Riwaya - Gereza la Kifo

Riwaya - Gereza la Kifo

Gereza la Kifo - 10

Mtunzi - HAMISI KIBARI

ILIPOISHIA

Walari ambaye alikuwa anapeleka mkono kufungua mlango aligeuka na kumtazama. "Afande, alikufa Yesu, alikufa Mtume Muhammad, wamekufa watu mashuhuri katika bara hili kama Nkrumah (Kwame), Nyerere (Julius) hadi Firauni aliyejiita Mungu sembuse mimi. Wewe niue tu. Kila nafsi, sisi Waislamu tunasema, itaonja mauti, ikiwa ni pamoja na ya kwako."
"Bado unanijibu jeuri. Nitakuua ufe kibudu," akazidi kufoka yule askari akiwa bado kamwelekezea bastola Walari ambaye alikuwa kasimama akiuangalia mtutu wa bastola.

Endelea...

"Sikiliza afande. Wewe fyatua tu risasi, ninakuruhusu kwa sababu mimi napenda kufa kishujaa kama wewe unavyoogopa kufa. Isipokuwa lazima nikujulishe kwamba hivi tunavyoongea bosi wangu anajua niko hapa kwako, kwa hiyo utakaponiua usijidanganye hata kidogo kwamba nitakufa kibudu kama unavyoita. Sana sana utanogesha habari itakayoandikwa juu yangu na kitu nilichokuwa ninakifuatilia kwako pia kiko mbele ya bosi wangu. Huo ndiyo ukweli."
Askari yule aliyekuwa akitetemeka kwa hasira hakujua ujasiri ule Walari anautoa wapi. Akashusha bastola yake na kumruhusu aende zake na kumuonya tena kwamba kama ataandika kile alichoita umbeya na upuuzi basi ajue atakuwa amejitumbukiza katika matatizo makubwa yeye na gazeti lake.
Mwandishi huyo wa habari alitoka nje ya ofisi hiyo na kupita kwa karani wa bosi huyo wa gereza. Alimuaga kwa upole huku akimshukuru kwa kumruhusu kwenda kuonana na bosi wake, kisha akatoka nje kabisa ya jengo hilo ambalo liko umbali wa mita 200 kutoka mahala lilipo gereza kuu la Magamaga mjini Bulibuli.
Wakati akisubiri daladala katika kituo ambacho kiko jirani tu na ofisi hiyo, akaona yule karani wa mkuu wa gereza akimjia haraka haraka, kisha akamuita.
"Unasemaje dada?" Akauliza huku akigeuka kumfuata.
"Bosi Masunju anakuita," akajibu karani yule.
"Bosi wako amenifukuza kwa vitisho. Anataka nini tena, au ndiyo anataka akaniue. Hivi unajua kanishikia bastola wakati sina kosa lolote! Au kaniitia hao walinzi wanikamate?"
"Sidhani. Naomba tu ukamsikilize tafadhali. Unajua nyiye waandishi labda umemhoji kitu kibaya. Bosi wangu ninamjua, ni mtu wa hasira za harakaharaka na anaweza kufanya kitu kibaya na kuja kukijutia baada ya muda mfupi. Ninakuhakikishia kama alikasirika muda ule sasa hivi kapoa. Ndivyo alivyo na sisi tumeshamzoea," akazidi kumshawishi karani yule ambaye ni kicheo alikuwa sajenti wa jeshi la magereza.
Walari alifikiri kidogo, akawa kama anasita, kisha akakata shauri kurudi tena kwenye ofisi ya ofisa huyo.
"Liwalo na liwe, ngoja nikamsikilize," alijisemea huku bado akihisi uoga fulani.
Tofauti na awali, safari hii uso wa mkuu yule wa gereza ulikuwa umekunjuka na kuonyesha bashasha kidogo.
"Karibu kiti," alikaribisha ofisa huyo, kisha akamwita karani wake kumfungulia mwandishi kinywaji anachotaka kwenye jokofu. Walari aliomba soda.
"Mfungulie bia... Unakunywa bia gani?" Akauliza Masunju.
"Hapana. Mimi sinywi pombe. Nipe Fanta."
"Nimekuita tena Mr. Saire, nadhani sikukutendea haki kwa kutosikiliza maswali yako yote," akaanza kusema ofisa yule wa magereza wakati Walari akitumbukiza mafunda ya kinywaji kile baridi kwenye koo lake. "Pengine hayo maswali yako yakanisaidia kujua mambo fulani fulani kwa faida yangu kama mkuu wa gereza."
"Anyway! Maswali ya msingi umeyajibu na hakuna lililoharibika," akajibu Walari.
"Usiwe na wasiwasi. Uliza tu hayo mengine yaliyobaki hata kama si ya msingi nadhani leo niliamka vibaya."
"Labda maswali ya muhimu ni haya yafuatayo. Inadaiwa kuwa wafungwa wengi hawana nguo na pia inadaiwa kwamba nyiye maofisa, hasa wewe, ndiyo mnaofaidika na kuwaumiza wafungwa kwa kuchukua nguo za wafungwa na kuuza pamoja na dawa zinazoletwa kwa ajili ya wafungwa. Kuhusu dawa inadaiwa kuwa mnapeleka kwenye maduka yenu au kwa familia zenu," akasema Walari huku Masunju akimtumbulia macho.
Akaendelea: "Sambamba na hilo, inadaiwa pia kwamba kuna kiwanda kimoja chako wewe, ingawa gereza pia lina ubia, wafanyakazi ni wafungwa ambao hawalipwi. Kibaya zaidi inadaiwa kuwa kuna kemikali ambazo ni hatari kwa afya zao na wengi wameathirika kwa vile hawana zana za kujilinda. Pia inadaiwa tenda nyingi gerezani kwako ni hewa, ndiyo maana umetajirika sana na wafungwa wana hali duni sana."
"Sikiliza bwana mdogo, huu wote ni uzushi tu na chuki za watu, wala hakuna kitu kama hicho. Hizi habari za uzushi umezipata wapi wewe. Unaweza kunitajia aliyekuletea uzushi woote huu?"
"Nimezipata kwenye vyanzo mbalimbali na zingine nimeshuhudia mimi mwenyewe kwa macho."
"Najua nyiye waandishi mnasikiliza sana umbea na majungu ya mahabusu au watu wanaomaliza vifungo vyao pamoja na wabaya wangu. Naomba uache kufanyia kazi majungu. Kama nilivyosema awali, gereza letu ni dogo kulinganisha na idadi ya wafungwa. Tuna wafungwa karibu mara nne zaidi ya kiwango kinachostahili. Mimi nadhani tunastahili pongezi badala ya lawama kwa sababu tunajitahidi sana kadri ya uwezo wetu," akasema ofisa huyo.
Walari akamgeukia: "Kuna hili pia. Juzi nasikia kuna mahabusu katika gereza lako wamepigwa risasi wakati walipokuwa wanapelekwa mahakamani kwa madai kwamba walikuwa wanatoroka. Tena mmoja ni binamu yangu kabisa. Ingawa mahabusu hawa walikuwa chini ya polisi lakini inadaiwa kuna mkakati maalumu wa kuua wafungwa na mahabusu wakorofi au wenye tuhuma za ujambazi. Tena hii si mara ya kwanza. Wewe unasemaje kuhusu hilo?"
"Mr. Saire, suala la kuuawa kwa mahabusu kawaulize polisi, lakini nakuhakikishia hakuna mkakati wowote wa kuua wafungwa. Tuwaue hivihivi tu kwa nini? Sisi siyo wendawazimu?"
"Lakini inadaiwa kuwa mnataka mahabusu wafe wapunguze msongamano... Basi, tuliache hilo. Kuna hili suala la mavazi kwa wafungwa. Inasemekana kwamba baadhi ya wafungwa katika gereza lako hawana nguo pamoja na baridi kali la hapa Bulibuli. Inadaiwa kuwa watu wanakaa vifua wazi tu muda mrefu. Wewe unasemaje kuhusu hilo?"
"Aliyekupa haya majungu kakueleza kitu ambacho hajakifanyia utafiti. Pamoja na ukweli kwamba kuna upungufu wa nguo, lakini karibu wafungwa wote wana nguo za kutosha," akajibu.
Walari alimshukuru yule ofisa, akasimama na kuongea sentensi aliyopanga iwe ya mwisho: "Ninashukuru kwa majibu yako lakini fahamu kwamba wengi wanaona mtu akiingia katika gereza ambalo wewe ndiye mkuu wake, basi ni aghalabu kutoka akiwa salama."
Lakini mkuu wa gereza alimketisha chini. "Wewe ni mgeni wangu leo. Huwezi kuondoka hivihivi. Maswali yako yamenipa changamoto lakini sidhani kama utakwenda kuandika majungu kama haya. Hata hivyo, nimekupenda."
Yule ofisa wa gereza mwenye umbo kubwa alitulia kidogo kisha akaendelea kusema: "Kitu kimoja nakuomba, ukisikia neno lolote huko likisemwa kuhusu gereza njoo tu uniambie na mimi nitakuwa ninakulipa gharama za kunisaidia. Tena nitawaambia hapo makarani kwamba wewe ukifika tu wasikusumbue. Upite moja kwa moja kwangu.
Kwa vile nimekupenda, nitakuandikia kibali cha kuchukua mboga za majani toka kwenye gereza letu kila siku, na njia rahisi ni hii; gari litakuwa linakupitishia kwako ama ofisini. Na kule kwenye viwanda vyetu vya mafuta ya kula na sabuni, kesho njoo nitakupa kibali cha kupata dumu moja la mafuta, lita 5, kila mwezi pamoja na mche wa sabuni ya kufulia."
Alimeza mate kidogo kisha akaomba simu ya Walari. Mwandishi huyo alimjibu kwamba hakuwa na simu ya mkononi baada ya simu yake kuibiwa na vibaka na kwamba ndiyo kwanza alikuwa anashughulikia simu ya kawaida ya waya ofisini kwake. Siyo kwamba hakuwa nayo lakini aliamua kumdanganya na akaanza kuwa na hofu kama ingeliita.
"Lakini kuna duka moja jirani tu na ofisi yangu. Ukipiga muda wowote wananiita. Ni sekunde tu nitakuwa tayari niko kwenye simu. Lile duka ni kama langu," akasema.
"Kumbe hauna simu. Zinahitajika shilingi ngapi kuingiza simu ofisini kwako?" Akauliza ofisa huyo mnene.
"Kama shilingi laki moja."
"Basi hilo usihofu. Nitashughulikia. Baadaye nitakusaidia upate simu ya nyumbani," akasema Masunju akivuta mtoto wa meza.
"Hapana afande. Simu ya ofisi makao makuu wameahidi watashugulikia muda si mrefu."
"Haya chukua hii simu," alisema ofisa huyo akitoa simu moja, kubwa kidogo kwa umbo ndani ya mtoto wa meza, "Hii simu ni ya mke wangu mdogo, ameikataa eti anataka nyingine ya kisasa zaidi. Kama unaipenda chukua. Utaweka tu laini."
Walari alifikiri kidogo kwani simu ile ilionekana kuwa nzuri kuliko ya kwake, lakini alihisi mkono unakufa ganzi kuchukua simu hiyo ya bure. Alijua kwa kuchukua simu hiyo ofisa yule alikuwa anataka kumziba mdomo.
"Nashukuru sana afande. Simu ya mkononi sina kwa sasa lakini makao makuu pia wameshaniahidi kuniletea simu ya mkononi muda wowote. Nashukuru sana."
Masunju alimshurutisha achukue simu hiyo hata kama awe akiitumia kwa muda wakati akisubiri yake kutoka makao makuu. Pia akaahidi kumwekea dola tano kila wiki, lakini Walari aligoma kabisa kuchukua.
Mwandishi huyo wa habari alisimama tena kuaga na ndipo ofisa huyo akavuta tena mtoto wa meza na kutoa sh. 50,000 ambazo aliziita ni nauli.
"Chukua teksi hapo nje. Nakushukuru sana. Siku nyingine ukisikia majungu kama haya niletee. Na kwa kuwa wewe ni mwandishi uliyeiva sawasawa, sikutegemei kuandika majungu kama haya. Wewe sasa utakuwa kama mdogo wangu," akasema yule ofisa.
Mwandishi huyo ambaye aliondoka nyumbani huku akiwa ameacha hali si nzuri sana kifedha, alizitamani zile pesa lakini kwa vile aliamini zinatolewa si kwa lengo jema akakataa kuzipokea akijibu kwamba alikuwa haendi moja kwa moja kwa hiyo hakutegemea kupanda teksi.
"Kuna mahala napitia hapahapa karibu. Toka hapo nitakuwa naingia ofisi moja hadi nyingine. Nashukuru sana," akajibu.
Hata hivyo, ofisa huyo alizidi kumshurutisha kuchukua pesa alizoita nauli, lakini Walari akagoma kabisa kuchukua. "Labda nipe sh. 2,000 tu inatosha."

Itaendelea kesho...
Nilisahau. Kama maiti atanyanyuka na kukufuata usikimbie. Ongea naye taratibu. Kama ni mwanamke mwambie mimi nimeshaoa," akatania mhudumu huyo.

maiti anyanyuke usikimbie kuna matani sio mazuri kabisa
 
Nilisahau. Kama maiti atanyanyuka na kukufuata usikimbie. Ongea naye taratibu. Kama ni mwanamke mwambie mimi nimeshaoa," akatania mhudumu huyo.

maiti anyanyuke usikimbie kuna matani sio mazuri kabisa
Hahahaaaa 😀😀😀...
 
Back
Top Bottom