Kama tumerudi nyuma hivi, ila huyu meja kaongezeka
Aiseee unatukanganya si kidogo
Frida na Isha walijaribu kumshauri, aliwasikiliza kwa makini na kuahidi kubadilika lakini kamwe haikuwa hivyo.
Kila yatima aliyekuja katika kituo cha MWANA ilimradi alikuwa ni mrembo George alifanya juu chini ili aweze kushiriki naye mapenzi.
Yote haya yalifanyika kimyakimya. Bila mtu yeyote kutambua.
George alitumia pesa!!
Kweli pesa mwanaharamu.
George alijisahau kuwa aliyekifungua kituo kile ni Mwanaidi, askari makini bila gwanda mwilini mwake.
Tabia hii ilizidi kukomaa huku ikiwa siri ya watu wachache tu siri iliyoendelea kumwacha akiwa na nguvu ya kuishawishi jamii yake, nguvu ya kusema neno na kuaminika kwa asilimia zote.
Tabia hii ingeweza kudumu kwa kipindi kirefu sana tena bila jamii kutambua iwapo tu usingefika usiku huu, usiku wa aina yake. Ulikuwa mrefu kuliko giza lolote lile ambalo George amewahi kuliishi.
USIKU huu George akapata mgeni wa maajabu mgeni ambaye hakuwa na ahadi ya kumtembelea lakini akafika usiku mnene .
Alikuwa na lake jambo ..jambo lililozua mjadala mkubwa kisha kubadilika na kuwa utata .
*****
George alijilazimisha kufumbua macho yake kwa ukubwa ambao hajawahi kufumbua ili aweze kubaini iwapo yu ndotoni ama la! Lakini aliona hali halisi, ile sura ni kama aliwahi kuiona mahali lakini hakujua yule mtu anaitwa nani. Alitaka kumuita lakini sauti haikutoka, na bila kukaribishwa yule mtu ama kiumbe akaketi katika upande mmoja wa kiti. Kisha akafanya mfano wa tabasamu .George akaduwaa.
Haujambo mheshimiwa!!. Hatimaye yule mgeni alimsemesha. George akashindwa kujibu akabaki kuduwaa. Mgeni wake hakujishughulisha na mshangao uliomkumba bwana George, aliendelea na shughuli zake ambazo kwa utashi wake anaamini ndizo zilimleta pale ndani, alifunua huku na kule akiwa anatafuta anachojua yeye mwenyewe hatimaye akakipata kipande cha karatasi, akaipata na kalamu. Akaandika maneno fulani katika mweandiko mbovu kabisa kisha akampatia George aweze kuangusha saini yake. George akasita, yule mtu akamuangalia kwa macho makali sana. Macho yaliyosisitiza amri. George akaweka sahihi. Yule mgeni akatabasamu, kisha akafungua matambala aliyokuwa ameyabeba. Akatoa mzigo ambao ulionekana wazi kukusudiwa kuachwa nyumbani kwa George.
George akaendelea kushangaa lakini safari hii alijikuta akiuliza, Wewe ni nani na na unataka nini? yule mgeni akasita alichokuwa anafanya, akamgeukia Georgekwa macho ya utulivu kabisa. Akafanya tabasamu kisha akajitambulisha kwa ufasaha.
Jina geni kabisa masikioni mwa George, alitaka kuuliza zaidi lakini yule mtu alikuwa na mzigo mkononi akamkabidhi George.
George akapokea pasina ubishi. Yule mgeni bila kuaga alifungua mlango akaondoka zake, mara kiza kikatanda baada ya George kubaini mzigo aliokuwa ameachiwa. Kiza kilekile ambacho George hakuwahi kukiishi kamwe. Kiza kizito tena kilichotanda ukimya wa hali ya juu.
Simu yake ya mkononi iliita ndipo aliposhtuka, akapapasa kisha akabofya hovyo bila kutambua iwapo alipokea au alikuwa ameikata. Akaendelea kuuchapa usingizi, mara ikaanza kuita tena.
Aaargh mamtu mengine bwanaa . Alilalama huku akifanya juhudi za kufumbua macho. Akaoitazama simu zilikuwa ni namba za Isha.i Aaaargh usumbufu tena Isha, si tumeshakubaliana kuwa hatuwezi kuwa wapenzi tena au? Nishamwambia kabisa dini haziruhusu hanidai wala simdai. Aah mi sipokei ..alizidi kughafirika George. Simu ikakatika.
Akapiga kite cha ghadhabu, mara ikaanza kuita tena. Akataka kuipokea kwa pupa na kumjibu hovyo Isha, lakini akakutana na jina la Suzi.
He! Inamaana wanaambizana kunipigia au? alijiuliza George ..
Sasa sipokei zote pumbavu kabisa!!! Akasema kwa sauti ya juu. Usingizi ulikuwa umekatika tayari. Akasimama wima huku akiwalaani wasichana hao kwa kuukatisha usingizi wake mtamu kupita yote aliyowahi kulala.
Alipofika sebuleni akakuta ustaarabu ukiwa umevurugwa, alishangaa kidogo na kujilaani kwa kuanza kuwa na tabia ya uzembe wa kutopanga chumba chake kama ilivyokuwa zamani. Akajilaumu zaidi kwa kumwajiri yule msichana wa kazi.
Monicaaaa!!!! Weee mwanahizayaaa!! aliita kwa ghadhabu. Sauti ya msichana kutoka nje ikaitika kwa ustaarabu .
Simu yake ikaita tena kutoka chumbani.
Sasa naenda kutukana mtoto wa mtu haki ya nani!!! Alisema kwa sauti ya juu yenye kutawaliwa na kitetemeshi cha hasira.
Aliifikia simu akiamini kuwa ni aidha Isha ama mwenzake Suzi.
Wakati anafika chumbani, Monica naye alikuwa amefika sebuleni akishangaa ni kitu gani bosi wake anatafuta hadi afanye vurugu kubwa kiasi kile.
Mpiga simu alikuwa ni Frida wakati huu. Hapa George akatuliza akili na kufikiri mara mbili, akaamini palikuwa na tatizo huenda tofauti kabisa na mawazo yake.
Akaipokea simu ile.
Frida badala ya kuongea alikuwa analia .kwikwi ilisikika na kuonyesha kuwa yule mtu alikuwa amezidiwa na kilio.
Vipi? Amepokea!!! Eeeh!! ilisikika sauti ya Isha pembeni ..George alizidi kusema halooo bila kupata majibu. Mara ile simu ikahamia katika sikio jingine.
Kaka George kuna tatizo huku, tafadhali njoo tupo hapa chumbani kwa Frida njoo tafadhali .
Tatizo? Tatizo gani? alihoji.
Isha kutoka upande wa pili hakuwa tayari kusema tatizo ni nini akamsihi afike.
George hakukumbuka kusafisha mwili wala kinywa chake, alikwapua suruali yake kutoka katika kiambaza cha mlango, akajivika na fulana aliyovaa siku iliyopita .akashika viatu mkononi, akaanza kutimua mbio akimpita Monica akiduwaa pale sebuleni bila kumsemesha lolote hadi alipofika nje.
We mwanamke wewe yaani unalipwa mshahara halafu naniii .ngoja nikirudi aliropokwa haya akiwa nje tayari.
Akaita taksi na kuamuru apelekwe Kinondoni Studio.
Upesi gari ikaondolewa, George alikuwa kimya kabisa. Baada ya nusu saa walikuwa eneo alilokuwa anahitaji kufika. Akafanya malipo upesi na kuendelea kutimua mbio kuifikia nyumba.
Hakika palikuwa na tatizo maana hata majirani walikuwa wapo katika mchanganyiko wa majonzi na hamaniko kama si mshangao.
Mungu wangu Mwanaidi!!! George alianza kuweka hisia zake kuwa mtoto wa Frida alikuwa matatani, ama la sivyo basi mama yake mzazi alikuwa matatizoni.
Jibu la kwanza lilikuwa sahihi. Mwanaidi alikuwa matatizoni. Na ingekuwa heri zaidi kama angekuwa matatizoni na anaonekana pale ili aweze kupatiwa huduma ya kuliondosha hilo tatizo. Ilishangaza kwamba mtoto Mwanaidi hakuwa mahali pale.
Mwanaidi alikuwa ametoweka katika mazingira ya kutatanisha sana. Alikuwa na miezi sita tu tangu azaliwe siku ambayo wajina wake alikuwa anaiaga dunia, sasa haonekani tena kama wajina wake.
Nimelala saa sita na nusu, kuna tamthilia nilikuwa naangalia na mama Mwana, wakati huo Mwana alikuwa amesinzia tayari ..kwa kweli hadi sasa ni maajabu ninaamka mama Mwana ananiambia eti mtoto hayupo kitandani . Mama mmoja ambaye alikuwa anaishi ujirani mwema na akina Frida alielezea. Mama George naye akadakia, Na ni mimi niliyeenda kumlaza, Mama Mwana alikuwa amejikita katika tamthilia mimi nikamchukua mtoto nikamlaza kisha nikaenda kujilalia huko. Yaani mbona kazi?
nilimkuta mwanangu kitandani jamaniii .niliangusha kioo akashtuka na kuanza kulia jamanii .kwa mikono yangu nikambeba nikampa titi anyone, aliponyonya akanyamaza tukaanza kucheza na mwanangu jamaniii uuuuuwi ..mamaa weeeeee!! Asubuhi naamka naikuta midoli tu uwiiiii mwanangu jamaniiiii nisaidieni mimiii Mwananidi wangu weeee Maneno ya Frida na kilio chake yakaamsha msiba wa ajabu msiba usiokuwa na maiti.
Mara Frida alipokaribia kunyamaza, vikasikika vilio vingine kutokea njea vilianza taratibu kisha vikazidi kuvuma na kufika ndani, walikuwa akina dada wawili. Isha na Suzi. Hawa walikuwa wameenda kutoa taarifa polisi juu ya tukio hilo, huko wakaambiwa hakuna taarifa yoyote juu ya mtoto kupotea.
E bwana ee!! Kuna watu hawanyamazishwi wakifungulia kilio. Isha na Suzi walikuwa wanaongoza.
Kila aliyejaribu kumtuliza kama asipoambulia tusi zito basi angeweza hata kungatwa meno.
Frida naye akaanza kulia, mama George akafunga orodha sasa akimlilia mjukuu wake. Huyu alilia hadi akapoteza fahamu.
Ilikuwa imetimia saa tatu asubuhi.
George akaaga kuwa anatoka mara moja kuangalia kipi kinaweza kufanyika, aliongozana na Isha ambaye alikuwa amejituliza mwenyewe. Wakaingia ndani ya taksi. Safari ya kuelekea nyumbani kwa George.
George alipokumbuka juu ya wapi wanaelekea akakumbuka juu ya mpangilio mbovu aliouacha pale sebuleni. Alijiuliza iwapo Monica atakuwa ameuweka sawa ama la anaenda kuabika na wageni wake .
Kuukumbuka mpangilio ule mara George akakumbuka kuwa usiku uliopita ni yeye alikuwa wa mwisho kukaa pale sebuleni pakiwa katika mpangilio mzuri kabisa. Lakini akakumbuka kuwa kuna muda alirejea tena pale na kuna jambo alikuwa anafanya na akamwona yule mtu aliyevuruga sebule yake, hakuwa Monica alikuwa ni kiumbe mwingine kabisa. Tena alijitambulisha jina, na kuna jambo la ziada alifanya..kuna mzigo alimpa naye akaupokea ..
Ni kama kiumbe hai .alipewa kiumbe hai. Akajaribu kuikumbuka sura yake lakini likatokea giza, hakika giza lilitokea hata kabla hajatabua sura ya kiumbe kile .
Mungu wangu weeee!! George alipayuka ghafla. Isha akamtazama kwa masikitiko bila kusema lolote.
George alitangulia mbele na Isha akafuata, wakaingia sebuleni. Monica alikuwa ameiweka sawa sebule na haikuonyesha dalili yoyote ya kashkash! Isha akaanza kuona mwenzake anakaribia kupandwa na wazimu, alimwona George akiishangaa sebule yake mwewnyewe.
Ehee alikuwa hapa hivi amesimama.
Nani tena? Isha aliuliza ndipo George akagutuka kumbe mambo aliyokuwa anayawaza kichwani aliyasema kwa sauti.
Aaah hapana basi tu kwani .nani karibu Isha. Alijiumauma.
Upo sawa G. Isha aliuliza kwa sauti ya kinyonge.
Aaah mimi? aliuliza swali la kipumbavu bila kutarajia.
Isha akamtazama bila kusema lolote. George akasimama na kuingia ndani chumbani mwake Isha akamsindikiza kwa macho.
Macho yaliyomsanifu kijana yule kama kwamba anaukaribisha uchizi kichwani mwake bila kujua.
Unadhani nina tatizo basi mimi hamna basi tu ujue yaani.. alitokwa na maneno hayo wakati anaingia chumbani huku akirusha mikono huku na kule na tabasamu la kujilazimisha midomoni.
Isha hakutia neno akabaki kumtazama tu. Hadi alipotokomea kabisa.
Kimya kilitanda kwa sekunde kadhaa Isha akiwa anatafakari jambo lilitokea alfajiri ya siku hiyo kama mkosi ambao unawafuata kwa nyuma.
Mtoto mwenye umri wa miaka mitatu kutoweka katika mazingira ya kutatanisha tena akiwa mikononi mwa mama yake. Ilistaajabisha hakika.
Mara mawazo yake yalikoma baada ya kusikia purukushani ikitokea katika chumba cha George, ni kama alikuwa akipambana na mdudu ama chochote kile ambacho kilikuwa chumbani mwake kimakosa. Isha aliendelea kuzisikiliza zile purukushani za uhakika, mara kianguke hiki mara kianguke kile.
We ni nani..unataka nini hapa eeh .Sikujui toka sauti ya George iliyokuwa inasota ilisikika ikihangaika. Isha akastaajabu, akavamiwa na hisia kuwa George alikuwa ameanza kuishi katika uchizi rasmi. Alifanya tabasamu la karaha kisha akajisemea mzimu wa majanga unaandamana nasi bado.
Neno lake la mwisho bado liliambatana na kishindo kikubwa baada ya yowe kubwa kutoka chumbani kwa George. Hapa sasa hakuendelea kukaa. Akasimama wima akakimbilia chumbani kwa George.
Macho yake yakakutana na mwili wa George ukitiririkwa jasho chumba kikiwa katika hali ya utulivu sana lakini kilichovurugika sana.
George alikuwa hajitambui
Isha akapagawa, hakuamini kilichokuwa kinatokea mbele yake, ulikuwa muendelezo wa ile filamu ya alfajiri ya kutoweka mtoto wa Frida katika mazingira tatanishi na sasa ilikuwa zamu ya George kupoteza fahamu katika mazingira ya kutatanisha vilevile.
Upesi akaitwaa simu yake akampigia Suzi. Simu ikapokelewa akamwomba afanye upesi akiongoza na wanaume kadhaa wafike nyumbani kwa George.
Vipi Mwanaidi ameonekana? Suzi aliuliza kwa kihoro.
Isha akamsisitiza afike upesi.
****
George alikurupuka kutoka katika usingizi mzito uliozigandamiza fahamu zake na kujikuta akiwa katika kitanda cha hospitali ya Mazengo katikati ya jiji.
Alijitazama huku na kule na kujikuta amezungukwa na watu kadhaa. Pole mfululizo zikafuata baada ya kujitambua.
George ni nani ulikuwa unajibizana naye ndani. Isha alimuuliza wakiwa wamekaa.
Mimi? Mimi nikajibizana na mtu. George aliuliza huku akijielekezea kidole kifuani kwake. Sijazungumza na mtu hata mmoja wala. Alimalizia sentensi ile.
Niliwaambia jamani . Isha aliwatazama Suzi na wale vijana wengine ambao aliwaambia kuwa ana mashaka kupotea kwa mtoto Mwanaidi kunaelekea kumpa wazimu George. Suzi akainama chini na kufanya ishara ya msalaba kuombea lisitokee hilo linalodhaniwa na Isha.
Ilikuwa tafrani hakika.
Wakati haya yakiendelea huku hospitali kuna jicho lilikuwa likiyatazama yote haya huku uso wake ukitabasamu kwa matumaini makubwa sana. Alikuwa analifanikisha lengo lake taratibu lakini kwa umakini mkubwa sana .hakuna aliyejua kuwa kuna jicho linawatazama kutokea katika kona moja ya kile chumba.
George alikuwa mtulivu sana, akitafakari juu ya tukio lililotokea chumbani kwake. Alitamani sana kuwashirikisha watu waliomzunguka lakini akayakumbuka masharti yaliyotajwa na mtu yule wa ajabu ..kingine kilichomtia uzito katika jambo hili ni ile hali ya kukumbuka kuwa kile kitu alichokabidhiwa katika ile hali aliyodhani kuwa ni ndoto sasa alitambua fika kuwa alikabidhiwa mtoto mdogo ambaye alikuwa anamjua kwa sura na historia pia.
Lakini hakulitambua jina lake kwa wakati ule.
George angeweza kuelezea juu ya ndoto hiyo lakini nani angeamini kama asingetimiza masharti aliyopewa na yule mtu wa ajabu ambaye hisia zake zinakiri kuwa hapo kabla aliwahi kumuona. Alipomuona ni wapi? Hilo lilikuwa swali gumu zaidi.
Kichwa kikawaka moto zaidi ya kawaida. Huu ulikuwa mtihani mkubwa sana kuupata maishani. Yale maneno ya mwisho ya yule kiumbe ndo yalimfadhaisha zaidi, kuna jambo zito alitakiwa kuliweka bayana mbele ya jamii. Jambo ambalo George alitaka libaki siri milele.
Lakini kama angesimamia msimamo wake basi kuna shauri jingine ambalo lilikuwa zito zaidi na iwapo lisipotimizwa basi kinazuka kizaazaa kisichokuwa na mfanowe.
Ni heri yale maisha ya uchokoraa ya kulala katika vichochoro bila kupata chakula. Ni heri kukimbizana na mgambo wa jiji kuliko kukumbana na kizaazaa. Na ilikuwa heri zaidi kuishi jela miaka yote kuliko kuishi katika dunia huru inayotawaliwa na kizaazaa.
Kizaazaa kinazuliwa na George bila chokoraa wale kufahamu, lakini kinasambaa na kuwakumba wote, lakini wakati huu anaongezeka mtu mwingine matata kabisa anayeondoka kwa jina la Suleiman Meja.
****
KITABU CHA PILI CHA CHOKORAA NI (KIZAAZAA)
ram Khantwe