MSITU WA SOLINDO
Mtunzi Richard Mwambe
Sehemu 10
Siku tatu baadae....
Ruperto Carola Cafe
Hellen na Stephan walionekana wenye furaha sana hasa kwa wazo lao lile
walilolipata maana walijua wazi kuwa pindi tu watapokamilisha zoezi hili watakuwa juu
sana kitaaluma, kiu yao ya kitafiti hasa juu ya mambo ya kale ilikuwa kubwa sana, lakini
bado hawakujua hasa ni nini wanachotaka kukifanya sasa, ni kitu cha hatari kiasi gani
wanachokifikiria, Hellen alijiuliza tu kama itakuwa safari kama ile ya Amazonia
iliyomchuku wiki tatu kuikamilisha akiishi na wa-Indios na wa-Amazonia ambako
alikutana na hatari ndogondogo tu, Stephan aliichukulia labda itakuwa safari kama ile
ambayo aliifanya huko Hamunatra katika jangwa la Misri ndani ya mapyramid
yaliyosadikiwa kuzikwa watawala wa nchi hiyo nyakati za kale kabisa, wote wawili
walijiona ni mashujaa sana kwa safari zao za utafiti walizozifanya katika maisha yao.
Stephan alishusha taratibu kikombe chake cha kahawa na kukiweka katika kijimeza
kidogo ndani ya mgahawa huo huku akiendelea na maongezi ya hapa na pale na Bi
Hellen. Binti mweusi alikuwa amekaa katika kimoja cha viti vitatu vilivyozunguka meza
hiyo akiwa na makaratasi machache mkononi mwake.
“Naitwa Saringo!” alijitambulisha kwa Hellen na Stephen, hili lilitukia mara baada ya
hawa wawili kujitambulisha kwake. Mazungumzo machache yalipita kati yao hasa ya
kufahamiana na kujuana zaidi, Stephen na Hellen walivutiwa na uchangamfu wa Saringo,
Saringo aliwaambia mambo mengi sana juu ya Africa hasa eneo ambalo yeye anatoka
Deutche Ost Africa, Stephen na Hellen walivutiwa sana na habari za huko na walipenda
kujua kama ni kweli au ni za kutunga tu za mababu wa kale. Saringo aliwasimulia mengi
sana hasa aliyosimuliwa na babu yake mzee Koloto, baada ya mazungumzo hayo saringo
aliwagusia juu ya stori ya babu yake alipokuwa askari wa wajerumani na alivyokuwa
akiongoza misafara ya wapagazi kuingia misituni na kuficha vitu visivyojulikana huko
kisha kuuawa, “No! Kwa nini waliwaua? Lazima kuna kitu” Hellen aliuliza kwa mshtuko
“Labda hawakutaka warudi tena huko, kuhofia kuchukua mali zao” Stephen alijibu
“ndiyo, ndiyo, hakika kabisa babu alinambia waliwaua ili wasiweze kurudi, lakini yeye
alinusurika na kufanikiwa kubaki hai” Saringo aliwaeleza na kutoa zile karatasi chache zenye michoro ya ajabu na maandishi ya kijerumani. Kwa Stephan haikuwa kitu kigeni
michoro ile kwani aliitumia sana alipokwenda huko Hamunatra, kwa haraka haraka
aliweza kuisoma na kutambua kilichofichwa katika michoro ile.
Stephen alitikisa kichwa kuashiria amegundua kitu, akanyanyua kikombe chake cha
kahawa na kunywa kidogo. “Vipi? Stephen!” Hellen aliuliza kwa shauku ya kutaka
kujua. Stephen alitikisa tena kichwa na kugeuza geuza mdomo wake, mara alionekana
kukunja uso, mara kutabasamu, akaiweka ile karatasi chakavumezani, na kunyanyua
kichwa kumwangalia Saringo. “Bingo!” Stephen alitamka neno hilo na kuamka alipokaa
akazungukazunguka huku akiwa amefungamanisha mikono yake kwa nyuma kisha
akarudi akaketi tena, “Saringo! Unajua Msitu wa Solondo?” Stephen alimrushia swali
Saringo, Saringo akaitikia kwa kutikisa kichwa, Stephen akaendelea “unajua Gereza
Saroge?” Saringo akaitikia tena kwa kutikisa kichwa, “good! We have to face a big
adventure!” .Stephen akachukua zile karatasi na kuzikunja vizuri kisha akampatia
Saringo “tunza, urithi ulioachiwa na babu yako” Saringo alizipokea na kuziweka
mkobani. “Kama tunaamua kufanya utafiti huu, basi na tujiandae vema sisi watatu ila
lazima tupate nguvu ya watu wa ziada kuukabili msitu wa Solondo.” Stephen aliwaeleza
akijua kwamba washaelewa kila kitu, “Stephen!” Hellen aliita “ tueleze kwanza kuna nini
ulichokiona kisha ndiyo tuone pamoja cha kufanya” Hellen alimueleza Stephan. “Ok!
Kadiri ya mchoro huu wakoloni wa kijerumani walipokuwa wanaitawala Deutch Ost
Africa walipata vitu vingi sana ikiwemo mali za aina mbalimbali, kwa hiyo
walichokifanya ni kuzificha ili vizazi na vizazi vyao vija kuchukua na kuupata utajiri huu
mnono, Babu yake Saringo aliifadhi kitu kikubwa asichokijua, huu ni urithi usiopimika
kwa mjukuu wake.” Stephen alimaliza maneno yake na kuwafumbua macho wadada
hawa wawili ambao walibaki kutazamana bila kujua wanachotazamania ni nini!
Walizungumza masuala machache na kukubaliana kuanza shughuli hii ya utafiti wa wapi
zilipo mali hizo, na jalada la utafiti huu wakaliita ‘Msitu wa Solondo’.
Saringo alizama kwenye mawazo mazito sana na daima alijaribu kuunganisha habari hii
aliyoisikia kwa Stephan na ile aliyoelezwa na babu yake mzee Koloto miaka mingi
nyuma, alijaribu kufikiria kama kuingia ndani ya msitu ule ni wazo linalowezekana au la,
kwa maana alishasikia mengi juu ya msitu ule, hakuwahi kufikiri kwenda huko hata siku
moja lakini sasa mawazo makubwa mawili yanagongana kichwani kwake moja likimtaka
aende na lingine likimzuia na kumuonesha hatari zote zinazomkabili, alifikiria juu ya
mali hiyo aliyoisema Stephen ambayo mpaka hapo hakuna alojua ni mali gani
iliyofichwa, Saringo alibaki hajui la kufanya.
Hellen kwa upande wake aliona wazo la kwenda huko ni zuri lakini alifikiria adha za
porini akilinganisha na zile alizopata akiwa huko Amazon, hakujua aamue nini, alifikiri
kuwa endapo watafanikiwa kufika mwisho wa safari yao salama atakuwa ni milionea wa
kutupwa mara alijiuliza itakuwaje endapo asirudi huko akaona kuwa maiti yake
haitaonekana hata kwa ndugu zake, alikata tamaa na kuona kuwa hilo ni wazo hasi kabisa
kwa wakati huo.
Stephen alikuwa na mambo mengi kichwani, alijua kama akifanikisha safari hiyo si tu
atakuwa kitaaluma lakini pia ataukwaa utajiri usokifani kutokana na mali hizo
zilizowekwa porini, alifurahi sana kwa ugunduzi huo hata siku hiyo maisha yake
yalibadilika na kuanza kuishi kama kibopa mmoja hivi, wanafunzi wake walimshangaa
sana alipoingia katika kipindi akiwa na furaha ya ajabu sana, alifundisha kiasi kwamba
muda wa kipindi chake ulikuwa hautoshi, kila saa aliangalia saa yake ile aliyoipenda sana.
Saringo aliona sasa ndoto zake zimetimia baada ya kujua kuwa amepata watu ambao
wameweza kugundua siri ile ambayo yeye hakuijua kirahisi, aliamua kwenda kusoma
katika chuo hicho ili naye apate kujua na kwa bahati mbaya au nzuri anakutana na watu
ambao wanafahamu na wameshafanya tafiti kama hizo. Saringo aliiona hiyo ni bahati
kubwa sana kwake na aliona kile alichokisubiri kwa miaka mingi kitendawili ambacho
hakukijua tatuzo lake sasa kimefika mwisho. Alishusha pumzi kwa nguvu na kujinyoosha
pale juu ya kitanda chake huku akitafakari hili na lile ‘nani wa kutupeleka msituni?’
alijiuliza lakini hakupata jibu, alikumbuka tu mahitaji aliyoambiwa na Stephen ‘mtu
anayejua misitu, mwenye nguvu na mkakamavu, nani! Cjui’ alijiuliza na kujijibu kwa
namna isiyosawa, Saringo alikuwa kama aliyechanganyikiwa katika kichwa chake,
hakujua anachofikiri wala anachokiwaza. Kila alipoamua kuingia ndani ya msitu ule akili
yake ilimtoa na kumuuliza maswali yasiyo na ukomo, alimkumbuka mjomba wake
Golam ambaye mara tatu alijaribu kuingia katika msitu huo wenye maajabu na kukutana
na vitu ambavyo havielezeki na hata mara ya mwisho aalikuwa kama mtu
aliyechanganyikiwa, bangi, gongo vurugu nyingi za mtaani ilikuwa ndiyo kawaida yake.
Lakini hakuna kitu kilichomsumbua sana saringo kama jinsi gani ya kupata sehemu ya
pili ya ramani ile maana ile ilkuwa ni nusu na nusu nyingine je ilikuwa wapi, hilo
lilikuwa swali ambalo halikupata jibu hata kidogo ‘hata kama tukienda msituni tutafikaje
kwenye maficho haya, hatuna sehemu ya pili ya mchoro huu, babu alinambia kipande
kingine kilibaki kwa yule askari wa kundi la pili, mh! Yuko wapi? Alikufa, mzima au
alikitupia wapi au kukificha wapi kipande kile, utata!!!’ Saringo alikosa jibu hata usingizi
ulimchukua.
7
Msituni Msituni
Kutoka juu ya kilima kile Hellen alinguka baada ya kuteleza vibaya alipokuwa katikati ya
msafara ule wa wale watu katili wasio na chembe ya huruma, alining’inia kwa kamba ile
iliyofungwa kiunoni mwake, akiwa amechoka na uso wake umesawajika vibaya kwa
matope, damu zilizoganda zilimfumba macho, njaa ya siku kadhaa haikupata tiba yake,
Hellen alibaki akining’inia kwenye korongo lile huku watesi wale wakimvuta kurudi juu,
msafara ulisimama kwa muda. Hellen alifikishwa juu na kujumuishwa na wengine na
msafara ule uliendelea, ‘Gwerino’ watu wanaokula nyama za watu daima walikuwa
wakifanya matambiko katika mawe na mapango makubwa yaliyopo katikati ya msitu wa
Solondo. Siku ya matambiko ilikuwa imefika na katika siku hii hutoa damu za watu na
kumwaga kwenye mawe yale ambayo wao waliamini Miungu yao ndimo inamoishi, siku
hiyo hawakula kabisa nyama za watu kwa kuwa zote walizipeleka Mzimuni. Msafara
ulizidi kuingia ndani kabisa ya msitu ule watu wapatao kama kumi na tano walifungwa
kamba viunoni na shingoni wakikokotwa huku wakipigwa sana. Hellen kati ya msafara
ule alikuwa amechoka sana hata alitamani afe na asifike anakopelekwa, wenzake
aliowakuta wamefungwa hakuwajua hata mmoja wao hakujuwa hata wametokea wapi,
hakuelewa lugha inayoongelewa na hawa Gwerino, kibaya zaidi alichokishuhudia ni jinsi
wanavyoua watu na kula nyama zao wengine wakinywa damu mbichi, Hellen aliona kuwa hii sio dunia aliyoijua kweli hili ni bara la giza, mara kadhaa amepoteza fahamu na
alipozinduka alijiuliza kwa nini alikuja kwenye safari mbaya kama hii. Msafara
uliendelea, watu walikuwa ni wengi sana wenye mienge mikononi, magongo makubwa,
mavazi yao yakutisha yaliyotengenezwa kawa ngozi wengine walivaa vidani ambavyo
vilikuwa ni mifupa ya vidole vya watu. Kila Hellen alipoona haya alihisi akili yake
kuchanganyika na ubongo, Hellen alichoka kabisa hakuweza kuendelea na safari ile
alianguka tena na sasa hali ilikuwa mbaya zaidi hakuweza kusogea hata kidogo. Msafara
ulisimama na yule kiongozi alishuka kutoka kwenye kiti kile cha enzi kilichobebwa na
wanaume wapatao nane hivi walioshiba kwelikweli. “Kusisi libiko?” yule kiongozi
aliwauliza waongoza msafara kwa sauti ya kutisha yenye kukwaruza akimaanisha
‘kumetokea nini’ huku akiwa anajongea taratibu na fimbo yake ambayo juu imepambwa
na fuvu la binadamu. “Libiko sinzota, kucholo londigo!” alijibiwa na kiongozi wa
msafara akimaanisha ‘hapa kuna kafara moja imechoka haiwezi kufika’ yule kiongozi
akatikisa kichwa kuashiria ameelewa alichoambiwa “Kucholo? Losa fo, libeso Kolilo, a
la to” aliongea kwa kufoka huku akizungukazunguka akimaanisha ‘imechoka, basi na
tuitoe sasa ili miungu ifurahi’ alimaliza na kuigonga chini fimbo yake kwa nguvu na
kupaaza sauti huku mkono wake mmoja ukiwa juu “I lee se?” na msafara wote ukajibu
“seeee!!!!” akimaanisha ‘ni sawa?’ msafara ukajibu ‘sawa’ . wale waliokuwa wakilinda
mateka wale wakamfungua kamba Hellen na kumnyanyua wakasonga nae mbele kidogo,
maana katika utaratibu wao kama kafara haiwezi kufika mzimuni basi mnaweza kutolea
popote na damu yake ndiyo mtayoipeleka mzimuni pamoja na moyo. Walifanya mduara
na wote walianza kugonga fimbo zao chini wakirudiarudia neno lile “Se, se, se, se”.
Hellen alifungwa mikono kwa nyuma na kupigishwa magoti kisha mtu mmoja lisimama
nyuma yake na kumuwekea mti wenye mfano wa kipago cha manati mgongoni na
kaamba moja iliyomzunguka shingoni ikavutwa nyuma mgongo wa Hellen ukapinda na
kifua chake kutangulizwa mbele tayari kwa kazi hiyo. Yule kiongozi alizunguka kwa
mbele na kukabidhiwa ule mti uliochongwa maalumu kwa kazi hiyo akaunyanyua juu na
alipotaka kuushusha kukipasua kifua cha Hellen alisita ghafla, akashusha mti ule taratibu,
watu wote walinyamaza kimya kabisa wakiwa hawajui nini kinachoendelea “Ifime, letose
seleke, ke la londigo, iso losabe?, bease keloya londigo” kiongozi yule aling’aka kwa
hasira akimaanisha ‘laana, hii sio kafara ni mwanamke huyu?, ivueni nguo hii kafara’
watumishi wa kiongozi yule mara moja walimfungua kamba Hellen na kumvua blauzi
yake iliyochakaa kwa uchafu wa aina tofauti, kiongozi yule akamwangalia Hellen na
kumeza funda kubwa la mate alipoona chuchu zile nyekundu zilivyosimama kama
mishale ya saa sita “seleke!” alitamka neno hilo huku akijipiga mkono wake wa kulia
kifuani mara kadhaa akimaanisha ‘laana’, katika utaratibu wao ilikuwa kafara lazima awe
binadamu wa kiume na si wa kike, muda wote walipomkamata Hellen hawakujua kama
ni mwanamke kwa jinsi alivyovaa suruali ile ya jeans, kilichomshtua kiongozi yule ni
jinsi alivyoona vitu vilivyotuna kifuani mwa Hellen ndipo alipofikiri kuwa huyu ni
mwanamke na walipomvua blauzi ile waligundua kuwa ni kweli. Wote walijipiga kifuani
kwa mkono wa kuume wakirudia neno lile ‘seleke’. Hellen aliondolewa kwenye kundi
lile la mateka wengine, akiwa bado amechoka sana alitembea kwa tabu, yule kiongozi
alimwita mmoja wa majemadari wake na kumnong’oneza kitu kisha alitoa ishara msafara
ule uendelee. Hellen aliingizwa kwenye kitu kama pango na kuwekwa pale huku akiwa
amefungwa kamba za miti ili asitoroke. Msafara uliendelea usiku ule na mateka wale sasa
walikuwa wamebaki kumi na nne.Akiwa mle pangoni, Hellen hakuwa na lolote la kufanya alitulia tu akisubiri mwisho
wake ufike, hakujua ni kwa nini alifungwa pale, macho yake yaliendelea kupambana na
giza nene lililotawala msitu ule, mbu na mbung’o walifurajhia kupata damu
wasiyoitarajia, hakika ilikuwa ni sherehe kwao usiku ule. Hellen alishuhudia mwanga ule
wa mienge ya watesi wake ukitokomea msituni, alitafakari sana lakini hakupata njia ya
kumtoa mahali pale, alibaki tu amejikalia huku machozi yakimtoka. Katika msitu ule ni
mivumo ya miti na upepo tu iliyosikika na milio ya ndege wasiyopendwa na binadamu,
bundi. Akiwa katika kutokujielewa Hellen allihisi vichaka vikitikisika aliogopa sana
akakza macho kuangali ni kitu gani kilichokuwa hapo, hakuweza kufanya lolote kwa
kuwa alikuwa amefungwa kwa kamba mikono na miguu yake, alibaki kuangali tu
kitachotokea, mara aliona kama mtu akitokea vichakani mle akinyata kuelekea pango lile,
Hellen alitulia akiangalia nyendo zote za kiumbe kile, mtu yule alizidi kunyata kana
kwamba kuna watu ambao hakupenda wamuone alisogea mpaka karibu kabisa na mlango
wa pango lile, akiwa anamulikwa kwa mbalamwezi hafifu iliyotoke nyuma yake Hellen
hakuweza kuona hata sura ya mtu huyu, alijua tu kwa vyovyote atakuwa ni mmoja wa
atesi wake ambaye labda amerudi kuja kujifaidia teka lile baada ya kujua kuwa alikuwa
ni mwanamke. Hellen alijibanza kwenye kiambaza cha pango lile akiwa kimya kabisa
bila hata kujitikisa alisubiri tu kuona mtu huyo atafanya nini kwake.
[emoji814][emoji814][emoji814]
Amata alipumzika vya kutosha katika kichaka kile ambacho alihifadhiwa na yule
nyani, alinyanyuka na kujinyoosha viungo na kujikuta yuko fiti kwani yule nyani
alimletea chakula pamoja na mizizi mbalimbali ili kumrudishia nguvu ambazo zilipotea
kwa mateso yale, Amata aligeuka huku na kule lakini hakumuona Kingusu eneo lile,
Amata alitoka ndani ya kichaka kile na kuangaza huku na huko akanyanyua mkono wake
na kubana vizuri midomo yake kisha akapiga mbinja kali ya kumuita Kingusu, alisubiri
kidogo lakini hakuona dalili ya Kingusu kuwa mahali pale, alipogeuka kurudi alipokaa
alikuta uta wake na podo viko pale akavichukua na kuvibeba tayari kwa safari lakini
aende wapi? Hata yeye hakujua. Alipiga hatua mbili tatu akasimama tena hakujua bado ni
nini anachotakiwa kufanya, baridi kali ilikuwa ikimpa taabu lakini alijitahidi kuivumilia
japo mara kwa mara alikuwa akitetemeka. Akiwa katika kutafakari hili na lile kwa mbali
aliona kitu kama moshi kikitokea katikati ya msitu ule, Amata aliangalia kwa makini sana
moshi ule na akagundua kuwa kule lazima kuna watu, lakini alibaki kujiuliza maswali
mengi ni watu wa namna gani hao, au ni vile viumbe vya ajabu ndivyo viishivyo huko
lakini hakupata jibu. Aliendelea kuuangalia moshi ule na akaamua kuelekea uko huko ili
akaone kulikoni ‘liwalo na liwe’ alipiga moyo konde na kuanza safari huku moyoni
akiwakumbuka wenzake wote ambao mpaka muda huo hakujua wapi walipo japo mmoja
wao tu, alijiona sasa kabaki peke yake na kilichobaki ni kufanya juu chini kutoka ndani
ya msitu ule na kurudi kijijini kwa kuwa hakujua hata aelekee wapi na upande gani, akili
yote ilikuwa ni kurudi alikotoka lakini sasa hakujua hata ni wapi alipo. Alitembea kwa
hadhari kubwa sana ndani ya msitu huo kuelekea kule alikoona moshi ule alidhamilia
kukabiliana na hatari iwayo yote atakayokutana nayo, mara kwa mara alitembea na
kuangalia nyuma maana alihisi kama kuna watu wanaomfuata lakini alipuuzia tu kwa
kuwa yeye alifahamu mambo mengi sana juu ya misitu. Amata alipita vichakani na
alipopata nafasi mara alikimbia na mara alitembea, alipoendelea mbele mara ghaflaalijikuta akitokea kwenye ukingo kama wa shimo kubwa alisimama na kuangaza macho
huku na huku hakuona mwisho wa bonde lile, bonge kubw lililofunikwa na miti mikubwa
iliyoshonana kwa namna ya ajabu, Amata alipigwa na bumbuwazi hakujua afanyeje
kuendelea na safari yake alipoangalia kule kulikokuwa kukitokea moshi ule aliona bado
unaendelea kufuka lakini mahali bado pakali mbali, alipoangalia bonde lile lilikuwa ni
kubwa na la ajabu hakuwahi kuona kitu kama hicho, Amata aliamua kushuka bondeni
kule kwa kutumia mizizi ya miti mikubwa iliyokuwa ikining’inia aliweka uta na podo
lake vizuri na kuanza kuteremka taratibu, kila mara aliangalia aendako na atokako lakini
aliona hafiki chini, mara ghafla mzizi ule ukakosa nguvu na kukatika Amata alipiga
ukelele na kuanguka kwa kasi kuelekea bondeni alijipiga kwenya baadhi ya miti na
kupata michubuko kadhaa mwilini aliendelea kupiga ukelele lakini hakukuwa na mtu
eneo hilo isipokuwa ndege wa mwituni, kasi ya kuporomoka chini iliongezeka kila nukta
Amata alijua sasa hata akifika chini asingepona, alijikuta anadondokea kwenye kitu kama
nyavu kubwa, hakuamini alichokiona uoto uliyojishonashona kama wavu ulimdaka
Amata naye alikuwa salama, aligeuka kuangali chini akaona sasa si mbali sana kumbe
angeweza hata kuteremka tu kwa kujirusha tu. Alijirusha mpaka chini na kutua kwenye
lundo la majani makavu akatulia dakika kadhaa lakini hakuona chochote, aliendelea
kutembea kwa hadhari kubwa sana na taratibu kuelekea kule alikoona moshi ule, katika
kutembea kule alisikia sauti ya mandege makubwa yakilialia Amata alijua popote penye
ndege wale lazima kuna mzoga, alisimama na kusikiliza kwa muda huku akijaribu na
kuvuta harufu kuona kama kuna harufu ya kitu chochote kilichooza, haikuwa hivyo.
Amata alichomoa moja ya mshale wake katika podo na kuupachika vizuri utani kauvuta
kwa mvuto wa wastani kisha taratibu alinyata kuelekea walikojaa ndege wale
alipokaribia eneo lile alitulia kimya kuangalia vizuri hakuelewa anachokiona kama ni
mzoga wa mtu au mnayama, Amata aliingiwa na woga kidogo aliushusha uta wake
uliokuwa tayari kwa kujeruhi na kuushika kwa mkono mmoja alipoangalia kwa makini
eneo lile hakukuwa na mzoga wowote Amata alisogea na kushuhudia tu madonge ya
damu nzito nzito yametapakaa eneo lile alipigwa na bumbuazi hakuelewa aliyepata
masaibu haya ni binadamu au mnyama aliiangalia damu ile kwa makini sana ilionekena
tukio hilo halikutokea muda mrefu, Amata alitazama huku na huku na kuona michirizi
mingine ya damu imeelekea porini aliifuata kwa hadhari kubwa huku uta wake ukiwa
umeshikwa tayari kwa kutoa pigo, akiangalia nyuma na mbele kwa haraka haraka
aliendelea kufuata damu zile, mbele kidogo alikuta damu zile zimepotea, alisimama na
kuangalia huku akijigeuza taratibu pande zote nne za dunia, akiwa pale chini alihisi kama
tone la maji limemdondokea, Amata akanyanyua kichwa chake kuona kulikoni,
hakuamini macho yake, mwili wa mwanadamu uliyoraluliwa vibaya ulikuwa kwenye
moja ya matawi ya mti ule ukining’inia, Amata aliuangalia mwili ule ukiwa pale juu,
machozi ya uchungu yalimdondoka nguvu zikamuisha na hasira ikaanza kuchukua nafasi
yake, alitamani amuone aliyefanya unyama ule kama ni mnyama au ni kiumbe wa aina
gani, Amata alikwea mti ule na kuuteremsha mwili ule mpaka chini akaulaza na
kuangalia vizuri ‘Stephan!’ alijisemea moyoni huku akilia aliugeuzageuza, akaweka
mkono wake shingoni mwa mwili ule labda angehisi joto lakini mwili ulishatawaliwa na
baridi, alijaribu kugusa kifuani kuona kama kuna dalili ya uhai ah wapi! Amata alijishika
kichwa na kukosa la kufanya ‘man down!’ alijisemea mwenyewe huku akibubujikwa na
machozi mwili wa Stephan ukiwa umelala bila uhai, aikuwa na majeraha ambayo
yalionesha kwa vyovyote kuwa ameuawa na mnyama mkali. Amata alibaki amekaakimya karibu kabisa na mwili ule, akiwa na maswali mengi kichwani mwake akijiuliza na
kujijibu ‘vipi wale wanawake wawili, bado wako hai au nao wamekufa?’
Amata akauchukua mwili ule na kufanya shimo la kumtosha Stephan ambaye kwa sasa
alishakuwa marehemu, akamsitili kwa heshima iliyomfaa, akafanya tuta mahali pale na
kuweka kitu kama msalaba, akasimama mbele ya kaburi lile na kutoa saluti ya heshima
“kwa heri kamanda, Hellen na ndugu zako hawatakuona tena”
Amata akachukua uta wake na kuanza kuondoka, mara akasita na kugeuka nyuma
alikumbuka karatasi zile ambazo Stephen daima alikuwa anazisoma ili kupata uelekeo
sahihi alitazama eneo lile hakuweza kuziona, taratibu aliamua kurudi kule michirizi ya
damu ilipotokea, Mungu si Athumani alizikuta japo zilipeperuka kwa upepo ila
hazikwenda mbali sana pamoja nazo aliokota na ile camera ndogo vyote akavitia kwenye
mfuko wake wa suruali ile ya jela na kuendelea na safari yake, poli kwa poli Amata
alitokea kwenye uwanda mkubwa ulioonekana kama umetadikwa zuria la kijani
aliangalia kwa makini akaokota kipande cha mti na kukirushia lol! Kumbe kuna maji,
akaendelea kuambaaambaa na ukingo wa bwawa hilo lakini lengo lake yeye ilikuwa ni
kuvuka na kuelekea upande wa pili lakini atavukaje ndiyo lilikuwa tatizo, aliendelea
kufuata ukingo ule mpaka alipokuta sehemu nyembamba ambayo aliona hapa angeweza
kuvuka kwa urahisi, alipokuwa akijiandaa mara akaona maji yale yakitikisika, akaangalia
kwa makini hakuona kitu, Amata akarudi nyuma kidogo mbali na mto ule ili kuona nini
kilichopo ndani yake, alikaza macho kutazama magugumaji yale yaliyotuama vizuri juu
ya maji ambapo kama huna subira basi unaweza kutumbukia ukijua ni ardhi kavu. Wazo
likamjia Amata akaingia porini na aliporudi alikuwa na digidigi mkononi akamrusha
majini, La haula! Mamba wakubwa walijinyanyua kugombania nyama ile ambayo hata
kwa vipi isingewatosha wote, Amata akapigwa na butwaa baada ya kuona jinsi
alivyogundua siri hiyo, akakaa chini akiwa hajui la kufanya lakini kichwani mwake
akiwa anafikiri jinsi gani angeweza vuka kwenda upande wa pili ambako lengo lake ni
kufika kule kunakofuka mosho akiamini kabisa lazima kuna binadamu wanaoishi huko
ila mara kwa mara alijiuliza itakuwaje kama watakuwa ni Gorino alijua kuwa huo
utakuwa ndiyo mwisho wake jinsi watakavyomtafuna.
Wazo likamjia, akaingia tena msituni na kufanya mawindo kidogo, akapata mnyama
mkubwa wa angalau, akamkatakata vipande vya kutosa kisha akasogea pale kwenye yale
maji, Amata akamwaga nyamazile kwa ustadi mkubwa na mamba wale walipokuwa
wakigombania yeye alitumia mwanya huo kupita juu ya migongo yao kwa kasi na
kufanikiwa kufika upande wa pili, alianguka kwenye majani kisha akaangalia kazi
aliyoifanya ilivyokuwa na mafanikio, mamba waliendelea kugombania nyama wakati
Amata alishafanikiwa lengo lake, aliamka na kujikung’uta majani yaliyoshikana na nguo
yake na kuendelea na safari kuelekea kule alikouona moshi ule, sasa Amata lijikuta
kwenye msitu wa upande wa pili, msitu wa kutisha wenye mawe mengi na makubwa,
yeye hakujali japo huku uoto mwingi ulikuwa wa miba, alihisi kupambana na hatari
nyingi kuliko alikotoka lakini alijipa moyo na kuendelea kutembea msituni mle japo kwa
taabu sana.