Riwaya: Hatia

Riwaya: Hatia

Duh hali si hali ama kweli siri ni ya mtu mmoja na si wawili wala zaidi. Martha sasa ana kibarua kizito cha kujitwisha siri zote zinazoendelea.
 
Duuuuh keep it up casuits. Endelea hivhivi kutudondoshea uhondo
 
RIWAYA: HATIA
MTUNZI: GEORGE Iron Mosenya


SEHEMU YA KUMI NA SITA


"Ooh!! Samahani sio mpenzi bali mzinzi mwenzako maana mpenzi ninaye" aligandamiza msumari mwingine Joram, Matha akaiuma midomo yake kwa ghadhabu, hofu ikachukua ubabe wake wa kurusha mateke.
"Sidhani kama una maanisha Joram!!"
"Aah!! Basi kama simaanishi ngoja niende, lakini wamuonaje John wewe, una hamu ya kufa?? Si unajua kufa hakujaribiwi" alisema huku akisimama.
"Joram!!!"
"Yes!! Darling" alijibu Joram, Matha akataka iwe ndoto yeye kuitwa hivyo na Joram lakini ilikuwa ni hali halisi. Joram alikuwa anataka penzi, kichefuchefu kikachukua hatamu!!! Akakimbia bafuni akatapika kidogo.
"Hivi ina miezi mingapi??" aliuliza Joram kwa mbwembwe.
"Joram usizungumze na John lolote nitakupigia simu" alisihi Matha.
"Jitahidi iwe kabla ya kesho jioni" alisema na kuondoka bila kuaga.




******


Kanisa la kilokole maeneo ya Mwenge jijini Dar es salaam lilikuwa limejaa watu wengi sana magari ya kifahari yalikuwa yamepangana na kuleta maana kuwa wafuasi wa kanisa hilo walikuwa ni watu wenye kipato cha juu, wale wa kipato cha chini hawakuwa na nafasi.
Ndivyo ilivyokuwa lakini mle ndani ulipofika wakati wa kutoa ushuhuda waliokwenda pale mbele walikuwa watu wa hali za chini sana, Swali lilikuwa je ni wao pekee wanaopata miujiza hiyo ama kulikuwa na namna.
Mamia ya waumini walikuwa wametega masikio ili waweze kusikia palikuwa na muujiza gani kwa siku hiyo.
Mama mmoja akisaidiwa kutembea alisogezwa mbele ya madhabahu na kuanza kutoa ushuhuda wake juu ya mwanaye ambaye amepotea katika mazingira ya kutatanisha baada ya kwenda katika mji wa Mugumu Serengeti kwa masuala ya kimasomo.
"Nilidhani mwanangu wamemuua, nimehangaika kwa waganga wengi sana hawakuweza kunipa jibu, sikuwa natambua kama lipo jibu la uhakika hapa duniani, sasa nimelipata jibu baada ya rafiki yangu kunikaribisha hapa kanisani nikakutana na mtumishi wa Mungu na kumuelezea alifanya maombi mazito juu yangu, kumbe mwanangu wanataka kumfanya msukule…" alishindwa kuendelea kuzungumza yule mama akaanza kulia akapepesuka akataka kuanguka chini mara akadakwa na watu waliokuwa wameandaliwa kwa shughuli hiyo.
Sijui huwa wanaambiwa kabisa kuwa ataanguka!!!!
"Bwana apewe sifaaaa" alipaza sauti mtumishi wa Mungu.
"Ameeeeeeen!!!" walijibu kondoo wa bwana kwa sauti kuu. Mtumishi akapiga hatua kwenda kushoto kisha akaenda kulia halafu akarejea katikati, tabasamu pana likiwa mdomoni mwake, akatoa kitambaa chake cheupe akajifuta jasho usoni halafu kwa madaha akaliondoa koti lake, akatokea mtumishi mwingine akawahi kulipokea na kulihifadhi mahali salama.
"Bwana apewe sifaaaa!!!!"
"Aminaaaaaa"
"Nilivisikia vyombo vya habari vikitangaza juu ya kupotea kwa huyu kijana nani nani!! Michael Msombe, kwa akili za kibinadamu wakasema huenda ameliwa na simba mara ameuwawa, nilicheka sana, hadi nikatokwa machozi. Mungu alizungumza na mimi, Mungu aliniambia ipo siku atawaonyesha ukweli kupitia mimi na hiyo siku ni leo, Bwana asifiweeee!!!!"
"Ameeeeen!!!" watumishi walijibu kwa pamoja shairi hili lililokaririwa hata na wale malaya na majambazi. Shairi ambalo halikuwa na maana tena bali kwa wale wachache wenye imani thabiti. Shairi lililotumika kuwalaghai wenye shida.
"Ndugu zanguni uchawi upo lakini katika jina lililo kuu jina la bwana hauwezi kusimama, mama aliwahi sana kutoa taarifa nipo napambana na hao wafalme wa Jehanamu, hawawezi tena kumfanya Michael kama wanavyotaka. Bwana anamuhitaji sana Michael kuliko wao wanavyomuhitaji haleluya haleluya!!!" alitia nakshi hizo mchungaji huyu ambaye tayari alikuwa ametumbua zaidi ya shilingi laki nane za mama huyu mjane, mama aliyekuwa yupo katika jitihada za kumsaka mwanae wa pekee, Michael Msombe.
Maneno ya mchungaji huyu yalikuwa matamu lakini hayakuonyesha tumaini lolote lililo hai. Mama yake na Michael taratibu akaanza kuingiwa wasiwasi lakini hakuwa na jeuri ya kumtamkia mchungaji.
Siku hiyo ya kutoa ushuhuda ndiyo siku ambayo waandishi wa habari nao walizinasa taarifa za mchungaji huyo wa kilokole kuthibitisha kuwa Michael amechukuliwa msukule. Bila kufanya utafiti magazeti ya udaku yakaandika, ilikuwa imepita miezi mitano tangu yaandike juu ya kupotea kwa wanachuo wawili Joyce na Michael katika mazingira ya kutatanisha. Polisi kama kawaida walitoa jibu la upelelezi unaendelea, upelelezi ambao haukupata ufumbuzi.
"MICHAEL APATIKANA!!!!"
"MWANACHUO ALIYECHUKULIWA MSUKULE AFUFULIWA NA JK"
"MAAJABU YA NANE YA DUNIA!!! JK AFUFUA MTU"
Vilikuwa baadhi ya vichwa vya magazeti!!!
Taarifa hizo za magazeti ziliamsha akili katika familia ya akina Joyce jijini Dar es salaam, baada ya tafakari ya muda mzee Keto alipuuzia na kuona ni jambo lisilowezekana kumrejesha Joyce kwa maombi, jawabu hilo likakubaliwa na watoto wake wawili pamoja na mdogo wake.
Alikuwa mama yake Joyce aliyeitwa Mariana ambaye hakukubaliana na jambo la kupuuza ushuhuda wa yule mama juu ya kupatikana kwa Michael, siku iliyofuata na yeye alifunga safari hadi Mwenge kumtembelea mchungaji huyo aweze kumueleza shida yake.
Mariana alikuwa amejaliwa mwili mzuri sana, licha ya umri wake wa miaka arobaini na tatu (43), bado urembo wake ule wa enzi za usichana wake ulikuwa unaonekana. Alikuwa ni mwanamke wa mjini haswaa. Alivijua vipodozi na aliujali mwili wake, ilikuwa vigumu sana kuamini kwamba Joyce Keto alikuwa mtoto wake wa kumzaa.
"Naitwa mchungaji Komanya!!"
"Naitwa Mariana"
"Bwana asifiwe!!"
"Emen!!"
Baada ya kusalimiana Mariana akiwa na mchungaji Komanya, alianza kujieleza shida iliyokuwa inamkabili, alisimulia jinsi Joyce Keto alivyopotea katika mazingira ya kutatanisha. Wakati wote aliokuwa anasimulia Mchungaji Komanya alikuwa anafumba macho na kuongea lugha zisizoeleweka huku akijipigapiga kifuani na kitabu cha dini alichokuwa ameshikilia.
Mariana alipomaliza kujieleza, Komanya alifumba macho yake akaanza kusali kwa lugha za ajabu kisha akamsogelea Mariana na kumuwekea mkono juu ya kichwa chake. Akamwombea kwa dakika kadhaa kisha akaketi.
"Mungu hakunipa macho ya kuona mbali, ila alinipa masikio ya kusikia vilio vyenu, ndugu zako wamekupinga sana, mume wako, watoto wote wameukataa ukweli, wewe ni jasiri sana!!!! Ooh!! My my my my!!!" Komanya alizungumza kwa hisia, Mariana akashtuka kwani alikuwa anaambiwa ukweli uliotokea nyumbani kwake.
Imani ikajengeka!!! Matumaini ya kumpata mwanaye yakarejea!!!
"Kwa kuwa familia haijakuunga mkono basi Mungu atafanya kitu juu yao, usiwashirikishe lolote hadi pale vitendo vitakapozungumza!!! Nakuhitaji kesho kutwa saa mbili usiku, lazima tufanye sala ya pamoja sala ya kuzivunja ngome za shetani!!!"
"Hamna shida baba mchungaji!!" alinyenyekea Mariana.
"Mungu akutangulie!!!! Nenda na amani!!" alimbariki akaondoka zake.






********




Kanisa la Familia ya furaha, lilianzishwa kama sala ya familia jioni ambapo familia mbili zilikuwa zinakutana kwa maombi ya mwisho wa juma, familia mbili zikazaa tatu, nne na kuendelea hatimaye wakaamua liwe kanisa. Hapakuwa na mchungaji, bali zilikuwepo zamu za kuongoza ibada. Kila familia ilikuwa inatoa muwakilishi wa kuongoza ibada kila mwishoni mwa juma.
Familia nyingi zikavutika na hatimaye wakaweka mahema kwa ajili ya kuwa wanafanyia ibada.
Hapakuwa na kiwango cha sadaka bali michango ya hapa na pale. Kila kitu kilienda juu ya mstari.
Familia ya mzee Komanya, ilikuwa na furaha sana katika wiki hii ya uwakilishi kwani tangu kanisa lianzishwe hawakuwahi kuweka mwakilishi mwanao wa pekee aitwae Jacob alikuwa masomoni nchini Nigeria ambapo alipelekwa kwa udhamini wa kanisa la Kirutheri.
Siku hii mtoto wao alikuwa ndiye anayekwenda kuwakilisha. Wazazi wake walikuwa wamewatangazia watu wengi sana juu ya tukio hilo la mtoto kusimama mbele ya madhabahu.
Siku ilifika umati ukawa umefurika, Jacob Komanya akasimama mbele ya jukwaa, sauti yake ikatikisa ngoma za waumini, mahubiri yake yakawavuta wapita njia, maombi yake yakawagusa wenye shida. Mkono wake ukawaangusha watu wenye mapepo. Madhabahu yakawa hayatoshi baada ya ibada kila mmoja alihitaji kumshika mkono. Jacob Komanya akageuka shujaa.
Wazazi wake walishangazwa sana na uwezo wa mtoto wao. Siri alibaki nayo yeye mwenyewe!!!!
Siri ya nguvu za giza, nguvu zenye masharti, masharti ya kuzini na wasichana wawili kila baada ya siku moja bila kuwarudia tena, masharti ambayo yaliziimarisha nguvu zake. Masharti yaliyomfanya JK aheshimike!! Masharti yaliyomuwezesha kuwa na sikio kali linalosikia mbali,
Sikio kuu la kishetani!!! Sikio lililofanya watu waogope kumsema vibaya kwani alikuwa akiwasikia yote waliyosema.
JK akapata heshima jijini Dar Es Salaam!!!
Baada ya mwezi mmoja akateuliwa kuwa mchungaji mkuu, hakukawia kujipatia ‘a.k.a' akajiita Mtume JK. Kanisa likatanuka upesi, wakajenga Mwenge kanisa kubwa ni huku Mama yake Michael na Mariana (mama Joyce) walizipeleka shida zao.
Mama Michael umri ulikuwa umekwenda hivyo aliponea chupuchupu lakini Mariana alimvutia JK, akaingizwa rasmi kwenye hesabu.
Masikini Mariana hakuyajua yote haya!!!




****




Joram aliondoka pale nyumbani kwa Matha akiwa na tabasamu kubwa sana. Aliamini kwa karata ile kamwe hawezi kumkosa Matha katika futi sita kwa sita.
Matha naye alibaki katika wakati mgumu sana.
Wanaume watatu aliokuwanao katika mapenzi aliamini walikuwa wengi sana na lazima wangemuumiza kichwa sasa alipofikiria suala la kuongeza tena wa nne akili iligoma kabisa. Lakini alipofananisha matokeo, aliamua kumkubalia Joram.
Sasa nikikataa halafu akimwambia John itakuwaje!!!, hakika bado sijajipanga kutoroka, na kumtoroka John sio suala dogo kabisa!! Moyo wa chuma ulihitajika kufanya jambo hili!! Litakalokuwa na liwe!!! Aliamua Matha. Akaichukua simu yake akampigia Joram.
"Nimekubali lakini…."
"Usijali nitaitunza siri kama kawaida yangu!!"
Matha alizishangaa akili za Joram maana kila alipotaka kuzungumza tayari alishatambua neno la mwisho. Akazishusha pumzi, akatweta akamuaga Joram kiunyonge na kisha akakata simu!!
Matha alipitiwa na usingizi na alipoamka alijishangaa kwamba yupo katika uhusiano na wanaume wanne, hakuwa na wasiwasi juu ya magonjwa lakini aliiangalia mimba yake iliyokuwa na miezi mitatu huku bado ikiwa ni mimba ya hisia kwani ilikuwa haionekani. Akajipiga piga kisha akatabasamu, akaifunga kanga yake vizuri akaingia bafuni, akaoga. Akarejea na kujiandalia stafutahi, chai ya rangi na kiporo cha wali akakipasha moto.
Akastafutahi kimya kimya kwa amani finyu moyoni!!!
Baada ya stafutahi akapokea ujumbe kwenye simu yake.
"Baby kwa hiyo leo tunaonana!" ilikuwa namba ya Joram. Matha akahamanika, akamwona Joram kama anayevuka mipaka mapema akampigia akiwa na hasira, mkononi alikuwa ameshikilia fagio.
Najua upo peke yako ndo maana nimetuma ujumbe huo!!!" aliwahi kuzungumza Joram. Matha hakuwa na la kusema akawa anahema juu juu.
Joram akacheka kisha akakata simu!!
Matha akaghairi kufagia akaenda bafuni, akataka kuoga akakumbuka tayari alikuwa ameoga, akapiga kite cha ghadhabu akatoka bafuni.
Alipotoka akampigia simu Adrian ili waweze kuonana, alihitaji kuilazimisha furaha yake lakini bado alikuwa na simanzi, kuonana na Adrian ndio lilikuwa suluhisho pekee.
Adrian alipeana na binti huyu miadi ya kukutana jioni.
Majira na ya saa kumi jioni Matha alikuwa anaelekea kukutana na Adrian, akiwa ndani ya taksi, mara simu ikaita alikuwa ni Joram. Almanusura asipokee lakini alihofia kumkera mtu ambaye alikuwa ameishikilia dhamana ya amani yake.
"Yes!! Joram"
"Nipo hapa Golden Crest Hotel chumba namba 104 naomba uje"
"Kufanya nini sasa hivi?" alihoji Matha. Joram hakujibu akakata simu. Matha akaumiza kichwa akawa katika jitimai la nafsi, hatia ikaanza kumtesa tena. Hatia aliyoamini Minja ameondoka nayo kwenda mkoani Singida sasa ilikuwa imerejea kwa kasi ya tofauti tena kwenye mikono ya mtu ambaye si wa lelemama. Mikono ya Joram!!!
Matha akapiga akili ya haraka haraka, akaamua kumtumia ujumbe Adrian kuwa amepata udhuru wataonana baadaye, baada ya Adrian kuelewa japo kwa shingo upande alimpigia simu Joram akamwomba amuelekeze ni wapi anapoishi. Joram kwa sauti ya ujivuni akampa maelekezo Matha!! Baada ya maelezo aliondoka pale Golden Crest na kurejea nyumbani kwake.
Baada ya nusu saa Matha alikuwa katika kitanda kimoja na Joram, hakupata raha yoyote ile kwani alikuwa na wasiwasi muda wote!!!
Joram pekee ndiye alifurahia.
"Joram pliz…."
"John hatagundua usijali" alimalizia Joram, Matha akawa amemzoea na hizo tabia zake za ajabu.
Baada ya kuoga akaaga na kuondoka!!!
Safari ya kwenda kwa Adrian!!
Alipokuwa na Adrian muda wote alikuwa amekilalia kifua cha Adrian, alijisikia amani sana katika mikono hii, alilia sana Adrian akawa anambembeleza, hakujua kwa nini malaika wake huyu alikuwa analia sana, hakujiuliza sana alichohakikisha ni kuwa anambembeleza.
Usiku huo aliupitisha akiwa na Adrian, tayari alikuwa amemdanganya John Mapulu kwa njia ya simu kuwa alikuwa ameenda kumsalimia dada yake maeneo fulani nje kidogo ya jiji.
Utu wa Matha ukawa unashuka kwa kasi sana alijiona kama hana umuhimu tena. Mtoto wake aliyekuwa tumboni pekee ndiye aliyebakia kuwa na umuhimu mkubwa.
Umuhimu wa mtoto wake ndio ulisababisha apitie matatizo hayo laiti kama angekuwa hana umuhimu angeweza kuwa ameitoa mimba hiyo na kubakia bila msongo wowote wa mawazo.
Matha akawa amefanya mapenzi na wanaume wawili, tena katika tofauti ya masaa machache.
Matha alijua Joram kishaonja asali atataka kuchonga mzinga. Wakati anarejea Buzuluga nyumbani kwake wazo la kutafuta muafaka likamjia wazo kuu likawa ni kuua. Matha akanuia kumpa onyo lisilokuwa na nafasi ya pili kijana Joram.
Roho ya kuua ikamwingia!!!
Teksi ilimshusha, akalipia na kuingia ndani ya chumba chake!!
Akalala!!!


****




Michael alikuwa katika matembezi yake ya hapa na pale nje ya nyumba ya John, alikisogelea kibanda kinachouza magazeti akaanza kupitia vichwa vya magazeti mbalimbali.
Macho yake yakavutiwa na gazeti la Ijumaa wikienda. Kichwa cha habari kilimshawishi akatoa pesa na kununua gazeti lile. Akarejea ndani upesi kwenda kuisoma habari ile. Kwanza alishtushwa na picha iliyofanana na mama yake, baadaye haikuwa inafanana alikuwa ni yeye na habari ilikuwa inamuhusu Michael mwenyewe, habari kwamba alikuwa amewekwa msukule na alikuwa ametambuliwa na Mtume maarufu jijini Dar kwa jina la JK yaani Jacob Komanya.
Machale yakamcheza Michael, mchezo mchafu wa kitoto!!!! Alisema Michael huku akilazimisha tabasamu. Tabia za ajabu ajabu zilikuwa zimemuathiri na maneno ya John yalikuwa yamemkaa akaamini kuwa huo ulikuwa ni mchezo wa kumtia hatiani kirahisi.
Kwa kipindi kirefu sana, Michael akawa amekumbuka kifo cha mwanadada Joyce Kindo ambaye alifia nyumba ya kulala wageni!!!
Sikamatwi kirahisi!!! Alimaliza kwa kusema kisha akalihifadhi lile gazeti kwa ajili ya kuwaonyesha akina John pia!!!
Hakuwa na wasiwasi!!!




*******




Mariana alirejea nyumbani akiwa na matumaini tele aliamini kuwa hatimaye alikuwa amepata suluhisho sahihi la kumrejesha mwanaye katika mikono yake.
Hakumshirikisha mtu yeyote kama alivyoshauriwa na mchungaji JK baada ya maombi. Alibaki kimya akiisubiri hiyo siku ya miadi iweze kufika aonane na mchungaji kwa ajili ya maombi mazito. Kila mara alimuombea afya mtumishi huyo wa Mungu asiweze kukumbwa na lolote baya.
Siku ya kwanza ikapita hatimaye siku ya siku ikafika!! Mariana akajiandaa na kumuaga mume wake kuwa anaenda kwa mama yake mdogo, mzee Keto hakupinga lolote alimuamini sana mke wake akampa ruhusa.
Mariana akaelekea nyumbani kwa Mchungaji Jacob Komanya.


Mariana alipishana na msichana rika la Joyce ambaye ni mwanae akitokea nyumbani kwa mchungaji majira ya saa moja na nusu. Yaani nusu saa kabla ya muda aliokuwa ameahidiwa na mchungaji kuwa wakutane.
"Bwana asifiwe…mchungaji yupo!!" Mariana alimsalimia na kuuliza. Yule binti alimkazia jicho la wasiwasi kisha akamuuliza, "Una shida naye??"
"Ndio nina miadi naye!!" alijibu
"Mh!! Haya yupo wala hakuna mtu zaidi ya mlinzi mlangoni…kaombewe" alijibu kwa sanifu kisha akaondoka.
"Mh!! Atakuwa na mashetani huyu!!! Haleluya bwana niepushe na roho hawa wachafu!!" alikemea mwanamke huyu aliyekuwa amevaa nguo sawa kabisa na wanawake wa nchini Nigeria.
Taratibu akagonga geti na kufunguliwa mlango, mlinzi alikuwa bado anamkumbuka hivyo hakumuwekea kipingamizi. Haraka haraka akatembea na kuufikia mlango, akaugonga akatokea mchungaji akamfungulia.
"Oooh!! Glory be to God, Mariana ni wewe!!! Bwana apewe sifa"
"Ni mimi ameeen!!!" alijibu Mariana. Uso wa mchungaji haukuwa na furaha ya kweli na alikuwa na wasiwasi.
Mariana hakujua kuwa binti aliyepishana naye nje ya geti alikuwa ametoka kulazimishwa kufanya mapenzi na mchungaji Komanya. Lakini mashetani yake yaliwazidi ujanja mashetani wa Mchungaji hivyo hakufanikiwa.
Jacob Komanya, alikuwa katika mtihani mkubwa sana kwani kwa siku hiyo alikuwa amefanikiwa kuzini na msichana mmoja pekee jambo ambalo lilikuwa kinyume na masharti aliyopewa nchini Nigeria wakati akiwa masomoni.
Mariana hakuwa na kiburi cha kumuuliza lolote JK, aliingia ndani. Akakaribishwa kinywaji akaachwa peke yake sebuleni. Baada ya muda mrefu kidogo mchungaji alirejea alikuwa amevaa suti nyeupe iliyoukamata mwili wake vizuri. Mguuni alikuwa amevalia kiatu cheupe aina ya ‘four angle', kifuani alikuwa na cheni nzito iliyotengenezwa kwa madini ya dhahabu, ndevu zake zilizochongwa katika mfumo wa herufi O zilimfanya apendeze sana, Mariana alikiri unadhifu huo kimya kimya.
"Tunaweza kwenda Mariana!!" JK alizungumza Mariana akasimama na kumfuata.
JK hakumuaga mlinzi zaidi ya kuwasha gari na mlinzi kufungua geti. Ndani ya gari la kifahari aina ya Hummer, Komanya alikuwa anaendesha mwenyewe, Mariana alikuwa kushoto kwake ametulia tuli huku akijaribu kupitia maandiko hapa na pale.
Tayari ilikuwa saa tatu usiku!!!
Gari lilikuwa katika mwendo wa kawaida kutokana na foleni za hapa na pale lakini baada ya kuiacha Mbezi mwisho, mwendo uliongezeka kidogo hadi liliposimama maeneo ya Kibaha.
Mchungaji alichukua kichupa kidogo kilichokuwa kimehifadhi utuli, akajipulizia kidogo kisha akatabasamu, Mariana naye akajibu kwa tabasamu lakini hilo lilikuwa tabasamu la mwisho kabla ya pepo la ngono halijampanda mama huyu, alijikuta anarembua macho yake, aibu zilikuwa mbali naye, alijisogeza karibu na mchungaji.
"Jacob nahisi baridi!!!" alisema kimahaba, JK akatabasamu na kuifanya ile staili yake ya kunyoa ndevu kuonekana vizuri!!
Hakujibu kitu badala yake aliwasha gari na kuendesha umbali mfupi. Akalifikia bango dogo lililoandikwa Kibaha Yetu Lodge, akakata kulia na kukanyaga mafuta tena akawa ameifikia nyumba hiyo ya kulala wageni.
"Karibu baba!!!" alipokelewa kwa shangwe.
"Nilipiga simu, mmepewa maelekezo tayari!!!" aliuliza.
"Ndio chumba namba 18 kipo tayari!!!" alijibiwa na msichana aliyekuwa muhudumu wa pale.
"Naona upo na mama mchungaji!!!" alitania yule binti!! JK akacheka kwa staha, Mariana akajisogeza karibu yake akamshika kiuno wakaelekea chumba walichoelekezwa.
Haikuwa mara ya kwanza kwa mchungaji huyu kufika eneo hili!!!
Bila kujitambua Mariana akazini na mchungaji, bila shaka hiyo ndio ilikuwa sala ya kumuombea Joyce Keto huko alipo aweze kurudi. Fahamu zilimrudia Mariana wakati wakiwa wamemaliza kufanya tendo, alimkasirikia sana mchungaji lakini JK hakuzungumza kitu zaidi ya kumwambia.
"Nenda ukatangaze na ndoa yako ivunjike!!!" maneno hayo yalikuwa kama kisu kikali kwa Mariana, yalipenya kama ubaridi na kisha uchungu ukalipuka akaanza kulia, mchungaji akacheka kwa sauti ya juu kidogo huku akivaa nguo zake. Kicheko hicho kikawa shambulizi baya kwa Mariana akajiona amebakwa katika mazingira ya ajabu tena uzeeni.
Akaondoka haraka haraka pale chumbani akiwa na akili ya kurejea jijini Dar es salaam. Alipofika barabarani akagundua kuwa hakuwa na nauli, mwenyeji wake alikuwa ni Jacob Komanya peke yake eneo lile. Mariana hakuwa na namna nyingine akarejea kwa aibu kubwa sana akakutana na JK anatoka mapokezi kukabidhi chumba.
"Ulitaka kurejea Dar kwa miguu" aliuliza kwa dharau kuu JK, Mariana akapatwa na kigugumizi cha kujibu. Jacob Komanya akatoa pochi yake ya rangi nyekundu na nyeupe akachomoa noti sita zenye rangi nyekundu. Akawa amempatia Mariana shilingi elfu sitini za kitanzania.
"Nahitaji elfu mbili tu!!" alileta jeuri Mariana huku akishindwa kumkazia macho mchungaji!!!
"Na hiyo ya kutoa mimba atakupatia mume wako??" Jacob aliuliza swali lililomshtua Mariana, akawa amezidiwa ujanja alitamani kupiga kelele lakini hakuwa na ushahidi wa kumwezesha kufanya hivyo.
Akasonya kwa hasira na kisha akajiondokea!!! Huku nyuma JK akacheka kidogo halafu akasikika akisema, "Naenda hapo Mlandizi kwenye maombi!! Twende wote basi!!!"
Mariana hakugeuka!!!


Mariana hakuweza kurudi nyumbani kwake kwani alikuwa amemuaga mume wake kuwa atachelewa sana kurejea hivyo aliamua kuchukua chumba katika nyumba za kulala wageni. Hakuwa na hamu ya chakula alilala hivyohivyo!!!
Saa nne kamili asubuhi alifika nyumbani kwake, hakukuta watu zaidi ya mfanyakazi wa ndani alisalimiwa lakini hakujibu salamu hiyo, akaingia mpaka chumbani akajifungia.
Punde tu baada ya kuufunga mlango, alianza kuisikia nafsi yake ikitamka neno HATIA, akajiuliza lina maana gani kwa wakati huo, macho yake yakatua katika mkono wake, akakutana na pete ya ndoa, kumbukumbu ya usaliti ikamchukua na kumlegeza akakaa kitandani bado alikuwa anaiangalia pete ile. Picha ya Mchungaji JK akiwa anatabasamu ikajijenga mbele yake, Mariana akauma meno kwa uchungu, kisha akazivuruga nywele zake, uchungu ukapita kipimo. Akapatwa na hasira kali chuki nayo haikubaki nyuma lakini hatia ya usaliti ndio ilitawala kichwa chake.
Mzee Keto na upendo wake atanielewaje?? Alijiuliza Mariana, mara bila kutegemea, ule uasili wa kabila lake uasili usioaminiwa na watu wengi lakini ni uasili wa asili, uasili wa kurithi kutoka kwa chifu Mkwawa, ‘kuliko kudhalilika heri kufa!!!', Mariana akajikuta akiwaza kujiua tena kwa kujinyonga. Maneno machache yalichafua karatasi, kanga yake ilimtosha kabisa muhehe huyu, Mariana akajinyonga chumbani mwake!!!
Hasira, mfadhaiko na uasili ukawa umemuua Mariana. Hatia yake ilikuwa nzito kujibu kuliko kuikwepa. Mariana kitanzini akapanda na hatia yake.


*****


***HATIA ya usaliti imemtafuna MARIANA ambaye amejikuta harakati zake za kumkomboa mwanaye aliyepotea kuishia mikononi mwa mtu mbaya JK........MARIANA akajitia kitanzi!!!

***JORAM ameanza kumnyanyasa MATHA kingono!! Nini hatma yao???

***Wapi JOHN MAPULU...wapi JOYCE KETO.....DEFAO.....


NYIRO master09 Khantwe KABERWA2013 mbalu Honey Faith Sangomwile Jullie Z mugaru VAN HEIST binti kiziwi Donatila
 
ram baada ya hisia zangu tupo pamoja tena huku...bhana napenda vijana wanavyojituma kusumbua akili zetu!

Pamoja sana mkuu though siku hizi niko busy sana naingia huku kwa nadra sana but nafuatilia mkuu
 
Last edited by a moderator:

Similar Discussions

Back
Top Bottom