Riwaya: Konstebo Nguzu

iddy eba

JF-Expert Member
Aug 28, 2015
575
1,169
RIWAYA: KONSTEBO NGUZU
NA: George Iron Mosenya
"Nimekosa magoli zaidi ya 9000 katika maisha yangu, nimepoteza mechi zaidi ya 300 katika maisha yangu, niliaminiwa mara 26 kuwa nitaipatia timu yangu ushindi lakini nikashindwa. Nilishindwa tena na tena na tena katika maisha yangu NDIO MAANA NIKAFANIKIWA- Michael Jordan, mchezaji wa zamani wa mpira wa kikapu."
NA HII NI SEHEMU YA KWANZA
HALI haikuwa shwari katika kota za polisi maeneo ya Mabatini jijini Mwanza, shida ya maji ilisababisha baadhi ya maaskari kwenda kazini pasi na kuiloweka miili yao panapo maji. Umeme nao uliwalazimu wengi wao kuzipiga saluti huku nguo zao zikiwa hazijanyooshwa.
Hii haikuwa shida sana kwa kundi kubwa.
Majira ya saa tatu kasorobo gari la maji liliwasili, lilikuwa ni agizo la serikali baada ya vilio kuwa vingi kutoka kwa wafanyakazi hawa watiifu.
Akina mama wakatoka nje na kuikimbilia ile gari na kujikuta wameunda foleni ya kutisha huku kila mmoja akimuhimiza mwenzake asiruhusu mtu kuingia mbele yake kwani kila mmoja ana haraka na anayahitaji sana hayo maji.
Kama ilivyo ada, panapo shida ustaarabu husafiri kwenda mbali.
Akinamama watu wazima walikuwa wakipigana vikumbo haswa, huyu anamsukuma mwenzake aliyesukumwa naye anasukuma.
Vijembe vya hapa na pale vinarushwa wanaonuna wananuna, wanaocheka wanayaonyesha meno yao.
Muda unasogea! Foleni nayo inapiga hatua.
Ilikuwa ni vita ya kimyakimya.
Mwanamke mmoja mkimya alikuwa anatokwa jasho kutokana na kusimama muda mrefu katika ile foleni. Alikuwa akiitumia kanga yake kujipangusa lile jasho huku moyoni akilaumu sana kampuni inayohusika na usambazaji maji jijini humo kutokana na kushindwa kurekebisha tatizo hili lililoendelea kudumu hadi kwa siku kumi.
Wakati anapanga foleni mbele yake walimtangulia watu wasiopungua thelethini, lakini sasa walibaki takribani saba. Akapata ahueni na tumaini jipya likazaliwa katika moyo wake wa subira.
Macho yake yakiwa yanatazama mbele muda wote mara akagutushwa na mguso wa kusisitizwa katika bega lake. Akageuka taratibu...
"Naomba unijazie hizi ndoo mbili foleni yako ikifika." Sauti kavu ya kike ikamweleza, akashindwa kuelewa kuwa lilikuwa ombi ama amri.
"Mama, nenda ukapange foleni tafadhali." Akajibu kwa mkato kisha akapiga hatua mbele baada ya foleni kusogea.
"Kwani ukinijazia utapungukiwa nini, watu wengine wana roho mbaya kama nini... ndoo mbili tu!" Mama mtaka kutekewa maji akabwatuka huku macho yake yakitawaliwa na aina ya kusuta.
"Kha! we shangazi vipi, we mwenzetu ushakoga unanukia pafyumu hapa, sie twanuka jasho halafu unataka urahisi tu. Ebwaneee kapange foleni huko..." Sasa mwanadada akajibu jeuri.
"Na nitachota kabla yako, malaya mgeni wewe..." Akabwatuka huku akiondoka zake kama aendaye kupanga foleni.
Yule binti akatamani kuendeleza shari lakini mmoja kati ya wanawake waliosikia mtafaruku huu akamwonya kuachana na ile shari.
Akatii!kichwani kwake ikabaki kuelea ile kauli ambayo aliitafsiri kama maneno ya mkosaji. ‘na ninachota kabla yako’
Baada ya dakika mbili anamwona yule mama akiongoza njia kuelekea katika bomba.....
Macho yakamtoka pima asiamini kuwa ni kweli yule mama mnukia manukato anachota kabla yake, hasira zikajijenga katika moyo na kichwa chake.
Kweli akateka ndoo mbili. Akajitwika moja kichwani na nyingine ikaning'inia katika mkono wake wa kuume. Kisha kusudi kabisa akajipitisha mbele ya hasimu wake ambaye alikuwa akisota bado katika foleni.
"Kinyamkera utangoja mpaka miguu izame tumboni..." Neno chafu likamtoka yule mama mkosa adabu.
Uvumilivu ukampiga chenga mwanadada akachomoka katika foleni akamvamia yule mama, ndoo ikamtoka kichwani na ile ya mkononi ikatua chini.
Ukafuata ugomvi mkubwa kati ya mama mtu mzima na mwanadada. Mwanadada alikuwa hodari akamrarua vyema yule mama mtu mzima huku akimpa zawadi ya kapu la matusi.
"Wewe Janeth wewe.... mke wa Inspekta huyo. Mungu wangu eeh! umefanya nini sasa... ungevumilia Janeth. Tumeshamzoea huyu hapa kota mbona sisi... ndo tabia zake."
Janeth akabaki kuduwaa, yaani kuwa mke wa inspekta ndo awe na tabia kama hizo. Janeth hakuwa akielewa sawa juu ya hivyo vyeo, kwake ikawa kama ndoto tu.
Baada ya saa moja kupita askari wawili wakafika kota za polisi mabatini wakamkamata Janeth ambaye alikuwa akiishi peke yake kwa wakati huo baada ya kaka yake ambaye ni askari kusafiri na mkewe kwenda kijijini.
Akawekwa rumande kwa siku nne!
Ilikuwa ni mara yake ya kwanza, hivyo aliteseka mwili na akili.
Alitoka akiwa amekonda mno.
Akapewa onyo kali juu ya kosa lake la kumshambulia mke wa Inspekta.
__________________
KILA aliyekuwa nje alimwona Janeth alivyokuwa anapepesuka, kijana mmoja akawahi kumpokea tofauti na wengine waliobaki kusikitika bila kutoa msaada.
Akamfikisha hadi ndani, akatoka nje na kumletea maji ya kuoga, kisha akamkaribisha chai.
Baada ya huduma hizi Janeth akachangamka kidogo. Wakazungumza mawili matatu kisha kijana akajitambulisha wakati anataka kuaga.
"Naitwa Martin, Konstebo Martin Nguzu"
"Lipi jina lako, Konstebo ama Martin?. Maana umeanza Martin ukasita kisha ukaanza na Konstebo...." Janeth akahoji.
Martin akatokwa na tabasamu hafifu kisha akamfafanulia Janeth kuwa Konstebo sio jina bali ni cheo katika jeshi la polisi.
Hakumweleza kuwa ni cheo cha chini kupindukia...
___________
JIJINI Dar es salaam hali ya hewa ilikuwa tulivu lakini joto halikutoroka liliendelea kuweka kambi jijini humo.
Joto hili halikuyaathiri maji ya bahari ya hindi, hivyo watu walijazana katika fukwe mbalimbali kwa ajili ya kupambana na joto hili linalokera.
Katika ufukwe maarufu wa Koko mamia walikuwa wamejitosa katika maji wakijaribu kuzisahau shida zao kwa kuogelea.
Kijana mmoja alikuwa pembezoni akitazama watu wanavyoshindana kuyakata mkaji kwa mbwembwe. Alifurahia kutazama zaidi kuliko na yeye kujumuika katika maji yale.
Si kwamba alikuwa hajui kuogelea la! Maamuzi tu...
Na vile alikuwa mgeni jijini Dar hakutaka kuleta ujuaji aje aibiwe nguo zake aishie kudhalilika kwa kutembea nusu uchi na nguo za kuogelea barabarani.
Wakati anaendelea kutazama waogeleaji hakuacha kuangaza fahari nyingine ya macho.
Mabinti warembo wa Dar es salaam!
Alikiri kuwa hayakuwa maneno matupu, ni kweli ni warembo mno. Urembo ambao unaweza kusababisha mwanaume kukiuka viapo vyake vyote alivyoapa huko kijijini wakati anaagana na mp-enzi wake wa siku nyingi waliyeahidiana kuoana.
Katika kutazama vivutio hivi likapita kundi la watu watatu. Mwanaume mmoja na wanawake wawili.....
Akaisikia sauti ambayo haikuwa ngeni sana katika masikio yake. Akasimama wima na kuanza kufuatilia kundi lile ili aweze kuona ni nani anayezungumza sauti ile.
Akaongeza mwendo na kulifikia lile kundi. Kisha akapiga moyo konde na kuwasemesha....
Wakasimama!
"Samahani.... kuna sauti naifananisha kati yenu." Akarusha kete yake.
Wakacheka!
"Ehee! sauti yako dada, si ngeni kabisa katika masikio yangu. Sijui kama tumewahi kuonana..."
"He! kaka, wenzako wanafananisha sura wewe unafananisha sauti, utajuaje labda uliisikia kwenye Televisheni ama huduma kwa wateja..." Akajibu kwa nyodo kiasi.
"Au ndo yaleyale anayoyasema mama yenu... mnafanana misauti hiyo hatari..."
"Eti kaka labda ulimsikia Zubeda ukadhani ndo mimi..." akajazia dada yule mrefu na aliyeumbika vyema hasa hasa miguu yake.
"Mimi naitwa Nguzu, Martin Nguzu. Sijui kama umewahi kulisikia jina hili." Akajaribu kujitambulisha huenda atakumbukwa.
"Samahani kaka, sijawahi kusikia hilo jina hakika." Alijibu kiupole. Upole wa kujivesha!
"Labda umewahi kukaa Mwanza. Huku Shamaliwa, Igoma ama Nyegezi..." Alizidi kutafuta uthibitisho.
"Mh! kaka huyo mtu unamdai ama maana si kwa kulazimisha huko. Huu ni msako haswa..." Dada wa pembeni akachombeza.
"Hebu ngoja, kwanini tuandikie mate...." Dada aliyefananishwa akasema kisha akachukua simu yake akabofya na kuweka sikioni.
"Eh! Da Zuu kuna mtu kakufananisha huku...." Aliongea huku anacheka.
"Anaitwa Zungu sijui nani..."
"Naitwa Nguzu..." alirekebisha upesi Martin.
"Anaitwa Nguzu, hebu ongea naye bwana. Maana alivyotuganda looh!" Akampasia simu Martin Nguzu.
"Habari, naitwa Martin, Konstebo Martin Nguzu..." Akafanya utambulisho kama alivyowahi kufanya jijini Mwanza kwa mwanadada aitwaye Janeth lakini huyu wa sasa anaambiwa ni Zubeda.
Maongezi yalichukua takribani dakika moja kabla simu haijarejea mikononi mwa dada aliyefananishwa.
"Ndiye.." akashusha pumzi Martin huku akitokwa na tabasamu la ushindi.
"Kumbe ni askari looh! ningeshangaa mlugaluga tu aje kuhangaika na watu asiowajua." Hatimaye yule mwanaume akazungumza. Mwanaume aliyekuwa pamoja na mabinti hao.
"Amesema nikupatie nambari yangu umtumie sasa hivi anipigie." tabasamu halikujipa likizo katika midomo yake pindi alipokuwa akiyatamka hayo.
Ikawa hivyo. namba ikatumwa lakini hakupigiwa simu...
Usiku wa saa nne simu yake ikaita...
Alikuwa ni Janeth ambaye kwa sasa anajulikana kwa jina la Zubeda.
Ni miaka mitatu ilikuwa imepita tangu waonane mara moja tu jijini Mwanza. Wamekutana tena jijini Dar es salaam!
Maisha ya Martin yalikuwa tulivu bila ubaya na mtu.
Huenda yangedumu katika utulivu huu kwa miaka mingine mingi, lakini kukutana na Janeth aitwaye Zubeda kwa sasa ikawa ni safari nyingine ya kutisha!
 
872b8b844480ea376b06825c8ae22bb5.jpg
 
RIWAYA: KONSTEBO NGUZU
NA: George Iron Mosenya
"Nimejifunza katika maisha yangu kuwa walimwengu watasahau vyote ulivyosema, pia watasahau vyote ulivyofanya lakini kamwe hawatasahau ULIVYOWAFANYA WAJISIKIE aidha vibaya ama vizuri...."
HII NI SEHEMU YA PILI
Honi ya gari ilisikika mlinzi akafungua kizingiti kidogo kilichopo getini akaisoma nambari na kutambua kuwa ilikuwa nambari ya bosi wake. Upesi akalifungua geti vyema gari ikaingia ndani.
Tofauti na siku zote, siku hii gari lilipita hadi nyuma ya nyumba. Mlinzi hakufuatilia kwa sababu tayari alimuona bosi wake kupitia kioo cha mbele.
Gari lilizimwa kisha akashuka mwanadada ambaye hakuhitaji kukuonyesha mali zake nyingi ili uweze kumweka katika kundi la wanadada wapambanaji wa mjini ambao wamefanikiwa kuzikusanya noti na kuizoea harufu yake.
Alikuwa amevalia sketi fupi iliyoruhusu mapaja yake kuonekana japo kwa kuibiaibia, mkononi alishikilia simu mbili ambazo kwa bei ya harakaharaka unajenga nyumba kijijini kwenu kwa kutumia tofali za kuchoma na kuezeka kwa bati zenye hali nzuri na zinabaki senti kadhaa za kununulia jenereta dogo litakalofanya nyumba yako iwe kivutio kwa watoto mpaka wazazi wa hicho kijiji unachoishi nyakati za usiku.
Kwa mwendo wa madaha akaufungua mlango wa nyuma, akashuka kijana ambaye hawakuwa wakiendana hata kidogo ikiwa utaelezwa kuwa ni mpenzi wake.
Huyu alikuwa mrefu wa haja mweusi na ambaye alionekana kuwa mwingi wa mazoezi kwa jinsi umbile la kifua chake lilivyogawanyika.
"Nguzu, hapa nd'o ninapojilaza walau siku ziende..." Alizungumza mwanadada ambaye Nguzu alipaswa kumtambua kama Zubeda na kusahau kabisa kama aliwahi kulijua jina la Janeth maishani mwake.
Nguzu alikuwa amejiandaa kisaikolojia kuanzia awali kuwa yule Janeth wa Mwanza aliyeswekwa rumande kwa sababu ya kumzongazonga mke wa inspekta atakuwa amebadilika mno. Lakini hakudhani kuwa angeweza kuwa anaishi katika nyumba nzuri kiasi kile, kuendesha gari zuri namna ile.
Umbo lake nalo lilikuwa limenoga, hakuwa yule kimbaumbau wa Mwanza mabatini.
Mate ya matamanio yakamruka Nguzu.
Akatamani gari, akatamani nyumba na maisha mazuri kwa ujumla.
Lakini angeyapata kwa wepesi gani ilihali alikuwa amegotea katika cheo cha ukonstebo katika jeshi la polisi na hapo alikuwa na majukumu lukuki yaliyojua kuutafuna vyema mshahara wake mdogo kila ulipokuwa unaingia.
Alipoingiza mguu wake sebuleni akazidi kughafirika, maisha ya Zubeda yalikuwa yanamkera si kwa sababu ni mabaya la! alikuwa na maisha mazuri kupindukia.
Akajaribu kuanza kujifananisha naye walau kidogo, Zubeda anamiliki luninga bapa yeye anamiliki ile modeli ya zamani yenye kisogo mfanowe kilele cha mlima Kilimanjaro.
Nguzu akasonya na kupuuzia uwiano aliotaka kuuweka.
"Huenda ameolewa na kibopa hapa mjini! Acha matamanio Nguzu!" alijionya Nguzu na hapo akamuuliza Zubeda juu ya masuala ya mahusiano.
Upesi Zubeda akajibu kuwa hajaolewa na hatarajii kuolewa hivi karibuni.
Matamanio ya Nguzu yakarejea upya!.
"Njoo uione nyumba yangu Martin, Konstebo Martin Nguzu!" Zubeda akaiga namna Nguzu alivyokuwa akijitambulisha.
Nguzu akatokwa na cheko la haja!
Wakapita huku na kule hadi wakakifikia chumba cha Zubeda. Hapa ndipo Nguzu akahisi kuwa Zubeda ni mwongo tu hakuwa akiishi peke yake, na hii ni baada ya kuiona sare ya jeshi la polisi katika chumba kile.
"Hivi wanawake wataacha lini uongo wao jamani! kwani akiniambia kama ameolewa mimi nitapoteza fahamu ama?" Alijiuliza huku hamu ya kukisaili chumba ikimwisha.
"Zubeda una uhakika haujaolewa?" Kwa ghadhabu kiasi fulani akahoji.
"Eeh! sijaolewa vipi unataka kunitolea mahari." akajibu na kutupa utani juu yake.
Utani ambao haukumwingia Nguzu aliyepandwa na jazba zisizokuwa na msingi.
"Na hizo sare.." Akahoji huku akikodoa macho ya kumsuta Zubeda.
"Ooh! sijakueleza kumbe, unapaswa kunipigia saluti Konstebo Martin Nguzu, mimi ni koplo Zubeda Msangi." alijibu kiuchangamfu sana.
Nguzu akabaki mdomo wazi, moyo ukaingiwa uchungu asiamini kuwa yule binti ambaye miaka kadhaa nyuma hakuwa akijua hata nini maana ya Konstebo leo hii ni Koplo. Cheo kimoja juu yake.
"Nadhani mwakani naweza kuwa sajenti kama Mungu akipenda!" Alimalizia Zubeda.
Mungu akipenda?? akajiuliza Nguzu, ina maana Mungu haoni kuwa mimi ninahitaji zaidi kuliko huyu mwanamke au? akajiuliza katika nafsi yake na asipate majibu mujarabu.
Zubeda akatoa picha mbalimbali na kumwonyesha Nguzu, siku akiwa anaapa na picha kadhaa akiwa mafunzoni.
Nguzu akapwaya!
Kumbe kweli!! Akagutuka
Akapigia mstari kuwa hana hadhi yoyote mbele ya Zubeda.
Kikubwa alichomzidi ni kwamba yeye alikuwa mwanaume na Zubeda mwanamke, lakini hata akijitoa ufahamu kuhusu hilo bado Zubeda naye angejitapa kuwa yeye ni mwanamke na Nguzu hajawahi wala hatakuja kuwa mwanamke.
Nimepatikana leo! Alikiri Nguzu huku kijasho chembamba kikiulowanisha mgongo wake.
Bahati iliyoje kiyoyozi kilikuwa kinapepea, la sivyo kile kijasho cha usoni kile kinachoibuka ghafla mtu akiwa katika taharuki kingemuumbua Nguzu.
Zubeda alijitahidi kadri alivyoweza kumfanya Nguzu ajisikie yu huru lakini haikuwa heri katika moyo wa Nguzu.
Lakini jitihada za Zubeda kuujenga ukaribu baina yake na Nguzu hatimaye ile safari yao ambayo ilianzia jijini Mwanza ikafikia palipotarajiwa.
Ilikuwa ni siku nyingine ya kukutana kwao, walianza kwa kukumbushiana juu ya lile sakata la shida ya maji kota za polisi jijini Mwanza wakaunganisha na sekeseke la Zubeda kukabana na mke wa Inspekta. Wakafikia lile tukio la Nguzu kujitolea kumsaidia Zubeda kuanzia maji ya kuoga na baadaye chai.
Sasa Zubeda akamtaka Nguzu amtengenezee tena chai, Nguzu akafanya zaidi ya chai akampikia Zubeda ugali wa dona, nyama na mboga za majani.
Pishi likamnogea Zubeda akajikuta anataka tena na tena......
Mwishowe mapishi yakawa mapishi.
Uhusiano wa kimapenzi ukaibuka.
Lakini ulikuwa uhusiano wa kisasa uliotawaliwa na lugha za kisiasa.
Uliojaa masharti lukuki.
"Martin, sina la kukuficha safari yangu hadi hapa nilipo imetawaliwa na mikato mingi. Hadi sasa ninajihusisha kimapenzi na mume wa mtu, sio kwamba ninampenda kwa dhati ila nitakosa adabu nikisema kuwa simuheshimu. Ninamuheshimu sana moyo wangu unanishuhudia katika hili. Ujue niliwapuuzia vijana vijana hawa ama niwaite watoto, wao wanachoweza kukufanyia kwa ustadi mkubwa ni kukuburudisha mwili tu lakini kwenye masuala ya maisha wanakudumaza. Halafu wanabana sana yaani, ikitokea amekulipia kodi basi anataka kila siku aje kuifaidi kodi yake chumbani... looh!" Martin Nguzu akajikuta anatokwa na kicheko kwa jinsi Zubeda alivyokuwa analalamika.
Ni kweli lakini haikuwa masihara!
"N'do hivyo Martin yaani inafikia hatua unajuta, na vile damu inachemka anaweza akakuvunja mgongo. Nikaona hapana siwezi, nikajiweka kwa kile kibabu kina pesa na kuja hapa ni mara moja moja..... Jiulize Martin, kibabu kimenitafutia cheti cha fomfoo kwa jina hili la Zubeda, kimepambana nimeenda jeshini, kimepambana sijapitia msoto jeshini na hatimaye nimepata kazi. Kwanini nikidharau..... nakuapia kwa mizimu yote Martin, katu sijawahi kujihusisha na mapenzi na mwanaume mwingine tangu nianze kuwa na Inspekta. Wewe unakuwa wa kwanza tafadhali nakuomba sana usije ukaniharibia, usijekuwa kama vijana wenzako wanaopenda ngono kama walitangaziwa kuwa ukifanya sana unaongeza umri wa kuishi....." Akamalizia kwa utani kisha akampiga busu baridi kabisa Konstebo Nguzu katika papi za midomo yake.
Konstebo akajiona yu daraja moja na inspekta ama ikibidi hata mkuu wa majeshi.
Busu pekee!
Mahusiano yakaanza.
Hawakuliona giza lililokuwa linawanyemelea.
Wakapumbazwa na mwanga wa mwishomwisho wa mshumaa!.
Mbaya zaidi Nguzu hakutaka japo kulijua jina la inspekta ambaye anammiliki Zubeda.
Penzi likanoga Nguzu akambatiza Zubeda jina maridadi la kimahaba. Jina linalotamkika kwa sauti tulivu ya kiume na kuleta hamasa panapo faragha.
Akamuita Zuu!
_____________
MUHARIRI wa gazeti la SIRI KALI alikuwa akiiendesha gari yake kwa mwendo wa kasi isiyohatarisha maisha yake ili awahi nyumbani. Kuna kitu alihitaji sana kupata uhakika kama kinaenda sawa na anavyodhania.
Ilikuwa kawaida yake kutopenda kuwa mtu wa kuacha mambo juu juu kama ilivyokawaida ya wengine. Tangu akiwa shuleni alitambulika kwa walimu wote kutokana na usumbufu wake, alikuwa hakubali kitu kimpite asikielewe kisha akae kimya tu.
Aliwasumbua sana walimu kiasi kwamba ada yake ilikuwa inakwenda kihalali kabisa.
Tabia yake hii ikaendelea hata katika utu uzima wake akiwa kazini, aliifanya kazi yake kiustadi pasi na kubahatisha na pale alipohisi kuna utata aliwahi kutafuta uhakika kwa wanaojua zaidi yake.
Kutokana na gazeti alilokuwa anafanyia kazi kujihusisha sana na masuala ya siasa muhariri huyu alijiundia urafiki na na vitabu vya siasa ya afrika na dunia kwa ujumla lakini hakuwa mbali na masuala yahusuyo jeshi la polisi ambalo aligundua kuwa lipo jirani sana na siasa kuliko majeshi ya nchi za bara la ulaya ama Amerika.
Utendaji kazi wake wa kiwango cha juu ukamsababisha apewe jina ambalo hakuwahi kulisikia waziwazi zaidi ya tetesi pekee.
Wafanyakazi wenzake wakamuita Juma kimbelembele badala ya jina lake la kuzaliwa Juma Kiwele.
Hakujali maisha yakaendelea.
Alipofika nyumbani akabadili nguo zake na kisha bila kupumzika akamuaga mkewe akaondoa hadi mtaa wa tatu, akaimalizia safari yake kwa mzee wa kale ambaye alikuwa na rundo la magazeti ya miaka ya nyuma. Kuna kitu aliwahi kukiona akahitaji kukiona tena kiuhakika.
Mzee akamwachia ukumbi, akafukunyua kwa juhudi bila papara hatimaye akalipata gazeti la mwaka 1982. Kuna waraka ulikuwa umechapishwa.
"Kwa macho yangu nilitazama mwanangu wa kwanza akiuwawa mbele ya macho yangu, ni heri angefyatuliwa risasi moja na kupoteza uhai. Alinyanyasika kabla ya kupoteza uhai, walimkata sikio lake ili akiri kuwa tumehifadhi bunduki ndani ya nyumba yetu, walimvunja magoti yake ili akiri kuwa sisi si raia wa Tanzania. Roho iliniuma sana haswa nilipokumbuka zile harakati za kugombea uhuru angali nikiwa kijana mbichi sana, nilipigana kufa na kupona kwa ajiri ya nchi yangu leo hii mwanangu anavunjwa miguu ili akiri kisichokuwa na ukweli. Sikuwa na la kufanya, akapoteza maisha wakatangaza kuwa alijaribu kutoroka akatandikwa risasi akapoteza damu nyingi kabla ya kugeuka maiti. Haikutosha hii, wakamwendea mke wangu kipenzi, bahati nzuri kwake hakupitia mateso bali alipoteza maisha baada ya kugundua kuwa mwanaye angali mfu!
Sikuwahi kuwa na bunduki lakini sasa ninayo, sikuwahi kuwa na roho mbaya lakini niliyonayo ninakaribiana na ibilisi, ninapoandika waraka huu bila kujalisha kuwa utachapishwa ama la nitakayoyafanya naomba nisilaumiwe na ninajua kuwa ipo siku nitakufa. Mkibahatika kuyaona maiti yangu na myape adhabu kwa kushindwa kuwa na moyo wa kusamehe!
Wakati mnayaadhibu maiti yangu mjiulize kila mmoja kwa nafsi yake.
Je? ungelikuwa wewe ungelistahimili uliyoyashuhudia??
Walidhani mimi ni mfu kwa mabaya waliyoutenda mwili wangu, lakini Mungu akawa upande wangu nikabaki hai...
Florian Ngengekuzenza Nguzu, 1982."
Waraka ule wa aina yake ukakomea pale, na baada ya hapo ukimya ukatanda mpaka miaka mitatu baadaye ambapo liliibuka kundi lililotikisa nchi, ujambazi ukakithiri utekaji na mambo yote ya kutishia amani.
Waraka ule ukiwa umesahaulika mmoja kati ya watekaji anakamatwa anabanwa na kusema kuwa kiongozi wake anaitwa Nguzu Ngengekuzenza lakini katu hajawahi kumtia machoni.
Msako unapita lakini hakuna walichoambulia. Hakuna aliyetambua ni wapi mzee yule alikuwa amejificha....
Mtindo wa matukio aliokuwa akiutumia Ngengekuzenza ambaye alisadikika kuwa mkuu wa oparesheni hiyo isiyokuwa na jina ulikuwa mtindo wa akili nyingi kuliko nguvu. Wakilinda huku analipua kule, wakiachia hapa anaingia mzima mzima.
Lakini hakuna aliyewahi kumtia machoni.
Mnamo mwaka 1988, Ngengekuzenza anakutwa amepoteza maisha mtaroni bila kuwa na jeraha wala ujumbe wowote.
Maswali mengi yakabaki bila majibu. Wengine wakisema hili hawa wanalipinga bila kuwa na hoja za msingi.
Muhariri akamaliza kupitia alichotaka kupitia kisha akapitia majina yote ya askari waliokuwa wamehamishiwa katika vituo mbalimbali jijini Dar es salaam.
Konstebo Martin Nguzu!
Jina hili likamkuna sana Juma, akawa anatamani sana kuonana na askari huyu amuulize mawili matatu iwapo ana uhusiano wowote na mzee yule wa miaka ya themanini aliyetikisa nchi na kisha kukutwa amepoteza maisha bila jeraha lolote.
"Nitamtafuta taratibu tu.." alijisemea wakati akiyaweka sawa magazeti yale mengi ili aweze kuaga na kuondoka.
"Kama ni yeye nitaandika makala ambayo itanipa Tunzo ya mwandishi bora. Kupata Tunzo na ujana huu mbona ni fahari sana. Nitawakomesha ofisini watanitungia jina jipya kwa soni itakayowakumba" Alijisemea huku akiwa wima na tabasamu pana usoni.
"Babu kuna gazeti moja ninatoka nalo."
"Ukumbuke tu kurudisha na kulitunza vyema mjukuu wangu Juma." Babu akamsihi.
Juma akaaga na kutoweka. Hakuelekea nyumbani badala yake alifuata uelekeo tofauti ili ausogelee mwanga kuhusiana na Martin Nguzu.
Alisahau kuwa mwanga haumwepushi mtu kupotea njia, mamia kwa mamia hupotea njia mchana kweupe na jua likuwa linaimulika dunia.
____________
 
"Siku mbili za msingi katika maisha yako ni SIKU
YAKO YA KUZALIWA na ile siku utakayogundua
NI KWANINI UMEZALIWA...."
HII NI SEHEMU YA TATU
KUPENDWA RAHA, tena raha hii huja pale
unapoyaona waziwazi mazingira ya penzi lenu
kudumu sana.
Mapenzi mengi yanayohusisha watu wengi
wasiokuwa na uwezo mzuri kifedha huvunjika
mapema kwa sababu ya kutowajibika.
Sasa penzi la Konstebo Nguzu lingevunjikaje?
Zuu haombi kuongezewa salio kwenye simu,
halalamiki kununuliwa simu mpya, ukiona
anaomba kulipiwa kodi basi huo ujumbe
ameutuma bahati mbaya huenda alikuwa
anamaanisha ni yeye anataka kumlipia Nguzu
kodi ya pango, haombi kununuliwa nguo badala
yake analalamika kuwa kabati limejaa mno hana
pa kuweka nguo nyingine.
Sasa penzi linavunjikaje hapo, labda wachokane
tu!
Nguzu hakuwa na mpango wa kuchoka penzi hili.
Penzi lililomfanya anawiri na kujisahau kabisa
kuwa yeye ni Konstebo, kuna kipindi aliwahi
kujiona kuwa yungali Mkuu wa majeshi yote ya
ardhi na anga nchini Tanzania.
Mapenzi bwana!
Ikiwa imepita miezi takribani minne tangu gundi
ya huba iwaunganishe wawili hawa huku lile pepo
la wizi wakilihalalisha na kuwa halali.
Konstebo Nguzu alikuwa eneo lake la kazi majira
ya asubuhi.
Ilikuwa yapata saa mbili na dakika chache
asubuhi katika kituo cha polisi Magomeni
usalama, mgahawa ulikuwa umesheheni tayari
wateja ambao asilimia kubwa walikuwa ni askari
wa kituo kile. Nguzu akiwa mmoja kati yao
Si kwamba raia wema hawakuruhusiwa kutumia
mgahawa ule lakini kama ilivyo ada ya Tanzania,
raia wanawaogopa askari wao na askari
wanapenda kuogopwa.
Watachangamanaje?
Mama muuza alikuwa amejikita katika
kuwahudumiwa supu na chai askari waliokuwa
wakiwania, kila mmoja akitaka kuhudumiwa wa
kwanza ili aingie katika majukumu
yanayomuhusu.
Vyeo hadi kwenye chakula cha kulipia? Nguzu
alinung'unika katika nafsi yake baada ya
kuambiwa ampishe askari mwenzake ahudumiwe
kwanza kwa sababu tu alikuwa amemzidi cheo.
Akatii!
Kanuni muhimu kabisa katika jeshi, akawa
ameifuata.
Kitendo cha kukatishwa zamu yake kikamfanya
anune, kisha akaghairi kunywa supu akaagiza
soda baridi akaketi na kuanza kunywa.
Hata kabla soda haijafika robo, akatakiwa
kumpisha kiti mkubwa wake mwingine aketi.
Sasa ladha ya soda ikabadilika ghafla na kuwa
chungu mithiri ya pombe inavyokuwa kwa
mnywaji wa siku ya kwanza.
Akiwa ameegemea ukuta alijitazama begani
hakuwa na nyota hata moja mwenzake alikuwa
ameanza kuchafuka begani.
"Konstebo!" Sauti ikamtoa katika lindi la mawazo.
Akageuka huku na kule kutazama ikiwa ni yeye
anaitwa ama kuna konstebo mwingine jirani na
yeye.
Hakuwepo!
"Konstebo!" akaitwa tena kwa cheo chake, cheo
cha chini kabisa katika jeshi la polisi. Akaitikia
wito, akamwona yule bwana mwenye cheo cha
Inspekta akimwonyeshea ishara kuwa kiti kipo
wazi aketi.
Akaruka upesi akatua katika kiti.
Kitendo cha kupewa kiti na Inspekta kikarejesha
ladha ya soda ile na ubaridi ukapenya vyema
kooni.
Akiwa katika utulivu wa hali ya juu bila kuingilia
mazungumzo aliyoyakuta alibaki kuinywa soda
yake kwa hatua ndogo ndogo.
Lakini alikuwa anatetemeka, na hapa akagundua
kuwa kuketi na watu wanaomzidi vyeo lilikuwa
jambo lililomuathiri kupindukia.
Masiko yake yalikuwa wazi kusikiliza
mazungumzo ya wawili aliowakuta pale.
Ilikuwa ni kuhusu kesi fulani iliyoonekana
kuwasumbua vichwa, alitamani kuchangia hoja
kidogo lakini akakumbuka kuwa wenzake
walisahau ni lini mara ya mwisho kuwa katika
cheo chake cha chini.
Akaufunga mdomo.
Lakini kichwani alikuwa anazungumza akijaribu
kuwashauri wawili hawa ni kitu gani wanapaswa
kufanya kuhusiana na kesi iliyokuwa mikononi
mwao.
"Hawa watu nyota zao zote ni bure kabisa, sasa
wao wanaona suluhisho ni kumkamata mke wa
mshtakiwa. Je kama huyu bwana alimwoa huyu
mwanamke ili kumfurahisha mama yake tu..
atajali nini? Mi binafsi sioni kama ni
suluhuhisho...." akatokwa na tabasamu jepesi.
Inspekta akaliona.
"Vipi Konstebo mbona unatabasamu, ni utamu
wa haya mazungumzo ama..."
"Hapana afande, ni utamu wa hii soda, sijatumia
siku nyingi sana..." Akajibu kwa utulivu wa hali
ya juu.
"Unaitwa nani Konstebo..."
"Konstebo Nguzu, Martin Nguzu afande!"
"Unaitwa nani.." akauliza tena, Konstebo Nguzu
akajitambulisha tena kwa ukakamavu.
"Sawa Konstebo Nguzu. Unaweza kutupisha
kidogo sasa!" Inspekta alimwamuru, Konstebo
Nguzu akajiondokea huku kichwani akiona ni
jambo la fahari sana kujihusisha kimapenzi na
Koplo Zubeda. Kwani kwa kufanya hivyo
anayapooza maumivu yake yote ya kuamrishwa
hovyo kila mara.
Amri alizoamini kuwa ni dharau!
Akiwa yu katika fukuto la ghadhabu, simu yake
ya mkononi ikaitwa. Akalitazama jina na kupokea
upesi.
Walau alikuwa amepigiwa na Koplo Zubeda,
mwanamke aliyekuwa anamfariji na kumpa raha,
hali iliyomfanya kuzisahau shida zake.
Wakazungumza kwa dakika kadhaa kujuliana hali
kisha wakaagana huku wakipeana ahadai
kedekede.
Kisha wakaingia kazinui, kila mmoja katika kituo
chake.
Nguzu Magomeni na Koplo Zuu Chang'ombe
polisi Temeke.
_______
SIMU YA JUMA (Kimbelembele) ilimweka, bado
alikuwa kitandani maana hiyo ilikuwa ni siku yake
ya mapumziko.
Koplo Mtani, jina lilisomeka. Akapokea upesi.
"Amakweli ukiwa unakitafuta kitu kwa dhati sana
unaweza usikipate ila huwa kinajileta wakati
umekata tamaa tayari." Alianzisha maongezi bila
kusalimia.
"KUnani tena afande."
"Leo nimekutana na Nguzu wako. Tena tumeketi
meza moja asubuhi kweupe pee! Kumbe ni ka
konstebo, kapole halafu kakijana tu. " Alijibu kwa
bashasha Koplo Mtani.
Juma akaketi kitako, na kuuliza maswali
mfululizo. Koplo akayajibu yote kiufasaha na
kumweleza kuwa siku inayofuata afike kituoni
amwonyeshe mtu wake.
Damu ya muhariri wa gazeri la Siri Kali
ikachemka, ubinafsi alioanza nao ukaendelea
kumtawala hakumwambia mtu ni mpango gani
anao dhidi ya Konstebo Martin Nguzu.
Kwanini amshirikishe mtu angali aliamini kuwa
anenda kuandika makala pekee??
Amakweli maarifa mengi, mbele kiza!
Maarifa ya muhariri Juma Kihwele
(Kimbelembele) hayakumfanya ang'amue kuwa si
kila mtembezi hujua uelekeo.
Akatamani siku iliyotajwa ifike upesi.
Masaa akayaona hayasogei, hayawi hayawi
mwezi ukaondoka zake baada ya kumaliza
utawala wake wa muda, jua likatoka katika
usingizi wake na kuisalimia dunia.
Akaianza siku na kauli dogoshi ya Koplo Mtani,
'Ni ka konstebo , kapole halafu kakijana tu'.
# Naam ! Muhariri anataka kuandika makala
kuhusu Konstebo Nguzu huku akitaka kujua zaidi
juu ya Frolian Ngengekuzenza Nguzu....... nini
kitajiri?
 
"Ukihisi unaweza kufanya jambo fulani, sawa
UPO SAHIHI.
Ukihisi hauwezi kufanya jambo fulani, sawa UPO
SAHIHI pia.
Maamuzi ya KUWEZA ama KUTOWEZA yapo
katika himaya yako......"
Hii ni SEHEMU YA NNE
KIMBELEMBELE kilimfanya Juma Kihwele akose
usingizi kabisa, alijigeuza huku mara ageuke
kule. Alijisemesha kwa sauti ya chini na kucheka
mwenyewe.
Mzigo wa kimbelembele kile ulikuwa mzito sana
na dhahiri ulionekana kumwelemea. Akaamini
kabisa bila kukigawa kidogo kile kimbelembele
basi huenda pasingekucha.
Akamuita mkewe chumbani.
"Dear, nimeshindwa kulala mwenzako"
"Ushaanza! hapo unataka kuniambia matukio
yenu ya kisiasa huko. Mi siyawezi." Alijibu
mkewe huku akiketi.
"Bora ingekuwa habari za siasa, ya leo kubwa
kuliko. Jamani mapenzi haya.." akasita
akajikohoza kisha akaendelea.
"Unamfahamu Koplo Zubeda Msangi."
"Eeh! namfahamu si huyu mama wa hapo mtaa
wa pili. Uliyeniambia wakati ule kuwa ni nyumba
ndogo ya Inspekta nani vile."
"Eewala! Inspekta Kobo." Akahitimisha kwa
madoido muhariri Juma Kihwele wa gazeti la
SIRI KALI.
"Kafanya nini tena maana we nawe na kazi yako.
Kuna habari kaandikwa ama..." Akahoji kwa
utulivu akionekana kuwa bado hajavutiwa na
simulizi hiyo ya mumewe.
"Bora angekuwa ameandikwa... Sikia ipo hivi,
nilikuwa namfuatilia kijana mmoja hivi ni askari.
Kuna vitu kadhaa nahitaji kujua kuhusu yeye.
Huwezi amini katika kumfuatilia nikamwona
anakuja hadi nyumbani kwa Koplo. Kama
kawaida yangu nikitaka kujua jambo sichoki,
nikaendelea kusubiri hadi walipotoka. Kwa kifupi
Koplo Zubeda Msangi anajihusisha kimapenzi na
hako kakijana kapole Konstebo Martin Nguzu
ambaye nahitaji kufahamu mambo kadhaa
kuhusu yeye." Akamaliza na kumtazama mkewe.
Bado hakuonekana kuvutika!
"Ubaya ni kwamba huyo sijui Konstebo sijui
Inspekta wote siwajui vizuri. Nd'o nashindwa
kuelewa unashindwa kulala kwa nini haswa. Kisa
Zubeda anajihusisha na mtu mwingine amakiasa
nini. Nifafanulie basi...."
"Mke wangu, katika kazi yetu ya uandishi kuna
mambo mengi. Kuna baadhi ya fursa huja
zenyewe machoni, hapa unabaki kupima mzani
nani anakupa pesa nyingi. Je? ni bosi wako
ofisini ama ni huyo muhusika wa hii habari..."
"Kwa hiyo unataka kuigeuza biashara hiyo
habari? Na wewe ulipolala na yule dada wa
mapokezi nani aligeuza biashara lile tukio lako
ama wewe tu nd'o wayaona mabaya ya
wenzako..... nilijua umeniitia mambo ya maana
kweli mume wangu. Huo muda ningekuwa
nimemfundisha Mariam kuhesabu moja hadi kumi
na ameelewa kabisa. Yani we sijui upoje tu..."
Akasimama na kutoka nje akiuacha mlango wazi.
Juma akabaki kimya kabisa, mkewe alikuwa
amemgusa pabaya mno. Hakutaka kuikumbuka
kabisa siku aliyofumaniwa na mkewe juu ya suala
hilo la kujihusisha kimapenzi na msichana wa
ofisini kwao. Ni kweli haikuandikwa popote, lakini
hii haikuwa sababu nzito ya yeye kuachana na
hili aliloligundua.
Ukimya huu haukumaanisha kuwa Juma aliamua
kuachana na jambo hili. Akaona mtu sahihi wa
kumshirikisha ni Koplo Mtani ambaye alimfahamu
fika kuwa alikuwa ni mojawapo kati ya askari
wasiokuwa waadilifu, rushwa ilikuwa rafiki yake
wa karibu mno.
Kuisubiri asubuhi aliona ni kosa la jinai.
Akanyanyua simu na kumpigia kisha
akamshirikisha hatua kwa hatua huku akiweka
sharti la kutomtaja Inspekta anayejihusisha
kimapenzi na Zubeda...
Licha ya kuwa mahiri sana katika kazi yake,
lakini aliwapuuza wakongwe waliotangulia mbele
ya haki waliponena kuwa hakuna siri ya watu
wawili.
Juma Kimbelembele alikuwa ameisambaza na ipo
kwa watu wawili naye akiwa wa tatu.
Kumshirikisha jambo lile Koplo Mtani kukampa
ahueni, akajigeuza mara kadhaa akasinzia huku
akiwaza kuigeuza habari hii mtaji. Aliamini fika
kuwa hatakosa milioni kadhaa kibindoni ikiwa
atazipanga karata zake vyema.
Wakati yeye anasinzia salama akiwa
amejipunguzia uzito kiasi fulani katika mawazo
yake. Upande mwingine nd'o kwanza palikuwa
panakucha.
_____
MAPENZI RAHA, nilikuelezeni awali. Lakini huwa
raha iso' kifani wakutanapo wawili wanaopendana
kwa dhati. Halafu wasipishane sana umri na
mitazamo katika uwanja huo wa mahusiano ya
kimapenzi.
Muunganiko kati ya Konstebo Nguzu pamoja na
Koplo Zuu ulikuwa wa aina yake, waswahili
wanasema upele ulikuwa umepata wakunaji.
Siku hii hakuingia kazini mapema, aliwasiliana na
mwenzake aliyekuwa na askari mwenzake aweze
kumwakilisha katika majukumu yake hadi majira
ya saa sita mchana.
Ikawa hivyo!
Nguzu akaamkia nyumbani kwa Zuu, wawili hawa
walioshibana wakaanzia kupata kifungua kinywa
kilichoandaliwa na Zuu mwenyewe.
Walikula kisha wakalishana huku wakisifiana
mambo kadha wa kadha. Baada ya kula
wakashushia maji ya matunda.
Kilichofuata ni Zuu kumshika mkono na
kumkongoja chumbani Konstebo Nguzu, haikuwa
mara yao ya kwanza kuingia katika chumba hiki.
Awali Nguzu alikuwa akiogopa sana kufumaniwa
lakini mazoea yakajenga kibanda cha kudumu
katika mwili wake, kisha kwa sifa mazoea
yakajibadili jina yakawa tabia.
Chumbani wakagida mvinyo wa bei ghali, kisha
wakakubaliana waende kuogeshana bafuni.
Simu ya Nguzu ikaita ikawakatili uhondo wao.
"Jamali ananipigia, ngoja nimsikilize." Alimweleza
Zuu kabla hajapokea ile simu.
Zuu akaelewa.
Baada ya kuongea kwa sekunde chache akakata
simu, taharuki kiasi ikamvaa usoni.
"Nahitajika kituoni muda huu, mkuu wa kituo
ananihitaji ni amri." alizungumza konstebo Nguzu
huku akiwa amemkazia macho ya matamanio
koplo Zubeda Msangi (Zuu).
Uzuri Zuu naye alikuwa ni askari alijua vyema
maana ya amri. Kwa unyonge akakubali
matokeo.
Akamuaga Nguzu kwa kumbusu katika papi za
midomo yake. Machozi yakamtoka Zuu na asijue
ni kwa nini yanamtoka wakati Nguzu akimuaga.
Wakakubaliana kuonana jioni ya siku hiyo
wamalizie walichopanga kufanya asubuhi hiyo.
Wakabusiana tena kwa mara ya pili.
Nguzu akatoweka, uzuri alikuwa amebeba sare
zake za kazi na alikuwa amezivaa tayari.
Akachukua usafiri wa pikipiki moja kwa moja
kuelekea kituoni.
_____
UKIMWONA mtu mzima yu katika kilio pasi na
sababu za msingi basi ana matatizo ya ziada
katika akili zake, ama la ana tabia ya kulialia
tangu utoto wake.
Lakini ukimwona mwanaume aliyekabiliana na
majambazi kwa kutumia silaha,
akawasambaratimba licha ya kupigwa risasi
kadhaa zilizouvunja mguu wake. Ukimkuta huyu
analia peke yake, kaa mbali kidogo kwanza
uumize kichwa, si kilio cha kawaida asilani.
Inspekta Kobo alikuwa analia kama mtoto mdogo
ofisini kwake.
Alikuwa na miaka arobaini na nane, heshima ya
kuwa inspekta pekee haikutosha kuthamini
mchango wake katika jeshi la polisi. Wakati wa
ujana wake alitambulika kwa jina la Vandame
kwa jinsi alivyokuwa akiyapenda mapambano,
kwake tukio la ujambazi likitokea nd'o alikuwa
anafurahi kwenda kukabiliana nao. Tena alipenda
sana wakiwa na silaha.
Na hapo alikuwa na cheo cha chini bado, juhudi
zake zikampandisha juu na hatimaye anazeeka
akiwa Inspekta.
Haikutosha lakini walau.
Mlango wake uligongwa, akajifuta machozi upesi
na kisha akamkaribisha aliyehitaji kuingia.
Mlango ukafunguliwa akausikia mshindo wa
ukakamavu kisha ikafuata saluti.
Akaipokea kinyonge sana!
"Konstebo Martin, Martin Nguzu afande
nimeitikia wito wako afande!" Kikakamavu mgeni
akajitambulisha.
"Keti" akamsihi.
Nguzu akajitua katika kiti kilichokuwa jirani yake.
"Una umri gani konstebo?"
"Miaka ishirini na saba afande!"
"Ninaitwa Mathew Koboko, ama inspekta Kobo.
Naamini hatujawahi kuonana, zaidi ya yote mimi
sijawahi kukuona." akatulia akamtazama Nguzu.
Nguzu akatikisa kichwa kukubali.
"Nina miaka arobaini na nane sasa, umri
umenitupa mkono, siko imara sana nilivunjika
mguu nikiwa nalitumikia jeshi, mkono wangu wa
kuume pia unatetemeka mara kwa mara kwa
sababu ya kutumia sana bunduki, mgongo wangu
sio mzima sana nikiketisana naumia, nikitembea
sana naumia. Akili yangu pekee nd'o ipo salama.
Salama kwa asilimia zote" Akatulia na
kumtazama Nguzu usoni. Kisha akamwomba
radhi kabla hajapenga kamasi nyepesi zilizokuwa
zikimwandama.
"Umeoa Nguzu?"
"Sijaona afande!"
"Mimi nimeoa mtoto wangu wa kwanza unamzidi
miaka michache lakini ana mwili mkubwa zaidi
yako." Akatulia na kulazimisha tabasamu kisha
akaendelea tena.
"Nimekuita hapa ili nizungumze na wewe. Mimi
kama Kobo na wewe kama Nguzu tena ni sawa
na kijana wangu, lakini hapa tuzungumze kama
wanaume wastaarabu walioketi baa kabla pombe
hazijachanganya vichwa vyao. Najua wewe
umekunywa pombe lakini sidhani kama
umepitisha kiasi..."
"Nipo timamu afande!"
"Lakini umekunywa kidogo sivyo."
"Hapana afande!" Akakanusha Nguzu.
Inspekta Kobo akasimama taratibu, akayaendea
maboksi kadhaa yaliyokuwa pale ofisini, akapekua
boksi moja na kutoa chupa akaiweka mbele ya
Nguzu.
"Nimekusamehe kwa kunidanganya kwa mara ya
kwanza, usinidanganye tena kwa sababu hivi
vyuma katika mguu wangu havinizuii kuurusha
ukakufikia." akaiacha ile chupa na kurejea katika
kiti chake.
"Haukuishia kunywa pombe pekee, Martin Nguzu
umejipulizia marashi niliyoyanunua jijini Paris
Ufaransa. Kwa kifupi umetoka nyumbani kwangu
bwana mdogo. Nyumba inayonipa mimi faraja...."
Akasita na kumwacha Nguzu apagawe kwanza.
Hakika alipagawa, hakuamini kuwa siku
yaikeinaanza hivyo. Akatambua kuwa yupo ana
kwa ana na mume mwenzake.
"Nilikwambia nimeoa Nguzu, lakini nipo salama
zaidi nikiwa na Zubeda. Simtumii kwa sababu ya
pote nilipomtoa, najua hajakwambia kiundani ni
wapi nimemtoa... hawezi kukueleza kuwa
nilimkutaanajiuza nikamnunua na hapo nikawa
nimeyanunua maisha yake jumlajumla. Alikuwa
amefyatuka akili zake na alikuwa amekata
tamaa, nilitumia muda na uwekezaji mkubwa
sana kumkomboa kutoka janga lile. Narudia tena
ninaye mke ninayempenda hata kama yeye
hanipendi, lakini kwa Zubeda ni sehemu
ninayokuwa salama zaidi.
Siwezi kukulaumu eti umeniingilia katika anga
zangu, kama ningekulaumu hata usingeiona sura
yangu bali ni mimi ningeiona sura yako baada ya
wewe kukatwa kichwa na vijana wangu. Nimeona
niwe mstaarabu kidogo, maana na huu uzee
nikiwa mkaidi haina maana ya kuwa mzee sasa.
Nguzu, imetosha kuingia nyumbani kwangu,
niache basi nisije kufa na magonjwa ya moyo
wakati risasi hazikuweza kuniua. Ujue nimelia
sana leo hadi nimejishangaa, nimetambua wazi
kuwa ninampenda sana Zubeda. Nawe
ninakuomba uwe balozi wangu wa kweli, mtafute
Zubeda mwambie mzee Kobo anampenda sana
na sijawahi kumuwazia mabaya hata siku moja.
Msihi haswa kuwa asinirudishe katikaujana
wangu kwa namna yoyote ile. Unaweza kuondoka
Konstebo Nguzu Martin Nguzu...." Alimaliza
Inspekta Kobo kinyonge.
Nguzu akasimama akiwa anatetemeka sana,
jasho likimtoka.
"Nenda nyumbani ukapumzike ukitoka humu
ndani, nimekupatia mimi ruhusa hii Nguzu."
Nguzu akasimama huku akihema juu juu akapiga
saluti na kutoweka pale ndani. Inspekta
akamsindikiza kwa macho hadi alipotoweka.
______
Simu yake ilimgutusha kutoka katika dimbwi la
mawazo. Ilikuwa ni namba ya Zubeda.
Akatambua kuwa tayari mambo yamezidi
kuharibika.
Akapokea huku akiwa anatetemeka sana, moyoni
mwake akitamani hii iwe ndoto ya mchana.
"Laazizi! ukwapi?" Sauti tulivu kabisa ikahoji.
"Nyumbani vipi kwani?"
"Kuna tatizo Nguzu... tena linaweza kuwa tatizo
kubwa sana tukilipuuzia."
"Ni kuhusu inspekta?" Nguzu akauliza.
"Si bora kingekuwa kile kibabu ninakiweza kile.
Kuna mtu anaitwa Juma Kihwele sijui
unamfahamu?"
"Hapana jina hilo ni geni kwangu Zuu. Kuna nini?
na ni nani huyu?"
"Amenipigia simu anasema yeye ni muhariri na
anahitaji tuonane kwa mazungumzo juu ya mimi
kujihusisha kimapenzi na Inspekta halafu na sasa
nipo na wewe. Sijui ameyatoa wapi haya maneno,
Nguzu atatuharibia huyu wakati ambao sio
muafaka hata kidogo. Nimekupigia maana hili
linatuhusu mimi na wewe, nataka tumuwahi."
Aakaweka kituo. Nguzu akapagawa, wakati
anawaza kuwa ni jambo juu ya inspekta linakuja
jingine khusu mwandishi.
"Nakusikiliza wewe, tunamuwahi vipi sasa?"
akauliza kinyonge mno.
"Njoo nyumbani usiku tupange, kama saa tatu
hivi."
"Hapana Zuu sitaweza kuja hapo usiku wa leo.
Huoni kama tutazidi kulikuza tatizo... kwanini
tusikutane sehemu ambayo sio hapo kwako?"
"Sawa panga wewe halafu utanifahamisha
basi..." Akamaliza na kukata simu.
Nguzu akahisi kuugua, kama sio homa basi ni
Malaria kali kupindukia.
Utamu utamu sasa ukageuka uchungu!
Hata kabla hajamweleza Zubeda yaliyojiri katika
ofisi ya Inspekta Kobo yanatokea haya mengine
ghafla!
Akapanga kukabiliana na hili jambo kabla
halijakomaa, akasimama imara akapiga saluti na
kujiapiza kuwa hatalala tena na kulialia kama
mtoto badala yake atapambana kiume.
Hakujua kuwa wakati yeye akiamua
kusimama,kuna ambao walikuwa wakikimbia
mbio kali kwa nia ya kumzamisha katika shimo
lenye kiza kinene.
________
 
"WAKATI mzuri zaidi wa kufanya mabadiliko
katika maisha yako ulikuwa ni miaka kumi
iliyopita..... WAKATI mwingine mzuri zaidi ni
SASA! Usije ukathubutu kusema kuwa
umechelewa kufanya mabadiliko katika maisha
yako......fanya SASA"
Hii ni SEHEMU YA TANO
ALIJARIBU kujiaminisha kuwa huenda amesikia
vibaya, akazidi kujikunja kitandani ili asinzie
vizuri. Lakini mlango ulipiga kelele tena, kuna
mtu alikuwa anaugonga.
Akiwa na mawenge ya usingizi aliufikia mlango
na kuufungua bila kuuliza ni nani alikuwa
anahitaji kuingia. Hakuwa katika fahamu zake
taslimu.
"Nani?" aliuliza baada ya kuwa ameufungua
mlango na kukutana na kiza kinene.
Badala ya kujibiwa akasukumwa ndani, kisha
tochi kali ikayamulika macho yake akashindwa
kutambua kunani mbele yake.
Akajaribu kutokwa na pigo la 'Karate' aliyojifunza
akiwa kambini lakini akaishia kupiga ukuta na
kutokwa na ukelele wa maumivu.
Mwanga ule ukapotea na kisha taa ya chumbani
kwake ikawashwa. Akayapikicha macho yake na
hatimaye aliweza kuona ni nani alikuwa mgeni
wake asiyetoa taarifa.
Mkojo ukatoka mbio katika kibofu usiangalie
kuwa pale si maliwatoni ama msalani. Ulipofika
karibu na mlango wa kutokea ukamstahi.
Haukutoka!
"Nguzu, mbona unawahi sana kulala." Ilikuwa
sauti tulivu kabisa ya Inspekta Kobo ndani ya
nyumba anayoishi Konstebo Nguzu.
Konstebo Nguzu aliishiwa hamu zote, akabaki
katika hali isiyoeleweka.
Inspekta Kobo akaketi. Nguzu akajilazimisha
akapiga saluti.
"Nguzu, ni masaa mangapi yamepita tangu
tuzungumze?" aliuliza kwa utulivu uleule. Kabla
Nguzu hajajibu yeye aliendelea.
"Umenogewa na mali yangu ama? Yaani kweli
nimekuita kwa upole na ustaarabu wa hali ya juu
kiasi kile lakini kumbe usiku huu umepanga tena
kukutanana Zubeda! Mbona unanifanyia hivyo
konstebo...." Alizungumza kwa kulalamika
Inspekta.
Nguzu kimya!
"Naomba unitazame machoni wakati unajibu
swali hili." Akasita kisha akaendelea baada ya
NGuzu kumtazama.
"Unampenda Zubeda kwa dhati ya moyo ama
unampenda kwa sababu ni yule mwanamke
ambaye hawezi kukulilia shida badala yake wewe
nd'o waweza kumlilia shida?" Swali zito
likamponyoka inspekta Kobo.
Nguzu akabaki kimya tena huku akionekana wazi
kuzidiwa na uzito wa swali lile na pia alikuwa
hajaizoea hali ya inspekta kuwa ndani ya nyumba
yake.
"Martine Nguzu kwa kumbukumbu zako
unafahamu inachukua muda gani kupanda kutoka
cheo kimoja kwenda kingine katika jeshi la
polisi?"
"Miaka mitatu.." Sasa alijibu huku amani ikiwa
imetoweka.
"Unajua kuwa yaweza kukugharimu miaka walau
kumi na nane kufikia cheo changu.... lakini mimi
sikutumia miaka kumi na nane kuwa inspekta,
nilifanya makubwa sana... nilikuwa nina roho
mbaya mno na nilikuwa nikiikamata bunduki
nakuwa shetani kamili." akaupitisha mkono wake
na kuichomoa bastola yake kutoka mahali
alipokuwa ameihifadhi.
Sasa Martin Nguzu aliweza kuzungumza hata
ambayo hajaulizwa. Mara aseme Zubeda ndiye
alimlaghai mara aseme hatarudia tena...
"Sina maana mbaya kuiweka bastola hii katika
mkono wangu, ninajaribu kukueleza na unielewe
vyema. Ningekuwa nimekuvamia hapa kwako kwa
sababu unahusika na uuzaji wa madawa ya
kulevya ama ujambazi, muda huu mguu wako
mmoja ungekuwa unasubiri muda tu ukakatwe.
Lakini sipo hapa kupambana na wewe Nguzu
nipo hapa kukusihi tu, kama inawezekana
naomba uniachie Zubeda wangu, nasisitiza
ninajaribu kukusihi tu na wala sio kukulazimisha.
Niachie huyu binti, amepitia mengi magumu
nimejaribu kuitafuta furaha yake walau kidogo tu,
nimewaumizawengi kwa kutumia bunduki sitaki
kuumiza tena kwa kutumia moyo." akasita na
kumwomba Martin maji ya kunywa, bahati nzuri
hayakuwa mbali.
"Konstebo mfano mimi najitoa katika maisha ya
Zubeda nakuachia wewe, je? utaweza kumjazia
mafuta ya gari lake? utaweza kumnunulia nguo
za gharama kiasi kile, utaweza kumbadilishia
samani za ndani ya nyumba yake? utaweza
kuwalipa wafanyakazi wake? Utaweza Nguzu?.
Kama jibu ni hapana basi nikikuachia Zubeda
kuna watu watakuja kukusaidia majukumu nawe
utajikuta unaumia moyo huku ukilia kama mtoto.
Kwanini nikuache uyapitie hayo sasa.... kwanini
nikuone upo katika njia mbovu nisikueleze ukweli.
Nguzu kama Zubeda anakueleza ukweli, atakuwa
amekueleza kuwa ninaenda kwake mara ngapi na
ninashiriki naye tendo mara ngapi..... nadhani
huwa anahisi mimi nimezeeka, ila sijazeeka
Nguzu nipo imara mno tatizo ni moja tu, sio
ngono iliyoniweka pale..... sio ngono Nguzu"
Akashindwa kuendelea kuzungumza, chozi la mtu
mzima likaiangukia sakafu ya Nguzu.
Huruma kali ikamshika Nguzu, akataka kusema
neno lakini Inspekta akamzuia na hapo akaaga
na kuondoka zake bila kuhitaji hitimisho.
Huu ulikuwa mtihani mkubwa sana kwa Nguzu,
akaitazama saa yake tayari ilikuwa saa nne
kasoro dakika chache usiku.
_____
JUMA KIHWELE alikuwa nje akipunga upepo huku
akingojea kwa hamu simu kutoka kwa Koplo
Zubeda ili waweze kumaliza zoezi lao. Alikuwa
nje kwa maksudi makubwa, hakutaka mkewe ajue
kuwa ameendelea na ule mpango wa kuitumia ile
habari ya Zuu kujihusisha na wanaume wawili
kujiingizia kipato jambo ambalo mkewe hakuwa
ameliunga mkono kabisa.
Kila mara alitazama simu yake kama kuna
ujumbe wowote kutoka kwa Zuu, lakini hadi
majira ya saa tatu usiku bado hali ilikuwa ya
ukimya. Moyo wa subira ukaanza kuingiwa
uchovu akafikiria kumpigia simu na kumchimba
mkwara kuwa iwapo hatafanikisha kuonana kwao
basi asimlaumu pakikucha.
Akiwa katika kusubiri kule akaliona gari likipaki
eneo fulani jirani na upeowa macho yake kisha
akashuka mtu ambaye anamfahamu vyema.
Kimbelembele kikachukua nafasi yake. Akataka
kuhakikisha kuwa anamfahamu vipi mtu yule.
Inspekta! akastaajabu.
"Jamani si inspekta Kobo huyu." akajiseme huku
akisubiri kuona anaenda uelekeo gani, alipopita
naye akafuata nyuma. Moyoni alijua wazi kuwa
Zuu atakuwa amemweleza kila kitu inspekta, ile
mipango yake ya kuvuna chochote kitu akaiona
inapoteza uelekeo.
Macho yake yaliyolizoea giza yakamwona
inspekta akienda moja kwa moja nyumbani kwa
Martin Nguzu.
"Wanaenda kukubaliana nini hawa viumbe eeh!"
alijiuliza hukiu akitamani kujisogeza hadi jirani na
ile nyumba aweze kuvuna mawili matatu. Lakini
alihofia kufumaniwa kisha kudhalilishwa.
Akarejea ndani ya nyumba yake, alipofika
nakuiona kamera yake akapata wazo jipya.
"Hawa wawili wanajihusisha na mwanamke
mmoja, kwa namna yoyote ile kuna namna fulani
ya kutoelewana itajitokeza. Na kama wakipigana
basi nitanasa picha nyingine muhimu kwa ajiri ya
gazetini." Wazo hili jipya likamfanya atoke nje na
kamera yake akaenda hadi chini ya mti akaketi
huku akiiona vyema nyumba ya Nguzu.
Kiupepo chenye ubaridi wa wastani kikaungana
na mawazo tele ya Juma Kihwele na kuunda
usingizi.
Jumaakajikutaamesinzia akiwa eneo lile.
Alikuja kushtuka baada ya kusikia makelele...
akakurupuka akidhani kuna wizi umetokea
mahali.
Macho yake yakakutana na moshi ukifuka katika
nyumba ya Nguzu.
Nyumba ilikuwa inatetekea katika namna ya
kutisha sana. Moshi mweusi tii uliichafua anga.
Mungu wangu! akahamaki Juma, kisha akaiweka
sawa kamera yake na kwenda kupiga picha
kadhaa jinsi tukio lilivyokuwa likiendelea.
Moyo wake ulikuwa unadunda sana. aliulaumu
usingizi uliompitia chini ya mti na kusababisha
asiweze kuona tukio lilitokea katika mazingira ya
namna gani.
Akatimua mbio mpaka pale lilipokuwa
limeegeshwa gari alilokuja nalo Inspekta.
Hapakuwa na kitu.
"Inspekta amemchomea ndani Nguzu?" alijiuliza
Juma huku akiwa na kimuhemuhe kipya kuliko
kile cha awali cha kugundua kuwa wawili hawa
wanajihusishakimapenzi na mwanamke mmoja.
Magari ya zimamoto hayakufika usiku ule...
nyumba ikateketea yote na kusalia majivu.
Juma alirejea nyumbani kwake akiwa hayuko
sawa kabisa, alimfikiria mkewe na kutaka
kumshirikisha juu ya kitu kilichokuwa kimetokea
lakini alikumbuka majibu yake wakati anataka
kufuatilia mkasa ule yalivyokuwa. Akasita
kumshirikisha, hili la sasa lilikuwa zito mno na
lingeweza kumtia hatiani angefanya kuliropoka.
"Kwa hiyo kulikuwa na watu ndani?" Mkewe
alimuuliza juu ya hiyo nyumba iliyoungua, kwani
tayari alikuwa amesikia kwa majirani na alijua
wazi mumewe hawezi kupitwa na habari ile.
"Yaani hapa sina moja wala mbili." alijibu kwa
ufupi. Na hakutaka kuzungumzia tena jambo lile
akaingia bafuni kuoga kisha akalala.
Kitu cha kwanza asubuhi ni kujua kama habari ile
tayari imepata mwanga.
Naam! Ikatangazwa kuwa nyumba imeungua kwa
chanzo ambacho bado hakijajulikana na
inasadikika kuwa askari mmoja amepoteza
maisha akiwa ndani ya nyumba hiyo.
Nambari ya askari yule ikatajwa na kisha jina
likatambuliwa baadaye.
Konstebo Nguzu alikuwa katikati ya moto ule na
alikuwa ameangamia.
_____
Taarifa hii ya habari ikasikilizwa na masikio ya
Koplo Zubeda Msangi aliyekuwa anaendesha gari
lake kuelekea nyumbani kwa Nguzu ambaye
alikuwa hapatikani katika simu ilihali walipanga
kuonana usiku ule.
Zubeda akiwa amevimba kwa hasira alikuwa
anaenda kumlaumu waziwazi Nguzu kuwa si mtu
anayejali hata chembe.
Kulisikia jina lake likitajwa kuwa hayupo duniani
tena, Zubeda akajikuta akikanyaga pedeli ya
kuongezea mwendo wa gari badala ya kupunguza
mwendo na mara akajikuta akikwepa kitu
asichokijua gari ikatumbukia mtaroni, Zubeda
ambaye hakuufunga mkanda wake akajibamiza
katika kioo na kupoteza fahamu palepale huku
damu nyingi ikimtiririka.
Kwa sababu ilikuwa asubuhi, askari waliokuwa
barabarani waliwahi sana kumtambua koplo
Zubeda ambaye alikuwa ndani ya sare zake za
kazi. Simu za upepo zikapigwa upesi kutoa
taarifa ile.
____
 
"ANZIA hapo ulipo, TUMIA hicho ulichonacho,
FANYA kile unachoweza...."
HII NI SEHEMU YA SITA
KILIANZA kitanda kumsaliti, kila mtindo aliojaribu
kukilalia ukagoma kumburudisha. Akastaajabu
kitanda chake mwenyewe lakini amtii.
Akasimama wima na kukitazama kwa sekunde
kadhaa jinsi kilivyokosa nidhamu.
Akaondoka bila kukiaga na kuelekea
sebuleni,huko akajibwaga katika kochi kubwa
lililokuwa sebuleni, hili likampokea vyema na ule
mbonyeo ukamfurahisha.
Heri yako bado unanitii! akajisemea, huku
akiukunja mguu wake na kujaribu kuvuta taswira
ya kitu kilichomfanya ashtuke usiku wa manane
na kuanza kubabaika.
Moshi mnene! hiki nd'o kitu kilichokuwa kikitishia
afya ya akili yake kwa wakati ule.
Akainyanyua simu yake na kujaribu kupiga katika
nambari alizokuwa amepiga awali na hazikuwa
zikipatikana.
"Ni kweli Sule anavuta bangi tena sana tu, lakini
sidhani kama bangi yake inaweza kumfanya
akafanya upuuzi mkubwa namna hii..."
Akajisemea huku akiketi.
Alipoketi na kuwa kimya kwa muda kidogo
akakumbwa na kitu ambacho kilimfanya
ashindwe kuketi bali kusimama wima kabisa.
Kuna vitu viwili vilikivamia kichwa chake, ulikuwa
ni mfano wa picha ambazo zilikuwa gizani na
sasa akabaini kuwa aliziona lakini pasi na
uhakika.
Picha ya kwanza ilikuwa ni mtu chini ya mti.
Ni nani yule? akajiuliza huku akijilazimisha
kuing'arisha picha ile katika kumbukumbu zake.
Haikung'aa!
Picha ya pili ni ya mwanaume akizungumza, na
haikuwa ngeni sauti ile katika masikio yake.
Haikuwa sauti aliyokuwa akiishikia mara kwa
mara kama ilivyo sauti ya mkewe ambaye ni
daktari. Hii ilikuwa sauti ambayo aliwahi kuisikia
asijue mwaka wala tarehe, hakukaribia
kukumbuka hata mahali alipowahi kuisikia.
Ila aliwahi kuisikia.
Baada ya miaka mingi ya mapambano na kisha
kuamua kutulia tuli baada ya kuvunjika mguu
wake, akabaki katika mapambano ya kalamu na
karatasi huku akiwa yu katika chumba tulivu
chenye urafiki wa dhati na kiyoyozi.
Kwa jicho lake pevu kabisa Inspekta Kobo
akajiona anaungiza mguu wake mbovu katika
mapambano mapya.
Licha ya mkewe kuwa daktari inspekta
alipendasana kumshirikisha masuala yake pindi
yanapomwendea kombo.
Na hili lilikuwa limemnyima usingizi, akabofya
simu yake na kumpigia mwenza wake, simu ikaita
lakini haikupokelewa.
"Yupo chumba cha upasuaji huyu..." alijisea na
hakujaribu tena kupiga.
Akafikiria kumpigia mpenzi wake wa siri, koplo
Zubeda, akajiuliza mara mbilimbili kisha
akaikumbuka ile kauli mbiu ya 'ukivuka mipaka
basi siri mweleze mkeo unayempenda kwa dhati
lakini kamwe usitapike siri zako mbele ya
hawara. HAWARA hana dhamana...
Inspekta akakiri kuwa anampenda sana Zubeda
lakini tahadhari lilikuwa jambo la muhimu sana.
Akarejea katika kochi akaketi.
"Nguzu atakuwa amekufa ama? na kama hajafa
itakuwaje upande wangu..." alijiuliza Inspekta
asipate wa kumjibu.
Watoto wake walikuwa wanaelea katika dimbwi la
usingizi mzito.
Mawazo juu ya mawazo hatimaye usingizi
ukamwonea imani, ukamsomba na
kumuunganisha katika dimbwi walilokuwqa
wakisafiri watoto wake kwa wakati ule.
Dimbwi la usingizi.....
Asubuhi akaamka akijisikia ahueni na akijaribu
kujisahaulisha kuhusu kiza kilichojiri usiku
uliopita.
Akiwa anafanya jitihada za kuyafuta haya
akaipokea taarifa juu ya kuchomwa kwa nyumba
aliyokuwa akiishi konstebo Nguzu, kilichosalimika
ni nguo zake zilizokuwa zimeanikwa katika
kamba iliyokuwa mbali kidogo na nyumba.
Si kichwa wala fuvu lake kilichosalia katika moto
ule wa kutisha.
Inspekta akazishusha pumzi zake, akaanza
kutembea huku na kule katika himaya ya nyumba
yake. Akaunda mfano wa mzazi mdogo katika
kichwa chake, akahisi uhai wa Nguzu ungeweza
kuwa hatari sana kwake.
Hatari kwa sababu alikuwa na ubaya naye nafsi
ya Kobo ikakiri kuwa ilikuwa imechefukwa haswa
kutokana na uwepo wa Nguzu.
Kwa hatua hii ya kuzimika moja kwa moja
akahisi kuwa itakuwa ni nafuu kubwa kama mtu
aliyeingiliwa na mchanga jichoni akifanikiwa
kuutoa na kisha jicho lake kubaki huru.
Lakini uhai huohuoungeweza kumweka matatani
kwa sababu Nguzu angehojiwa juu ya nani
amehusika katika moto ule, angwataja watu
ambao ana ubaya nao, kwa nini asilitaje jina la
inspekta Kobo kama jina la muhimu zaidi!!
Ni heri amezimika. Alihitimisha Inspekta Kobo.
Akahamia upande wa pili wa mzani, Nguzu
amekufa vipi?
Je? ninahusika? akajiuliza, kisha akachukua simu
na kupiga tena nambari aliyokuwa akihangaika
nayo usiku uliopita.
Haikuwa inapatikana...
Hapo akarukia sehemu ya pili, ni nani alikuwa
chini ya mti, na ni sauti ya nani aliisikia upande
mwingine...
Haya yalikuwa maswali magumu zaidi. Maswali
yaliyosababisha aamue kuwa upande wa yeyote
yule ambaye amefurahia kifo cha Konstebo
Nguzu.
Akaufunga ukurasa wa mawazo mazito juu ya ni
nini atafanya ili Zubeda atulie na kuachana na
Nguzu. Sasa aliwaza ni kitu gani amfanyie asije
akazama kwa mwanaume mwingine kama
ilivyokuwa kwa Nguzu.
Akaamua kumfanyia ugeni wa ghafla
utakaotawaliwa na upya mkubwa sana kutoka
kwake...
Akiwa mwenye kubwa tabasamu aliingia
maliwatoni kujisafi mwili wake.
Kisha akalivamia jokofu na kutoa maji ya
matunda. Akaigida kwa fujo glasi ya kwanza
mpaka ikamalizika. Kisha glasi ya pili akainywa
taratibu huku akiwa anaipanga ratiba yake kwa
siku hiyo.
Simu yake ya mkononi ikatoa mlio kumaanisha
kuwa kuna ujumbe mpya umeingia.
Akaifungua upesi kwa sababu simu ilikuwa
kiganjani kwake.
"Bosi, shemeji kapata ajali yuko Temeke
hospitali. Amekula mzinga na Suzuki yake"
Ujumbe ule wa maandishi ukawa kama
ulioambatana na umeme mkali kuzidi kipimo,
ukautekenya mkono wa inspekta glasi ikamtoka
mkononi, kisha akaanguka chini kama mzigo
baada ya miguu kuelemewa.
Mpasuko wa glasi na kishindo cha mwili mzito
wa inspekta vikawashtua watoto waliokuwa
wameamka tayari.
Balaa jingine likaibuka.
Walipiga mayowe huku wakiiitana kwa kusisitiza
kuwa baba yao angali katika tatizo kubwa.
Inspekta Kobo alijaribu kusimama ili alete amani
kwa watoto wake lakini akabaini kuwa hawezi
kusimama, ule mguu wake ulioungwa kwa vyuma
ulikuwa umeyumba.
Tusi pekee katika lugha ya kiitaliano alilolifahamu
likamponyoka huku akiipigapiga sakafu.
Kelele zilivyozidi akatoa onyo, akawafokea
watoto wake huku akijinadi zaidi ya mara mbili
kuwa yeye ni mwanajeshi kamili wasihamanike.
Maneno ya shujaa huyu yakatuliza munkari,
akafikishwa hospitali katika hali ya utulivu kabisa
bila papara za kuwafanya majirani watambue
kuwa inspekta Kobo amekumbwa na balaa.
_______
MAJIRA YA saa nne usiku kiwiliwili cha kiume
kikiwa katika koti kubwa lililoungana na kofia
yake kilikuwa kikikatiza katika wodi ya wanawake
kwa mwendo wa haraka huku kichwa chake kila
mara kikinyanyuka juu kutazama uelekeo wa
mbele na kisha kuinama tena.
Safari ile iliyojaa umakini iliishia katika chumba
kilichojitenga mbali na wodi za wanawake.
Watu wawili walimpokea kimyakimya na
kumwingiza chumbani, akamwona mgonjwa
wake.
"Nakupenda sana Zubeda." Lilikuwa neno la
kwanza kumnong'oneza yule mgonjwa kisha
akainama na kumbusu.
Zubeda akajaribu kutabasamu kidogo.
Inspekta Kobo alizungumza machache na Zubeda
kisha akamweleza kuwa siku inayofuata atakuwa
na muda mrefu zaidi wa kuzungumza mengi.
Akaaga na kuondoka!
Alitumia usafiri wa pikipiki, upesi akarejea
nyumbani kwani kwa ratiba ya mkewe ilivyokuwa
siku hiyo alipaswa kuwa nyumbani majira ya saa
tano usiku.
Inspekta aliwasili baada ya dakika chache tangu
saa tano ilipotimia. Hofu ilimtawala kidogo kwa
sababu ya maswali ambayo angepokea kutoka
kwa mkewe lakini pia angelaumiwa sana kwa
kuanza mizunguko mapema kiasi hicho badala ya
kupumzika.
Hakumkuta mkewe nyumbani, akaanza kujilaumu
sana kwa kuhofia ujio wa mkewe, huenda
angeweza kuendelea kuzungumza na Zubeda kwa
muda mrefu zaidi.
Wakati akiwaza haya, Daktari Kobo ambaye ni
mkewe alikuwa katika chumba cha mgonjwa
akijaribu kuzungumza naye kwa lugha ya upole
kabisa, ni kawaida ya madaktari kuitumia lugha
inayoleta tumaini kwa mgonjwa.
Tofauti na ulivyokuwa utaratibu wa siku zote
aliouzoea mgonjwa yule alistaajabu kuona
mlango wa chumba kile alicholazwa unafungwa
kwa ndani na yule daktari mwanamke.
Kisha mwanamama yule akakisogelea kitanda na
kumjulia hali.
Mapigo ya moyo ya yule mgonjwa yakaanza
kwenda mbio kupita kawaida.
"Bila shaka sina haja ya kujitambulisha.... na
hakika sijaja kwa ubaya humu ndani. Unaitwa
Zubeda na unajihusisha kimapenzi na mume
wangu wa ndoa Inspekta Kobo." Akaweka kituo
kisha akamwinamia mgonjwa yule.
"Nimekusudia kuzungumza na wewe kwanza kwa
sababu wewe ni mwanamke mwenzangu,
unafahamu nini kuhusu kifo cha Konstebo
Nguzu?" Swali lile lilikuwa kama upinde wenye
moto mkali mbele yake. Likamchoma haswa
Zubeda.
"Sijui lolote." alijibu kwa ufupi mno.
"Zubeda, narudia tena, sipo hapa kwa sababu ya
wivu wa kimapenzi, nina umri wa miaka thelathini
na tisa sasa, nimeishi na inspekta kwa zaidi ya
miaka kumi na nane. Nilikuwa ninao wivu zamani
sio sasa.... ninawapenda sana watoto wangu
sitaki wakose huduma zababa yao na huenda
katika hili ni msaada pia kwako.Kuna taarifa
ambayo haijazagaa kuwa wewe na inspekta
mmeshirikiana kuichoma nyumba ya Nguzu huku
yeye akiwa ndani na kusababisha mauti yake. Hili
nd'o lililonileta hapa..... ungekuwa ni wivu wa
mapenzi ningeagiza wakuchome sindano moja tu
na siku inayofuata ungehamishiwa mochwari
tayari kwa maziko, na mwili wako unmgeoza
licha ya kupigwa na ubaridi wa mochwari. Sina
nia mbaya... naomba unipe ushirikiano. Wewe na
inspekta mpo matatani. Kumbuka kuwa IGP
hapatani na inspekta Kobo sana, atawanyoosha
katika hili. Niambie kama mmehusika ili tuweke
kando masuala ya mapenzi kisha tuketi pamoja
na kuitafuta suluhu kabla vithibitisho
havijatapakaa."
Maneno ya dokta Kobo yalikuwa mazito mno,
Zubeda hakuamini kile alichokisikia, hakuwahi
kuzungumza na inspekta Kobo hata siku moja juu
ya mpango huu wa kinyama kiasi hicho.
"Ukiachana na hiyo njama, sijawahi hata siku
moja kuzungumza na inspekta juu ya konstebo
Nguzu."
"Sema hayati..." Dokta alimrekebisha.
Marekebisho haya yakamuumiza Zubeda katika
moyo wake, alikuwa amemzoea mno Martin
Nguzu. Sasa anaambiwa amepoteza maisha.
"Inspekta Kobo nd'o mtu wa mwisho kuingia
nyumbani kwa marehemu kabla moto haujaimeza
nyumba ile. Hivi unadhani wakuijumlisha na
tatizo la wewe kuwa na wapenzi wawili kwa
waikati mmoja kuna mtu atahitaji ushahidi wa
ziada. Zubeda utapotea vibaya mno, mimi sijui
sana sheria lakini kama nikichaguliwa kutoa
hukumu katika hili basi nikiwapeleka gerezani
miaka michache kabisa ni thelathini thelathini.
Wauaji wakubwa nyinyi.." Jazba ikataka
kuchukua nafasi akatulia kwa muda kujizuia na
hali ile.
"Shangazi, sijui lolote kuhusu huu mpango
unaousema, sijawahi kuzungumza na Inspekta juu
ya lolote kuhusu Nguzu. Hii ni kweli ya moyo
wangu..."
"Sawa kama haujui. Mimi naondoka..."
alizungumza doktahuku akiyanyanyua mabega
yake juu. Akauendea mlango na kutoweka.....
_______
LILIANZA kuwa saa moja, kisha likafuata la pili
yalipofika matatu subira ikafikia kikomo. Inspekta
Kobo akachukua simu yake na kujaribu kumpigia
mkewe amuulize nini kinajiri hadi hajafika
nyumbani hadi muda huo.
Simu iliita kidogo kisha ikakatwa. Alipojaribu tena
haikuwa ikipatikana. Akajaribu kupiga ofisini
wakaelezea kuwa Dokta Kobo alitoka kazini
tangu saa mbili usiku, wakastaajabu kupokea
simu usiku wote huo wa kuuliziwa kwake.
Inspekta Kobo ambaye tayari alijiona ni mtu
ambaye ameandamwa na majanga ya ghafla
akaingiwa mchecheto, haikuwa kawaida kwa
mkewe hata kidogo kuchelewa nyumbani.
Akafikiria kuwapigia rafiki zake wachache
aliowafahamu lakini mshale wa saa ulimfanya
aone haya.
Saa nane usiku kumuulizia mke!
Hapana.... Akaendelea kungoja huku pepo la wivu
likianza kumchokonoa, akajiuliza ikiwa yeye
ameweza kuwa na mwanamke nje inashindikana
vipi kwa mkewe?
Swali hili likamghadhabisha na kujiona hatendewi
haki hata kidogo ikiwa ni kweli mkewe amediriki
kufanya hayo.
Usingizi ulimsomba majira ya saa kumi na moja
kasoro dakika chache.
Akagutuka saa moja na nusu asubuhi na bado
mkewe alikuwa hajarejea nyumbani wala simu
yake ya mkononi haikuwa ikipatikana.
Hofu ikatanda maradufu.....
# Yu wapi Dokta Kobo..... na ni nani alimueleza
juu ya mahusiano ya Zubeda na mumewe....
 
SEHEMU YA SABA.
ILIPOISHIA.....
Dokta Kobo amemvamia Zubeda hospitalini na
kumweleza maneno mazito kisha anatoweka na
mume wake asijue ni wapi ameelekea.
ENDELEA
LILIANZA kuwa saa moja, kisha likafuata la pili
yalipofika matatu subira ikafikia kikomo. Inspekta
Kobo akachukua simu yake na kujaribu kumpigia
mkewe amuulize nini kinajiri hadi hajafika
nyumbani hadi muda huo.
Simu iliita kidogo kisha ikakatwa. Alipojaribu tena
haikuwa ikipatikana. Akajaribu kupiga ofisini
wakaelezea kuwa Dokta Kobo alitoka kazini
tangu saa mbili usiku, wakastaajabu kupokea
simu usiku wote huo wa kuuliziwa kwake.
Inspekta Kobo ambaye tayari alijiona ni mtu
ambaye ameandamwa na majanga ya ghafla
akaingiwa mchecheto, haikuwa kawaida kwa
mkewe hata kidogo kuchelewa nyumbani.
Akafikiria kuwapigia rafiki zake wachache
aliowafahamu lakini mshale wa saa ulimfanya
aone haya.
Saa nane usiku kumuulizia mke!
Hapana.... Akaendelea kungoja huku pepo la wivu
likianza kumchokonoa, akajiuliza ikiwa yeye
ameweza kuwa na mwanamke nje inashindikana
vipi kwa mkewe?
Swali hili likamghadhabisha na kujiona hatendewi
haki hata kidogo ikiwa ni kweli mkewe amediriki
kufanya hayo.
Usingizi ulimsomba majira ya saa kumi na moja
kasoro dakika chache.
Akagutuka saa moja na nusu asubuhi na bado
mkewe alikuwa hajarejea nyumbani wala simu
yake ya mkononi haikuwa ikipatikana.
Hofu ikatanda maradufu.....
Asubuhi akapokea ujumbe mfupi kutoka kwa
mkewe.
"Nipo salama mume wangu, nipo kwa mama
mdogo. Kuna jambo limenichanganya naomba
uniache kidogo natafuta suluhisho. Watazame
watoto..."
Inspekta akaufuta ujumbe ule. Alimjua vyema
mkewe, haikuwa mara ya kwanza kuwa katika
hali hiyo na kuamua kuwa mbali na mumewe.
"Nimemkwaza nini huyu?" alijiuliza lakini akipata
ahueni kuwa mkewe yupo salama.
_____
Mwanaume mweusi sana mwingi wa misuli katika
mikono yake alikuwa amejitwika mfano wa gunia
katika bega lake, mwili wake ulitokwa jasho
lililoufanya ung'are kana kwamba ametoka
kuogelea katika dimbwi la mafuta ya kula.
Alijitutumua na gunia lile huku akitweta.
Lilionekana kumzidia, lakini hakuwa tayari
kukubaliana na hali ile moja kwa moja.
Macho yake makali mithiri ya nyoka yalikuwa
makini kutazama huku na kule ikiwa kuna kitu
kibaya aweze kujihadhari.
Zaidi alililinda lile gunia kuliko alivyowaza
kujilinda yeye mwenyewe.
Alipoufikia mlima aliliweka chini lile gunia
akapumzika kidogo kisha akajitwika tena na
kuendelea na safari ile ambayo mwisho wake
haukuwa bayana ikiwa ni wa matumaini ama la.
Kilima kikamalizika akaanza kupita katika vichaka
vya hapa na pale, mwisho akaufikia mto na
kuanza kuogelea. Gunia likiwa juu kabisa, japo
lililowana lakini haikuwa kwa kiasi kikubwa sana.
Mkondo wa maji ulikuwa una nguvu sana lakini
bwana yule mwenye misuli mingi alifanikiwa
kuwa imara zaidi akapenya na kutokea upande
wa pili.
Huko akapokelewa gunia lile huku akipongezwa
na wenzake wawili waliosaidiana lile gunia.
Hawa nao walikuwa imara sana mmoja akiwa
mfupi na mwingine mrefu. Wote weusi miili yao,
wakaendelea na safari ya gunia lile kuelekea
pahali lilipohitajika kufikishwa.
"Hivi mali itakuwa salama kweli?" Mmoja akahoji
wakati wa pumziko fupi la kubeba gunia lile.
Swali lile likazua ukimya wa muda, wakalitazama
gunia kwa pamoja. Kisha wakaangaliana kana
kwamba waliambiana sekunde za kulitazama na
sekunde za kutazamana.
Ukafuata mguno kwa pamoja tena.
"Unahisi jamaa atakuwa amefanya madhara
yoyote?" aliyeulizwa swali naye akauliza swali
kabla hajajibu alichoulizwa.
"Au tufungue kidogo?" Swali tena kutoka kwa
muulizwa.
Swali hili likawafanya tena walitazame lile gunia
kwa muda, halafu bila kukubaliana wala
kupingana wakalibeba lile gunia safari
ikaendelea.
Hawakulifungua!
Ilikuwa safari ya masaa kadhaa hadi walipolitua
gunia mahali lilipostahili. Wakatulia wakilitazama
kwa takribani dakika moja kisha wakainama na
kulifungua gunia lile.
Waliacha wazi kisha wakatoweka.
Zikapita dakika kadhaa akaingia bwana aliyebeba
bakora mkononi mwake, akalifikia lile gunia bila
kusema neno lolote akaanza kuishusha bakora
yake mara kadhaa guniani.
Gunia lilikuwa limetulia tuli bado.
Akazidisha juhudi kuliadhibu gunia lile na
chochote kilichokuwa ndani yake huku
akizungumza maneno mengi ya kulifokea na
mengine ya kusihi. Jasho lilikuwa limemlowesha
mwili mzima na alikuwa anatetemeka sana.
Baada ya bakora ya kwanza kuonekana haitoi
adhabu ipasavyo akabadilisha bakora, akachukua
ndefu zaidi.
Akaizungusha kwa ghadhabu zote akaitua katika
gunia.
Gunia likatikisika!
Mchapaji akatulia tuli asiamini kile alichokuwa
anakiona, akaanza kupiga mayowe akiwaita
wenzake kutokea katika giza.
Kelele zile zikawa tishio kwa mali iliyokuwa
katika gunia lile.
Kilianza kidole kutikisika na kisha macho
yakaanza kulazimisha kuiona nuru.
Akajaribu kugeuka lakini akahisi maumivu makali
yanamwandama na kuna kitu kizito kilikuwa
kimeuegemea mwili wake.
Akajaribu kuongea akahisi koo limekauka sana
huku kiu kikuu kikimwandama.
"Nini hiki?" alijiuliza baada ya kugundua kuwa ile
si ndoto bali ni kweli tupu.
Akatuliza akili na kujaribu kufikiri tena na tena
lakini hakuna jibu alilopata.
Akatumia nguvu ili aweze kujigeuza tena
ikashindikana. Alipovuta pumzi zake akagundua
kuwa hapumui vizuri sana. Kuna kitu kingine
kilikuwa kimebana katika kifua chake.
"Hakikisheni amekufa aisee! Ishu sio nyumba
ishu ni yeye..." Masikio yake yakazisikia sauti
zikihimizana.
"Kina nani hawa Mungu wangu!" alihamaki akiwa
palepale katika wakati mgumu.
Akajikuta anaijiwa na fikra mbili za ajabu
zilizooana, akajihisi kuwa muda si mrefu alisikia
shangwe na maneno ya kuhimizana huku akiwa
amefunikwa katika kitu asichokijua na sasa
anasikia maneno mengine akiwa mahali tofauti
kabisa.
Ni nani hawa watu? alijiuliza.
Na nipo wapi hapa sasa eeh!
Milango ya fahamu yote ilikuwa imefanya kazi
yake kwa ukamilifu, macho yaliishia kuona giza,
masikio yakisikia sauti za ajabu, ngozi ilikuwa
imebanwa na kitu asichokijua, ulimi ulibaini kiu
kikali kutokanana ukavuu wa mdomo na koo, pua
yenyewe ilikuwa imelala huku ikisahau wajibu
wake.
Ikakurupuka na upesi baada ya kugundua kuwa
bosi wake ameamka.
Ikanusa na kumweleza bosi wake kuwa kuna
harufu ya petroli na moshi.
Moto! Akili ikaungana na pua kutoa majibu.
Mungu wee! nilichomewa ndani mimi! akajisemea
na ili kuhakikisha kama haoti akajaribu
kujipapasa.
Alikuwa uchi wa mnyama.
Ndio, mara ya mwisho alivua nguo zake
harakaharaka baada ya kugundua kuwa hawezi
kuukwepa moto ule upesi lakini angeendelea
kubaki na nguo moto ungemvamia upesi kulikoni
alivyokuwa mtupu.
Inspekta amenichoma moto! alijaribu kutoa sauti.
Akaishia kunong'ona, zile sauti alizozisikia nje
zikawa zimetoweka kwa wakati huo.
"Mzee Majenga ni nani kwani?" alijiuliza swali lile,
ilikuwa mara ya kwanza kabisa jina lile kuja
katika fikra zake lakini alihisi amelisikia sehemu
wakati akihangaika katika moto ule.
"Zile shangwe ndani ya lile gunia ina maana
ilikuwa ndoto?" alijiuliza huku sasa akiutumia
uimara wake wa jeshini kukinyanyua kile kifusi
kilichokuwa kimemgandamiza.
Akafanikiwa.
Hamadi! Nyumba yote ilikuwa imeteketea. Kuta
zilizoanguka ndizo zilisalia pamoja na bati.
"Nimeponaje mimi" alijiuliza huku akijaribu
kusimama wima.
Mguu wake ulikuwa una maumivu makali sana.
Kutokana na lile giza hakuweza kuona kilichojiri
katika ule mguu.
Akatembea uchi vilevile, akitafuta muafaka
wowote usiku ule.
Akaelekea hadi lilipokuwa bomba la maji,
akafungua na kunywa maji ya kutosha.
Karibu na bomba palikuwa na kamba ya kuanika
nguo. Akachukua nguo ambayo haikuwa yake,
kumbukumbu za kuanika nguo zilikuwepo lakini
angeutoa wapi muda wa kuitafuta?
Nguo ile ikamvaa lakini hakujali.
Akatoweka eneo lile huku jina Majenga likigoma
kukimbia katika kumbukumbu zake.
_______
 
SEHEMU YA NANE
Inspekta akashukuru na kukata simu.
"Huyu mjinga kuna kitu anajua, hawezi kukaa
kimya siku zote hizi." alijisemea huku akichukua
kalamu yake na karatasi kisha akaainisha mambo
kadhaa.
MOJA, Juma Kihwele anaijua hii habari lakini
ameogopa kuiandika kwa jina lake.....
PILI, haijui hii habari lakini alivyo na
kimbelembele anaifuatilia kwa kina akiandika
awalipue wahusika.
Yote mawili yalimaanisha kuwa Juma ni mtu
muhimu sana katika hili jambo.
Inspekta akaingia chumbani kwake, akaitoa
bastola yake mafichoni na kuitazama kwa muda
kisha akasema nayo.
"Let's go to work boy! (Twend'zetu kazini)"
Simu yake ya mkononi ikaita wakati akiipachika
bastola yake pahali alipozoea kuipachika.
Ilikuwa ni simu kutoka kwa mkewe.....
Mapigo ya moyo yakaenda mbio sana.
Akaipokea ile simu huku akiwa anatetemeka
mikono yake katika namna iliyomtishia amani.
Alipoiweka simu sikioni kimya kikatanda kutoka
upande wa pili.
"Mama! Mama! Mke wangu... ongea basi mama."
alizungumza kwa upole wa hali ya juu.
Badala ya kujibiwa akaanza kusikia pumzi
zikipishana kwa kasi sana na hapo akaanza
kukisikia kilio.
Dokta Kobo alikuwa analia.
Suala la mkewe kuangua kilio ikawa kama
msumari wenye ncha kali unasukumwa katika
paja lake angali ana fahamu zote.
Maumivu!
"Mama Melinda! una nini mke wangu nieleze... au
niambie basi upo wapi nije sasa hivi." Alisihi
Inspekta Kobo lakini simu ikakatwa bila kusikia
neno lolote.
Akapagawa.
______
SHAMALIWA, Mwanza.
Umati wa watu haukuwa mkubwa sana. Walikuwa
ni wanafamilia walioridhia ile taarifa ya kifo cha
ndugu yao.
Mama mzazi wa Nguzu hakuisha kulia na
kulalamika kuwa alimkanya mwanaye asijiunge na
jeshi lakini hapohapo akikiri kuwa ugumu wa
maisha ulikuwa chanzo cha yote hayo.
Waliojaribu kumbembeleza walikuwa wamefikia
kikomo na sasa walimwacha alie kuzimia na
kisha kuzinduka peke yake.
Kuzika majivu! Mama yake alikataa kata kata,
alidai kuwa hakuyaaga majivu katika kituo cha
basi bali alimuaga mwanaye tena kwa
kumkumbatia, leo hii akubali kuyazika majivu
asiyoyajua?
Hapana... akasimama kidete na wanafamilia
wakamuunga mkono, hawakufanya maziko hayo.
Ambaye aliamini Martin Nguzu amefariki sawa,
ambaye hakuamini sawa.
Mama Martin hakuwa katika upande wa
walioamini.
Na kila alipojaribu kuamini, lilikuja wazo jingine
kuwa yawezekana mwanaye amefanyiwa ubaya
tu. Sio kifo cha kawaida.
Ndivyo walivyo akinamama.
Ule uchungu wa mwana unasababisha haya.
Siku ya tano ikiwa inayoyoma na jambo hililikiwa
limepunguza makali mioyoni mwa wengine kasoro
mama mtu.
Majira ya usiku ule uliingia ugeni ambao hakuna
aliyeutilia maanani, maana kwa kipindi hicho
watu walikuwa wanakaa nje, ndugu na jamaa
wanacheza mchezo wa karata mpaka usiku wa
manane na wengine kulala nje kabisa.
Huyu bwana alikuwa mkimya kabisa na koti lake
kubwa la kuzuia baridi, alijitikisa kwa sababu za
msingi tu na hakugeuka huku wala kule, alikuwa
amejiinamia.
Kadri muda ulivyozidi kwenda na watu walizidi
kupungua, wengi walienda kulala.
Huu nd'o muda ambao yule bwana alijitikisa tena
kwa kiasi kikubwa.
Alisimama!
Akapiga hatua kadhaa bila mtu yeyote kumtilia
mashaka, akasogea pembezoni akaichomoa pakti
ya sigara na kutoa moja, akaiwasha na kuuvuta
moshi wake ndani ya kifua chake na kwa
umaridadi kabisa akaupuliza angani kisha
akautazama unavyotokomea angani.
Akafanya vile takribani mara tatu, kisha akaizima.
Akapiga hatua nyingine tena akaufikia mti kisha
akaanza kuyatazama mazingira ya pale kwa
uchache akahisi ni wakati muafaka wa kufanya
kusudio lake na hakuona jambo lolote la
kumzuia.
Akapiga hatua huku mkono wake ukiwa katika
mifuko yake, akajipitisha jirani kabisa na kundi la
akina mama wawili waliokuwa wamejilaza.
Akamwona muhusika wake.
"Ndiye!" akajisemea.
Kisha kwa kitendo cha upesi sana akainama,
akamziba mdomo na kisha akaichomoa silaha
yake na kwa lugha ya vitendo akazungumza
naye.
"Ukileta vurugu nitakuchinja."
Huku akiwa amemdhibiti vyema kabisa
akamnyanyua wakaondoka kutoka katika eneo
lile.
Alipomfikisha pembeni kiasi akampiga teke kali
miguuni, kisha akatua naye chini.
"Mzee Majenga anaishi wapi?" lilikuwa swali kavu
kabisa kutoka katika sura ngumu.
Mama akabaki kuhangaika asijue ni nini hiki
kinatokea angali ana kovu la msiba wa mwanaye
wanatokea watu kumuuliza juu ya mzee
Majenga.
"Alihamia Shinyanga." alijibu kwa ufupi.
"Nitakuua sina masihara. Alihamia lini na awali
alikuwa ana anishi wapi? nani ndugu zake?"
Alijaza maswali mazito.
"Kama mwanangu mmemchoma moto, ukinichinja
hautakuwa umefanya dhambi mpya. Nipeleke
kwa mwanangu, sina jibu jingine...." Alijibu
kikaidi. Huku nafsi yake ikiwa radhi kabisa yule
bwana amuue ili aondokane na huu uchungu wa
kuishi bila mwanaye.
Mkono wenye nguvu ukashusha ngumi katika
bega la yule mama kisha kiganja kikawahi kuziba
mdomo.
Maumivu yakanyimwa kilio.
Yule mama akabaki kuhema juu juu huku akiwa
ameyakodoa macho yake.
"Sasa utanijibu vizuri kabisa sivyo. Mzee Ma..."
hakuweza kumalizia akahisi kuna mguso fulani
kwa mbali katika bega lake.
Akageuka bila hofu yoyote, akakutana na giza
likiwa ndani ya giza.
Lakini hili halikuwa giza ambalo linaweza
kutembea.
Ngumi kali ikatokea katika lile giza la maajabu,
ngumi moja ikatua katika koo la yule bwana.
Akajaribu kukohoa akawa ameikohoa roho yake.
Umauti ukamfika.
"Mama!" giza lile likaita.
Mama aliyekuwa anahema juu juu huku akiwa
anafanya dua maalumu kwa ajili ya kuiaga dunia
akarejea katika fahamu zake.
Haikujalisha giza lile lilikuwa totoro kiasi gani,
mama alitambua ubini wake ipasavyo.
"Martin!" akaita.
"Nipo hai mama." akajibiwa.
Mama akaamka akaketi kitako asiamini kuwa
alikuwa anapokea miujiza katika uzee wake.
Ubaya wa wanawake siku zote ni pale akili zao
zikitulia.
Mwanzo alikuwa ametulia tuli akizungumza na
lile giza, lakini baada ya akili kukaa sawa
akaanza kupiga mayowe.
Mkono ukawahi kumziba mdomo.
"Mama, huyu alikuwa anataka nini kwako."
"Simjui."
"Mama, sijauliza kama unamjua. Alikuwa anataka
nini?"
"Muulize labda wewe atakueleza vizuri."
"Hakuna mzoga uliowahi kuzungumza katika
dunai hii mama. Nieleze.."
"Amemuulizia mzee Majenga.... yule mzee
alikuwa rafiki sana na babu yako. Wewe
humjui..." alitoa maelezo yale.
Majenga!
Jina lile likapiga katika kichwa chake kwa
kujirudiarudia, ni jina hili lilimjia punde tu baada
ya kurejewa na fahamu asijue nani aliliingiza
katika kichwa chake.
"Uliponaje mwanangu, nyumba iliteketea yote ile.
Tuliona kwenye Televisheni.." mama alimuuliza.
"Mama usimwambie mtu yeyote kama umeonana
na mimi, mimi nipo hai na ninaamini nina kazi
kubwa ya kufanya kabla sijasimama hadharani na
kuutangazia uma kuwa ninaishi." Alisihi Nguzu.
Kisha akamkumbatia mama yake na kumbusu
shavuni.
Upesi mama akaipapasa shingo ya nguzu katika
giza lilelile.
Na hapo akatokwa na tabasamu pana
lililosindikizwa na machozi ya furaha.
Aliyekuwa mbvele yake alikuwa yuleyule mtoto
aliyetoka katika tumbo lake.
Martin Nguzu!
Ameponaje? hilo halikuwa swali lililomuhangais
ha......
Bora uzima.
Walizungumza kwa dakika kadhaa kuhusu
Majenga kisha wakaagana.
Akiwa anafanana na giza kwa jinsi alivyovaa
alitembea kwa tahadhari kubwa huku akiamini
wapo wengine wanaweza kuvaa kama yeye na
kufanana na giza, akapiga hatua na kutoweka
eneo lile.
Begani akiwa na mzoga wake...
_______
LILIANZA tumbo la kuhara, kila akiingia chooni
linapoa anarejea chumbani. Linaanza tena
anakimbilia chooni, linapoa.
Alikuwa amechanganyikiwa mno.
Hali hii ikamkumbusha kuwa angali akiwa
mwanafunzi alikuwa anaugua haswa akisikia
kuwa kuna bakora kwa ajiri ya wachelewaji ama
ambao hawajafanya vyema kazi waliyoachiwa.
Hivyo alikuwa mstari wa mbele kabisa kufanya
kazi zote ipasavyo, kuheshimu sheria na kanuni
za shule.
Na hata ilipotokea migomo hakutaka kushiriki,
wenzake wakambeza na kumweka katika kundi la
wanafunzi waitwao 'MBWA WAOGA' shuleni.
Alikuwa tayari kuitwa majina yale lakini alitambua
kuwa anaitii sheria vyema.
Akaishi hivyo na akakua hivyo.
Akiwa katika utu uzima wake ana familia na yupo
kazini, anajaribu kuisahau asili yake anaitaka
pesa nyingi kwa njia zisizokuwa halali. Jaribio
lake la kwanza linakuwa kuuza habari aliyoinasa
mahali.
Kabla mchezo haujanoga anajikuta matatani.
Akatamani nyakati zirudi nyuma kidogo tu
asijihusishe na hili jambo asilani. Lakini ni saa
pekee inaweza kurudi nyuma na si wakati.
Juma Kihwele alikuwa amekamatika.
Akafikiria mtu wa karibu yake wa kuweza
kumshirikisha hilo jambo, hasahasa ujumbe
kutoka kwa Dokta. Kobo uliomfanya kupata
tumbo la kuhara ghafla.
Mkewe, hapa asingethubutu kugusa hata kidogo
kwa sababu tayari alikuwa amemwonya
kuachana na masuala ya kufuatilia habari
zisizomuhusu.
Akafikilia kukimbilia msikitini walau amweleze
kiongozi wake wa dini. Huku napo akaona
pagumu kuingilika, maana huku ni mambo
kunyooshwa tu hakuna kona kona.
Kila sehemu aliyoiwaza akaona haiingiiliki.
Mwisho akajiwekea maamuzi ambayo aliyapa jina
la 'NANI ATAMFUNGA PAKA KENGELE'
Katika maamuzi haya yeye alikuwa panya.
Akawavika vyeo vya U-paka Inspekta na mkewe.
Kisha akamchagua inspekta Kobo kwa kujipa
imani kuwa yule ni mwanaume mwenzake hivyo
watazungumza na yatamalizika tu.
Akaingia bafuni akausafisha mwili wake, akavalia
nadhifu kisha akaamua kujihukumu. Akachukua
simu yake na kuipekua nambari za Inspekta
Kobo. Akajihisi kutetemeka wakati anapiga simu
ile.
Kitetemeshi kikaisha alipogundua kuwa simu ile
haipatikani. Akachukua maamuzi ya kumpigia
Koplo Mtani yule aliyemsababisha akajiingiza
katika mchezo huu asioujua. Lakini maamuzi
yake yakayeyuka baada ya kujiona kuwa atakuwa
anawaingiza watu wengi katika hili jambo
aliloliita kuwa ni maongezi ya kiume dhidi ya
Inspekta Kobo.
Kwa sababu alipajua ofisini kwake akaamua
kwenda kimyakimya wakayamalize.
Akatoka na kuingia katika gari yake, akaitazama
tasbihi iliyokuwa inaning'inia katika kioo cha
ndani cha gari lake.
Kisha akawasha gari na kuondoka zake.
Baada ya dakika moja, gari jingine dogo
likatoweka na kumfungia tela.
Hakujua kuwa wakati anawaza kumfunga paka
kengele na wengine waliwaza hivyohivyo juu
yake.
Kwa wakati mmoja Juma 'kimbelembele' alikuwa
panya na hapohapo paka.
Kiumbe wa ajabu kupindukia!
Aliiendesha gari yake kwa utulivu huku kila mara
akijilaumu nafsi yake kwa tamaa za ajabu ajabu.
"Tazama nimejenga nyumba nzuri kabisa, hata
kama sijahamia bado lakini nina uhakika wa
kuhamia siku yoyote, nina gari na nimekaribia
kumnunulia mkewangu la kwake, nina amani ya
nafsi, mtoto wangu anaishi vizuri kabisa,
anasoma shule nzuri. Hiki nini kiliniingilia
kichwani nikapatwa na tamaa mimi lakini, eeh!
Ninaheshimika ofisini, bosi ananipandishia
mshahara kila leo. Ni kipi nilitaka tena Juma
mimi. Yaani shuleni waliponiita kimbelembele
nilichukia na kuwaona hawanipendi, sasa
najionea mwenyewe. Ona sasa naanza
kuhangaika na kimbelembele changu, mtu
mwenyewe Inspekta unakuta ana hasira zake
huko anipige mabuti, mi kupigana sijui, jeshi
lenyewe sijapitia..... Hivi Juma nilikuwaje mimi
eeh!" alilalamika kwa sauti ya chini, malalamiko
yaliyopelekea machozi kuanza kumbubujika.
Akashindwa kuona mbele vizuri, akaamua
kuegesha gari lake kando.
Akajifuta machozi. Akaitazama simu yake na
kugundua kuwa ilikuwa inaita pasi na kutoa mlio.
Akakumbuka aliiweka simu yake iwe katika hali
ile. Akaishika kwa utulivu na kutazama. Ni
mkewe alikuwa amempigia.
Akampigia kuuliza kulikoni.
"Mume wangu naomba urudi nyumbani muda
huu, sasa hivi mume wangu... atawaua watoto
huyu. Njoo mume wangu..." Alizungumza huku
amepagawa mno mke wa Juma.
Simu ikakatwa bila kusubiri majibu kutoka upande
wa pili.
Lile tumbo la kuhara lililosumbua kuanzia akiwa
nyumbani likayasikia mazungumzo haya, kwa
kirehere cha hali ya juu likatamani kusikia zaidi.
Likatoa wawakilishi palepale akiwa ameketi
katika kiti chake cha gari....
Hali ya hewa ikachafuka....
# Wapi Koplo Zubeda? Nguzu ndani ya Mwanza,
alifikaje?
Ni akina nani hao wanaomtafuta Majenga?
 
SEHEMU YA TISA
ILIPOISHIA.
Kimbelembele anapata tetemeko la kwanza zito
anaharibu hewa ndani ya gari, familia yake
imetekwa. Anarejea nyumbani bila kujua kuwa
wakati wote ule kuna kundi la watu lilikuwa
linamfuatilia..... ni akina nani hao??
Nguzu amerea na ameondoa uhai wa mtu jijini
Mwanza... alifikaje na huyu aliyeuwawa ni nani?
Kichwani mwake anasumbuliwa na jina
MAJENGA.... ni nani huyu?
ENDELEA....
"Mume wangu naomba urudi nyumbani muda
huu, sasa hivi mume wangu... atawaua watoto
huyu. Njoo mume wangu..." Alizungumza huku
amepagawa mno mke wa Juma.
Simu ikakatwa bila kusubiri majibu kutoka upande
wa pili.
Lile tumbo la kuhara lililosumbua kuanzia akiwa
nyumbani likayasikia mazungumzo haya, kwa
kirehere cha hali ya juu likatamani kusikia zaidi.
Likatoa wawakilishi palepale akiwa ameketi
katika kiti chake cha gari....
Hali ya hewa ikachafuka....
ALIBAKI katika mzubao kama mwanaume
aliyemwona mwanadada mwenye mvuto
akijongea kwenda upande wake akajilaghai katika
kichwa chake kuwa amekutana na bahati ya
mtende akajiandaa kumpokea, kisha mrembo
yule anatokwa na neno la ghafla.
"Kaka umesahau kufunga zipu yako.."
Mzubao huo ulimkumba Juma Kihwele, alipotoka
katika mzubao akahamia katika mlowano katika
suruali yake.
Chozi likamtoka alipotambua kuwa haikuwa
ndoto bali alikuwa kama anavyojiona.
Mbele na nyuma palikuwa pameshirikiana
kumfedhehesha.
Ubahili akauweka kando, kabla harufu ile
haijawafikia wasiohusika Juma Kihwele
akapandisha vioo vya gari lake kisha akawasha
kiyoyozi.
Alitambua wazi kuwa kiyoyozi hakitakuwa na
msaada mkubwa lakini walau linatimia lile neno
la 'Mchuma janga hula na wa kwao' kwanini yeye
ale na wasiomuhusu?
Acha ale na kiyoyozi....
Akaigeuza gari kwa kasi akiwa ametaharuki.
Akawa amebadilisha uelekeo na kuelekea
alipokuwa ametoka.
Jambo lile likawa na maana nyingine kwa
waliomtazama...
____
KITENDO kile cha kubadilisha uelekeo
kikawashtua wale waliokuwa katika gari iliyokuwa
ikimfuatilia toka alivyoliacha geti la nyumbani
kwake.
Dereva akabweka na kuwashtua wenzake, wote
hawakuamini walipoiona gari ile ikiondoka kwa
mwendo mkali. Kila mmoja akabaki kumlaumu
mwenzake kwa kuukosa umakini.
Lawama zisingekuwa na msaada wowote dereva
akapambana naye kutafuta njia ya kugeuza gari
ili afukuzane na lindo lao walilolivizia kuanzia
linatoka nyumbani
Sasa lindo limewatoroka ghafla. Wakabaki
kujiuliza ni wapi ambapo waliteleza hadi yule
bwana akawaona....
Swali hili likawafanya waanze kuamini kuwa
bwana Juma ana watu wengi nyuma yake ambao
wanamsaidia katika suala la ulinzi.
Hapa wakaongeza umakini na ile hali ya
kumchukulia Juma kama mwandishi asiyekuwa
na tahadhari katika maisha yake ikatoweka.
Hawakujua kuwa Juma Kihwele alikuwa
amevurugwa vibaya mno, na hata ule mwendo
kasi wa ghafla ulikuja ghafla kama ulivyoonekana
na hakujua kama alikuwa anafuatiliwa.
JUMA aliwasili nyumbani, bila kujali kuwa alikuwa
amechafua nguo yake alishuka upesi na kuingia
ndani ya nyumba yake huku akiwa amenyoosha
mikono yake juu kama namna ya kujisalimisha ili
wavamizi wakijitokeza kwa nia ya kushambulia
basi awe amejitetea tayari kuwa hana madhara
yoyote kwao.
Huenda wataingiwa na huruma juu yake.
Hicho nd'o kitu pekee alichoweza kufanya kwa
wakati ule.
Alilivuka geti lake huku akijilaumu kwa ubahili
wake uliokithiri wa kushindwa kumlipa mlinzi ili
awe analinda masaa ishirini na nne badala yake
akaona usiku nd'o wakati pekee wenye hatari
akaamua kulipia masaa kumi na mawili.
"Mlinzi mwenyewe analinda na rungu?" Alitoa
kauli ya kupuuzia majuto yake.
Alitembea hatua kwa hatua hadi akaufikia mlango
wa kuingilia ndani ya nyumba yake akabaini
kuwa ulikuwa umefungwa kwa nje.
Bila shaka mvamizi yupo nje.
Huku akiwa anatetemeka akaufungua ule mlango,
akaikuta familia yake yote ikiwa inatazama
ukutani. Mama mwana pamoja na shemeji yake
aliyekuwa pale kwa ajili ya likizo.
"Jamani.... kuna nini mke wangu?" Akamuuliza,
mkewe akageuka huku akiwa anatetemeka na
asiamini kuwa aliyesema naye alikuwa ni
mumewe.
Akaanza kuangua kilio huku yote anayoyasema
yasisikike vyema kiasi cha Juma kuanza
kumkaripia kuwa anapaswa kuzungumza kwa
utulivu ili wajue ni kitu gani kinaendelea.
"Ni nani alivamia hapa na kukueleza upige simu."
"Simjui, sijawahi kumwona hata siku moja."
"Anafananaje? na ni kitu gani anataka kwangu..."
Mkewe akamsogelea Juma na kumkumbatia,
hakuwa na sababu nyingine ya kumkumbatia bali
kumsihi waende chumbani.
"Hapana... tuzungumze hili jambo kwanza
tuelewe muafaka!" alipinga vikali.
Mke akamsogelea tena na safari hii akamueleza
ukweli kuwa alikuwa ananuka, anapaswa kwenda
kusafisha mwili wake kwanza.
Akili ya Juma ikaingiwa na mchecheto,
akatembea kinyonge kabisa kuelekea chumbani.
______
NJE ya nyumba ya Juma wale waliokuwa
wakimfungia tela walikuwa wamewasili tayari na
waliegesha gari lao mbali na nyumba yake.
Walikuwa watatu na walitembea kama
wasiofahamiana katika suala hili. Kila mmoja
alijiweka katika shughuli zake, ilimradi iwe ngumu
kujulikana kuwa kuna jambo wanafuatilia.
Umakini wa sasa ulikuwa umezidi wa awali
ambapo walimchukulia Juma kirahisi sana. Sasa
walikuwa makini kana kwamba wanapambana na
adui mwenye hatari sana zaidi yao.
Silaha zao ziliwekwa tayari tayari.
Jicho moja pevu lilikuwa katika kona ngumu
kufikika, lilikuwa limewapokea kuanzia
walipowasili awali, wakamfungia tela Juma
akiwashuhudia. Kisha akatengeneza vamizi la
kumrejesha Juma nyumbani bila maafa yoyote, ili
aendelee kuwasoma watu wanaomfuatilia Juma.
Akaivamia nyumba na kutoa kitisho kikali.
Zoezi likafanikiwa Juma amerejea na wao
wamerejea.
Ni akina nani hawa? na wanataka nini kwa Juma?
haya yalikuwa maswali ambayo yalihitaji
kupatiwa majibu upesi sana kabla naye hajajua ni
kitu gani anaweza kufanya katika mchakato huu.
Aliitoa taarifa hii ya mashaka yake juu ya watu
anaowaona eneo hilo, taarifa ikapokelewa huku
akisisitizwa kuwa makini zaidi.
Masaa yalizidi kwenda bila kuona juhudi za watu
wale kuingia ndani ya nyumba ya Juma, walibaki
kurandaranda huku na kule bila kujua kuwa
wanafuatiliwa.
Kwa kuwatazama jinsi walivyokuwa wanatembea
na kufanya mawasiliano alihisi yawezekana ni
askari waliopo kazini, ama waliopoteza kazi zao,
na kama si maaskari basi yawezekana waliwahi
kupata mafunzo ya kijeshi kwa sababu maalumu.
Akajinyoosha kidogo mwili wake na kujipima
ikiwa anaweza kukabiliana na vijana wale.
Wakati anajinyoosha akabaki kujicheka kuwa
anauhangaisha mwili wake wa nini wakati ana
kijana wake wa kazi ambaye kamwe hazeeki.
bastola kiunoni!
Majira ya saa tatu usiku akapiga hatua na
kujichanganya barabarani, na hapohapo akageuka
muigizaji, akazuga kuwa amelewa na
anayumbayumba.
Lengo lake likiwa kumfikia mmoja kati ya wale
vijana.
Akafanikiwa kupita jirani na kijana mmoja,
akajikuta akicheka ndani ya moyo wake
alipotambua kuwa hata kijana yule naye alikuwa
katika fani ya maigizo na alikuwa yu katika
kitengo cha kuigiza kuwa ni kijana anayetumia
madawa ya kulevya na sasa ametulia tuli baada
ya kujidunga.
Safi! akajisemea kisha akamchokoza.
Akamsema maneno yanayoudhi huku akiendelea
kujiweka katika hali ileile ya ulevi.
Yule bwana hakujibu kitu badala yake aliendelea
kuwa mtulivu.
Wakati wote huu alipokuwa anamfanyia
bughudha katika sikio lake alikuwa na kifaa
kidogo kilichokuwa kinatumika kwa ajiri ya
mawasiliano.
Yule bwana aliyekuwa amejiweka kama mtumiaji
wa madawa ya kulevya ahatimaye alinyanyua
kichwa chake na kumtazama huyu mlevi kwa
chati jinsi alivyokuwa anahangaika kumchokoza.
"Naomba uondoke hapa." alizungumza maneno
machache kisha akainama.
Mlevi akaanza kucheka huku akidiriki
kumzongazonga yule bwana, alifanya vile kwa
sababu alijiamini kuwa yule bwana hana ubavu
walau wa kuingiza hata ngumi moja katika mwili
wake iwapo watakusudia kutupiana makonde na
hata akifanikiwa kutupa konde halitamletea
athari.
"Naomba uniache uondoke hapa wewe mlevi."
alisisitiza. Lakini yule mlevi bado aliendelea kuwa
pale. Mara atukane hivi mara aimbe vile.
Bwana aliyeketi akazidiwa na kero zile,
akasimama wima na kumrushia ngumi kali yule
mlevi, mlevi akaikwepa bila kujibu pigo.
Kukwepwa kule kukamfanya awe makini zaidi na
yule mlevi. Macho yakamkagua haraharaka huku
wakitazamana kama majogoo.
Akajaribu kurusha teke, mlevi akakwepa.
Wakati yule mlevi anakwepa teke lile, yule bwana
aliyekuwa akikabiliana naye akaona kitu
kilichomtisha.
Aliiona bastola.
Na hapohapo akazungumza maneno
yaliyomchanganya yule bwana mlevi wa kuigiza.
"Angusha mbuyu kuna nyoka."
Maneno yale yakasafiri upesi katika akili ya yule
mlevi wa kuigiza, akajaribu kuyafanyia kazi upesi
lakini hakuweza kupata maamuzi sahihi.
Jicho likamtazama mlevi yule kutokea mbali
kabisa katika kifaa maalumu, mlango wa chuma
ukafunguliwa kisha mwanga ukatoka bila mlio
wowote, mwanga ukasafiri kwa kasi kubwa na
kisha ukaweka makazi ya muda katika kifua cha
yule mlevi wa kuigiza.
Akatokwa na yowe kidogo kisha akaanza kujitupa
huku na kule. Maneno aliyoongea hayakuwa
nyoofu akaamua kunyamaza huku damu
ikimtiririka.
Yule bwana aliyekuwa ameweka kambi chini ya
mti ule akampekua na kutoa bunduki katika kiuno
chake.
"Zahoro! huyu mjinga alikuwa na bunduki, huyu
hakuwa mlevi aisee. Katumwa huyu hakutakiwa
kuuwawa...... dah!" alizungumza kwa kutumia
kifaa kilichokuwa sikioni.
Maneno yale aliyozungumza yakapita moja kwa
moja kwenda mahali ambapo hawakutaka yafike.
Na hawakujua kama yanavuka mipaka hiyo.
Yule bwana marehemu alikuwa akiwasiliana na
mtu mwingine kabla hajauwawa. Hivyo alisikia
yote hadi mwisho.
____
INSPEKTA KOBO akachanganyikiwa upya, hii ni
baada ya kuyasikia maneno yaliyozungumzwa
katika kifaa kilichokuwa sikioni mwa kijana wake
aliyemtuma kufuatilia mienendo ya Juma
Kihwele.
Alisikia sauti yake wakati akitapatapa na mwisho
akaisikia ile sauti ya mtu aliyekuwanaye.
"Ni akina nani hawa?" alijiuliza huku aking'ata
vidole vyake baada ya kukiri kuwa kuna watu
hatari katika sakata hili ambalo kwa namna
yoyote ile linaelekea kumwangukia na kumzika
kabisa.
Kijana wake alikuwa ameuwawa!
"Angusha mbuyu kuna nyoka..." Hii sauti ikawa
inajirudia katika kichwa chake. Ni kama aliwahi
kusikia mahali...
"Yeees!" akarusha ngumi hewani, alikuwa
amekumbuka kuwa sauti ile aliisikia usiku ule
alipokwenda kwa Nguzu kwa ajili ya kumsihi
aachane na Zubeda wake na alipoondoka
nyumba ile ikachomwa moto na kuaminika kuwa
imeondoka na uhai wa Nguzu.
"Huyu ni nani lakini? na kwanini wamchomee
kijana wa watu ndani eeh!" akawaza na kuwazua
kisha akaamua kutoka nje.
Akaingia katika gari yake na kunyoosha moja kwa
moja hadi hospitali aliyokuwa amelazwa Zubeda.
Akaingia moja kwa moja katika kile chumba kile
ambacho alikuwa amekiwekea walinzi wa siri
hasahasa baada ya mkewe kuingia mle ndani na
kumuhoji Zubeda mambo mazito.
"Zubeda kila kitu kimeharibika na mambo
yanazidi kuharibika, huu sio wakati wa
kuzungumzia kilichotokea hapo katikati, huenda
hicho kina unafuu. Naomba usikilize hii sauti kwa
umakini na unieleze kama umewahi kuisikia...
naomba usinifiche hata kama umeiskia katika
mazingira ambayo haupendi mimi niyafahamu."
Akamwinamia na kumwekea kifaa sikioni kisha
akakiwasha kile kifaa, Zubeda akaisikia sauti ya
yule mwanaume ikizungumza yote iliyozungumza.
Koplo Zubeda akatikisa kichwa kuwa hakuna
anachokielewa. Inspekta Kobo akashusha pumzi
zake kwa juhudi zote, mambo yalikuwa yanazidi
kuwa magumu.
"Vipi kuhusu Zahoro? unalifahamu hili jina?"
"Nawafahamu Zahoro kadhaa, ila sina ukaribu
nao."
"Kuna mjinga anaitwa Nasoro nahisi amemuua
kijana wangu." alizungumza kwa uchungu
Inspekta huku akitazama juu.
Na alipoushusha uso wake alizungumza na
Zubeda.
"Hautaendelea kulalia hiki kitanda, kuna watu
wanaisaka roho yako wakati huu. Hakuna
ninayemuamini kukulinda, nataka nikulinde mimi
mwenyewe." Inspekta akanong'ona kwa hisia kali
huku akiwa anamtazama Zubeda moja kwa moja
machoni. Kabla Zubeda hajasema lolote Inspekta
akaendelea, "Mke wangu ana hasira sana najua,
lakini si sababu ya mimi kukuacha wewe katika
hali isiyokuwa salama. Yameniumiza mengi katika
hii dunia ya mapambano, nitajitonesha upya
nikishuhudia maiti yako"
"Mlinde zaidi mkeo..." Zubeda akaingilia kati
katika hilo.
"Yupo katika ulinzi wa hali ya juu." Alijibu
Inspekta na hakutaka maongezi yaendelee,
akatoweka kwa ajili ya kufanya hatua zote za
kumwondoa Zubeda katika hospitali ile.
Zoezi likafanikiwa.
_____
KUKUTWA ametupwa mtaroni?
Tena akiwa hana jeraha bali alama moja tu
katika shingo lake...
Pigo la aina gani hii?
Nani alitoa pigo hilo barabara!
Haya yalikuwa maswali mfululizo yaliyopita katika
kichwa cha kiongozi wa oparesheni isiyokuwa na
jina rasmi. Hii ni baada ya kupokea taarifa kutoka
jijini Mwanza kuwa kijana wake anayemuamini
kupindukia alikuwa ameuwawa kwa kupigwa pigo
moja kali kabisa shingoni.
Tabasamu hafifu lilimdondoka wakati anajaribu
kufikiria upya juu ya jambo hili.
Akanyanyua mkonga wa simu yake, akataka
kupiga mahali akaghairi na kubaki akielea katika
mzani wa maamuzi.
Akaushusha ule mkonga na kunyanyua simu yake
ya mkononi. Akabofya nambari zilizokuwa
zimetoka kumpatia taarifa kutoka jijini Mwanza.
"Kwa hiyo umesema hakuna sehemu nyingine
aliyojeruhiwa? Je ujumbe wowote kwa ajili yetu?"
akatulia na kusikilizia upande wa pili ukijibu.
Baada ya majibu akazungumza kwa ukali kidogo.
"Ongea na Cheyo, aamrishe askari wake
wazunguke kila kona hapo Shamaliwa wakamate
vibaka wote wanaorandaranda kijinga jinga
mitaani. Wawabane watasema kama waliona hilo
tukio. Mwambie asiache mtu hata mmoja."
Waliendelea kuzungumza kwa sekunde kadhaa
kisha simu ikakatwa.
Jijini Mwanza baada ya masaa mawili eneo la
Shamaliwa nje kidogo ya jiji hapakuwa mahali
salama hata kidogo, ukizurura unakamatwa,
ukikaa unakamatwa ukicheka unakamatwa ukilia
unakamatwa.
Hadi waliokutwa wanakata majani ya ng'ombe
nao walikamatwa.
Katika kamata kamata ile ikazua jambo juu ya
jambo
_____
KONSTEBO MARTIN NGUZU alikuwa anajaribu
kuutafuta usingizi katika kitanda ambacho
kilitawaliwa na kunguni waliokuwa na maksudi
mabaya, taa ikiwashwa wanatoweka na ikizimwa
wanaingia uwanjani kuinyonya damu ya Nguzu.
Mchezo huu wa kunguni wale ukawa kikwazo
kikubwa kabisa kwake. Lakini hakuwa na yeyote
wa kumlaumu kwa sababu alikusudia kujihifadhi
katika nyumba ile ambayo lingetokea lolote lile
angeweza kupiga ngumi moja pamoja na teke
kisha dirisha likahama pahali pake na kuacha
njia.
Bughudha hii ikamnyanyua mpaka nje, akazurura
huku na kule pasi na uelekeo maalumu.
Katika kuzurura huku akaona haitakuwa jambo la
heri kuzurura huku kichwa chake kingali wazi.
Akafanya tathmini ya muda mfupi huku
akijishangaa namna ambavyo yu hai, lakini zaidi
zilikuwa ni hisia mpya zinazokisumbua kichwa
chake.
Majina mapya na mtazamo mpya katika fikra
zake, jina Majenga lilikuwa la kwanza kabisa
kujenga naye urafiki.
Sanjari na jina hili kuna ndoto ambazo zimekuwa
zikimfuata bila kukoma, mara amuote mama yake
mzazi na alipoifuata ndoto ile na kurejea jijini
Mwanza anamkuta mama yake akiwa mikononi
mwa mtu mbaya.
Anatokwa na pigo moja, pigo lililomwangusha
yule bwana moja kwa moja.
Kuhusu lile pigo akajiuliza upya, ni lini amekuwa
na uwezo wa kuangusha mtu kwa ngumi moja
pekee?
Jibu lilikuwa rahisi sana kuwa hakuwahi kuwa na
uwezo huo hapo kabla.
Utata mwingine uliomsumbua ni kuhusu magazeti
yaliyoandika kuhusu kifo chake.
Kifo gani? Alijiuliza, lakini swali hili halikumshtua
hata kidogo.
Kufa si jambo dogo ujue? alijisemea huku
akiendelea kuzurura.
Hata tukio la kukuta pesa katika nguo aliyoianua
katika kamba usiku ule baada ya kujinasua katika
kifusi katika nyumba iliyokuwa imeanguka bado
kilimtatanisha.
"Nani wa kusahau pesa katika nguo ndani ya jiji
la Dar es salaam!!" alijisemea na kujikuta
akitokwa na tabasamu kubwa sana kulikumbuka
jiji lile na vituko vyake.
"Mzee Majenga kuna kitu anapaswa kunieleza,
sidhani kama nipo kawaida." aliweka hitimisho
lile.
Wakati anarejea katika chumba chake akaanza
kumuwaza tena mama yake mzazi.
Nini kinatokea? alijiuliza huku hofu ikianza
kumwingia.
Hakutaka kupuuzia hii hisia iliyomjia ghafla,
akajiahidi kuwa siku inayofuata atalazimika
kurejea jijini Mwanza.
Akarejea katika kile chumba chenye kunguni
wapenda sifa. Akajilaza na kusinzia.
Alfajiri ilimkuta barabarani, akadandia gari na
kurejea jijini Mwanza.
Ilikuwa kama hisia zake zilivyomuelekeza,
alipoingia jijini Mwanza hata kabla hajajikita
katika upelelezi wa chinichini akatambua juu ya
kamakakamata ya wakazi wa Shamaliwa nje
kidogo ya jiji la Mwanza.
Akajipeleka Shamaliwa kuhakikisha tu!
Mama yake alikuwa mojawapo kati ya watu
waliokuwa mikononi mwa polisi.
Cheko la hasira likamponyoka, akatembea hadi
katika kituo cha mabasi akajiweka katika basi
ndogo iliyokuwa inafanya safari zake kuelekea
Nyegezi. Akatulia katika nafasi iliyokuwa wazi.
Mkononi akiwa na pesa kamili kwa malipo ya
nauli ya kutoka Shamaliwa hadi Mabatini.
Alishuka mbali kidogo na kutembea kwa miguu
taratibu hadi zilizopokuwa nyumba za polisi.
Nyumba zilezile alizoishi pale miaka kadhaa
nyuma.
Nyumba zile zikaikamata akili yake,
akaukumbuka ule ugomvi kati ya Janeth ambaye
baadaye alibadili jina na kuitwa Zubeda jinsi
alivyokwidana na mke wa inspekta na mwisho
kujikuta akitupwa rumande kwa siku kadhaa.
Kumbukumbu zaidi za kumwandalie binti yule
kifungua kinywa zikamfanya ayakumbuke
mapenzi yao motomoto baada ya kukutana jijini
Dar es salaam huku Zubeda akiwa ni Koplo na
yeye akisalia katika nafasi yake ya ukonstebo.
Tabasamu liliunda kibanda katika uso wa Martin,
akatembea upesiupesi hadi katika nyumba
mojawapo akaitazama kwa sekunde kadhaa,
kisha akapita kwa kasi akaelekea nyumba
nyingine, hii nayo akaitazama upesi upesi.
Akafanya vivyo hivyo katika nyumba nane. Baada
ya kuridhika kuwa alikuwa makini kabisa kwa kila
hatua aliyopita katika makazi yale pasi na mtu
kumshtukia akaamua kuzua balaa alilopanga
kulizua.
Lilikuwa balaa haswa!
______
# Ni hekaheka kila kukicha....... nini kinajiri katika
mkasa huu, kuna pande zinapambana
kimyakimya..... nani ni nani?
 
SEHEMU YA KUMI
Alishuka mbali kidogo na kutembea kwa miguu
taratibu hadi zilizopokuwa nyumba za polisi.
Nyumba zilezile alizoishi pale miaka kadhaa
nyuma.
Nyumba zile zikaikamata akili yake,
akaukumbuka ule ugomvi kati ya Janeth ambaye
baadaye alibadili jina na kuitwa Zubeda jinsi
alivyokwidana na mke wa inspekta na mwisho
kujikuta akitupwa rumande kwa siku kadhaa.
Kumbukumbu zaidi za kumwandalie binti yule
kifungua kinywa zikamfanya ayakumbuke
mapenzi yao motomoto baada ya kukutana jijini
Dar es salaam huku Zubeda akiwa ni Koplo na
yeye akisalia katika nafasi yake ya ukonstebo.
Tabasamu liliunda kibanda katika uso wa Martin,
akatembea upesiupesi hadi katika nyumba
mojawapo akaitazama kwa sekunde kadhaa,
kisha akapita kwa kasi akaelekea nyumba
nyingine, hii nayo akaitazama upesi upesi.
Akafanya vivyo hivyo katika nyumba nane. Baada
ya kuridhika kuwa alikuwa makini kabisa kwa kila
hatua aliyopita katika makazi yale pasi na mtu
kumshtukia akaamua kuzua balaa alilopanga
kulizua.
Lilikuwa balaa haswa!
MARTIN Nguzu hakuwa mgeni eneo lile la kota
za polisi Mabatini, hivyo hata sasa hakutembea
eneo lile kama mgeni.
Udhaifu wa ulinzi aliufahamu vyema na uwepo
wa kiwanja cha mpira katika maeneo yale ya
kota yalisababisha iwe ngumu sana kwa mtu
kupatwa na hisia zozote za kutisha juu ya ugeni
wa hapo kota.
Nguzu alilifikia upesi eneo alilohitaji kufikia kisha
akatazama kama kuna mabadiliko.
Hapakuwa na mabadiliko ya aina yoyote ile,
akatabasamu na kujiwekea alama za ushindi
waziwazi.
Majira ya usiku wa saa mbili akarejea eneo lile
kwa ajili ya kutekeleza agano lake la kuhakikisha
kuwa mama yake anakuwa huru kwa namna
yoyote ile.
Wakati huo alikuwa ameanza kupata majibu
kuwa mtihani uliopo mbele yake haukuwa mdogo
hata nukta.
Mfumo wa umeme eneo la kota ya polisi
Mabatini ulikuwa mbovu kupindukia, nyaya za
umeme zilipita chini kwa chini katika namna
iliyotia kero kutazama.
Wazazi wenye watoto nd'o walijitahidi kupigia
kelele hili suala lakini majibu yalikuwa yaleayale
ya siku zote.
"Kilio chenu kimesikilizwa!"
Hiki kilio kikaenda miaka nenda rudi huku
kikigeuka kuwa kichekesho na si kilio tena.
Hakuna jema lililoboreshwa.
Kama nyumba zenyewe zinatia kichefuchefu vipi
kuhusu huo umeme??
Nguzu aliikuta hii hali katika safari yake ya
kutoka kuzimu na kurejea tena duniani na sasa
yupo katika ile ardhi aliyozaliwa miaka mingi
iliyopita.
Zile kota za polisi alizoziona angali akiwa
anasoma, sasa hazitamaniki zinazidi kukera
kuzitazama.
Anarejea katika anga zile kwa sababu maalumu.
Anatazama pande zote na kuzichimua kwa
umakini zile waya. Akautazama uelekeo na
kuchagua dakika ya kufanya balaa alilopanga
kulifanya.
Akazihesabu dakika akachuchumaa kisha
akaziachanisha nyaya kadhaa.
Giza likaingia katika eneo lile ghafla.
Sauti za manung'uniko zikasikika huku na kule.
Manung'uniko yale hayakudumu kabla Nguzu
hajazua taharuki kubwa.
Akazigusanisha zile waya na hapo mlipuko
mkubwa ukasikika eneo la chooni.
Akatimua mbio na kwenda upande mwingine na
huko akagusanisha nyaya ukatokea mlipuko wa
kushtukiza eneo ambalo zamani lilikuwa
likitumika kama bwalo la chakula.
Sasa hali ikawa mbaya, wapo waliotoka nusu uchi
ndani ya nyumba zao, wengine wakabeba vigoda
badala ya watoto.
Hali ilikuwa tete!
Nguzu naye akachanganyikana katika ile taharuki
na kujifanyaamepotea njia, akaingia katika
nyumba mojawapo ambayo watu walikuwa
wametoka kwa hofu.Akaikwapua simu na
kuondoka nayo, upesiupesi akaitumia simu ile ya
upepo kutoa taarifa ya kutisha kwa maneno
machache mno.
"NINGEWEZA KULIPUA HIZI KOTA NA KUUA
KILA KIUMBE HUMU NDANI. SIJASHINDWA ILA
NI SALAMU TU. WAACHWE HURU WOTE
WALIOKAMATWA BILA MAKOSA. OVA!"
Hakujitambulisha jina akaiacha simu ile
ikizungumza peke yake huku akiuliza yeye ni
nani.
Kama salamu za kivita hii ilikuwa imetangazwa
katika namna ya kutisha kutoka kwa adui.
Ule upande uliofanya ukatili huu wa kuwakamata
watu wasiokuwa na hatia ukaanza kutetemeka
huku kila mmoja akijutia maamuzi haya ya ajabu.
Na hapo likaongezeka swali jipya juu ya adui
mpya aliyejiamini kiasi kile cha kupitiliza
akavamia kota za polisi na kuchafua hali ya
hewa.
Wakati wanaukosa usingizi, Martin Nguzu alikuwa
amelala katika nyumba ya kulipia yenye hadhi ya
kawaida.
Uzuri wale ndugu zake wa Shinyanga
hawakumtembelea usiku huu.
Hapakuwa na Kunguni!
______
GARI iliingia kwa mwendo wa kawaida na
kulikaribia geti la nyumba aliyokuwa akiishia
Juma Kihwele. Namna gari ilivyoingia haikutisha
hata kidogo, lakini namna alivyoshuka aliyekuwa
ndani ya gari ndiyo iliyovuta umakini wa watu
waliopendezwa na kujua yasiyowahusu.
Ni wachache tu yaliwahusu.
Alishuka mwanamama na kuubamiza mlango,
kisha kwa mwendo wa harakaharaka alitembea
kulielekea geti kuu la kuingilia ndani.
Mlangoni akamkuta mlinzi, kwa mbali
wakaonekana kuzozana. Mlinzi anamzuia asiingie
naye analazimisha kuingia.
Mlinzi akazidiwa nguvu, yule mama akaingia
mbiombio ndani ya ile nyumba.
Akaufikia mlango na hapo akakutana na mwenye
nyumba.
Ujio ule wa ghafla ukampagawisha Juma
Kihwele. Lakini hakupata nafasi ya kujiandaa
kabla yule mama hajamvamia na kumkwida shati
lake.
"Nipatie pesa zangu Kihwele, muda huu
nazihitaji." Alikoroma yule mama aliyekuwa na
misuli imara.
Juma Kihwele huku akitweta akajaribu kumtuliza
yule mama, lakini ilikuwa kazi bure kabisa. Mama
alizidi kufoka kwa sauti ya juu sana. Hatimaye
mke wa Juma akatoka akiwa amembeba mtoto
wake. Kulikuta sakata lile akamtua mtoto wake
na kuingia katika tukio lile moja kwa moja.
Wivu wa mapenzi!
Hicho ndo cha kwanza kilichovamia kichwa cha
mke wa Juma!
Mke mwenza...
Hili nalo likamvamia na kumsulubu, ni kitu
ambacho hakutaka kitokee japokuwa dini ilikuwa
inaruhusu kabisa. Lakini ingekuwa kwa amri yake
angezuia hili jambo kwa mume wake pekee, kwa
wengine angeliacha kama lilivyo.
"Huyu ni nani Juma?" Aliuliza kwa shari kiasi.
Juma akashindwa kujibu.
"Wewe ni nani mama, na nini kinatokea hapa?"
Akamgeukia yule mwanamke mpenda shari.
"Naitwa Dokta Kobo, ninamdai mumeo. Naomba
anipatie pesa zangu nijiondokee hapa." Alijibu
kwa kirefu.
Juma Kihwele akafanya kosa kubwa kupinga
kuwa hadaiwi kitu chochote na yule mwanamke.
Dokta Kobo hasira zikamjaa, akamkwida vyema
zaidi Juma. Na hapa sasa ukazuka ugomvi,
mlinzi akasogea eneo la tukio kwa ajili ya
kumsaidia bosi wake.
Kuona kuwa wanaompinga wamekuwa wengi,
Dokta Kobo akaingiza mkono katika pochi yake
kubwa kiasi. Akarudi nyuma na hapo akatoa
bunduki.
Wacha wee!
Wivu ukasahaulika, ubabe wa mlinzi nao ukaenda
likizo huku rungu lake likimtoka mkononi, Juma
akakaza mwendo wakamfuatia wenzake
wakitimua mbio. Huyu akiita mama yule anaita
Mungu wangu na mwingine haongei.
Mbio!
Dokta Kobo akamtazama vyema Juma
Kimbelembele anavyokimbia kwa uoga huku
akipiga mayowe, ndani ya sekunde chache
akayahesabu maovu yote kutoka kwa bwana
huyu na hapo akaufikia uamuzi wa kumuhukumu.
Akaielekeza silaha yake kule alipokuwa Juma
Kimbelembele, kisha akaanguka chini na kutua
kwa kutumia goti moja, akamweka Juma katika
shabaha. Vilevile kama alivyowahi kufundishwa
na mume wake ambaye ni ana cheo cha inspekta
katika jeshi la polisi.
"Kafie mbele mwanaharamu mkubwa wewe..."
Likamtoka neno lile na kisha akakifikia kitufe cha
kufyatulia.
Mlio mkubwa ukasikika!
_______
GIZA lilikuwa limetanda wakati fahamu zikirejea
kinyonge katika mwili wa dokta Kobo. Alijihisi
maumivu kwa mbali lakini alipojipapasa hakuwa
na jeraha.
Akatulia kwa muda kisha akakumbuka kwa juhudi
zote ni wapi alitoka hadi kulifikia giza lile.
Kama kawaida yake hakuwa mwenye papara, hili
ni moja kati ya jambo lililopelekea inspekta Kobo
kumtolea mahari upesi na kumuoa moja kwa
moja.
Akazikusanya fikra zote na tabasamu hafifu
likamtoka.
"Nimetekwa!" alijisemea huku akijiandaa
kukabiliana na huo ukweli.
Akaukumbuka mlio mkali wa risasi uliopelekea
ashindwe kukivuta kitufe cha kufyatulia na
kumwondoa duniani Juma Kihwele.
Kwa maksudi akaanza kukohoa ili wenyeji wake
waweze kujisogeza karibu yake.
Kimya! akabaki kuusikia mwangwi wa kikohozi
chake mwenyewe.
Akakohoa tena, bado hali ilikuwa ileile.
Akasitisha zoezi lile akasimama na kuanza
kupapasa gizani akijaribu kutafuta mwanga wa
kutoka katika eneo lile ikiwa ni kweli hajatekwa.
Aliendelea kupapasa bila kukutana na kitu
chochote kile.
Akajipapasa na kukuta amepungukiwa bunduki
pamoja na mkoba wake. Akatambua wazi kuwa
alikuwa amepekuliwa. Hakuwa na hofu kubwa.
Hiyo ilikuwa ni asili yake. Katika kazi yake ya
udaktari alishuhudia wagonjwa wengi wakipoteza
maisha, wengine mikononi mwake wengine katika
mikono ya madaktari wengine.
Hivyo hakuwa akikihofia sana kifo. Alijua ipo siku
atakufa...
Na sasa alijiona katika mdomo wa kifo.
Aliendelea kutembea zaidi akipapasa huku na
kule.
"Ni akina nani hawa? na wanataka nini?" Alijiuliza
huku akiendeleza bidii katika kupapasa.
"Mamaaaaaa!" kelele kubwa zilisikika ghafla
mbele yake na hapo akasikia vishindo vikiambaa
kwa kasi.
Mungu wee! nini hiki? alijiuliza huku kwa mara ya
kwanza akianza kupatwa na wasiwasi moyoni.
Akatulia tuli katika giza lile akisubiri kitakachojiri.
Hakuna aliyesogea, akasikia gari likiwashwa na
kisha akauona mwanga kwa mara ya kwanza.
Mwanga ulipenya katika mboni ya macho yake
katika namna ya kumsumbua.
"Tulia hapohapo mwanga mkubwa wewe!" sauti
ikamuamrisha. Akatulia tuli huku akikumbuka
nidhamu ya kunyoosha mikono yake juu.
Hatua zilizizidi kusogea hadi alipokuwa.
"Toa hicho kitambaa" Akaamrishwa.
Akaanza kujitazama.
"Toa kitambaa usoni!!" sauti ikaamrisha tena.
Ni hapa ambapo akili ya daktari Kobo ilifanya
kazi.
Wakati wote aliokuwa akipapasa katika kiza
kinene alikuwa na kitambaa usoni.
Ajabu!
Akajipapasa na kukifungua kile kitambaa. Ndio
palikuwa na giza lakini sio kiza totoro kama
alichokuwa akitembea kwa kupapasa.
Taa za gari zilikuwa zinammulika, akaendelea
kunyanyua mikono yake juu hadi alipofika
mwanaume mmoja akiwa na mkuki na rungu.
"Wewe ni nani usiku huu hapa na umefika vipi
hapa. Tiketi yako ipo wapi? na kwanini haujatoka
ndani hadi wakati huu..." Maswali debe
yalitiririka.
"Sijui kitu chochote jamani." alijibu kwa shida,
koo lake lilikuwa limekauka.
"Unajua hapa ni wapi?"
"Sijui lolote, sijui hata nilipotoka mpaka kufika
hapa." aliendelea kusisitiza.
Taa zikazimwa! sasa aliweza kuwaona watu
wawili zaidi, wote wanawake na kwa mbali
akauona ufukwe.
Alikuwa jirani kabisa na bahari.
Kuhusu ni kitu gani kimetokea hakujua pa
kuanzia lakini bado alihisi kuwa hajapaa hadi
kufika katika ufukwe ule asioufahamu.
"Nipo wapi hapa jamani?" aliuliza ili apate
mwanga.
Kabla jibu halijatoka, vikasikika vishindo na miale
ikaanza kuonekana kuanzia mbali. Wote
wakageuka nyuma kutazama kinachojiri.
"Kuna hatari hapa ndugu zangu. Ikiwa vyema
tuondoke hapa" Yule bwana aliyefanania na
mlinzi alitoa shauri.
Na hapo wale wanawake wawili wakaingia garini,
kisha akafuata mlinzi na katukatu wakagoma
kumbeba Dokta Kobo hata alipowasihi zaidi kuwa
huenda alikuwa ametekwa.
Gari ikaanza kuondoka taratibu ikipambana na
ule mchanga mwingi wa ufukoni mwa bahari.
Tulivu haikudumu, risasi zikaanza kufyatuliwa
kuelekea lilipokuwa gari.
Dokta Kobo, akakimbia kwa kasi sana kuelkea
yalipokuwa maji.
Shukrani za dhati zilikuwa kwa tabia yake ya
kupenda kufanya mazoezi ya viungo kila siku.
Aliyafikia maji na kujirusha upesi ndani yake.
Risasi ziliendelea kurindima huku gari lile ambalo
sasa tairi moja lilikuwa limepasuliwa tayari
likipambana kujinasua kutoka katika eneo lile.
Akiwa ndani ya maji dokta Kobo aliliona balaa
jingine likimnyemelea, aliiona mbwa yenye afya
ikijongea kule alipokuwa yeye huku ikibweka
sana.
Mbwa ilizama majini, sasa haikuwa ikibwrka tena
lakini ilikuwa na usongo wa hali ya juu.
"Come on lazy dog!!" alijisemea huku akijaribu
kufanya hichoalichopanga kufanya.
Akaendelea kuyakata maji huku kila mara
akikumbuka kuiita ile mbwa.
Alijua hawezi kuendelea kuogelea tu bila
kupambana. Na alichokipanga wakati wake
ukafika.
Mbwa ikamrukia na kumrarua na makucha yake.
Dokta Kobo akaukumbuka utoto wake
akaujumlisha na ujana wake jinsi alivyokuwa
fundi katika kukata maji. Wakati akiwa
mwanafunzi wa shule ya msingi alikuwa
akiwazidi hadi wanafunzi wa kiume katika kukata
maji.
Sasa yu katika maji kwa sababu maalumu sio
mashindano ya kawaida ya mshindi kutunukiwa
cheti, katika hili mshindi angetunukiwa uhai.
Dokta Kobo anayeyajua maji akavuta pumzi na
kutoa nje mara kadhaa kisha akajigeuza na
kumweka mbwa chini yake kisha wote
wakazama.
Kilichofuata yalikuwa mashindano ya nani
awezaye kuzitunza pumzi zake kwa muda mrefu
awapo ndani ya maji.
Ni mbwa ama ni dokta Kobo.
Mbwa alisahau kuwa alikuja pale kwa lengo la
kushambulia, sasa alikuwa anahaha huku
akinywa maji mfululizo bila mpangilio.
Dokta Kobo alikuwa makini katika kuzitunza
pumzi zake na wakati huo alimdhibiti yule mbwa
asiweze kupanda juu kuvuta hewa.
Sekunde zake za uvumilivu zilipofikia ukomo.
Akaiunganisha mikono yake miwili katika shingo
ya yule mbwa kisha akairuhusu ile mbwa
ifurukute.
Ikafurukuta na kumleta juu, akavuta pumzi za
kutosha. Mbwa asiye na akili kama za Dokta
Kobo akabaki kuhema hovyo.
Dokta Kobo akazama tena ndani ya maji, na hii
ikawa safari ya mwisho.
Alipoibuka alikuwa hai peke yake, mbwa iligeuka
mzoga wa ajabu unaoelea ndani ya maji kwa
mara ya mwisho.
Dokta Kobo katika kichwa chake mpambano wa
uhai ulikuwa haujamalizika nd'o kwanza ulikuwa
unaanza.
Aliwaza na kuwazua akaukumbuka ule usemi wa
wanamtaa usemao mume/mke si ndugu yako.
Akajaribu kuuhalalisha usemi ule katika hili
linaloendelea.
"Ina maana Kobo mume wangu amemuua Nguzu
na sasa anataka kuniua mimi kwa sababu
nimejua ama?" alijiuliza huku akiendelea kuyakata
maji kwa makini kabisa kujiweka mbali na hatari.
Akayakumbuka mema yote waliyoyapitia katika
ujana wao, na sasa katika utu uzima huu
yasahaulike?? Alijiuliza na kuingiwa na ukakasi
mkubwa sana katika kuupata usahihi.
Zubeda!
Jina hili likamshambulia ghafla, akahisi wawili
hawa lao ni moja. Wamekolezana kimahaba
wamemuua Nguzu na sasa hawataki usumbufu
wowote ule wanataka uhuru wameamua
kumtokomeza.
"Koboko mume wangu? Hapana.... hawezi
kunifanyia hivi mimi." Alijiuliza na kujipatia jibu
japokuwa hakutaka jibu lile limuathiri na kuwa
jibu la uhakika.
Baada ya kukatab maji kwa juhudi zote na
kuamini kuwa yu mbali na ile shari. Alienda hadi
ufukweni akajinyoosha na kuvuta pumzi za
kutosha.
Hakujua ilikuwa ni saa ngapi na mbaya zaidi
hakujua maadui wake walikuwa upande gani kwa
wakati ule.
Subira! ndo kitu pekee kilichohitajika kwa wakati
ule pale alipokuwa.
Akaendelea kutulia mtaalamu yule wa magonjwa
ya moyo.
Dakika takribani arobaini zilitimu bila purukushani
yoyote, lakini hapakuwa tulivu zaidi.
Miale ikaanza kuonekana, akiwa ametuliapalepale
akajigeuza upande wake wa kushoto na kuona
kundi la watu wakirandaranda huku wakimulika
maeneo mbalimbali.
Daktari Kobo akajipima nguvu katika mwili wake,
asingeweza kukimbia walau mita mia mbili bila
kuanguka.
Maji yalikuwa yamemdhaifisha sana.
Mapigo yake ya moyo yakaongeza kasi na
kujiona kuwa ule ulikuwa mwisho wa ujanja wake
katika hili tukio.
Akayafumba macho yake na kutazama angani.
Akajilazimisha kutabasamu lakini haikuwezekana.
Hofu ya kifo ilikuwa jirani yake.
# Naam ! Kuna nini kinafichwa katika sakata hili,
je ni mapenzi pekee ama kuna kubwa limejificha?
-Nguzu amezua balaa Mwanza, huku Dar
hakukaliki.
-Zubeda hajarejea mchezoni, MAJENGA naye
anangojewa katika sakata......
 
SEHEMU YA KUMI NA MOJA
Miale ikaanza kuonekana, akiwa ametuliapalepale
akajigeuza upande wake wa kushoto na kuona
kundi la watu wakirandaranda huku wakimulika
maeneo mbalimbali.
Daktari Kobo akajipima nguvu katika mwili wake,
asingeweza kukimbia walau mita mia mbili bila
kuanguka.
Maji yalikuwa yamemdhaifisha sana.
Mapigo yake ya moyo yakaongeza kasi na
kujiona kuwa ule ulikuwa mwisho wa ujanja wake
katika hili tukio.
Akayafumba macho yake na kutazama angani.
Akajilazimisha kutabasamu lakini haikuwezekana.
Hofu ya kifo ilikuwa jirani yake.
_______
UMATI mkubwa wa watu ulikuwa unasukumana
kutazama tukio lile la kustaajabisha.
Huyu alisema hivi yule naye akapinga na kusema
vile.
Baadaye majira ya saa nne asubuhi umati
ulitawanyishwa baada ya askari kufika eneo lile
na kuwasihi wasogee mbali.
Wakiwa wametangulizana na wataalamu wa afya,
polisi waliwaacha wataalamu wale wawapatie
majibu ikiwa mwili uliolala pale chini ulikuwa hai
ama tayari kwa kuzikwa.
Ule ubishani uliokuwa kwa raia juu ya mwili ule
ukahamia kwa maaskari watatu, na wao
wakaanza kubishana chini chini juu ya mwili ule.
Askari mmoja alisimamia upande mmoja na
wawili wakiunganisha nguvu kutetea hoja yao.
"Yupo hai lakini moyo wake unapiga kwa tabu
sana." Mtaalamu wa afya alitoa majibu, askari
wakafuata taratibu zote na kuuingiza mwili katika
gari ya wagonjwa huku wakikumbuka kupiga
picha eneo lote ambalo waliukuta mwili ule.
Waliondoka pale na kuucha ubishani ukiendelea,
na wale askari nao waliendelea kubishana lakini
hii ya sasa ilikuwa katika namna ya utani tu.
Gari likaingia barabarani huku likipiga ving'ora.
Kutoka Kariakoo sokoni hadi Muhimbili sio
kitambo kirefu sana hasahasa kwa gari hili
ambalo linapishwa njia na magari mengine.
Hivyo hata msafara huu haukuchukua kitambo
kirefu kuifikia hospitali.
Mwili ukashushwa huku ukipokelewa na wauguzi.
Askari wakiwa bado na wawakilishi wao katika
hili.
Hapa sasa hapakuwa na kufananisha tena,
ulikuwa ni mwili ulioibeba sura iliyokuwa
ikifahamika vyema katika hospitali ile ya taifa.
Sura ya dokta Kobo!
Jina ambalo umaarufu wake sasa ulikuwa
umezidi tangu apotee kazini pasi na taarifa
yoyote ile, kupotea huku kukakifanya kitengo
kinachohusika na masuala ya moyo kupwaya
sana.
Dokta Kobo alikuwa mtaalamu sana, lakini
ucheshi wake na moyo wa upendo vilimfanya
kuacha pengo alipokosekana.
Sasa anarejea akiwa katika machela, hana
fahamu na hajulikani kama atapona.
Wauguzi na madaktari walilia huku
wakimwombea dua aweze kupona.
Kutokea hospitali ya Muhimbili, simu ikapigwa
kwa mume wa dokta Kobo yaani Inspekta Kobo.
SIMU hii ilifika katika wakati mbaya sana.
Inspekta Kobo alikuwa amechanganyikiwa mno.
Walinzi wa siri aliowaweka kumwangalia mkewe
na nyendo zake walikuwa wamemueleza kuwa
dokta alikuwa ameshindia siku nzima ndani ya
chumba cha hoteli aliyofikia, walipojaribu
kupeleleza chumba kile wanatanabai kuwa dokta
Kobo alipitia mlango wa dharula kutoweka ndani
ya chumba kile hivyo hawakujua ni wapi
ameelekea.
Jitihada za kumsaka zikagonga mwamba.
Asubuhi akiwa bado hajajua nini hatma ya mke
wake kipenzi anapokea ujumbe wa kitisho.
"MKEO AMETAPIKA KILA KITU." Ujumbe huu
ulimaanisha kuwa mkewe amesema kila kitu.
Kuhusu hili hakushtuka sana kwa sababu alikuwa
akimuamini sana mkewe jinsi alivyokuwa jasiri
pengine kuwazidi wanaume wengi tu.
Hofu yake ilikuwa usalama wa mkewe ambaye
kufikia hapo alijua kuwa alikuwa ametekwa
tayari.
Mawazo yake yalizunguka huku na kule na
kumlazimisha kuwa watu hao wamemuua mke
wake.
"Kama mmemuua mke wangu, mtaijua gharama
halisi ya mguu wangu uliopotea kwa sababu ya
kupambana..." Akamalizia na tusi lake la
kiitaliano. Lakini kwa mara ya kwanza akajikuta
akilitoa tusi hilo kinyonge sana.
Inspekta Kobo akagundua kuwa alikuwa yu na
uoga wa ajabu mno, uoga ambao hajawahi kuwa
nao hapo kabla.
Ni hapa alipokiri kuwa yumkini damu nzito kuliko
maji lakini penzi ni zito kuliko vyote, maji na
damu ukivichanganya pamoja.
Inspekta akakiri kuwa katika mapambano ya
zamani hakuwa muoga kwa sababu aliingia
katika mapigano huku katikati ya uwanja wa
mapambano pakiwa hakuna ndugu yake wala
mtu anayempenda, hivyo hata akifa mtu kwake
haikuwa tatizo.
Sasa anawatukana watu walioshika hatamu ya
maisha ya mkewe kipenzi.
Inspekta akatubu kimyakimya.
Wakati anakiri kuwa anawaogopa watekaji, simu
yake ikaita.
Nambari ilikuwa ngeni, akajua wazi kuwa huyo
atakuwa ni mtekaji na sasa anataka kutoa
masharti ili mkewe apatikane huku akiwa hai ama
akaidi na kupokea kichwa cha mkewe kikiwa
kimelowa damu mbichi na ujumbe wa kukera
'tengeneza supu unywe kama kweli ulikuwa
unampenda'
Inspekta akaipokea simu ile kwa upole kabisa.
"Inspekta Kobo!" sauti kutoka upande wa pili
ikamuita. Akaitikia 'rabeka'
"Samahani kwa usumbufu mkuu, lakini mimi ni
daktari hapa Muhimbili. Sijui kama una taarifa
zozote kuhusu mke wako. Daktari Anna Kobo."
Sijakuelewa taarifa kuhusu nini?" aliuliza kwa
upole vilevile huku akiketi chini.
"Yupo hospitali hapa, naona amepatwa na hitilafu
kidogo ila kila kitu kipo sawa. Itafaa ukifika
huku." Taarifa iliishia pale.
Inspekta alitamani kuuliza maswali mengi lakini
hakuna hata moja lililotoka hadi simu inakatika.
Jasho lilikuwa limeulowanisha mgongo, uso,
kwapa na kifua.
Inspekta alikuwa ameoga jasho huku amekaa tu
bila kukimbia.
Jasho lile likamfadhaisha mno, aakaanza
kujipepea na gazeti lililokuwa mbele yake.
Bado halin hii ilimbughudhi, akajikaza kikakamavu
na kusimama akaukaza mwili wake kisha
akajikumbusha kanuni za kijasiri za jeshini.
Alipomaliza akabiga saluti, kisha akajiwekea
kiapo kuwa hatatumia tena muda mwingi
kutetemeka, kutokwa jasho na kunung'unika
badala yake atautumia muda mwingi kutafuta
majibu ya maswali yanayokielemea kichwa
chake.
Akaipapasa bastola yake na kisha akasemanayo.
Kana kwamba inamsikia.
"Unaonaje kama nikizitoa hizi risasi kwenye
chemba kisha ziwe eneo husika tayari tayari kwa
kupasua kichwa cha mtu atakayethubutu
kunishambulia. Maana si unajua hawa wapinzani
wangu wananijua nami siwajui..... sema nawe
unazingua ungekuwa na macho tungesaidiana.
MI naangalia kulia we kushoto...." Alizungumza
huku akiziweka risasi katika njia yake. Watoto
waliozoea kutazama picha za mapigano
wanasema 'akaukoji mjegeja wake'.
Safari ya kuelekea hospitali kupokea taarifa
mbaya kabisa kuwa mkewe alikuwa hai lakini
alikuwa amezikosa fahamu zake. Kwa lugha ya
kigeni 'alikuwa katika coma'.
Ni heri angekuwa amepoteza fahamu, dokta Kobo
hakuwa kabisa na fahamu zake.
Na haikujulikana zitarejea lini.
Inspekta alichoka!
Alijikaza chozi lisimtoke, hakuweza.
Yalibubujika kama mtoto mdogo.
Akatoweka hospitali na kwenda kumalizia kilio
chake katika kitanda alicholala Zubeda kule
kwenye eneo la siri aliloamua kumuhifadhi.
Kwa wakati huo hakujali jambo jingine zaidi ya
watu wake wa karibu wanaoingia matatani kwa
sababu yake.
Hasira zake akazihamishia kwa Juma Kihwele.
Kumbukumbu za jina lile zikasababisha sharubu
zake kusisimka. Akaendelea kuhisi kuwa huyu
bwana ndiye aliyeandika zile habari, na kama
aliziandika basi kuna mawili. Anasakwa na
waliompa tenda hiyo chafu ili wammalize asije
kutoa siri, ama la yupo mikononi mwa watu
wabaya tayari kwa kuuwawa.
"Zuu, hivi bi mkubwa hakukueleza ni nani
aliyempa maneno yale mazito?" Inspekta
alimuuliza koplo Zubeda kwa upole kabisa.
"Hapana hakutaja jina lolote wala hakuelekea
kufanya hivyo. Alikuwa anajua anachokifanya
wakati anazungumza na mimi." Alijibu kwa kirefu
huku akiwa ameketi.
Hali yake kiafya ilikuwa inaridhisha.
"Vipi kuna kitu kipya unahisi?" Zubeda akajazia
swali.
Kimya kikatanda kabla inspekta hajaelezea hisia
zake juu ya mwandishi wa habari aitwaye Juma
Kihwele. Ili kuusadikisha ukweli akazimwaga
hadharani sifa za kimbelembele alizonazo
muhariri huyo.
Sifa zile zikamfanya Zubeda amuunge mkono
inspekta katika hisia zake zile.
"Nilimsikia daktari akizungumzia juu ya risasi
kushambulia nyumba ya Kihwele, usiku uliopita
nadhani."
"Risasi? nani na nani walikuwa wanarusha?" Swali
la kipuuzi likamponyoka. Akawa mnyonge
alipogundua kuwa ameuliza kipuuzi.
Hakurekebisha!
Akatwaa simu yake na kupiga kwa rafiki yake wa
kitengo cha mawasiliano.
Akamuuliza nini kimejiri.
Taarifa zikatoka kuwa inasadikika kuwa familia
ya Juma Kihwele yaani mke na mtoto pamoja na
ndugu mmoja ilikuwa imepotea.
Nguo zilizotapakaa damu zimeonekana na
hazijulikani kama ni majeraha ama zinamaanisha
vibaya kwa wahanga.
Hadi wakati huo hakuna anayehusishwa na tukio
hilo moja kwa moja.
Taarifa ile iliyakaanga maini ya inspekta Kobo,
uzuri sauti ilikuwa yasikika vyema hivyo hata
Zubeda alisikia kila kitu.
"Zuu mpenzi wangu, huu mkasa utanizeesha
upya. Nilijidanganya mkasa huu utanichangamsha
na kuwa kijana..... ajabu nazeeka tena kwa kasi
mno. Sijui kuwaza vizuri, sijui kujikaza, yaani
nimekuwa kama fala hivi aliyevuta sigara bwege
halafu hana uhakika wa chakula cha mchana
wala usiku.
Badala ya kulia kiume nalia kama mwanamke.
Looh! mkasa huu unanibadili hadi jinsia mimi
inspekta Kobo." Alilalama kwa uchungu mno
huku akijitahidi chozi lisimdondoke.
Zubeda akafanya kosa kumbembeleza, Inspekta
akaanza kulia kama mtoto.
"Wameanza na wewe wamekusababishia ajali,
wamemzimisha mke wangu huko, na bado
wanaendelea kuniumiza kichwa.....aah! Si
wanikamate na waseme nini wanataka eeh!
Kwani mimi ni mwanadamu wa kwanza kumsaliti
mke wangu eeh! Mimi ni wa kwanza nauliza,
mbona wameniandama hivi mimi lakini."
Kwa kilio hiki Zubeda alikiri kuwa inspekta
alikuwa amekamatwa pabaya.
Wakati kilio hiki kikiendelea simu yake ya
mkononi ikatoa mwanga.
"Angalia ni nani anapiga, kama ni namba mpya
naomba usipokee. Sitaki kufia humu ndani,
waniache nikafie ndani ya nyumba yangu."
Alizungumza kwa hisia za malalamiko.
"Anapiga Komredi Kitengo." Zubeda akamtajia
jina linaloonekana pale.
Inspekta akaipokea simu huku akiilazimisha sauti
yake iwe ya kawaida tena.
"Halafu komredi, si uliniambia kuwa unapenda
sana samaki aina ya Sato na Sangara wa
Mwanza?" Mpigaji aliuliza lile swali.
Inspekta mdomo ukamfunguka asiamini aliyepiga
simu ile alikusudia kumsumbua kwa swali la
kizembe namna ile.
Zubeda yeye alijikuta anatabasamu.
"Mbona kimya komredi ama pweza wa jiji
washakuvuruga hutaki tena sato." aliendelea.
"Komredi... najisikia usingizi mkuu. Niache
nilale..." alijitahidi sana kulinda heshima iliyopo
kati yao.
"Hivi Sato hata Shinyanga wapo au ni Mwanza
tu?" Mpiga simu hakujali zile busara.
Inspekta akatamani kulitoa lile tusi lake la akiba
lililo katika lugha ya kiitaliano lakini huyu mpiga
simu licha ya kuwa na utani waliheshimiana
sana.
Akabaki kujichekesha tu..
"Haya jiandae kwenda kula sato, hakikisha
unaniletea walau mapande matatu yaliyokaushwa
na mimi nijue utamu wa sato wa Mwanza."
"Una maana gani komredi?" Akauliza inspekta.
"Ndani ya siku mbili hadi tatu mtapelekwa
Shinyanga nyie mnaojifanya mnajua sana
kutumia bunduki na kulenga shabaha. Kuna kazi
inawaita huko, nimekuibia siri tu ili usije ukasema
sikukuagiza mapema sato." Alizungumza kwa
utulivu kwa kuamini taarifa ile itakuwa njema
kwa inspekta Kobo ambaye alikuwa mpenzi wa
mapambano enzi zake.
"Komredi lakini mimi nimezeeka tayari na
nimevunjika mguu mnajua... mbona.." Akataka
kuendelea kulaumu akasita kwa kugundua kuwa
analalamika sehemu isiyokuwa sahihi hata
chembe.
"Sio wewe pekee kuna wenzako pia wamestaafu
lakini umaridadi wao katika mapambano
unawarudisha kazini."
Mazungumzo yalimalizika na kumwacha inspekta
akiwa katika mtihani mwingine mzito.
Mkewe yu katika 'coma' hawara yake anajiuguza
bado na sasa anatakiwa kwenda Shinyanga kwa
oparesheni maalumu.
Oparesheni asiyoijua. Na alimtambua vyema
mkuu wake akisema amesema. Ukimjibu kuwa
una mgonjwa anakuomba vyeti vyako ulivyofuzu
mafunzo ya udaktari hadi ubaki kumtibu
mgonjwa, ukisema unaumwa anakuambatanishia
daktari katika msafara wa kwenda katika tukio.
Kwa kifupi hapakuwa na sababu ya kukwepa
majukumu akiyatoa.
Na kingine kibaya ni uhasama uliokuwepo baina
yake na kiongozi wake wa juu.
IGP!
Uhasama usiokuwa na historia maalumu. Ila
uliendelea kuwepo.
Njia pekee ya kukwepa majukumu kiutoka kwa
IGP ilikuwa ni kujiua.
Alikuwa hakwepeki!
Inspekta Kobo alichoka sana. Ndani ya masaa
machache akausikia waziwazi udhaifu uliouchota
mwili wake.
Alipoupeleka mguu wake ofisini akakumbana na
barua aliyoitarajia.
Wito!
_______
# Naam ! Inspekta Kobo katika mitihani migumu
iso'kifani.
BADO hauoni mwanga..........
 
SEHEMU YA KUMI NA MBILI.
GIZA lilikuwa ndani ya giza kwa mara nyingine,
Konstebo Martin Nguzu alikuwa amempokea
mama yake ambaye alikuwa mmoja kati ya
wahanga wa ile kamatakamata iliyofanywa kwa
masilahi ya watu wachache waliokuwa
wamekerwa baada ya mwenzao mmoja kuuwawa
kifedhuli.
Ghafla bin vuu mambo yakabadilika, kota
zikatishiwa kuchomwa. Wakagwaya na kuwaachia
huru wale waliokuwa wamekamatwa katika
namna ya uonevu.
Ni giza hilihili sasa lipo ndani ya giza tena, ana
kwa ana na mama yake mzazi.
Martin Nguzu alimpa pole mama yake huku akiwa
na haraka sana ya kujua ni wapi hasa anapoweza
kumpata Majenga waweze kuzungumza na
kutambua ama kujitambua upya yeye ni nani na
kwa nini haya yote yanatokea.
Hasira zake bado zilikuwa dhidi ya inspekta Kobo
aliyeamini kuwa alimchomea ndani ya nyumba
kisa mapenzi.
Alipona vipi na nini kinaendelea katika maisha
yake haya nd'o makuu aliyojiuliza.
Kuhusu kutafutwa kwa Majenga na watu
asiowajua kukapunguza ile hisi yake kuwa
chanzo cha kiila kitu ni mapenzi.
Akabaini kuwa lipo la nyongeza.
Mama Martin ambaye hakuwa ameimarika sana
kiafya safari hii alionyesha ushirikiano wa hali ya
juu, usiku uleule alimpeleka Martin hadi nyumba
aliyowahi kuishi mzee Majenga ambapo baadaye
alipangisha na kuondoka zake kuelekea
Shinyanga.
"Ila Shinyanga sijamuona kabisa..." Nguzu
alizungumza wakati wanaelekea katika nyumba
ile.
"Bado haujabadilika mwanangu, yaani Shinyanga
kubwa vile wewe umtafute mtu usiyemjua na
ukampata kabisa. Labda muujiza ama maigizo."
Mama alimkata juu kwa juu Nguzu, haikuwa mara
ya kwanza hali ile. Tangu utoto wake.
Mtoto hakui kwa mama!
Walipewa ushirikiano mkubwa sana walipowasili
eneo lile, uzuri mtoto wa mzee Majenga alikuwa
anaishi katika chumba kimojawapo, na alikuwa
pale kama msimamizi wa nyumba ile.
"Kumpata kwa leo itakuwa ngumu sana, maana
leo watu wametoa kodi. Na yule akipata kodi
anamalizia katika ulevi wake.” Mtu aliyekuwa
anawapa maelekezo alisema kwa masikitiko.
“Unaweza kujua baa ambazo hupenda
kuzitembelea?” Nguzu aliuliza kwa udadisi.
“Bora angekuwa anaenda baa, huyu anaingia
vilabuni, ana usemi wake unaosema kwamba mia
mbili ya baa ni elfu kumi ya kilabuni”
Martin akajikuta anatokwa na tabasamu hafifu
kwa kusikia haya.
Ghafla wakamwona yule mwenyeji akiwafanyia
ishara ya kusikiliza kwa makini zaidi, wakasikia
sauti ya mtu akiimba.
“Ni yeye... looh! leo amewahi kurudi hivi?”
alishangaa na kuwashawishi Nguzu na mama
yake washangae pia.
“Halafu..... halafu..... mama huyu kamfanana....
aahm! eeeh!” akaanza kujiuma uma. Alikuwa
amemtazama Nguzu vizuri.
“Ninafanana naye sana alikuwa binamu yangu....”
Nguzu akaiwahi hii kesi na kuisawazisha.
Mtarajiwa akawasili akiwa anaendelea kuimba
nyimbo zake, nyimbo zilizomburudisha yeye
pekee.
Hakuwa peke yake.....
Alikuwa na chupa kadhaa za pombe.
“Mnataka kuhama.... mnahama hama na
hamjalipa kodi yangu.” Alizungumza huku akiwa
hana hata uwezo wa kuona mbele vizuri,
sembuse kung’amua kuwa kuna mtu anataka
kuhama.
Akasogea kwa kunesanesa bila kuvunja chupa
hata moja akawafikia.
“Shkamoo mama..... eeeh! mama nawe
umehadimika kweli.” Alisalimia baada ya
kumtambua mama Martin.
Salamu ilijibiwa, yule mwenyeji akajitoa katika
mkutano huu akawaacha watatu hawa
wakizungumza.
Walijitahidi hivyohivyo kuelewana japokuwa
ilikuwa ngumu kwani yule mlevi kila mara alikuwa
anasahau alichozungumza dakika kumi nyuma.
Mlevi huyu hakujua ni kiasi gani alikuwa faida
kwa Martin Nguzu.
______
ASKARI aliyetegemewa na kuaminiwa zaidi
alikuwa makini na silaha yake, alikuwa
amejinyoosha chini na kunyanyuka kidogo sana
usawa wa kifua na kuendelea. Bunduki yake
kubwa ilikuwa imelazwa vyema katika muinuko
huku akiona kila kitu kilichokuwa kikikatiza mbele
yake.
Alitulia katika lindo lile kwa dakika nyingi
akingoja walilotarajia litokee waimalize vyema
siku yao.
Kilikuwa ni kikosi cha watu saba tu cha siri
kilichokuwa kikitambua nini kinaendelea katika
giza hili.
Majira ya saa nane usiku mchakacho ulisikika
kutoka katika kichaka kimojawapo, mlengaji
akatulia tuli bila kufanya shambulizi.
Alihitaji kupata uhakika wa kile alichokuwa
anakwenda kukishambulia.
Barua kutoka kwa IGP ilielezea kuwa jambazi
aliyekuwa anasakwa miaka mingi alikuwa mjini
Shinyanga na huko alitarajia kuanzisha kampeni
ya kuvamia na kuiba katika taasisi mbalimbali za
kifedha.
Huu ukawa wakati wa askari kujitafutia nyongeza
ya nyota kwa kumtia mikononi jangili huyo
aliyekuwa anasifika kwa hatari yake na roho
mbaya.
Simu ya upepo ilikuwa imeshikiliwa na askari
mwingine, kazi yake ilikuwa moja tu kumweleza
mlengaji nini cha kufanya ikiwa patakuwa na
mabadiliko. Mlengaji hakupaswa kutikisika ama
kujihusisha na mawasiliano mengine kwa sababu
angeweza kuipoteza shabaha yake.
Mchakacho ule ukaongezeka tena, mlengaji
akaendelea kutulia.
Na hapo redio ya upepo ikakoroma ikitoa taarifa
kutoka upande wa pili.
“ANGUSHA MBUYU KUNA NYOKA! ANGUSHA
HUO MBUYU...”
Sauti ile ikamfikia mlengaji, akaanza kutetemeka
mikono nyake. Ile sauti haikuwa ngeni na lile
neno hakuwa akilisikia kwa mara ya kwanza. Ni
siku kadhaa nyuma alilisikia katika simu ya upepo
kutoka kwa kijana wake wa kazi aliyeuwawa kwa
kupigwa risasi.
Mikono ikazidi kutetemeka, sauti ile nayo ikazidi
kusisitiza neno lilelile.
‘angusha mbuyu’
Mapigo ya moyo yakaongezeka kasi yake.
Adui akajitokeza kutoka katika kichaka, mlengaji
akatakiwa kufyatua na kumwangusha adui.
“Afande Kobo, fyatua!!” mshika simu
alimwamrisha Kobo aliyekuwa aanatetemeka na
silaha yake.
Inspekta Kobo akaachia risasi ya kwanza,
ikaenda malikiti.
Haikumkaribia adui badala yake ilimpa taarifa
kuwa kuna hatari inawazunguka.
Kobo akamuona adui akirudi mbio kichakani, na
baada ya sekunde chache hakutoka peke yake,
lilikuwa jopo la maana lenye silaha za
maangamizi.
Mpambano ukaanza.
Kobo akajaribu kutupa risasi nyingine, akakosa!
Ile kauli ya angusha mbuyu ilikuwa ikimsumbua
kichwa chake.
Anayeitoa sauti ile ni nani? na kwanini alimuua
kijana wake? na ni kipi kinamfanya amfuatilie
Juma Kihwele kama yeye alivyokuwa
anamfuatilia.
Mlolongo huu wa maswali ukazidi kumpoteza,
kwa mara ya kwanza katika maisha yake
anafyatua risasi tatu na hakuna hata moja
iliyomlenga muhusika.
Kitimtimu kikaanza.
Askari saba ambao umri umewatupa mkono dhidi
ya jopo la vijana majangili kumi na watano.
Risasi ziliruka hewani kwa fujo, huyu anarusha
yule anajibu.
Inspekta Kobo alikuwa kama mpira wa kona,
anakimbia huku na kule angali silaha anayo,
badala ya kumkabili adui yeye anajiuliza ni nani
mwenye ile sauti inayosema ‘angusha mbuyu’
Wasiwasi mara mbili, kwanza dhidi ya hao vijana
majangili na pili juu ya adui ambaye wapo naye
katika mpango huu kamambe.
Nguzu akatamani kumuuliza askari mwenzake
ambaye alikuwa anashikilia simu, amuulize yule
ni naji alitoa ile amri.
Lakini, licha ya kuamini kuwa ule wakati haukuwa
wa kuuliza maswali bali kila mmoja kuutetea uhai
wake. Hata nafasi hiyo pia hakuipata kabla ya
kukiona kichwa cha yule askari kikisambaratish
wa vibaya mno na risasi iliyotoka inapotokea.
Madonge mazito ya damu yakamrukia wakati
akijirusha pembeni zaidi asijekukumbwa na balaa
la kusambaratishwa.
Inspekta Kobo alikuwa anahema juu juu huku
akiomba dua Mungu amtunze asife usikun huo.
Taswira ya mkewe ambaye yu katika kuzimia
ilimvamia. Akahisi kuwa kifo chake kitasababisha
mkewe akirejewa na fahamu zake naye apoteze
maisha kwa mshtuko wa kupoteza mume.
Sasa hofu ya kifo ilimtawala waziwazi......
Akaiweka sawa silaha yake na kujipa maneno ya
ujasiri kupindukia ambayo yangeweza
kumrejeshea ari yake ya upambanaji.
Aliiweka vyema silaha mkononi, ikawa inateleza.
Kwa mara ya kwanza bunduki yake ikawa
inamsaliti. Akairudisha katika bega lake na
kujipapasa kiunoni, akaichukua ile bastola yake
anayoiamini kupindukia akaiweka sawa mkononi,
hii yenyewe ilimuheshimu ikakaa sawa.
“Serenaserena afande Kobo.... Kobo...” Sauti
ikamuita kutokea gizani. Ilianza na utambulisho
wao wa siri waliokuwa wamepeana.
Inspekta Kobo akabonyea chini kisha akatoka
‘mkuku’ hadi alipoisikia sauti ile.
Alimkuta mwenzake akiwa katika dimbwi la damu
akiogelea bila kupenda.
Hali yake ilikuwa mbaya sana, na alionekana
muda si mrefu ataikimbia dunia kuelekea popote
anapoamini kwa imani yake.
“Kimbia, hatari.... viumbe hawa hatari.
Tunateketea wote....” Alizungumza kwa sauti ya
chini sana. Akaweka kituo na kuhema kwa nguvu
zote.
“Hakikisha unaishi ili kuwa shuhuda.... viumbe
hatari sana wana siri zote. Usimuamini mtu
jiamini wewe mwenyewe kuanzia sasa..... kuna
wasaliti kati yetu.” alizidi kusihi.
“Na... naku.. nakuf... nakufa afande.”
Alizungumza huku akizidi kukauka koo lake na
sauti kufifia.
Ikawa kama alivyojitabiria!
Inspekta akazidisha umakini, akabaki na maswali
lukuki, ni kwanini bwana yule anamweleza kuhusu
wasaliti ndani yao, kwanini amemchagua yeye na
amemuamini vipi kuwa yeye sio msaliti?
Mwenzao huyu!! alijisemea huku akiondoka
kutoka eneo lile.
Sasa kila upande ulikuwa umetulia, ilikuwa ni vita
ya kuviziana baina ya pande hizi mbili. Inspekta
hakutaka kumuamini mtu yeyote zaidi.
Alitilia maanani uhai wake pekee.
Akakimbia hadi alipolifikia shimo asilojua
matumizi yake, akatumbukia na kutulia ndani
yake.
Alikuwa macho kabisa kisije kumdhuru chochote
kitu.
Aliendeleakutulia hadi palipokucha akauona
mwanga.
Lakini mwanga huu ulikuwa ukingojewa na watu
wengi.
Ile Inspekta anatoa kichwa chake nje akakutana
na sauti kali zikimkaripia asithubutu kufanya
jambo lolote lile atue silaha zake chini na kisha
kunyanyua mikono yake juu.
Alijitahidi kujitambulisha lakini hakuna ambaye
alimsikiliza.
Akatii, kwa umakini wa hali ya juu askari wenye
sare wakamkaribia na kumtia pingu mikononi na
miguuni.
Ajabu!
Alistaajabu ni kipi kimejiri hadi kujikuta katika
balaa kubwa kiasi kile tena ghafla.
Alionywa asithubutu kusema jambo lolote lile.
Akaingizwa katika gari lenye ulinzi mkali
kupindukia.
Hawakutaka kulala tena Shinyanga.
Amri ikatolewa kuwa iwe isiwe lazima inspekta
Kobo afikishwe jijini Dar es salaam, na hiyo
ilikuwa ni amri na sio ombi.
Inspekta Kobo hakuamini, vijana walio chini yake
ki-cheo walikuwa wanamlinda huku wakimkaripia
mara kwa mara.
Alifedheheka ila hakuwa na la kufanya.
Huu ukawa mwanzo wa safari mbaya na ya
kutisha.
Wakati anaiacha ardhi ya Shinyanga, katika ardhi
hiyohiyo harakati mpya ilianza kusukwa.
 
SEHEMU YA KUMI NA TATU
FLORIAN NGENGEKUZENZA NGUZU.
USHINDANI wa nani kwao matajiri nilishindwa
mapema sana, kila walichokuwanacho sisi
tuliishia kukiona tu. Hatukuwanacho wala
hatukukaribia kukipata.
Miaka ya elfu tisa mia na arobaini (1940), ni wale
watoto ambao baba zao walikuwa wakijipendeza
kwa wakoloni pekee ndo wangeweza kuwa na
maisha yenye unafuu.
Katika hapa sikuwa mshindani wake.
Tulipata nafasi mara chache sana kucheza
michezo ya kitoto, hatukuwa tukishindana sana.
Miaka ikazidi kwenda hatimaye ikafika wakati wa
kwenda shule, huku napo hapakuwa na ule
ushindani wowote. Alisoma katika shule ambazo
walivaa viatu na sare nzuri angali sisi miguu yetu
iliunda urafiki wa kinafiki na miba pamoja na
matope.
Kitu pekee tulichopata katika maisha yetu duni ni
aibu za wazazi wetu pindi waliponyanyaswa na
mkoloni. Kisha baada ya hapo wanatusimulia
simulizi za mashujaa wao ambao na wao
walikuwa wakikiri kuwaogopa hawa watu wenye
ngozi nyeupe.
Simulizi hizo zilinijenga barabara, katika akili
yangu. Nikajikuta ni kijana ambaye uzalendo
ulikuwa katika moyo wangu.
Baba yangu mzazi ambaye alipigana vita ya
Majimaji huko Songea alikuwa akiniongezea
ujasiri, ni kweli alikuwa akinyanyaswa na
wazungu na aliwaogopa kweli lakini alikuwa
akinieleza kuwa katika vita ile kwa mkono wake
wa kuume akiwa na rungu kubwa aliwauawa
wazungu watano.
Kwake ulikuwa ni ushindi mkubwa sana
kumtandika mkoloni na bunduki yake mkononi.
Ni kweli watanganyika wengi walipoteza maisha
lakini hii ilikuwa alama kubwa sana kuwa
waliutaka uhuru kwa namna yoyote.
Baba alinieleza kuwa baba yake ambaye ni babu
yangu alipoteza maisha kwa kunyongwa, na ni
yeye ndiye alikuwa mmiliki wa jina la Nguzu
ambalo maana yake ni NGUVU.
Jina Florian nilipewa na hawa ngozi nyeupe
waliojifanya miungu katika ardhi yetu, silipendi
jina hilo.
Naitwa Ngengekuzenza Nguzu. Yaani ‘Aliyerithi
Nguvu’.
Baba yangu alinipatia jina lile kwa sababu
aliniamini sana, nami nikajikuta najiamini mno.
Maisha magumu hayakuiathiri akili yangu, sijui
mnaitaje kwa kizazi chenu hiki cha Tanzania,
lakini wakati wa Tanganyika tulisema akili
zinachaji, akili zangu zilikuwa zinachaji mno.
Nilifanikiwa kulimaliza darasa la nne la mkoloni.
Wakoloni bwana licha ya unyanyasaji wao lakini
walikuwa makini sana, wakiona mtu ana akili
sana wanamuwahi ili baadaye aje kuwa upande
wao na aseme mazuri tu juu yao. Mkoloni
akupatie elimu utaanzaje kumsema kwa mabaya
angali tayari unaweza kusema’yes no’ kwa
sababu yake!!
Hata mimi waliniwahi na hapa ndipo nilikutana na
Joseph Kazeze.
Na upinzani ukaanza rasmi.
Wakatupeleka shule ya upili ambayo kwa sasa
mnaiita Tabora boys lakini wakati ule iliitwa
Tabora Central school. Ilikuwa shule ya vipaji
maalumu haswa. Wanafunzi wengi walikuwa ni
watoto wa machifu, ni baadaye sana walianza
kuchukua wanafunzi wa kawaida.
Kwa wakati ule nadhani ni mimi na wengine
wachache sana tuliokuwa tunasoma pale lakini si
watoto wa machifu.
Mitihani ya hapa ilikuwa ni kutoka vyuo vya
uingereza. Hawakutufundisha kuhusu yetu bali
walitaka tuyajue yao.
Hata hayo yao bado nilipata alama za juu.
Urafiki kati yangu na Joseph Kazeze ukaanza
kuyeyuka, hakutaka kupitwa alama na mtoto wa
kimasikini kama mimi.
Tulipoenda jeshini mwisho wa kidato cha tatu
kama ilivyokuwa ada nilikuwa bora zaidi yake
katika kila kitu.
Hakupenda kabisa, ila mimi sikujua kama ni kwa
kiasi kikubwa vile.
Tukarejea tena kumalizia kidato.
Katika uchaguzi nikateuliwa kuwania uongozi,
Joseph naye akawania.
NIkamwangusha na kuwa kiongozi wake!
Wakati ananipa mkono wa hongera ndipo niliiona
chuki katika macho yake.
Nikapuuzia.
Nikasema ikiwa wote tunatoka Mwanza, ya nini
kuchukiana sasa. Nikadhani yale yataisha...
Kutingwa na uongozi nikasahau kabisa kuketi na
Joseph tuzungumze.
Chuki ikakomaa!
Baadaye yakaibuka mapenzi, nadhani hapa ndipo
chuki ilibalehe na kuota mapembe!
Joseph alimpenda binti ambaye alikuwa
akinipenda mimi. Kuzidiwa huku kete Joseph
akaleta ubabe na kunivimbishia kifua.
Mara ya kwanza nilimwacha, ya pili akanifuata
tena akinitaka ugomvi, nikamweleza bayana kuwa
sisi ni ndugu wa mji mmoja asiwe vile.
Akanipuuzia na siku hii akanisukuma nikaanguka.
Nilipoinuka nilimfundisha kuhesabu moja mpaka
kumi kwa lugha ya kirusi.
Somo lilikuwa gumu na kila mara alianguka chini,
kila akijaribu kunyanyuka namtandika ngumi ya
uso. Akapasuka juu ya jicho lake, nami nikawa
napiga palepale.
Siku hii nikatambua kuwa majina yana maana
yake.
Ngengekuzenza Nguzu (Aliyerithi Nguvu)
Nilikuwa nimerithi haswa.
Ugomvi huu ulitikisa shule.
Ajabu yake ilikuja katika maamuzi, tulipigana na
mgomvi alikuwa Jose lakini katika adhabu
nikachukuliwa mimi.
Tabora Central School ilikuwa shule ya kijeshi
wakati wetu, hata sare zetu zilikuwa za
kijeshijeshi, tulivalia kombati za kaki kama
wanazovaa wanamgambo, kila kitu kiliendeshwa
kikakamavu, hapakuwa na adhabu za viboko.
Nilivyoadhibiwa nikikusimulia unaweza ukahisi
huyu bwana kachanganyikiwa na sasa
ananidanganya.
Niliingizwa katika chumba chenye giza nene na
hapo nikaanza kulazimishwa kwenda mbele, kadri
ninavyokwenda mbele ninazidi kuinama chini
kutokana na muundo wa kile chumba, hatimaye
paji la uso likayakaribia magoti.
Chumba kikabanwa nikawa siwezi kusogea mbele
wala kurudi nyuma.
Niliumia mno, nikaamini kuwa sasa ninakufa.
Waliniacha kwa masaa mengi sikumbuki hata.
Waliponitoa nilikuwa nyang’anyang’a.
Wakanipelekaq msituni, huko sasa niliadhibiwa na
wazungu. Walimwachia mbwa wao anikimbize na
nilipewa ruhusa ya kukimbia kumzidi.
Nilivyochoka vile ningeweza vipi, si waliutaka
uhai wangu tu wapuuzi wale.
Basi kama ni mchezo basi mbwa alipata wa
kucheza naye, nakimbia hatua kadhaa naanguka
mbwa anafika na kuning'ata wanamfukuza.
Wananiambia nisimame tena ninakimbia
wanamwamuru mbwa anikimbize, ananifikia na
kuniangusha ananing'ata.
Niliteseka mno!
Baada ya hapo nikapokea viboko kumi na viwili
vya mkoloni.
Nilinyooka.
Joseph hakuadhibiwa nilipotoka kule kwenye
adhabu nyinginyingi za kutisha nikaelezwa kuwa
nimefukuzwa shule na wakati huohuo aliyechukua
nafasi yangu katika uongozi ni Joseph Kazeze.
Nililia! Nililia sana.
Nikapakiwa katika gari moshi, elimu yangu
ikaishia pale nikarejea kuwa mtumwa.
Nilipambana hivyohivyo hadi siku ile mwalimu
Julius Kambarage Nyerere alivyokabidhiwa nchi
huru.
Walau hali ikaanza kuwa ya heri, sikutamani
kusoma tena.
Tayari nilikuwa nina familia ya mtoto mmoja
niliyempa nikiwa Mwanza baada ya kufukuzwa
shuleni.
Sikupata mtoto huyu na yule mwanamke
aliyetuletea uhasama baina yangu na Jose.
Nilizaa na maskini mwenzangu tukalea kimaskini
hivyohivyo.
Niliamua kuanzisha familia kwa sababu sikuwa
na familia tena, baba yangu alifariki na mama
vilevile.
Halikuwa jambo la ajabu kwa wakati ile kupoteza
familia yako.
Nikamsahau Joseph Kazeze katika kichwa
changu. Niliamini yote yaliyotokea Tabora Central
School ni mambo ya ujana tu.
Nilikuja kulisikia jina hili katika siasa.
Eti Joseph Kazeze ni mjumbe sijui wa kamati
gani katika chama tawala. Hii ilikuwa mnamo
mwaka 1977. Niliamua nisijihusishe na habari
zozote kuhusu Jose kwa sababu kwa kufanya
hivyo nilikuwa nakumbuka chanzo cha mimi
kuishia kati katika masomo yangu na sasa sina
thamani yoyote katika jamii.
Miaka mitatu baadaye yule mwanaharamu
akaanza kunizongazonga tena.
Alinibomolea nyumba yangu. Japokuwa hakuja
yeye moja kwa moja lakini nilijua kupitia
waliokuja, akanibambikiza kesi kadhaa bahati
nzuri ilikuwa upande wangu nikawa natoka
salama.
Huwezi kuamini, akavuka mipaka baada ya kuona
kila analofanya si kitu kwangu.
Hivi unaweza ukaamini Jose Kazeze akaamua
kumposa upya mke wangu!
Andika kila ninachokueleza usiache walau neno
moja, yote yana maana sana.
Nd’o hivyo bwana Joseph akamlaghai mke wangu
ajuavyo yeye, alikuwa na gari lake aina ya Land
Rover ya chama tawala basi aliitumia hii kuishika
akili ya mke wangu.
Yule mwanamke naye alikuwa mjinga kweli, ujue
nilishamweleza kinagaubaga kuhusu uhuni wa
Jose lakini akashawishika akaniacha eti.
Hivi kama sio kuumizana nafsi ni nini hiki, kweli
Joseph ambaye alikuwa ana pesa tayari anaamua
kuniingilia anga zangu, tena bora ingekuwa kwa
mwanamke ambaye ni kigoli, mwanamke huyu
alikuwa amecharazwa bakora za mkoloni haswa
hatamaniki, alikuwa amechanjwa mwili mzima
chanjo za kinga ambazo ziliaminiwa na makabila
mbalimbali. Haya yote akajifanya hayaoni....
akaamua kuniadhibu.
Alifanikiwa!
Nilimwambia mwanangu juu ya alichonifanyia
mama yake. Nilimweleza huku ninalia.
Akatangaza kumchukia milele!
Basi rafiki yangu akabaki kuwa huyo mwanangu
wa pekee, niliyemuita jina Salama.
Mama Salama akahamia katika maisha ya
Joseph Kazeze.Iliniuma mno, huyu bwana
katumia cheo chake kulipiza kisasi angali mimi
sikufanya lolote enzi zile Tabora kwa
kumkomesha.
Sasa mwanamke nikamuachia, sifa zote
nikamuachia lakini yule bwana kumbe
hajaridhika.
Hapo sasa zile jazba za enzi za shule zikarejea
nikajisema kuwa nchi hii ni huru kabisa, tena sio
uhuru wa bendera. Hakuna utumwa tena labda
ukusudie mwenyewe. Ajabu anajitokeza mjinga
mmoja mwenye ngozi kama yangu ananirudisha
utumwani.
Siku ya tukio sikumuaga Salama!
“Naomba kwa leo tuishie hapo mzee wangu
Majenga..... sitaki kusikia kilichotokea.
Nakuomba sana alfajiri tutaendelea na mkasa
huu. Nimefurahi sana kukukuta ukiwa hai mzee.
Na badi nashangaa uliweza vipi kutunza karatasi
hizi kila ulipoenda na kutarajia siko moja
utamsomea mtu” Martin Nguzu lizungumza kwa
hisia kali, sauti yake ilikuwa baridi mno. Alikuwa
ameguswa mno na maandishi yale.
“Niliwahi kumsomea mama yako, sijui hata kama
alinisikiliza kwa makini maana alikuwa analia kila
akisikia lolote kuhusu hayati Ngengekuzenza
Nguzu ambaye ni baba yake mzazi.” Alijibu
Majenga kwa utulivu.
Na hapo akaitoa miwani yake usoni.
Akajifuta machozi.
“Babu yako alikuwa mtu wa aina yake sana.
Namuona hai ndani ya macho yako...”
Akaongezea huku akimshika begani Martin
Nguzu.
Nguzu akamsaidia kuinuka, akamkokota mpaka
ndani akamsaidia kukiandaa kitanda chake
akamwacha akilala. Naye akaenda katika chumba
kingine akalala.
____HAYA sasa Ngengekuzenza Nguzu
huyoooo.....
___Majenga naye huyoooo
 
SEHEMU YA KUMI NA NNE
Wakati Martin Nguzu na mzee Majenga
wanakubaliana kulala ili siku inayofuata
waendelee kusoma maandishi yale ambayo
Nguzu aliamini kuwa si haba yatampa mwanga
kidogo juu ya matukio yote yanayotokea. Upande
mwingine palikuwa panapambazuka.
Inspekta Kobo akiwa na pingu miguuni na
mikononi mwake alikuwa katika mahojiano
mazito sana.
Mdomo wake ulikuwa umeanguka na na kubaki
wazi kutokana na kipigo kikali alichopokea,
midomo hii iliyokosa ushirikiano ilisababisha
udenda ulioambatana na damu umwagike katika
namna ya kusikitisha sana.
Mguu wake uliokuwa umeunganishwa kwa vyuma
ulikuwa umepigwa na sasa baadhi ya vyuma
vilikuwa vinachungulia nje.
Damu nzito iliyoganda katika chuma kile ilisaidia
kuficha ukweli wa mambo.
Inspekta hakuwa na uwezo wa kutembea na
hakulazimishwa kutembea badala yake
aliburuzwa hadi akafika mahali alipohitajika.
Macho yake mekundu yalikuwa makubwa sana,
na yalikuwa yakiviringika huku na kule katika
namna ya kuomba huruma ya yeyote yule
mwenye mamlaka ya juu yake.
Hakutokea japo mmoja wa kumtetea.
Maelezo aliyokuwa ameyatoa waliosikiliza
hayakuwakuna kabisa na hivyo wakaona suluhu
ni kumbana vyema kwa kumuumiza ili aweze
kutapika siri zote alizomeza.
"Inspekta Kobo, hili ni agizo la mwisho kabisa la
kukubembeleza wewe kusema ukweli wote ili
ubaki kuwa salama ama la tutatumia nguvu. Na
hatushindwi!" Sauti ya kusihi iliyojaa madaraka
iliunguruma.
Inspekta akastaajabu, hawa mabwana tayari
walikuwa wameitengua taya yake, wakaupoteza
njia mguu wake na sasa yungali mahututi katika
bahari ya maumivu, sasa anaelezwa kuwa
asiposema ukweli watatumia nguvu.
Nguvu! alistaajabu...
Nguvu gani zaidi ama watamkaliza katika kiti
chenye shoti ya umeme, au watampiga risasi?
Hizi nd'o nguvu ambazo walikuwa hawajatumia.
"Mkuu nilichokiandika katika maelezo yangu ni
hicho hicho sijaongopa hata nikishtuliwa usiku
wa manane siwezi kupindisha ukweli huo." Alijibu
kwa shida sana.
"Kama uliweza kupindisha shabaha yako maksudi
na kumwacha hai jambazi mkorofi ambaye
tumehangaika miaka nenda miaka rudi kumsaka
unashindwa vipi kuupindisha ukweli?" Alihoji kisha
akasimama wima na kuendelea kuzungumza.
"Kobo, katika maisha yako ya kulenga shabaha
umeangusha mibuyu mingapi iliyoleta ukorofi?"
"Mingi sana afande." alijibu kwa sauti ya chini.
"Umetunukiwa shani ngapi kutokana na kulenga
kwako shabaha?"
"Tano afande."
"Unaikumbuka shabaha yako ngumu kupita zote?"
"Ahh! mmh! ndio afande, ni ile ya kutoka ghorofa
moja kwenda nyingine." aliendelea kujibu
upesiupesi. Bila kujua nini hatma ya maswali
yale.
"Unaukumbuka umbali kimakadirio?"
"Mita mia tano...." alijibu kwa utulivu. Na safari
hii sauti ilikuwa chini zaidi kwa sababu aliijua nia
ya maswali yale.
"Yaani nusu kilometa sivyo? Na haukuwa katika
utulivu wowote, na uliweza kuipata ile shabaha
bila kukosa. Na ilikuwa ni usiku..... halafu leo hii
unapiga risasi tatu maksudi unamkosa adui
anayetikisa taifa. Kobo! Kwa kitendo chako hicho
cha kumuacha adui wa taifa unadhani
watanzania wapo radhi kukusamehe? Mimi kama
mtanzania siwezi kukusamehe... nastaajabu
wanakuchelewesha nini kukutia kitanzi bazazi
wewe.... uliyechagua kumlinda mwanaharamu
mwenzako!" Sasa alikuwa amewaka yule bwana
aliyekuwa anamuhoji Inspekta Kobo. Na alikuwa
anatetemeka mno.
Inspekta alikuwa amekamatwa pabaya.
"Ok! unalipwa shilingi ngapi kila anapofanya
uhalifu wake.... tuzungumze kama wanaume na
haya mambo yaishe. Maana Tanzania mambo ya
kitanzi tulishayafuta, na hata ukifungwa maisha
huyo mwanaharamu atakuja kukutoa tu utakuwa
huru. Haya nieleze tu, unapewa kiasi gani
kulisaliti jeshi la polisi katika oparesheni
kabambe namna ile." Swali likatupwa.
Inspekta Kobo akafadhaika mno, kwa sababu
hakuwa kama walivyodhania.
Alipojaribu kupinga, hasira za yule bwana
zikamuangukia.
Akapokea teke kali katika shingo yake,
akarushwa na kutua pembeni akabaki kukoroma
huku damu ikimtoka puani.
Akatamani kuelezea ukweli wa kila jambo lakini
hakuona kama ataeleweka maana katika
maandishi yake hakuandika kuhusu mashaka
yake juu ya ile sauti inayotamka 'ANGUSHA
MBUYU'. Hakuandika kuhusiana na kifo cha utata
cha Martin Nguzu na hakugusia hata kidogo juu
ya mahusiano baina yake na koplo Zubeda.
Angeanza kuelezea hayo angeonekana ni muongo
mara mia zaidi ya alivyochukuliwa awali.
Inspekta akaamua kubaki kimya.
"Inspekta Kobo hivi unajua kuwa hii kesi yako
inaweza kuhesabiwa kama kesi ya uhaini na
itakuweka pabaya wewe na familia yako, ama
unajitazama wewe na masilahi yako pekee
hauitazamani familia yako. Haumtazami mkeo
ambaye hadi sasa hajui kinachoendelea
ulimwenguni, hujali kuhusu watoto wako
unajitazama wewe pekee. Sasa mimi nimekusihi
sana imetosha naandika ripoti tusilaumiane katika
hili." Alizungumza kwa sauti tulivu kabisa huku
akiwa anamtazama Inspekta Kobo.
Maneno yale juu ya familia yake yalimvuruga
Kobo aliyejitambua wazi kuwa hana kosa lolote
lile, lakini la kufanya nd'o hakuwa nalo.
Akarejeshwa katika chumba alichokuwa
anafungiwa mle akiwa peke yake.
Tofauti na siku nyingine ambapo chumba hiki
kilikuwa kinazimwa mwanga wa taa na kubaki
katika giza siku hii kilikuwa kina mwanga na zaidi
kiliongezeka kiti.
Nanyongwa!!
Hisia zikakipiga kichwa cha inspekta Kobo,
tumbo likaanza kuunguruma kwa hofu ya
kuupoteza uhai wake.
Akaingizwa pale chumbani.
Kimya kikatanda kwa dakika zisizopungua tatu.
Kisha zikasikika hatua zikijongea katika kile
chumba.
Mlango ukafunguliwa na askari wawili, kisha kwa
mwendo wa taratibu akaingia Inspekta jenerali
wa polisi (IGP).
Mwili wa inspekta Kobo ukaingiwa na ubaridi
mkali sana, akaunyanyua uso wake na
kumtazama bwana yule nadhifu kabisa aliyekuwa
katika mavazi yake ya kazi.
"Funga mlango!" akawaamuru wale askari.
Wakatii! kisha wakaondoka na kuliacha eneo lile
likiwa na watu wawili pekee.
Mwili wa Kobo ulikuwa umesulubika sana, lakini
kwa kumtazama bwana huyu mwili ukajiona kuwa
inayokuja nd'o suluba taslimu.
Kobo alitambua kuwa IGP aliisubiri hii nafasi kwa
hamu sana ili aweze kumnyoosha na sasa
alikuwa ameipata. Iwe isiwe atamwadabisha.
"K" IGP akaita kwa upole.
Inspekta akamtazama kisha akaitika kwa shida
sana.
"Pole sana rafiki yangu. Pole!" IGP aliketi vyema.
Unafiki! Kobo akajisemea.
"Kabla sijazungumza mengi na wewe ninapenda
kukueleza kuwa ninakupenda sana rafiki yangu,
huwezi kuamini haya lakini elewa kuwa
nimejaribu zaidi ya mara tano kuonana na wewe
lakini nimeshindwa kwa sababu sikuwa tayari
kukuona katika hali hii. Umeteseka sana K"
alizungumza kwa hisia IGP.
Hali hii ilimtisha Kobo, akajiuliza anachokisikia ni
sahihi ama kuna namna ya ulaghai.
Yaani huyu bwana ajisikie vibaya kwa yeye kuwa
katika wakati ule mgumu.
Haiwezekani.
Inspekta Kobo akakumbuka vitisho vyote
alivyowahi kupewa na IGP wakati huo akiwa
hajapewa dhamana hii ya juu katika jeshi la
polisi.
"K, yale yote yalikwisha kwa upande wangu.
Nimetafiti sana na nikagundua kuwa wewe
haukuwa chanzo cha mke wangu kuwa mlemavu.
Niliumia sana awali na kujikuta nikikuchukia lakini
nimeikubali hiyo hali na nipo hapa kwa ajili ya
kukusaidia tu! Tafadhali sema nami"
"Niliyoyasema ni hayohayo." Akajibu kwa ukaidi
Kobo, bado alikuwa na hisia za chuki dhidi ya
IGP bado hakuamini kuwa wao ni marafiki tena.
"K, sikiliza ndugu yangu. Ukaidi hautasaidia kitu
chochote kwa wakati huu. Laiti kama ningekuwa
juu ya sheria ningeamuru uachiwe huru na ubaki
kujuta na nafsi yako ikiwa ni kweli umefanya yote
hayo ama la. Lakini kwa hili mimi sina
ninalazimika kuiheshimu sheria ya nchi, sio
kuivunja kisa ninakuonea huruma. K, tafadhali
nieleze ni nini kilitokea...." IGP alizungumza
kiukarimu kabisa.
Inspekta Kobo akaamua kurusha karata yake ya
kwanza. Akaelezea kwa ufupi sakata la Nguzu,
hakulitaja jina la mwanamke ambaye alikuwa
anahusika.
Akaitaja ile sauti ambayo aliisikia usiku wa tukio
la Nguzu kuchomewa ndani na kisha akaitaja
tena sauti ileile ilisikika siku ambayo alikuwa
ameishika bunduki yake tayari kwa kufanya
shambulizi.
"Nikapagawa sana kugundua kuwa licha ya
kwamba nimelenga shabaha kwa ajili ya
kummaliza adui ila ndani yetu pia kuna adui.
Tena adui asiyekuwa na huruma aliyeiteketeza
kwa moto nyumba ya askari mwenzetu pasi na
huruma kabisa. Nilitetemeka sana, hata lile agizo
alilonipa la kuushusha mbuyu lilinikwaza badala
ya kunihamasisha. Hakika nilikuwa
natetemeka..."Alimalizia.
Palepale IGP akamsogelea na kumnong'oneza
jambo kwa kusihi.
"Usiyaseme maneno haya popote pale.
Umeniamini mimi imetosha sana na ninakuahidi
italeta manufaa. Nimeupata mwanga."
IGP akatulia kidogo kisha akarusha suala jipya
kabisa ambalo lilikuwa jipya kwa inspekta Kobo.
"Umesema juu ya Nguzu kuchomewa ndani ya
nyumba yake, unadai ulienda kuzungumza naye
usiku ule. Sawa kabisa.... na je Majenga
unamfahamu vipi?"
"Ma nani?"
"Majenga" Aklajibu IGP huku akimtazama kwa
ukaribu kabisa inspekta Kobo.
"Sijawahi kulisikia jina hili katika maisha yangu."
"K, mbona hutaki kuamini kuwa ningali upande
wako? nieleze nijue ni wapi nakusaidia rafiki
yangu. Ujue kuna watu watatu wameuwawa huko
Shinyanga na huu mlolongo wote unakuangukia
wewe. Ndugu zao wamechachamaa si kidogo,
huyo Majenga ni nani Kobo! Tell me..." alianza
kupandwa na ghadhabu IGP.
"Simjui na sijawahi kulisikia jina hilo Gervas,
mbona unanilazimisha kutema maneno ambayo
akili yangu haijawahi kuyameza. Simjui huyo
Majenga for God's sake!!" Aling'aka inspekta
Kobo huku akimtaja IGP kwa jina lake.
IGP akaanza kufura kwa hasira, akajitahidi
kujiweka katika hali ya kawaida. Akauliza tena na
tena bila majibu kubadilika.
Inspekta Kobo akasimamia analoliamini!
IGP akamtazama kwa sekunde kadhaa, akatoa
kitambaa chake mfukoni na kujipangusa matone
ya jasho na mwisho akamtupia Kobo neno la
mwisho.
"Pambazuko hili litakuwa baya sana kwako na
sitakuwa na namna ya kukusaidia. Nimejaribu
sana Kobo nawe umeona. Umekataa kumtaja
Majenga na unamjua waziwazi...."
Akasubiri kidogo, Kobo akamtazama kisha
akalazimisha tabasamu na kisha akazungumza.
"Nimekuwa na mapambazuko mabaya sana tangu
mke wangu apate janga lile, nimekuwa na
mapambazuko mengine mabaya tangu vijana
wako, vijana niliowafundisha ukakamavu jeshini
walipougawana mwili wangu na kufanya kwa
vitendo yale niliyowafundisha, mapambazuko
mabaya hayataanza leo ama kesho yalianza
tangu uliponituhumu kuwa nimeshiriki kumfanya
mkeo awe mlemavu wa miguu angali nilijaribu
kadri ya uwezo kuokoa maisha yake, niliokoa
maisha yako pia Gervas kwa kukusukuma ili
usipigwe risasi, nikawa na mapambazuko mabaya
ulipozisahau fadhila zangu, ni pambazuko gani
baya zaidi unaloniahidi sasa... eeh! pambazuko
gani unalolisema, pambazuko la kupoteza uhai?
Kuteswa? Kufungwa gerezani maisha yangu
yote? Hakuna pambazuko la ajabu hata moja kati
ya hayo, ni wewe utayaishi mapambazuko ya
ajabu siku utakapoujua ukweli angali
nimenyamaza katika kile kimya cha milele,
Attaccati a sto cazzo."
akaweka kituo huku akimalizia kwa kutokwa na
lile tusi lake murua katika lugha ya kiitaliano.
IGP akabaki kuganda, midomo ikimchezacheza
asijue ni maamuzi gani ayachukue.
Akatoweka pale na kwenda nyuma ya mlango.
Akajibanza pale na machozi yakaijua njia yake,
yakayalowanisha mashavu, kamasi nyepesi
zikatoka kuchungulia nini kinaendelea katika uso
wa IGP.
IGP alikuwa analia kiume!
_____
Majira ya saa sita usiku aligutuka kutoka usingizi
huku jasho likimtoka sana.
Majenga! jina hili likakivamia kichwa chake,
akaketi kitako na kuanza kukumbuka juu ya
maneno yale aliyokuwa akiyasoma yule mzee.
Akatamani asubuhi ifike upesi aweze kuendelea
kusikiliza ni kipi ambacho kitakuwa na faida
kubwa sana kwake.
Akamaizi kuwa licha ya kushtuka vile na
kuandamwa na jina hilo lakini pia alikuwa pia
amebanwa na haja ndogo.
Na choo kilikuwa mita nyingi kutoka chumba
alichokuwa amelala.
Akapatwa na uvivu sana huku akijilaumu kwa
kukataa kunywa maji mengi baada ya chakula
cha ili asije kupata shida kama hizi usiku na sasa
amezipata shida zilezile.
Akajivuta taratibu kuelekea choo kilipokuwa. Nje
palikuwa kimya sana, walisikika wale viumbe
wanaopenda kulala mchana kisha usiku
wanazurura kusumbua viumbe wengine.
Popo!
Umbali wa choo ulimtatiza sana, akajiona mpuuzi
sana giza lote lile kuna vichaka vya hapa na pale
ni kwanini ahangaike na choo.
Akakiendea kichaka kidogo alichokiona karibu
yake.
Akakidhi haja yake lakini hakuweza kugeuka
kabla ya kusikia sauti ikimuamuru asimame.
Akasimama tuli!
"Kwanini unakojoa vichakani we tahira?" sauti
ikakaripia.
Martin Nguzu akastaajabu, tangu afike pale
Shinyanga sauti karibia zote zilikuwa
zinaambatana vyema kabisa na lafudhi ya
kisukuma, iweje hii sauti inakuwa na miporomoko
ya pwani ama Zanzibar?
Hakujibu kitu!
"Nakuuliza weye mwanaharamu..."
"Nisamehe tafadhali..." Hatimaye akazungumza.
"Mzee Majenga analala chumba kipi hapa? na ni
nani ako...." Swali likatupwa.
"Analala nyumba kubwa!"
"Geuka utupeleke upesi.."
Nguzu akageuka na kukutana na mambo
aliyoyazoea.
Mitutu ya bunduki.
Walioibebwa waliishika kizembe sana. Ni vile
hawakujua kuwa ile hatari inayodhaniwa kuzikwa
katika tanuru la moto, iliishia kung'arishwa na
kuwa dhahabu yenye thamani kali huku ikiwa na
makali ya kisu kipya.
Walisimama wanaume wawili, mmoja akiwa na
bastola mkononi mwake. Huyu aliielekeza kwa
Nguzu.
Nguzu akajitia kutetemeka huku akiwasihi
wasimuue. Kutetemeka kule kukawazidishia
uzembe.
Mmoja aliyebaki akasikika akizungumza kwenye
simu kuwataarifu wenzake kuwa wamefika eneo
la tukio na muda si mrefu watauchukua mzigo
wao.
Walitembea hatua kumi kuelekea ilipokuwa
nyumba ya mzee Majenga na familia yake.
Nguzu alizihesabu zile hatua vyema huku macho
yake yakiwa makini sana kutazama kitu.
Hatimaye akakifikia, kilikuwa ni kigogo
kilichokuwa njiani. Akakikanyaga na kujikwaa
maksudi.
Akaanguka chini huku akitokwa na yowe la hofu.
"Inuka hanithi wewe..."
Kauli hii aliisubiri Nguzu kwa hamu, mkono wake
ulikuwa tayari na jiwe, akatumia sekunde chache
kubaini kuwa mshika bastola yule hakuwa
anakaribia kufyatua, kidole chake kilikuwa mbali
kabisa na kifyatulio.
Safi sana! akajisemea na hapo akajitutumua
ainuke.
Alipoinuka akaliachia lile jiwe likampata bwana
mwenye lafudhi ya kipemba usoni, kapiga yowe
huku bunduki ikimtoka.
Yule mwenzake akajiweka sawa kufanya
shambulizi kwa kutumia bunduki.
Nguzu akajirusha huku goti lake likitangulia
mbele hadi katika kifuani kwa adui.
Akambwaga chini.
Nguzu akaitwaa ile bunduki.
"Acha ujinga dogo, vita sio kama kunywa urojo
unakunywa hata kama ni kibogoyo. Vita inahitaji
watu majasiri." Alimwonya alipomuona akitafuta
bastola.
Yule bwana akatulia asiamini kuwa kibao
kimewageukia wao.
Mwenzake alikuwa amekodoa macho.
"Mwambie jamaa aje moja kwa moja eneo la
tukio, ukiongeza neno nakuua muda huu, na
usipoongeza nitakuua baadaye." Nguzu
akaamrisha.
Simu ikapigwa jamaa akazungumza aliyopaswa
kuzungumza. Kisha simu ikakatwa.
"Nilikueleza ukiongeza neno nakufanyaje?"
"Unaniua!"
"Na usipoongeza?"
"Utaniua baadaye. Nisamehe tafadhali sisi
tunatumwa tu" alijibu huku akitetemeka.
Nguzu akamgeukia yule mpemba.
"Shehe! mwenzako kaongeza neno tayari,
anasema nimsamehe na sikusema hivyo."
Hakusubiri jibu, akaigeuza bunduki, hakutaka
kupoteza risasi akaizamisha bunduki katika kifua
cha yule bwana singe ikaingia nzima nzima.
Akagalagala kuusaka uhai wake.
Mpemba akakurupuka akairukia bastola. Lakini
hakuweza kufyatua kabla Nguzu naye hajamrukia
na kumkanyaga mkono.
"Swahiba, nakukumbusha tena huu sio urojo kila
mtu anakunywa." akamtia ngumi kali katika paji
la uso wake.
Ilikuwa ni vita ya kistarabu sana, mtu akianguka
chini waliolala wanajua ni maembe yanaanguka,
wanajigeuza upande wa pili na kuendelea kuota
ndoto zao.
Hawakujua kuwa roho zilikuwa zinatoka na
uwanja ule ulikuwa umegeuka kuwa wa kivita.
Nguzu akambana maswali yule mpemba, akajibu
kuwa huyo anayekuja ndiye kiongozi wao,
wenyewe hawajui kiundani juu ya tukio lile.
"Kwa maana hiyo unamaanisha wewe hauna
umuhimu wowote kwangu sivyo."
"Walah! naapa mie wanionea bure tu sina
nijualo." Jibu lile likawa la mwisho.
Kama hauna maana unabaki na Nguzu kufanya
nini.
Akaunganishwa katika safari ya mwenzake
aliyekuwa ametulia tayari.
Nguzu akaweka windo lake kumngojea huyo
aliyeitwa mjua mengi.
Windo hili likazua safari mpya ya Konstebo
Martin Nguzu kurejea jijini Dar es salaam.
Jiji ambalo linaamini kuwa yu kwa muumba
akijibu tuhuma zinazomkabili. Huku wengine
wakiamini bado anahangaika na adhabu ya
kaburi.
 
SEHEMU YA KUMI NA TANO
ILIKUWA safari iliyojaa katika kichwa chake
ghafla baada ya vita ile ya usiku iliyoondoka na
uhai wa watu watatu ambapo mmoja kati yao
alikuwa ni kiongozi wao kwa mujibu wa maelezo
yao.
Martin Nguzu ambaye sasa hakuwa akiushangaa
uwezo wake wa kukabiliana na maadui alikuwa
amewaangusha wengine watatu huku akifanikiwa
kuwapokonya bunduki tatu pamoja na risasi za
kutosha kabisa.
Hakutaka kulala baada ya kuhakikisha
ameitelekeza ile miili mbali na ngome ya mzee
Majenga. Alimwamsha mzee Majenga na
kumweleza kwa ufupi juu ya kilichotokea.
Tofauti na matarajio yake kuwa taarifa ile
itamtisha sana Majenga, hii ilikuwa kinyume.
Mzee Majenga akatokwa na kicheko kidogo kisha
akampigapiga kifuani Martin Nguzu na kumwita
kwa jina la babu yake.
"Ngengekuzenza Nguzu umezaliwa upya..." Kauli
ile ilimtoka na kumwacha Martin Nguzu katika
pumbazo asielewe ni kitu gani bwana yule
alimaanisha.
"Mimi nimezeeka kijana wangu, niliisubiri sana hii
vita kwa muda mrefu lakini imekuja nikiwa mzee
tayari. Nenda ukapambane hii ni vita yako na
inakuhusu. Nakuachia haya maandishi
niliyoyaandika bila kuongeza wala kupunguza
neno kutoka katika kinywa cha hayati babu yako
anayeishi sasa katika nafsi yako. Hakikisha
unayamaliza yote kabla haujaivaa hiyo vita......
mimi nitakuwa salama kabisa na tutakutana
nikiwa hai, na hata nikifariki ni kwa sababu ya
uzee tu..." Aliongea kwa ujasiri mkuu. Kisha
akachechemea hadi ndani na kuchukua
makaratasi yaliyoandikwa kwa kalamu
akamkabidhi Martin.
"Nilikuwa napenda sana kuandika na babu yako
alikuwa anapenda sana kunisimulia, nadhani ni
maneno hayo kwa ufupi yatakupa jawabu
nilikutana vipi na babu yako." Majenga alitoa
kauli ile na Martin akaipokea lakini alikuwa na
swali la ziada.
"Niliokoka vipi katika ule moto jijini Dar es
salaam?"
"Mzee wako asingeweza kukuacha uangamie.
Wazee wa zamani hawakuwa wa kawaida,
akinuia jambo linakuwa kama lilivyo, nadhani ni
kutokana na kutenda dhambi chache nd'o maana
Mungu alikuwa akiwasikiliza." Alifafanua na
kuzidi kumvuruga Martin.
Akagundua mvurugano ule, akaongezea "Kasome
haya yote kabla hujaamua wapi pa kuanzia"
Maongezi yakaishia hapo.
MAANDISHI YA NGENGEKUZENZA.
Ubaya ni kwamba wakati wa ukoloni, sisi watu wa
rangi nyeusi hatukuishia tu kunyanyaswa na
ngozi nyeupe katika uhai wetu, hata ulipokuja
ustaarabu wa kuhifadhi maiti zetu sisi tuliwekwa
katika kundi la mbwa koko aliyefia jaani baada ya
kukabwa na mfupa aliodhani ni mnofu.
Ukipata bahati sana unafukiwa, ila ni waafrika
wachache waliokuwa na bahati, wengi
tulitunukiwa nuksi.
Ukiwa na nuksi unaachwa hapohapo ulipofia ama
unasogezwa kidogo porini, ukawe chakula kwa
wanyama wenye tabia ya uvivu katika suala la
kuwinda na ndege wanaoona sifa kudonoa
donoa.
Hata babu yangu alikuwa na nuksi vilevile baada
ya kufariki alitupwa, akaipata bahati akiwa maiti
tayari waafrika kadhaa wakamfukia.
Baada ya kuupata uhuru wetu nikawa
naitembelea ile sehemu niliyoaminishwa kuwa
babu yangu alifukiwa pale, pakawekwa alama
nami nikawa naenda kumsalimia na kuzungumza
naye bila kujali ananisikia ama la!
Sasa yule mwanahizaya baada ya kuona haitoshi
kumchukua kiharamia mke wangu na kuniacha
katika jitimai, akaona hata! hii haitoshi huyu
bwege bado anapata raha. Akaanza kuniandama
kivingine, najua aliwatuma mashushu wake
waliokiamini na kukiabudu chama chao kuliko
Mungu wa mbinguni na miungu ya porini.
Hawa wakamfikishia habari kuwa ninayo furaha
nyingine, furaha ya kuzungumza na babu yangu
makaburini.
Ikapita ajenda katika siku nisiyoijua na baadaye
ikawa ni amri bila kutahadhalishwa.
Eneo lile lilipaswa kupandwa miti, mara lilitakiwa
kupita barabara.
Sikuelewa hata kidogo, na hakuna aliyesubiri
nielewe.
Kwani Ngengekuzenza nani mpaka aelewe?
Lile nililoamini kuwa ni kaburi likavunjwa na huyu
mkoloni mshenzi mwenye rangi kama yangu huku
akiiga miondoko ya wazungu na afro yake
kichwani akiipaka kalikiti na kuwa laini kama
nywele za mkoloni.
Lugha yake pia ilifanana na yao.
Poor Joseph Kazeze!
Kama ni kunipiga, hapa alinipiga na mjeledi wa
chuma nikaangukia pua huku mikono yangu
ikishika makaa ya moto.
Huyu mjinga aliniweza hakika!
Uchungu wangu ule nikamshirikisha mwanangu
Salama nikamweleza kuwa Jose anataka kuvuka
mipaka ambayo ameivuka tayari, yaani sielewi
anachotaka.
Salama alinisihi niachane naye, nikaona hajui
uchungu ninaoupitia kwa kupokonywa mke na
kisha hapohapo nikapokonywa furaha yangu.
Babu yangu!
"Salama, nikiachana naye akagundua nina furaha
kuwa na wewe atakuchukua na wewe pia...."
nilimwambia Salama. Wazo hili likamkuna na
kuiona hatari ya waziwazi.
"Sasa utamfanya nini?"
"Yule ni mjinga tu kwangu, nataka nimfanyie yale
mambo ambayo wajanja huwafanyia wajinga
wanaodhani pesa nd'o ujanja." nilimweleza huku
nikiona wazi kuwa hanielewi.
"Unataka upigane naye?" aliniuliza.
"Nikipigana naye wote tutakuwa levo ileile ya
ujinga, nataka nimpige ili tuunde daraja katika ya
nani mjinga na nani mjanja."
"Lakini baba, huyu ana pesa na cheo
atakusumbua sana. Yaani nina uhakika hautafikia
hata nusu ya azma yako."
"Kwanini unasema una uhakika." nilimuuliza
salama.
"Si kila kitu kipo wazi, ana pesa na vyeo."
"Sikiliza mwanangu Salama na uliweke hili milele
katika maisha yako, hapa duniani kuna kitu
kimoja tu nd'o cha uhakika vingine vyote si vya
uhakika. KIFO pekee ndo jambo la uhakika, kila
mtu atakufa hii haina mjadala. Ujiue, unyweshwe
sumu, ugongwe na gari ama hata ukilala
usiamke. Vyote vina maana moja tu ya
uhakika.... asije akakudanganya mtu kuwa jambo
hili ni uhakika... anakulaghai nawewe
unayemsikiliza na kumkubalia unakuwa upande
wa mjinga. Sipendi uwe mjinga siku moja...."
Nilimsomea mambo yale. Yakamuingia na kumpa
ujasiri naye akanibariki katika uamuzi wangu na
hiyo ilikuwa ni mnamo mwaka elfu tisa mia
themanini na tatu ama nne kama sijasahau.
Sijui itakuwaje miaka ya huko mbele lakini enzi
zetu hizi hapakuwa na ulinzi wa kutosha kwa
viongozi, ulinzi huo tuliusikia tu na kuuona
walipokuja viongozi kutoa nje, Mwalimu Julius
Nyerere alihamasisha sera za kuishi kijamaa,
nasi tukaamua kuishi kama ndugu.
Hapakuwa na wa kumpinga kirahisi mwalimu.
Ukitaka kumpinga sisi tunakwambia nenda
ukapambane kuileta Tanganyika huru ndipo
ujilinganishe na mtaalamu huyu.
Hivyo tuliishi kijamaa sana, halikuwa jambo la
ajabu kukutana na mwalimu Nyerere barabarani.
Sasa vipi kuhusu mjinga huyu anayeitwa Joseph
Kazeze?
Sidhani kama kwa miaka yenu huko mbeleni
itakuwa hivi. Nahisi hata balozi naye atatafuta
ulinzi...
Nilikueleza awali kuwa tangu nilipokuwa mtoto
nilikuwa nina uwezo mkubwa sana darasani, hata
akili yangu haikuwa ndogo katika kufikiri.
Nikaamua kuitumia akili yangu kumwonyesha
yule bwana nini maana ya mwanaume kutoa
machozi.
Kwakweli nilimkosesha amani!
Kwanza nilifurahia kile kitendo cha mwalimu
Nyerere kutowafukuza wazungu baada ya
kutupatia uhuru, hivyo upatikanaji wa silaha hadi
miaka ya themanini bado ulikuwa ni mwepesi
sana, unaweza kuipata bunduki hata kwa
kubadilishana na gunia la mahindi pekee.
Zilikuwa zimezagaa.
Nami nikajipatia bunduki yangu, uzuri nilipitia
jeshini hivyo sikuhitaji kufundishwa lolote.
Nikamuaga mwanangu kuwa naanzisha
mapambano rasmi.
Sikuwahi kuua ila nilijeruhi sana.
Nilianza na baba yake mzazi, akiwa katika
mizunguko yake. Nikamteka na kumpiga kipigo
cha mbwa mwizi, akavunjika mkono.
Sikumtumia salamu Jose Kazeze kama ni mimi ili
aendelee kuhadaika.
Akafuata mdogo wake, huyu nilimfungia safari
hadi Morogoro, nikamkamata na kumfunza adabu
asiweze hata kuiona sura yangu.
Jose Kazeze kitu alichosahau ni kwamba sisi
tulikuwa marafiki na nilimfahamu vyema yeye na
familia yake.
Niliendelea kumpa presha bwana yule kwa kufikia
hatua ya kuvamia kwake nikarusha risasi
zikavunja vioo vya nyumba aliyokuwa akiishi
lakini sikumdhuru mtu na sikutaka kumdhuru.
Uwezo wangu katika kupanga matukio ulianza
kunishangaza hata mimi, kila nikilala na kuamka
nawaza pigo jingine.
Jose akaanza kukonda!
Mara akaachana na yule mwanamke
aliyenipokonya.
Nami sikurudiana naye mjinga yule aliyekosa
hata nukta ya akili.
Nilikuwa nina hasira kali.
Baadaye baba yake alifariki, kwa magonjwa
mengine sijui kama na kile kipigo kilichangia.
Siku mbili baada ya kuzikwa nikaenda makaburini,
huku nikaweka bomu nililolipata kwa bei nzuri tu.
Likafanya mlipuko uliotikisa nchi.
Hakuna kilichobaki zaidi ya jeneza kusambaratika
huku na kule.
Hili lilikuwa pigo kubwa zaidi, wanandugu
wakalundikana nyumbani kwa Jose Kazeze
kujadiliana nini kinaendelea.
Nikavamia na huko na kurusha bomu jingine
katika choo kilichokuwa mbali kidogo na nyumba
na hii ni baada ya kuhakikisha hapakuwa na mtu
ndani yake.
Mparangano uliojitokeza nilijikuta nacheka
mwenyewe.
Amakweli mtenda akitendwa....
Jose akazidi kuzorota kiafya.
Ni hapa ndipo nikaamua kumweleza bayana ili
kama ni kufa kwa mshtuko afe tu, who cares?
Hakufa!
Ila alipagawa vibaya mno, na hapo ndipo
ikaanzishwa oparesheni ya Ngengekuzenza
Nguzu anasakwa auwawe.
Kisa ni jambazi, yakaundwa matukio ya
kushangaza kunihusu mimi na hapo nikaanza
kusakwa rasmi.
Nilijua kuwa hali ni mbaya, nikaraejea kwa
mwanangu... usiku wa mwisho kumwona
mwanangu.
Akanieleza kuwa yu mjamzito, nikamweleza
kuhusu kinachoandikwa na magazeti ya serikali
huku nikimweleza kuwa moyo wangu u radhi
kuwa nimemuweza yule bwana.
Zaidi ya hayo nikamsihi kuwa iwapo atazaa
mtoto wa kiume basi amwite Nguzu!
Tulikumbatiana huku sote tukishindwa kuyazuia
machozi.
Nikaondoka na kuja kwako Majenga unihifadhi
nikusimulie ya kuandika kama ulivyohitaji wewe
kijana wangu.
Na nimejitahidi sana kukusimulia.
Maandishi yale yaliacha nafasi kubwa kisha
ikafuata aya ambayo mwandishi wake alikuwa ni
Majenga.
Mnamo mwaka 1988 mwezi wa kumi na moja
mzee Ngengekuzenza mwenye msongo wa
mawazo kwa kuishi maisha ya mashaka kila
kukicha aliniaga kuwa anakwenda msalani,
ilikuwa majira ya usiku. Hakurejea mapema
nikalazimika kutoka pamoja na mbwa kwenda
kumtafuta.
Nilimtafuta sana hadi pambazuko likanikuta
nikiwa namtafuta, mbwa asiyechoka ndiye
alinihimiza kumdaka mzee wangu nimpendaye.
Hatimaye nikaufikia mti ambao alikuwa amejitia
kitanzi.
Nasikitika kuwa sikuwahi kukiri kuwa
ninamfahamu mzee yule kwa sababu za
kiusalama, alikuwa anasakwa sana na jeshi la
polisi kama jambazi sugu.
Niliporejea ndani nikakutana na karatasi katika
kitanda alichokuwa akilalia. Haikuwa na maneno
mengi sana aliniandikia kama nilivyokuwa
nimefanya tayari.
"Umenihifadhi kwa moyo wote wa upendo, wewe
ni kijana wangu nikupendaye. Ninaomba uendelee
kunitunzia maneno yangu..... utawapatia wajukuu
zangu ili wajifunze kuwa babu yao hakuwahi
kuwa mtu dhaifu hata kama nilionewa, babu yao
sikuwahi kuwa jambazi hata kama watayaona
maandishi hayo, pia kwa imani yangu kuu
naamini kuwa sijafa kirahisi rahisi. Mizimu ya
mababu zangu waliouwawa kifedhuli utumwani
imeniambia kuwa najipumzisha ila ipo siku
nitazaliwa na nitazaliwa katika damu yangu
mwenyewe. Ninapumzika Majenga ila nikizaliwa
tena usishangae. Naamini mizimu hii kulikoni dini
walizotuletea wakoloni, dini zilizotuongopea kuwa
Mungu ni mzungu, zikaenda mbali na kusema
kuwa Mungu anaishi katika majengo yao
waliyoyajenga.
Dini za kishenzi zilizonipatia jina la kishenzi,
Frolian na kunipokonya jina la kishujaa kutoka
kwa babu yangu.
Dini zilizotulaghai kuwa kila asemacho yule mzee
mweupe anayesimama mbele yetu basi ni sawa,
anatuona tunateseka na anasema tumwachie
Mungu, nasi tukijaribu kupambana anasema tena
sisi ni watu wabaya sana na hatufai kuwekwa
kundi la wanadamu.
Dini zao hazijaniambia kuwa siku moja nitarejea,
lakini wazee wangu ambao tuliwalilia njaa
wakatusikia katika miti, tuliwaomba kila kitu na
walikuwa wakweli.
Wazee hawahawa wamesema nami, acha
nipumzike ila ipo siku nitarejea na sitakuwa wa
kujificha tena.
Kwaheri mjukuu wangu!"
Kisha akwakeka hitimisho Majenga kwa wino
mzito.
"MNAMO MWAKA 1988 BABU YETU
Ngengekuzenza aliaga dunia na ni mwaka huohuo
mwanaye Salama alipata kujifungua... yule mtoto
akaitwa NGUZU"
______
NGUZU alibaini kuwa alikuwa anatetemeka baada
ya kuimaliza sentensi ile ya mwisho.
Akaituliza akili yake na kutaka kumaizi ni kitu
gani kimempa majibu katika maandishi yake.
Kwanza, aliamini katika mizimu na kimyakimya
akakiri kuwa mzimu wa babu yake ungali ndani
yake.
Pili, Jose kazeze yawezekana aliweka kisasi cha
kudumu, baada ya familia yake kunyanyaswa
akaisambaza ile chuki kwa wajukuu na vitukuu
kama wapo.
Hivyo yawezekana mmoja kati ya kitukuu ama
mjukuu alikuwa akilishambulia jina la Nguzu
popote atakapokutana nalo hivyo naye alikuwa
ameshambuliwa.
Mambo haya mawili yakamwacha katika
sintyofahamu nyingine mpya.
Akajaribu kulitaja jina la Inspekta Kobo......
akatazama kisa chake hadi kuja kumchomea
ndani ya nyumba yake.
Hili akaliweka katika mabano, yawezekana kuna
watu wengine walihusika katika hili jambo.
Akayakumbuka maneno ya yule kiongozi wa
waliotumwa kumkamata Majenga.
Akakumbuka kuwa yule bwana ndiye
aliyemueleza juu ya Inspekta Kobo kuwa yungali
rumande akituhumiwa kwa kesi mbaya kabisa
inayoweza kumtokomeza uraiani, lakini alimtajia
jina la kiongozi wao mkuu ambaye hata wao
hawakuwahi kumwona hapo kabla.
Zumbe!
Nguzu akafuatilia katika mitandao mbalimbali
kutazama huyu mtu ni nani katika serikali ili ajue
je? ana uhusiano na ukoo wa Kazeze? na kama
hana uhusiano ni kitu gani anataka?
Kichwa kikamuuma alipojikuta anayo orodha
kubwa sana katika kichwa chake.
Na kadri basi lilivyoikaribia ardhi ya jijini Dar es
salaam,mara moyo wa Nguzu ukapiga kwa nguvu
sana.
Kuna kitu alikuwa amekisahau kwa muda mrefu.
Koplo Zubeda!
Mungu wangu! Akahamanika kutokana na hali ile
ambayo ilimtokea naye asijue ni kwanini imekuwa
hivyo ghafla wakati analikaribia jiji na si wakati
yupo mbali?
 
SEHEMU YA KUMI NA SITA
MAJIRA YA saa saba usiku Martin Nguzu alikuwa
akirandaranda katika kona mbalimbali za jiji la
Dar es salaam kusaka hoteli ambayo angeweza
kulala kama si kupumzika mpaka patakapokucha
na kuutaza uelekeo ambao anapaswa kuanza
nao.
Hakuwa na mashaka yoyote ya kuufichaficha uso
wake, habari zake zilikuwa zimesambaa lakini si
picha yake.
Wasambaze picha yake kwa cheo chake cha u-
konstebo kwani hawana mambo mengine ya
kuandika.
Alifanikiwa kupata hoteli ya bei ya wastani,
akafanya malipo na kujiandikisha kwa jina batili.
Akakabidhiwa chumba.
Alipoingia na kuufunga mlango akaiwasha taa,
akakiona kioo kikubwa jirani na mlango.
Akajitazama jinsi alivyokuwa, kimaumbile alijiona
yungali vilevile lakini ndani ya mwili wake alijihisi
yupo ngangali sana tofauti na awali.
Bila kutarajia akajikuta akimuwaza tena Zubeda.
Akiwa palepale mkabala na kioo alifikiria ule
ukaribu wao jinsi ulivyokuwa ukimpa raha ya
kipekee, raha iliyomfanya ajikute akimwonea wivu
inspekta ambaye alisemekana kummiliki Zubeda,
kuna kipindi alikuwa akitamani hata kumdhuru
yule inspekta ambaye ndiye kikwazo pekee
kilichokuwa kati yake na penzi la uhuru baina
yake na Zubeda.
Nguzu alikuwa akitamani kumtambulisha Zubeda
kwa marafiki zake kama shemeji yao, ukiachana
na kuufurahisha moyo wake na pia kuuweka wazi
udhibiti wake dhidi ya Zubeda, Sifa pia kilikuwa ni
kigezo cha kutamani uhuru ule.
Nani ambaye angeacha kumsifia kuwa anamiliki
'mtoto mkali'
Zubeda alikuwa mzuri, urembo wake haukufichika
hata alipojitundika katika gwanda zake za kazini.
Askari wengi walikiri kuwa binti huyu alikuwa wa
aina yake, na hii ni sifa waliyoitoa huku akiwa
katika gwanda zake.
Nguzu alikuwa amepata fursa ya kuziondoa zile
gwanda kisha akamvesha kanga moja nyepesi
mwanadada huyu na kisha kuambatana naye
maliwatoni.
Macho yake mawili yenye nguvu yakifanikiwa
kutazamana ana kwa ana na mzigo wa matiti
ambayo yalikuwa yamevuka kidogo ule muda
maarufu wa 'saa sita' lakini hayakuwa mbali sana
kufananishwa na muda huo hasahasa yakipewa
msaada mdogo wa sidiria.
Macho ya Zubeda yangeuamuru mwili wa
mwanaume yeyote atakayemtilia maanani
kujikuta ukisisimka na donge la hamu kumshika.
Macho yake makali angali akiwa kazini yalikuwa
yanatepeta wakiwa wawili na Nguzu na kumfanya
Nguzu ashangazwe na hali hii.
"Huyu mtu aliupata vipi ukoplo wa polisi? Kwa
macho haya tepevu?" Haya ni baadhi ya maswali
aliyojiuliza kabla hajachoshwa na mikono laini ya
Zubeda. Mikono ambayo hakuamini hata kama
inao uwezo wa kuzishika pingu na kumlazimisha
mtuhumiwa azivae.
Ajabu Zubeda alisifika kwa kuwahenyesha
watuhumiwa.
Kuhenyesha watuhumiwa??
Ilishangaza!
Lakini Nguzu naye akajikuta anahenya
kupambana na msisimko uliokuwa ukimkumba
kila mara mikono ile ilipomgusa.
Na hapo akakiri kuwa hata yeye ni mtuhumiwa
pia na alikuwa anahenyeshwa wawapo chumbani
wawili.
Kweli Zubeda ni kiboko!
Kumbukumbu hizi zikajirejesha nyuma kwa kasi
ya ajabu, Nguzu akakumbuka jinsi alivyokutana
na Zubeda jijini Mwanza.
Akaukumbuka utambulisho wake wa kijivuni dhidi
ya Zubeda ambaye hakuwa na cheo chochote
wakati ule na hata jeshini alikuwa hapajui.
"Naitwa Martin, Konstebo Martin Nguzu!"
Tabasamu likamponyoka na kujikuta akipiga saluti
ya kihuni.
Akakiendea kitanda na kujirusha hapo kwa fujo
zote.
Kitanda kikahimili kishindo!
Na hapo kikaanza kuufyonza ule uchovu wote na
kuugeuza kuwa raha ya kipekee.
Usingizi ukampitia.....
_____
MAHAKAMA kuu ya Tanzania ilikuwa imesheheni
haswa, maaskari walikuwa wanafanya kazi ya
ziada kuwazuia watu waliozidi kumiminika pale
mahakamani.
Punde ikasikika amri ya kumaanisha kuwa jaji na
baraza zima la wazee lilikuwa linaingia pale
mahakamani.
Kimya kikuu kikatanda ikiwa ni ishara ya
kuheshimu mahakama.
Akiwa na pingu miguuni na mikononi kisha pingu
hizo za miguu na mikono zikaunganishwa na
mnyororo mgumu aliongozwa hadi katika
kizimba.
Alipofikishwa kizimbani akafunguliwa zile pingu,
akaingia akiwa huru kizimba kikafungwa.
Macho yake yaliyozama ndani na kuzidi
kuonekana kuwa ni makubwa yaligeuka huku na
kule, safari hii hakuwa na uoga tena alikuwa
ameikubali hali halisi.
Macho yake yakatua katika kiti alichokuwa
ameketi mama yake aliyepooza upande mmoja.
Licha ya kwamba alikuwa amelia sana hadi
machozi kumkauka aliweza kuhisi machozi ya
moyoni yakimlowanisha.
Wakagonganisha macho yao, akamwona mama
yake akizungumza maneno yasiyoweza kusikika
hata kidogo huku machozi yakimtoka kwa wingi.
Aliamini kuwa mama yake alikuwa akimwombea
kwa Mungu ili kesi ile ipate muujiza wa yeye
kushinda.
Uchungu uliomshika alitamani angepewa walau
nafasi moja tu ya upendeleo naweze
kuzungumza na mama yake, amkumbatie na
kumfariji.
Jicho lile likaendelea kubarizi pale ndani ili
aweze kuwaona watu wengine ambao huenda
anawajua.
"Marafiki hawana maana!" Alijisemea baada ya
kuhakikisha kuwa hakuna rafiki yake hata mmoja
aliyefika mahakamani hapo.
"Kwa hiyo wameogopa kuwa nitawachoma ama?"
alijiuliza.
Hakupata muda wa kujiuliza zaidi wakati jicho
lake likitua katika kiti kingine upande wa kushoto.
Macho yakagongana tena na huyu mkaaji wa kiti
hicho.
Zubeda!
Walitazamana kwa sekunde kadhaa kabla Martin
Nguzu hajakwepesha macho yake.
Hakutaka kumwangalia binti huyu aliyekonda
sana na kuonekana wazi alikuwa akitawaliwa na
uchungu mkubwa.
Alipomaliza kuzungusha macho yake akamwona
jaji akitoa ruhusa ya mwendesha mashtaka
kumuuliza maswali mshtakiwa.
Maswali yalikuwa magumu sana, akayajibu kadri
alivyoweza. Mengi alikuwa ameyasahau kabisa.
Miaka sita mahabusu bila kesi kusikilizwa,
angekumbuka nini sasa.
Wakati wote huu alikuwa akishangaa kumwona
wakili kwa ajili ya kumtetea.
"Lakini nilimkataza mama kuhangaika kuweka
wakili." Martin Nguzu alijiuliza huku akitikisa
kichwa chake kama namna ya kusikitika.
Akakiri kuwa katika ulimwengu huu mzazi ni
mzazi lakini mama ni bora zaidi kuliko baba.
Mama anaumia sana akimwona mwanaye katika
wakati mgumu wakati baba huhesabu ugumu ule
kama changamoto na kusema 'kijana wangu
amekua na atatatua changamoto hizo' mama
huinama chini na kusema 'mtoto wangu
anateseka'
Ni hii tofauti aliikiri katika kesi yake hii. Mama
mzazi aliyepooza mwili alikuwa mahakamani
kushuhudia kile kiumbe alichokileta duniani
baada ya suluba ya miezi tisa, kisha kuhangaika
katika malezi.
Hakujali kupooza kwake, hakujali kuwa
yawezekana mwanaye akahukumiwa kifungo cha
maisha gerezani ama kunyongwa kabisa kwa
jinsi kesi ilivyokuwa.
Alichokifuata pale ni kumwona mwanaye kwa
jicho lake mwenyewe. Kama alivyomuona wakati
amemzaa, alihitaji kumwona tena katika ugumu
huu, ugumu wa kukondeana kwa sababu ya
mateso na lishe duni, ugumu wa kuwaza kufia
jela.
Mama alibaki kuwa shuhuda wa mwisho!
Ni nani kama mama kwani?
Wakili alisimama na kutema vifungu vya sheria ili
kumnusuru Martin Nguzu kutoka katika janga lile.
Alionekana kuijua vyema sheria lakini upande wa
mashtaka ulionekana kuwa imara zaidi, sura
nyingi zilitawaliwa na hasira kali. Hasira hii
iliboreshwa zaidi na mavazi yao, walifanania na
kundi la mafia ambalo limemshukia mwenzao
baada ya kuwasaliti na sasa wanataka kumpa
adhabu ya kumzika huku akiwa hai akaupiganie
uhai wake akiwa chini ya ardhi.
Nguzu akamgeukia jaji ambaye alionekana
mwingi wa chuki kuliko haki.
Jaji alipounyanyua uso wake Nguzu akajikuta
anagundua kitu kipya kabisa. Ile sura ya jaji
haikuwa njgeni machoni mwake hata kidogo.
Hofu ikamjaa ya kutotendewa haki juu ya kesi ile
ambayo alitambua wazi kuwa ni vile tu amekosa
mashahidi lakini haikuwa ikimuhusu kabisa na
alitakiwa kuwa mtu huru.
Jaji yule akaanza kusoma vipengele kimoja baada
ya kingine kwa utulivu sana.
Ni kama aliyeelekea kutoa hukumu, hii
ilimshangaza sana Martin.
Hukumu inatoka vipi kirejereja hivi bila kesi ile
kupewa muda wa baraza la wazee kuipitia na
kutoa mitazamo yao.
Jaji alisoma taratibu huku kila mahali akijaribu
kumbana Nguzu.
Na hatimaye kauli ikamtoka.
"UTANYONGWA MPAKA UFE"
Mungu wangu! Nguzu akamwona mama yake
mzazi akitua chini kama mzigo, watu
wakakimbilia alipokuwa ili kumwokoa.
Palepale akawaona askari wanne wenye
ghadhabu wakisogea katika kile kizimba na pingu
kwa ajiri ya kumchukua na kumpeleka katika
mahabusu ya mahakama kabla hawajampeleka
gereza la Ukonga.
Gereza pekee ambalo washtakiwa
waliohukumiwa kunyongwa mpaka wafe
huhifadhiwa huko mpaka siku ya hukumu yao.
Kuwaona watu wale kukamchanganya Nguzu, na
jaji alikuwa amefunga mjadala tayari.
Nguzu akaona haiwezekani, akawahi kujirusha
akaidaka silaha ya askari mmoja na mara moja
akaielekeza alipokuwa yule jaji.
Jaji akakodoa macho yake alipojikuta anatazama
ana kwa ana na bunduki iliyoshikwa na mtu
asiyekuwa na masihara hata chembe.
Akafyatua risasi kiufundi lakini yule jaji akawahi
kujificha chini ya meza.
Na hapohapo Nguzu akaisikia sauti ya kike
ikimpigia kelele kumtahadhalisha.
Ilikuwa sauti ya Zubeda!
Akageuka na kukuta amechelewa tayari, bunduki
nyingine ilikuwa inaelekea kufyatuliwa ili yeye
adhurike.
Ilielekezwa kifuani pake.
Akajikuta anapiga mayowe ya hofu huku akikiziba
kifua chake kwa mikono yake.
Bunduki ikacheua.
"Mamaaaa nakufaaa!" alipiga kelele kubwa sana
na hapo akajikuta akibiringita kama chaguo lake
la mwisho.
Akashangaa kujikuta anaelea hewani. Akaanza
kutapatapa akirusha miguu huku na kule.
Hatimaye akasimama wima tena.
Hakuwa mahakamani! alikuwa amesimama katika
kitanda huku akiwa amejifumbata mikono yake
katika kifua chake.
Ndoto!
Jasho lilikuwa linamwagika vibaya mno, bado
moyo ulikuwa unapiga kama unaotaka kutoka nje
ya kifua chake.
Alikuja kutulia baada ya dakika kumi na hapo
ndipo akakiri kuwa ile ilikuwa ni ndoto lakini
ndoto ya ajabu sana.
"Yule jaji yule! Yule jaji ni nani!? Jaji, jaji...."
Nguzu alibaki kusema kama ambaye anajaribu
kulazimisha kung'amua vitu kutoka katika ile
ndoto ya ajabu ambayo hakutaka kuamini eti
ilikuwa ndoto ya kawaida.
Alihisi yule ni babu yake anasema naye. Hofu
ikatanda alipokumbuka kuwa alihukumiwa
kunyongwa katika ndoto yake.
Hofu ya kifo ikamjaa, akaanza kuhofia uwepo
wake katika jiji la Dar es salaam.
Jiji ambalo ipo ile mahakama ya ndotoni na pia
lile gereza wanalohifadhiwa wafungwa wa
adhabu ya kunyongwa mpaka kufa.
Hiki nini? alijiuliza.
Bado hofu iliishi naye, akamkumbuka mama yake
alivyokuwa akimlilia na hata alivyoanguka baada
ya hukumu ile kutolewa.
Hofu ya kifo ikiwa haijaisha ikapanda hofu
nyingine.
Hofu ya kumpoteza mama yake mzazi pindi
atakaposhuhudia matatizo yakimpata.
Nguzu akakiri kuwa huu mpambano ulikuwa maji
ya shingo kwake naye alikuwa hajui kuogelea
vyema. Akaamini kuwa alikuwa anahitaji watu
watakaosimama pamoja naye.
Kwa mara nyingine tena jina Zubeda
likakiandama kichwa chake.
"Kwanini Zubeda?" alijikuta katika swali hili.
Hisia mbili zikaanza kupambana, mojawapo
ilikuwa hisia za mapenzi. Nguzu akakiri kuwa
alikuwa akihangaishwa na jina Zubeda kwa
sababu tu aliwahi kumpa burudani ambayo
ilikatishwa ghafla bila kufika ukingoni.
Pili alihisi kuwa anahitaji kupata msaidizi na
msaidizi wa kweli katika vita hii ni koplo Zubeda.
Kujua hisia ipi ni ya kweli nd'o ukawa mtihani
mzito.
"Ngoswe penzi kitovu cha uzembe" Usingizi
ulimkuta Nguzu akiwa katika uchambuzi hafifu
wa kitabu hiki maarufu , alianza kwa kumpa
kongole mwandishi Edwin Semzaba kwa kuandika
kitabu hiki, kisha akahamia kwa Ngoswe na
Mazoea na hadi anasinzia alikuwa amefikia
mahali ambapo Mazoea ameanza kuzoeana na
Ngoswe! Hii ni baada ya Ngoswe kumuhadaa
kuwa atamtorosha waende wote mjini......
Alisinzia akiwa anatabasamu, bila shaka ni vile
visa vya Ngoswe vilimpa tabasamu.
 
SEHEMU YA KUMI NA SABA
ASUBUHI ilimkuta konstebo Martin Nguzu katika
ofisi ya gazeti mojawapo kati ya yale
yaliyoandika habari ya kifo chake na kisha
kusemekana aliyeandika ni 'mwandishi wetu.
Kama ilivyomkera inspekta Kobo na kujikuta
akiponyokwa na matusi ya kiitaliano, kwa Nguzu
ilikuwa vilevile lakini hakuwahi hata siku moja
kuota ndoto za kiitaliano.
Yeye aliponyokwa na matusi mfululizo ya
kisukuma.
Lakini hakuishia kutukana tu, aliamua kupiga
hatua na aliamini hatua hii inaweza kuwa ya
muhimu zaidi kumfikisha katika hatua nyingine.
Akalisoma gazeti lile na kuyapata mawasiliano ya
muhariri mkuu wa gazeti hilo.
"Huyu jamaa lazima anawajua waandishi wake
wote, wenye majina na wasiokuwa na majina
wanaojiita 'mwandishi wetu'. Atawataja ama
atakula maumivu yao..." Alizungumza konstebo
wakati akizungusha macho yake huku na kule
kabla hajazama ndani ya ile ofisi.
Awali alipanga kwanza kumjua sura huyu bwana
na kisha ajiweke katika lindo zuri aweze kuijua
gari yake.
Baada ya kujua hayo angeachana naye na kisha
kumpangia siku ya shambulizi.
Alijua kuwa amezisahau taarifa zile tayari, na
hata hao akina'mwandishi wetu' walikuwa
wanaendelea na maisha yao mengine.
Mambo yakaenda tofauti, Nguzu akiwa
amejivesha miwani ya jua katika uso wake huku
akiziachia nywele zake wazi kwa maksudi kabisa.
Hazikufanania na nywele za askari, hasahasa wa
cheo cha konstebo.
Nguzu alikuwa katika hali ya utofauti.
Alianzia mapokezi na kuulizia ni wapi atampa
muhariri, katibu muhtasi akauliza ikiwa ana shida
binafsi ama ya kiofisi.
Maswali yao yaleyale kila siku! Nguzu alijisemea
kabla hajajibu, "Shida ya kiofisi dada."
"Ok! nyoosha moja kwa moja hadi katika ile
korido kisha pinda kushoto utaiona ofisi, keti
katika foleni subiri huduma."
Nguzu akainama chini kidogo huku akijishika
kifua chake kama ishara ya kushukuru.
Akatoweka!
Alimkuta bwana mmoja mwenye mvi akiwa
anangoja kuingia, akaketi pembeni yake.
Bwana mwenye mvi akaanzisha soga kuhusu
siasa mara ahamie katika mpira wa miguu, huku
ndipo alizidi kumpoteza Nguzu.
Ushirikiano wake pekee ukawa 'ndio' ama
kujichekesha.
Hatimaye mzee akaingia na kutoka baada ya
muda mfupi.
Bila shaka muhariri hakuwa tayari kusikiliza soga
nyingi kutoka kwa yule bwana.
Ikawa zamu ya Nguzu.
Hofu ikamwingia hakutambua kama yupo sahihi
katika hatua ile ama ameitupa karata yake
vibaya.
Akaufungua mlango na kuingia ndani huku
akitambua kuwa yeyote yule anaweza kustaajabu
kuhusu ile miwani lakini alifurahi kwa sababu ni
watanzania wachache sana anaweza kukuona
haupo sawa katika jambo fulani naye akawa
kimya asikwambie badala yake anamweleza
rafiki yake kisha wanacheka!
Hee! Watanzania?! Tusaidiane kujishangaa.
Kweli! hakuna aliyemuuliza.
"Karibu!" Sauti nyembamba lakini ya kiume
ilimkaribisha huku mikono ikimwonyesha mahali
pa kuketi.
Martin akaketi.
"Naitwa Sebastian! natokea Temeke Dar es
salaam." Alianza kujitambulisha.
Muhariri hakuonyesha kujali juu ya lile jina,
Nguzu akaendelea.
Sasa akayafungua magazeti kadhaa aliyokuwa
ameyashika mkononi akayatua mezani.
"Nakusikiliza bro.." Sauti ile iliyotawaliwa na
kiburi cha kuwa muhariri ilizungumza.
"Nilikuwa nataka kuuliza..."
"Ulikuwa unataka ama nd'o unataka kuuliza
mkuu?!" Muhariri akamuwahi Nguzu.
Nguzu akafadhaika na kuamua kutuliza akili yake,
tayari alishagundua kuwa alikuwa anakosa
kujiamini.
Akajipa sekunde kadhaa akaingia tena
kushambulia.
"Nauliza, hizi habari ambazo anaandika
mwandishi wetu,ni nani anaziandika na kwa nini
asijitambulishe kwa majina yake." Akaweka kituo.
"Samahani umeuliza ama umetoa lalamiko!"
Muhariri mwenye nyodo akazungumza, sasa
aliachana na kazi alizokuwa anafanya
akamtazama Nguzu huku akiyabetua mabega
yake.
"Nimeuliza."
"Ni utaratibu wa kiofisi. Ukihitaji ubadilishwe
utapaswa kuandika barua na kuiweka kuleee
kwenye sanduku la maoni. Sijui kuna la ziada
lililokutoa Temeke bwana.... bwana..." Akalisahau
jina lake na kulipuuzia.
Konstebo Martin Nguzu akanywea na kujiona
anazidiwa karata hivihivi mchana kweupe.
Akapaniki!
Akasimama wima, akawa anayetafuta neno la
kuzungumza linakikataa kinywa linarudi kichwani.
Akaona haifai kuendelea kusimama hivyohivyo.
"Huyu aliyeandika hii habari ni nani?" Akafoka.
Bado alikuwa wima.
Muhariri hakuligusa lile gazeti badala yake
akainyoosha shingo yake na kuona nini
anaonyeshwa.
Akakutanisha macho yake na habari juu ya kifo
cha Nguzu na kuhusishwa sababu za kimapenzi
na mengineyo.
Akajikuta anarudi nyuma kwa kasi, uso wake
ukiitangaza wasiwasi yake.
Akaishika simu na kutaka kubofya nambari
kadhaa, palepale Nguzu akauwahi ule mkono na
kuugandamiza.
Kisha ili kuimarisha usalama akachomoa kisu
kikubwa kutoka katika ficho lake.
"Huwa ninaua bila taarifa maalumu, sipendelei
ufe hivyo. Jibu swali langu." Hakuonekana
kuonyesha mzaha.
Muhariri akalitambua hilo.
"Sijaandika mimi."
"Mwandishi wetu ni nani?"
"Mwandishi wetu... sim... simj.."
Ngumi kali ikatua katika shingo ya muhariri.
Ilikuwa ngumi maalumu kwa ajili ya kumzuia yule
mwanadamu anayependa kuongea kwa sauti ya
juu, kumpunguza uwezo wa kupiga kelele na
kujikuta akinong'ona.
Nguzu alimwacha akihangaika pale akauendea
mlango na kuufunga!
"Simu yako ya mkononi..." Alisema kisha
akautega mkono wake. Muhariri akaikabidhi huku
akilia kwa sauti yake ile nyembamba ambayo
ngumi kali ilizidisha ule wembamba na kujikuta
akigumia kama mtoto wa kike.
Nguzu aliipekua ile simu upesi upesi katika
sehemu za jumbe mbalimbali, hakupata ujumbe
wa kumvutia.
"Unapendelea kufia ofisini ama nyumbani
kwako?"
"Si... aahm! nisamehe si... nitasema lolote
utakalo."
"Unanijua mimi?"
"Sikujui."
"Ni nani huyu mwandishi wetu na anapatikana
wapi?"
"Niliandika mimi... lakini hata mimi nilipewa."
"Nikilize we fala.... ndoto yangu moja ambayo
nahitajin kuitimiza ni siku moja nimuue mtu
akiwa ofisini nimkatekate nimtie kwenye mfuko
wa rambo, kisha nitokea na ule mfuko niingie nao
katika daladala niutelekeze huko. Vyombo vya
habari vishindwe kuelewa vitaandika nini kuhusu
kifo hicho...... Nina hasira ya kutimiza ndoto
zangu. Nakupa nafasi ya mwisho kujieleza
ukitetereka natimiza ndoto yangu. Nakuhakikishia
kuwa sitaacha walau tone la damu humu ndani
kwa ajili ya wapelelezi." Nguzu alizungumza huku
akiwa amemkazia macho muhariri.
Kijasho kikamwagika...
Akatapika kila alichokuwa anakijua katika ile
habari iliyoandikwa na 'mwandishi wetu'.
_____
JAMBO la kwanza lililokituliza kichwa cha Martin
Nguzu ni juu ya inspekta Kobo.
Nguzu alistaajabu asimini hata kidogo kuwa
aliachoelezwa kipo kama kilivyo. Licha ya kukiri
kuwa yule muhariri alikuwa 'chamtoto' sana na
asingeweza kuficha lolote kwa kitisho
alichompatia lakini bado hakutaka kumpatiliza na
kumwamini kwa asilimia zote.
Nguzu alitoka pale moja kwa moja akisimamia
wazo lake kuwa kwa namna yoyote ile ni lazima
afike nyumbani kwa Koplo Zubeda, alimini kuwa
ni huku ambapo angeweza kuupata mwanga zaidi
katika hatua zake.
Alikiri kuwa kuonekana kwake mbele ya Zubeda
kutazua kizaazaa cha aina yake ambacho
kinaweza kusababisha majirani wakajazana
kutaka kujua nini kinatokea.
Nguzu akajipa tahadhari kubwa sana kuwa ni
lazima umakini utangulie mbele kuliko kiherehere
cha kutaka kukutana na Zubeda ambaye
kichwani anaamini Nguzu ameuwawa.
Ili kuondoa macho mengi kumfuatilia juu ya
alichokuwa anahitaji kufanya Nguzu akaamua
kufanya uvamizi wake mchana kweupe.
Alilipenda giza lakini alijua linavutia wengi
sana....
Akauchagua mchana kwenda nyumbani kwa
Zubeda.
Akajiapiza kuwa Zubeda akionyesha dalili zozote
za kuwa upande usiokuwa wake basi hatasita
kumshukia kama mwewe anavyomshukia
kifaranga na kumwacha mamaye akipiga kelele
asiweze kutoa msaada.
Majira ya saa nane mchana alikuwa analitazama
geti la kuingilia nyumbani kwa Zubeda.
Hali ya ukimya ilitawala sana, akategea mpaka
alipowaona wanaume wawili wakipita kuelekea
njia ile naye akaunga tela ili asionekane kama
anajihusisha kwa lolote na nyumba ile.
Akapita na kuangaza huku akiulazimisha ule
ukimya umwingie akilini na kumpatia jawabu la ni
kitu gani kinaendelea.
Kimya kilimtatanisha!
Si kwamba hapajawahi kuwa kimya ama huwa ni
sehemu yenye kelele za kutisha, ila ni mwili
uligoma kuupokea ukimya ule katika namna ya
kawaida.
Alilipita geti lile kwa mara ya kwanza huku
akifanikiwa kujifunza kuhusu mazingira yale
upesiupesi, mara ya pili aliporudi alilifikia geti na
kubisha hodi.
Mlinzi akajitokeza na kufungua.
Hakusema kitu akabaki kumsikiliza Nguzu
mwenye miwani nyeusi.
"Ni mgeni wa Zubeda! Koplo Zubeda.." Nguzu
akajitambulisha huku akigundua kuwa huyu mlinzi
ni mpya sio yule wa awali.
Akasaili eneo lililomzunguka yule mlinzi na
kugundua kuwa hata silaha imebadilika.
Sub Machine gun!
Akaduwaa, kunani mpaka Zubeda aamue kuajiri
mlinzi ambaye ana utaalamu wa kutumia silaha
hii tena mchana kweupe.
"Sub machine gun!" akajikuta anajisemea
kichwani kwake, kana kwamba ni mashairi ya
wimbo anaotaka kuukariri.
"Wewe ni nani?" Mlinzi akauliza.
Polisi! Machale yakamcheza Nguzu kwa jinsi mtu
yule alivyouliza lile swali, hakuwa mlinzi wa
kawaida huyu alikuwa polisi.
"Naitwa Sebastian Madeko. Ni jirani..."
alijitambulisha.
"Nisubiri hapa!" mlinzi alimwamrisha kisha
akapiga hatua kwenda katika mlango wa nyumba
ya Zubeda.
Nguzu akamwacha hadi alipoufikia mlango akawa
makini kumtazama atazungumza na nani.....
Alishatambua kuwa hali haikuwa shwari, ni aidha
Zubeda alikuwa matatani ama la alikuwa analeta
matata.
Mlinzi akarejea baada ya dakika mbili.
"Twende!" akamwambia huku akimkazia macho.
Nguzu hakutaka kuionyesha hofu yake badala
yake alijiandaa kwa mapambano.
Mlinzi akalifunga geti vyema kabisa kabla ya
kumwongoza Nguzu kuelekea katika mlango wa
kuingilia nyumba ya Zubeda.
Wakaufikia mlango, Nguzu hakuendelea kuwa
kondoo.
Katika mlango ule wa kioo, aliweza kumsoma
yule mlinzi, kuna shambulizi alijiandaa kumkumba
nalo kabla hawajaingia ndani ama kuishia
palepale.
Nguzu akawa sekunde moja mbele, akatokwa na
teke maarufu kwa jina la 'Shukrani ya punda'.
Lilikuwa teke la nyuma!
Mlinzi ambaye hakutarajia pigo lile akapepesuka
mpaka chini, alimanusura bunduki yake imuue
yeye mwenyewe kwa kumchoma kooni.
Macho yakamtoka pima!
Nguzu akawahi kukitoa kisu chake na kujitoa
mpaka pale chini kisha akadidimiza katika mkono
wa mlinzi.
Akatokwa na yowe kubwa kwa muda mfupi,
Nguzu akachomoa ile ngumi yake ya kupunguza
sauti.
Ikamwingia yule bwana na palepale akaiondoa
miwani yake.
"Naitwa Martin, Konstebo Martin. Sikijui kifo
bado, ukifanya mfano wa kunidanganya utakijua
kifo kabla yangu." Alifoka Nguzu huku midomo
yake ikitetemeka.
Mlinzi hakuamini alichokuwa anakiona, alijiona
akiwa anatazamana na mzimu wa Nguzu ambaye
anasadikika kuwa ni mfu.
"Ni nani amekuagiza kulinda eneo hili na ni nani
yupo ndani ya nyumba hii zaidi yako?"
Mlinzi akajifanya hajasikia.
Nguzu akatokwa na ngumi kali hii ikatua katika
sikio la kuume la mlinzi.
Hakuweza kutokwa na yowe kubwa, damu
ikaanza kumtoka.
Nguzu akatokwa na tabasamu wakati akimuuliza
kuwa ni kipi chepesi kusikia swali ama ngumi?
Mlinzi yule ngangari akaanza kutokwa na kamasi.
Bwege alikuwa amepatikana!
"Nipo mwenyewe.... nipo mwenyewe usiniue."
"Amekuagiza nani?"
"Inspekta.... Inspekta Kobo." Alijibu kwa utulivu.
Nguzu akaishiwa hamu! hakutarajia jibu lile.
Huu ukawa ni mkanganyiko mpya kutoka katika
majibu ya muhariri na huyu bwana mlinzi.
____MUHARIRI alitoa maelezo gani?
 
SEHEMU YA KUMI NA NANE
"Nipo mwenyewe.... nipo mwenyewe usiniue."
"Amekuagiza nani?"
"Inspekta.... Inspekta Kobo." Alijibu kwa utulivu.
Nguzu akaishiwa hamu! hakutarajia jibu lile.
Huu ukawa ni mkanganyiko mpya kutoka katika
majibu ya muhariri na huyu bwana mlinzi.
Akamtazama kwa jicho lililotangaza chuki ya
waziwazi kabla hajamtundika swali jingine katika
namna ya kisharishari.
"Muonekano wake upoje huyo bwana wa kuitwa
Kobo.
Huku akikumbuka kuwa akijifanya hajasikia swali
lile basi kifuatacho ni kubamizwa ngumi na
kuulizwa swali la kukera safari hii aliwahi kujibu.
Akauelezea wajihi wa inspekta Kobo.
Nywele ndefu nyeupe zinazojaribu kuuficha
uwalaza wake, ndevu fupi zenye uwiano sawia na
nywele zake katika rangi.
Umri wake ukichezea miaka sitini hadi sitini na
nane.
Konstebo Nguzu akachoka upya!
Huyu hakuwa inspekta Kobo aliyekuwa
akimfahamu yeye.
Lakini kilichomjaza nguvu upya ni ule utambulisho
ulikaribiana na ule ambao alielezwa na muhariri
wa gazeti baada ya kumbana vizuri.
Konstebo akiwa anajiandaa kumuuliza tena yule
bwana swali jingine, akafanya kosa kuitazama
anga kama anayefikiria aulize kwa namna gani
nyingine ili apate mwanga mkali anaouhitaji
katika giza lile nene.
Yule muhanga alitokwa na teke kali likatua
vyema katikati ya mapaja ya Nguzu, teke lile
likamfanya Nguzu ainame.
Naam! adui alihitaji hivyo.
Uso ukawa jirani naye, akatokwa na teke kali
sana lililoongezewa uzito na kiatu kigumu
alichokuwa amevaa.
Uzito huu ukatua barabara katika uso wa Nguzu.
Ilikuwa mchana ghafla ukawa usiku kwa Nguzu
pekee. Pigo lile lilimsukuma mpaka mlangoni.
Akaingia na ule mlango, kiuno kikapokea
maumivu stahiki.
Konstebo Nguzu akajaribu kurejea katika
mapambano lakini giza lilikuwa linamuharibia,
hakumwona adui yake. Sanjari na hilo alikuwa
akipambana kuilamba damu iliyokuwa inamtoka
puani.
Adui alikuwa amechachamaa.
Alijaribu kutapatapa lakini adui hakumwachia
nafasi, ni kama alimaanisha kutaka kuondoka na
roho ya Nguzu na hakuhitaji kumuuliza swali
lolote lile.
Nguzu alibaki kuikumbatia sakafu wakati mateke
yasiyokuja kimpangilio yakimwandama.
Pumzi zikaanza kumsaliti, na hapa akajaribu kwa
mara ya mwisho kuusaka uhai wake ambao yule
bwana alitaka kumpokonya angali hajamaliza
shughuli yake.
Akaituliza akili katika maumivu. Kitu ambacho
wanadamu wachache sana wanaweza.
Kasumba ya mwanadamu akisikia mlio wa risasi
anaanza kukimbia asijue kama anaikimbia ama
anaikimbilia risasi.
Nguzu akautafuta uelekeo wa yale mateke makali
yaliyomaanisha kuua. Akaupata uelekeo wa
mpigaji, na jinsia livyokuwa anapiga hovyo
akatambua bayana kuwa anatumia zaidi hasira
na hapohapo anapoteza muhimili wa umakini.
Teke lilipomwingia akajitutumua na kusimama
wima, na kujirusha kulekule katika uelekeo wa
adui yake.
Karata sahihi!
Akamsomba yule bwana na kutua naye chini.
Majogoo mawili yaliyochoka haswa yalikuwa
yamelaliana.
Na heri tele kwa jogoo lililomlalia mwenzake.
Martin Nguzu alikuwa juu.
Hakuweza kurusha ngumi, kuchimba mikwara
wala lolote lililoonyesha umwamba. Wote
walikuwa wanahema juu juu.
Martin akapambana na kufanikiwa kuyafumbua
macho yake.
Likafumbuka jicho moja kwa shida sana.
Akamwona adui yake akiwa mdomo wazi,
anahema juu juu!
Akaiona shingo ikiwa wazi.
Akajitutumua akaifikia na kuikaba, anayekabwa
akaanza kurusha mikono kuzuia kitendo kile.
Hakika walikuwa wamechoka!
Vishindo vilisikika kwa mbali, Nguzu akahisi
hatari kubwa inakuja mbele yake.....
Uwezo wa kupambana kwa wakati ule
hakuwanao, kama huyu aliyechoka anashindwa
hata kummalizia vipi hao wanaokuja huku wakiwa
na nguvu mpya.
Akajigeuza na kutua chini kisha ukaanza
mpambano mpya wa kila mmoja kujaribu
kusimama.
Nguzu akajaribu akaanguka, mwenzake naye
yakamkuta yaleyale.
Nguzu akakerwa na hali hii ya kujikuta mnyonge
angali oparesheni ikiwa mwanzo kabisa.
Hali ikazidi kuwa mbaya alipomwona yule mlinzi
akifanikiwa kusimama wima, akayafuatilia macho
yake yakiwa yanaangaza huku na kule hatimaye
kwa pamoja wakajikuta wakiitazama bastola
iliyokuwa imetulia sakafuni ikisubiri yeyote ajuaye
kuitumia na aitumie.
Nguzu alitamani nguvu zimjae na akimbilie kule
kuiwahi lakini hakuwa na nguvu za kutosha na
alikuwa katika maumivu bado.
Kifo kikanukia katika namna ya kukera. Yule
mlinzi akaanza kujivuta kwa kasi kuifuata bastola
ile, Nguzu akaanza kujiona yu mjinga kukisubiri
kifo chake bila dalili zozote za kupambana.
Akapitiwa na fikra za harakaharaka juu ya hayati
babu yake, aliyemrithisha jina hilo lenye maana
kubwa.
Nguzu 'chikichia' hapa hapafai tena! alijionya
huku akiangaza lilipo kimbilio.
Hakuliona kimbilio kabla hajamwona yule mlinzi
akigeuka huku akiwa na bastola mkononi.
Akafyatua hovyo kwa mara ya kwanza, bastola
isiyokuwa katika kiwambo cha kuzuia sauti ikatoa
mlio mkubwa.
Mlio huu ukamuhamasisha Nguzu kujitutumua na
kukimbia.
Alikimbia ndani ya ile nyumba huku akiamini
kuwa ataukuta wazi ule mlango aliokuwa
anaufahamu ili aweze kutokea upande mwingine.
Hofu ya kifo ilizidi kujenganaye urafiki,
alijitutumua akaufikia mlango.
Mungu wangu!! ulikuwa umefungwa kwa kutumia
mnyororo.
Hakuwahi kuiona hali kama hii hapo kabla. Huku
nyuma akawa anamsikia yule mlinzi akitoa
matusi yote huku kila mara akimaanisha kuwa
iwe isiwe lazima amuue.
Nakufa! Hatimaye Nguzu akakiri, lakini hakubaki
kibwegebwege afe bila kupambana.
Akausukuma mlango wa chumba cha Zubeda
ambacho enzi zile alikuwa akiingia huku
amebebwa mgongoni na koplo yule mwenye asili
ya Tanga lakini akiishi zaidi Mwanza.
Sasa aliingia katika chumba hiki huku akiwa
anasota, jicho moja likiwa linaona kwa tabu huku
lile jingine likiwa limefumba kabisa.
Hamadi! mlango ulikuwa umezuiwa na kitu kwa
ndani.
Hofu ya kichwa chake kusambaratishwa na risasi
ikamfanya Nguzu ajitupe mzima mzima na
kufanikiwa kukisogeza kizingiti.
Akajikuta ndani ya chumba.
Sauti ya yule mlinzi nayo ikazidi kutapatapa
ikitishia kuua.
Chumba kilimkaribisha Nguzu katika hali ya
utulivu, utulivu ule ulimtisha zaidi, akajaribu
kufikiri ni wapi atajificha ili kumkwepa mshika
bunduki.
Uvunguni! hili lilikuwa wazo la kizembe lakini
walau naye aliwaza.
Akaanza kujitutumua aingie uvunguni, akaanza
kujivuta kwa kutumia tumbo.
Hakuzama sana kabla hajabamizwa ghafla na kitu
kigumu katika paji la uso wake.
Ile anajaribu kujiweka sawa akatandikwa teke kali
usoni, akajikuta yungali nje ya ule uvungu huku
akiwa nusu hai nusu mfu.
Alikuwa amepiga magoti damu zikimvuja.
Hazikupita sekunde nyingi kiumbe akauona
mdomo wa bunduki ukitangulia kutoka katika ule
uvungu.
Nipokee baba nakufa mimi Nguzu! alijifanyia dua
upesiupesi.
Na hapo mlango ukasukumwa akamsikia yule
mlinzi akiendelea kuropoka.
Nguzu akatambua kuwa nyuma yake palikuwa na
mtutu na pia mbele yake alijionea waziwazi.
Swali likabaki juu ya nani atakayekuwa wa
kwanza kufyatua ili auondoe uhai wake.
Yule wa uvunguni akawa wa kwanza kufyatua.
Risasi ikapenya jirani kabisa na sikio la Nguzu,
ikafanya mlio kama wa nyuki mwenye hasira.
Kisha kishindo kikafuatia, Nguzu akatua chini
akiangukia tumbo.
Kichwa chake kikawa jirani kabisa na ule mdomo
wa bunduki iliyotokea uvunguni.
Na hapo akaviringika na kutoa uvunguni
mshambuliaji yule aliyemkosa Nguzu maksudi na
kumlipua aliyekuwa nyuma yake.
"Nilijua kuwa umekufa duniani, lakini si katika
moyo wangu. Nikaamini tutakutana mbele ya
haki, sijui kama ni mahali sahihi tulipokutana
Martin, konstebo Martin Nguzu." Sauti imara ya
kike ilizungumza.
Nguzu hakuhitaji macho yake katika hili, masikio
pekee yalitosha kutambua kila kitu. Hatimaye
kinywa kizito kikajitutumua na kuzungumza.
"Koplo Zuu!"
"Nihakikishie kuwa sitakiwi kukulipua kwa sababu
u mmoja kati yao..."
"Si..sijui kitu hapa. Usilipue koplo." Alisihi Nguzu.
Zubeda akamdaka na kumsimamisha. Nguzu
akakosa muhimili akataka kuanguka, Zubeda
akatega mgongo wake kama alivyokuwa akiutega
zama zao za furaha.
Nguzu akatua juu yake.
Zubeda akaanza kupiga hatua kutafuta uelekeo,
Nguzu akiwa anakoroma.
Hali yake ilikuwa mbaya sana. Zubeda naye
alikuwa anajitutumua, mguu wake mmoja ulikuwa
haujaimarika..
Zubeda akiwa ndiye anayetegemewa alijaribu
kufikiria juu ya uwepo wao pale ndani. Hapo
kabla alikuwa amefanikiwa kuua na kisha
kumpokonya bunduki mtu aliyewekwa kwa ajiri ya
kumlinda asiweze kuleta bughudha yoyote.
Walimpatiliza kwa sababu ya miguu yake kuwa
na mushkeli.
Dharau zao zikawafanya wapunguze ulinzi na
kumwacha mbabe mmoja.
Yakamtokea puani!
Wakati Zubeda akiendelea kufikiria ni nini
kilitokea hadi akabadilishiwa ulinzi ghafla,
kutokea ule ulinzi aliowekewa na inspekta Kobo
hadi ulinzi huu wa ajabuajabu. Akalishuhudia geti
likifunguliwa na gari ikaingia huku askari watano
waliovalia sare wakitangulia mbele.
Balaa!
Akajaribu kumshirikisha Nguzu aliyekuwa bado
hoi. Nguzu hakuwa na la kuchangia.
Askari yule imara ndani kwa ndani na legelege
kwa umbo la nje alitoweka mpaka chooni. Huku
aliweza kuona kila kitu kilivyokuwa kinaendelea
nje.
Alimtua Nguzu na kumsihi anywe maji
yanayotoka katika bomba ili aweze walau kupata
nguvu kiasi. Wakati huo akiendelea kuilazimisha
akili yake ifanye kazi kwa kasi zaidi kuhusu tukio
linalokuja mbele yao, alifahamu fika kuwa hakuna
namna ya kuwa salama angali mle ndani kuna
maiti mbili.
Kwa namna yoyote yeye na Nguzu watayamalizia
maisha yao gerezani.
Maji yalikuwa msaada mkubwa sana kwa Martin
Nguzu. Hayakumfanya kuwa imara sana lakini
walau macho yake yaliweza kuona na aliweza
kupumua vyema kwa sababu aliweza kuyaondoa
mabonge ya damu yaliyounda uzio mbele ya pua
zake na kumsababisha apumue kwa mdomo
badala ya kutumia pua.
"Martin, Martin!" Zubeda aliita kwa kunong'ona.
Konstebo Martin akaupokea wito ule kwa kutulia
akimsikiliza.
"Askari wote wanatuzingira." alimweleza kana
kwamba Nguzu alikuwa anafahamu tayari juu ya
uwepo wa ugeni ule..
"Akina nani? wako wapi?"
Zubeda hakumjibu badala yake alimsaidia
kunyanyuka na kisha akamwelekeza kila
alichokuwa akikiona kwa nje.
Walichoka!
____
BAADA ya kukataa kata kata kubadili maelezo
yake, amri ilitolewa ya kwenda kupekua nyumba
ya inspekta Kobo ili iweze kubainika kama anayo
mawasiliano yoyote aliyowahi kufanya na kikosi
cha majambazi kilichoinyanyasa Shinyanga kwa
wakati ule huku askari kadhaa wakiangushwa na
kupoteza maisha.
Msako wa kwanza haukuzaa matunda yoyote
waliyoyatarajia.
Walikata tamaa huku wakianza kuamini
yawezekana kuwa inspekta Kobo aidha hajuani
na lile kundi ama la ni mafia aliyefuzu mafunzo
yote stahiki.
Yaani hata umkate mguu akisema sijui ni sijui.
Anameza maneno yake na kuingia nayo
kaburini...
Wakiwa wanakaribia kuondoka, askari mmoja
akafika na kitu kipya.
Akamtupia swali Kobo.
"Hii nyumba unayoishi ni mali ya nani?"
"Binafsi." Alijibu kwa sauti iliyokata tamaa.
"Umeijenga mwaka gani na umeanza kuishi humu
lini?"
"Huu ni mwaka wa kumi sasa naishi humu."
Jibu lile likamfanya askari yule afanye tabasamu
hafifu kabla hajamtundika pagumu bila yeye
kujua.
"Umejenga nyumba nyingine tofauti na hii?"
"Hapana!"
"Mtu akifika hapa kukutafuta na asikupate je? ni
wapi zaidi anaweza kukupata?"
"Kazini kwangu."
Jibu la sasa likayafanya meno ya yule askari
yaonekane kwa sababu ya kicheko kidogo.
Na hapo akayabwaga makaratasi kadhaa mbele
ya maaskari wenzake na Kobo akayashuhudia.
Alikuwa ni mnyonge lakini haya yalimtia unyonge
zaidi.
Mikataba!
Mikataba baina yake na mmiliki wa nyumba
aliyokuwa akiishi hawara yake.
Koplo Zubeda!
Alitamani ardhi ifunguke atumbukie humo,
alijiona waziwazi kuwa alikuwa anaelekea
pabaya.
Kwanza alidanganya kuwa hana makazi mengine
zaidi ya hayo, pili mikataba yote aliiandikisha
kwa majina yake na si ya Zubeda.
Mkataba wa mwisho aliuandikisha miezi miwili tu
iliyopita.
Anakwepa vipi rungu la sheria?
Watamuhesabu kama mnyang'anyi ambaye analo
eneo la siri kwa ajiri ya kufanyia shughuli zake
haramu.
Inspekta Kobo akaumia zaidi kwa sababu alikuwa
anakwenda kumweka Koplo Zubeda na maaskari
aliowaweka kumlinda matatani.
Wote hawa watahesabika kuwa ni chama kimoja
cha kimafia na wataminywa kama alivyominywa
yeye hadi kufikia hapo alipo.
Akaunganisha meno yake kwa uchungu mkubwa.
"Tunaenda moja kwa moja hadi katika nyumba
hii. Ukithubutu kutudanganya utajutia uongo
wako" Akachimbwa mkwara, akamtazama yule
bwana kwa jicho kali, akajilaumu sana kwa
sababu alikuwa na pingu, vinginevyo angefanya
shambulizi kwake.
Hakupendelea masuala ya kuchimbwa mkwara!
Inspekta Kobo akawaelekeza nyumba ile
inapopatikana, na hata asingewaelekeza bado
kuna namba ya nyumba iliorodheshwa katika ile
mikataba.
Bila kusahau kiherehere cha mmiliki wa nyumba
ile kuweka nambari yake sahihi kabisa ya simu
ya mkononi na ile ya ofisi.
Wakatoweka kuelekea nyumbani kwa Zubeda!
__Wapi Juma Kiherehere?
 
SEHEMU YA KUMI NA TISA
Na hapo akayabwaga makaratasi kadhaa mbele ya
maaskari wenzake na Kobo akayashuhudia.
Alikuwa ni mnyonge lakini haya yalimtia unyonge
zaidi.
Mikataba!
Mikataba baina yake na mmiliki wa nyumba
aliyokuwa akiishi hawara yake.
Koplo Zubeda!
Alitamani ardhi ifunguke atumbukie humo,
alijiona waziwazi kuwa alikuwa anaelekea
pabaya.
Kwanza alidanganya kuwa hana makazi mengine
zaidi ya hayo, pili mikataba yote aliiandikisha kwa
majina yake na si ya Zubeda.
Mkataba wa mwisho aliuandikisha miezi miwili tu
iliyopita.
Anakwepa vipi rungu la sheria?
Watamuhesabu kama mnyang'anyi ambaye analo
eneo la siri kwa ajiri ya kufanyia shughuli zake
haramu.
Inspekta Kobo akaumia zaidi kwa sababu alikuwa
anakwenda kumweka Koplo Zubeda na maaskari
aliowaweka kumlinda matatani.
Wote hawa watahesabika kuwa ni chama kimoja
cha kimafia na wataminywa kama alivyominywa
yeye hadi kufikia hapo alipo.
Akaunganisha meno yake kwa uchungu mkubwa.
"Tunaenda moja kwa moja hadi katika nyumba hii.
Ukithubutu kutudanganya utajutia uongo wako"
Akachimbwa mkwara, akamtazama yule bwana kwa
jicho kali, akajilaumu sana kwa sababu alikuwa na
pingu, vinginevyo angefanya shambulizi kwake.
Hakupendelea masuala ya kuchimbwa mkwara!
Inspekta Kobo akawaelekeza nyumba ile
inapopatikana, na hata asingewaelekeza bado
kuna namba ya nyumba iliorodheshwa katika ile
mikataba.
Bila kusahau kiherehere cha mmiliki wa nyumba ile
kuweka nambari yake sahihi kabisa ya simu ya
mkononi na ile ya ofisi.
Wakatoweka kuelekea nyumbani kwa Zubeda!
____
ZUBEDA hakuamini macho yake pindi
alipomshuhudia inspekta Kobo akishushwa garini
huku akiwa hajiwezi walau kutembea, nguo yake
kwa mbali kabisa ilionekana kumpwaya, na ilikuwa
imefubaa huku mabakamabaka yaliyoashiria
kugandiana kwa damu yalionekana.
Donge la uchungu likamkaba kooni, akajikuta
yungali katika mfadhaiko mkubwa sana.
Hakujua ni kwanini Kobo yu katika hali ile lakini
kichwani aliitabiri kuwa haikuwa ya heri hata
kidogo.
"Martin...... Inspekta Kobo..." Alimwita kutoka
pale alipokuwa ameinama bafuni.
Martin akajikuta akisimama wima na hapo akawa
amejitonesha mbavu zilizokuwa katika maumivu
makali.
Hakujikunja tena, akanyoosha shingo akakiona
kile ambacho Zubeda alikuwa anakiona.
Mpango huu ulikuwa maridhawa kabisa.
"Hatuchomoki!" Zubeda alijikuta akitokwa na kauli
ile ya kukata tamaa.
Kauli ile haikuelea sana hewani kabla mlipuko
mkubwa haujasikika na palepale askari wawili
walio katika sare wakaanguka chini.
Mmoja aliyekuwa amemshika Kobo ili aweze
kutembea alimwachia na Kobo akatua chini
mzimamzima.
Akatulia!
Hapoikazuka vita mpya, Nguzu na Zubeda
wakashindwa kuelewa hii vita inahusisha pande
ngapi.
Wakati wanaamini kuwa ni pande mbili pekee sasa
wanashangaa kuwa wao hawahusishwi na wakati
huohuo vita inaendelea.
Milio ya risasi za kuviziana ikaendelea huku askari
wakipokea amri kalikali kutoka kwa kiongozi wao.
Mambo yalikuwa magumu haswa!
Asakari walikuwa wamepagawa, ni kama walikuwa
hawajatarajia upinzani wa aina ile kutoka katika
nyumba ile aliyokuwa akiishi Zubeda.
_______
HAKUWA katika mavazi yake yaliyowatisha wengi
pindi walipomuona, hakuwa katika kiti chake cha
kuzunguka huku akipokea taarifa zilizopaswa
kumfikia yeye na kisha kutoa maamuzi.
Hakuwa katika nafasi yake ya kuwasiliana na raisi
wa jamuhuri wa muungano.
Alikuwa katika fulana yake pamoja na bukta laini,
na alikuwa chumbani kwake.
Vyeo vyote aliamua kuviweka kando.
Alichoingia nacho pale chumbani ni thamani ya
urafiki.
Hakuwa na roho mbaya, na hilo alilitambua vyema
bali alikuwa ni mtu anayesimamia haki na usawa.
Ukimwona ana roho mbaya kwa sababu tu
amekushinda kwa kuusema ukweli basi alikuwa
tayari kuonekana hivyo.
Aliijua mipaka yake vyema, hakuwa shabiki wa
mateso wala vifo vya hovyohovyo.
Alikuwa na weledi wa kutosha na hii
haikuwashangaza wenzake baada ya kusikia jina
lake likitajwa kuwa atakuwa mkuu wa majeshi ya
polisi.
Hata yeye hakushangaa, maana hakupewa cheo
kile kwa bahati mbaya.
Alistahili!
Sasa alikuwa hayafikirii yote haya, alikuwa
akimfikiria Kobo, ambaye alitokea kuwa rafiki
yake sana mpaka mtafaruku ulivyokuja kuwaweka
mbali kidogo kisha madaraka yakahakikisha wapo
mbali kabisa.
Kwa kufumba ama kufumbua macho IGP hakuacha
kuiona sura ya Kobo ikiitaka huruma yake,
akayakumbuka maneno ya Kobo juu ya mkewe
ambaye yu katika kuzimia.
"Nampenda sana mke wangu, ninapaswa kumuomba
msamaha. Kama haitafaa mimi kubaki huru
nakusihi rafiki yangu na mkuu wangu nifanyie
upendeleo nisining'inie katika kitanzi kabla mke
wangu hajazinduka."
Maneno haya yalimuumiza mno, akajaribu
kuelekeza macho huku na kule ili asahau kuhusu
Kobo lakini akajikuta akilitazama tukio la Kobo
kujitoa muhanga na kumsukuma kando ili asipatwe
na risasi iliyomkusudia.
Akajikaza hisia zisimwendeshe lakini chozi
likamsaliti.
Akajikuta analia!
Akayakumbuka maneno makali ya Kobo juu yake
alipomwambia kuhusu pambazuko baya kupindukia.
"Jitazame yawezekana pambazuko hili
likakuandama wewe pindi utakapogundua kuwa
sikuwa nyuma ya maovu haya."
IGP akasimama na kujifuta machozi pamoja na
jasho lililoanza kumtoka.
Akachukua simu yake na kumpigia msaidizi wake,
ambaye pia alikuwa ni rafikii yake nje ya
madaraka hayo.
Akajaribu kumweleza kwa kifupi, akaeleweka na
hatimaye wakachukua maamuzi ya kutuma watu
watatu wa ziada katika tukio hili kutazama jinsi
linavyokwenda.
Walikuwa ni vijana wanaoaminika sana kiuwezo
katika mapambano na pia katika umakini.
Walau IGP aliweza kulala vyema baada ya kufanya
hatua za mwisho kabisa za kutambua ikiwa Kobo
anastahili jela ama la?
Majira ya saa kumi jioni alishtuliwa na simu yake
ya mkononi.
Ni nambari aliyompatia msaidizi wake ili lolote
litakalotokea waweze kupeana taarifa.
Akaipokea upesi ile simu.
"KIjana mmoja ameuwawa na mwingine
amejeruhiwa begani." Taarifa ile ilimtisha mno
IGP.
Alitambua kuwa jambo hili lina uzito lakini
hakukadiria uzito ule kufikia huku kwa vijana
ngangari kama wale kutetemeshwa.
Akamsihi aongeze vijana na amri iwe moja tu,
warejee na majibu.
"Kiongozi kuna kitu kingine cha ziada." Alisema
kisha akamwacha IGP apumue kidogo.
"Ile sauti uliyoniambia imesikika tena. 'SHUSHA
MBUYU KUNA NYOKA..."
"Ni sauti ya nani?" Aliuliza kwa utulivu wa hali ya
juu.
"Aliyeisikia ni marehemu tayari. Lakini ni mmoja
kati ya timu uliyoipa dhamana ya kwenda kuikagua
nyumba ya Kobo."
"Na ni nani anayeshambulia ikiwa sio hao
wapekuzi?"
"Kuna safu nyingine kutoka katika kona za
nyumba waliyoenda kuipekua. Kuna vita ya pande
zaidi ya mbili mkuu."
"Ongeza vijana, fanya wanane. Wahakikishe
wanaleta majibu."
"Sawa. Afande..." Alijibu na kukata simu.
Hali ilikuwa mbaya tayari.
_____
INSPEKTA KOBO alianguka mwili wote lakini
hakuzimika macho yake. Alitulia kama
aliyekwishapoteza uhai tayari.
Aliendelea kutazama mashambulizi yalivyokuwa ya
kutisha, kuna jambo alikuwa akilisoma.
Wapinzani waliokuwa wamejificha katika kuta na
dari walikuwa wakifanya mashambulizi ya akili
sana huku hawa waliomsindikiza kukagua nyumba
walikuwa wengi lakini bure kabisa.
Walikuwa ni watu wanaotii sheria tu, wakiambiwa
waachie risasi wanamimimina hovyo bila
kumaanisha kudhuru!
Akiwa palepale alizungusha macho yake huku na
kule, na mara akatua katika madirisha ya nyumba
ile.
Akaona kama kivuli kikivuka upesi kwa kuinama
chini.
Kivuli kile alikuwa amekizoea sana, kama
kisingekuwa chenyewe basi kingekuwa ni pacha ya
kile alichokizoea.
Zubeda! Inspekta akatokwa na jina lile huku
akiwa bado amenasa pale chini, kulia kwake
pakiwa na mwili wa askari aliyetokwa na uhai
tayari.
Kwa umakini wa hali ya juu akajisogeza mita
kadhaa taratibu hadi akawa jirani kabisa na yule
askari. Muda wote macho yake yaliwatazama wale
washambuliaji waliojificha.
Alishagundua tayari kuwa washambuliaji walikuwa
wanaye mdunguaji wao na alijua vyema kazi ya
kudungua maana alikuwa hakosi kila akishambulia.
Faida kuu kwa Kobo ni kwamba huo ulikuwa moja
kati ya mchezo wake uliompandisha cheo upesi na
mchezo huohuo ulikuwa umemuingiza matatani.
Shabaha!
Kobo akainyakua silaha ya askari mfu pale chini.
Akatabasamu baada ya kuitambua kuwa ni silaha
aipendayo.
Akatulia tena kama mfu huku akiangalia ni wapi
anapoweza kuanza kushambulia. Alitambuwa wazi
kuwa hawezi kushambulia kwa muda mrefu kabla
nguvu hazijamwisha na pia kuchabangwa risasi na
kupoteza maisha hivyo alihitaji akifanya
shambulizi liwe kubwa na lenye maana kubwa.
Akiwa bado katika kuliandaa shambulizi aliisikia
simu ya upepo jirani na lile gari waliloingia nalo
pale ikiunguruma maneno kadhaa ya kusihi.
Hakuwa na uhakika kama msikilizaji wa ile simu
aliamua tu asiijibu ama simu ilikuwa haina
msikilizaji.
"Shusha mbuyu kuna nyoka. Shusha sasa hivi ova!"
Sauti ile ilitokea nyuma ya gari ambalo lilikuwa
limeharibika vibaya kutokana na milipuko ya
risasi.
Mapigo ya moyo yakaongeza kasi, umakini
ukatoweka akataka kukurupuka lakini
alipokumbuka kuhusu 'sniper' aliyejificha mahakli
fulani aliendelea kutulia.
Punde baada ya amri ile kutoka mita kadhaa hadi
kuufikia ukuta mrefu kiasi ulioizunguka nyumba
ile akasikia kishindo kikali, na kisha kikasikika
kilio.
Kuna mwanaume alikuwa amemezeshwa risasi
tayari. Alikisia
Huyu ni nani? alijiuliza kisha akajigeuza na
kuilalia ile bunduki na kuendelea kubaki kana
kwamba hana uhai.
Alikuwa na uhakika wote kuwa alichokisikia katika
simu ni sauti ileile iliyomkosesha shabaha na
utulivu mjini Shinyanga na kisha kumletea
majanga.
Lakini safari hii ilisikika katika simu ya upepo.
Hakufahamu fika ni nani mzungumzaji na alikuwa
upande upi.
Na punde baada ya kauli ile shambulizi
likafanyika.
Ni nani huyu? likabaki kuwa swali zito kwa Kobo.
Tukio la Kobo kuichukua bunduki hadi kuilalia
lilikuwa likifuatiliwa vyema na mdomo wa bunduki
iliyokuwa tayari kukohoa risasi.
Kobo hakujua, aliamini kuwa umakini wake ulikuwa
wa kiwango cha juu zaidi.
Baada ya shambulizi lile akazisikia hatua
zikisogea kwa kujiamini kuja mahali alipokuwa.
Akazivuta pumzi zake kisha akaanza kuzitoa nje
taratibu kabisa.
Akakisikia kiatu kigumu kikimkanyaga mguuni.
"Huyu tayari... hamna kitu humu." bwana
aliyekuwa anamkanyaga akatoa jibu lile.
"Chapa risasi kabisa kujihakikishia, hakawii kuwa
hai akatuharibia." Iliamrisha sauti nyingine kwa
ukali iliyotawaliwa na madaraka.
Kobo akaanza kuweweseka pale chini,
alijilazimisha kuendelea kutulia kana kwamba ni
mfu lakini kitendo cha kusikia kuwa anapaswa
kuchapawa risasi ili kuhakikisha juu ya uzima ama
kifo chake, hii ilikuwa ni sahihihi mbaya kabisa.
Kobo hakumsikia yule aliyeamriwa akijibu kitu
chochote, alishindwa kuelewa nini maana ya kimya
kile.
Hakutaka kucheza bahati nasibu ya 'nitakufa ama
wataniacha'
Akaamua kutumia nguvu zake za mwisho na njia
pekee iliyosalia katika kujitetea.
Akageuka upesi mtutu wa bunduki katika mikono
yake tayari kwa kufyatua.
Lakini hakuwa na mwendokasi wake wa zamani,
Kobo huyu alikuwa mgonjwa, mzito, asiyeweza
kuona vyema.
Hakuwa Kobo anayetisha tena.
Inspekta Kobo alikuwa amechelewa tayari.......
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom