SEHEMU YA MWISHO
SIMU: 0755-697 335
Askari wale waliendelea kumimina risasi hadi
zilipowaishia kulipokuwa kimya, ndipo walipiga
simu kituoni na kuomba waongezewe nguvu. Muda
si muda gari nyingine iliyokuwa na askari wa
kutosha wenye silaha ikafika.
Polisi waliokuwepo wakawapa wenzao taarifa kwa
ufupi, ambapo kundi la askari wenye silaha
wakaizunguka nyumba ya Dr Masurufu ili
kuimarisha ulinzi. Wengine wakaingia ndani
kwenda kumkamata Steve na Masurufu, .
Kule ndani Samson alijitahidi alivyoweza kupiga
kelele za kuomba msaada na kufungua mlango
haikuwezekana. Alipochoka kabisa akampigia simu
Mkuu wake wa kazi Anderson Chilonga pamoja na
msaidizi wake Assia na kuwaeleza kinachojiri
katika nyumba ya Dr. Masurufu na kule
alikofungwa yeye.
Hawa wakamtoa hofu na kumwambia wanakwenda
huko mara moja. Samson akashukuru na kuendelea
kuangalia sinema ile kupitia dirishani.
Ndani askari wale walilikuta gari likiwa tupu.
Wakiongozwa na michinzi ya damu ambayo bila
shaka ilitoka katika jeraha la Steve, Polisi wale
waliingia mpaka katika chumba fulani ambacho
kulikuwa kama stoo hivi.
Ndani ya kile chumba kulikuwa na vikorokoro vingi
na mfuniko wa kitu kama chemba ya choo hivi.
Pembeni ya chemba hiyo kulikuwa na kidimbwi
kidogo cha damu ambacho askari wale walihisi
kama Steve aliitumia sehemu ile kujiganga. Askari
walipojiridhisha kuwa hakukuwa na mahala
pengine ambapo mtu angeweza kujificha,
wakaifunua chemba ile ambayo haikuwa
imefunikwa vizuri
Ngazi zinazoelekea chini zikawalaki.
Handaki! Wakapigwa na butwaa la mshangao
wakati wakiingia chini Haraka. Ndani kulikuwa na
vyumba vinne, vyenye shehena mbalimbali za
mizigo ambayo hawakuitambua mara moja.
Hakukuwa na muda wa ukaguzi, silaha zao zikiwa
tayari tayari wakaongoza kukifuata kijinjia
chembamba chenye kiza kilichokuja kuwatoa
ufukweni mwa bahari ya Lindi.
Mahala walioibukia kulikuwa na boti mbili speed
boat! Katikati ya Boti hizo kulikuwa na uwazi
mkubwa ulioashiria kuwa Speed boat moja ilikuwa
imeondoka. Walipotupa macho Baharini
hawakuweza kuona chochote zaidi ya giza
lililotamalaki na kufunika bahari nzima.
Mawasiliano yakafanyika haraka kuwataka askari
walio mjini waagize boti za Doria zilizomo katika
Bahari ya Hindi waitafute, kuifukuza na kuikamata
haraka boti hiyo ambayo ilikuwa ikiwatorosha
watuhumiwa wao Dr Masurufu Hussein Masurufu
na mlinzi wake Steve.
Wao wakarudi kuwapa taarifa wenzao.
Wakakuta tayari Inspekta Kimaro ameshafika,
alikuwa anawaangalia askari wake waliouawa na
Steve kwa uchungu na masikitiko makuu, hali
majeruhi wakimueleza ilivyokuwa. Inspekta Kimaro
hakuwa pekee, alikuwa pamoja na Mkurugenzi
msaidizi wa Usalama wa Taifa Chilonga Anderson
Chilonga, Msaidizi wa Samson Assia Khalifa
pamoja na maafisa wengine wa polisi.
Vitu aina kwa aina vya Dr Masurufu vikiwa
vimekusanya pamoja baada ya kumfungulia
Samson kwa kutumia Mtaalamu wa mitambo ya
kijasusi kutoka jeshi la Polisi la Tanzania.
Kutoka hapo safari ya kuelekea Makao makuu na
baadae Usalama wa Taifa ilianza ambako Samson
kidude alikuwa na mengi ya kueleza mbele ya
Inspetka Kimaro, Anderson Chilonga, Mkurugenzi
wa Usalama wa Taifa, Katibu Mkuu wa chama,
Mwenyekiti wa Chama Tawala pamoja na Rais
anayemaliza muda wake.
Mwisho wa maelezo yake, Samson aliwakabidhi
Mkakati wa Dr Masurufu wa kuelekea Ikulu, ule
mkataba wa kishetani baina ya Dr Masurufu na
G-8 Original, pamoja na taarifa za uwepo wa
mabilioni kwa mabilioni ya shilingi katika Ofisi na
handaki la Dr Masurufu kule Mbezi Beach.
Viongozi wa usalama pamoja na Rais
walibubujikwa na machozi ya furaha wasiamini kile
wakisikiacho. Kwa mara nyingine tena Samson
kidude kwa kushirikiana na jeshi la Polisi na
Vyombo vya Usalama alikuwa wameliepusha taifa
toka katika hujuma hizo nzito.
Kwao hizi zilikuwa taarifa za ushindi kwa kila hali.
Taarifa za matumaini. Taarifa ambazo zingetoa
onyo kwa G-8 Original na kuwajulisha kuwa huu
ulikuwa mwanzo wa Tanzania kujinasua toka
katika ukoloni mamboleo. Ukoloni wa kifikra,
ukoloni wa kuandaliwa sera na mifumo isiyokuwa
na tija kwa wananchi wa kawaida.
Naam! Taarifa hizi zilikuwa sawa na pigo
lililonyooka.
Rais aliwataka wakuu wa vyombo vya ulinzi na
usalama kuhakikisha Dr Masurufu anakamatwa na
kurejeshwa kizimbani ili sheria ichukue mkondo
wake pamoja na wote walioshiriki katika kadhia la
Dokta Masurufu. Akawaamrisha viongozi wa
chama kumchukulia hatua za kinidhamu ndani ya
chama kwa jinsi alivyoshiriki kukichafua na
kukipaka matope na akataka hatua hizo
zichukuliwe haraka.
Akawataka wakurugenzi wa Usalama waiboreshe
ofisi ya Samson na kuhakikisha anapata kila
anachohitaji. Kwa upande wa rasilimali fedha
zilizokamatwa nyumbani kwa Masurufu, Rais
aliamua kuwa zitaelekezwa katika shughuli za
maendeleo ya jamii ili kuchangia katika harakati za
kupunguza umasikini wa kipato na kuboresha
maisha.
Ilikuwa ni baada ya kila mmoja kuahidi kuyafanyia
kazi maagizo ya Rais ndipo, Samson Kidude
alipoanza kupokea pongezi za dhati kutoka kwa
kila mmoja. Sidhani kama nastahili pongezi hizi
peke yangu! Akasema kwa upole na kuendelea
Kila mmoja amefanya kazi, hivyo yafaa
tujipongeze wote hasa jeshi la Polisi!
Wakampigia makofi.
* * *
SURA YA KUMI NA MOJA
MALIPO YA UHALIFU
Tarehe mbili, mwezi Mei, Kamati kuu ya Chama
ilikutana katika kikao chake cha dharura, na
pamoja na mambo mengine. Ililiondoa jina la Dr
Masurufu Hussein Masurufu kutoka miongoni mwa
watu wanaotarajiwa kuwa wagombea Urais kupitia
Chama cha Mapinduzi.
Kamati pia ilichuja baadhi ya majina na kumfuta
John Tengeneza ambaye alikuwa amepoteza
maisha hata hivyo haya hayakuvuruga ratiba ya
uchaguzi.
Akiongea na vyombo vya habari katika ukumbi wa
mikutano wa Dodoma Hotel, Katibu Mkuu wa
Chama alisema walikuwa na wajibu wa kuondoa
jina la Dokta Masurufu toka miongoni mwa
wagombea kwa kuwa alikiuka, miiko maadili na
kanuni za chama cha Mapinduzi wakati akishiriki
katika kinyanganyiro hicho.
Katibu alisema Dr Masurufu amekiuka kanuni hizo
kwa kuingia mkataba wa kihuni na mabepari
wanaotaka kufaidi rasilimali za Tanzania bila
jasho, kushiriki kwa vitendo vya ufisadi na kupora
rasilimali za taifa na kujilimbikizia mali toka wakati
wa vita vya Kagera, Azimio la Arusha, Uhujumu
Uchumi hadi katika misamaha ya kodi zaidi akiwa
mshirikiana.
Hata hivyo aliwataka wananchi kutoihukumu CCM
kwa vitendo vya Dokta Masurufu kwamba hivyo
vilikuwa vitendo binafsi vya mtu na kwamba licha
ya kila dini kuhubiri mema na kukataza mabaya,
bado baadhi ya waumini wa dini hizo wamezama
katika mambo yote waliyokatazwa kama ulevi,
uzinzi, uongo, ulaghai, wizi, usenganyaji na
kadhalika. Kwa hiyo huwezi kuihukumu dini kwa
kuwa na watu kama hawa.
Alisema watu kama Dr Masurufu waliingia katika
chama kwa bahati mbaya kama vile jiwe lipatavyo
fursa ya kuingia katika sahani ya ubwabwa na
katu huu sio mpango wa chama kuwa na watu
kama hawa na ndio maana kila wanapobainika
hutemwa mara moja kam jiwe liliko katika
ubwabwa linavyotemwa pindi likiingia kinywani na
kutafunwa.
Akifafanua zaidi alisema safari ya jiwe kuelekea
katika sahani ya ubwabwa ilianzia mbali toka
shambani. Ambapo mpunga ulivunwa na
kukusanywa. Ni pale tu ulipoanikwa ndipo jiwe
lilipojiingiza kinyemela! Hata ulipoanuliwa juani na
kupigwa au kutwangwa na pengine kukobolewa
jiwe liliendelea tu kungangania.
Safari ya kuupeleka mchele sokoni, mama akaja
kuununua na kuuchagua, kuupepeta na kuuchuja,
Bado tu jiwe liliendelea kuwemo. Hatimaye mchele
unapikwa na kugeuka wali, unapakuliwa katika
sahani, jiwe bado limo tu. Na lilivyo na tabia
mbaya, jiwe hili hukimbia katika sahani ya baba au
ya mgeni na kutoa tafsiri kwamba mama hajui
kupika.
Akawataka wananchi wajue kuwa hata katika CCM
bado kuna mawe mengi na wataendelea kuyatoa
kadri yatakapobainika kwani sio matarajio ya
chama kuwa na mawe! Akawataka wananchi
wajitokeze kwa wingi siku ya uchaguzi na
kuichagua CCM kura nyingi.
Hotuba yake iliwasisimua na kuwavutia wengi.
Habari hizo zilipotoka zikawafanya watu washike
vichwa kwa uchungu na mshangao. Wasiamini
kama Masurufu huyu, aliyezaliwa na mpigania
Uhuru, akasomeshwa na kulelewa na baba wa
Taifa ndiye anayefanya haya.
Laiti Mwalimu angelikuwepo na kujionea kizazi
alichokilea na kukisimamia kinavyopotoka? Baadhi
waliwaza kwa hitimisho, wakisikitika na kuondoka.
Naam! Siku chache baadae Profesa Zonga, Frank,
Kuho, Robison na wauaji wenzao wa raia wenye
ulemavu wa ngozi nao walifikishwa mahakamani.
Ushahidi wao ukiwa dhahiri na mwingine wakiwa
nao, upelelezi ulifanyika haraka na muda mfupi
baadae wakawa wamehukumiwa kifungo cha
maisha na kazi ngumu jela.
* * *
Baada ya chenga za hapa na pale zilizowachukulia
muda na fedha za kutosha, hatimae Steve na
Masurufu walifika Afrika Kusini wakiwa
wamemaliza akiba yao yote. Steve akampigia simu
Christopher McDonald ambaye aliwatumia ndege
ya kukodi iliyowafikisha Uingereza.
Christopher aliwapokea vizuri akaenda nao mpaka
ofisini kwake na wakampa habari za kina kwa
mara nyingine, habari ambazo zilikuwa zaidi ya zile
alizozipata kupitia vyombo vya habari vya BBC na
CNN.
Hongera Steve!Akamwambia baadae. Umefanya
kazi nzuri kumleta Masurufu. Hii ni theluthi
nyingine ya malipo yako. Kesho utamaliziwa
theluthi iliyobakia na tutakuruhusu urudi zako
Miami! Tayari tumekuandalia hoteli nzuri ya
kufikia.
Akatua na kujiwashia sigara, akatoa moshi mwingi
na kupuliza hewani. Halafu akamgeukia Masurufu,
Wewe nenda kapumzike bila shaka G-8
watapenda kuyasikia haya unayonieleza.
Chris naomba tena, niko chini ya miguu yenu. Im
very very sorry Chris! Machozi yakamtoka.
Najua! Lakini kesho tutaongea mengi zaidi!
Alipomaliza kusema hayo walikuja watu wawili,
mmoja akamchukua Masurufu na mwingine
akamchukua Steve wakaondoka nao hadi katika
Hotel ya nyota tano pale Uingereza. Kila mmoja
akakabidhiwa chumba chake.
Steve alipobaki peke yake akainua ile briefcase
yake yenye fedha na kuifungua. Badala ya fedha,
ukatoka moshi fulani mweupe. Ulikuwa na harufu
nzuri hujaona na ulimuingia Steve moja kwa moja
puani.
Steve alipokuja kutahamaki kwamba anavuta sumu,
tayari alikuwa amekwisha chelewa, nguvu zilikuwa
zikipungua mwilini mwake kwa kasi ya ajabu.
Akajitahidi kuinuka akimbilie bafuni akapate maji
ambayo yalikuwa dawa ya sumu hii, hakuweza,
akaanguka vibaya, mwili ukikosa nguvu hata ya
kujikokota.
Shiit! Akajitahidi kujuta akijilaani na kuilani
bahati yake. Sauti pia haikutoka. Akili ikapoteza
uwezo wa kufikiri akaanza kudidimia katika shimo
lefu la kiza ambalo halikuwa na mwisho. Ukawa
mwisho wake.
* * *
Dr Masurufu alikuja kuchukuliwa siku ya pili
asubuhi na kupelekwa katika chumba fulani
ambako alikuta timu yote ya G-8 Original
ikimsubiri.
Hapo tena akatakiwa kueleza kilitokea nini, hata
mpango wao ukafeli licha ya wao kuwekeza
mamilioni kwa mamilioni ya shilingi. Akijua hii
ndiyo nafasi yake ya mwisho, Masurufu alieleza
hatua kwa hatua mpaka hali ilipofikia.
Umenisikitisha sana Masurufu! Akasema
Christopher mwisho wa simulizi. Ulishindwa nini
kuomba ushauri kabla? Kwa hasara uliyotuingiza
tuambie ni kwa nini hustahili kufa!
Kufa? Masurufu akashtuka. Oh! Hapana jamani
No
Nooooh! Nina mipango mbadala ambayo
itarejesha fedha mliyotoa na faida. Nina familia na
wazazi wanaonitegemea! Nina
Nina
!Alisema
mengi ambayo hayakuwaelea G-8 Original, zaidi
akiomba msamaha na kwamba katika mpango
mwingine atakuwa makini zaidi. Ataomba ushauri
na kadhalika.
Okay!Unaweza kwenda! Akaambiwa alipomaliza
kusema.
Masurufu hakuyaamini masikio yake, kirahisi hivi.
Akawaza na kuuliza kutaka uhakika Eti
umesema?
Unaweza kwenda!
Je Akatua akiwatazama mmoja baada ya
mwingine Mmenisamehe?
Wajumbe wakatikisa kichwa juu na chini kukubali.
Dr Masurufu akaomba dua, kumshukuru Mungu na
kuwashukuru Christopher McDonald na wenzake.
Kabla hajainuka akaanza kuvuta hatua na
kuondoka.
Alipoukaribia mlango tu, Christopher McDonald
akatoa bastola na kumpiga Dr Masurufu risasi ya
kisogo ambayo ilimpaisha na kumsomba mzima
mzima, ikampigiza ukutani kwa nguvu. Alipotua
chini alikuwa maiti.
Number one! Masurufu akasema baada ya
kubonyeza mahala ukutani. Dakika hiyo hiyo
akaingia mwanaume mmoja mwenye asili ya
kichina aliyechanganya damu na mjapani. Huyu
alikuwa Ben Tapeli.
Niko hapa Sir!
Vipi kazi ya hotelini? Akamsaili.
Imekwenda vizuri sana. Steve ameingia kuzimu
jana jioni kwa kutumia ileile sumu hatari tuliyoipata
South Korea. Hakukuwa na upinzani kabisa. Alikufa
mara moja. Bila shaka anamkaribisha mwenzie
sasa hivi! Akihitimisha kwa utani.
Akina Christopher wakacheka.
Ilikuwa ni lazima afe. Uzembe wake wa
kutomsimamia Masurufu vyema umemgharimu!
Kabisa bosi!
Tafadhari tuondolee huu mzoga ndani. Unastahili
kuwa chakula cha samaki baharini! Akaamrisha.
Jamaa akaanza kutekeleza kazi aliyotumwa,
akiacha Christopher akiwaomba radhi wenzie kwa
kufeli kwa mpango wao.
Walipomsamehe ndipo walipoanza kuumiza vichwa
kutafuta namna ya kulipiza kisasi kwa watanzania
na serikali yao kufidia hasara waliyoingia.
Walidhamiria kutoka na mkakati ambao utakuwa
sawa na pigo takatifu sana. Pigo lenye nguvu
kupita kiasi. Pigo litakalofanya sio tu Tanzania na
Afrika ilie pekee bali na kusaga meno!
Waliendelea kutafuta.
* * *
Maiti ya Dr Masurufu yaliokotwa kando kando mwa
ufukwe wa Bahari katika jimbo moja nchini
Ufaransa. Iliwachukua muda mfupi tu Polisi
kugundua kuwa walikuwa wameuokota mwili wa
aliyekuwa anataka kugombea urais wa Tanzania
kutokana na nyaraka zilizokutwa mfukoni mwake.
Habari hizi zilipofika Tanzania, hakuna aliyelia!
MWISHO.
KITABU HIKI KINAPATIKANA MITAANI, KWA
MAELEZO ZAIDI WASILIANA NA MTUNZI KWA
NAMBA ZAKE HAPO JUU.