Riwaya: HOFU

iddy eba

JF-Expert Member
Aug 28, 2015
575
1,169
RIWAYA: HOFU
MTUNZI: George Iron Mosenya
SIMU: 0655 727325
MWAKA WA KUANDIKWA: 2013
"Tunayaweza yote ambayo akili zetu zinafikiri,
lakini kamwe hatutaweza kuyatekeleza vyema
kwa kuziamini akili zetu pekee..... Yupo aliyetupa
akili hizi. Kila tunapopiga hatua kulianza jambo
tumsihi atujaze nguvu, uvumilivu na mioyo imara
isokata tamaa....

Twayaweza yote kwa jina lililo kuu kuliko yote.
MUNGU!"
Na hii ni sehemu ya kwanza.......
“OLE!! OLE WAKO KINDO” maneno haya
yaliendelea kujirudia katika kichwa chake hata
siku ilipobadilika baada ya mshale mfupi wa saa
kuielekea namba kumi na mbili na ule mrefu nao
ukielekea katika namba moja.

Ilikuwa saa sita na dakika tano usiku!! Siku ya
jumanne.
Kindo hakuwa amepata usingizi tangu Salome
aondoke majira ya saa tatu usiku huku akitoa
viapo visivyoeleweka.
“Aaaargh! Aende zake huko, mimba wampachike
watu wengine halafu aniangushie mkasa huu
mimi. Hamna kitu kama hicho, maisha ya kulea
mtoto mimi nayatoa wapi sasa, chandarua hiki
nimeshindwa kukibadili mbu wanafurahia tu,
mama mwenye nyumba ananidai hadi leo
sijamlipa kodi yake.

Nguo zangu zimetoboka nimeziba na viraka hadi viraka navyo vinazibwa
na viraka vingine. Naanza vipi Kindo mimi kupata
pesa ya kununua maziwa ya mtoto…. No no!!
hata kabla ya mtoto, hilo tumbo nalilea vipi kwa
miezi tisa.

Mbaya zaidi ni tumbo lisilonihusu
kabisa hata kidogo, yeye kama walimlewesha
huko wakambaka bila kujua na asubuhi
anajidanganya ni mimi nimempachika mimba
shauri zake!!” alizungumza peke yake kwa sauti
ya juu huku akitupa mikono huku na huku. Kifua
kikiwa wazi na jasho likimchuruzika.

Kindo alikuwa ametaharuki huku akijaribu
kuudhibiti mwangwi wa sauti ya Salome. Mwangi
uliompa onyo lisiloeleweka!!
Kitanda kilicholegea kikapiga kelele na
kuwafanya panya katika dari kucheka katika
lugha zao za maudhi.

Kindo alikuwa ametelemka kwa ajili ya kujifuta
jasho lililokuwa linazidi kuchuruzika.
Joto la leo….!! Alilalamika huku akijipangusa.
Kisha akarejea kitandani tena, kulilalia godoro
lililokuwa katika siku za mwisho za uhai wake.
Miale ya radi ikawaka huku na kule, kisha
ngurumo zikapasua anga.

“Nd’o maana nikashangaa mbona joto hivi…
kumbe mvua inataka kunyesha!!” kauli hii
haikumalizika kabla Kindo hajakurupuka na
kuanza kuhangaika kuhamisha kitanda kwenda
upande mwingine.

Maana upande sahihi kilipokuwa palikuwa na tatizo la kuvujia maji.
“Salome angekuwepo angenisaidia kuhamisha
hiki kitanda….” Kindo akajikuta akisema tena
huku akiikaza misuli kwa nguvu zaidi.
Mvua kubwa sana ikafuatia!!

Joto likakimbia na sasa Kindo akaanza kulalama
kuwa baridi imekuwa kali sana!!
Mvua haikukoma hata pale usingizi mzito
ulipomtwaa Kindo.
****

“Kindooo, oyaa we Salome muachie mwenzako
muda wa kazi huu”
“We Kindo wewe!!! Kindooo….”
“Kindo tunakuacha sisi….”
“Kindo tusilaumiame ohoo shauri zako utamla
huyo mwanamke!!!”

Kindo akajigeuza upande wa kushoto huku
akitamani sautri zile ziendelee kuwa ndoto. Lakini
haikuwa, sauti zikazidi akalazimika kufunua
macho yake.

“Kwani saa kumi na moja imefika?” aliuliza kwa
sauti iliyokuwa inakoroma.
Matusi ya nguoni yaliyofuatia yalimfanya atoke
kitandani. Alishawazoea rafiki zake watatu jinsi
walivyokuwa mabingwa wa kutukana.
Alilala na nguo zake zote, alichofanya ni kuvaa
viatu na kutoka nje. Huko napo akapokelewa na
tusi la nguoni, naye akajibu.

Usingizi ulikuwa umeenda zake!!
“Mbona mikono mitupu mwenzetu..” rafiki mmoja
akahoji. Kindo akarejea upesi ndani, akainama
uvunguni na kutoka na koleo.
“Salome… shem eeeh pole bwana kwa
kukupeperushia ndege wako…” Maulidi
mmojawapo wa marafiki alisema huku
wakitoweka. Kindo akatikisa kichwa kushoto na
kulia.

Hakuna aliyejua!! Na hakutaka wajue mapema
hiyo kabla ya kazi.
MITARO ilikuwa imesheheni mchanga haswa, na
vijana hawa walikuwa wamedamka wakati
muafaka kabisa. Walikusanya mchanga vichuguu
kwa vichuguu bila kuchoka.
Kufikia majira ya saa tatu asubuhi walikuwa
wamejiridhisha kwa kazi yao ya siku hiyo.

Maulidi akauendea mfuko, akatoa viazi, John
akatoa dumu la maji. Hakuna aliyengoja
kukaribishwa.
Njaa kali iliwafanya wale kwa pupa sana kana
kwamba viazi vitaisha, lakini shibe ikawalegeza
na kila mmoja akaviona viazi vilivyosalia kama
mzigo wa uchafu.
Kila mmoja alikuwa ameshiba.

“Wewe Kindo uliyeoa kabla ya muda utabeba hivi
vilivyobaki umpelekee Shem Salome.” Masalu,
rafiki wa tatu alisema kwa lafudhi yake ya
kisukuma. Mauled na John wakacheka lakini
Kindo ambaye alikuwa mwepesi wa kucheka siku
zote akastaajabisha.
Hakucheka!!

“Salome mshenzi sana, ujue mliponiambia
wanawake akili zao fupi sikuwahi kuamini kuwa
hata Salome anaweza kuwa hivyo. Si
unakumbuka Maulidi tulitaka kugombana siku
moja…” Kindo alitokwa na kauli hiyo akiwa
ameinama.

Kimya kikatanda, hakuna aliyeamini kuwa Kindo
anasema vibaya juu ya Salome. Wote walijua ni
kiasi gani Kindo alimpenda Salome na hakuwahi
kuwa na msichana mwingine zaidi yake, na hata
hao marafiki walikiri kuwa Salome pia hakuwa na
mwanaume mwingine zaidi ya Kindo.

“Salome kafanya nini tena…”
“Ameondoka zake kwenda kwa wanaume zake…”
alijibu kwa mkato.
“Wanaume wake??” wote watatu kwa pamoja
waliuliza.
Kindo akatabasamu kidogo kwa kujilazimisha
kabla ya kuwaelezea mkasa uliomkumba hatua
kwa hatua.

“Uzuri ni kwamba rafiki zangu wote niliwaeleza
kila jambo, siku ile niliowaeleza kuwa nina
wasiwasi Salome ana ujauzito kwa sababu haoni
siku zake, tena nikawaeleza kuwa ikiwa kweli ana
mimba basi ni yangu. Na baada ya hapo ni siku
ile nilipowaita na kuwanunulia soda ili kufurahia
Salome kuingia siku zake.

Wote mlikuwepo, sasa jamani kama aliingia katika siku zake vizuri
kabisa hii mimba mimi nahusika nayo vipi? Hebu
vaeni viatu vyangu na nyinyi muwe upande wa
maamuzi…” Kindo alimaliza, hakuna hata mmoja
aliyesema neno zaidi ya kuguna tu.
Viazi vilizidi kusahaulika na nzi wakajifanyia
sherehe.

“Walah huu mtihani hakiyanani!!” Maulid aliapa
huku akisimama asijue kwa nini amesimama.
John na Masalu wakabaki kumtazama.
“Yaani aingie siku zake halafu aseme tena ana
mimba yako…. Kindo kaka, kama kweli haujalala
na yule mtoto tena baada ya pale kama
asemavyo Mau…

Walah huu mtihani…” John aliiga
lafudhi ya kipemba ya Mau na kusababisha
vicheko. Kasoro Kindo tu!! Hakucheka. Aghalabu
kutabasamu.
“Kindo, kule kanda ya ziwa, wakurya wanasema
hivi ‘Mang’ana ghasalikiree’ yaani mambo
yameharibika!!” Masalu alisema kwa kumaanisha
lakini sasa kila mmoja hata Kindo naye alicheka.
“Na alisema anaenda wapi?” John aliuliza.

“Hakusema yaani aliimba mashairi mengi wee,
mara ole wako sijui nini na nini… mwisho
akaondoka, yaani akaubamiza ule mlango hadi
nikasema ameuvunja. Yule binti yule dah!!”
“Kindo nenda nyumbani, Salome ninayemjua mimi
walah hawezi kuishi mbali na wewe, mama yake
mwenyewe anajua kabisa kuwa yule ni wako.

Nenda nyumbani kama hayupo nenda kwa mama
yake. Mweleze kilichotokea na usithubutu
kusema kuwa ulimfukuza Salome.. usithubutu
kabisa.” Maulid alitoa ushauri uliokubaliwa na
kila mmoja.

“Na kitu ambacho nahisi..... huenda hata hana
mimba yule amefanya kunizingua tu anione
msimamo wangu eti eeh!!” Kindo alizungumza
huku akiwa na furaha. Wakaagana na kumwacha Kindo aende nyumbani
na wao wakabaki kungoja wateja wa mchanga
waweze kuuza na kujipatia ridhiki.
***


MANENO ya marafiki yakaijenga faraja moyoni
mwa Kindo, nguvu zikamjaa tele akatembea upesi
upesi akiwa amebeba koleo lake na lile furushi
laviazi akakaza mwendo kwenda nyumbani huku
akiwa na matumaini tele kuwa anaenda kuonana
na Salome tena.

Mvua iliyokuwa imenyesha ilifanya ardhi
isiongope iwapo itakanyagwa.
Naam!! Alama za kandambili alizokuwa amevaa
Kindo wakati wa kutoka alfajiri zilionekana
vyema, hata alama za miguu pekupeku ya rafiki
zake waliokuja kumgongea asubuhi zilionekana
pia.

Lakini kulikuwa na alama za ziada, zilikwenda
mlangoni na kisha kutoweka tena.
Alama za viatu visivyojulikana kama ni vya kike
ama vya kiume.
“Salo….. Salomeee!!” Kindo alianza kuita kwa
sauti ya chini kiasi.

“Salome mke wangu!!” sasa aliipaza huku
akiufuata mlango.
Akaufungua kwa kuusukuma taratibu akitarajia
kukutana na uso wa Salome.
Mlango ukafunguka, Kindo akaingia ndani lakini
alikuwa yeye na kitanda chake ambacho sasa
aligundua kuwa kilikuwa kimevunjika upande
mmoja.

Bila shaka wakati wa kukihamisha.
Akashusha pumzi kwa nguvu!! Akatamani kuketi
kitandani lakini akahofia kitavunjika zaidi.
Akakivuta kigoda na kukaa hapo.

“Kama hayupo, nenda kwa mama yake!!”
akaikumbuka sauti ya Maulidi. Akafanya
tabasamu hafifu. Akayaendea madumu mawili ya
maji, moja lilikuwa tupu na jingine lilikuwa na maji
kiasi.

Akalitwaa ili aweze kwenda kuoga na kisha
afanye safari ya kwenda kwa mama mkwe.
Wakati anatoka nje akamuona mwanaume mgeni
kabisa machoni pake akijongea moja kwa moja
kuja katika mlango wake.

Aidha alikuwa anakuja hapo ama la!! Kindo
akalazimika kungoja.
“Habari za asubuhi bwana!!.. bwana Emmanuel
kama sijakosea..”
“Kha!! Hapa… eehm ndio Emmanuel….” Alijiuma
uma Kindo, akistaajabu huyu ni nani amjuaye kwa
ufasaha namna hiyo.

“Karibu ndani!!” alimkaribisha yule bwana ambaye
hadhi yake haiukufanania hata kidogo na
muonekano wa mle ndani.
Kindo akavuruga baadhi ya nguo zake stuli
ikabaki wazi akamkaribisha yule bwana ambaye
aliingia ndani pasipo kuvua viatu.

“Emmanuel Kindo….. Kindo Kindo Emmanuel….”
Kwa sauti ya chini huku akiipigapiga kalamu yake
huku na kule yule bwana aliliimba jina la Kindo.
“Wewe ni nani samahani bwana!!” Kindo
akamkata kauli. Sasa alimkazia macho.

“Hiki kitanda huwa mnalala vipi watu wawili
sasa?” badala ya kujibu aliuliza.
Kindo akaonekana kukerwa na swali lile. Lakini
hakusema neno zaidi ya kuhimiza juu ya
utambulisho.

“Hata kama asingekufa nisingekubali hata kidogo
aolewe na mtu wa namna hii… “ aliendelea
kusema peke yake. Hali iliyozua wasiwasi kwa
Kindo hasahasa baada ya kusikia juu ya kufa na
kuoana.

Bila shaka hapa anamzungumzia msichana!!
Kindo akaomba kwa kila namna msichana huyo
asiwe Salome.
“Wewe ni nani kaka, nina mashaka kuwa
umekosea nyumba….”

“Weee koma komea hapo hapo nasema shwain
wewe!!!” ghafla yule bwana akapaza sauti
akimkaripia Kindo, alikuwa amesimama huku
akiielekeza fimbo yake ya kutembelea machoni
pake Kindo.

“Nasema kaa kimya kabisa mwanaharamu
wewe!!” alizidi kuonya. Kindo akanywea na kukaa
kimya.
“Wewe Emmanuel Kindo, ni kitu gani kilikufanya
ukamlaghai mwanangu, akatoroka shuleni na
kunidanganya kuwa shule imefungwa sijui
anapitia kwa shangazi yake gani huko…… eeh
wewe mwanaharamu wewe nakuuliza….”

Akasita na kufanya kicheko kidogo kikisindikizwa na kauli
nyingine ya kustaajabisha, “ Yaani watoto wa
siku hizi, yaani Kindo kiukweli mlijitahidi
kuongopa yaani mama yake ujue akadhani kweli
kabisa, ila tatizo ni siri haina watu wawili,
mwenzako alimshirikisha rafiki yake ndo huyo
aliyeniambia…….”

Kicheko kikafuata tena. Halafu
ghafla tena akabadilika.
”We mpumbavu, unanikodolea macho hapa…. Ni
kwanini ulimdanganya mwanangu…” kimya
kikatanda, Kindo akawa kama zezeta tu
aisyeelewa chochote.

Lazima aduwae!! Maana kama huyu alikuwa
mzee wa Salome basi huyo Salome mwenyewe
aliishia darasa la saba tu tena miaka mingi
ilikuwa imepita tayari.
“Mzee sikuelewi bado….”

“Naitwa mzee Gaspari Nshomile mzazi wa
Rebeka Nshomile mliyembatiza jina la Rensho….
Yeye ndo Re na mimi ndo Nso…..RE-NSHO….mimi
ni baba yake mzazi na Rensho….” Alijitambulisha
yule mzee kwa kujiamini kabisa akitarajia labda
Kindo atashtuka lakini ndo kwanza alizidi
kushangaa.

Rensho!! Jina geni kabisa.
“Mzee!!”
“Nani mzee wako shenzi wewe…… mimi ni mzazi
wa Rensho, mwanafunzi wa kidato cha tano hapo
Tabora girls unajifanya humjui eeeh….. hauna
redio humu ndani ama….punda kasoro mkia
wewe. Umemrubuni msichana halafu amekufa
ndo unajifanya humjui…

umenichefua tayari na sasa utajua nini maana ya nshomile.” Alipandwa
na jazba yule mzee na kuanza kushusha kipigo
kwa Kindo, alijaribu kuruka huku na kule lakini
hakufua dafu.

“Huwezi kunikimbia mimi punguani wewe, vita
vya Kagera wananijua walioshiriki, mimi
nilimkung’uta teke Iddi Amini hakuwahi kunisahau
hata leo ukifukua kaburi lake ukamuuliza
atakwambia …..” haya yalimtoka huku akimchapa
bakora Kindo ambaye muda wote alilalamika
kuwa hamjui wala hajawahi kusikia jina la
Rensho.

“Nitarejea baadaye hapa. Shida yangu ni moja tu
mkoba wa Rensho uliouchukua. Sijali kama
utakuja kumzika ama hautakuja, cha muhimu
mkoba halafu mimi na wewe tunayamaliza haya
mambo kiume.

Vinginevyo nitakukabidhi kwa
polisi ukafungwe maisha.” Alitoa onyo, kisha
akajiweka sawa kwa kuondoka.
“Na kabla sijasahau, meseji yako uliyotumiana
naye kuwa mnaagana imekutwa katika simu
yake… hauna ujanja pumbavu wewe….” Alimaliza
akasonya na kutoweka.

Simu? Aliduwaa Kindo akiwa ardhini akiugulia
maumivu. Tangu lini mimi nikawa na simu!! Mbona niliiuza
huu sasa ni mwezi unapita. Amenifananisha huyu
mzee maskini wa Mungu mimi. Alijisemea Kindo
huku macho yakimsindikiza yule mzee hadi
akatoweka.

“Mzee Nshomile…..Nshomile kivipi wakati mzee
wake Salome anaitwa Wilbard…. Ndio, Salome
Wilbard na Rebeca Nshomile wapi na wapi?” sasa
alizungumza kwa sauti huku akijikongoja na
kusimama akaegemea ukuta wa chumba chake.

**HOFU!!! Imeanzia hapa, Kindo akiwa
amekorofishana na SALOME mpenzi wake kisha
akatoweka anapata ugeni, baba yake Rebeka
Nshomile (Rensho)…… mzee anadai mkoba wa
binti yake ambaye ni marehemu sasa……
Kindo hamjui wala hajawahi kumsikia…..

TUKUTANE BAADAYE
 
"Katika maisha ukijitazama wewe pekee bila
kuutazama upande wa pili kila siku utajikuta
kuwa mtu wa kulalamika tu na kuhisi unaonewa.
Iwapo ukifanyiwa jambo tambua kuwa na wewe
unaweza kumfanyia mwenzako kwa wakati
mwingine aidha kwa kukusudia ama bahati
mbaya. Jifunze kufikiri kabla ya kutenda,
ukiiruhusu akili yako kuwa hivyo si kwamba
utakuwa mkamilifu la! Bali utaziepusha shari
nyingi."
Na hii ni SEHEMU YA PILI
“Wazee wengine wamechanganyikiwa sijui?”
alijiuliza kwa sauti ya juu huku akiamua kukikalia
kitanda chake ambacho kimevunjika. Safari hii
hakujali kama kitavunjika zaidi ama la!
Alikuwa amevurugwa!
Lakini!...... amenijuaje kwa jina kamili kabisa la
Emanuel Kindo? Alijiuliza huku akiwa
amejiegemeza ukutani na kichwa chake
kikipakatwa na mikono yake miwili.
Swali hili likawa gumu zaidi. Na asingeweza
kuendelea kukaa bila kuwa na jibu. Akakumbuka
kuwa alitakiwa kwenda kuonana na mama yake
Salome ili aweze kupata uhakika kama ni kweli
Salome atakuwa yu nyumbani kwao ama la!
Alitamani kunyanyuka na kuanza safari lakini
maumivu kwa mbali kutokana na kipigo
alichopokea kutoka kwa mzee Gaspar Nshomile
yalimfanya apitishe uamuzi wa kulala kidogo
huku akiapa kuwa akiamka tu anaoga kisha
anaenda nyumbani kwa mama yake Salome.
Kindo aliusahau ule usemi wa liwezekanalo leo
lisiongoje kesho, akafumba macho yake na
kuusaka usingizi.
Wakati yeye akiusaka usingizi na hatimaye
kuupata na kuanza kukoroma, mitaa fulani mbali
kabisa kutoka alipokuwa amelala yeye liliendelea
tukio ambalo laiti kama angeamua kuupuuzia
uamuzi wa kulala basi angeweza kulishuhudia na
kulipinga kwa nguvu zote. Kidogo imani ingeweza
kurejea labda!! Lakini tukio hilo la aina yake
lilitokea huko mbali kabisa yeye akiwa amelala
kisha tukio lile likahama kwa kasi ya ajabu.
Mlango ukamshtua kutoka usingizini, ulikuwa
umesukumwa kwa nguvu sana. Akayapikicha
macho yake na kitu cha kwanza kuona baada ya
akili kutulia ni saa ya ukutani.
Saa kumi na moja na robo!!
Kindo alikuwa amelala sana!!
“Mtazame asivyokuwa na aibu!!” sauti ikasema
katika namna ya kusuta!! Sauti haikuwa ngeni
hata kidogo katika masikio yake. Na kama akili
ilivyoishika sauti ile ndivyo macho yalivyoleta
uthibitisho.
Alikuwa ni yeye mwenye ile sauti.
Mwanamama akiifunga kanga yake kuukuu
kiunoni huku akingoja Kindo azungumze.
“Shkamoo mama!!... karibu mama..yaani…leo
nilitaka nije…”
“Shhhhhhh!! Ishia hapo hapo Kindo, mtoto mbaya
wewe. Umejivika ngozi ya kondoo ilhali u chui
mkali.” Mama yake Salome alimkatisha Kindo.
Kindo akastaajabu!! Hakuwahi hata siku moja
kuingia katika mtafaruku na mama yake Salome,
sasa iweje leo.
“Kindo, Kindo ni wewe. Kindo ambaye ulikuwa
unaugua Salome anakuja kunililia nyumbani,
nachukua shilingi zangu kadhaa. Kindo, shilingi
pekee zilizopo ndani nakununulia dawa kwa moyo
mmoja na kwa ajili ya furaha yako na Salome.
Kindo ni mara ngapi Salome amechukua unga wa
ugali nyumbani ili usilale njaa wewe, ni mara
ngapi Kindo. Mnafiki mkubwa wewe ukachonga
mdomo wako kunilaghai kuwa utamuoa
mwanangu wewe, na sasa naingia hapa
unanirubuni na shkamoo yako hiyo ya kinafiki….
Kindo wewe ni muuaji mkubwa, hufai kuwekwa
katika kundi la wanaume. Hufai Kindo…. Yaani…”
mama Salome akashindwa kuendelea
kuzungumza akabaki kutetemeka na sasa
machozi yalikuwa yanamtiririka.
Kwa mara ya kwanza Kindo anashuhudia uso wa
mama huyu maskini ukikosa tabasamu na
kutawaliwa na hasira. Kindo akataka kusimama
aweze kumnyamazisha akakutana na karipio kali
lililomrejesha kuketi kitandani.
Akaketi kwa pupa, kile kitanda kilichomvumilia
mwanzo kikamtia aibu safari hii kikaachia, Kindo
akaenda nacho chini!
Akawahi kusimama upesi!!
“Lakini mama, Salome na mimi tulizungumza na
kuelewana. Hata ungekuwa wewe mama…. Labda
kama Salome amesema vingine tu… unatakiwa
kunisikiliza mama..”
“Mlielewana katika huo upuuzi, ujinga mkubwa
mtoto wa kiume unakuwa dhaifu kiasi kile.
Salome mwanangu hajasoma hata hilo la saba
alifeli lakini narudia Salome sio mjinga hata
kidogo wa kuchekelea mahusiano yako sijui ndoa
yako na huyo sijui Recho sijui Rensho, kamwe
Salome si mjinga. Alikupenda sana ujue, Salome
alikupenda sana hujui tu hayawani wewe.
Kweli Kindo, pesa za ukoo wa mwanamke
zinakufanya unamkana mwanangu mimi.
Unaamua kumuumiza mwanangu mimi kwa
sababu ya mwanamke mwingine mwenye pesa…..
hivi unaoa ama unaenda kuolewa Kindo, ona aibu
… ona aibu Kindo wewe si wa kufanya
ulichofanya kwa Salome.
Unasimama kabisa kuwaambia rafiki zako akina
Mau na John, eti Salome mshenzi sana kupita
wasichana wote uliowahi kuona. Mpuuzi mkubwa
wewe, unamuita Salome mshenzi kwa sababu
umepata mwanamke mwenye pesa, mbingu na
ardhi zikuzomee na aibu iwe juu yako.” Alitema
cheche mama Salome, machozi hayakuisha
kububujika.
"Chozi hili linanitoka Kindo, siujui umri wangu
mimi lakini nina uhakika ni makamo ya mama
liyekuzaa... umemtoa cghozi mama yako Kindo.
Chozi hili halitaanguka bure nasema.... mimi ni
maskini sana sina lolote la kukufanya lakini
Kindo.... Kindo..." Sasa hakuweza tena
kuzungumza lolote la ziada...... kilio kikamzidia.
Kindo akabaki kuduwaa asielewe mama Salome
anachokizungumza hadi anatokwa na machozi
amekitoa wapi.
“Mama…. Upo sawa kweli?” Kindo aliuliza kwa
upole akidhani ataeleweka na kushusha jazba ya
mama Salome.
“Dharau!! Dharau zitakuua maskini wewe,
mtazame. Kumpata huyo Rensho sasa kila mtu
unamuona mwendawazimu, umemtukana Salome
wangu na sasa unanitukana mimi. Wanadamu
wanadamu…” alimaliza kwa kicheko cha dharau.
Kindo akazidi kuhamanika akihangaika kujiuliza ni
kitu gani kinatokea. Baba yake Rensho amekuja
kudai mkoba wa marehemu mtoto wake, na sasa
mama yake Salome anakuja kumlalamikia kuwa
kwa sababu anakaribia kuoana na Rensho basi
ameamua kuachana na Salome.
Hiki nini sasa? Alijiuliza. Wakati huo mama
Salome alikuwa anajiandaa kuondoka na
hakuonekana kama ataaga.
“Kindo!!” aliita kisha akamtazama machoni, “ Sijui
Salome yupo wapi muda huu baada ya
kumweleza hayo maujinga yako, ila napenda tu
kukutahadharisha kwamba iwapo Salome
atakumbwa na kitu chochote kibaya. Basi
itafahamika kama sisi watu wa tabaka la
kimaskini tuna haki ama hatuna haki, naapa
Kindo. Ole wako Salome aathiriwe na kitendo
ulichofanya, nasema ole wako. Ama zangu ama
zako na hiyo ndoa haitafungwa labda wewe na
matajiri wenzako mniue kwanza.” Akafanya kiapo
kisha akabamiza mlango bila kuaga akatoweka
asiijali sauti ya Kindo iliyoendelea kuita mama
mama!!
Siku hii ikawa chungu zaidi kwa Kindo ambaye
hakujua ni kitu gani kinatokea na yeye
kuandamwa na vitu asivyovijua. Kwanza Rensho
katika upande wa baba yake na sasa huyu huyu
Rensho anasemwa na mama yake Salome.
Kizaazaa!! Alikiri Kindo huku akipiga hatua hapa
na pale katika chumba chake. Mara akakoma
ghafla mlango ulipofunguliwa tena.
“Mguu huu utarejea tena hapa iwapo tu
mwanangu atakumbwa na jambo baya, lakini
kama atakuwa salama…. Kindo usitegemee
kuniona tena hapa katika kibanda chako na wewe
usikanyage nyumbani kwangu!!” mama Salome
alikoroma tena kisha akaondoka, wakati huu
hakuubamiza mlango.
Kindo akabaki katika hali isiyoelezeka, hakuwa
katika mshtuko wala mshangao, akarejea
kitandani kujilaza huku akitafakari ni kitu gani
kinatokea katika maisha yake.
Rensho ni nani?
Akajaribu kuvuta picha miaka ya nyuma huenda
kuna mwanamkie waliwahi kupendana aliyeenda
kwa jina la Rebeka Nshomile, alihangaika sana
kufikiri lakini bahati mbaya hakupata kabisa jina
linaloendana na hilo hata kwa mbali.
Wamenifananisha na nani sasa mimi jamani?
Swali likapita kichwani mwake
****
WAKATI Kindo akitafakari mambo yanayomtokea
na kujiuliza maswali kadhaa, abiria wa basi
mojawapo liendalo mkoani wa Mwanza walikuwa
katika malalamiko. Kila mmoja na lalamiko lake
lakini yote haya yakiwa katika jambo moja tu.
Kuharibikiwa gari njiani. Yalikuwa yamepita
masaa manne tangu basi liharibike na mbaya
zaidi hapakuwa na basi la kampuni hiyo ambalo
lingeweza kufika na kuwachukua waendelee na
safari.
Wanaume walikaa katika makundi na wanawake
waliunda makundi yao pia. Walikuwa na nyuso za
furaha awali wakitarajia kuwa muda si mrefu
basi litatengemaa na safari kuendelea lakini
baadaye kila mmoja alikuwa amenuna baada ya
kugundua kuwa walivyodhani sivyo. Hapakuwa na
dalili ya basi hilo kutengemaa mapema.
Joram alitambua waziwazi kuwa uwezekano wa
basi lile kutengemaa ulikuwa mdogo sana, lakini
asingeweza kumwambia mtu yeyote yule kasoro
tu mafundi wenzake. Ambao kama yeye na wao
walishagundua shida hiyo.
Taarifa ama uhakika huu ulikuwa mbaya sana
kwa Joram. Tayari alikuwa amefanikisha
alichokuwa anataka na sasa lilibaki hitimisho tu
na sasa kinatokea kikwazo kikubwa kiasi kile.
Joram akaangaza macho yake huku na kule
kisha macho yakatua kwa mwanadada Salome
ambaye tofauti na abiria wengine yeye alikuwa
amejitenga na kukaa peke yake akiwa ameinama,
Joram akashikwa na imani akikumbuka kila kitu
alivyosimuliwa na Salome usiku uliopita kabla ya
kuamua kumchukua na kumsafirisha kinyemela
ilimradi tu afike Mwanza
“Salome yaani hapa sina hata senti!!! Sijui hata
tunafanyaje” alijisemea Joram kimoyomoyo huku
akimtazama yule binti tena.
Joram alikuwa katika hisia kuwa Salome huenda
anahisi njaa kwani tangu alivyomnunulia soda na
keki asubuhi basi hakuwa ameingiza kitu kingine
tena tumboni.
Lakini wakati huo Salome hakuwaza hata kidogo
juu ya njaa bali kichwani mwake zilipita
kumbukumbu mbaya na nzuri alizowahi kupitia
akiwa na mpenzi wake, Kindo. Akazikumbuka
ahadi zote walizowahi kupeana kipindi cha
nyuma. Akaikumbuka ahadi ya kutosalitiana
kamwe, neno usaliti likawa kama linamwandama
kichwani mwake na kujihisi mkosefu ajuaye kosa
analotaka kufanya. Salome alikuwa katika miadi
ya kutoa rushwa ya ngono kwa Joram iwapo tu
atamfanikishia safari yake ya Mwanza kwa
sababu hakuwa na pesa lakini alitakiwa kuondoka
na kuwa mbali kabisa na Kindo aliyeikataa
mimba yake. Machozi yakamtiririka Salome na
kujiona kama mzigo alionao kichwani ni mkubwa
zaidi tena ni kama uonevu uliokithiri.
Sasa gari lilikuwa limewaharibikia!! Tatizo jingine.
Kumbukumbu zikaendelea hadi alipoukumbuka
usiku usiosahaulika alipoamua kujiweka mbali na
Kindo huku akiweka kiapo.
“Kweli Kindo ni wa…..” kauli hii haikufika mwisho.
Mara akahisi kitu kikikimbia kwa kasi kubwa sana
katika mwili wake, hali hii huwa inamtokea akiwa
katika hali ya kawaida, lakini kwa hali aliyonayo
hatakiwi kuwa na hali hiyo.
Sintofahamu ikamkabili, akadhani hayupo sahihi
kufikiria juu ya kinachotaka kumtokea. Muda nao
haukumpa nafasi ya kufikiri mara mbili zaidi.
Damu!!
Salome alikuwa anavuja damu ya hedhi!!!
Hana pedi mahali popote pale.
“Joraaaam…. Joraam….” Aliita huku akipepea
mkono, kondakta aliyekuwa akihisi kuwa Salome
anaweza kuwa na njaa kali, alitimua mbio akiwa
na wazo hilohilo kuwa ni njaa inamsumbua.
Akamfikia na kukutana na kitu tofauti kabisa.
Salome alikuwa anavuja damu!!
Joram akafedheheka katika namna ya pekee,
hakutegemea jambo lile kabisa. Si kwamba
alimuonea huruma Salome bali alijionea huruma
yeye na kujipa pole kwa sababu alichokitaka
katika mwili wa Salome kisingeweza kutimia tena
akiwa katika hali ile ya kutokwa damu, Salome
akamweleza kuwa awaulize wanawake kama
wanaweza kuwa na pedi za akiba.
Joram akaondoka akiwa katika hali ya simanzi,
hakujali juu ya wakati mgumu anaopitia Salome
bali alijitazama yeye pekee na kujihisi anaonewa
kwa kuukosa mwili wa Salome baada ya msaada
wake wote ule hadi kumfikisha pale.
Joram hakurejea tena kwa Salome, badala yake
alifika mwanamama mwingine kabisa na
kumsaidia Salome, Salome akajisafisha na kuvaa
kinga ile.
Haya yalifanyika kichakani!!
Ina maana sina mimba ama!! Alijiuliza Salome
huku mapigo yake ya moyo yakienda kasi sana.
Asingeweza kupata jibu palepale, akajiahidi kuwa
akifika Mwanza kwa mwenyeji wake lazima
aende hospitali.
Akiongozana na yule mama waliporejea upande
lilipokuwa basi lao walikuta basi jingine limekuja
kwa ajili ya kuwachukua abiria baada ya lile
jingine kushindikana kutengemaa.
Utaratibu wa kuingia katika basi hili ambalo
lilikuwa la kampuni nyingine sharti uonyeshe
tiketi yako mlangoni ndipo unaruhusiwa kuingia.
Salome akajiweka kando akingoja wenye tiketi
zao waweze kuingia na mwisho yeye kwa
usimamizi wa Joram aingie na kuketi popote ama
kusimama kama basi limejaa.
Si anasafiri bure!! Atafanyaje?
Watu waliingia hadi mtu wa mwisho akaingia,
Salome alizunguka huku na kule kutazama ni
wapi Joram yupo. Hakumuona, akaanza kuulizia
wahusika juu ya kijana aitwaye Joram.
Ajabu! Hakuna hata mmoja aliyetambua jina hilo.
“Ni mfanyakazi wenu lakini, na nilimuona akiwa
hapa anashirikiana nanyi.” Salome alisisitiza
lakini kila mmoja alikuwa na haraka.
“Wewe leta tiketi huyo Joram sio tiketi dada…”
alikaripia dereva huku akiungurumisha gari na
kupiga honi mara kwa mara.
“Nimesafiri nanyi kutoka Dar es salaam jamani,
nilikuwa na Joram… nisaidieni tafadhali.”
“Ulikuwa umekaa siti namba ngapi?” kijana
mwingine mwenye daftari aliuliza huku akikagua
namba kadhaa. Salome akabaki kutumbua macho
tu kwa sababu hakuwa amekaa katika siti, bali
kujibanabana tu hapa na pale.
“Joram ndiye anajua….. sikuwa katika siti kaka
yangu, lakini nimesafiri nanyi….” Alizidi kujitetea.
“Duh… ningeweza kukusaidia dada yangu lakini
basi letu huwa hatusimamishi abiria hata mmoja,
yaani ni ‘level seat’……” wakati anamalizia kauli
ile tayari basi lilianza kuondoka, akalirukia na
kufunga mlango.
Likatoweka kwa mbwembwe.
**SALOME ameachwa na basi, yule aliyekuwa
amemshika mkono amemwachia!!!
Huku nyuma Kindo hamjui Rensho lakini
anatupiwa kombora na mama Salome juu ya
kutaka kuoana naye......
 
SEHEMU YA TATU
Basi lilitimua vumbi Salome asiamini kama ni
kweli ameachwa katika safari ile.
Joram alienda wapi sasa? Alijiuliza asipate jibu
na hapo akapatwa na hisia za hatua za mtu
nyuma yake. Akageuka na kukutana na sura ya
kijana ambaye amechafuliwa na oili na vumbi.
“Gari limekuacha sista?” aliuliza yule kijana,
Salome akatikisa kichwa kuashiria kukubali.
“Sijui hata nitafanya nini mimi…..” Salome
alisema kwa sauti ya chini huku akichuchumaa.
“Huna la kufanya zaidi ya kulala katika hilo gari
bovu halafu kesho utajua la kufanya…” ilijibu ile
sauti.
“Nini? Yaani nilale katika gari…. Hapana kaka
yangu, sidhani kama nitakuwa salama.”
“Kama kulala hapa nje ni salama zaidi waweza
kulala pia.” Alijibiwa kisha yule bwana alianza
kuondoka, ndipo Salome akagundua kuwa yule
mtu alikuwa muhimu kwake kwa muda ule tofauti
na makuzi aliyotaka kumletea.
“Samahani kaka yangu.. ni kuchanganyikiwa
huku, nisamehe maana sijui hata nimejibu nini….”
Salome alimsihi huku akimfuata kwa nyuma.
Kijana yule akasimama akiwa karibu na lile basi
bovu ambalo awali walikuwa wamepanda.
“Usijali, ingia ndani ya basi wenzangu wameenda
kutafuta chakula watarejea baada ya muda.”
Salome kwa kusuasua akapanda ndani ya lile
basi. Akachukua nafasi katika kiti chenye uwezo
wa kuchukua watu watatu. Kigiza kilishaanza
kuingia na bado waliendelea kuwa wawili tu
katika mazingira yale, mmoja akiwa chini na yeye
akiwa ndani ya basi.
Mapigo ya moyo yalikuwa yakiongeza kasi na
wakati mwingine yakirejea katika hali ya kawaida.
Salome kwa mara ya kwanza katika maisha yake
alijikuta akikosa amani kwa kiwango cha juu
kabisa na kuziona siku hizo mbili alizopitia kuwa
ngumu kupindukia katika maisha yake.
Hofu!
Dakika zilizidi kusogea na hatimaye likawa giza.
Wasiwasi nao ukazidi kuwa rafiki yake.
“Sista….” Sauti ikamkurupua kutoka katika
mawazo akaruka kutoa kiti alichokuwa amekaa
na kujisogeza pembeni kidogo kabla hajagundua
kuwa ilikuwa sauti ya yule kijana asiyemjua jina.
“Bee… naam!!...” akajiumauma akiwa haamini
kuwa yu katika giza nene kama lile yeye na
kijana asiyemjua jina.
“Naona wenzangu wamechelewa hawa sijui nd’o
wamepita kwenye vilabu vyao vya pombe huko
maana hawa….” Alijibu yule kijana sasa alikuwa
ndani ya basi akipiga hatua kuelekea alipokuwa
yule dada.
“Jikinge na baridi….” Kijana akamrushia shuka
lililokuwa likitoa harufu kali. Bila shaka liliwahi
kufuliwa zamani hizo na halikufuiliwa tena.
“Unaitwa nani ulisema….”
“Sal…Salome…naitwa Salome…” alijibu kwa sauti
iliyojaa uoga.
“Salome juu ya kaburi lako naliaaa….ule wa Dully
Sykes….” Alitania yule kijana. Salome
akajilazimisha kutabasamu huku akiikumbuka siku
anayomkubalia Kindo kuwa naye penzini, siku
hiyo Kindo alimuimbia wimbo huo kuanzia
mwanzo hadi mwisho.
“Mara kwa mara huwa mnalala barabarani kama
hivi..”
“Hapana ni mara moja moja tu kama leo hivi…”
alijibiwa.
“Hamuogopi..”
“Hata tukiogopa, je tuache kazi na kukaa
nyumbani tukisubiri kazi isiyokuwa na
changamoto. Salome, kila kitu katika maisha yetu
kina changamoto, ukiona kila kitu kimekunyookea
basi shtuka utajikuta ukiwa kitandani na
kutambua kuwa ulikuwa katika ndoto…basi ili
usiishi katika ndoto ni vyema kukabiliana na kila
hali. Kama hivi…” alielezea kwa kirefu yule kijana
na kisha akajitambulisha kuwa anaitwa Evans.
Hatimaye mwanga wa tochi ukaonekana na
kukatisha mazungumzo yao. Uoga wa Salome
ulikuwa umepungua.
“Wamefika hao na matusi yao… nilijua tu
walienda kulewa hao.” Evans alimweleza Salome
huku akiinuka na kuelekea nje.
Salome alibaki pale alipo kungojea nini kitatokea
nini. Evans alichelewa kwa takribani nusu saa, na
aliporejea alikuwa akiongozana na wenzake
wawili. Harufu kali ya pombe za kienyeji
ikatawala ndani ya basi.
“Wanadamu watu wa ajabu sana….” Alisikika
mmoja wa wale walevi kisha akaendelea, “yaani
unaua wenzako ili upate mali, matajiri wanatafuta
mali na sisi maskini hivi ni kitu gani tunatafuta
sasa. Wanadamu hawatosheki kabisa……”
“We Raja nawe umekariri….”
“Hakuna cha kukariri hapa yaani hii ya leo
inakuwa mara ya nne, kila huyu mzee akija
kuchukua magari bandarini, basi linachinja tena
barabara hii hii….”
“Yaani kesho ikitokea tena nd’o ntaamini
sasa…..” alijibu mlevi wa pili na kisha kimya
kikatanda takribani dakika ishirini, kila mmoja
akijaribu kuusaka usingizi. Salome na Evans
wakila ‘chipsi’ na maji.
Maneno waliyokuwa wakirushiana wale walevi
yalimfikia Salome lakini hakuyatilia maanani
sana. Akayapuuzia.
Simu ya Evans ilikatisha mlo kwa muda kidogo,
akajipekua na kupokea.
“Nini?....acha weeee!!!..Bonta kuwa siriasi
bwana….ehee….eheee…. Mungu wanguuu…”
Salome naye alijikuta amesita kula akabaki
kumtazama Evans aliyetaharuki.
“Ni nini tena…” Salome aliuliza.
“Ajali, basi limepinduka…”
“Basi gani?” aliuliza kwa mshangao..
“Salome mimi huwa siamini mambo ya ushirikina
lakini kwa hili sasa naamini..” alisita kisha
akaishusha sauti zaidi na kuwa katika
mnong’ono, “Si uliwasikia hao jamaa
walichokuwa wanabishana……yaani mwenye haya
mabasi kila akija kuchukua mabasi mapya
bandarini lazima basi lake moja lipate ajali na
kuua watu…. Basi lililokuacha limeua watu
Salome. Mungu wako mkubwa!!” alimaliza Evans,
Salome akatamani kuuliza kitu lakini hakujua ni
kitu gani alipaswa kuuliza, hofu ilikuwa
imemtawala. Yaani ameokoka kutoka katika ajali
katika namna ile ya kustaajabisha.
Ilishangaza!!!
****
SAA NANE kamili juu ya alama mishumaa
iliwashwa na sasa kila mmoja aliuona uso wa
mwenzake. Lakini hawakutazamana kwa muda
mrefu kabla ya kuanza kunong’ona kila mmoja
akimuuliza mwenzake imekuwa vipi hadi wapo
eneo hilo ghafla kiasi hicho. Hakuna aliyekuwa na
jibu lililonyooka.
Ikatoka amri ya kuizima mishumaa, kwa pamoja
ikazimwa halafu ikafuata amri ya kuwasha tena
mishumaa.
Sasa walikuwa wakitazamana na mshumaa
mkubwa zaidi mbele yao.
“Samahani nyote kwa usumbufu mlioupata ghafla
kwa kuwakurupusha majumbani mwenu na
kuwaita eneo hili. Lakini nadhani nyote mnajua
kuwa hii ni kwa madhumuni yetu sote. Na kama
ningewaacha mwendelee kulala basi
mngenilaumu kwa nini sikuwaamsha.
Basi namkaribisha katibu aweze kusema neno
kwa ufupi kisha kila mmoja afanye tafakari.”
Alimaliza na kumkabidhi rungu katibu ambaye pia
sura yake ilizibwa katika mwanga mkubwa.
“Salaam sana!!”
“Salaam!!”
“Kwa masikitiko na majonzi makubwa napenda
kuwaeleza kuwa mkakati umeingia doa. Mkakati
haujaweza kutimia. Ametutoroka tena bila
kutarajia!!! Ametorokea mbali kabisa… na kama
tulilala na kujipongeza kuwa tumemaliza basi si
kweli ametutoroka na hatujui ni nani
amemtorosha.” Aliweka kituo na kuacha wajumbe
kumi na wawili waanze kunong’ona wao kwa
wao.
“Kwani bila yeye hatuwezi kuendesha mkakati
wetu lakini.” Swali hili lilitoka kwa mjumbe
mmoja.
“Hapana hata kidogo, tunaweza kujipa moyo
katika siku za awali lakini baadaye yatazuka
mambo magumu sana na tutakuwa tumechelewa
sana. Wakati huu…” katibu alijibu kisha
akaendelea, “Kwa kifupi mkakati wa mjumbe wa
tatu na wenyewe pia ni batili……kazi hii
inahamishiwa kwa mjumbe wan ne Yakuza
Wenje. Tunahitaji utendaji mapema sana. Na
muwe na usiku mwema.” Alimaliza na kisha kila
mmoja akazima mshumaa wake, giza likatanda.
****
USIKU ulipita bila kuingiza chakula chochote
kinywani, akili yake kwa kiasi kikubwa ilikuwa
imevurugwa na watu wawili. Mama yake Salome
na mzee Gaspar Nshomile aliyeleta jina la
Rensho katika maisha yake.
Kindo aliamka kivivu vivu akikumbuka kuwa mzee
Gaspar na mama yake Salome wote waliahidi
kurejea tena.
Kindo aliutwaa mswaki wake akautia dawa na
kutoka nje kusafisha kinywa. Redio yake ndogo
ilitangaza habari za ajali mbaya ya gari yeye
akiwa nje na hakusikia lolote lile.
Aliporejea ndani akili yake iliwaza juu ya kula.
Tumbo lilikuwa wazi sana, lakini kabla ya kula
aliamua kukirekebisha kitanda chake kilichokuwa
kimevunjika, zoezi lililomchukua takribani dakika
kumi.
Akiwa tayari kuondoka, anakutana na fadhaa.
Mama yake Salome akiongozana na binamu yake
salome, nyuso zao zikitangaza shari walikuwa
wakijongea katika chumba chake. Kindo alitamani
kuyakimbia makazi yake, lakini akakumbuka
kwamba kuyakimbia makazi yake ni kuufanya
uongo kuwa ukweli, Kindo hakutaka kujiharibia
zaidi ilikuwa ni heri kupambana kuliko kukimbia.
“Karibuni, mama shkamoo!!”
Badala ya kujibu mama Salome alimkazia macho
yaliyotangaza chuki.
“Mama, hebu….. Kindo habari” binamu yake
Salome alimsalimia Kindo.
“Njema shem!!”
“Kindo, ni kitu gani kimetokea hadi ukafikia hatua
hiyo..”
“Joyce, hakuna kumuuliza uliza huyu…..
mwambie kilichotuleta.” Mama mtu aliingilia kati.
“Nisikilize shem walau kidogo tu nijieleze maana
mama hakunipa nafasi ya kujieleza…”
“Joyce…Joy…usitake kunipandisha hasira zangu
tena dakika hii…..hiyo iwe kauli yangu ya mwisho
kabla hujabadili mazungumzo hayo na kueleza
kilichotuleta…” aling’aka mama Salome. Joyce
binamu yake Salome akatii amri.
“Kindo, mguu wetu huu ni kituo cha polisi,
tunaenda kutoa taarifa juu ya kupotea kwa
Salome ambaye mara ya mwisho alikuwa kwako.
Sijui utajibu nini lakini hiyo ni taarifa
tumekuletea. Lakini huna haja ya kuwa na
wasiwasi, wakikusumbua sana Rensho na baba
yake watakuja kukutoa” Joyce alimaliza kujieleza,
mama Salome akamvuta mkono wakaendelea na
safari yao.
Kindo akaisahau njaa aliyokuwanayo, mambo
yalikuwa yamezidi kuwa magumu. Neno polisi
lilikuwa limemchanganya zaidi Kindo, hakuwahi
kuingia katika kosa lolote lililomsukumia katika
mkondo huo katika maisha yake yote, sasa
anaziona dalili zote za kuingia matatani.
“Salome rudi nyumbani mpenzi wangu!!!” Kindo
alizungumza peke yake huku akijikunakuna hapa
na pale pasi na sababu ya msingi.
Kindo hakutamani tena kuwa karibu na eneo lile
akakusudia kutafuta mahali ambapo atayatua
mawazo haya.
Upesi kama anayehofia kupokea ugeni mwingine
wa mashaka alifunga mlango wake. Na huku
akikimbia akafuata njia ambayo huipita mara
moja moja sana. Alianza kwa kutembea upesi
upesi, kisha akawa anakimbia kidogokidogo
hatimaye mbio zikaongezeka akawa anakimbia
kabisa kama anayefukuzwa.
Alikimbia bila kukoma hadi akakifikia kibanda
kimoja akaingia kwa pupa huku akiita jina la
‘mama’.
“Una nini wewe mtoto, mbona umekuja kwa kasi
hivyo. Amekwambiaje huyo mdogo wako kwani.”
“Nd’o nafika muda huu mama, sijaonana naye.”
“He! Yeye nd’o nimemuagiza akufuate kwako,
hamjazungumza!!” mama aliduwaa.
Kindo akamweleza kuwa hajafuatwa na mtu bali
amejileta mwenyewe hapo kwa mama yake.
“Hebu pumua kidogo halafu unidanganye sasa ili
nishawishike na hii kadi.”
“Kadi gani mama?”
“Kwani kadi ulizosambaza wewe huzisomi ama
tumepewa za aina tofautitofauti.” Alisema mama
yake na Kindo huku akiendelea kusuka ukili.
“Mama ujue sikuelewi, kadi.. kadi gani mimi
sijatoa kadi.” Alilalamika Kindo huku akijifuta
jasho.
“Hii kadi sio wewe unayetaka kumuoa huyu
Rebeca wa Nshomile wewe….. ama kutokwenda
kwangu shule unadhani hata majina sijui kusoma.
Mtazame aibu zimekushika umeshindwa kuileta
mwenyewe unaagiza watu, Salome wa watu
amekuvumilia weee!! Msichana wa watu yule
mchapakazi kweli. Unakurupuka kwenda kwa
huyu Re nani nani sijui…. Watoto wa kisasa
bwana…” mama yake Kindo alilalama katika
namna ya kumlaumu mwanaye.
Kindo akashusha pumzi kwa nguvu.
Alikuwa amechoka!!
**Akina nani hao waliofanya mkutano wa siri, ni
kitu gani wanahitaji?
* Rebeka Nshomile asiyejulikana kwa sura wala
jina mbele ya Kindo ni nani?
*Nini hatma ya Salome na utata wa mimba yake
 
SEHEMU YA NNE
“Kindo mwanangu yaani umeniaibisha ila basi
tu… yaani kati ya watoto wangu ambao
sikutarajia watanitia aibu basi ni wewe lakini
kumbe nilikuwa najidanganya tu. Wewe na baba
yako mmefanana akili kabisa….”
“Mamaaaa…mama!! Unafika mbali mama, ni nani
ameleta habari hizo za uzushi uliokithiri, ni nani
mama….mimi sijaagiza mtu yeyote kwako na
sielewi unaloniambia.” Kindo aligutuka na
kumkatisha mama yake.
Na hapo ghafla akashtukia amenaswa kibao.
Akajutia kumsahau mama yake alivyokuwa na
mikono myepesi anapokasirishwa na jambo.
“Pumbavu wewe, unadhani Salome ni muongo
kama wewe, unadhani mama yake Salome naye
ni mjinga eeh. Hujamfukuza Salome usikuusiku
na matusi juu mbwa wewe. Mama yake Salome
ametusaidia mambo mangapi, si ningekuwa
nimekufa mimi kama asingenipunguzia damu…
Kindo mwanangu pesa sio kila kitu katika maisha,
pesa ni makaratasi tu zinatafutwa zinapatikana
na zinapita. Utu wa mtu hausahauliki kamwe,
umemkosea sana heshima mama Salome kwa
ulichomfanyia mwanaye. Sio kumkosea mama
Salome tu, hata Mungu umemkosea sana Kindo,
hivi ndivyo nilivyokufundisha mimi eeh…. Sasa
naomba nisimalize kuhesabu hadi tano, uwe
umetoweka mbele ya macho yangu.. nadhani
nikisema hivyo unajua namaanisha nini.. moja,
mbili..” Kindo alimtambua mama yake vyema, si
yeye tu hata mtaa ulimtambua mama huyu kwa
jinsi alivyokuwa akizitendea haki hasira zake kwa
kupigana ama kupiga mtu. Kindo aliijua vyema
shughuli hii, na kwa sababu hakutaka kuadhirika
akaamua kutimua mbio kama alivyoamriwa ili
aweze kurejea tena baadaye mama huyu akiwa
ametuliza mzuka wake.
Wakati Michael anatimua mbio kuna mtu
alimtazama kisha akafanya tabasamu kisha
akanyanyua simu yake na kubofya namba kadhaa
na kisha kuzungumza maneno machache tu
kuelekea upande wa pili.
“Kimenuka kwa mama yake!!” kisha akakata
simu. Akamtazama tena Kindo alivyokuwa
amehamanika.
***
MAPAMBAZUKO yaliivamia anga na kuliondosha
giza, Salome akawa wa kwanza kuiona nuru,
akayapikicha macho yake na kutazama kushoto
na kulia. Akamuona Evans akiwa hoi usingizini
akakohoa kuweka koo lake sawa Evans
akayafunua macho yake.
“Mhh!! Asubu…..aah kumekucha..” alijing’atang’a
ta huku na yeye akiyapikicha macho yake
kujiweka sawa.
Wakapeana salamu, kisha Evans akasimama na
kupekua sehemu ya kuhifadhia mizigo.
“Kaoshe uso dada Salome..” alimweleza huku
akimkabidhi kopo la maji. Salome akapokea na
kutoka nje.
Wale walevi wa usiku nao walikuwa wameamka
tayari. Wakistaajabu kuwa Salome alilala katika
basi moja na wao wasijue, utani wa hapa na pale
ukazuka na kisha kupotea baada ya mafundi
wakiwa na spea kutoka mjini kuingia pale
kulishughulikia basi.
“Salome sasa hili basi linarudi Dar… itakuwaje
kuhusu safari yako wewe.” Evans alimvuta kando
Salome na kuzungumza naye.
“Kitu ambacho naweza kukushauri ni kimoja tu…
turejee wote Dar, kwa sababu umesema huna
nauli. Tukifika Dar basi mimi nitakufanyia
mpango pale staendi ili upate nafasi katika
mabasi ambayo kuna rafiki zangu wanahusika
nayo….. unaonaje wewe huo utaratibu maana
hapa barabarani kupata gari la bure dah sikufichi
dadangu itakuwa ngumu na hawa jamaa
hawawezi kunisubiri mimi nikupandishe gar indo
tuondoke” alieleza kwa ufasaha Evans na Salome
akabaki kuwa mwamuzi wa mwisho.
Hana pesa, hana simu ili ajaribu kufanya
mawasiliano na mtu yeyote. Kitu pekee
alichokuwanacho ni Evans…..
“Ulichosema ni sahihi Evans kaka’ngu, lakini huko
Dar penyewe ni uhakika wa kufika na kupata gari,
na kama si uhakika, mimi nitaishi wapi sasa.
Maana…ni stori ndefu sana kuhusu Dar lakini
amini kuwa sina mahali sahihi pa kufikia.”
“Usijali, usijali kuhusu pa kufikia na kuhusu
kupata gari hilo la bure hakika tunatakiwa kuvuta
subira siku mbili tatu…si unajua cha mtu eeh…”
“Nimekuelewa sana bro…”
“Twend’zetu sasa..” alimalizia Evans huku
akielekea kwenye basi.
Safari ya kurejea jijini Dar es salaam!!
Salome akiwa msichana pekee ndani ya basi lile.
***
“Ndo wenyewe”
“Sio hao bwana…”
“Ndio wenyewe aisee….”
Sauti mbili zilikuwa zikipingana huku zikitilia
umakini muungurumo wa gari lililosikika kutokea
mbali. Lakini licha ya kupingana hakuna hata
mmoja aliyesahau wajibu wake. Umakini ulikuwa
wa hali ya juu!!
Mtego ukanasa!!
Walikuwa wenyewe waliokuwa wakiwangoja.
Upesi gogo kubwa likarushwa barabarani
likifuatia na jingine.
Gari ile ilipofika ikafunga breki za ghafla, na huo
ukawa mwisho wa safari ile.
Mtutu wa bunduki ukalitazama basi lile na kisha
amri ya upesi ikatolewa kuwa abiria wote
watelemke kutoka katika basi hilo.
Bunduki haiongopi na haina mjanja!!
Salome akawa wa kwanza kutelemka huku akitoa
kilio cha woga na kitetemeshi cha taharuki.
Macho yalikuwa yamemtoka pima, nyuma yake
alifuata Evans na wenzake.
Walikuwa wametekwa!!
Mteka nyara mmoja akasogea kando akaitoa
simu yake na kubofya namba kadhaa kisha
akasikiliza upande wa pili.
“T 670 AJZ…..Ok ndo wenyewe….. binti
mmoja…..sawa sawa bosi” alimaliza na kurejea
kundini. Bila kupoteza muda jumla ya watu
watano wakaamuliwa kulala chini, wakatii amri.
Kishja kama kipanga anyakuapo vifaranga,
mtekaji mmoja mwenye mwili mkubwa
akamnyakua abiria mmoja akamziba macho na
mdomo na kuanza kutimua naye mbio.
Abiria waliosalia wakawekewa tego kana kwamba
bado wapo chini ya ulinzi, wakabweteka na
kuendelea kulala chini bila kujitikisa.
Walikuja kuteguliwa na raia wengine baadaye
kabisa.
Evans akawa wa kwanza kubaini kuwa Salome
hakuwa pamoja nao.
Salome alikuwa kusudio la watekaji wale.
“Maskini wee!! Salome weee.. hakuniambia hata
kisa chake cha kumkimbiza Dar.. Mungu wangu
wee…” aliugulia Evans asieleweke hata kwa mtu
mmoja.
Kila mmoja akaujali uhai wake.
Hakuna aliyekubali kuendelea kuwa porini kule
kwa ajili ya kumsaka msichana wasiyemjua. Kwa
shingo upande Evans akaungana nao.
Wakatoweka.
Salome hakujulikana yu wapi tena!!
***
“WELLDONE BOYS!!” Sauti nzito kutoka kwa
pande la mtu ilisifia huku akiwagongagonga
migongo yao vijana wanne waliokuwa mbele
yake.
“Yaani mmefanya kwa uhakika na kwa muda
muafaka!! Nimependa sana.” Alizidi kuwatukuza
vijana wake.
“Lazima watambue mimi ni nani…..” alihamia
upande wake na kujisifia. Kisha akanyanyua simu
yake ya kiganjani akapiga mahali.
“Naam!! Yakuza Wenje naongea….Nimeimaliza
kazi yako mkuu… sasa tunaweza kuendelea…”
Alisema na upande wa pili huku akijisikia fahari
sana kwa maneno yaliyokuwa yakimtoka.
“Don, jioni uje peke yako nikukabidhi halali yenu.”
Alimaliza na kuwaaga wale vijana. Tabasamu
halikukauka katima uso wake wenye furaha.
Baada ya Don na wenzake kuondoka. Yakuza
alicheka kwa sauti ya juu, alicheka hadi machozi
yakamtoka.
“Watanikoma mwaka huu wajingawajinga wa
Sinza Lego…. Yaani lazima wanijue Yakuza kama
nimerejea tena kushika usukuni, pumbavu zao.
Walidhani nd’o nimeanguka moja kwa
moja…..sasa narejea kwa kishindo..” alisema
haya kama anayeapiza kwa sauti ya juu. Kisha
akajimiminia waini katika glasi na kuimimina kwa
mipigo miwili mdomoni, glasi ikawa tupu.
Yakuza aliitazama saa yake na kuona kama
muda hausogei mbele hata kidogo, alikuwa na
kiherehere cha kupata alichokitaka baada ya kazi
iliyoonekana ngumu halafu yeye akaifanya
nyepesi.
Yalikuwa majira ya saa nane mchana Yakuza
alitakiwa kungoja hadi majira ya saa mbili usiku
ili aweze kupata uhakika wa ahadi aliyopewa
yeye na wenzake iweze kutimia.
“Mwenyekiti na katibu lazima washangae,
nimeweza vipi kufanya upesi kiasi kile.” Aliwaza
huku akijitafutia mahali pa kwenda kupoteza
muda ili muda wa ahadi ufike.
****
“Kindoo!!” sauti kali ilimuita kwa mbali, akageuka
huku akiwa bado anakimbia. Mtu aliyekuwa
anamuita na yeye alikuwa anakimbia. Kindo
akapatwa na uoga huenda mtu yule ameagizwa
na mama yake aweze kumkamata na kumrudisha
nyumbani kitu ambacho Kindo hakuwa tayari.
Akalazimika kuendelea kukimbia zaidi na zaidi,
lakini yule aliyekuwa anamfukuza alikuwa
anakimbia zaidi yake, kadri Kindo alivyoenda
mbili ndivyo yeye alivyozidi kumrudisha nyuma
katika namna ya kumkaribia zaidi.
Hatimaye Kindo akasalimu amri, akaamua
kutumia mpango mwingine wa kumdhibiti yule
bwana. Akaokota jiwe kubwa huku akiwa
anahema juu juu.
“Uki….ukiniso….ukinisogelea nakupasua jiwe…
nakupa…” Kindo akiwa anahema alimchimba
mkwara yule bwana ambaye walikuwa
wakifahamiana lakini hakuwa mtu wake wa
karibu kiasi kile.
“Kindo la!! Ni kitu gani tena kimekusibu unataka
kuniponda mawe mimi….Kindo..” alitahamaki yule
bwana.
“Nani amekutuma unikimbize…..nani?” alihoji
Kindo akiwa bado amekamata jiwee mkononi.
“Kindo..sijaagizwa na mtu ujue lakini hii ni kwa
usalama wako.”
“Usalama wangu naujua mwenyewe, nyie watu
mbona mnanifuatafuata sana…. Kwanini, si
mniache lakini….” Alilalama Kindo, yule bwana
akamsogelea na kumfiukia, akaushusha ule
mkono wake ulioshika jiwe. Kindo akakubali
kuliachia jiwe.
“Kindo, ni kitu gani kimefanya mpaka utafutwe
eeeh!! Mimi ni jiranmi yako, sawa tuliwahi
kugombana lakini bado wewe ni jirani yangu.
Ugomvi wa kuwania kukinga maji bombani
hauwezi kuvunja ujirani, ni kitu gani umekosa
Kindo hadi utafutwe…”
“Nani ananitafuta, mimi sitafutwi na mtu..”
alipinga Kindo.
“Kindo! Difenda imeshuka na kuvamia chumba
chako, maaskari wenye sare kabisa wamevamia
kwako na sasa unasema hautafutwi, watu
wamekuja na picha yako unakataa hawakutafuti
wewe….Kindo unachanganyikiwa mdogo wangu.
Sikia Kindo kama lipo ulilofanya na sistahili
kuambiwa basi mimi nimekupa tu hii taarifa. Kazi
ni kwako kusuka ama kunyoa….” Alimaliza kwa
kauli hiyo na kisha akaanza kuondoka akimwacha
Kindo akiwa anatetemeka.
“Dula!! Dula…. Nani wananitafuta mimi… dulla
wame…” akasita kuzunmgumza baada ya
kugundua kuwa Dulla hamsikilizi tena na tayari
yupo mbali…..
Kindo akaketi chini na kuanza kulia.
Kilio cha mtu mzima!!!!
Hajui kosa lake lakini anasakamwa kila upande!!!
**KINDO bado hana nafuu…..
**SALOME ametoweka kusikojulikana…
***YAKUZA ni nani na anafurahia makubaliano
yapi??
 
"Ni jambo jema sana kuchukua MAAMUZI....
Maamuzi hayo yakiwa sahihi ni faida sana kwako,
Maamuzi yasipokuwa sahihi yawezekana ukapata
muda wa kujirekebisha... lakini kutochukua
MAAMUZI kabisa ni ugonjwa ambao utakula
mwili na moyo wako. Utakuwa mfu angali
unapumua bado! Jifunze kuchukua MAAMUZI!"
Na hii ni sehemu ya TANO!
Kutokwa machozi? Hii haikuwa namna ya kupata
suluhu ya tatizo lilokuwa linamkabili. Kindo
alisimama tena na kutazama pande kuu nne za
dunia kana kwamba zote zimewekwa miba na
hawezi kuvuka hatua moja mbele.
Alifikiria kusonga mbele, lakini kile kitisho kutoka
kwa jirani yake kuwa anasakwa na polisi wenye
hasira kilimfanya asifikirie hata kidogo kwenda
nyumbani kwake.
Mama yake mzazi alikuwa amecharuka haswa na
asingeweza kukabiliana naye kwa wakati huo.
Akawakumbuka marafiki zake watatu, ambaye
alikuwa jirani zaidi alikuwa ni Maulidi. Kindo
akaamua kuchagua eneo hilo kama sahihi zaidi
kwa wakati huo.
Kwa mwendo wa kiaskari alikamata njia moja
kwa moja kwenda nyumbani kwao Maulid.
Mwendo wa dakika kumi na tano alikuwa
ameikaribia nyumba ambayo Maulid alikuwa
akiishi humo, kufikia hapo alipunguza mwendo
huku akiuongoza uso wake usiwe katika uoga
aliokuwanao.
Chumba kimoja cha Maulid kilikuwa wazi, kwa
jinsi walivyozoeana Kindo hakuona ajabu kuingia
bila kubisha hodi.
Akamkuta Maulid kitandani akiwa ameuchapa
usingizi.
Kindo akamtikisa kidogo Mau akashtuka.
“Yalaweeeee!! Yalabi…..” akataharuki huku
akiuegemea ukuta kwa mgongo, mikono yake
ikimsihi Kindo asimfanyie jambo baya lolote lile
kama alikuwa na nia hiyo. Kindo alistaajabu na
yeye akaganda vilevile asipige hatua yoyote
mbele.
“Mau…. Umekuwaje wewe…. Mimi nakuja hapa na
matatizo yangu na wewe unaanza kupiga
makelele tena, kulikoni!!” alihoji Kindo, sasa
alipiga hatua mbele na kutaka kuketi kitandani.
“Weeeee!! Kindo Kindo…. Naomba usiguse
kitanda changu nakuomba tafadhali shehe!!”
alitoa onyo Mau kisha akaendelea, “Kindo ka
wewe ni mzaliwa wa Iringa ukafungwa hirizi za
huko basi mimi nitakusulubu kizanziberi yahe…
niache Kindo…”
Macho yakamtoka Kindo baada ya kusikia
maneno hayo mapya kabisa kutoka kwa rafiki
yake.
“Mau… Mau ujue nina matatizo acha utani
wako…” wakati anamalizia kauli hii huku
akijilazimisha kutabasamu kama kwamba
hajakerwa na lolote Mau alichomoa sime kutoka
chini ya godoro lake na kulishikilia kikakamavu.
“Upige hatua moja mbele niichomoe hiyo shingo
yako mara moja!! Upige hatua moja nyuma
nisambaratishie mbali huo uti wako wa mgongo
mwanga mkubwa weye!!” alibwata Maulid, macho
yake akiwa ameyakodoa kumwelekea Kindo.
Hakuonyesha dalili hata chembe ya utani,
alikuwa anamaanisha anachoamuru.
Kindo akafadhaika na kubaki akiwa ameachana
midomo yake kwa mshangao.
“Bwan’Kindo sie twakuamini rafikizo, kwamba
twapambana pamoja kumbe mwenzetu mwanga
mkubwa wewe. Waizuia riziki isikae nasi bali
ikufuate weye. Watuongopea Salome mpumbavu
kumbe umemtoa kafara mwanaharamu wewe
mpenda utajiri, sasa umekuja kunitoa na mimi
kafara nasema Kindo hapa umegonga mwamba
na iwapo utatoka hai ndani ya nyumba hii basi
nisikuone tena mbele ya macho yangu tena na
usikumbuke kama mimi Mau nimewahi kuwa
rafiki yako walah… na nikikumbwa na madhara
yoyote yale Kindo, walah nakutafuta popote ulipo
nakuua. Sasa kabla John na Masalu hawajaja
kukuulia hapakutokana na ushirikina wako
uliokubuhu naomba utoweke mara moja hapa
ndani, toweka mshirikina wewe!!” alitoa karipio
kali huku jasho likimtoka na mikono
ikimtetemeka. Kindo hakuweza kutabasamu tena,
akajikaza na kuomba huruma ya Maulid, “Mau
rafiki yangu nakuomba tafadhali nisikilize japo…”
akiwa hajaimaliza kauli yake Maulid akamkatisha,
“Nitaitenganisha shingo yako sasa hivi walah!!”
na hapo akaanza kuiburuza panga sakafuni kama
anayejaribu kuitia makali zaidi.
Kindo hakungoja kushuhudia kifo chake. Upesi
akaanza kutimua mbio, akijigonga katika ndoo
iliyokuwa na maji, akayumba akajikwaa kwenye
beseni tupu lililokuwa nje. Kisha akauona uelekeo
na kuendelea kukimbia akiwa na hofu kuu juu ya
hali inayomkabili.
Macho yalimchonyota na machozi yakamtoka.
Machozi ya uchungu na uoga. Machozi yaliyoziba
macho yake asiweze kuliona bonde lililokuwa
mbele yake, akaliingia bonde lile na kupiga
mweleka chini.
Kiza kikatanda machoni!!
****
MUZIKI uliwaburudisha wateja wa rika mbalimbali
walioamua kuimaliza siku yao katika baa hiyo
maarufu sana pembezoni kidogo mwa jiji. Wateja
ambao walishaanza kulewa waliinuka na chupa
zao mikononi na kuanza kukata mauno huku
wakijaribu kwenda sawa na ala za muziki huo.
“Dennis hivi huwa unapapendea nini hapa?”
kijana mmoja alimuuliza mwenzake.
“Kwani tangu ufike hapa umeboreka, ukimaliza
bia moja basi anakuja muhudumu mrembo
anakuhudumia, ukianza kunywa mara mlevi
mwingine anakata mauno halafu usiku sasa yale
mambo yetu.. wanawake na kanga moja
iliyolowanishwa maji wanajiweka pale kati, yaani
hata kama unajifanya we mlokole vipi kwa wale
yale mambo lazima utamani!!!” alijibu Deniss
huku akifurahia kila neno analosema.
“Halafu ukishatamani…”
“Ukishatamani basi pesa yako inazungumza tu…
bei zao za kawaida sana!!”
“Yaani unanunua wanawake tena!!”
“Yah! Ulidhani watakupa bure tamu yao….” Deniss
alijibu huku akimshangaa rafiki yake.
“Yaani we jamaa kwa wanawake nd’o maana
huwa mnagombana na Sam kila siku….”
“Sikia Don, yule Sam yule atakuwa na matatizo
yule si bure atakuwa hanithi..” Deniss akatoa
kauli iliyowafanya wacheke kwa pamoja.
Kicheko walichotoa kilikuwa kicheko cha pesa,
naam! Pesa nyingi kwa kazi ndogo kabisa. Na
Don alikuwa akihesabu masaa ili aweze kukutana
na mzee Yakuza waweze kumalizana.
Baada ya dakika kadhaa Don aliaga kuwa
anaenda msalani. Aliondoka kwa mwendo wa
kuyumbayumba huku akipiga mluzi. Deniss
akamsindikiza kwa macho nyang’anyi mwenzake
hadi alipotokomea.
“Yaani Don bwana….” Akatokwa na kauli ile kisha
akatikisa kichwa kushoto na kulia akaendelea
kunywa pombea yake.
Baada ya dakika kumi na tano Don akarejea,
lakini safari hii hakuwa kama alivyoondoka
alikuwa amejawa wasiwasi na akili yake haikuwa
na nutulivu kabisa jambo ambalo Deniss
aliling’amua mapema kabisa.
“Don! Vipi kaka!!”
“Aaamh!! Hapana, hakuna kitu….”
“Hakuna kitu wakati unaonyesha wasiwasi kabisa
usoni.”
“Nimesema hakuna kitu Denny vipi mbona hivyo.”
Sasa alijibu kwa jazba.
“Ushakasirika mtoto wa mama wewe ninaenda
msalani akija muhudumu mwambia aongezea bia
hapo…” Deniss hakujali jazba za Don, akaaga na
kuondoka. Kabla hajafika msalani akambana
muhudumu mmoja kwenye kona. Don hakuwa na
muda wa kumtafakari Denny maana kuna jambo
lilikuwa linapita katika kichwa chake lililoondoka
na utulivu wote.
Dakika kumi baadaye Deniss machachari naye
akarejea akiwa ametaharuki zaidi ya Don!! Yeye
hakuweza kuhimili wasiwasi wake. Ikaja zamu ya
Don kumuuliza mwenzake kulikoni!
“Don, nimekojoa damu kaka…. Damu nyingi Do…
Don nini hiki eeh!!”
“Whaaat!! Damu?” alishangaa Don
“Sio damu Don, damu nyingi sana..nimechafua
choo huko…halafu nimebanwa tena Don… nini hiki
eeeh!!” akiwa amepagawa waziwazi Denis alihoji.
Don hakuwa na la kusema akabaki kumtazama
Don anavyoropoka kwa sauti yenye kitetemeshi.
“Denny, tuondoke hapa.. maana usivyojua
kuishusha sauti yako basi kila mmoja atajua
unakojoa damu…” Don akazungumza huku
akisimama, Denny akafuata nyuma. Wakakodi
taksi iwapeleke Ilala boma. Nyumbani kwa Don.
Walipoingia ndani sebuleni kwa Don, Don
akafanya jambo lililomuacha Denny mdomo wazi.
Akaifungua zipu yake upesi upesi akashusha
suruali yake chini.
Denny akatazamana na tupu ya Don iliyotapakaa
damu!!
Na yeye bila kujua nini anafanya akaangusha
suruali yake.
Wote walikuwa wanavuja damu. Lakini kwa
Denny kulikuwa na la ziada, damu yake
ilichanganyika na usaha!!
Hakuna aliyeweza kusema neno lolote. Kila
mmoja alikuwa anatetemeka!!
“Denny….nini hiki sasa!!”
“Damu hiyo Don ama unaona nini wewe!!” alijibu
kwa dhihaka huku akizidi kujishangaa.
Simu ya mkononi ya Don iliita lakini hakunyanyua
mkono wake kuipokea, kisha ikaanza kuita simu
ya Deniss na yeye alisonya tu bila kufanya
jitihada zozote zile za kuipokea!!
Hali walizokuwanazo zilisikitisha.
WAKATI Don na Deniss wakihaha juu ya tatizo
lililowatokea ghafla. Mwenzao aitwaye Samson
ama walivyomzoea kwa jina la Sam alikuwa
katika dimbwi la mawazo akifikiria juu ya jicho la
mwanadada likimwaga machozi huku likimsihi
msaada. Hakuwahi kulitambua jina lake lakini
sura ilikaa vyema katika kichwa chake.
Kufikia wakati huo alikuwa amebwia chupa
kadhaa za ulabu akiwa nyumbani kwake lakini
hali ile iliendelea kumweka katika wakati mgumu.
Aliwahi kushuhudia maiti na amewahi kuua
kikatili sana mara kadhaa na akasahau mara
moja. Ajabu safari hii ambayo hakuua mtu
anastaajabu sura ya mlengwa inasafiri katika
kichwa chake kwa kasi ya ajabu.
Yule ana nini lakini? Eeh yule msichana ni nani
kwani? Samson aliiuliza chgupa yake ya bia lakini
haikumjibu lolote.
Akaamua kuinyayua simu yake ili awaulize
wenzake kama wanakumbwa na hali hii.
Akaanza kumpigia Don, simu ikaita kwa muda
mrefu bila kupokelewa. Akapiga kite cha
ghadhabu kisha akapandisha juu kidogo
akakutana na namba ya Deniss na yenyewe
ikaita bila kupokelewa.
“Mabwege wamelewa hadi wamezima kabisa…
shenzi kabisa!!” akajipatia majibu yake juu ya
wenzake ambao bila yeye kujua kama waliziona
simu zake zikiita wakashindwa kupokea.
“We binti ni nani nakuuliza si unijibu, kama hauna
jibu na utoke katika akili yangu. We unadhani
ningeweza kukusaidia katika eneo lile, hukuona
kama wenzangu walikuwa na bunduki, wangeniua
wale ohoo!!” Sam aliendelea kuzungumza peke
yake huku akiwa amefumba macho yake akijenga
taswira ya binti huyo.
“Sikia binti ujue unanikosea sana kuendelea
kuniandama mimi niliwazuia na wewe ulikuwa
shuhuda kabisa. Ningefanya nini sasa baada ya
pale eeh niambie sio kukaa unaniandama mimi tu
hapa. Ningewakaba mashati ili wanipige risasi
eeh ndo ulitaka nife siyo … nakuuliza wewe
nijibu….aaaargh!!” hatimaye alipiga kelele na
kufumbua macho yake. Hakika alikuwa
anaathiriwa na kitu alichokuwa anakiona
kichwani mwake.
Alisimama akatembea kwenda mbele na kurudi
nyuma akiwa na bia yake mkononi akiibugia kwa
fujo.
“Hata hivyo unatakiwa kujua kuwa nilikuwa kazini
binti sawa eeh!! Nilikuwa nasaka pesa…”
alimalizia kwa kauli hii sauti ikiwa chini kabisa
kama anayemnong’oneza mtu. Bia ikiwa kando
na mikono yote miwili ikikisugua kichwa chake na
kukibinyabinya.
Hatimaye akapitiwa usingizi akiwa palepale
katika kochi na mikono yake ikikipakata kichwa
chake.
Alikuja kustuka baadaye akiusikia mlango wake
unagongwa kwa nguvu sana. Akapiga mwayo
mkubwa huku akisimama na hapo akili yake
ikawakumbuka akina Don na Deniss juu ya ahadi
ya kugawania pesa yao nyumbani kwake.
Akafanya tabasamu dogo kisha akajongea
mlangoni.
Akaufungua mlango pasi na kuitazama saa
iliyoonyesha kuwa ilikuwa imetimia saa nane na
dakika kadhaa usiku. Yeye alidhani kuwa ni saa
mbili bado na ikizidi sana saa tatu.
Alipotoa komea mara mlango ukasukumwa ndani
kwa nguvu, akajirusha kando akiamini ni vurugu
za rafiki zake baada ya kupata pesa.
Lakini macho yakashuhudia kitu tofauti. Kiumbe
kisichotambulika sura yake kikivuja damu katika
kichwa chake, mikononi na uso usionekana walau
kidogo kiliangukia magoti, kisha huku kikikoroma
kikatokwa na maneno machache sana.
“Mmeniu….uua…”
Kisha mdomo ukatangulia ardhini, na mwili wote
ukafuata kwa kishindo. Kiumbe kile kikahema
kwa nguvu mara moja kisha kikatulia tuli!!
Sam akatokwa na yowe la uoga, na alipoitazama
saa yake akaingiwa uoga zaidi.
Ilikuwa saa nane usiku!!!
**NINI KIMEWATOKEA DON na DENISS
**KINDO amekataliwa na rafiki zake….
Atakimbilia wapi na ni nani anayezua haya
 
SEHEMU YA SITA
Alipotoa komeo mara mlango ukasukumwa ndani
kwa nguvu, akajirusha kando akiamini ni vurugu
za rafiki zake baada ya kupata pesa.
Lakini macho yakashuhudia kitu tofauti. Kiumbe
kisichotambulika sura yake kikivuja damu katika
kichwa chake, mikononi na uso usionekana walau
kidogo kiliangukia magoti, kisha huku kikikoroma
kikatokwa na maneno machache sana.
“Mmeniu….uua…”
Kisha mdomo ukatangulia ardhini, na mwili wote
ukafuata kwa kishindo. Kiumbe kile kikahema
kwa nguvu mara moja kisha kikatulia tuli!!
Sam akatokwa na yowe la uoga, na alipoitazama
saa yake akaingiwa uoga zaidi.
Ilikuwa saa nane usiku!!!
___
KIZA kilichotanda katika macho yake kilianza
kufifia na baadaye ikafuata nuru baada ya
mauzauza ya hapa na pale. Alijaribu kuunyanyua
mkono wake lakini ulikuwa mzito hakuweza!!
Akayahisi maumivu mguuni mwake, akatamani
kulalamika lakini midomo ikawa mizito
kufunguka. Akabaki kulalamika katika nafsi kisha
akajikakamua na kisha kujinyanyua kwa nguvu
zote.
Akafanikiwa kukaa kitako, harufu ya ubani na udi
kwa mbali ikafuatia katika pua zake.
Mara ya mwisho alikuwa anamkimbia Maulid na
hatimaye akajikwaa katika bonde na kupoteza
fahamu lakini hayupo tena bondeni, amevikwa
suti ya gharama na yupo mahali asipopajua.
“Nipo wapi hapa?” aliuliza kwa sauti ya chini
ilhali yupo peke yake. Hakuna wa kumjibu!!
Mara mlango ukafunguliwa, wakaingia wanaume
wawili walipotazamana wao wakatabasamu na
kutoweka. Baada ya sekunde nyingi kidogo
akaingia mzee mtu mzima.
Baba yake Rensho!!
Mauzauza!!
Safari hii hakuwa katika sura yake ya kikaidi
ambayo inasadifu kauli yake ya kupigana vita vya
Kagera.
“Kindo… Emmanuel Kindo….mkwe wangu
mwenyewe huyooo… dume la mbegu.” Mzee
Gaspar Nshomile alimsifia huku akichanua
tabasamu mwanana. Tabasamu lile likaifungua
akili ya Kindo upya. Kabla mzee Nshomile
hajamtembelea pale nyumbani kwake na
kumweleza juu ya mahusiano baina yake na
mwanaye kuna mahali aliwahi kumuona miaka
kadhaa nyuma tena akiwa katika mavazi ya aina
ile ya suti za bei mbaya.
Nilimuona wapi huyu mzee? Kindo alijiuliza huku
akizidi kujilazimisha kukumbuka. Lakini hakupata
kumbukumbu zaidi ya aliyokuwanayo….
Mzee Nshomile akatoweka akimwacha Kindo
katika dimbwi la mawazo. Mlango ukafungwa
tena!!
Baada ya dakika takribani tano wakaingia wale
wanaume tena, wakamuamuru Kindo asimame,
aliposuasua wakamsaidia kunyanyuka.
“Mnanipeleka wapi lakini? Mimi nimewakosea nini
jamani ndugu zangu…. Na hapa ni wapi jamani…”
aliuliza maswali mfululizo lakini hakuna hata
aliyekaribia kumjibu.
Wakamwongoza hadi katika chumba kingine,
wakaufungua mlango na kumsukumia ndani ya
chumba hicho kisha wakafunga kwa nje
wakizipuuzia kelele alizowapigia za kuomba
msaada.
HOFU NDANI YA CHUMBA.
Macho ya Kindo yalishuhudia mandhari ya
kuvutia, japo alikuwa anatetemeka alikiri kuwa
chumba kile kilikuwa cha kifahari. Alitazama
kabati akatazama marumaru, akakitazama na
kitanda….. hapo macho yakasita, kitanda kile
kikubwa hakikuwa kitanda pekee.
Palikuwa na kiumbe juu yake, kiumbe laini kabisa
upande wa mgongo uliokuwa wazi, kisha ile nguo
laini ambayo kilijivika kiumbe kile ilifanya umbo
lake lililokatika vyema na kuichora miinuko miwili
katikati ya umbo lake kuonekana vyema. Mgongo
wake ulifunikwa kiasi na nywele ndefu nyeusi.
Mapigo ya moyo ya Kindo yakaongezeka kasi,
hofu ikahama na kuingiwa na matamanio kiasi
flani. Alikiri kuwa yule binti alikuwa ni mrembo
zaidi ya Salome wake.
“We we ni nani….” Aliuliza kwa sauti ya chini
kabisa Kindo bila kufanya hatua yoyote ile mbele.
Kile kiumbe kikatoa sauti ya chini pia ya kicheko.
“Unacheka wakati nakuuliza we ni nani na hapa
mmenileta kufanya nini?” akahoji kwa ukali…. Kile
kiumbe kikacheka tena na sasa kikajigeuza
taratibu na kuuonyesha uso wake kwa Kindo.
Asalalee!! Kifua cha yule binti kilibeba mzigo
mdogo kabisa wa matiti na hapakuwa na
njitihada zozote za kuyaziba. Kindo uroho
ukamwingia, akasahau kuwa hajapata jawabu la
kwanini amevalishwa suti, akakutana na mzee
Nshomile na sasa yu pamoja na yule binti katika
chumba asichokijua.
Macho ya Kindo yakabaki kutumbulia kifua cha
yule binti.
“Kindo umekuwa mkaka kweli…..” kauli ya
kimahaba kutoka kwa yule binti ikarejesha
wasiwasi.
Amenijuaje huyu kiumbe!! Aliduwaa Kindo.
Akanyanyua macho yake kumtazama yule
mwanadada.
Akamuta anatabasamu na vishimo vidogo
vikaonekana katika mashavu yake.
Sura ngeni kabisa!!
“We ni nani na umenijuaje…” alihoji Kindo.
“Emmanuel Kindo….. si ndo wewe jamani ama…
hivi ulishaacha kukojoa kitandani hahahahah!!”
sauti laini ikazidi kumjaribu Kindo.
Kukojoa kitandani!!! Huu msamiati ukamduwaza,
ni kitendo cha miaka mingi iliyopita alipokuwa
mtoto mdogo bado.
“Hivi ulifaulu kuingia form one maana ulikuwa na
akili we mtoto…”
Huyu ni nani lakini jamani!!! Kindo alizidi
kuhamanika.
“Wewe ni nani nakuuliza? Nitakujeruhi
usipojieleza na hatakuwepo wa kunifanya
lolote…” alikaripia Kindo huku akijikaza na kupiga
hatua kumsogelea.
Binti yule akacheka sana kisha akasema, “Yaani
ulikuwa unapigwa nakusaidia mimi kila siku leo
hii unipige looh! Unafurahisha Kindo wewe….”
Lahaula!! Kindo akaruka nyuma na kujibana
ukutani akimwacha yule binti akiwa anacheka
hadi kutokwa na machozi.
Kindo alizidi kujigandamiza ukutani, kijasho cha
uoga kikimtoka.
“We Re…Rebeka wewe…..we Rebeka…..” Aliita
huku akizidi kujigandamiza ukutani…
Kindo alikuwa amekutana na ajabu zito na
mauzauza ya aina yake, macho yake yalikuwa
yakimtazama mtoto wa zamani ambaye alizikwa
akiwa na miaka kumi tu! Alizikwa akasahaulika
enzi hizo na kisha akafutika katika vichwa vya
waliomjua baada ya miaka kadhaa.
“Kindo mkeo amefariki pole sana!!” Kindo
akaikumbuka kauli ya mzee wake ambaye
alikuwa amezoea kumwita Rebeka kuwa ni mke
wa mwanaye.
Yule mtoto yu hai sasa akiwa mbele ya Kindo, si
mtoto tena bali mtu mzima.
“Ulikufa Rebeka…..ulikufa..” sauti yenye
kitetemeshi cha uoga ilizidi kutoka katika kinywa
cha Kindo.
“Hata wewe unakufa muda si mrefu!!” yule binti
akamjibu kwa furaha kabisa.
“Noo.. usiniue Rebeka usiniue…” alisihi.
“Sina ujanja Kindo lazima niku…..” akasita kisha
akatega sikio kama anayesikiliza kitu.
“Anakuja… anakuja Kindo… anakuja…”
“Nani…eeh!” Kindo akauliza, lakini hilo likawa
swali la mwisho kabla yule binti hajaanguka chini
ghafla na kuanza kuvuja damu puani na
masikioni!! Kindo akataka kukimbia lakini mlango
ulikuwa umefungwa kwa nje.
Akahaha huku na kule, likaja tukio kubwa zaidi.
Kile chumba kilichokuwa kisafi na cha kuvutia
kikapatwa na joto kali sana na kisha kama mvua
inavyonyesha nje, ndivyo damu ilivyoanza
kunyesha ndani ya kile chumba.
Kindo akapagawa, hakuna alichoona tena zaidi ya
damu nzitonzito. Akajaribu kukimbia pasi na
uelekeo akateleza na kuanguka chini, mdomo
wake ukitangulia sakafuni.
Akatulia kama Rebeka!!
____
MKUTANO haukuanza kwa wakati kwa sababu
alisubiriwa mtu mmoja ambaye alikuwa kiungo
muhimu sana kwa siku hiyo. Wajumbe wengine
walikumbwa na pepo la wivu kutokana na
mafanikio ya muda mfupi ya mjumbe mwenzao.
Kila mmoja alimfikiria Yakuza Wenje na kutamani
kusimama katika nafasi yake kwa wakati huo,
waliamini kuwa kwa mafanikio aliyoyapata katika
jambo la msingi kama lile basi ilikuwa siku yake
ya neema na kujazwa mapesa na kugeuka kuwa
tajiri mkubwa kabisa.
Muda ulizidi kusonga mbele na bado muhusika
hakufika, hivyo mishumaa haikuwashwa
kumaanisha kuwa mkutano ulikuwa haujaanza
rasmi.
Minong’ono ya hapa na pale kutoka kwa
wajumbe haikuisha, walikuwa wakilalamikia tabia
ya Yakuza kutojali muda inawaharibia wengine
ratiba zao. Malalamiko hayakupata wa kuyajibu,
wengine wakavuta midomo yao kimanung’uniko
lakini hii haikusaidia.
Ghafla, tofauti na utaratibu wa siku zote mlango
unaotumiwa na wajumbe kuingia katika ukumbi
ule na wakiwa wanaamini kabisa kuwa amesalia
mjumbe mmoja tu kuingia, ukafunguliwa kwa
pupa.
Yakuza huyo!! Kila mmoja akawaza na kutoa
miguno ya kukereka.
“Washa mishumaa… washa mishumaa upesi!!”
sauti iliyokatika taharuki kali iliamuru, wajumbe
wakaitambua kuwa ilikuwa ya katibu wao.
Mambo yalikuwa tofauti kabisa tena yasiyofuata
utaratibu!!
Wakawasha mishumaa yao, na kwa mara ya
kwanza taa kali ya katibu wao haikuwashwa na
wakaweza kuiona sura yake kwa mara hiyo ya
kwanza.
“Mambo yamevurugika… mambo yamevurugika
wajumbe…” alianza kuelezea huku akihema juu
juu.
“Eti…”
“Mambo si mambo tunatakiwa kujilinda na
kuchukua hatua za haraka haraka kabla jambo
hili halijatudhuru wote….” Akakohoa kisha
akavuta pumzi na kuzitoa kwa nguvu kisha
akaendelea, “hatujui wapi pa kuanzia lakini
Yakuza ameharibu mambo yetu tayari. Yakuza
ametuweka katika hatari kubwa sana na hadi
dakika hii hapokei simu yake ya mkononi… halafu
tulichomwagiza hajakifanya ametulaghai”
akasema kwa ukali, wajumbe wakaguna kwa
mshangao.
“Kiumbe hakijulikani kilipo…… hakijulikani kilipo
wajumbe …..” alipoimaliza kauli hii aliendelea,
“Watolewe upesi na kulindwa, mkawatoe upesi
jamani……” akasihi, na kisha wote wakabaki kimya
wakiutazama mlango uliofunguka ghafla kisha
upepo mkali ukaanza kuvuma!!
Woga ukatawala, wajumbe kila mmoja
akalalamika ajuavyo huku wakijaribu kutiana
moyo kuwa ile ni hali ya kawaida.
“Pereza… kafunge mlango haraka!!” katibu akatoa
amri kuu…. Pereza ambaye alikuwa kamati ya
ulinzi alisimama huku akijutia cheo chake. Hofu
ilikuwa inaishi naye, akajitutumua kiume akaufikia
mlango akaanza kupambana na upepo akiuvuta
mlango ndani.
Mara upepo ukakoma ghafla!!
“Aaah!!” wakaduwaa wajumbe!! Pereza akacheka
ki9fedhuli kisha akajitapa, “Nimeuamrisha
ukome….” Akajaribu kuuvuta mlango, mlango
haukusogea.
“Chibe…. Upesi njoo tusaidiane…” Pereza
akaamrisha, msaidizi wake akajongea
kiukakamavu mlangoni. Akaushika mlango
kinguvu.
“Nenda ukausukume kwa nyuma mi navuta
mbele.” Pereza akaamuru. Chibe ambaye ni
mjumbe na pia makamu katika kamati ya ulinzi
akatii. Akazunguka nyuma ya mlango.
“Mamaaaaa… nakufaaaaa” Chibe akatokwa na
ukulele wa ghafla. Pereza akaruka pembeni
kimazoezi kisha na yeye akaenda nyuma ya
mlango kutazama nini kinamtokea mwenzake
huko nyuma.
Hakumkuta!!
“Watoe vyumbani ….mkawatoe vyumbani upesi….”
Katibu alihamasisha juu ya Kindo na Rebeka
kutolewa vyumbaniu, sasa kila mjumbe alihaha
huku na kule.
“Funguo haupo… funguo!!” mjumbe mmoja
alilalama.
“Pereza… funguoooo!!” katibu aling’aka.
Pereza akaduwaa, kisha mdomo ukabetuka
wakati anajibu, “alifunga Chibe na hayupo hapa
tena….”
“https://jamii.app/JFUserGuide!! https://jamii.app/JFUserGuide! https://jamii.app/JFUserGuide….!!” Aliropoka katibu mkuu.
Mihangaiko hiyo ikawa kama imeruhusu ule
upepo wa maajabu kuanza kuvuma tena. Safari
hii hakuna aliyeweza kuuzuia tena. Ukavuma hadi
ndani.
Na hapo ukabadilika haukuwa upepo wa kawaida
tena. Ukaleta joto badala ya ubaridi, na mvua
yake haikunyesha nje ikanyesha ndani, si mvua
salama ya maji bali mvua ya aina yake.
Mvua ya damu!!
Upepo haukuja na ile damu, ile damu ilitoka kwa
wajumbe. Upepo ulivuma ukianza na katibu,
ukambamiza huku na kule bila kumruhusu kutulia,
damu zikamvuja kila kona. Upepo huu wa
maajabu ni kama ulikuwa na mikono mingi sana,
ukanyanyua mjumbe mmoja baada ya mwingine
na hatimaye wote wakawa angani wakibamizwa
katika kona hii na ile.
Damu zao zikageuka kuwa mvua iliyosababishwa
na upepo ule.
Na janga lililotokea katika nyumba hiyo lilizua
kizaazaa nchi nzima!!
Kila aliyesikia tukio hilo akajawa na HOFU!!
**NINI kipo nyuma ya tukio hili…….
 
SEHEMU YA SABA
Na hapo ukabadilika haukuwa upepo wa kawaida
tena. Ukaleta joto badala ya ubaridi, na mvua
yake haikunyesha nje ikanyesha ndani, si mvua
salama ya maji bali mvua ya aina yake.
Mvua ya damu!!
Upepo haukuja na ile damu, ile damu ilitoka kwa
wajumbe. Upepo ulivuma ukianza na katibu,
ukambamiza huku na kule bila kumruhusu kutulia,
damu zikamvuja kila kona. Upepo huu wa
maajabu ni kama ulikuwa na mikono mingi sana,
ukanyanyua mjumbe mmoja baada ya mwingine
na hatimaye wote wakawa angani wakibamizwa
katika kona hii na ile.
Damu zao zikageuka kuwa mvua iliyosababishwa
na upepo ule.
Na janga lililotokea katika nyumba hiyo lilizua
kizaazaa nchi nzima!!
Kila aliyesikia tukio hilo akajawa na HOFU!!
****
MSHAHARA aliokuwa anapokea kwa shughuli ya
kukata majani katika nyumba ya kizito
ulikaribiana na ule wa wafanyakazi wanaolipwa
katika ofisi nyingine.
Mshahara huu uliyafanya maisha yake kuwa
mazuri, akaihudumia familia yake ya mtoto
mmoja na mke, akapanga nyumba nzuri na baada
ya mwaka mmoja akanunua gari ambalo
hakutaka tajiri wake ajue.
Hakubadili muonekano wake wa mavazi, na kila
siku akaendelea kuonekana maskini na
mnyenyekevu sana. Hii hali iliimarisha kibarua
chake.
Kama ilivyo kawaida yake Kelvin Mgonja, siku
hiyo aliwahi tena kazini asubuhi sana akitarajia
kuhudumia nyasi za bosi wake mapema kisha
aingie katika shughuli nyingine.
Tofauti na siku nyingine ambapo mlinzi
humfungulia geti upesi upesi. Siku hii ya maajabu
alibisha hodi hadi akaingiwa na kero ya kuwa
mwajiriwa katika nyumba ile.
Hadi inatimu saa mbili asubuhi hapakuwa na dalili
yoyote ile ya kufunguliwa geti. Ilipofika saa tatu
asubuhi wasiwasi ukaanza kumwingia, haikuwa
kawaida ya bosi wake kulala hadi saa hizo.
Au anaumwa!!! Kelvin alijiuliza huku akijaribu
kusaka upenyo aweze kuchungulia. Hakuupata
upenyo wa kujua nini kinaendelea ndani ya
nyumba ile.
Majira ya saa tano asubuhi Kelvin akaenda kutoa
taarifa katika serikali za mitaa juu ya hali ile
inayoendelea nyumbani kwa bosi wake. Kwa
sababu alikuwa mtu mzito na anayefahamika
mwenyekiti alikurupuka na kuacha shughuli zake
nyingine, akawachukua wanamgambo watatu
wakaongozana naye pamoja na Kelvin hadi
nyumbani kwa Patrick Massawe kijana ambaye
alitarajiwa kugombea ubunge baada ya miaka
miwili na alikuwa na asilimia zote za
kuchaguliwa.
Hali aliyoiacha Kelvin bado haikubadilika,
hapakuwa na mlinzi getini.
Mwenyekiti wa mtaa akajaribu kupiga simu ya
Patrick, ikaita bila kupokelewa. Hali hii ikazidisha
hofu!!
Mwenyekiti kwa kutumia wadhifa wake
akaruhusu wanamgambo waruke lile geti na
kutua ndani ya ile himaya. Wanamgambo
wakajitutumua wakachumpa ndani ya ile himaya
. mwenyekiti na Kelvin wakaendelea kungoja nje!!
“Tazama kila pande!! Kuwa makini zaidi…”
mwenyekiti akaamuru jeshi lake lililokuwa ndani.
Kimya kikatanda kwa takribani dakika kumi, kisha
mlipuko wa kelele za hamaniko.
“Mamaweee… tunakufaaa…. Mamaaaa” vilio vya
wanamgambo vilisikika, kisha wakaliparamia geti,
wakatua upande wa pili hawakutulia
wakaendelea kukimbia.
Mwenyekiti na Kelvin nao wakaanza kukimbia
huku wakipiga kelele kana kwamba wanajua nini
kilichowasibu wenzao.
Wanamgambo walipopata akili ya kutulia huku
wakihema juu juu wakasimulia juu ya hali
iliyokuwa ndani ya ile nyumba ya mheshimiwa
Patrick Massawe.
“Damu, damu kila kona……maiti kila upande…. Ni
balaa…” alijieleza mmoja wao kisha mwingine
akatikisa kichwa kuunga hoja mkono.
Mwenyekiti akatoa taarifa polisi!!
Baada ya nusu saa nyumba ya Patrick ilikuwa
imezingirwa na utitiri wa askari. Wakafanya
utendaji wao, geti likavunjwa komeo lake likabaki
wazi wakati miili zaidi ya kumi ikitolewa katika
jumba hilo huku waandishi wa habari wakifanya
jitihada zao katika kupiga picha hapa na pale.
Lilikuwa tukio la kustaajabisha!!
Patrick Masawe alikuwa mmoja katika ya
waliopoteza uhai katika tukio hilo!!
***
AKIWA katika nyumba ya kulala wageni huku
hofu ikiwa imemtawala juu ya tukio lililotokea
majira ya saa nane usiku nyumbani kwake na
jingine lililotokea saa tisa usiku. Kutembelewa na
mgeni anayevuja damu kisha akapoteza maisha
mbele yake huku akisema neno moja tu
‘mmeniua’. Sam alikuwa akihaha kujigeuza huku
na kule kitandani na kujiuliza ni nani alikuwa mtu
yule maana alivyokuwa anavuja damu sura yake
haikuweza kuonekana hata kidogo.
Tukio lile likamfanya afunge safari ya ghafla
kwenda nyumbani kwa rafiki zake, nia yake
kuwashirikisha wenzake ili wafahamu usiku
huohuo ni kitu gani sahihi wanatakiwa wafanye
juu ya ule mzoga.
Huku akakutana na kubwa kuliko.
Don na Deniss walikuwa maiti wenye aibu kabisa,
walikuwa uchi huku damu zikitapakaa kila mahali.
Bila shaka walihangaika kabla ya kufa.
Sam akatimua mbio hadi alipoipata nyumba ya
kulala wageni, akajifungia ndani huku akili
ikicheza huku na huko na kusababisha aukose
usingizi kabisa.
Don na Deniss wamekufa wakiwa uchi na huko
nyumbani kwake ametembelewa na mgeni
ambaye ni kama alichagua kufia nyumbani
kwake.
Maskini Don na Deniss, au wamechomana visu
kwa sababu ya pesa? ..lakini mbona walikuwa
wanaelewana sana hawa rafiki zangu!! Sam
alijiuliza kwa utulivu huku akizidi kutafuta chanzo
kikuu.
Lakini, yaani wachomane visu wakiwa uchi… uchi
wa mnyama… hapana!! Kuna kitu, ama niseme
kuna mtu amewaua!! Alizidi kujiuliza na kujipatia
majibu kwa sauti ya juu.
Mtihani!!
Asubuhi na mapema akawasha runinga iliyokuwa
pale chumbani ili aweze kubaini kama taarifa juu
ya yule mtu aliyefia nyumbani kwake zimevifikia
vyombo vya habari pia alihitaji kujua ni kitu gani
kimewaua Don na Deniss kama kipo.
Habari zilikuwa za siku iliyopita na hapakuwa na
habari mpya kabisa.
Sam akaizimisha runinga na kuendelea kujilaza,
usingizi ulipomnyemelea akapiga simu mapokezi
na kumzuia mfanya usafi asihangaike na chumba
chake katika suala la hilo muda ukifika.
Majira ya saa saba alipowasha tena runinga
akakutana na habari mpya asiyoijua hata kidogo.
Kila kituo kilizungumzia juu ya mauaji ya kutisha
katika nyumba ya mzee Patrick Masawe.
Picha zilionyeshwa huku kituo kikiomba radhi kwa
picha zile, hakika walikuwa sahihi kuomba radhi
kwa sababu zilikuwa zinatisha haswa.
Mwingine hana mguu, mwingine mkono, jicho na
miili mingine ikiwa ni viwiliwili pekee bila vichwa.
Ilitisha kutazama!
BAADA YA SIKU TANO
HABARI ya mauaji yale ikiwa imezoeleka, vifo
vya Don na Deniss vikiendelea kupepelezwa na
kifo cha Yakuza Wenje nyumbani kwa Samson
kikimweka kijana yule matatani, na jeshi la polisi
lilikuwa likimsaka na kuwaamisha wananchi kuwa
kupatikana kwa Samson utakuwa ufumbuzi
mkubwa wa janga hilo la ghafla lililotokomea na
roho nyingi.
Wakati haya hayajatulia na Sam akiwa hana dalili
ya kupatikana. Ahueni nyingine ikapatikana.
Kijana aliyekutwa akiwa mahututi ndani ya jumba
lile ambalo roho lukuki zilipotea sasa alianza
kupata nafuu. Aliweza kujitikisa kidogo kisha
akafumbua macho yake na kubaki akiduwaa.
Uangalizi wa madaktari ulichukua nafasi kubwa
ili kuokoa maisha yake ili aweze kutatua utata
huo uliogubika. Jeshi la polisi nalo halikuwa
nyuma kuimarisha ulinzi kwa kiwango cha
kutishia waogopa mitutu ya bunduki, nia ikiwa
kuhakikisha kuwa yule kijana hadhuriwi na yeyote
mpaka atakaposema ni nini chanzo cha yote yele
katika nyumba ya hayati Patric Masawe.
Jitihada zikazaa matunda, afya yake ikaimarika.
Lakini alikuwa kimya bado asiseme lolote. Na
alipokuja kusema neno moja la kwanza neno hilo
likakikamata kinywa chake na kuwa neno lake la
kila siku.
“Rensho!!” nd’o neno pekee aliloweza kulitamka.
Alipoulizwa Rensho ina maana gani alijibu tena
kwa kusema 'Rensho'
Hakuwahi kuongeza neno la ziada! Hata
alipoulizwa jina lake ni nani alijibu 'Rensho',
anatoka wapi alijibu 'Rensho' umri wake...
'Rensho'
Nani ajuaye Rensho ni kitu gani?
Hayupo!
Picha za kijana huyu zikasambazwa katika
vyombo vya habari....
Nia ikiwa kuwapata nduguze wamchukue kijana
wao ambaye madaktari walikiri kuwa alikuwa
amepatwa na athari mbaya katika ubongo
wake....
Baada ya picha zake kusambaa magazetini,
akatambulika kuwa aliitwa Emmanuel Kindo.
Mama yake Kindo akahojiwa na kudai kuwa huyo
Rensho anayetajwatajwa na Kindo, alikuwa ni
mwanamke ambaye mwanaye alitarajia kuoana
naye siku za usoni na hakujua jingine la ziada
tena hadi mwanaye alipokutwa na janga hilo
akiwa ndani ya suti.
Rensho ukaendelea kuwa mtihani!
***
SIKU zilizidi kukatika na Sam akiendelea kuishi
maisha ya kujificha. Hakuwa na ujanja mwingine
wa kujitoa katika kesi iliyounganishwa na kutajwa
kuwa yote inamuhusu yeye.
Katika kujificha huku, alitawaliwa na taswira
mbili, moja ya yule binti akimlalamikia na ile ya
pili ikiwa ya yule bwana mwenye kuvuja damu
akimlilia na kisha kukata roho.
“Au walivyombaka…” Sam alipitiwa na wazo hilo
kisha akalikumbuka tukio la Don na Deniss
kumwingilia kinguvu yule binti kabla ya kumtosa
katika mkondo wa maji fahamu zikiwa zimemtoka
tayari. Binti yule alimlilia sana Sam awe msaada
kwake lakini hiyo ilikuwa ngumu sana kwa
sababu Don na Deniss walikuwa na bunduki na
kiubavu walimzidi Sam
Sam akalazimika kuwa mpole, Don na Deniss
wakatimiza haja zao kwa kujirudia mara kadhaa
na kisha kumtosa katika maji yule binti.
Hata kabla hawajalipwa pesa yao linatokea janga
hili la kutisha Don na Denny wanakufa huku
wakiwa uchi!!
Yakuza naye anakufa na anayetuhumiwa kwa hili
ni Sam ambaye yupo mafichoni.
Yule binti ni nani hasa!! Sam akajiuliza, huku kwa
mbali akiamini kuwa huenda yule binti akawa na
ushahidi wowote wa kumweka huru tena.
Akakusudia kumtafuta, lakini mara akakata
tamaa kwa kuamini kuwa iwe isiwe lazima yule
binti alipoteza uhai siku ileile.
Akaamua kuanza harakati zake za kusaka chanzo
cha yote haya kwa kuanzia kukutana na mpenzi
wa Don.
Akaifanya safari majira ya usiku kabisa!!
Bila taarifa akaingia mitaa ya Temeke mwisho,
akapita nyumba kadha wa kadha akaifikia
nyumba ya Sarah aliyojengewa na Don enzi za
uhai wake. Sam akaugonga mlango taratibu sauti
ya Sarah ikajibu huku ikitokea ndani, akamuuliza
ye ni nani anayegonga mlango.
“David..” akadanganya ili Sarah aweze kufungua.
Kweli akafungua!
Sam akaingia ndani akimuacha Sarah akiwa
katika mshangao wa hali ya juu…..
“Shem, tulia tuzungumze sijaja kwa ubaya na
unayoyasikia yote katika vyombo vya habari ni
uongo mtupu!! Mimi naweza kumuua Don, mimi
naweza kuutoa uhai wa Deniss… Sarah nawe
uliamini hivyo…” alihoji kwa kusihi. Sara badala
ya kujibu akabaki kutoa machozi tu!!
“Sarah, hapa kuna jambo zito sana limejificha
ambalo si la kawaida. Mimi sijaua…. Nashindwa
hata kuelezea nini kinatokea.”
“Shem, sijaamini kuwa ni wewe uliyeua na
sitakaa niamini. Lakini ni kitu gani sasa hiki
kinanitokea baada ya kifo chake.,…,”
“Kitu gani tena….” Alihoji Sam kwa umakini.
“Naota ndoto, au niseme kuwa niliota ndoto gani
hata sijui… msichana hivi amejilaza haonekani
sura yake bali mapaja tu, halafu anavuja damu.
Niliposhtuka…..” akasita akaanza kulia, Sam
akaenda kumyamazisha.
“Usilie sasa shem ndo maana mimi nimekuja
hapa ili tujue la kufanya… si unajua natafutwa eti
nimeua mimi…”
“Najua….” Alimalizia Sarah!!
“Sawa ikawaje baada ya ndoto..”
“Nikaingia katika siku zangu ghafla…. Yaani
ghafla na …na hazijakata hadi leo…navuja damu.
Nimekuwa wa kubadili pedi tu kila kukicha”
akalia kwa sauti ya juu wakati anamalizia kauli
yake.
“Unatokwa damu?.... mbona…eeh..”
Badala ya kujibu Sara akabaki kulia tu asijue kipi
cha kujieleza zaidi.
“Hata kazini siendi mara kwa mara… yaani damu
inanitoka sana…. “ akasita kisha akaendelea,
“bora basi ingekuwa inatoka tu…. Yaani inatoka
halafu nakuwa nanuka shem nanuka vibaya…”
Sam akakisikia kichwa chake kikivurugika haswa!!
Hii ilikuwa habari mpya zaidi tena tatanishi.
“Hivi Sam, Don na Deniss walifanya nini kwani?”
“Deniss ameingiaje tena hapa kwani….”
“Maria naye aliota….ndoto hii hii” Alisema kwa
sauti ya chini.
“Heh! Maria mpenzi wake Deniss?”
Sara akatikisa kichwa kuafikiana na Deniss.
Sam akachoka!!
# Naam ! Kindo kapagawa...... Sam naye haelewi
nini kinaendelea.... ni HOFU!
 
SEHEMU YA NANE
Badala ya kujibu Sara akabaki kulia tu asijue kipi
cha kujieleza zaidi.
“Hata kazini siendi mara kwa mara… yaani damu
inanitoka sana…. “ akasita kisha akaendelea,
“bora basi ingekuwa inatoka tu…. Yaani inatoka
halafu nakuwa nanuka shem nanuka vibaya…”
Sam akakisikia kichwa chake kikivurugika haswa!!
Hii ilikuwa habari mpya zaidi tena tatanishi.
“Hivi Sam, Don na Deniss walifanya nini kwani?”
“Deniss ameingiaje tena hapa kwani….”
“Maria naye aliota….” Alisema kwa sauti ya chini.
“Heh! Maria mpenzi wake Deniss?”
Sara akatikisa kichwa kuafikiana na Deniss.
Sam akachoka!!
“Shem….kwani Don alikuwa anafanya kazi gani?
Wewe ni rafiki yake mkubwa tafadhali
usinifiche!!” Sara akauliza swali ambalo lilikuwa
la ghafla sana.
“Nani, Don!!” Sam akauliza kipumbavu huku
akipepesa macho huku na kule kumkwepa Sara.
“Don, alikuwa anafanya biashara zake tu
mikoani… alikuwa mfanyabiashara.” Sam akajibu
huku akitetemeka wazi wazi.
“Nilidhani alikuwa dereva tu wa magari
makubwa!!” Sara akakebehi huku akikumbuka
kuwa awali Don aliwahi kumweleza kuwa yeye ni
dereva.
Aibu zikamkumba Sam!! Hakujibu chochote.
Sarah akaanza kulia kilio cha chinichini, kisha
akamlalamikia Sam kwa kumdanganya. Sam
alihofia kumweleza waziwazi kuwa walikuwa
majambazi na tukio lao la mwisho kikazi zaidi
walikumbana na binti safarini wakamteka na
kisha kufanya waliyomfanyia.
“Ni kweli shem Don ni dereva wa magari
makubwa, hilo la biashara alinionya nisikueleze,
nasikitika nimepitiwa nimesema….” Sam
akaupigilia msumari kisha akaupaka rangi uongo
wake ukawa ukweli. Sarah akaamini!!
***
VIDOLE vyake vilikigonga kichwa chake mara
tatu usawa wa utosi, kisha akaitoa miwani yake
akaipangusa vyema na kuibandika machoni.
Kisha akaitoa tena na kuiweka kando. Akaivuta
meza yake ikatoa ukelele kidogo, akauma meno
yake. Kisha akatoa bahasha yenye ukubwa wa
A3. Kabla hajaifungua na kuitazama vyema
akavunja kijiti kidogo na kujichokonoa meno yake
kisha akabeua.
Akaivamia bahasha na kuigeuza chini juu, juu
chini. Kila kilichokuwa ndani yake kikamwagika
mezani. Zilikuwa picha nyingi sana zinazoelezea
tukio moja matata sana la mauaji katika nyumba
ya kifahari ya bwana Patrick Massawe aliyekuwa
mbunge mtarajiwa.
Picha hizo ambazo zilihitaji Inspekta shupavu
kama yeye kuzitazama zilipigwa na mpiga picha
ambaye anajua haswa nini maana ya picha.
Zilipigwa kwa umakini mkubwa na ukaribu wa
kuridhisha!!
Akapitia moja baada ya nyingine.
Hazikumtisha hata punje, kwa sababu kwa
macho yake aliwahi kushuhudia mauaji ya
kutisha sana hakutishika, sembuse hizi picha
zisizokuwa na uwezo wa kusema.
Karibia picha zote zilikuwa zinafanana....
almanusura aghaieri kuendelea kutazama picha
nyinginezo lakini kanuni za jeshi la polisi,
Kuhakikisha hata kile ambacho unahisi macho
yako pekee yamekiamini.
Akaendelea kuzipekua hadi akaifikia picha
ambayo ilikuwa tofauti kabisa na picha nyingine
alizozitazama.
Hii ilikuwa haitishi sana na badala yake ilikuwa
inavutia kuitazama.
Inspekta aiasaili kwa macho kiutulivu kabisa, na
bila kujua mawazo yake yakapaa maili nyingi
kutoka pale akaisahau kazi yake.
Na hapo akaisikia suruali yake ikianza kumbana.
Shabash!! Akatokwa na kauli hiyo lakini bado
alikuwa akiitazama picha ya binti kigori amejilaza
chali huku akiwa ameikunja miguu yake na
kuifanya kuumba nambari nne, kinguo chake cha
rangi ya pinki kilikuwa kimemruka na hapa
Inspekta akayaona mapaja laini sana
yaliyomeremeta.
Inspekta akaupenyeza mkono wake hadi ndani ya
suruali yake na kuyaweka vyema maungo yake
yaliyotaka kumdhalilisha
“Pumbavu yaani natamani maiti? Ila…. Ila alikuwa
mrembo sana aisee…. Kwa hiyo huyu alikufa bila
kuwa na jeraha ama?”
Akanyanyua simu yake ili amuulize
anayehusika…. Baada ya kuingiza namba za
muhusika na kupeleka sikioni hapo hapo simu
yake ikaita, akashtuka na kutaka kuirusha kando,
alipoitazama aliyekuwa anapiga ni mtu muhimu.
“Jambo Inspekta! Uchunguzi wa alama za vidole
umeonyesha kuwa kuna vidole vya mwanamke
katika miguu na mikono ya miili yote kasoro miili
miwili tu, yule ambaye yupo hai na mwili wa yule
msichana pekee katika tukio hilo…”
“Zuia miili isizikwe.. na yule fala anayesema
Rensho Rensho ameweza kusema zaidi…”
“Hapana hajasema neno la ziada tena….”
"Mmetandika vibao kidogo... kama
hamjamtandika naomba mmtengue hata kiuno ili
aongee vizuri... ana timamu huyo sema
mnamdekeza nyie...."
Simu ikakatwa!!
“Mwanamke aue watu kinyama namna hii…
mbona balaa hili..” alijisemea huku akirejesha
zile picha katika bahasha.
Na huyu mwanamke ambaye hakuguswa ni kwa
nini hakuguswa!! Wazo lilisafiri katika kichwa
chake wakati anaufunga mlango wa ofisi yake,
akaingia garini na kuendesha hadi hospitali
ambayo maiti zilikuwa zimehifadhiwa zikiwa chini
ya ulinzi mkali wa polisi.
Ilikuwa tayari saa tano asubuhi wakati anazima
injini za gari yake mbele ya hospitali. Supu
aliyokunywa asubuhi bado ilikuwa imemshibisha.
Akabeua tena!
Maaskari waliopishana naye walipiga saluti,
akazipuuzia salamu hizo akaenda moja kwa moja
kwa askari mkuu wa ulinzi aliyepewa jukumu lile,
akamwomba waongozane akauone mwili wa
msichana asiyejeruhiwa.
Moyoni alitamani sana kuiona sura ya maiti yule
ambaye alimsababishia matamanio katika picha
na kusababisha mauongo yake muhimu
kunyanyuka ghafla, pili alitaka kujua ni kwa nini
hajadhurika hata kidogo, na tatu alihitaji kujua
kama aliwahi kumwona mahali ama la kuikariri
sura ile kwa ajili ya kuanza upelelezi mapema.
Waliongozana hadi mochwari baada ya kufuata
hatua zote muhimu. Muhudumu wa mochwari
akaliendea jokofu ambalo alikuwa amehifadhi ule
mwili wa yule binti asiyekuwa na jina.
Akavuta kwa nguvu, akakutana na maiti nyingine
tofauti akafunga upesi huku akidhani kuwa
alikosea namba ya sanduku. Akaangaza huku na
kule na kuvuta jingine huko napo akakutana na
hali ileile ya mwili mwingine.
“Kijana unapoteza muda!!” Inspekta akakoroma
huku akirusha mikono yake huku na kule. Yule
kijana mwenye upara wa kimaskini akaendelea
kuhaha bila mafanikio.
“Hayupo…. Hayupo pale alipohifadhiwa!!” alijibu
huku akitetemeka.
“Hayupo! Una maana gani kijana, unaleta utani…
utani na serikali.” Inspekta akatoa miwani yake
usoni na kumkazia macho yule bwana aliyekuwa
anatetemeka tu.
“Alikuwa sanduku gani?” Inspekta akamgeukia
afande kwa swali lile, afande akanyoosha kidole
kuelekea ile sehemu sahihi kabisa ambayo hata
bwana kipara alikuwa anaamini.
“Na ni nani alikuwa zamu jana ya kulinda hapa..”
“Afande Christopher…” alijibu kwa nidhamu ya
hali ya juu.
“Kahakikishe kuwa hayupo huyo maiti ili tumpigie
simu Chris haraka….”
Askari akaruka hatua nne kubwa za kikakamavu
akalifikia jokofu na kulivuta, Inspekta akimtazama
kwa makini.
“Mamaaaa!!” akatokwa na ukelele mkubwa wa
hofu!
Inspekta akasita kukurupuka, zaidi akajipa
umakini.
“Ni nini…” akahoji huku mapigo yake ya moyo
yakienda kasi sana.
Askari alikuwa anatetemeka bado huku
ameyatumbua macho yake, mzee kipara alikuwa
anashangaa tu!
“Askari ni nini hapo?” akakoroma tena.
“Afande… njoo ujionee afande…..”
“Nimekuuliza ni kitu gani hapo?” akakaripia.
“Afande… afande Christopher…”
“Whaaat!!!” akaruka na kulifikia lile jokofu,
akakutana na mwili wa askari ambaye alikuwa
anatokea kituo chake, alikuwa ametulia tuli ndani
ya jokofu la kuhifadhia maiti na yeye akiwa maiti
tayari.
Alikuwa ameingia sehemu ambayo awali
alihifadhiwa mwanamke mapaja wazi asiyekuwa
na jina.
“Hii inawezekanaje askari…”
“Sielewi hata kidogo afande!! Sielewi..”
“Weka walinzi wa kutosha hapa na kisha nimkute
huyu sungura pori kituoni, upesi!!” aliamuru huku
akimtazama mlinzi wa mochwari kwa jicho
lililojaa chuki.
“Lakini mimi…afande….” Hakumalizia kauli yake
akajikuta akiona maluweluwe kadhaa mbele yake.
Alikuwa amepokea kofi barabara katika shavu
lake.
Inspekta akatoka nje akiwa mwenye ghadhabu
vilevile, akachukua simu yake na kubofya namba
kadhaa.
“Upo nyumbani…..aah… sawa nakuja!!” akamaliza
na kuirejesha mfukoni. Akachukua gari lake na
kutoweka.
Akaelekea alipopajua yeye!
****
KATIKA kipindi cha miaka miwili ambacho
amekuwa katika mahusiano ya kiwiziwizi hakuna
kipindi kigumu alichokuwa anapitia kama wakati
huo.
Kuwachanganya wanaume wawili hilo kwake
halikuwa tatizo hata kidogo kwa sababu penzi
lake alilitoa kimasilahi zaidi. Na alijua jinsi ya
kuzichanga karata zake vyema, kwenye joka
akaweka joka na kwenye kopa akaweka kopa.
Aliweza kuwahudumia wote kimwili pasi na wao
kujishtukia.
Sasa mpenzi wake mmoja alikuwa amefariki
ghafla!
Kilichomuumiza Maria si kifo cha mwenza wake
huyo, bali ni hii hali ambayo ilikuwa imekuja
kuleta mabadiliko makubwa katika mwili wake na
kumkosesha amani kabisa.
Alijitahidi kulichukulia kuwa ni jambo la kawaida
lakini siku zikasogea na likawa katika taswira
mbaya.
nani amueleze? Hili lilikuwa swali. Aliamini kabisa
hakuna hata rafiki yake mmoja awezaye
kumvumilia na kumsikiliza kwa kina na kisha
kumshauri vizuri.
Kwa ukaribu zaidi akamfikiria mama yake mzazi,
mama Maria!
Akapanga siku hiyo aende kumtembelea
nyumbani kwake maeneo ya Mbezi Luis.
Akajipanga kuanzia asubuhi kwa safari hiyo,
lakini wakati anaanza kuvaa akapokea simu
kutoka kwa Kisembe, hapakuwa na maongezi
marefu. Kisembe alimuuliza iwapo yupo
nyumbani alipokiri kuwa yupo basi alihitaji
kuonana naye haraka iwezekanavyo hapohapo
nyumbani kwake.
Utamu wa pesa za kuhongwa ukageuka uchungu
katika hali hii hakuwa na lolote la kupinga, kwani
alimjua vyema Kisembe asivyokuwa na dogo.
Ukali wake kwa watuhumiwa huko alikuwa
akiuleta hadi katika mapenzi.
Inspekta Kisembele!
Maria akaketi kitandani na kuchukua kioo
akaendelea kujipamba kiuchovuuchovu hadi hapo
aliposikia mlango ukigongwa.
Akajongea kufungua, akaingia ndani bwana
Kisembe kwa fujo akairukia midomo ya Maria
iliyokuwa inameremeta!!
Maria akampokea kwa kujilazimisha mzee huyu.
Wakakutanisha ndimi, wakakokotana hadi
chumbani, Kisembe akamtupa Maria hapo na
kisha akaanza kuyaondoa mavazi yake kwa fujo.
“Mpenzi….nipo katika siku zangu please!!” maria
akasihi lakini Kisembe hakuacha kuondoa nguo
zake.
Hakuna neno alilosikia kwa wakati huo, alikuwa
amejiandaa kwa shughuli ile ya chumbani.
Maria alitaka kujieleza zaidi lakini Kisembe tayari
alikuwa kifuani kwake akimtomasa huku na kule.
“Kisembe bwanaa… yatachafuka mashuka
Kisembe acha!! Acha basiii” aliendelea kusihi
Maria.
Kisembe mwenye nguvu akambana Maria na
kuondosha nguo zake.
Ile picha ya maiti ilikuwa imempagawisha haswa!
Na wapi pa kuponea kama sio kwa Maria?
“Umeanza kunifanya mimi mtoto eeh… unadhani
tarehe zako sizijui… haya kuna nini hapa….”
Kisembe alimbana Maria kwa swali hilo.
Lahaula!! Maria kujitazama, hakika hakuwa na
yale mauzauza ya kutokwa damu mfululizo.
Kisembe hakumpa muda wa kushangaa
akamvamia kwa fujo.
Alishaizoea sura ya Maria, haikumpa hisia tena.
Akafumba macho na kujenga ile picha ya
marehemu, lakini akajitahidi awezavyo zile damu
zisiingie akilini mwake, alimsikia Maria akiguna tu
kama kawaida yake wawapo sirini.
“N’talala hapa leo!!” baada ya kumaliza awamu
ya kwanza Kisembe alimweleza Maria. Maria
akajitetea kimahaba kuwa mama yake amemuita
nyumbani hivyo lazima aondoke.
“Nimesema nitalala hapa, sio kwamba nitalala na
wewe.. endelea na ratiba zako wewe” Kisembe
akajibu kwa hasira kidogo. Maria akakubaliana
naye, akaingia kuoga upya.
Kisha akamuaga na kutoweka!!
Njia nzima alikuwa katika mshangao, asimini
kuwa ni muda mfupi uliopita alikuwa
akisumbuliwa na tatizo la kutokwa damu ya hedhi
bila kikomo na sasa haipo tena.....
***
Alianza kwanza kuukosa usingizi akiwaza namna
ambavyo maiti ya yule binti imetoweka hospitali,
akawaza pia ni kwa namna gani yule askari wake
mtiifu ameuwawa na kuwekwa katika jokofu bila
mtu yeyote kugundua hilo.
Aligeukia tena upande mwingine, mara akajihisi
kubanwa mkojo.
“Aaargh Maria naye na hili linyumba choo cha
nje….mi sitoki, nakojoa katika beseni akija
ataenda kumwaga… na hii ndo itakuwa komesha
akatafute nyumba za kueleweka” alilalamika huku
akisimama na kupapasa bila kuwasha taa.
Akalipata beseni akaliweka katika mlengo sahihi,
akaanza kumwaga haja zake.
Mkojo mrefu!
Mkojo gani huu! Alijiuliza huku akihisi waziwazi
kuwa hakuna dalili ya mkojo ule kukatika,
akajaribu kuubana lakini haikuwezekana.
Akajisogeza akiwa na beseni lake katika kitufe
cha kuwashia taa. Akawasha!!
Asalaale!! Beseni jeupe lilibeba mkojo
mwekundu…. Haukuwa mkojo ule zilikuwa ni
damu.
Macho yakamtoka pima Kisembe.
Akajitahidi kuzibana damu hizo zisimtoke, na
hapo akaisikia sauti ile ya Maria iliyokuwa
inamlilia kuwa yupo katika hedhi asimuingilie
lakini hakukoma akamuingilia bila kuona japo
chembe ya damu.
Kasembe baada ya kufanikiwa kuidhibiti ile damu
kidogo, akavaa nguo zake hovyohovyo. Akatoka
nje na kuingia ndani ya gari lake, nia yake ikiwa
kuwahi huduma hospitali yoyote ile…
Haikuwa nyepesi kama alivyoweza kudhani!!
Asubuhi ya siku iliyofuata taarifa za kustua nchi
zikatapakaa.
Inspekta Juma Kisembe amekutwa amekufa
baada ya kuvuja damu nyingi akiwa ndani ya gari
lake kando kando ya barabara ya Mandela jijini.
Inspekta alikuwa akivuja damu katika sehemu
zake za siri!!
Kifo kama cha mume mwenzake kwa binti Maria,
Dennis!!
**Nini hiki kinatembea katika riwaya hii…..NI
HOFU TUPU MJINI!!!
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom