuiuza roho yake akijaribu kuliokoa taifa lake.