Riwaya: ISABEL
Sehemu: 15
Katika uwanja ule ukimya ulitawala usiku ule utafikiri hakuna mtu, ni mingurumo ya gari tu iliyosikika lakini binadamu wote walikuwa kimya wakasubiri hatima ya ndege hiyo na kamanda Amata aliyepo ndani yake, kila mtu alisali kwa dini yake, Ee Mungu iokoe Tanzania. Madam S alibubujikwa kwa machozi akiwa anauma meno hakujua afanye nini alibaki kutazama tu saa yake iliyomwambia bado sekunde takribani kumi, hakuna Amata wala dalili za kuonekana kwake nje. Alipogeuka nyuma hakumuona waziri wa ulinzi, ambaye muda wote alikuwa hapo nyuma yake. Hakulifuatilia hilo macho yake yote yalikuwa juu ya Amata na ile ndege ya Rais yenye thamani kubwa kabisa Africa ‘Airforce one ya Tanzania'.
Kamanda Amata, huku mikono ikimtetemeka alikata waya wa kwanza kati ya zile nne, wa pili na alipokata wa tatu ‘Ignition Timer' saa ile ilisimama na kuacha kutoa ule mlio wake ikiwa imebaki sekunde moja kulipuka, saa ile ilisimama ikiwa imejiandika 00:00:01.
Amata alishusha pumzi ndefu, alijishika mikono kifuani moyo wake ulikuwa ukienda mbio, alijihisi kama mtu aliyetoka mautini.
Huko nje, ilipobaki sekunde tano makomandoo wa jeshi waliamuru watu wote kulala chini, na zilipokwisha bado hakuna mlipuko uliotokea. Walianza kusimama mmoja mmoja.
Madam S sasa alitokwa na machozi ya furaha alipomuona Amata akitoka katika ule mlango wa ndege mkononi akiwa amekamata lile bomu ambalo limeshindikana kulipuka.
Hakuna aliyeamini anachokiona, waandishi waliokuwa wamesimama mbali walisogea na kupata picha za shujaa huyu na kumhojo maswali mbalimbali, ilikuwa fujo uwanjani hapo.
Kamanda Amata aliingizwa kwenye gari na kufungiwa milango na gari ile iliondoka eneo lile.
Gari aina ya Toyota Altezza ilisimama karibu kabisa na ile gari ndogo iliyofanywa kama imeharibika tairi, Tonton alitoka kwenye kichaka cha michingoma na kuisogelea kwa hadhari kubwa kwa maana aliijua ile gari ilikuwa ikitumika na Jomse.
"Hali si nzuri tuondoke haraka," waziri wa ulinzi bwana Machura alimwambia Tonton na wote wakaingia ndani gari hiyo na kutokomea pande za Gongo la mboto.
"Mzee vipi?" Ton aliuliza
"Mambo si mambo kijana, hapa ni kujiokoa tu, na jinsi ninavyojua nchi hii si ajabu wameshabana kona zote"
"Oh God" Ton alisikitika. Gari ile iliendeshwa kwa kasi sana, walipita Pugu na kufika Chanika kisha mvuti mpaka mitaa ya Samvula Chole.
"Madam S, naomba uombe kibali cha kumuweka chini ya ulinzi mheshimiwa Machura" Amata alimueleza madam S huku akifyatua kiti kujilaza.
"Kwa nini?"
"Naomba utekeleze hilo haraka madam, wewe ndiye mwenye sauti, si mimi"
Bila kupinga madam S alipiga simu kwa mkuu wa polisi msaidizi baada ya kifo cha IGP na kuomba kibali hicho, bila kipingamizi kibali kilitolewa. Defender ya polisi ikiwa na polisi wenye silaha nyumbani kwa Machura, waziri wa ulinzi, walipigwa na butwaa nyumba ilikuwa tupu, hakuna mtu, si familia wala yeye mwenyewe, ni mlinzi tu ndiye alikuwa amebaki pale. Maelezo waliyoyapata kutoka kwa mlinzi yule yaliwakata maini, walielezwa kuwa familia ya Machura iliondoka yote jana asubuhi, lakini haikujulikana ni wapi ilielekea, taarifa ilifikishwa kwa haraka mahali husika.
Akiwa njiani kuelekea kituo cha polisi kati, kamanda Amata aliipata taarifa ile kupitia simu iliyopigwa kwa madam S.
"Shiiiit" Amata aliongea kwa hasira, "Hawezi kutukimbia hata kidogo," alichomoa simu yake mfukoni na kubofya namba fulani, kisha akaiweka sikioni.
"Hello … sio kivile… sasa sikia naomba uwasiliane na watu wa uwanja wa ndege ikiwezekana upate orodha ya abiria walioondoka jana kwa kila ya kila kampuni, haraka tafadhali" akakata simu mara tu baada ya kumaliza kuongea.
Madam S aliipaki gari yake pembeni kidogo ya kituo cha polisi, haraka Amata alishuka na wote wawili wakaelekea ndani.
"Upande huu tafadhali" afande aliyekuwa kaunta aliwaelekeza kuwa waingie kushoto, huko walimkuta Inspekta Simbeye akiwa amefura kwelikweli na Jomse akiwa kwenye kiti cha chuma akiwa na hali mbaya.
"Bastard!" Madam S aling'aka kwa hasira alipomuona Jomse, "Ulifikiri hii nchi ni ya baba yako?!, ‘Mimi mwanamapinduzi, mxiuuuuui, kawapindue hao hao'" alimuiga kwa sauti ya kubana pua.
Jomse hakuweza hata kuinua kichwa kwa jinsi alivyokuwa na maumivu makali, aliisikia tu sauti ya mwanamama yule aliyempa kibarua kigumu kule ofisini kwake. Wakiwa katika majadiliano hayo waligundua kuwa Jomse hali yake ilizidi kuwa mbaya.
"Hebu pelekeni Muhimbili, hakikisheni anapona ili atumikie kifungo chake ndani ya nchi hii" Amata alisema hayo na kutoka akifuatiwa na madam S. Baada ya kupata ripoti ya kuwa Isabel tayari yuko hospitali ya jeshi, Amata na madam S walifarijika, wakaagana na Inspekta Simbeye "Kama kuna lolote basi tutakutaarifu", kisha wakaondoka zao.
Simu ya Amata ikaita.
"Yes, niambie…"
"Tayari nimepata orodha zote, amri nyingine tafadhali" sauti ya kikakamavu ya Gina ilisikika.
"Vizuri, msichana mrembo, tukutane ofisini sasa hivi, bila kuchelewa." Dakika tano tu wote walikuwa ofisini pamoja na madam S, Amata akiwa na madam S walizipitia orodha zote, wakiwa karibu na kukata tama, chati ya mwisho kabisa ya shirika la ndege la Kenya ndipo waligundua majina ya familia ya Machura, ilionesha wametoka Dar kwenda Kigali kupitia Nairobi. Madam S alitikisa kichwa chake juu chini kuonesha amegundua kitu.
"Madam, mheshimiwa Machura, waziri wa ulinzi anahusika kwa kiasi kikubwa sana katika kuandaa mapinduzi haya ushahidi upo, kwa nini aondoshe familia yake? Ai alijua kuwa kitakaponuka familia yake iwe salama wakati Watanzania wanateketea"
Madam S alionekana kushikwa na hasira mpaka paji la uso wake likawa na mikunjomikunjo kadhaa, alipiga ngumi mezani na kujishika kiuno akimwangalia Amata.
"Hakuna kuchelewa, mpigie simu Simbeye msako uanze mpaka atiwe nguvuni kabla jua kuchomoza, kisha sisi twende kwa mzee ametuita haraka sana"
Dakika chache tu nchi nzima ilikuwa kwenye tahadhari kubwa hasa sehemu za mipakani ambako ilisemekana kuwa tayari kuliandaliwa majeshi ya waasi ambao walipata mafunzo maalumu katika misitu ya Nyakanazi, mapakani kabisa mwa Tanzania na Burundi, operesheni maalum ikatangazwa na kwa kuwa vijana wetu wa JWTZ walikuwa makini kazi hiyo haikuwa na mzaha hata kidogo, huku vijana wa polisi wakiwa wamelibana jiji la Dar es salaam katika kila uchochoro unaotoka nje ya jiji hilo ili Machura asitoroke.
Mheshimiwa Rais, alionekana kuchanganyikiwa kwa namna Fulani, hakuamini ni nini kinachoendelea. Akiwa amekaa kwenye meza yake kubwa na ile ya mbele walikuwapo waziri wa mambo ya ndani, jeshi la kujenga taifa, mkuu wa kitengo maalum usalama wa taifa madam S, na pembeni yake alikuwapo Kamanda Amata, kiti kimoja kilikuwa wazi.
Mheshimiwa Rais aliwaangalia wote kwa zamu.
"Asante sana kijana pamoja na madam pale, si kwamba mmeniokoa mimi bali mmeliokoa taifa, ambapo lingeingia kwenye mapinduzi na mauaji ya kimbali ambayo yangesababisha na watu wachache wenye uchu wa kutawala dunia" alinyanyuka na kuwapa mikono "Naomba nipate taarifa fupi ya yote haya ili sasa tujue kama tumemaliza au la" macho yote ya waliokuwa kikaoni yakaelekea kwa madam S na kamanda Amata.
Taarifa fupi ilitolewa na kila mtu katika kikao kile alibaki mdomo wazi.
Mheshimiwa Rais alielezwa kila kitu na hatua zilizochukuliwa na vyombo mbalimbali vya usalama nchini, kwa hatua hizo alitoa pongezi za dhati kwa wote, lakini kama kuna jambo lilimuuzi ni juu ya waziri wa ulinzi, hakuamini kabisa kama mzee huyo aliyeheshimika sana angeweza kuingia katika wimbi hilo la kupanga mapinduzi. Mheshimiwa alitikisa kichwa kwa masikitiko.
"Naomba kwa udi na uvumba, akamatwe ili aje ajibu maswali yake" Rais alitoa msisitizo.
Miaka mine nyuma
Kinshasa-RDC
Mkutano uliowakutanisha mawaziri wa ulinzi wote wa nchi za SADC ulifanyakia katika hoteli ya kimataifa ya Hilton mjini Kinshasa. Kama kawaida ya mikutano hiyo ilikutanisha watu wa aina mbalimbali, Tanzania iliwakilishwa na mheshimiwa Godfrey Francis Machura mzaliwa wa Kigoma, ambaye kiasili kabisa wazazi wake walihamia Kigoma wakitokea Congo, yeye alisoma na kujenga maisha yake yote hapo hata kujiunga na siasa katika chama cha TANU enzi hizo mpaka sasa CCM.
Jioni moja katika hoteli hiyo alikutana na wageni asiyowatarajia, wanaume watatu wa kizungu, mmoja akiwa kama chotara, pamoja na mwanamama mmoja wa Kiafrika mwenye maringo ya kuvutia mwanaume yeyote rijali.
Walikuwa na sera kubwa moja tu, kumhadaa mheshimiwa huyu ili kuweza kuipenya ngome ya kiulinzi ya Tanzania na kuweza kutekeleza mpango wao dhalimu walioudhamiria kama walivyofanya katika nchi kadhaa hapa Afrika. Kwa pesa nyingi walizo nazo, walimuahidi yeye mwenyewe kupata utajiri wa hali ya juu kama hilo lingetekelezwa.
Baada ya mkutano ule, mheshimiwa Machura hakuishiwa na ziara za mara kwa mara kwenda Kigali na Bujumbura, huko ndiko walikokuwa wakipanga huo Mpango Hasi. Ilishapangwa kuwa pindi tu mambo yakiwa sawa yeye na familia yake wangeenda kuishi Kigali ambako alishapewa nyumba kubwa na yenye hadhi. Tamaa ya pesa iliufanya moyo wake kuwa tayari kulisaliti taifa lililomlea na kumpa njia ya maisha, hakika shukrani ya punda ni mateke.
Kama kuna habari iliyomfariji mheshimiwa Rais katika kikao kile ni juu ya msichana Isabel.
"Bado taifa lina wazalendo, kama msichana huyu angepuuza juu ya hilo nini kingalitokea?!" aliuliza kwa mshangao.
Wote walibaki kimya, hakuna hata aliyekohoa katika kkao kile, kwa kila mmoja wazo tofauti lilikuwa likipita kichwani mwake akiwaza hiki na kuwazua kile kule. Kila mtu kwa muda huo alikuwa amekodolea ukutani ambapo kwa kutumia projector waliweza kuusoma mpango hasi hatua moja baada ya nyingine. Na walipomaliza kusoma kila mtu alishika tama kwa msikitiko, kimya kikatawala.
Baada ya kimya cha muda mheshimiwa aliuvunja ukimya huo "Sasa naomba turudi kwenye majukumu, halafu nitwaomba tena tukutane baada ya mambo haya kutulia, siku za usoni" alimaliza na kunyanyuka, wote walinyanyuka na kutoa heshima zao kisha kupeana mikono na kuondoka eneo hilo nyeti.
**********
Riwaya: ISABEL
Sehemu: 16
Kigali – Rwanda
Chiba aliipaki gari yake katika maegesho, kabla hajashuka katika gari hiyo aliiweka tayari bastola yake na kuibana sawia katika mkanda maalumu uliofungwa kwa kifuani, aliivaa miwani yake myeusi yenye uwezo wa kuona nyuma na kurekodi sauti ya mtu anayeongea naye. Alipoona kuwa amejikamilisha aliinyanyua simu yake ya upepo na kuwasiliana na watu walio nje kidogo ya maegesho hayo ambao walikuja kwa kazi moja tu, kazi muhimu. Alipoona kuwa wako tayari, aliteremka na kuliendea ghorofa moja wapo kati ya mengi ya yaliyojengwa eneo hilo kwa madhumuni ya kupangisha watu, bila kujua kuwa wengine wanaowapangisha hawana utu hata kidogo. Alikwea ngazi kwa kukimbia kidogo mpaka ghorofa ya pili, milango mingi ilimzunguka aliinua macho na kusoma vijinamba vilivyobandikwa milangoni. B 6T, akatikisa kichwa kuonesha kuwa ni sahihi kama alivyoelekezwa, alichomoa earphone yake na kuipachika sikioni kwa minajiri ya kuwasiliana na wale walo nje, kisha akabonyeza kitufe chekundu kilichopo mlangoni hapo. Sekunde kadhaa, mlango ulifunguliwa na msichana wa kadirio la umri wa miaka ishirini alijitokeza kichwa tu.
"Karibu, nikusaidie nini?" alimkaribisha Chiba kwa lugha ya Kinyarwanda. Msichana huyu mwenye mwili mwembamba na shingo ndefu alitoa tabasamu ambalo lilimfanya Chiba atulie kwanza baada ya network zake kukatika ghafla kwa kukutana na binti mwenye shingo ya upanga.
"Naitwa Tonton, nimemkuta madam Rose?" Chiba aliongopa jina.
Yule msichana alisita kidogo akamwangalia kijana huyo ambaye mkono mmoja wa kulia ulikuwa ndani ya koti lake kana kwamba anataka kutoa hela katika mfuko wake wa shati.
"Hayupo," alijibu msichana yule huku akirudisha mlango kuufunga, Chiba aliweka mguu na kuuzuia.
"Msichana! Nina shida ya muhimu, nahitaji kumuona madam Rose sasa hivi"
"Nimekwambia hayupo"
"Amekwenda wapi?"
"Mi sijui, nimemuona akiondoka tu." Chiba alibaki hana la kufanya, alitafakari kwa muda kidogo na kupata uamuzi.
"Ok" akageuka kuondoka, hamad, domo la bastola lilikuwa likimtazama usoni pindi tu alipogeuka.
"Tulia! Toa bastola yako" amri ilitoka kwa mtu huyo chotara, Frank, aliyekuwa tayari katika nyumba hiyo. Chiba aliitoa bastola yake na kuiweka chini, kisha yule msichana akaichukua.
"Ingia ndani," amri ya pili ilifuata na Chiba akatii.
Katika sebule ile kubwa Chiba aliketishwa kwenye moja ya sofa zilizo hapo na Frank akaketi kwenye sofa lingine kwa mtindo wa kutazamana.
"Mmemuua Mandi, na wengine, mmeona haitoshi sasa mmekuja hadi huku, mnajifanya FBI au Interpool?" Frank alimuuliza Chiba huku akinyooshea ile bastola iliyoonekana wazi haina masikhara.
"Zaidi ya hapo" Chiba alijibu kwa dharau. Frank alichukizwa na jibu lile na kufayatua risasi moja iliyochimba kwenye sofa lile sentimeta chache katikati ya mapaja yake, Chiba alitetemeka na kijasho cha ghafla kilimtoka kwa mbali.
"Ha ha ha ha kumbe unaogopa kufa, ha ha ha ha!" Frank alicheka kwa dharau, "Kwa taarifa yako madam Rose, hivi tunavyozungumza bado dakika kumi tu apae kuelekea Belgium kwa mapumziko, madam ni untouchable," alipokuwa akisema hayo Chiba hakupoteza muda, alijisukuma kwa nguvu pamoja na lile sofa na kupindukia upande wa pili, sofa lile likamfunika, kitendo hicho cha haraka kilimchanganya Frank, akaweka vizuri bastola yake na kufyatua risasi kadhaa kwenye sofa lile lakini tayari Chiba alishaliacha sofa lile peke yake. Hakuwa na silaha, alinyanyua bilauri iliyokuwa mezani na kuirusha, moja kwa moja ilitua katika uso wa Frank na kumpoteza malengo, yule msichana kule jikoni alikimbilia sebuleni ndipo alipodakwa na Chiba na kuwekwa ngao, huku Chiba akiwa tayari na kisu kutoka mikononi mwa msichana yule.
"Weka bastola chini, au la nakata koromeo la Malaya huyu" Chiba aliongea kwa gadhabu wakati huo tayari matone ya damu yalioneka yakidondoka sakafuni, kisu kile kilianza kuikata ngozi ya juu ya shingo la msichana yule. Frank hakuwa na ujanja aliiweka bastola chini, kisha Chiba alimuamuru kutoka eneo lile na kuuelekea mlango, naye akatii. Chiba hakuujua ujanja wa Frank, alipoufikia mlango kitendo bila kuchelewa aliichomoa bastola iliyokuwa upande wa nyuma wa suruali yake na kufyatua risasi mbili mfululizo, la, Chiba alijitupa upande wa pili na kuikamata bastola aliyoiacha Frank. Risasi za Frank ziliishia kifuani mwa yule msichana, akajibwaga chini akiwa marehemu. Frank aliduwaa alionekana wazi kachanganyikiwa kwa kitendo kile.
"Rooooosssseeee! Madam Roooooseeeee" alilia kwa uchungu, ndipo Chiba alipogundua kuwa kumbe yule alikuwa ndiye madam Rose lakini alipata shaka kutokana na picha aliyopewa ofisini. ‘Ni yeye au si yeye?' alijiuliza, mara akakumbuka kuwa yupo katika mapambano.
"Freeze" alimpigia kelele Frank, "Weka bastola chini" alimuamuru na Frank akatii. Mara mlano ukafunguliwa na watu wawili wakaingia, kwa ishara waliyopewa na Chiba wakamtia pingu Frank.
"Tuambie huyu ni nani?" Chiba alimuuliza Frank huku akielekeza mkono wake kwa yule marehemu msichana. Frank hakujibu alibaki kumwangalia tu usoni, "Nakuuliza wewe!" Chiba aling'aka lakini alichokipata ni kutemewa mate usoni kitendo kilichomuudhi sana, kwa hasira alimvamia Frank na kumchoma na peni ya chuma eneo la shingoni, Frank alitoa yowe la uchungu.
"Sema, madam Rose yuko wapi?" Chiba aliuliza tena. Lakini kabla hajapata jibu simu iliyokuwa juu ya kikabati kidogo ikaita kwa sauti kali, Chiba akaiendea na kuinyanyua ‘madame Rose' ilijiandika kwenye kioo, Chiba aliichukua na kumpelekea Frank.
"Ongea naye, kwa lugha yenu ya kawaida, weak loud speaker wote tusikie mwambia aje hapa haraka, ukigeuza neno nautawanya ubongo wako" Chiba alimaliza na kutegua kiguu cha usalama cha bastola yake na kuruhusu risasi kuingia chemba kisha akainyooshea kwa Frank usawa wa paji la uso.
"Yes, madame" Frank alipokea
"Hey Francoise, unikute hapa Kichukiro highway, nimeshapata ndege ya kukodi tuondoke joni hii"
"Sawa madame lakini tuna…"
"…Mna nini Francoise, mambo yameharibika kama kuna kinachoshindikana acha njoo wewe"
"Eh madam hali ya dada ako ni mbaya uje mara moja" mara simu ikakatika. Frank akanyanyuliwa na kuwekwa juu ya sofa kubwa pamoja na wale watu wawili, wakawasha television na kusubiri windo lao.
Ama kweli ndege mjanja hunasa kwenye tundu bovu, madam Rose aliingia kwenye maegesho kwa kasi ya hatari na gari yake aina ya Rambolghin, akapaki na kutembea harakaharaka kuelekea ngazi za jengo hilo, hakushtuka kabisa alipompita mwanaume mmoja katika ngazi hizo akiongea kwa simu huku akicheka, moja kwa moja aliuendea mlango na kuufungua kuingia ndani, nusura azimie baada ya kulakiwa na mwili wa marehemu uliyolala bila kuguswa kwenye dimbwi la damu mbichi.
"Uuuuuuiiiiiii !" alipiga ukelele wa mshtuko na kujikuta akidakwa na watu asiyowajua na kutiwa pingu, kisha kuwekwa juu ya sofa lingine na kumuona swahiba wake Frank akiwa amelowa damu katika shati lake.
"Idara ya usalama wa taifa Tanzania kushirikiana na idara kama hiyo ya nchini Rwanda tunawaweka chini ya ulinzi kwa jaribio la kufanya mapinduzi huko Tanzania." Madam Rose alishindwa afanye nini alibaki mdomo wazi, kapatikana. Hakuamini jinsi alivyonasa kwenye mtego wakijinga wakati amekwishakwepa mbinu nyingi za watu kama hawa sehemu mbalimbali za ulimwengu.
Bila ubishi, waliongoza chini na gari maalum yenye vyoo vyeusi na vinene visivyopitisha risasi lilifika hapo na kuwapakia.
"Mnatupeleka wapi?" madam Rose aliuliza.
"Hupaswi kujua, utaona ukifika" Chiba alimjibu. Safari hiyo ikaishia uwanja wa ndege, wakiwa na soksi katika vichwa vyao hawakuweza kuona hata wapi wanaelekea, walipakiwa kwenye ndege maalum na safari ya kwenda Dar es salaam ilichukua nafasi yak echini TSA namba 2, Chiba wa Chiba.
"Ina maana hamnijui mimi? Mbona mnaleta mambo ya ajabu?" Machura aliongea kwa hasira aliposimamishwa na askari wa checkpoint maeneo ya Igumbilo, Iringa. Alikuwa akijaribu kutoroka kwa kutumia njia hiyo mpaka Mbeya ambako angeweza kuingia nchi jirani lakini alipofika hapo check point gari yake haikuwa na budi kusimama kutokana na mageti yaliyowekwa hapo kuzuia njia. Ilikuwa ni saa nane usiku, kibaridi kikali kikipuliza.
"Nitapiga simu kwa RPC wenu na ninyi wote mtimuliwe kazi" aliendelea kung'aka huku akiwa anazungukazunguka huku na kule. Mabishano yalipokuwa yamezidi, Machura alipiga simu kwa RPC Kamuhanda wa Iringa, kweli akili ni nywele. RPC Kamuhanda aliona simu yake ikiwakawaka alipoiinua kwenye kioo alikuta jina la mheshimiwa mkubwa serikalini, akaitazama kisha akaiweka sikioni na kuipokea.
"Hello mheshimiwa waziri …"
"…Yes, .. a a a … Kamanda, vijana wako wananizuia njia hapa Igumbilo, hawajui kama nipo katika majukumu ya kiserikali? Naomba uwaamuru haraka waniruhusu kupita na kisha hawa wote walio zamu sasa hivi wachukuliwe hatua za kinidhamu"
"Ok, naomba ngoja niwapigie mara moja, hawana nidhamu kabisa kwa nini wakuzuie, wana kigezo gani? Lazima niwaadabishe," RPC Kamuhanda aliikata simu ya Machura na kuivuta simu yake ya upepo tayari kutoa taarifa hiyo.
"Na mtaona sasa…ninyi hamjui kuwa mimi namuwakilisha Rais!" alimaliza kuongea huku akiingia katika gari yake.
"Vipi?" Ton aliuliza.
"…Check point Igumbilo, iruhusu gari ya mheshimiwa ipite mara moja ni amri, ova"
"….Tumekusoma, tunatekeleza, ova"
Geti likafunguliwa na gari ile ikapita kuendelea na safari, huku Machura akiwaoneshea kidole cha kati askari wale.
Karibu kabisa na njia panda ya kupandishia Iringa mjini, Land Rover Defender ya kituo cha polisi Iringa ilisimama katikati ya barabara ikwa imewasha taa zote full, juu ikiwa na vijana wawili wenye SMG na chini kulikuwa na vijana wanne wenye silaha pia. Ton aliendesha kwa mwendo wa taratibu,
"Aaaggghhh! Shit, nini tena!" Machura alipiga kelele huku akipigapiga mikono yake kwenye mapaja yake kwa hasira.
"Unaombwa kujisalimisha, wewe pamoja na uliyekuwa naye garini" sauti ilisikika kutoka nyuma, Machura alipogeuka alikuta Land Cruiser ya buluu ya polisi ikiwa nyuma yao, mbio za sakafuni huishia ukingoni.
"Unaombwa kujisalimisah, kwa kutoka nje ya gari hiyo mikono hewani, tii sheria bila shuruti" sauti ile ilirudia tena kutoka kwenye megaphone.
"Napambana!" Ton alimueleza Machura huku akimuonesha bomu la kurushwa kwa mkono.
"Ha ha ha ha…" sawa kijana umejiandaa vyema nakuaminia.
Ton alifungua mlango na kutoka nje huku mikono ikiwa hewani lakini ilikuwa ni vigumu kumgundua kama kashika kitu mkononi, walipotaka kumfuata alirusha bomu lile kwenye Land cruiser na kishindo kikubwa kilisikika, ile Cruiser ikanyanyuliwa kama box tupu lipeperushwavyo na kimbunga, hali ya mkanganyiko ilitwaa nafasi badala ya utulivu, Ton na bastola yake mkononi alijaribu kuwalenga polisi wale, kwa shabaha yake nzuri aliweza kumpata wa juu katika defender iliyosimama upande wa pili. Machura alishindwa kuvumilia alitoka garini na bastola mkononi akijaribu kufyatua hewani huku akijitahidi kukimbia lakini tumbo lilimzidi uzito. Moshi ukiwa umetapakaa kila mahali, ving'ola vya gari za faya na polisi vilisikika kutoka Iringa mjini. Machura alimshuhudia Tonton akichakazwa kwa risasi kutoka kwa polisi aliyefika na pikipiki, hapo akaona hapamfai bora aiponye nafsi yake, alianza kutimua mbio kufuata barabara ya kuelekea Mbeya lakini hakufanikiwa, alipoambiwa asimame aligeuka na kumfyatulia risasi polisi yule ambaye alibwagwa chini na kupoteza uhai, kabla Machura hajajiweka tayari alijikuta akichakazwa na risasi zilizotoka katika SMG ya polisi mwingine aliyebaki juu ya defender na kumlaza juu ya daraja hilo akiwa hana uhai.
"Mwanaharamu we! Nani aliyekwambia unaweza kuukimbia mkono wa dola?" ilikuwa ni sauti ya RPC alipokuwa akiuangalia mwili wa Machura ukiwa kwenye machela tayari kuhifadhiwa kwenye chumba cha maiti cha hospitali ya mkoa wa Iringa.