SIMULIZI.... BALAA
MWANDISHI.. HALFANI SUDY
SIMU; 0757 633010
SEHEMU YA KUMI NA MBILI
"Jamani tunakufaaa" sasa ndio alizisikia kelele za Mwanasheria kule mapokezi.
Dokta Yusha alitoka nje kumwangalia Mwanasheria alikuwa ameumia sehemu gani. Alimfikia Mwanasheria na kumkagua mwili mzima. Mwanasheria hakuwa na jeraha lolote zaidi ya zile damu zilizompakaa. Dokta Yusha akawaza labda Mwanasheria kaumia ndani kwa ndani. Wakati akimwangalia Mwanasheria ndipo alipomuona Fred kwa mbali, rafiki yake wa siku nyingi. Na ndiye alikuwa mpambe wake wa harusi siku ile.
"Vipi Fred"
"Ebana wameumia vibaya sana, afadhali nimekuona, nimewafata madaktari mpaka nyumbani kwao, hawapo, sijui wameenda wapi?"
"Kwani kilitokea nini Fred?" Dokta Yusha aliuliza kwa sauti yake yenye kwikwi.
"Mimi kanipigia simu huyo jamaa anayelia, muda mfupi tu nilipofika nyumbani kutoka kwenye sherehe, sijui hata namba yangu aliitoa wapi, yeye alikuwa analia tu, huku akisema wote wamekufa. Alinielekeza mahali ilipotokea ajari. Nilienda haraka kwa gari, na kukuta familia ya Nasra wamepata ajari mbaya sana ya gari aisee, majeruhi wako ndani huko" Fred alisema bila kujua kama Dokta Yusha kashaingia mle ndani na kujionea mwenyewe athari za ajari ile.
Kule nyuma ya chumba cha kuhifadhia maiti, Tano alikuwa anasubiri ujio wa Dokta Yusha. Alikuwa amejiandaa vema kumuua Dokta Yusha pindi atakapotokea tu. Alijibanza konani na kisu chake mkononi. Hakujua kabisa kuwa kwa wakati ule Dokta Yusha alikuwa amesahau kabisa habari ya simu ya mtu yule.
Tano alisubiri na kusubiri.
Alfajiri, mji wa Kilwa Masoko, waliamka na habari kuu mbili.
Habari ya kwanza ilikuwa ni kutokea kwa ajari katika kona inayoelekea mtaa wa Lumumba. Vijiwe vyote vinavyojadiri habari ngumu waliijadiri sana habari hiyo. Habari iliyohusisha ajari mbaya waliyoipata familia ya Mzee Mpaukha.
Habari ya pili ni kukimbia kwa bwana harusi katikati ya sherehe. Habari iliyopambwa na kusimuliwa vizuri sana na mafundi wa kusimulia. Tena wengine hawakuwepo hata katika ile sherehe yenyewe lakini ndio walikuwa wasimuliaji wakubwa. Vijiwe vyote vya waambea waliipa sana 'airtime ' habari hii ya bwana harusi kukimbia katikati ya sherehe kuliko habari ile ya ajari.. .
ITAENDELEA KESHO MUNGU AKIPENDA